-
Jinsi Dini Ilivyoshambuliwa na SovietiAmkeni!—2001 | Aprili 22
-
-
Jinsi Dini Ilivyoshambuliwa na Sovieti
MUUNGANO wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti ulianzishwa mwaka wa 1922, na Urusi ndiyo iliyokuwa jamhuri kubwa na maarufu zaidi kati ya jamhuri nne za kwanza za muungano huo. Baadaye muungano huo ulipanuka na kuwa na jamhuri 15 na kumiliki takriban sehemu moja kwa sita ya dunia yote. Lakini Muungano wa Sovieti ulivunjika ghafula mwaka wa 1991.a Muungano huo ulikuwa Serikali ya kwanza kujaribu kuzuia watu kumwamini Mungu.
Vladimir Lenin, kiongozi wa kwanza wa Muungano wa Sovieti, alikuwa mfuasi wa Karl Marx. Karl Marx aliona kwamba Ukristo ulitumiwa kuwakandamiza watu. Marx alisema dini huwapumbaza watu, naye Lenin akasema hivi baadaye: “Wazo lolote la kidini, wazo lolote juu ya mungu awaye yote, . . . ni uovu usiowazika.”
Kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Urusi, Tikhon, alipokufa katika mwaka wa 1925, kanisa halikuruhusiwa kuteua kiongozi mwingine. Dini ilishambuliwa na majengo mengi ya kanisa yakaharibiwa ama kutumiwa kwa makusudi mengine. Makasisi walipelekwa kwenye kambi za kazi ngumu, ambamo wengi walifia. Kichapo Encyclopædia Britannica chaeleza kwamba “kanisa lilinyanyaswa kinyama na maelfu wakauawa wakati wa utawala wa Joseph Stalin mwishoni mwa miaka ya 1920 na 1930. Kufikia mwaka wa 1939 ni maaskofu watatu au wanne tu wa Kanisa Othodoksi ambao walisalia na makanisa 100 ndiyo yaliyokuwa yakitumiwa kwa ibada.”
Lakini, badiliko kubwa sana lilitokea ghafula.
Vita ya Ulimwengu ya Pili na Dini
Vita ya Ulimwengu ya Pili ilizuka mwaka wa 1939, wakati Ujerumani ya Nazi, iliyokuwa rafiki ya Muungano wa Sovieti wakati huo, ilipovamia Poland. Baada ya mwaka mmoja, Muungano wa Sovieti ulikuwa umenyakua jamhuri 4 za mwisho kati ya jamhuri zake 15—Latvia, Lithuania, Estonia, na Moldavia. Hata hivyo, Ujerumani ilishambulia vikali Muungano wa Sovieti mnamo Juni 1941, jambo hilo lilimshtua sana Stalin. Mwishoni mwa mwaka huo, wanajeshi Wajerumani walikuwa wamefikia vitongoji vya Moscow, na Muungano wa Sovieti ulielekea kushindwa.
Stalin alijitahidi kwa hofu kutayarisha taifa lake kwa pambano ambalo Warusi waliliita Vita Kuu ya Kizalendo. Mamilioni ya watu bado walikuwa wafuasi wa dini. Kwa hiyo Stalin aling’amua kwamba alihitaji kulirudishia kanisa mapendeleo fulani ili wafuasi wamwunge mkono katika vita hiyo. Kubadilika kabisa kwa maoni ya Stalin kuelekea dini kulikuwa na matokeo gani?
Kwa kushirikiana na kanisa, Warusi waliunga mkono vita, na Sovieti ikashinda kabisa Wajerumani kufikia mwaka wa 1945. Sovieti ilipoacha kushambulia kanisa kwa muda, idadi ya makanisa ya Othodoksi iliongezeka hadi 25,000, na idadi ya makasisi ikafikia 33,000.
Mashambulizi Yaendelea
Hata hivyo, viongozi wa Sovieti bado walikuwa na lengo la kuwazuia watu kumwamini Mungu. Kichapo The Encyclopædia Britannica chaeleza hivi: “Waziri Mkuu Nikita Khrushchev alianzisha mbinu mpya ya kukomesha dini mwaka wa 1959-1964, akiruhusu tu makanisa yasiyozidi 10,000. Pimen aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Kanisa mwaka wa 1971 baada ya kifo cha Alexis, lakini kanisa lilielekea kutokomea lijapokuwa na mamilioni ya wafuasi.”b
Baadaye tutazungumzia jinsi Kanisa Othodoksi la Urusi lilivyookoka shambulizi hilo jipya la Sovieti. Lakini dini nyingine katika Muungano wa Sovieti zilikabilianaje na hali hiyo? Kati ya dini hizo, ni ipi iliyokuwa shabaha hasa ya mashambulizi, na kwa nini? Maswali hayo yatazungumziwa katika makala ifuatayo.
[Maelezo ya Chini]
a Nchi 15 zifuatazo zilizo huru zilikuwa jamhuri za Sovieti hapo awali: Armenia, Azerbaijan, Belarus, Estonia, Georgia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Latvia, Lithuania, Moldova, Tajikistan, Turkmenistan, Ukrainia, Urusi, na Uzbekistan.
b Nyakati nyingine majina ya Alexis wa Kwanza, kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Urusi kutoka mwaka wa 1945 hadi 1970, na Alexis wa Pili, ambaye ameongoza tangu 1990 hadi leo, hutamkwa Alexy, Aleksi, Aleksei, na Alexei.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Lenin alisema ‘wazo lolote juu ya Mungu ni uovu usiowazika’
[Hisani]
Musée d’Histoire Contemporaine—BDIC
-
-
Shabaha ya Mashambulizi ya SovietiAmkeni!—2001 | Aprili 22
-
-
Shabaha ya Mashambulizi ya Sovieti
LICHA ya maelewano yaliyokuwapo kati ya serikali na Kanisa Othodoksi la Urusi ili kushinda Vita ya Ulimwengu ya Pili, Muungano wa Sovieti uliendelea kukandamiza shughuli za kanisa. Kwa hiyo, kama vile kitabu The Sword and the Shield, kilichoandikwa mwaka wa 1999 chenye historia ya KGB (Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti), kilivyosema, “shirika la KGB lilihangaishwa hasa na shughuli za ‘uchochezi’ za Wakristo ambao halikuweza kuwadhibiti moja kwa moja.” Ni dini zipi hizo?
Dini kubwa zaidi ilikuwa Kanisa Katoliki la Ugiriki la Ukrainia, ambalo sasa laitwa Kanisa Katoliki la Ukrainia. Lilikuwa na wafuasi wapatao 4,000,000. Kulingana na kichapo The Sword and the Shield, “maaskofu wanane kati ya maaskofu wake kumi, na maelfu ya makasisi na waumini, walikufa katika kambi za kazi ngumu huko Siberia kwa sababu ya imani yao.” Shirika la KGB lilichukia pia makanisa ya Kiprotestanti yasiyosajiliwa, ambayo pia hayakudhibitiwa na Serikali. Mwishoni mwa miaka ya 1950, shirika la KGB lilikadiria kwamba vikundi hivyo vya Kiprotestanti vilikuwa na jumla ya washiriki 100,000.
Shirika la KGB liliwaona Mashahidi wa Yehova kuwa kikundi cha Kiprotestanti, kilichokadiriwa kuwa na washiriki wapatao 20,000 katika Muungano wa Sovieti mnamo mwaka wa 1968. Mashahidi walikuwa wachache sana mwanzoni mwa Vita ya Ulimwengu ya Pili mwaka wa 1939. Hawakujulikana sana. Lakini hali ilibadilika sana wakati maelfu ya Mashahidi walipotokea ghafula katika Muungano wa Sovieti. Hilo lilitukiaje?
Mwanzo wa Ongezeko Kubwa
Walter Kolarz ataja sababu mbili za ongezeko hilo kubwa katika kitabu chake Religion in the Soviet Union, kilichochapishwa mwaka wa 1961. Alisema sababu moja ni kwamba “maeneo yaliyotwaliwa na Muungano wa Sovieti mwaka wa 1939-1940”—Latvia, Lithuania, Estonia, na Moldavia—yalikuwa na “vikundi [vingi] vyenye bidii vya Mashahidi wa Yehova.” Isitoshe, Muungano wa Sovieti ulitwaa maeneo fulani mashariki mwa Poland na Chekoslovakia, yaliyokuwa na Mashahidi zaidi ya elfu moja, na kuyafanya kuwa sehemu ya Ukrainia. Kwa hivyo, Mashahidi hao wote walihamishwa ghafula hadi kwenye Muungano wa Sovieti.
Jambo jingine lililochangia ongezeko zaidi, “amini usiamini,” akaandika Kolarz, lilikuwa “kambi za mateso za Ujerumani.” Wanazi waliwatia gerezani maelfu ya Mashahidi kwa sababu ya kukataa kumwunga mkono Hitler na harakati zake za vita. Kolarz alieleza kwamba wafungwa Warusi waliokuwa kwenye kambi hizo “walivutiwa na ujasiri na ushikamanifu wa ‘Mashahidi’ na huenda hilo liliwafanya wapendezwe na mafundisho yao.” Tokeo ni kwamba vijana wengi Warusi waliokuwa kwenye kambi hizo walirejea kwenye Muungano wa Sovieti wakiwa wamemwamini Yehova Mungu na makusudi yake mazuri kwa dunia.—Zaburi 37:29; Ufunuo 21:3, 4.
Sababu hizo zilichangia kuongezeka kasi kwa maelfu ya Mashahidi katika Muungano wa Sovieti. Kufikia mapema mwaka wa 1946, kulikuwa na Mashahidi wapatao 1,600, nao walizidi 8,000 mwishoni mwa miaka ya 1940. Wapelelezi wa KGB walihofia ongezeko hilo, na kama ilivyotajwa awali, walihangaishwa hasa na “shughuli za Wakristo ambao hawakuwa chini ya udhibiti wao.”
Mashambulizi Yaanzishwa
Punde si punde serikali ya Sovieti ilianza kuwashambulia Mashahidi waliokuwa wakihubiri kwa bidii katika Muungano wa Sovieti. Huko Estonia mashambulizi yalianza mwezi wa Agosti mwaka wa 1948 wakati wasimamizi watano wa kazi hiyo walipokamatwa na kufungwa gerezani. “Muda si muda ikawa dhahiri kwamba wapelelezi wa KGB walinuia kuwakamata Mashahidi wote,” akasema Lembit Toom, Shahidi wa Estonia. Mashahidi wote katika Muungano wa Sovieti walikabili hali hiyohiyo.
Viongozi wa Sovieti waliwataja Mashahidi kuwa wahalifu wabaya sana na kwamba wao ni tisho kwa Serikali ya Sovieti isiyoamini kuwapo kwa Mungu. Kwa hiyo, walisakwa kila mahali, wakakamatwa, na kufungwa gerezani. Kichapo The Sword and the Shield kilisema hivi: “Wasiwasi mkubwa ambao maofisa wakuu wa KGB walikuwa nao kuelekea Mashahidi wa Yehova unaonyesha waziwazi jinsi walivyowachukia watu waliokuwa na maoni tofauti.”
Wasiwasi wao ulidhihirishwa wakati waliposhambulia Mashahidi mnamo mwezi wa Aprili 1951. Miaka miwili tu iliyopita, mnamo mwaka wa 1999, Profesa Sergei Ivanenko, msomi Mrusi anayeheshimiwa, alisema katika kitabu chake The People Who Are Never Without Their Bibles kwamba mapema mwezi wa Aprili 1951, “familia zaidi ya 5,000 za Mashahidi wa Yehova kutoka jamhuri za Sovieti za Ukrainia, Belorusia, Moldavia, na Baltiki zilihamishwa hadi ‘makao ya kudumu’ huko Siberia, Mashariki ya Mbali, na Kazakhstan.”
Tukio Linalostahili Kukumbukwa
Hebu wazia jitihada zilizohusika katika shambulizi hilo—kukusanya maelfu ya familia za Mashahidi kutoka kwenye eneo kubwa hivyo kwa siku moja tu? Wazia kukusanya mamia, ama maelfu ya watu, ili wafanye kazi ya kutambulisha Mashahidi, kisha kuvamia ghafula nyumba zao zote usiku mmoja. Halafu, kulikuwa na kazi ya kupakia watu kwenye mikokoteni, magari yanayokokotwa na wanyama, na magari mengine. Kisha kuwapeleka kwenye vituo vya magari ya moshi, na kuwapakia kwenye mabehewa ya mizigo.
Fikiria pia mateso yao. Je, waweza kuwazia pia jinsi walivyolazimishwa kusafiri kwa maelfu ya kilometa—kwa muda wa majuma matatu au zaidi, huku wakiwa kwenye mabehewa machafu, yaliyosongamana watu ambayo hayakuwa na vyoo ila ndoo ya kujisaidia tu? Jaribu kuwazia ukiachwa tu kwenye nyika ya Siberia. Nawe wafahamu kwamba si rahisi kuishi kwenye mazingira hayo magumu.
Mwezi huu ni ukumbusho wa miaka 50 tangu kuhamishwa kwa Mashahidi wa Yehova mnamo Aprili mwaka wa 1951. Masimulizi ya wale waliookoka ambayo yamerekodiwa kwenye ukanda wa vidio yanaonyesha jinsi walivyodumisha uaminifu licha ya kuteswa kwa miaka mingi. Masimulizi hayo yaonyesha kwamba jitihada za kuzuia watu kumwabudu Mungu haziwezi kufaulu. Hata Wakristo wa karne ya kwanza hawakuacha licha ya vizuizi.
Matokeo ya Uhamisho Huo
Serikali ya Sovieti iligundua upesi kwamba kuzuia Mashahidi kumwabudu Yehova hakukuwa kazi rahisi kama ilivyodhaniwa. Bila kujali malalamiko makali ya askari, Mashahidi walimwimbia Yehova sifa walipokuwa wakipelekwa uhamishoni. Waliangika ishara zilizosema hivi kwenye mabehewa yaliyowabeba: “Mashahidi wa Yehova Garini.” Shahidi mmoja alieleza hivi: “Tulipokuwa njiani tulikutana na magari mengine ya moshi vituoni, yaliyobeba wahamishwa, nasi tuliona ishara zilizoangikwa kwenye mabehewa.” Tulitiwa moyo kama nini!
Kwa hiyo badala ya kuvunjika moyo, wale waliokuwa wakihamishwa walidhihirisha roho kama ya mitume wa Yesu. Biblia yasema kwamba baada ya kupigwa viboko na kuagizwa wakome kuhubiri, ‘waliendelea bila kuacha kufundisha na kutangaza habari njema juu ya Kristo.’ (Matendo 5:40-42) Kwa kweli, ni kama Kolarz alivyosema kuhusu uhamisho huo, “haukuwa mwisho wa ‘Mashahidi’ nchini Urusi, ila ulikuwa mwanzo tu wa kazi yao ya kuwahubiria wengi. Hata walijaribu kuwahubiria watu vituoni wakiwa njiani kuelekea uhamishoni.”
Mashahidi walipowasili sehemu mbalimbali, walisifiwa kuwa wafanyakazi watiifu na wenye bidii. Lakini, kama mitume wa Kristo, ni kana kwamba waliwaambia wale waliowanyanyasa: ‘Hatuwezi kukoma kusema juu ya Mungu wetu.’ (Matendo 4:20) Wengi walisikiliza mafundisho ya Mashahidi na kujiunga nao kumtumikia Mungu.
Kolarz aeleza matokeo: “Serikali ya Sovieti ilipowahamisha ilisaidia sana kusambazwa kwa dini yao. ‘Mashahidi’ walihamishwa kutoka kwenye vijiji vyao vilivyojitenga [katika jamhuri za magharibi mwa Sovieti] na kupelekwa sehemu mbalimbali zenye watu wengi, kwenye kambi za mateso au za kazi ngumu.”
Jitihada za Kukabiliana na Ongezeko
Viongozi wa Sovieti walijaribu mbinu mbalimbali ili kukomesha kazi ya Mashahidi wa Yehova. Walianzisha mpango madhubuti wa kueneza habari za uwongo kuhusu Mashahidi, kwa kuwa mnyanyaso mkali haukufaulu. Walitumia vitabu, filamu, na vipindi vya redio. Wapelelezi waliozoezwa wa KGB walijiunga na makutaniko kisirisiri.
Habari za uwongo zilizoenezwa kote ziliwafanya watu wengi wahofu na kutowaamini Mashahidi bila sababu, hilo lathibitishwa na makala moja katika kitabu Reader’s Digest cha Agosti 1982, Chapa ya Kanada. Makala hiyo iliandikwa na Vladimir Bukovsky, Mrusi aliyeruhusiwa kuhamia Uingereza mwaka wa 1976. Aliandika hivi: “Jioni moja niliona ubao kwenye jengo moja jijini London uliotangaza hivi: MASHAHIDI WA YEHOVA . . . Sikuweza kuendelea kusoma, nilipigwa na bumbuazi na kushtuka sana.”
Vladimir aeleza kilichomfanya ahofu: “Haya ndiyo madhehebu ambayo wenye mamlaka nchini mwetu huita mahayawani katili ili kuwaogopesha watoto . . . Katika Muungano wa Sovieti, ‘Mashahidi’ wako gerezani na kwenye kambi za mateso tu. Na sasa nilisimama mbele ya jengo na kutazama ubao wenye jina lao. Je, kweli mtu yeyote angeweza kuwatembelea tu kirafiki?” akauliza. Ili kukazia sababu iliyomfanya ahofu, Vladimir alimalizia kwa kusema hivi: “‘Mashahidi’ wanasakwa sana katika nchi yetu kama vile wahuni wa Mafia wanavyosakwa Uingereza, nao hawaeleweki hata kidogo.”
Lakini Mashahidi walivumilia na kuongezeka sana licha ya mnyanyaso mkali na uenezaji wa habari za uwongo kuwahusu. Vitabu vya Sovieti kama vile The Truths About Jehovah’s Witnesses, kilichochapishwa kwa nakala 100,000 za Kirusi, katika mwaka wa 1978, kilidokeza kwamba habari za uwongo zinazokashifu Mashahidi zinahitaji kuenezwa kwa mapana na marefu. Mtungaji wa kitabu hicho, V. V. Konik, ambaye alieleza jinsi Mashahidi walivyokuwa wakihubiri wajapozuiwa, alishauri hivi: “Wasovieti wanaochunguza dini wanapaswa kubuni njia bora zaidi za kukomesha mafundisho ya mashahidi wa Yehova.”
Mbona Wakawa Shabaha ya Mashambulizi?
Kwa ufupi, Mashahidi wa Yehova walikuwa shabaha kuu ya mashambulizi ya Sovieti kwa sababu waliwaiga wafuasi wa mapema wa Yesu. Katika karne ya kwanza, mitume waliagizwa ‘wasifulize kufundisha juu ya msingi wa jina [la Yesu].’ Hata hivyo, wale waliowashtaki walilalamika hivi baadaye: “Tazameni! mmejaza Yerusalemu fundisho lenu.” Mitume hawakukana kwamba walikuwa wakihubiri wajapokatazwa, badala yake walijibu hivi kwa heshima: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”—Matendo 5:27-29.
Mashahidi wa Yehova leo huchukua kwa uzito agizo ambalo Yesu aliwapa wafuasi wake la ‘kuwahubiria watu na kutoa ushahidi kamili.’ (Matendo 10:42) Katika kitabu chake The Kremlin’s Human Dilemma, Maurice Hindus alieleza kwamba Mashahidi “walichukiwa na Moscow na kuendelea kusakwa na polisi wa Sovieti” kwa sababu “hasa ya bidii yao ya kueneza evanjeli bila kukoma.” Akaongezea hivi: “Hawawezi kukomeshwa. Wanapogandamizwa mahali fulani, wanaibuka kwingineko.”
“Nijuavyo ni kwamba,” akaandika mwanahistoria Mrusi Sergei Ivanenko, “Mashahidi wa Yehova ndiyo dini pekee katika Muungano wa Sovieti iliyopata ongezeko la watu licha ya marufuku na mnyanyaso.” Bila shaka, dini nyingine pia ziliendelea kuwapo, kutia ndani Kanisa Othodoksi la Urusi lililokuwa mashuhuri zaidi ya zote. Utapendezwa kujua jinsi makanisa mengine na Mashahidi walivyoweza kustahimili mashambulizi ya Sovieti.
[Picha katika ukurasa wa 6]
“Dini Iliyonyanyaswa Vikali Zaidi”
Kichapo A Concise Encyclopaedia of Russia cha mwaka wa 1964 kilisema kwamba Mashahidi wa Yehova “walieneza imani yao kwa bidii.” Ndiyo “dini iliyonyanyaswa vikali zaidi katika Muungano wa Sovieti.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
FAMILIA MOJA KATI YA MAELFU—Fyodor Kalin Asimulia Kuhamishwa kwa Familia Yao
Familia yetu iliishi katika kijiji cha Vilshanitsa, magharibi mwa Ukrainia. Alfajiri na mapema Aprili 8, 1951, maofisa waliokuwa na mbwa walikuja na kutuamsha sote. Walituambia kuwa serikali ya Moscow iliamuru tuhamishwe hadi Siberia. Lakini hatungehamishwa endapo tungetia sahihi hati iliyosema kwamba sisi si Mashahidi wa Yehova tena. Familia yetu yenye watu saba, wazazi wangu na ndugu zangu, tuliazimia kwamba hatutakana imani yetu. Nilikuwa na umri wa miaka 19 wakati huo.
Ofisa mmoja alisema hivi: “Bebeni maharagwe, mahindi, unga, vyakula vilivyohifadhiwa, na kabichi—la sivyo, watoto wenu watakula nini?” Tuliruhusiwa pia kuchinja kuku kadhaa na nguruwe na kubeba nyama hiyo. Vigari viwili vya kukokotwa na farasi vililetwa, na kila kitu kikapakiwa ndani yake na kupelekwa mji wa Hriplin. Huko tulijazwa kwenye behewa la mizigo watu 40 au 50 hivi, na mlango ukafungwa.
Behewa hilo lilikuwa na mbao chache za kulalia—hazikutosha kila mtu. Kulikuwa pia na jiko lenye makaa na kuni. Tulipika kwa jiko hilo, na kutumia vifaa vya kupikia tulivyobeba. Lakini hakukuwa na choo—tulitumia ndoo tu. Kisha tulitoboa shimo sakafuni, na kuitia ndoo shimoni, halafu tukaizingira kwa mablanketi kwa ajili ya faragha.
Tulisongamana sana kwenye behewa hilo na kusafiri polepole kwa maelfu ya kilometa na kuelekea tusikojua. Mwanzoni, tulivunjika moyo kidogo. Lakini tulipata shangwe tulipoimba pamoja nyimbo za Ufalme kwa shauku sana kiasi cha kupoteza sauti. Kamanda wa jeshi alifungua mlango na kutuamrisha tunyamaze, lakini hatukuacha kuimba hadi mwisho wa wimbo. Tuliposimama kwenye vituo njiani, wengi walikuja kujua kwamba ni Mashahidi wa Yehova waliokuwa wakihamishwa. Hatimaye, baada ya kusafiri kwa siku 17 au 18 tukiwa behewani, tulishushwa Siberia karibu na Ziwa Baikal.
[Picha]
Nimesimama mstari wa nyuma, kulia
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
ARMAGEDDON Filamu ya Sovieti Iliyoeneza Uwongo
Serikali ya Sovieti ilitayarisha filamu ya Armageddon ili kuharibu sifa ya Mashahidi wa Yehova. Ilikuwa hadithi ya kubuniwa ya mapenzi kati ya mvulana mmoja wa jeshi la Sovieti na msichana aliyeshawishiwa kuwa Shahidi. Mwishoni mwa filamu hiyo, dada mchanga wa msichana huyo alikufa katika aksidenti iliyosababishwa na mwangalizi mmoja Shahidi, ambaye alionyeshwa kuwa kibaraka wa shirika la upelelezi la Marekani.
Gazeti The Red Flag la Ukrainia la Mei 14, 1963 lilisema hivi kuhusu filamu hiyo iliyowaudhi watu: “Hivyo ndivyo wale wasiomwamini Mungu wanavyoeneza kwa matokeo habari za uwongo zinazosadikisha. Filamu hiyo inaweza kuonyeshwa katika vijiji vingine nchini.”
[Picha katika ukurasa wa 6]
Maelfu walisafirishwa kwa mabehewa ya mizigo hadi Siberia
-
-
Jinsi Dini Ilivyookoka MashambuliziAmkeni!—2001 | Aprili 22
-
-
Jinsi Dini Ilivyookoka Mashambulizi
KABLA ya Ujerumani ya Nazi kuvamia Urusi mnamo Juni 1941, serikali ya Sovieti ilikuwa karibu kukomesha Kanisa Othodoksi la Urusi. Lakini baada ya uvamizi wa Wanazi, serikali ya Sovieti ilianza kubadili maoni yake kuelekea dini. Mbona ikabadili maoni?
Richard Overy, profesa wa historia ya kisasa katika King’s College, London, alieleza sababu katika kitabu chake Russia’s War—Blood Upon the Snow: “Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Sergei [Sergius], aliwasihi waumini siku hiyohiyo ya uvamizi wajitoe mhanga ili kushinda Ujerumani. Miaka miwili iliyofuata alichapisha angalau barua ishirini na tatu, na kuwaomba waumini wote wapambane kwa ajili ya serikali yao isiyomwamini Mungu.” Kwa hiyo, kama Overy alivyoendelea kusema, ‘Stalin aliruhusu dini isitawi tena.’
Hatimaye, Stalin aliidhinisha Kanisa Othodoksi mwaka wa 1943 alipomteua Sergius kuwa kiongozi mpya wa kanisa hilo. “Viongozi wa Kanisa hilo waliitikia kwa kuchanga pesa kutoka kwa waumini kwa ajili ya kikosi cha magari ya vita cha Sovieti,” akasema Overy. “Makasisi na maaskofu walisihi makundi yao yamtii Mungu na Stalin.”
Mrusi Sergei Ivanenko ambaye ni msomi wa dini aliandika hivi kuhusu kipindi hicho katika historia ya Urusi: ‘Kichapo rasmi cha Kanisa Othodoksi la Urusi cha The Journal of the Moscow Patriarchate, kilimsifu Stalin kuwa kiongozi na mwalimu mkuu zaidi ya wote duniani, aliyetumwa na Mungu ili kuokoa taifa hilo na uonevu, wamiliki wa mashamba, na mabepari. Kiliwasihi waumini wapigane kufa na kupona ili kulinda Muungano wa Sovieti na adui zake na kusitawisha Ukomunisti kwa hali na mali.’
“Kanisa Lilithaminiwa Sana na KGB”
Kanisa Othodoksi liliwasaidia sana Wakomunisti hata baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili kukoma mwaka wa 1945. Kichapo The Soviet Union: The Fifty Years, kilichohaririwa na Harrison Salisbury, kilieleza jinsi ilivyokuwa: “Baada ya vita kukoma, viongozi wa kanisa waliunga mkono madai ya Stalin kuhusu sera ya nchi za kigeni wakati wa Vita Baridi.”
Kitabu kilichoandikwa hivi karibuni cha The Sword and the Shield chaeleza jinsi viongozi wa kanisa walivyoendeleza masilahi ya Sovieti. Chaeleza kwamba Kiongozi wa Kanisa Alexis wa Kwanza, aliyechukua cheo cha Sergius mwaka wa 1945, “alijiunga na Baraza la Kuleta Amani Duniani, chama cha Sovieti kilichoanzishwa mwaka wa 1949.” Kitabu hicho pia chasema kwamba yeye pamoja na Askofu Mkuu Nikolai “walithaminiwa sana na wapelelezi wa KGB [Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti] kuwa watu waliosaidia serikali kutekeleza malengo yake.”
Jambo la ajabu ni kwamba mwaka wa 1955, Kiongozi wa Kanisa, Alexis wa Kwanza alitangaza hivi: “Kanisa Othodoksi la Urusi linaunga mkono kikamili sera ya amani ya serikali yetu, si kwa sababu Kanisa halina uhuru, bali kwa sababu sera ya Sovieti ni ya haki na inapatana na mafundisho ya Kikristo yanayohubiriwa na Kanisa.”
Katika toleo la Januari 22, 2000, la gazeti The Guardian la London, Uingereza, kasisi mpinzani wa Othodoksi Georgi Edelshtein alisema: “Maaskofu wote waliteuliwa kwa uangalifu ili waweze kushirikiana na serikali ya sovieti. Wote walikuwa wapelelezi wa KGB. Inajulikana kote kwamba Kiongozi wa Kanisa Alexy aliyeajiriwa na shirika la KGB, alibandikwa jina la siri la Drozdov. Leo, maaskofu hao wana siasa zilezile walizokuwa nazo miaka 20 au 30 iliyopita.”
Watumishi wa Serikali ya Sovieti
Kuhusu uhusiano kati ya Kanisa Othodoksi na Serikali ya Sovieti, gazeti Life la Septemba 14, 1959, lilisema hivi: “Kanisa lilimwona Stalin kama kiongozi kwa sababu lilipata mapendeleo fulani. Kuna wizara maalumu ya serikali inayodumisha ushirikiano na Kanisa Othodoksi. Wakomunisti wametumia kanisa tangu wakati huo kuwa chombo cha serikali ya Sovieti.”
Matthew Spinka, mtaalamu wa masuala ya kanisa nchini Urusi, alikiri katika kitabu chake The Church in Soviet Russia cha mwaka wa 1956 kuwa kuna ushirikiano wa karibu kati ya Kanisa na Serikali. Aliandika kwamba “Kiongozi wa Kanisa aliyepo sasa, Alexei, amefanya Kanisa kuwa chombo cha serikali.” Kwa hivyo, Kanisa Othodoksi liliokoka kwa sababu lilitumikia Serikali. ‘Lakini kuna ubaya gani?’ huenda ukauliza. Fikiria maoni ya Mungu na ya Kristo kuhusu jambo hilo.
Yesu Kristo alisema hivi kuhusu wanafunzi wake wa kweli: “Nyinyi si sehemu ya ulimwengu, bali nimewachagua nyinyi kutoka ulimwenguni.” Na Neno la Mungu lauliza hivi waziwazi: “Wanawake wazinzi, je, hamjui kwamba urafiki na ulimwengu ni uadui na Mungu?” (Yohana 15:19; Yakobo 4:4) Kwa hivyo, kulingana na Biblia, kanisa lilijifanya kuwa kahaba wa kidini ambaye “wafalme wa dunia walifanya uasherati naye.” Limejithibitisha kuwa sehemu ya yule anayeitwa na Biblia “Babiloni Mkubwa, mama wa makahaba na wa mambo yenye kuchukiza sana ya dunia.”—Ufunuo 17:1-6.
Jinsi Mashahidi Walivyookoka Mashambulizi
Kinyume cha hilo, Yesu Kristo alisema jinsi ambavyo wafuasi wake wa kweli wangetambuliwa: “Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.” (Yohana 13:35) Upendo huo uliwasaidia sana Mashahidi kuokoka mashambulizi katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti, kama ionyeshwavyo na ripoti ifuatayo katika kichapo The Sword and the Shield. “Mashahidi wa Yehova wanawasaidia wafuasi wa dini yao walio katika kambi za [kazi ngumu] au waliohamishwa, wanawapa pesa, chakula na mavazi.”
Wale waliokuwa kwenye kambi za gereza walipewa “chakula” cha kiroho pia—Biblia na vichapo vya Biblia. Biblia ina ‘matamko ya Mungu,’ ambayo Yesu alisema yanahitajiwa ili kuendeleza uhai wetu wa kiroho. (Mathayo 4:4) Watu walijihatarisha sana ili kuingiza vichapo kisiri kwenye kambi hizo, kwani mtu yeyote aliyeshikwa akifanya hivyo aliadhibiwa vikali.
Helene Celmina, mwenyeji wa Latvia, alifungwa katika kambi ya watumwa ya Potma nchini Urusi kuanzia mwaka wa 1962 hadi 1966. Aliandika kitabu kiitwacho Women in Soviet Prisons, na kueleza hivi: “Mashahidi wengi wa Yehova wanaadhibiwa vifungo vya miaka kumi ya kazi ngumu kwa sababu tu ya kupatikana na magazeti machache ya Mnara wa Mlinzi katika nyumba zao. Si ajabu kwamba wasimamizi wanahangaika na kuudhika sana kupata vichapo hivyo kambini, kwa kuwa watu hushikwa na kufungwa wakiwa na vichapo hivyo.”
Bila shaka, kuhatarisha uhuru wa kibinafsi na uhai ili kuandaa msaada wa kiroho kulithibitisha upendo wa Kikristo! Mbali na jambo hilo, kuna jambo jingine muhimu sana lililowasaidia Mashahidi kuokoka. “Hakuna mtu awaye yote,” akasema Helene Celmina, “aliyeweza kuelewa jinsi vichapo vilivyopigwa marufuku vilivyoingizwa kwenye kambi hizo zenye ulinzi mkali ambamo watu hawakuruhusiwa kuwasiliana.” Hilo lilionekana kuwa jambo lisilowezekana, kwa kuwa kila mtu aliyeingia gerezani alipekuliwa sana. “Ni kana kwamba malaika walivileta vichapo hivyo wakati wa usiku,” akaandika mwandishi huyo.
Kwa kweli, Mungu aliahidi kwamba hangewaacha watu wake. Kwa hiyo Mashahidi wa Yehova katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti wanakiri hivi kama mtunga-zaburi wa Biblia: “Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia.” (Zaburi 54:4; Yoshua 1:5) Kwa kweli, msaada huo uliwasaidia sana Mashahidi kuokoka mnyanyaso katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti!
Hali Zilivyobadilika
Katika Machi 27, 1991, tengenezo la Mashahidi wa Yehova lilisajiliwa katika Muungano wa Sovieti. Lilisajiliwa baada ya kutiwa sahihi kwa hati ya kisheria iliyotangaza hivi: “Kusudi la Tengenezo hili la Kidini ni kuendesha kazi ya kidini ya kujulisha jina la Yehova Mungu na maandalizi yake ya upendo kwa wanadamu kupitia Ufalme wake wa kimbingu unaoongozwa na Yesu Kristo.”
Baadhi ya njia za kuendesha kazi hiyo ya kidini zinazotajwa na hati hiyo ni kuhubiri hadharani na kuzuru watu nyumbani, kuwafundisha wale wanaotaka kusikiliza kweli za Biblia, kuongoza mafunzo ya Biblia bila malipo kwa msaada wa vichapo vya kujifunzia Biblia, na kusambaza Biblia.
Miaka kumi imepita tangu kutiwa sahihi kwa hati hiyo. Na Muungano wa Sovieti umevunjika, hali ya dini imebadilika sana katika jamhuri 15 za ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Dini nchini Urusi na kote ulimwenguni zitapatwa na nini?
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Ushirikiano wa Kanisa na Sovieti
Edmund Stevens aliandika hivi katika kitabu chake Russia Is No Riddle cha mwaka wa 1945: “Kanisa lilitahadhari sana kutopinga mhisani wake. Kanisa lilitambua kabisa kwamba Serikali ilitarajia liunge mkono utawala wa Sovieti na kutii sheria zake baada ya kupewa mapendeleo.”
Stevens aliendelea kueleza hivi: “Ilikuwa rahisi sana kwa Kanisa Othodoksi kushirikiana na Serikali ya Sovieti kwa sababu kwa karne nyingi Kanisa Othodoksi lilikuwa dini rasmi ya Kitaifa.”
Taasisi ya Keston ilichunguza kindani ushirikiano kati ya Wasovieti na Alexis wa Pili, ambaye ni kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Urusi leo. Ripoti yake ilimalizia hivi: “Ushirikiano wa Aleksi haushangazi kwani karibu viongozi wa dini zote zilizosajiliwa—kutia ndani Wakatoliki, Wabaptisti, Waadventisti, Waislamu na Wabudha—walikuwa vibaraka wa KGB. Hata, ripoti ya kila mwaka inayoeleza ushirikiano wa Aleksi na KGB inataja pia vibaraka wengine wengi, baadhi yao walikuwa viongozi wa Kanisa la Kilutheri la Estonia.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]
Kuhubiri Kambini
Viktors Kalnins, mwandishi wa habari Mlatvia, aliyefungwa kwa miaka kumi (1962-1972) aliishi muda mrefu wa kifungo hicho katika kambi kuu ya Mordovia, iliyokuwa kilometa 400 hivi kusini-mashariki ya Moscow. Kalnins aliulizwa hivi na mwandishi wa Amkeni! aliyekuwa akimhoji mwezi wa Machi 1979: “Je, Mashahidi walio kifungoni wanajua mambo ambayo Mashahidi wengine wanafanya nchini Marekani au katika nchi nyinginezo?”
“Wanajua,” akajibu Kalnins, “kupitia vichapo wanavyopokea. . . . Hata walinionyesha magazeti yao. Sikujua kamwe walikoficha vichapo hivyo. Walivificha mahali mbalimbali. Lakini kila mtu alijua kwamba kulikuwako vichapo kambini. . . . Mashahidi wa Yehova walijaribu kuficha vichapo daima nao walinzi walivitafuta daima!”
Kalnins alipoulizwa “Je, Mashahidi wa Yehova walijaribu kuzungumza nawe kuhusu mafundisho yao?” alijibu hivi: “Bila shaka! Mafundisho yao yanajulikana sana. Tunajua habari zote kuhusu Har-Magedoni . . . Walisema sana kuhusu mwisho wa magonjwa.”
[Picha]
Mashahidi katika kambi za Mordovia waliendelea kufundisha kweli za Biblia kwa ujasiri
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Vovchuk na mkewe walihamishwa hadi Irkutsk, Siberia, mwaka wa 1951 nao wangali Wakristo waaminifu leo
[Picha katika ukurasa wa 10]
Stalin aliruhusu dini kusitawi kwa muda kwa sababu kanisa lilimwunga mkono wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili
[Hisani]
U.S. Army photo
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kiongozi wa Kanisa Alexis wa Kwanza (1945-1970) alisema hivi: ‘Sera ya Sovieti yapatana na mafundisho ya Kikristo ambayo yanahubiriwa na Kanisa’
[Hisani]
Central State Archive regarding the film/photo/phono documents of Saint-Petersburg
-