-
Tatizo la Ulimwenguni PoteAmkeni!—2001 | Oktoba 22
-
-
Tatizo la Ulimwenguni Pote
“Kujiua ni tatizo kubwa kwa afya ya jamii.”—David Satcher, ofisa mkuu wa afya wa Marekani, mwaka wa 1999.
HIYO ndiyo mara ya kwanza kabisa kwa ofisa mkuu wa afya wa Marekani kutaarifu kwamba tatizo la kujiua ni jambo la kuhangaikiwa na jamii. Idadi ya watu wanaojiua nchini humo yazidi idadi ya watu wanaouawa. Haishangazi kuwa Bunge la Marekani lilitangaza kwamba kuzuia visa vya kujiua ni jambo linalopasa kushughulikiwa kwanza kotekote nchini humo.
Hata hivyo, visa vya kujiua nchini Marekani, ambavyo vilikuwa 11.4 kati ya kila watu 100,000 mwaka wa 1997, havijafikia vile vya ulimwenguni pote vilivyochapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni mnamo mwaka wa 2000, yaani, visa 16 kati ya kila watu 100,000. Visa vya kujiua ulimwenguni pote vimeongezeka kwa asilimia 60 katika miaka 45 iliyopita. Sasa, katika mwaka mmoja tu, watu wapatao milioni moja ulimwenguni pote hujiua. Yaani, yakadiriwa kuwa baada ya kila sekunde 40, mtu mmoja hujiua!
Hata hivyo, takwimu hazionyeshi tatizo hilo waziwazi. Katika visa vingi, familia nyingi hukana kwamba mshiriki wao alijiua. Isitoshe, yakadiriwa kwamba kila mara mtu mmoja anapojiua, watu 10 hadi 25 huwa wamejaribu kujiua. Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba asilimia 27 ya wanafunzi wa shule za sekondari nchini Marekani walikubali kwamba walikuwa wamefikiria sana kujiua katika mwaka uliotangulia; asilimia 8 ya wale waliohojiwa walisema kwamba walijaribu kujiua. Uchunguzi mwingine umefunua kwamba asilimia 5 hadi 15 ya watu wazima wamefikiria kujiua wakati fulani.
Tofauti za Kitamaduni
Watu huwa na maoni yanayotofautiana kuhusu kujiua. Wengine huona kujiua kuwa uhalifu, wengine huona ni tendo la woga, na bado wengine huona ni njia ya heshima ya kuomba radhi kwa kosa. Hata wengine huona kujiua kuwa njia bora ya kuendeleza harakati fulani. Kwa nini kuna maoni tofauti-tofauti? Utamaduni huchangia sana. Kwa hakika, jarida la habari la The Harvard Mental Health Letter ladokeza kwamba huenda hata utamaduni “ukachangia uwezekano wa kujiua.”
Fikiria nchi moja katika Ulaya ya kati—Hungaria. Dakt. Zoltán Rihmer afafanua kiwango cha juu cha kujiua nchini humo kuwa “‘utamaduni’ unaohuzunisha” wa Hungaria. Béla Buda, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Afya nchini Hungaria, alisema kwamba Wahungaria huwa tayari kujiua kwa sababu yoyote. Kulingana na Buda, hili ni itikio moja la kawaida: “Anaugua kansa—anajua jinsi ya kukomesha hali hiyo.”
Hapo zamani kulikuwa na desturi ya kidini nchini India iliyoitwa suttee. Ijapokuwa desturi hiyo ya mjane kujitupa juu ya rundo la kuni za kuchomea mwili wa mumewe ilikatazwa kwa muda mrefu, bado haijakwisha kabisa. Mwanamke mmoja alipojiua kwa njia hiyo, watu wengi wa eneo hilo walisifu sana msiba huo. Kwa mujibu wa gazeti la India Today, katika eneo hilo la India ‘wanawake wapatao 25 wamejichoma kwenye marundo ya kuni za kuchomea miili ya waume zao katika kipindi cha miaka 25.’
Kwa kushangaza, idadi ya watu wanaojiua nchini Japani ni mara tatu ya idadi ya wanaokufa kupitia aksidenti za barabarani! Kichapo Japan—An Illustrated Encyclopedia chasema hivi: ‘Utamaduni wa Japani ambao haujashutumu kamwe kujiua, unatambuliwa kwa desturi fulani maarufu ya kujipasua matumbo (seppuku au hara-kiri).’
Katika kitabu chake Bushido—The Soul of Japan, Inazo Nitobe, ambaye baadaye alikuwa msaidizi wa katibu mkuu wa Ushirika wa Mataifa, alieleza desturi hiyo ya kufurahia kifo. Aliandika hivi: ‘Desturi hiyo [seppuku] iliyoanzishwa katika enzi za kati, ilitumiwa na maaskari wa vita kulipia matendo yao ya uhalifu, kuomba radhi kwa makosa yao, kuhepa aibu, kulipia maovu waliyowatendea rafiki zao, au kuonyesha unyofu wao.’ Ijapokuwa desturi hiyo ya kujiua haionekani sana siku hizi, bado watu wachache huitumia ili kuathiri jamii.
Kwa upande mwingine, katika Jumuiya ya Wakristo, kujiua kulionwa kwa muda mrefu kuwa uhalifu. Kufikia karne ya sita na ya saba, Kanisa Katoliki liliwatenga watu waliokuwa wamejiua na likakataa kuwafanyia ibada ya mazishi. Katika sehemu fulani, ushupavu wa kidini umetokeza desturi za kiajabu kuhusu watu waliojiua kama vile kuning’iniza mwili wa mtu aliyejiua, na hata kudunga moyo wake kwa mti uliochongoka.
Kwa kushangaza, wale waliojaribu kujiua wangeweza kuhukumiwa kifo. Mwingereza mmoja wa karne ya 19 alinyongwa kwa sababu alijaribu kujiua kwa kujikata koo. Hivyo, wenye mamlaka walitimiza jambo ambalo mtu huyo alishindwa kufanya. Ijapo adhabu ya jaribio la kujiua ilibadilika baadaye, ni katika mwaka wa 1961 tu ndipo Bunge la Uingereza lilitangaza kwamba kujiua na majaribio ya kujiua hayakuwa tena matendo ya uhalifu. Katika Ireland, kujiua kulionwa kuwa uhalifu hadi mwaka wa 1993.
Siku hizi waandishi fulani husema kwamba kujiua ni njia nyingine ya kusuluhisha matatizo. Kitabu kimoja cha mwaka wa 1991 kilichozungumzia jinsi watu wanaougua ugonjwa usio na tiba wanavyoweza kusaidiwa kujiua, kilidokeza njia mbalimbali za kufanya hivyo. Baadaye, watu wengi ambao hawakuugua ugonjwa usio na tiba walitumia mojawapo ya madokezo hayo.
Je, kweli kujiua husuluhisha matatizo? Au, je, kuna sababu nzuri za kuendelea kuishi? Kabla hatujajibu maswali hayo, acheni kwanza tuchunguze mambo yanayofanya watu wajiue.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Katika mwaka mmoja tu, watu wapatao milioni moja ulimwenguni pote hujiua. Yaani, baada ya karibu kila sekunde 40, mtu mmoja hujiua!
-
-
Kwa Nini Watu Hukata Tamaa ya Kuishi?Amkeni!—2001 | Oktoba 22
-
-
Kwa Nini Watu Hukata Tamaa ya Kuishi?
“Kila mtu anayejiua huwa na sababu zake mwenyewe: za kibinafsi, zisizojulikana, na zinazohangaisha.”—Kay Redfield Jamison, mtaalamu wa magonjwa ya akili.
“KUISHI ni kuteseka.” Hivyo ndivyo Ryunosuke Akutagawa, mwandishi maarufu wa Japani aliyeishi katika miaka ya mapema ya karne ya 20, alivyoandika muda mfupi kabla ya kujiua. Hata hivyo, alianza sentensi hiyo kwa maneno haya: “Kwa wazi, sitaki kufa, lakini . . . ”
Kama Akutagawa, watu wengi wanaojiua hawataki kufa lakini wanataka “kukomesha mambo yanayotukia,” ndivyo alivyosema profesa mmoja wa saikolojia. Barua ambayo watu wanaojiua huandika huonyesha hivyo. Sentensi kama vile ‘Singevumilia zaidi ya hapo’ au ‘Kwa nini niendelee kuishi?’ huonyesha tamaa kubwa ya kuepuka magumu ya maisha. Lakini kama vile mtaalamu mmoja alivyoeleza, kujiua ni “kama kutibu mafua kwa kutumia bomu la nyukilia.”
Ijapokuwa visababishi vya kujiua hutofautiana, kwa ujumla mambo fulani hususa maishani huwachochea watu kujiua.
Mambo Yanayowachochea
Si ajabu kwamba vijana hufadhaika na kujiua hata kwa sababu ya mambo yanayoonekana kuwa madogo kwa watu wengine. Wanapofadhaika na kutoweza kubadili hali hiyo, huenda vijana wakaona kuwa wakijiua watakuwa wakilipiza kisasi dhidi ya watu waliowaumiza. Hiroshi Inamura, mtaalamu anayeshughulika na watu wanaotaka kujiua nchini Japani, aliandika hivi: ‘Watoto hukuza tamaa ya kumwadhibu mtu aliyewanyanyasa kwa kujiua.’
Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi huko Uingereza ulionyesha kwamba watoto wanapodhulumiwa sana, uwezekano wa kujiua huwa karibu mara saba zaidi ya ilivyo kawaida. Watoto hao huumia sana kihisia. Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 13 aliyejitia kitanzi, aliacha barua iliyowataja vijana watano waliomnyanyasa na kumlazimisha awape pesa. Aliandika hivi: “Tafadhali waokoeni watoto wengine.”
Huenda wengine wakajaribu kujiua wanapokuwa na matatizo shuleni au wanapovunja sheria, uhusiano wao wa kimapenzi unapovunjika, wanapoanguka mtihani, wanapofadhaishwa na mitihani, au wanapolemewa sana na mahangaiko kuhusu maisha ya baadaye. Vijana wanaobalehe ambao hufanya vyema shuleni na kupenda kufanya mambo barabara kabisa wanaweza kujaribu kujiua wasipofanikiwa au wanapokabili kipingamizi iwe ni jambo halisi au la kuwazia tu.
Mara nyingi, matatizo ya kiuchumi au ya kikazi huwachochea watu wazima kujiua. Baada ya uchumi kuzorota kwa miaka mingi nchini Japani, hivi karibuni watu zaidi ya 30,000 walijiua katika mwaka mmoja. Kwa mujibu wa gazeti la Mainichi Daily News, robo tatu hivi ya watu wa umri wa makamo waliojiua walifanya hivyo “kwa sababu ya matatizo yanayosababishwa na madeni, kufilisika kwa biashara, umaskini na kukosa kazi.” Matatizo ya familia yanaweza pia kuwafanya watu wajiue. Gazeti moja la Finland liliripoti kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa “wanaume wa umri wa makamo waliopata talaka hivi majuzi” kujiua. Uchunguzi uliofanywa huko Hungaria ulifunua kwamba wasichana wengi wanaofikiria kujiua ni wale waliolelewa katika familia zilizovunjika.
Kustaafu na ugonjwa ni mambo mengine pia yanayochochea watu kujiua, hasa wazee-wazee. Mara nyingi mgonjwa huamua kujiua ili kuepuka mateso, si tu anapougua ugonjwa usio na tiba, bali wakati anapoona kuwa hawezi kuvumilia kuteseka.
Hata hivyo, si watu wote wanaojiua wanapokabili matatizo hayo. La, watu wengi wanapokabili hali hizo zenye mikazo hawajiui. Basi, ni kwa nini watu fulani hufikiri kujiua ni suluhisho, na wengine hawafikiri hivyo?
Visababishi Visivyoonekana Wazi
Kay Redfield Jamison, profesa wa magonjwa ya akili kwenye Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, asema hivi: “Uamuzi wa kujiua hutegemea hasa jinsi mtu anavyoelewa mambo.” Aongezea hivi: “Akili za watu wengi, zinapokuwa timamu, hazioni kuwa jambo lolote lile linaweza kumfadhaisha mtu hata ajiue.” Eve K. Mościcki, wa Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili, asema kwamba visababishi vingi—vingine visivyoonekana wazi—hujumlika kuwaongoza watu kujiua. Visababishi hivyo visivyoonekana wazi vyatia ndani magonjwa ya akili na magonjwa yanayosababishwa na uraibu, maumbile ya chembe za urithi, na utendaji wa kemikali ubongoni. Tutachunguza baadhi ya visababishi hivyo.
Visababishi vikuu zaidi ni magonjwa yanayosababishwa na uraibu na magonjwa ya akili, kama vile kushuka moyo, magonjwa ya hisia zinazobadilika-badilika, sizofrenia (kuchanganyikiwa kiakili), na kutumia vibaya vileo au dawa za kulevya. Uchunguzi uliofanywa huko Ulaya na Marekani unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaojiua huugua magonjwa hayo. Kwa kweli, watafiti wa Sweden waligundua kwamba visa vya kujiua miongoni mwa wanaume wasiougua magonjwa hayo vilikuwa 8.3 kati ya wanaume 100,000, lakini miongoni mwa wale walioshuka moyo viliongezeka hadi visa 650 kati ya wanaume 100,000! Na wataalamu wanasema kwamba hivyo ndivyo visababishi vya kujiua pia katika nchi za Mashariki. Lakini, hata mambo yanayochochea watu kujiua yakijumlishwa pamoja na kushuka moyo, bado yawezekana kuepuka kujiua.
Profesa Jamison, ambaye wakati mmoja alijaribu kujiua, asema hivi: “Watu huonekana kuwa wanaweza kustahimili au kuvumilia kushuka moyo maadamu wanatumai kwamba mambo yatakuwa afadhali.” Hata hivyo, amegundua kwamba mtu asipoweza kustahimili mfadhaiko unaoongezeka hatua kwa hatua, uwezo wa mfumo wa akili wa kuzuia tamaa ya kujiua hupungua pole kwa pole. Analinganisha hali hiyo na jinsi breki za gari zinavyokwisha kwa sababu ya mkazo mwingi.
Ni muhimu kutambua mwelekeo huo kwani yawezekana kutibu mshuko wa moyo. Mtu anayehisi kuwa hajiwezi anaweza kurudia hali yake ya kawaida. Visababishi visivyoonekana wazi vikishughulikiwa, watu wanaweza kutenda kwa njia tofauti wanapokumbwa na maumivu ya kihisia na mikazo ambayo mara nyingi huchochea watu kujiua.
Watu fulani hufikiri kwamba maumbile ya chembe za urithi ni kisababishi kisichoonekana wazi cha visa vingi vya kujiua. Ni kweli kwamba chembe za urithi huchangia hisia za mtu kwa njia fulani, na uchunguzi umefunua kwamba familia nyingine huwa na visa vingi vya kujiua zaidi ya nyingine. Lakini, “mwelekeo wa kujiua uliorithiwa haumaanishi kamwe kwamba mtu hawezi kuepuka kujiua,” asema Jamison.
Utendaji wa kemikali ubongoni ni kisababishi kingine kisichoonekana wazi. Mabilioni ya chembe za neva huwasiliana ubongoni kupitia utendaji wa kemikali. Kwenye ncha zilizotengana za nyuzi za neva kuna mapengo madogo yanayoitwa sinapsi. Vitu fulani hupitisha habari kwenye sinapsi kupitia utendaji wa kemikali. Huenda kiasi cha serotonin, kimojawapo cha vitu vinavyopitisha habari, huchangia uwezekano wa kibiolojia wa mtu kujiua. Kitabu Inside the Brain chaeleza hivi: “Kiasi kidogo cha serotonin . . . chaweza kumnyang’anya mtu furaha maishani, kwa kupunguza tamaa yake ya kuishi na kuongeza uwezekano wa kushuka moyo na kujiua.”
Hata hivyo, jambo la hakika ni kwamba hakuna mtu aliyepangiwa kujiua. Mamilioni ya watu hukabiliana na maumivu ya kihisia na mikazo. Wengine hujiua kutokana na jinsi ubongo na moyo unavyotenda wanapokabili mikazo. Mbali na kushughulikia mambo yanayochochea watu kujiua, ni lazima visababishi visivyoonekana wazi vishughulikiwe pia.
Hivyo basi, ni jambo gani linalopasa kufanywa ili mtu awe na maoni yanayofaa yatakayomfanya afurahie tena kuishi?
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Jinsia na Kujiua
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa huko Marekani, ingawa uwezekano wa wanawake kujaribu kujiua ni mara mbili au tatu ya ule wa wanaume, uwezekano wa wanaume kufaulu kujiua ni mara nne ya ule wa wanawake. Uwezekano wa wanawake kushuka moyo ni mara mbili ya ule wa wanaume. Huenda hilo likaonyesha ni kwa nini wanawake wengi hujaribu kujiua. Hata hivyo, huenda magonjwa yao ya kushuka moyo hayawafanyi kuwa hatari sana. Hivyo hawatumii njia hatari sana za kujiua. Kwa upande mwingine, huenda wanaume wakatumia njia hatari za kujiua ili kuhakikisha kwamba watafaulu.
Hata hivyo, nchini China, wanawake ndio hufaulu kujiua zaidi ya wanaume. Kwa hakika, uchunguzi unafunua kwamba asilimia 56 hivi ya visa vya wanawake wanaojiua ulimwenguni hutukia China, hasa katika maeneo ya mashambani. Yasemekana kuwa mojawapo ya sababu za wanawake kujaribu na kufaulu kujiua nchini humo ni kwamba ni rahisi kupata dawa hatari za kuua wadudu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Kujiua na Upweke
Upweke ni mojawapo ya mambo yanayofanya watu washuke moyo na kujiua. Jouko Lönnqvist, ambaye aliongoza uchunguzi mmoja kuhusu visa vya kujiua nchini Finland, alisema hivi: “Watu wengi [waliojiua], walihisi upweke kila siku. Walikuwa na wakati mwingi lakini hawakushirikiana sana na watu.” Kenshiro Ohara, mtaalamu wa magonjwa ya akili kwenye Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Hamamatsu nchini Japani, alitaarifu kwamba “kujitenga” kulisababisha ongezeko la hivi majuzi la idadi ya wanaume wa makamo waliojiua nchini humo.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Mara nyingi, matatizo ya kiuchumi au ya kikazi huwachochea watu wazima kujiua
-