-
Wokovu na Kushangilia Chini ya Utawala wa MesiyaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
13. (a) Isaya atoa wazo gani lenye kuchangamsha moyo? (b) Twajuaje kwamba amani anayoifafanua Isaya yahusisha mambo mengi kuliko tu usalama kutokana na wanyama wa mwituni?
13 Sasa Isaya atoa wazo lenye kusisimua moyo kuhusu hali ambazo Mungu ataleta nchini humo. Asema: “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA [“Yehova,” “NW”], kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Isaya 11:6-9) Je, maneno hayo hayachangamshi moyo? Ona kwamba amani inayofafanuliwa hapo hutokana na kumjua Yehova. Basi, yanayohusika ni mengi kuliko tu usalama kutokana na wanyama wa mwituni. Kumjua Yehova hakutabadili wanyama, bali kutabadili watu. Waisraeli hawatahitaji kuogopa wanyama wa mwituni wala wanadamu walio kama wanyama wakiwa safarini wala wakiwa katika nchi yao iliyorudishwa.—Ezra 8:21, 22; Isaya 35:8-10; 65:25.
14. Ni upi ulio utimizo mkubwa zaidi wa Isaya 11:6-9?
14 Hata hivyo, unabii huo una utimizo mkubwa zaidi. Yesu, Mesiya, alitawazwa kwenye Mlima Sayuni wa mbinguni mwaka wa 1914. Mwaka wa 1919, waliobaki wa “Israeli wa Mungu” waliachiliwa kutoka katika utekwa wa Babiloni nao wakashiriki katika kurudisha ibada ya kweli. (Wagalatia 6:16) Tokeo lilikuwa kufunguliwa kwa njia kwa ajili ya utimizo wa kisasa wa unabii wa Isaya uhusuo Paradiso. “Ujuzi sahihi,” yaani ujuzi juu ya Yehova, umebadili nyutu za watu. (Wakolosai 3:9, 10) Watu waliokuwa wajeuri hapo awali wamekuwa wenye amani. (Waroma 12:2; Waefeso 4:17-24) Matukio hayo sasa yameathiri mamilioni ya watu kwa sababu unabii wa Isaya umekuja kuhusisha Wakristo wanaoongezeka haraka, walio na tumaini la uhai duniani. (Zaburi 37:29; Isaya 60:22) Hao wamejizoeza kutazamia wakati ambapo dunia yote itarudishwa kuwa paradiso salama, yenye amani, kulingana na kusudi la awali la Mungu.—Mathayo 6:9, 10; 2 Petro 3:13.
-
-
Wokovu na Kushangilia Chini ya Utawala wa MesiyaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
Ibada Safi Yarudishwa Kupitia Mesiya
16. Ni nini kilichokuwa ishara kwa watu wa Mungu mwaka wa 537 K.W.K.?
16 Ibada safi ilishambuliwa kwa mara ya kwanza katika Edeni Shetani alipofaulu kushawishi Adamu na Hawa wasimtii Yehova. Hadi leo hii, Shetani hajaacha lengo lake la kugeuzia mbali watu wengi iwezekanavyo kutoka kwa Mungu. Lakini Yehova hataruhusu kamwe ibada safi itoweke duniani. Jina lake lahusika, naye huwajali wale wanaomtumikia. Basi, kupitia Isaya, atoa ahadi maarufu: “Itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.” (Isaya 11:10) Mwaka wa 537 K.W.K., Yerusalemu, jiji ambalo Daudi alikuwa amelifanya kuwa jiji kuu la taifa, lilikuwa ishara, likiwaita mabaki waaminifu wa Wayahudi waliotawanywa warudi na kujenga hekalu upya.
17. Yesu ‘aliinukaje ili kutawala mataifa’ katika karne ya kwanza na leo pia?
17 Hata hivyo, unabii huo huelekeza kwenye mambo mengi kuliko hayo. Kama tulivyoona, huo huelekeza kwenye utawala wa Mesiya, Kiongozi pekee wa kweli wa watu wa mataifa yote. Mtume Paulo alinukuu Isaya 11:10 ili kuonyesha kuwa watu wa mataifa katika siku yake wangepata nafasi katika kutaniko la Kikristo. Akinukuu tafsiri ya Septuagint juu ya mstari huo, aliandika: “Isaya asema: ‘Kutakuwa na mzizi wa Yese, na kutakuwa na mmoja ambaye anainuka ili kutawala mataifa; juu yake mataifa yataweka tumaini lao.’” (Waroma 15:12) Mbali na hayo, unabii huo hufika mbali hata zaidi—kufikia siku yetu wakati ambapo watu wa mataifa waonyesha upendo wao kwa Yehova kwa kuunga mkono ndugu watiwa-mafuta wa Mesiya.—Isaya 61:5-9; Mathayo 25:31-40.
18. Yesu amekuwaje mahali pa kukusanyika katika siku yetu?
18 Katika utimizo wa leo, “siku hiyo” anayoirejezea Isaya ilianza Mesiya alipotawazwa kuwa Mfalme wa Ufalme wa mbinguni wa Mungu mwaka wa 1914. (Luka 21:10; 2 Timotheo 3:1-5; Ufunuo 12:10) Tangu wakati huo, Yesu Kristo amekuwa ishara dhahiri, mahali pa kukusanyika, kwa Israeli wa kiroho na kwa watu wa mataifa yote wanaotamani serikali yenye uadilifu. Chini ya mwelekezo wa Mesiya, habari njema ya Ufalme imefikishwa kwa mataifa yote, kama alivyotabiri Yesu. (Mathayo 24:14; Marko 13:10) Hiyo habari njema ina matokeo makubwa. “Umati mkubwa, ambao hakuna mtu [awezaye] kuuhesabu” unamtii Mesiya kwa kujiunga na mabaki watiwa-mafuta katika ibada safi. (Ufunuo 7:9) Watu wengi wapya waendeleapo kujiunga na mabaki katika “nyumba ya sala” ya Yehova ya kiroho, wao huongeza kwenye utukufu wa ‘mahali pa kupumzikia’ pa Mesiya, hekalu kubwa la kiroho la Mungu.—Isaya 56:7; Hagai 2:7.
Watu Walioungana Wamtumikia Yehova
19. Ni katika pindi gani mbili Yehova arudisha mabaki ya watu wake waliotawanyika duniani kote?
19 Kisha Isaya awakumbusha Waisraeli kuwa wakati fulani Yehova aliwaandalia wokovu, adui mwenye nguvu alipolikandamiza taifa hilo. Sehemu hiyo ya historia ya Israeli—Yehova kulikomboa taifa hilo kutoka utekwani Misri—yathaminiwa sana na Wayahudi wote waaminifu. Isaya aandika: “Itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari. Naye atawatwekea mataifa bendera [“atawainulia mataifa ishara,” “NW”], atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia.” (Isaya 11:11, 12) Huku akiwa kana kwamba anawashika mkono, Yehova ataongoza mabaki waaminifu wa Israeli na wa Yuda pia kutoka katika mataifa ambamo wametawanyika naye atawaleta salama nyumbani. Hilo latukia kwa kadiri ndogo mwaka wa 537 K.W.K. Lakini utimizo mkuu ni wenye utukufu kama nini! Mwaka wa 1914, Yehova alimwinua Yesu Kristo aliyetawazwa kuwa ‘ishara kwa mataifa.’ Kuanzia mwaka wa 1919, waliobaki wa “Israeli wa Mungu” walianza kumiminika kwenye ishara hiyo, wakiwa na hamu ya kushiriki katika ibada safi chini ya Ufalme wa Mungu. Taifa hilo la pekee la kiroho latoka katika “kila kabila na ulimi na watu na taifa.”—Ufunuo 5:9.
20. Watu wa Mungu watafurahia mwungano gani baada ya kurudi kutoka Babiloni?
20 Isaya sasa afafanua mwungano wa taifa lililorudishwa. Akirejezea ufalme wa kaskazini kuwa Efraimu na ufalme wa kusini kuwa Yuda, asema: “Wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu. Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii.” (Isaya 11:13, 14) Wayahudi warudipo kutoka Babiloni, hawatagawanyika tena kuwa mataifa mawili. Washiriki kutoka kwa makabila yote ya Israeli watarudi nchini mwao kwa mwungano. (Ezra 6:17) Hawataoneana uchungu wala kuchukiana. Wakiwa watu walioungana, watasimama kwa ushindi dhidi ya adui zao walio katika mataifa yanayowazingira.
21. Mwungano wa watu wa Mungu leo unatokezaje kwelikweli?
21 Jambo lenye kuvutia hata zaidi ni ule mwungano wa “Israeli wa Mungu.” Yale makabila 12 ya mfano ya Israeli wa kiroho, yamefurahia mwungano unaotegemea upendo kwa Mungu na kwa ndugu na dada zao wa kiroho kwa karibu miaka 2,000. (Wakolosai 3:14; Ufunuo 7:4-8) Leo, watu wa Yehova—Waisraeli wa kiroho na pia wale walio na tumaini la uhai duniani—hufurahia amani na mwungano wa ulimwenguni kote chini ya utawala wa Mesiya, hali ambazo hazipatikani kamwe katika makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Kwa pamoja, Mashahidi wa Yehova hukabiliana na jitihada za Shetani za kuingilia ibada yao. Wakiwa kikundi kimoja cha watu, wao hutekeleza utume wa Yesu wa kuhubiri na kufundisha habari njema ya Ufalme wa Mesiya katika mataifa yote.—Mathayo 28:19, 20.
Vizuizi Vitashindwa
22. Yehova ‘atauangamizaje ulimi wa bahari ya Misri’ na ‘kutikisa mkono wake juu ya Mto’?
22 Kuna vizuizi vingi, halisi na vya kitamathali, vinavyozuia kurudi kwa Waisraeli kutoka uhamishoni. Vitashindwaje? Isaya asema: “BWANA atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu.” (Isaya 11:15) Yehova ndiye atakayeondoa vikwazo vyote vinavyozuia watu wake kurudi. Hata vizuizi vyenye nguvu sana kama ulimi wa Bahari Nyekundu (kama vile Ghuba ya Suez) au visivyopitika kama vile Mto Frati ulio mkubwa, vitakaushwa kitamathali ili mtu avuke bila kuvua viatu vyake!
23. Kutakuwaje ‘njia kuu kutoka Ashuru’?
23 Katika siku ya Musa, Yehova alitayarishia Israeli njia ya kuponyoka kutoka Misri na kusafiri hadi Bara Lililoahidiwa. Sasa yeye atafanya jambo fulani linalofanana na hilo: “Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.” (Isaya 11:16) Yehova atawaongoza wahamishwa wanaorudi kama watu wanaotembea kwenye njia kuu kutoka mahali pao pa uhamisho hadi nchini mwao. Wapinzani watajaribu kuwazuia, lakini Mungu wao, Yehova, atakuwa pamoja nao. Vivyo hivyo leo, Wakristo watiwa-mafuta na waandamani wao hushambuliwa vikali, lakini wao husonga mbele kwa ujasiri! Wametoka katika Ashuru ya kisasa, ulimwengu wa Shetani, nao husaidia wengine watoke humo. Wanajua kuwa ibada safi itafanikiwa nayo itasitawi. Hiyo si kazi ya mwanadamu, bali ya Mungu.
-