Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Wimbo wa Sulemani
    Mnara wa Mlinzi—2006 | Novemba 15
    • MSIJARIBU “KUAMSHA UPENDO NDANI YANGU”

      (Wimbo wa Sulemani 1:1–3:5)

      “Na anibusu kwa busu za kinywa chake, maana maonyesho yako ya mapenzi ni bora kuliko divai.” (Wimbo wa Sulemani 1:2) Mazungumzo ya Wimbo wa Sulemani yanaanza kwa maneno ya msichana mnyenyekevu wa mashambani ambaye analetwa ndani ya hema la kifalme la Sulemani. Alifikaje humo?

      “Wana wa mama yangu mwenyewe walinikasirikia,” anasema. “Waliniweka kuwa mtunzaji wa mashamba ya mizabibu.” Ndugu zake wamemkasirikia kwa sababu mvulana mchungaji ambaye anampenda amemwomba aende pamoja naye matembezini siku moja nzuri ya masika. Ili kumzuia asiende, wanampa kazi ya kuchunga “mbweha wadogo wanaoharibu mashamba ya mizabibu.” Kazi hiyo inamfanya aje karibu na kambi ya Sulemani. Urembo wake unaonekana anaposhuka kwenye “bustani ya milozi,” naye analetwa kambini.—Wimbo wa Sulemani 1:6; 2:10-15; 6:11.

      Mwanamwali huyo anapoeleza jinsi anavyomtamani mchungaji wake mpendwa, wanawake wa makao ya mfalme wanamwambia ‘aende mwenyewe katika nyayo za kundi’ akamtafute. Lakini Sulemani hamruhusu aende. Akieleza jinsi anavyovutiwa na urembo wake, Sulemani anaahidi kumpa “vitaji vya dhahabu pamoja na vifungo vya fedha.” Hata hivyo, msichana huyo havutiwi naye. Mvulana mchungaji anaingia katika kambi ya Sulemani, anampata, na kusema hivi: “Tazama! Wewe ni mrembo, ewe msichana mwenzi wangu. Tazama! Wewe ni mrembo.” Mwanamwali huyo mchanga anawaapisha hivi wanawake wa makao ya mfalme: “Msijaribu kuamsha au kuwasha upendo ndani yangu mpaka wenyewe utake.”—Wimbo wa Sulemani 1:8-11, 15; 2:7; 3:5.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Wimbo wa Sulemani
    Mnara wa Mlinzi—2006 | Novemba 15
    • “MNAONA NINI KWA MSHULAMI?”

      (Wimbo wa Sulemani 3:6–8:4)

      Kuna kitu kinachokuja “kutoka nyikani kama nguzo za moshi.” (Wimbo wa Sulemani 3:6) Wanawake wa Yerusalemu wanaona nini wanapotoka nje ili kutazama? Tazama, Sulemani na watumishi wake wanarudi jijini! Na mfalme amemleta mwanamwali Mshulami.

      Mvulana mchungaji anamfuata mwanamwali na punde si punde anapata njia ya kumwona. Anapomhakikishia upendo wake, msichana huyo anaeleza jinsi anavyotamani kuondoka jijini kwa kusema hivi: “Mpaka mchana uvume upepo mtulivu na vivuli viwe vimekimbia, nitakwenda zangu kwenye mlima wa manemane na kwenye kilima cha ubani.” Anamwomba mchungaji huyo “aje katika bustani yake, ale matunda yake yaliyo bora kabisa.” Mchungaji anajibu: “Nimeingia katika bustani yangu, ewe dada yangu, bibi-arusi wangu.” Wanawake wa Yerusalemu wanawaambia hivi: “Kuleni, enyi wapenzi! Kunyweni, mlewe maonyesho ya mapenzi!”—Wimbo wa Sulemani 4:6, 16; 5:1.

      Baada ya kuwasimulia wanawake wa makao ya mfalme kuhusu ndoto yake, mwanamwali Mshulami anawaambia: “Nimelewa mapenzi.” Wanamuuliza: “Jinsi gani mpenzi wako ni bora kuliko mpenzi mwingine yeyote?” Anajibu: “Mpenzi wangu anametameta na ni mwekundu, mwenye kuvutia zaidi kati ya elfu kumi.” (Wimbo wa Sulemani 5:2-10) Sulemani anapomsifu-sifu sana, Mshulami anamjibu hivi kwa unyenyekevu: “Mnaona nini kwa Mshulami?” (Wimbo wa Sulemani 6:4-13) Akifikiri kwamba hiyo ndiyo nafasi ya kumpata, mfalme anamsifu hata zaidi. Hata hivyo, msichana huyo anabaki imara katika upendo wake kwa mvulana mchungaji. Mwishowe, Sulemani anamwacha aende nyumbani.

  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Wimbo wa Sulemani
    Mnara wa Mlinzi—2006 | Novemba 15
    • “MWALI WA MOTO WA YAH”

      (Wimbo wa Sulemani 8:5-14)

      “Mwanamke huyu ni nani, anayepanda kutoka nyikani, akimwegemea mpenzi wake?” wanauliza ndugu za Mshulami wanapomwona akirudi nyumbani. Muda fulani mapema, mmoja wao alikuwa amesema: “Kama akiwa ukuta, tutajenga juu yake mnara wa fedha; lakini akiwa mlango, tutamzuia kwa ubao wa mwerezi.” Kwa kuwa sasa upendo wa Mshulami umejaribiwa na kuthibitika kuwa imara, yeye anasema: “Mimi ni ukuta, na maziwa yangu ni kama minara. Basi nimekuwa machoni pake yeye kama msichana anayepata amani.”—Wimbo wa Sulemani 8:5, 9, 10.

      Upendo wa kweli ni “mwali wa moto wa Yah.” Kwa nini? Kwa sababu Yehova ndiye chanzo cha upendo wa aina hiyo. Yeye ndiye ametuumba tukiwa na sifa ya upendo. Ni mwali ambao miwako yake haiwezi kuzimwa. Wimbo wa Sulemani unaonyesha kwa njia nzuri sana kwamba upendo kati ya mwanamume na mwanamke unaweza kuwa na “nguvu [hauwezi kushindwa] kama kifo.”—Wimbo wa Sulemani 8:6.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki