-
Kusema kwa Njia Inayoeleweka WaziFaidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
-
-
SOMO LA 2
Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi
NI SHARTI useme kwa njia inayoeleweka ili watu wakuelewe vizuri. Huenda ikawa unataka kusema jambo linalopendeza, au hata muhimu sana, lakini ni kazi bure kulisema ikiwa maneno yako hayaeleweki kwa urahisi.
Watu hawachochewi na maneno ambayo hawaelewi vizuri. Hata kama una sauti kubwa inayosikika vizuri, lakini kama maneno yako si wazi, wengine hawatachochewa kutenda. Ni kana kwamba unaongea lugha ya kigeni ambayo haieleweki. (Yer. 5:15) Biblia inatukumbusha hivi: “Tarumbeta ikivuma wito usio dhahiri, nani atajitayarisha kwa ajili ya pigano? Katika njia hiyohiyo pia, nyinyi msipotamka usemi wenye kueleweka kwa urahisi kupitia hiyo lugha, linalosemwa litajulikanaje? Kwa kweli, mtakuwa mkisema hewani tu.”—1 Kor. 14:8, 9.
Ni Nini Ambacho Hufanya Usemi Usiwe Dhahiri? Huenda ikawa tatizo ni kutofumbua kinywa vizuri. Ikiwa misuli ya utaya haitaki kusogea na ikiwa midomo haifumbuki vizuri, maneno yanaweza kukosa kuwa dhahiri.
Pia inaweza kuwa vigumu kueleweka ikiwa unaongea haraka-haraka. Hiyo ni kama kuweka kaseti yenye mazungumzo icheze haraka kuliko inavyokusudiwa. Maneno yanasemwa, lakini hayafaidi.
Katika hali nyingine, maneno yasiyo dhahiri husababishwa na kasoro katika viungo vya usemi. Lakini hata wale ambao wamelazimika kukabili tatizo hilo wanaweza kutumia madokezo ya somo hili ili kujitahidi kuboresha usemi wao.
Hata hivyo, mara nyingi maneno yasiyo dhahiri husababishwa na hali ya kusema upesi hivi kwamba inakuwa vigumu kueleweka. Huenda tatizo likawa kuruka silabi fulani au kuruka herufi muhimu au kutotamka herufi za mwisho za maneno. Mtu anapoongea upesi, wale wanaomsikiliza wanaweza kushika tu maneno fulani lakini watakisia tu maneno mengine. Kwa hiyo, kutosema maneno yanayoeleweka wazi kunaweza kufanya ufundishaji wako usiwe na matokeo.
Jinsi ya Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi. Jambo moja ambalo litakusaidia kusema maneno yanayoeleweka wazi ni kufahamu muundo wa maneno ya lugha yenu. Katika lugha nyingi, maneno hufanyizwa kwa silabi. Silabi ni herufi moja au zaidi zinazotamkwa pamoja. Katika lugha kama hizo, kila silabi hutamkwa unapoongea, ingawa silabi zote hazitamkwi kwa mkazo uleule. Ikiwa unataka kusema kwa njia inayoeleweka wazi, punguza mwendo wako wa kusema na ujitahidi sana kutamka kila silabi. Mwanzoni, huenda ikaonekana unakazia sana kila neno kupita kiasi, lakini ukiendelea kufanya mazoezi, hatua kwa hatua utarudia kuzungumza kwa mfuatano wa kawaida. Ufasaha unaweza kufanya uzungumze upesi, lakini tunapaswa kuepuka kufanya hivyo ikiwa kuna uwezekano wa maneno mengine kutoeleweka wazi.
Lakini tahadhari: Ili uzoee kusema kwa njia inayoeleweka, unaweza kufanya mazoezi ya kusema na kusoma kwa kutaja kila neno kwa hususa kabisa. Lakini usiache hiyo iwe njia yako ya kawaida ya kusema. Itaonekana kana kwamba huongei kwa njia ya kawaida na unajifanya.
Ikiwa husemi kwa njia inayosikika wazi, jifunze kuinua kichwa chako ili kidevu chako kisiwe karibu na kifua chako. Unaposoma Biblia, uiinue juu kwa kiasi cha kwamba utainua kichwa kidogo tu kuwatazama wasikilizaji. Hiyo itafanya maneno yako yatokee bila kuzuiwa.
Pia, kujifunza kutulia kunaweza kuboresha usemi wako. Inajulikana kwamba mkazo kwenye misuli ya uso au kwenye misuli inayoongoza jinsi unavyopumua unaweza kuathiri usemi wako. Mkazo kama huo huzuia upatano uliopo kati ya akili, viungo vya usemi, na jinsi unavyopumua. Kwa kawaida kuna upatano mzuri sana kati ya viungo hivyo.
Misuli ya utaya inahitaji kulegea ili ubongo uweze kuiongoza kwa urahisi. Pia midomo inapasa kutulia. Midomo inapaswa kuwa tayari kupanuka na kujifinya haraka ili iweze kutokeza vizuri sauti nyingi zinazotoka kinywani na kooni. Ikiwa utaya na midomo zina mkazo, kinywa hakitafumbuka vizuri, na sauti italazimishwa kupitia meno. Hiyo itatokeza sauti yenye kukwaruza isiyosikika wazi. Lakini kutuliza utaya na midomo hakumaanishi kwamba tuwe wazembe katika usemi wetu. Tunapaswa kusawazisha jambo hilo na kusema maneno kwa njia inayoeleweka wazi.
Unapojichunguza kuhusiana na jambo hili, ingefaa usome kwa sauti. Chunguza kwa makini jinsi unavyotumia viungo vyako vizuri ajabu vya usemi. Je, wewe hufumbua midomo yako wazi ili sauti iweze kutoka bila kuzuiliwa? Kumbuka kwamba mbali na ulimi kuna viungo vingine pia vinavyohusiana na usemi, hata ingawa ulimi ni mojawapo ya viungo vya usemi vyenye utendaji zaidi. Shingo, utaya wa chini, midomo, misuli ya uso, na misuli ya koo, zote zinachangia usemi. Wakati unapoongea, je, huonekana kana kwamba uso wako hausongi? Ikiwa ndivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba husemi kwa njia inayoeleweka wazi.
Kama una ukanda wa kunasa sauti, rekodi sauti yako unapoongea kama kawaida, kama ambavyo ungezungumza na mtu katika huduma ya shambani. Rekodi mazungumzo yako kwa dakika kadhaa. Ukisikiliza sauti yako uliyorekodi, utaweza kuona tatizo lolote ambalo unaweza kuwa nalo la kutosema maneno fulani kwa njia inayoeleweka wazi. Kwa mfano, sikiliza pindi ambazo umesema haraka mno, au pindi ambazo umekosa kutamka maneno wazi, au pindi ambazo umekata-kata maneno, na ujaribu kutambua kwa nini unafanya hivyo. Mara nyingi unaweza kurekebisha udhaifu huo kwa kufuata madokezo ambayo yametajwa hapo juu.
Je, una tatizo fulani la usemi? Jizoeze kufumbua kinywa chako zaidi kidogo kuliko jinsi ambavyo umekuwa ukifanya na ujaribu kutaja kila neno kwa hususa zaidi. Vuta pumzi, kisha uzungumze polepole. Kufanya hivyo kumewezesha wengi wenye matatizo ya kusema waseme kwa njia inayoeleweka zaidi. Kama huwezi kutamka vizuri s na z, jaribu kuvuta ulimi wako mbali na meno yako ya mbele unapozitamka. Hata ingawa huenda hiyo isiwe suluhisho kabisa, usikate tamaa. Kumbuka kwamba ijapokuwa labda Musa alikuwa na tatizo la usemi, Yehova alimchagua atangaze ujumbe muhimu kwa Waisraeli na pia Farao wa Misri. (Kut. 4:10-12) Ukitaka, atakutumia pia, na atakubariki upate mafanikio katika huduma yako.
-
-
Matamshi MazuriFaidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
-
-
SOMO LA 3
Matamshi Mazuri
SI WAKRISTO wote wamesoma sana elimu ya kilimwengu. Hata mtume Petro na mtume Yohana walitajwa kuwa “watu wasio na elimu na wa kawaida tu.” (Mdo. 4:13) Lakini, ni muhimu kuepuka kukengeusha akili za watu kutoka kwenye kweli ya Biblia kwa kutamka maneno vibaya.
Mambo ya Kufikiria. Hakuna kanuni fulani hususa za matamshi zinazoweza kutumiwa na lugha zote. Lugha nyingi huandikwa kwa herufi za alfabeti. Mbali na alfabeti ya Kilatini, kuna alfabeti za Kiarabu, Kiebrania, Kigiriki, na Kirusi. Kichina huandikwa kwa herufi zenye sehemu kadhaa badala ya alfabeti. Kwa kawaida herufi hizo husimamia neno au sehemu ya neno. Ingawa Kijapani na Kikorea zinatumia herufi za Kichina, herufi zao hutamkwa kwa njia tofauti kabisa na huenda hata zisiwe na maana moja.
Katika lugha zinazotumia alfabeti, matamshi mazuri humaanisha kutaja kila herufi au herufi kadhaa kwa sauti inayotakikana. Ikiwa lugha kama hiyo ina kanuni za wazi za kufuata, kama vile Kigiriki, Kihispania, na Kizulu, haiwi vigumu kutamka maneno vizuri. Lakini, maneno ya lugha za kigeni yanaweza kuingiza katika lugha nyingine matamshi ya lugha hizo za kigeni. Basi, inakuwa kwamba kila herufi au herufi kadhaa zinaweza kutamkwa kwa njia nyingi au nyakati nyingine hata zisitamkwe kamwe. Huenda ikawa lazima kukumbuka matamshi kama hayo na kuyatumia mara nyingi unapoongea. Katika Kichina ni lazima mtu akariri moyoni matamshi ya maelfu ya herufi. Katika lugha nyinginezo, ubadilifu wa sauti hubadili maana ya neno. Mtu anaweza kueleweka vibaya asipozingatia jambo hilo.
Ikiwa lugha fulani imefanyizwa kwa silabi, ni vizuri kuweka mkazo unaotakikana kwenye silabi inayofaa. Lugha nyingi za aina hiyo zina njia za kawaida za kutia mkazo. Kama neno linapaswa kutamkwa kwa njia tofauti, alama ya matamshi inaweza kuwekwa kwenye neno hilo. Hiyo hufanya iwe rahisi kutamka maneno. Lakini, inakuwa vigumu kutamka maneno kama hakuna utaratibu maalumu wa kufuata. Katika hali kama hizo ni lazima ukariri moyoni jinsi ya kutamka kila neno vizuri.
Kuna lugha ambazo hutumia sana alama za matamshi. Baadhi ya alama hizo huonyeshwa juu ya herufi au chini yake. Ufuatao ni mfano wa herufi zenye alama za matamshi: ā, ō, é, ù, ĩ, ũ, ḥ, ị, ụ. Nyakati nyingine alama hizi za matamshi huandikwa na nyakati nyingine haziandikwi na katika hali hiyo msomaji mwenyewe huzitia kulingana na muktadha wa neno analosoma. Ikiwa alama za matamshi hazijaonyeshwa, msomaji anahitaji kujitayarisha vizuri sana ikiwa ana mgawo wa kusoma mbele ya watu.
Kuna mambo yanayohusu matamshi ambayo tunapaswa kuepuka. Kutamka maneno kupita kiasi kunaweza kufanya ionekane unajifanya, au hata kujionyesha. Ndivyo ilivyo na kutumia matamshi ambayo kwa ujumla hayatumiwi tena. Msemaji atakuwa akijielekezea tu fikira akifanya hivyo. Kwa upande mwingine, tusipite kiasi kwa kuongea na kutamka maneno kwa uzembe. Baadhi ya mambo hayo tayari yametajwa katika somo lenye kichwa “Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi.”
Maneno fulani ya lugha moja yanaweza kutamkwa tofauti katika nchi tofauti-tofauti, au hata yatamkwe tofauti katika sehemu mbalimbali za nchi ileile moja. Mtu wa nchi nyingine anaweza kusema lugha ileile moja kwa matamshi tofauti. Kamusi zinaweza kuorodhesha njia mbalimbali zinazokubalika za kutamka neno. Ikiwa mtu hakupata elimu ya kilimwengu au lugha anayosema si yake ya asili, anaweza kufaidika sana akiwasikiliza kwa makini wale wanaozungumza lugha hiyo vizuri na kujaribu kutamka maneno jinsi wanavyotamka. Sisi Mashahidi wa Yehova tunataka kuzungumza kwa njia inayotukuza ujumbe wetu na kwa njia ambayo watu katika eneo letu wanatuelewa kwa urahisi.
Katika mazungumzo ya kawaida, inafaa kutumia maneno ambayo unafahamu vizuri. Kwa kawaida matamshi huwa si tatizo unapozungumza. Lakini, unaposoma kwa sauti unaweza kupata maneno ambayo kwa kawaida hutumii katika mazungumzo yako. Na Mashahidi wa Yehova husoma sana kwa sauti. Sisi husomea watu Biblia tunapohubiri. Ndugu wengine hupewa migawo ya kusoma mafungu wakati wa Funzo la Mnara wa Mlinzi au kwenye Funzo la Kitabu la Kutaniko. Ni muhimu tusome kwa usahihi na tusikengeushe akili za watu kutoka kwenye ujumbe huo kwa kutamka maneno vibaya.
Je, unashindwa kutamka majina fulani katika Biblia? Katika Kiswahili, kwa ujumla ni silabi ya pili kutoka mwisho ndiyo inapaswa kutamkwa kwa mkazo.
Njia za Kufanya Maendeleo. Watu wengi hawajui kwamba wana tatizo la matamshi. Mwangalizi wa shule akikutajia mambo fulani kuhusu matamshi ambayo unahitaji kurekebisha, thamini fadhili yake. Baada ya kutambua tatizo, unawezaje kufanya maendeleo?
Kwanza, unapokuwa na mgawo wa kusoma kwa sauti, chunguza kamusi ikiwa kamusi za lugha yenu zina miongozo ya jinsi ya kutamka maneno. Tafuta maneno usiyoyafahamu. Kama hujazoea kutumia kamusi, fungua kurasa za kwanza zenye maelezo kuhusu alama zinazotumika katika kamusi hiyo, au mwombe mtu akufafanulie alama hizo. Kamusi za lugha nyinginezo huonyesha jinsi ya kutamka maneno. Kamusi hizo huonyesha sauti unazopaswa kutumia unapotamka vokali fulani na konsonanti fulani. Nyakati nyingine kuna maneno ambayo yanaweza kutamkwa kwa njia tofauti-tofauti ikitegemea muktadha. Rudia kutaja kwa sauti mara kadhaa neno lile unalolitafuta kabla ya kufunga kamusi.
Njia ya pili inayoweza kuboresha matamshi yako ni kusoma mbele ya mtu mwingine, mtu ambaye hutamka maneno vizuri, na umwambie akukosoe unapokosea.
Njia ya tatu ya kuboresha matamshi ni kusikiliza kwa makini wasemaji wazuri. Ikiwa kuna kaseti za vichapo vyetu, zitumie. Unaposikiliza, chunguza maneno yanayotamkwa kwa njia tofauti na jinsi ambavyo wewe ungeyatamka. Uyaandike kisha ufanye mazoezi ya kuyatamka. Baada ya muda, hutakuwa ukitamka maneno vibaya, na hiyo itakusaidia sana uwe msemaji bora.
-