-
Mkazo—“Muuaji wa Kichinichini”Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
Mkazo—“Muuaji wa Kichinichini”
“Dalili ya kwanza niliyoona ilikuwa msongo mkubwa sana. Msongo huo ulianzia karibu na mfupa wangu wa kidari; ukaenea haraka kwenye mabega yangu, shingo, na taya; na kuenea haraka tena kwenye mikono yangu yote miwili. Nilihisi kana kwamba tembo alikuwa amerukaruka kwenye kifua changu. Karibu nishindwe kupumua. Nikaanza kutoka jasho. Nilianza kushikwa na mipindo ya matumbo na kisha kichefuchefu kibaya sana. . . . Baadaye, wauguzi walipokuwa wakisaidia kuniweka kitandani katika hospitali, nakumbuka nikisema kwa mshangao, ‘Ninapatwa na mshiko wa moyo.’ Nilikuwa na umri wa miaka arobaini na nne.”
HIVYO ndivyo Dakt. Robert S. Eliot afafanuavyo jinsi alivyonusurika kifo zaidi ya miaka 20 iliyopita katika kitabu chake From Stress to Strength. Mapema asubuhi hiyo alikuwa amehudhuria mkutano mmoja na alikuwa ametoa hotuba—na kwa kushangaza, ilikuwa juu ya habari ya mishiko ya moyo. Kwa ghafula, Dakt. Eliot, ambaye ni mtaalamu wa moyo, alijikuta akiwa ndiye “mgonjwa katika chumba cha utunzaji cha matatizo ya moyo.” Anasema ni nini kilichochangia tatizo lake ambalo halikutazamiwa? “Ndani ya mwili,” asema Dakt. Eliot, “jinsi nilivyokuwa nikiitikia mkazo ilikuwa ikiniua.”a
Kama ambavyo mambo ya Dakt. Eliot yanavyoonyesha, mkazo waweza kutokeza hali zenye kutisha uhai. Kwa kweli, nchini Marekani, umehusianishwa na baadhi ya visababishi vikubwa zaidi vya kifo. Matokeo ya mkazo yaweza kuongezeka bila kutambuliwa katika kipindi fulani cha wakati kisha yatokee kwa ghafula. Kwa hiyo, ni kwa sababu nzuri kwamba mkazo umeitwa “muuaji wa kichinichini.”
Kwa kushangaza, si watu wenye utu wa aina-ya-A pekee—wale wenye tabia ya kukosa subira, wachokozi, na wenye makabiliano—wanaoweza kupatwa na misiba yenye kuhusiana na mkazo. Wale ambao huonekana kuwa na nyutu za upole waweza pia kuwa hatarini, hasa ikiwa utulivu wao ni wa kijuujuu tu, kama kifuniko kisichofungwa vizuri ambacho kimefunika jiko la mvuke. Dakt. Eliot ahisi kwamba hivyo ndivyo hali yake ilivyokuwa. Sasa, yeye awaonya wengine: “Unaweza kufa leo—bila kujua kwamba kwa miaka mingi mkazo umekuwa ukingojea kulipuka kama bomu lililotegwa.”
Lakini mshiko wa moyo na kifo cha ghafula si matatizo ya pekee yanayohusiana na mkazo, kama vile makala ifuatayo itakavyoonyesha.
-
-
Mkazo—“Muuaji wa Kichinichini”Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
[Maelezo ya Chini]
a Ingawa mkazo unaweza kuwa mojawapo ya mambo yenye kuchangia, katika visa vingi vya mshiko wa moyo, huwa kuna madhara makubwa katika ateri za moyo ambayo hutokezwa na mrundamano wa vitu vyenye mafuta-mafuta katika ateri. Kwa hiyo, si jambo la hekima kwa mtu kuchukua dalili za maradhi ya moyo kijuujuu tu, labda akiamini kwamba kupunguza tu mkazo kutamponyesha. Ona Amkeni!, Desemba 8, 1996, ukurasa wa 3-13.
-
-
Mkazo—“Sumu Inayodhuru Polepole”Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
Mkazo—“Sumu Inayodhuru Polepole”
“Sikuzote sisi husikia watu wakisema, ‘Usishindwe na mkazo usije ukawa mgonjwa.’ Labda hawatambui kwamba kuna ukweli uliothibitishwa kibiolojia juu ya jambo hilo.”—Dakt. David Felten.
JILL, ambaye ni mama aliye mzazi mmoja mwenye mvulana tineja, na ambaye akaunti yake ya benki ilikuwa inapungua, na pia alikuwa na uhusiano mbaya na wazazi wake, tayari alikuwa na sababu nyingi za kuhisi mkazo sana. Kisha, kwa ghafula vipele vyenye kuwasha vikatokea katika mkono wake. Alijaribu dawa za viuavijasumu, dawa za kupaka za cortisone, na dawa za mizio, lakini hizo dawa zote hazikumsaidia. Badala yake, vipele hivyo vikaenea kotekote mwilini mwa Jill, kutia ndani uso wake. Mkazo ulikuwa ukimfadhaisha kwelikweli.
Jill alirejezewa aende kwenye kliniki inayochunguza hali ya kihisia-moyo ya wagonjwa wake. “Tunajaribu kutafuta mambo yanayoendelea katika maisha zao,” asema Dakt. Thomas Gragg, mmojawapo wa waanzilishi wa kliniki hiyo. Mara nyingi yeye hupata kwamba kwa kuongezea kuhitaji utunzaji wa kitiba, watu wenye matatizo yenye kudumu ya ngozi huhitaji msaada wa kukabili mkazo. “Ni rahisi kusema kwamba jinsi unavyohisi au kutenda husababisha maradhi ya ngozi,” akiri Dakt. Gragg. “Lakini twaweza kusema kwamba hali ya mtu ya kihisia-moyo yaweza kuchangia sana kutokea kwa matatizo ya ngozi, na hatupaswi kudumu kuandika tu dawa za kupaka za steroidi bila pia kumsaidia mtu kuondoa mkazo alio nao maishani mwake.”
Jill ahisi kwamba kujifunza kudhibiti mkazo hasa kuliokoa ngozi yake. “Bado mimi hupatwa na matatizo hayo kwa ghafula-ghafula,” yeye asema, “lakini ngozi yangu si mbaya kama ilivyokuwa awali.” Je, hicho ni kisa cha kipekee? La hasha. Madaktari wengi huamini kwamba mara nyingi mkazo huchangia matatizo kadhaa ya ngozi, kutia ndani mabaka ya ngozi, psoriasis, chunusi, na mibambuko. Lakini mkazo waweza kuathiri zaidi ya ngozi yako tu.
Mkazo na Mfumo Wako wa Kinga
Utafiti wa wakati huu waonyesha kwamba mkazo waweza kudhoofisha mfumo wako wa kinga, labda ukisababisha ushikwe na maradhi kadhaa ya kuambukiza. “Mkazo haukufanyi uwe mgonjwa,” asema mtaalamu wa virusi Ronald Glaser. “Lakini unakuongezea hatari ya kushikwa na ugonjwa kwa sababu ya kile mkazo unachofanyia kinga ya mwili wako.” Kuna uthibitisho wa kutosha unaohusianisha mkazo na mafua, homa, na malengelenge. Ingawa nyakati zote sisi huweza kupatwa na virusi kama hivyo, kwa kawaida mfumo wetu wa kinga huendelea kupigana navyo. Lakini wataalamu fulani wasema kwamba mtu anapokuwa na mfadhaiko wa kihisia-moyo, kinga hizo zaweza kushindwa.
Taratibu za kibiolojia zinazohusika bado hazijafahamika vizuri, lakini wengine husema kwamba homoni ambazo hukuchochea unapokuwa na mkazo zaweza kudhibiti utendaji wa kinga yako zinapopitia mkondo wa damu. Mara nyingi, hilo si jambo la kuhangaisha mtu, kwa kuwa homoni hizi ni za muda tu. Hata hivyo, wengine husema kwamba ikiwa mtu ana mkazo ambao unaendelea na ambao ni mkali sana, mfumo wake wa kinga waweza kudhoofika kiasi cha kwamba yeye aweza kushikwa na magonjwa kwa urahisi.
Hilo laweza kusaidia kujua sababu inayofanya madaktari wa Kanada wakadirie kwamba asilimia 50 hadi 70 ya wagonjwa wanaokuja kuona daktari huwa na malalamishi yanayohusiana na mkazo, mara nyingi walikuwa na maumivu ya kichwa, wenye ukosefu wa usingizi, wakiwa wachovu, na wenye matatizo ya tumbo. Nchini Marekani, idadi hiyo inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 75 na 90. Dakt. Jean King ahisi kwamba hatilii chumvi asemapo: “Mkazo wa daima ni kama sumu inayodhuru polepole.”
Si Kisababishi cha Pekee cha Maradhi Wala Si Tiba ya Pekee
Japo mambo ambayo yametajwa, wanasayansi hawana hakika kama mkazo pekee waweza kuathiri mfumo wa kinga kwa kiasi cha kumfanya mtu awe mgonjwa. Kwa hiyo, haiwezi kusisitizwa kwamba kila mtu ambaye ana mkazo, hata ule wa kudumu zaidi, atashikwa na maradhi. Vilevile, haiwezi kusemwa kwamba ukikosa mkazo ni lazima utakuwa na afya bora, wala si jambo la hekima kukataa kutibiwa kwa kuamini wazo lisilo la kweli kwamba ugonjwa utapotea ikiwa wewe una matazamio mazuri na maoni chanya. Dakt. Daniel Goleman atahadharisha hivi: “Tokeo la kuwa na wazo lionekanalo kuwa lenye kuvutia la kwamba mtazamo wa mtu waweza kutibu ugonjwa wowote limesababisha mvurugo na kuchanganyikiwa ambako kumeenea sana kuhusu kadiri ambavyo ugonjwa waweza kuathiri akili, na, labda kwa ubaya zaidi, jinsi nyakati nyingine inavyofanya watu wahisi kuwa na hatia kwa kuwa wana maradhi, kana kwamba kuwa na maradhi ni ishara ya ukosefu fulani wa adili au kutofaa kiroho.”
Kwa hiyo, ni lazima itambulike kwamba kisababishi cha ugonjwa mara nyingi hakiwezi kuonwa kuwa jambo moja tu. Lakini, bado uhusiano uliopo kati ya mkazo na ugonjwa wakazia hekima ya kujifunza jinsi ya kuondoa “sumu inayodhuru polepole” wakati wowote iwezekanapo.
Kabla ya kufikiria jinsi ambavyo hilo laweza kufanywa, ebu tuchunguze kwa makini zaidi hali ya mkazo na jinsi unavyoweza kukunufaisha katika visa fulani.
-
-
Mkazo—“Sumu Inayodhuru Polepole”Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Magonjwa Fulani Ambayo Yamehusianishwa na Mkazo
• mizio
• yabisi-kavu
• ugonjwa wa pumu
• maumivu ya mgongo, shingo, na mabega
• mafua
• mshuko wa moyo
• kuhara
• homa
• matatizo ya tumbo
• maumivu ya kichwa
• matatizo ya moyo
• ukosefu wa usingizi
• maumivu ya kichwa ya kipandauso
• vidonda vya tumbo
• matatizo katika kufanya ngono
• matatizo ya ngozi
-
-
Mkazo Mzuri, Mkazo MbayaAmkeni!—1998 | Machi 22
-
-
Mkazo Mzuri, Mkazo Mbaya
“Kwa kuwa mkazo ni itikio la mwili lisilo hususa kwa mahitaji yoyote, kila mtu ana mkazo wa kadiri fulani nyakati zote.”—Dakt. Hans Selye.
ILI mcheza zeze aweze kutokeza muziki, ni lazima kamba kwenye chombo chake ziwe na mkazo—lakini kwa kadiri fulani tu. Kamba zikiwa na mkazo mno, zitakatika. Lakini kamba zikiwa legelege mno, hazitatokeza sauti kamwe. Mkazo ufaao upo mahali fulani katikati ya sehemu hizo mbili.
Ndivyo ilivyo na mkazo. Mkazo mwingi mno unaweza kudhuru, kama ambavyo tayari tumeona. Lakini namna gani kama hatuna mkazo kamwe? Ingawa tazamio hilo laweza kuonekana kuwa zuri, kwa kweli unahitaji mkazo—angalau kwa kadiri fulani. Kwa kielelezo, ebu wazia kwamba unapovuka barabara, kwa ghafula unaona gari likikuelekea kwa kasi. Ni mkazo unaokuwezesha kuepuka kujeruhiwa—haraka!
Lakini mkazo hausaidii katika hali za dharura pekee. Pia unahitaji mkazo ili utimize kazi zako za kila siku. Kila mtu ana mkazo wa kadiri fulani nyakati zote. ‘Njia ya pekee ya kuepuka mkazo ni kufa,’ asema Dakt. Hans Selye. Yeye aongezea kwamba ule usemi “ana mkazo” haumaanishi chochote kama ambavyo usemi “ana joto” usivyomaanisha chochote. “Tumaanishalo hasa na semi kama hizo,” asema Selye, “ni mkazo au joto la mwili la kupita kiasi.” Katika muktadha huu tafrija pia inahusisha mkazo, na ndivyo ilivyo na usingizi, kwa kuwa ni lazima moyo wako uendelee kupiga na mapafu yako yaendelee kufanya kazi.
Aina Tatu za Mikazo
Kama vile kulivyo na viwango mbalimbali vya mkazo, pia kuna aina mbalimbali za mkazo.
Mkazo mkali hutokana na mikazo ya maisha ya kila siku. Mara nyingi, hiyo huhusisha hali zisizopendeza ambazo zinahitaji kutatuliwa. Kwa kuwa hizo ni hali ambazo hutukia tu bila kutarajiwa na pia ni za muda tu, kwa kawaida mkazo huo waweza kudhibitiwa. Bila shaka, kuna wengine ambao hupata tatizo moja baada ya jingine—kwa kweli, utu wao huonekana kama umejaa mvurugo. Hata kiwango hiki cha mkazo mkali chaweza kudhibitiwa. Lakini, mwenye mkazo aweza kukinza hali za kubadili maisha yake, mpaka anapotambua matokeo ambayo mtindo-maisha wake wenye fujofujo humletea yeye na wale walio karibu naye.
Ingawa mkazo mkali ni wa muda tu, mkazo wa kudumu ni wa muda mrefu. Mwenye mkazo haoni njia ya kuondoa hali inayomletea mkazo, uwe ni ole wa umaskini au huzuni ya kufanya kazi inayodharauliwa—au kukosa kazi. Mkazo wa kudumu pia waweza kutokana na matatizo ya familia ambayo yanadumu. Kumtunza mtu wa ukoo asiyejiweza kwaweza kutokeza mkazo vilevile. Hata uwe unasababishwa na nini, mkazo wa kudumu hudhoofisha mtu siku baada ya siku, juma baada ya juma, mwezi baada ya mwezi. “Jambo baya zaidi kuhusu mkazo wa kudumu ni kwamba watu huuzoea,” chasema kitabu kimoja juu ya habari hiyo. “Watu hutambua mara moja mkazo mkali kwa sababu ni jambo jipya linalowapata; wao hupuuza mkazo wa kudumu kwa sababu ni jambo la zamani, ambalo wamelizoea, na, nyakati nyingi, hauwasumbui.”
Mkazo unaotokana na mfadhaiko ni athari ya msiba mkubwa, kama vile kubakwa, aksidenti, au msiba wa kiasili. Mashujaa wengi wa vita na waokokaji wa kambi za mateso hupatwa na mkazo wa aina hii. Dalili za mkazo unaotokana na mfadhaiko zaweza kutia ndani kumbukumbu zilizo dhahiri kabisa juu ya kisa kilichotokeza mfadhaiko huo, hata baada ya miaka mingi, pamoja na kuzidi kuwa mnyetivu kwa matukio madogo-madogo. Nyakati nyingine mwenye mkazo hupatikana kuwa anaugua hali iitwayo tatizo la mkazo unaotokana na mfadhaiko wa kisa kibaya kilichotokea (PTSD).—Ona sanduku juu.
Kuwa Mnyetivu kwa Mkazo
Wengine husema kwamba jinsi tunavyoitikia mkazo kwa wakati huu hutegemea sana kadiri ya mkazo na aina ya mkazo ambao tumepata kuwa nao katika wakati uliopita. Wao husema kwamba visa vibaya vyenye kuleta mfadhaiko vyaweza hasa kubadili “njia” ya kemikali ya itikio katika ubongo, ikimfanya mtu awe mnyetivu zaidi kwa mkazo katika wakati ujao. Kwa kielelezo, katika uchunguzi uliofanyiwa mashujaa 556 wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, Dakt. Lawrence Brass alipata kwamba wale ambao walikuwa wafungwa wa vita walikuwa na uwezekano wa mara nane wa kupatwa na mshiko wa moyo kuliko wale ambao hawakupata kuwa wafungwa wa vita—hata baada ya miaka 50 ya kisa cha kwanza cha mfadhaiko. “Ule mkazo anaopata mtu kwa kuwa mfungwa wa vita ulikuwa mkali sana hivi kwamba ulibadili jinsi watu hawa walivyoitikia mkazo katika wakati ujao—uliwafanya wawe wanyetivu kwa mkazo.”
Matukio yenye kuleta mkazo yaliyoonwa katika umri wa utoto hayapasi kupuuzwa, wataalamu wasema, kwa kuwa hayo yaweza kuwa na athari kubwa sana. “Watoto wengi wenye mfadhaiko hawapelekwi kutibiwa,” asema Dakt. Jean King. “Wao hupitia tatizo hilo, na kuendeleza maisha zao, na hatimaye kuja kutuona miaka mingi baadaye, wakiugua mshuko wa moyo au maradhi ya moyo.” Kwa kielelezo, fikiria, mfadhaiko wa kupoteza mzazi. “Mkazo wa kadiri hiyo unaotukia ukiwa ungali mchanga waweza kubadili njia ya itikio la ubongo,” asema Dakt. King, “ukifanya ubongo usiwe na uwezo sana wa kudhibiti mkazo wa kawaida, ambao hutukia kila siku.”
Bila shaka, jinsi mtu anavyoitikia mkazo inaweza kutegemea mambo mengine vilevile, kutia ndani hali yake ya kimwili na misaada mingi awezayo kupata ya kumsaidia kukabiliana na matukio yenye kuleta mkazo. Lakini, hata uwe umesababishwa na nini, mkazo unaweza kudhibitiwa. Kwa kweli, hilo si jambo rahisi. Dakt. Rachel Yehuda aonelea: “Kumwambia mtu ambaye amekuwa mnyetivu kwa mkazo kwamba atulie tu ni kama kumwambia mtu mwenye tatizo la kukosa usingizi alale tu usingizi.” Hata hivyo, kuna mengi ambayo mtu aweza kufanya ili kupunguza mkazo, kama vile makala ifuatayo itakavyoonyesha.
-
-
Mkazo Mzuri, Mkazo MbayaAmkeni!—1998 | Machi 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Mkazo Unaotokana na Kazi—“Tukio la Tufeni Pote”
Ripoti ya Umoja wa Mataifa yasema: “Mkazo umekuwa mojawapo ya masuala mazito zaidi ya kiafya katika karne ya 20.” Kuwapo kwa mkazo kazini ni dhahiri sana.
• Idadi ya madai yanayohusiana na mkazo yaliyofanywa na wafanyakazi wa serikali nchini Australia imeongezeka kwa asilimia 90 katika kipindi cha miaka mitatu tu.
• Uchunguzi uliofanywa nchini Ufaransa ulifunua kwamba asilimia 64 ya wauguzi na asilimia 61 ya walimu husema kwamba wao wamekasirika kuhusu mazingira yenye kusababisha mkazo ambamo wao hufanyia kazi.
• Magonjwa yanayohusiana na mkazo hugharimu Marekani karibu dola bilioni 200 kila mwaka. Inafikiriwa kwamba asilimia zipatazo 75 hadi 85 kati ya aksidenti zote za kiviwanda zimehusiana na mkazo.
• Katika nchi baada ya nchi, wanawake walipatikana kuwa wanaugua kutokana na mkazo kuliko wanaume, yaelekea kwa sababu wao hufanya kazi nyingi zaidi nyumbani na kazini.
Kwa hakika, mkazo wa kazi ni “tukio la tufeni pote,” kama inavyotajwa na ripoti moja ya UM.
-
-
Mkazo Mzuri, Mkazo MbayaAmkeni!—1998 | Machi 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
PTSD—Itikio la Kawaida kwa Tukio Lisilo la Kawaida
‘Miezi mitatu baada ya gari letu kupata aksidenti, bado nilishindwa kuacha kulia, au kulala usiku. Hata kuondoka nyumbani kuliniogofya sana.’—Louise.
LOUISE augua kutokana na mkazo unaotokana na mfadhaiko wa kisa kibaya kilichotokea (PTSD), ambao ni ugonjwa wenye kudhoofisha unaojulikana kwa kumbukumbu zenye kujirudia-rudia au ndoto za tukio lenye kutokeza mfadhaiko. Mtu mwenye PTSD pia aweza kuwa mwenye kushtuka kupita kiasi. Kwa kielelezo, mtaalamu wa mambo ya akili Michael Davis asema juu ya shujaa mmoja wa Vietnam ambaye katika siku yake ya kufunga ndoa aliruka vichakani aliposikia sauti ya gari likitoa mlipuko. “Kulikuwa na ishara zote katika mazingira hayo ambazo zingalimwonyesha kwamba hali ni shwari,” asema Davis. “Ilikuwa ni miaka 25 baada ya vita; alikuwa Marekani, wala si Vietnam; . . . alikuwa amevaa koti jeupe, bali si mavazi ya vita. Lakini kichocheo cha kwanza kilipotokea, alitoroka kujificha.”
Mfadhaiko unaotokana na mambo ya vitani ni mmojawapo tu wa visababishi vya PTSD. Kulingana na The Harvard Mental Health Letter, tatizo hilo laweza kutokana na “tukio lolote au matukio fulani ambayo yanahusu kifo au tisho la kifo, au majeraha mabaya au tisho la kujeruhiwa kimwili. Inaweza kuwa msiba wa asili, aksidenti, au tendo la kibinadamu: gharika, moto, tetemeko la dunia, aksidenti ya gari, kulipuliwa kwa bomu, kufyatuliwa kwa risasi, mateso, kutekwa, kushambuliwa, kubakwa, au kumtenda mtoto vibaya.” Kushuhudia tu tukio baya au kulijua—labda kupitia ushuhuda wenye kutokeza sana au picha—kwaweza kutokeza dalili za PTSD, hasa ikiwa watu wenye kuhusika ni washiriki wa familia au marafiki wa karibu.
Bila shaka, watu huitikia mfadhaiko kwa njia tofauti-tofauti. “Watu wengi zaidi ambao hupitia mambo yenye kusababisha mfadhaiko hata hawasitawishi dalili mbaya za matatizo ya akili, na hata kama kuna dalili, hizo si lazima zifanane na zile za PTSD,” yaeleza The Harvard Mental Health Letter. Vipi kuhusu wale ambao mkazo wao hutokeza PTSD? Baada ya muda, wengine huweza kudhibiti hisia zinazohusiana na mfadhaiko na kupata kitulizo. Wengine huendelea kung’ang’ana na kumbukumbu za tukio lenye kuleta mfadhaiko miaka mingi baada ya tukio hilo kutukia.
Kwa vyovyote vile, wale wanaougua PTSD—na wale wanaotaka kuwasaidia—wapaswa kukumbuka kwamba kupata nafuu kwahitaji subira. Biblia huwahimiza sana Wakristo ‘waseme kwa kuliwaza nafsi zilizoshuka moyo’ na ‘wawe wenye ustahimilivu kuelekea wote.’ (1 Wathesalonike 5:14) Kwa Louise, aliyetajwa mwanzoni, miezi mitano ilipita kabla ya yeye kuweza tena kuendesha gari. “Japo maendeleo ambayo nimefanya,” yeye alisema miaka minne baada ya hiyo aksidenti, “siwezi kufurahia kuendesha gari kama zamani. Ni jambo ambalo ni lazima nifanye, kwa hiyo nalifanya. Lakini nimefanya maendeleo sana tangu wakati ule ambapo sikujiweza baada ya hiyo aksidenti.”
-
-
Mkazo Unaweza Kudhibitiwa!Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
Mkazo Unaweza Kudhibitiwa!
“Sikuzote kutakuwa na mkazo maishani, na kwa kweli jambo ambalo tunahitaji kuchunguza ni jinsi tunavyoitikia mkazo badala ya kujaribu kuuondoa.”—Leon Chaitow, mwandikaji mashuhuri wa masuala ya afya.
BIBLIA ilitabiri kwamba katika “siku za mwisho,” kutakuwapo “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” Uthibitisho waonyesha wazi kwamba tunaishi katika wakati huo, kwa sababu watu—kama tu unabii ulivyosema—ni “wenye kujitanguliza, wenye kiburi, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio waaminifu-washikamanifu, wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, wachongezi, wasio na hali ya kujidhibiti, wakali, wasio na upendo wa wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kututumuka kwa kiburi.”—2 Timotheo 3:1-5.
Si ajabu kwamba ni vigumu sana kudumisha utulivu wa kadiri fulani! Hata wale wanaojaribu kuishi kwa amani waweza kuathiriwa. “Mateso ya mwenye haki ni mengi,” akaandika mtunga-zaburi Daudi. (Zaburi 34:19; linganisha 2 Timotheo 3:12.) Na bado, kuna mengi uwezayo kufanya ili kupunguza mkazo usije ukalemewa nao. Fikiria madokezo yafuatayo.
Jitunze Mwenyewe
Jihadhari na kile unachokula. Mlo wenye afya watia ndani protini, matunda, mboga, nafaka na mbegu nyinginezo, na vyakula vinavyotokana na maziwa. Jihadhari na unga mweupe uliochujwa na mafuta kifu. Jihadhari na ulaji wako wa chumvi, sukari iliyosafishwa, unywaji wa kileo, na kafeini. Boresha mlo wako, na huenda ukapunguza uwezekano wa wewe kushikwa na mkazo.
Mazoezi. “Mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa,” Biblia yashauri. (1 Timotheo 4:8) Kwa kweli, mazoezi ya kiasi lakini yenye kudumu—wengine wanapendekeza mara tatu kwa juma—huimarisha moyo, huboresha mzunguko, hupunguza kolesteroli, na kupunguza uwezekano wa wewe kupatwa na mshiko wa moyo. Zaidi ya hiyo, mazoezi huendeleza hisia ya kuwa na afya njema, yaelekea kwa sababu ya endorphin ambazo huachiliwa wakati wa utendaji unaohitaji nguvu.
Pata usingizi wa kutosha. Ukosefu wa usingizi hutokeza uchovu na kupunguza uwezo wako wa kudhibiti mkazo. Ikiwa unapata matatizo ya usingizi, jaribu kudumisha wakati mmoja wa kawaida wa kwenda kulala na wa kuamka. Wengine hupendekeza kwamba usingizi mfupi wa mchana usipite dakika 30 ili usihitilafiane na usingizi mzuri wa usiku.
Kuwa mwenye mpango. Watu ambao hudhibiti wakati wao wanaweza kukabiliana na mkazo vizuri zaidi. Ili kuwa mwenye mpango, kwanza tambua ni madaraka yapi ambayo yanastahili kutangulizwa. Kisha, fanyiza ratiba ili madaraka hayo yasisahauliwe.—Linganisha 1 Wakorintho 14:33, 40 na Wafilipi 1:10.
Dumisha Mahusiano Mazuri
Pata tegemezo. Katika nyakati zenye mkazo wale ambao wana marafiki wengi na ambao wanajuana na watu wengi angalau hupata kadiri fulani ya ulinzi dhidi ya kushindwa. Kupata rafiki mmoja tu mwenye kutumainika ambaye mtu aweza kuongea naye kisiri kwaweza kusaidia sana. Mithali moja ya Biblia yasema: “Rafiki hupenda sikuzote; na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.”—Mithali 17:17.
Tatua mahitilafiano. “Msiache jua litue mkiwa katika hali ya kuchokozeka,” akaandika mtume Paulo. (Waefeso 4:26) Hekima ya kusuluhisha tofauti haraka badala ya kufungia hasira inaonyeshwa katika uchunguzi mmoja wa waokokaji 929 wa mshiko wa moyo. Wale wenye viwango vya juu vya uhasama walikuwa na uwezekano wa mara tatu wa kufa kutokana na kuzimika kwa moyo katika miaka kumi ya kwanza baada ya mshiko wa moyo kuliko wenzao wenye hali ya upole. Waandishi wa uchunguzi huo wasema kwamba ingawa hasira inaonekana kuwa kisababishi kikubwa, hisia yoyote hasi yenye nguvu inayopeleka kiasi kikubwa cha homoni mwilini inaweza kuwa na tokeo ilo hilo. “Husuda ni ubovu wa mifupa,” yasema Mithali 14:30.
Panga kutumia wakati na familia yako. Wazazi Waisraeli waliamriwa watumie wakati na watoto wao, wakikazia kikiki kanuni nzuri katika mioyo yao. (Kumbukumbu la Torati 6:6, 7) Kifungo kilichotokea kiliendeleza muungano wa familia—jambo ambalo linakosekana sana leo. Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba wenzi wa ndoa wenye kufanya kazi hutumia wastani wa dakika 3.5 pekee za kucheza na watoto wao kila siku. Lakini, familia yako yaweza kuwa chanzo kikubwa sana cha msaada mtu anapokabili mkazo. “Familia inakupa ushirika wa daima ikiwa kikundi kinachokujua vizuri sana na hata kukupenda,” chasema kitabu kimoja juu ya mkazo. “Kufanya kazi pamoja kwa familia ni njia bora zaidi ya kupunguza mkazo.”
Weka Usawaziko Katika Maisha Yako
Uwe mwenye kiasi. Mtu ambaye nyakati zote hujisukuma kupita kiasi kimwili na kihisia-moyo yaelekea atapatwa na uchovu mno na labda mshuko wa moyo. Jambo kuu ni usawaziko. ‘Hekima ya kutoka juu ni yenye kukubali sababu,’ akaandika mwanafunzi Yakobo. (Yakobo 3:17; linganisha Mhubiri 7:16, 17 na Wafilipi 4:5.) Jifunze kukataa madai ambayo yanazidi kile uwezacho kutimiza ifaavyo.
Usijilinganishe na mtu mwingine. Kitabu cha Wagalatia 6:4 chasema: “Acheni kila mmoja athibitishe kazi yake mwenyewe ni nini, na ndipo atakuwa na sababu ya mchachawo kwa habari yake mwenyewe peke yake, na si kwa kujilinganisha na mtu yule mwingine.” Ndiyo, hata katika mambo ya ibada, Mungu hafanyi ulinganishi usiofaa, akidai zaidi ya vile hali za kila mmoja ziruhusuvyo. Yeye hukubali zawadi zetu na dhabihu ‘kulingana na tulicho nacho, si kulingana na kile ambacho hatuna.’—2 Wakorintho 8:12.
Panga wakati wa pumziko. Hata Yesu, japo alikuwa mwenye bidii, alipanga wakati wa pumziko kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya wafuasi wake. (Marko 6:30-32) Mwandikaji aliyepuliziwa wa Mhubiri alihisi kwamba pumziko lenye kufaa lilinufaisha. Yeye aliandika: “Kisha nikaisifu furaha, kwa sababu mwanadamu hana neno lo lote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, na kunywa, na kucheka; na yakuwa hilo likae naye katika amali yake, siku zote za maisha yake alizompa Mungu chini ya jua.” (Mhubiri 8:15) Raha zenye usawaziko zaweza kuburudisha mwili na kusaidia kuondoa mkazo.
Uuone Mkazo kwa Njia Ifaayo
Unapokabili nyakati zenye mkazo:
Usikate kauli kwamba umekataliwa na Mungu. Biblia yatuambia kwamba kwa miaka mingi, Hana, aliyekuwa mwanamke mwaminifu, alikuwa na ‘uchungu rohoni mwake’ (“alihuzunika sana,” Revised Standard Version). (1 Samweli 1:4-11) Katika Makedonia, Paulo “alikuwa na mkazo katika kila hali.” (2 Wakorintho 7:5, Byington) Kabla ya kifo chake, Yesu “alikuwa akiingia katika maumivu makali,” na mkazo wake ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba “jasho lake likawa kama matone ya damu yakianguka kwenye ardhi.”a (Luka 22:44) Hao walikuwa watumishi waaminifu wa Mungu. Kwa hiyo, unapokabili mkazo hakuna sababu ya kukata kauli kwamba Mungu amekuacha.
Jifunze kutokana na hali zako zenye kutokeza mkazo. Paulo aliandika kwamba alilazimika kuvumilia “mwiba katika mwili,” bila shaka tatizo la afya ambalo lilikuwa limemsababishia mkazo sana. (2 Wakorintho 12:7) Lakini, miaka mitano baadaye, aliweza kusema hivi: “Katika kila jambo na katika hali zote nimejifunza siri ya jinsi ya kushiba na pia jinsi ya kuwa na njaa, jinsi ya kuwa na wingi na pia jinsi ya kupatwa na uhitaji. Kwa mambo yote ninayo nguvu kwa njia ya yeye anipaye nguvu.” (Wafilipi 4:12, 13) Paulo hakufurahia “mwiba katika mwili,” lakini kwa kuuvumilia, alijifunza jinsi ya kutegemea Mungu zaidi kwa ajili ya nguvu.—Zaburi 55:22.
Sitawisha Hali ya Kiroho
Soma na utafakari juu ya Neno la Mungu. “Wenye furaha ni wale wenye kuona uhitaji wao wa kiroho,” Yesu alisema. (Mathayo 5:3) Ni muhimu kusoma na kutafakari juu ya Neno la Mungu. Mara nyingi, kwa kutafuta kwa bidii katika Maandiko, tunapata neno lifaalo la kututia moyo ambalo tunahitaji ili kutusaidia katika siku hiyo. (Mithali 2:1-6) “Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu,” akaandika mtunga-zaburi, “faraja zako [za Mungu] zaifurahisha roho yangu.”—Zaburi 94:19.
Sali kwa ukawaida. Paulo aliandika: “Acheni maombi yenu ya bidii yajulishwe kwa Mungu; na amani ya Mungu izidiyo fikira yote kwa ubora italinda mioyo yenu na nguvu zenu za akili kwa njia ya Kristo Yesu.” (Wafilipi 4:6, 7) Ndiyo, “amani ya Mungu” yaweza kushinda hisia zenye mfadhaiko na kuzituliza, hata wakati ambapo “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida” inapohitajiwa.—2 Wakorintho 4:7.
Hudhuria mikutano ya Kikristo. Kutaniko la Kikristo hutoa njia nzuri ya kutoa tegemezo, kwa sababu wale waliomo katika kutaniko wanahimizwa kwa bidii ‘wafikiriane ili kuchocheana kwenye upendo na kazi zilizo bora [kwa] kutiana moyo.’ Kwa sababu nzuri, Paulo aliwaambia Wakristo Waebrania wa karne ya kwanza ‘wasiachilie mbali kukusanyika pamoja.’—Waebrania 10:24, 25.
Tumaini Hakika
Ni kweli kwamba kupunguza mkazo mara nyingi kunatia ndani mambo mengi kuliko kufuata tu utaratibu fulani sahili. Mara nyingi, badiliko kubwa katika njia ya kufikiri huhitajiwa. Kwa kielelezo, mtu aweza kuhitaji kujifunza njia mpya za kuitikia hali ili zisimlemeze. Katika visa vingine kurudia-rudia au kuzidi kwa mkazo kwaweza kufanya liwe jambo bora kutafuta matibabu mazuri.
Bila shaka, hakuna mtu leo ambaye maisha yake hayana kabisa mkazo mbaya. Hata hivyo, Biblia yatuhakikishia kwamba karibuni Mungu ataelekeza uangalifu wake kwa wanadamu na kuondoa hali ambazo hutokeza mkazo wenye kudhuru. Katika Ufunuo 21:4, twasoma kwamba Mungu “atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe.” Baadaye, wanadamu waaminifu watakaa katika usalama. Nabii Mika alitabiri hivi: “Wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.”—Mika 4:4.
-
-
Mkazo Unaweza Kudhibitiwa!Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Mkazo na Upasuaji
Matabibu fulani hufikiria kiwango cha mkazo cha wagonjwa wao kabla ya kuwapeleka katika chumba cha upasuaji. Kwa kielelezo, Dakt. Camran Nezhat, ambaye ni daktari-mpasuaji asema:
“Ikiwa mtu aliyeratibiwa kufanyiwa upasuaji aniambia kwamba alikuwa na wasiwasi siku hiyo na anaogopa kupasuliwa, mimi hufuta upasuaji huo.” Kwa nini? Nezhat aeleza: “Kila daktari-mpasuaji anajua kwamba watu ambao huogopa sana hawafanyi vizuri wakipasuliwa. Wao hutoka damu sana, wanapatwa na maambukizo na matatizo mengi zaidi. Ni vigumu zaidi kwao kupata nafuu. Ni afadhali zaidi ikiwa wametulia.”
-
-
Mkazo Unaweza Kudhibitiwa!Amkeni!—1998 | Machi 22
-
-
a Jasho lenye damu limeripotiwa kuwa limetukia katika visa fulani vya mkazo wa akili ulio mkali sana. Kwa kielelezo, katika hali ya hematidrosis, kuna kutoka kwa jasho lililochangamana na damu au rangi ya damu au umajimaji wa mwili uliochangamana na damu. Hata hivyo, haiwezi kusemwa kwa uhakika kabisa, jambo hususa ambalo lilitukia katika kisa cha Yesu.
-