Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kujiua Tatizo Lililojificha Linaloenea Kasi
    Amkeni!—2000 | Februari 22
    • Kujiua Tatizo Lililojificha Linaloenea Kasi

      JOHN NA MARYa wana umri unaozidi miaka 50 na wanaishi katika nyumba ndogo kwenye eneo la mashambani huko Marekani. John ana ugonjwa unaofisha wa kuvimba mapafu na moyo unaovilia damu na kusita. Mary hawezi kuwazia kuishi bila John, naye hawezi kustahimili uchungu wa kumwona akidhoofika zaidi na zaidi, na kuwa hoi. Mary ana matatizo yake ya afya naye ameugua mshuko-moyo kwa miaka mingi. John amekuwa akihangaika sana karibuni kwa sababu Mary amekuwa akisema juu ya kujiua. Fikira zake zimekanganyika kwa sababu ya mshuko-moyo na dawa anazotumia. Anasema kwamba hawezi kustahimili wazo la kubaki peke yake.

      Dawa zimetapakaa kila mahali nyumbani—vidonge vya moyo, dawa zinazopunguza mshuko-moyo, dawa za kutuliza maumivu. Mapema asubuhi moja, Mary aingia jikoni na kuanza kubugia vidonge. Aendelea kumeza tu hadi John anapomkuta na kumpokonya vidonge hivyo. Yeye aita kikosi cha waokoaji huku Mary akiwa amezimia. Yeye asali kwamba isiwe kuchelewa mno.

      Yanayofunuliwa na Takwimu

      Mengi yameandikwa katika miaka ya karibuni kuhusu kuongezeka kwa visa vya kujiua miongoni mwa vijana—yafaa, kwa kuwa ni msiba gani mkubwa unaoweza kupita kifo cha mapema cha kijana, mchanga mwenye mataraja mema? Lakini, vyombo vya habari havitaji jambo hakika la kwamba visa vya kujiua katika nchi nyingi huongezeka kulingana na umri. Hilo ni kweli iwe jumla ya visa vya kujiua katika nchi fulani iko juu au chini, kama sanduku lililo katika ukurasa uliotangulia lionyeshavyo. Kuchunguza takwimu hizo hufunua pia hali ya tatizo hilo lililojificha linaloenea tufeni pote.

      Mnamo mwaka wa 1996 Vituo vya Kudhibiti Magonjwa vya Marekani viliripoti kwamba idadi ya visa vya kujiua miongoni mwa Wamarekani wenye umri wa miaka 65 na zaidi iliongezeka ghafula kwa asilimia 36 tangu mwaka wa 1980. Idadi kubwa ya Wamarekani wazee-wazee walichangia ongezeko hilo—japo si hao tu. Idadi halisi ya watu wenye umri unaozidi miaka 65 waliojiua mwaka wa 1996 iliongezeka pia, kwa asilimia 9, mara ya kwanza kwa muda wa miaka 40. Kuhusu vifo vilivyotokana na majeraha, Wamarekani wengi wazee-wazee walikufa kutokana na kuanguka na aksidenti za magari peke yake. Kwa kweli, huenda hata takwimu hizi zenye kushtua zikawa chini sana. “Yashukiwa kwamba takwimu hizo zinazotegemea hati zinazoeleza kisababishi cha kifo zinataja visa vichache sana vya kujiua,” chasema kitabu A Handbook for the Study of Suicide. Kitabu hicho chaongezea kwamba watu fulani wanakadiria takwimu halisi kuwa maradufu zaidi ya takwimu zilizoripotiwa.

      Matokeo ni nini? Marekani sawa na nchi nyinginezo nyingi, inakumbwa na tatizo lililojificha linaloenea kasi tufeni pote la kujiua kwa raia wazee-wazee. Dakt. Herbert Hendin, mtaalamu wa tatizo la kujiua, asema: “Licha ya kwamba visa vya kujiua katika Marekani huongezeka kwa kawaida kulingana na umri, kujiua miongoni mwa watu wazee-wazee hakuzingatiwi sana na umma.” Mbona iwe hivyo? Yeye adokeza kwamba sehemu ya tatizo hilo ni kwa sababu visa vya watu wazee-wazee kujiua vimekuwa vingi sikuzote, “havijazusha hofu ya ghafula kama ongezeko kubwa la vijana kujiua.”

      Kujiua Haraka Zaidi

      Japo takwimu hizo zinatisha, ni tarakimu tu zisizo na utu. Haziwezi kueleza maisha ya upweke pasipo mwenzi mpenzi, kujitegemea kunakokatisha tamaa, kuvunjika moyo kwa sababu ya maradhi sugu, hisia ya upweke na huzuni iletwayo na mshuko-moyo mkali sana, habari zenye kukatisha tamaa za kuwa na ugonjwa wa kufisha. Ukweli wenye kuhuzunisha ni kwamba ingawa vijana huenda wakajaribu kujiua kwa sababu ya kutenda bila kufikiri kwa sababu ya matatizo ya muda, kwa kawaida wazee-wazee hukabili matatizo yaonekanayo kuwa ya kudumu na yasiyoweza kutatuliwa. Tokeo ni kwamba, mara nyingi wao huazimia kujiua kuliko vijana nao hujiua haraka zaidi.

      “Si kwamba tu kujiua kumeenea sana miongoni mwa wazee-wazee, bali tendo la kujiua ladhihirisha tofauti muhimu kati ya vijana na wazee,” asema Dakt. Hendin, katika kitabu chake Suicide in America. “Hasa uwiano wa majaribio halisi ya kujiua hubadilika sana miongoni mwa wazee-wazee. Miongoni mwa watu wote kwa ujumla, uwiano wa majaribio ya kujiua na kujiua halisi umekadiriwa kuwa 10 kwa 1; miongoni mwa vijana (wenye umri wa miaka 15 hadi 24), umekadiriwa kuwa 100 kwa 1; na miongoni mwa wale wenye umri unaozidi miaka 55, umekadiriwa kuwa 1 kwa 1.”

      Hizo ni takwimu zinazohitaji kufikiriwa kama nini! Jinsi lilivyo jambo lenye kuvunja moyo kuzeeka, kudhoofika kimwili, na kuteseka kwa maumivu na ugonjwa! Si ajabu kwamba wengi hujiua. Hata hivyo, kuna sababu nzuri ya kuthamini sana uhai—hata chini ya hali ngumu sana. Fikiria kilichompata Mary aliyetajwa mwanzoni.

      [Maelezo ya Chini]

      a Majina yamebadilishwa.

      [Chati katika ukurasa wa 3]

      Visa vya Kujiua Kati ya Kila Watu 100,000, Kulingana na Umri na Jinsia

      Wanaume/Wanawake Miaka 15 Hadi 24

      8.0/2.5 Argentina

      4.0/0.8 Ugiriki

      19.2/3.8 Hungaria

      10.1/4.4 Japani

      7.6/2.0 Mexico

      53.7/9.8 Urusi

      23.4/3.7 Marekani

      Wanaume/Wanawake Miaka 75 na Zaidi

      55.4/8.3 Argentina

      17.4/1.6 Ugiriki

      168.9/60.0 Hungaria

      51.8/37.0 Japani

      18.8/1.0 Mexico

      93.9/34.8 Urusi

      50.7/5.6 Marekani

  • Wamepewa Tamaa ya Kuishi
    Amkeni!—2000 | Februari 22
    • Wamepewa Tamaa ya Kuishi

      MARY alikuwa na mshuko-moyo mkali sana kutia na matatizo mengine ya afya. Hata hivyo, hakuwa ametengwa na familia yake, wala kutumia vibaya vileo au dawa za kulevya. Kisa cha Mary chaonyesha kwamba jaribio hatari la kujiua halichangiwi tu na hali zinazoonwa kuwa visababishi.

      Kwa muda fulani ilionekana kana kwamba Mary angehesabiwa katika takwimu zinazoshuhudia jambo la kwamba wazee-wazee hujiua sana. Alizimia kwa muda mrefu, bila fahamu, katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya karibu, uhai wake ulikuwa hatarini. Mume wake John mwenye wasiwasi hakubanduka ubavuni mwake. Madaktari walimwonya John na familia yao kwamba huenda Mary akafa na hata akinusurika atapatwa na madhara ya kudumu ya ubongo.

      Mary alitembelewa kila siku na jiraniye, Sally, ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. “Niliisihi sana familia yake isife moyo,” asema Sally. “Mama yangu anayeugua kisukari, alizimia kwa majuma mengi miaka kadhaa iliyopita. Madaktari waliiambia familia yetu kwamba angekufa, lakini hakufa. Ningeushika mkono wa Mary na kusema naye, kama nilivyomfanyia mama yangu, na nilihisi ni kana kwamba kulikuwa na itikio hafifu.” Kufikia siku ya tatu, itikio lilikuwa lenye nguvu zaidi, na ilionekana kwamba Mary angeweza kuwatambua watu, ingawa hangezungumza.

      ‘Je, Ningeweza Kumzuia Asijiue?’

      “John alisumbuliwa sana na hisia ya hatia,” asema Sally. “Alikuwa na hakika kwamba yeye ndiye aliyekosea.” Hilo ni itikio la kawaida kwa kisa cha kujiua au kwa jaribio la kujiua la mtu umpendaye. “Nilimkumbusha kwamba Mary alikuwa akitibiwa mshuko-moyo mkali sana. Alikuwa mgonjwa na hangezuia mshuko-moyo kama ambavyo hangejizuia kuwa mgonjwa.”

      Wale ambao wapendwa wao wanajiua mara nyingi huteswa na swali hili, Ningeweza kufanya nini ili nizuie jambo hilo? Kuwa macho kuona dalili za kuonya na mambo hatari kwaweza kuzuia jaribio la kujiua. Ikiwa sivyo, kumbuka kwamba tendo la mtu mwingine la kujiangamiza si daraka lako. (Wagalatia 6:5) Hili ni jambo muhimu kukumbuka hasa kuhusu visa ambavyo mshiriki wa familia mwenye nia ya kujiua anataka kimakusudi kuwafanya wengine wahisi wakiwa na hatia. Dakt. Hendin, aliyetajwa mapema, asema: “Yapasa ikumbukwe kwamba majaribio hatari ya kujiua mara nyingi hutekelezwa na watu ambao hutumaini kuathiri au kuelekeza hisia za watu wengine hata ingawa hawatakuwapo ili kushuhudia kufanikiwa au kushindwa kwa jitihada zao.”

      Dakt. Hendin aendelea kusema hivi: “Wazee wenye nia ya kujiua, kwa kawaida hutaka kuathiri, kudhibiti, au kushurutisha watoto wao ambao ni watu wazima vilevile ndugu zao au wenzi wa ndoa watwae daraka la kumlinda. Kwa kawaida madai ya mhasiriwa hayawezi kamwe kutimizwa, mara nyingi anakuwa asiyeridhiana kuhusu madai hayo, na majaribio madogo ya kujiua hufuatwa mara nyingi na majaribio hatari.”

      Washiriki wa familia wanaokabili hali hizo huenda wakahisi kwamba kwa kweli wamebanwa mno, zaidi ya uwezo wao. Lakini, usisahau kamwe kwamba Yehova Mungu hufufua wafu na kwamba aweza kufufua wapendwa wetu waliojiua kwa sababu ya mshuko-moyo, maradhi ya akili, au kukata tamaa.—Ona “Maoni ya Biblia: Kujiua—Kuna Ufufuo?” katika Amkeni! la Mei 8, 1991, ukurasa wa 22-23.

      Ingawa kujiua hakuwezi kutetewa, inafariji kukumbuka kwamba matazamio ya wakati ujao ya wapendwa wetu yanamtegemea Mungu ambaye anafahamu kikamili kuwa udhaifu wetu na kupungukiwa kwetu kwaweza kumsukuma mtu atende kitendo hicho chenye kutamausha. Biblia husema hivi juu ya Yehova: “Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”—Zaburi 103:11-14.

      Matokeo Yenye Kufurahisha

      Kwa siku mbili Mary alipigania uhai wake, lakini akaokoka. Alirudiwa na fahamu pole kwa pole, kisha John akaenda naye nyumbani, na akafungia dawa zote. Sasa Mary huzuru wafanyakazi wa kijamii wa afya ya akili naye asema kwamba hawezi kueleza au kukumbuka wazo baya lililomchochea ajaribu kujiua.

      Sasa Sally, jirani ya John na Mary, hujifunza nao Biblia kila juma. Wamejifunza kutoka kwa Biblia kwamba matatizo yanayoonekana kuwa bila utatuzi, hasa kwa wazee-wazee, yatatatuliwa na Mungu hivi karibuni. “Bila shaka funzo la Biblia peke yake haliondoi matatizo,” aeleza Sally. “Ni lazima uthibitishe kutoka kwenye Maandiko kuwa ahadi hizo ni halisi, kisha unahitaji kutumia yale unayojifunza. Lakini nafikiri John na Mary wanapata tumaini halisi la wakati ujao.”

      Iwapo wakati wako ujao waonekana kuwa bila tumaini na ungependa kupata tumaini hakika, mbona usiwasiliane na Mashahidi wa Yehova? Sawa na John na Mary, acha wakuthibitishie kwamba Mungu anaweza na atatatua matatizo yote hivi karibuni. Bila kujali hali mbaya sana ya mambo sasa, kuna suluhisho. Tafadhali chunguza nasi tumaini hakika la wakati ujao ambalo limeamsha tena tamaa ya wengi ya kuishi.

  • Tumaini Hakika
    Amkeni!—2000 | Februari 22
    • Tumaini Hakika

      YAPATA miaka 2,000 iliyopita, Yesu, ambaye mara nyingi huitwa mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi, alihukumiwa kifo isivyo haki. Alipokuwa ametundikwa kwenye mti wa mateso, mtenda-maovu aliyetundikwa karibu naye alimwambia hivi kwa kumdhihaki: “Wewe ndiwe Kristo, sivyo? Jiokoe mwenyewe na sisi.”

      Ndipo, mtenda-maovu mwingine aliyehukumiwa kifo pia akamkemea yule mwingine: “Je, wewe humhofu Mungu hata kidogo, kwamba sasa wewe umo katika hukumu ileile? Nasi, kwa kweli, tuko hivyo kwa haki, kwa maana sisi tunapokea kwa ukamili kile tustahilicho kwa mambo tuliyofanya; lakini mtu huyu hakufanya jambo lolote lisilopaswa.” Kisha akamgeukia Yesu na kusihi hivi: “Nikumbuke mimi uingiapo katika ufalme wako.”

      Yesu akajibu: “Kwa kweli mimi nakuambia wewe leo, Utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.”—Luka 23:39-43.

      Yesu alikuwa amewekewa tumaini zuri ajabu mbele yake. Mtume Paulo alionyesha jinsi tumaini hilo lilivyomwathiri Yesu, aliposema: “Kwa ajili ya shangwe iliyowekwa mbele yake alivumilia mti wa mateso, akidharau aibu.”—Waebrania 12:2.

      “Shangwe” hiyo iliyowekwa mbele ya Yesu ilitia ndani kuishi tena mbinguni na Baba yake na hatimaye kutumikia akiwa Mtawala wa Ufalme wa Mungu. Isitoshe, angekuwa pia na shangwe ya kuwakaribisha mbinguni wafuasi wake waliothibitishwa na wanaotumainika ambao watatawala pamoja naye wakiwa wafalme juu ya dunia. (Yohana 14:2, 3; Wafilipi 2:7-11; Ufunuo 20:5, 6) Hivyo basi, Yesu alimaanisha nini alipomwahidi yule mtenda-maovu kwamba angekuwa katika Paradiso?

      Kuna Tumaini Gani kwa Yule Mtenda-Maovu?

      Yule mtu hakustahili kutawala pamoja na Yesu mbinguni. Yeye hatiwi miongoni mwa wale walioambiwa hivi na Yesu: “Nyinyi ndio mmeshikamana nami katika majaribu yangu; nami nafanya agano pamoja nanyi, sawa na vile Baba yangu amefanya agano pamoja nami, kwa ajili ya ufalme.” (Luka 22:28, 29) Lakini, Yesu alimwahidi yule mtenda-maovu kwamba angekuwa pamoja naye katika Paradiso. Ahadi hiyo itatimizwaje?

      Mwanamume na mwanamke wa kwanza, Adamu na Hawa, waliwekwa katika Paradiso na Yehova Mungu, bustani ya raha inayoitwa Edeni. (Mwanzo 2:8, 15) Edeni ilikuwa duniani, na Mungu alikusudia kwamba dunia nzima iwe paradiso. Hata hivyo, Adamu na Hawa walikosa kumtii Mungu nao wakafukuzwa kutoka kwa makao yao mazuri. (Mwanzo 3:23, 24) Lakini Yesu alifunua kwamba Paradiso ingerudishwa na kwamba ingeenea duniani pote.

      Mtume Petro alipomuuliza Yesu kuhusu thawabu ambayo yeye na mitume wenzake wangepokea kwa kumfuata yeye, Yesu aliahidi: “Katika uumbaji-upya wakati Mwana wa binadamu aketipo juu ya kiti chake cha ufalme chenye utukufu, nyinyi ambao mmenifuata mtaketi nyinyi wenyewe pia juu ya viti vya ufalme kumi na viwili.” (Mathayo 19:27, 28) Kwa wazi, katika simulizi la Luka la mazungumzo hayo, badala ya kusema “katika uumbaji-upya,” Yesu anukuliwa akisema “katika mfumo wa mambo unaokuja.”—Luka 18:28-30.

      Kwa hiyo, Yesu Kristo aketipo juu ya kiti chake cha ufalme chenye utukufu, pamoja na watawala-wenzi wake, atafanyiza mfumo mpya wa mambo ulio mwadilifu. (2 Timotheo 2:11, 12; Ufunuo 5:10; 14:1, 3) Kupitia utawala wa kimbingu wa Kristo, kusudi la awali la Mungu la dunia nzima kuwa paradiso litatimizwa!

      Wakati wa utawala huo wa Ufalme, Yesu atatimiza ahadi yake kwa yule mhalifu aliyekufa kando yake. Atamfufua, na mtu huyo atakuwa raia wa kidunia wa Yesu. Kisha yule mtenda-maovu atapewa fursa ya kutimiza matakwa ya Mungu na kuishi milele chini ya utawala wa huo Ufalme. Kwa kweli twaweza kushangilia tazamio linalotegemea Biblia la kuishi milele katika Paradiso duniani!

      Maisha Yaweza Kuwa na Kusudi

      Ebu wazia kusudi ambalo tumaini hilo tukufu laweza kuleta maishani mwetu. Laweza kulinda akili zetu kutokana na matokeo yenye msiba ya fikira zisizofaa. Mtume Paulo alilinganisha tumaini hilo na kifaa muhimu cha silaha za kiroho. Alisema kwamba ni lazima tuvae “tumaini la wokovu” kama “kofia ya chuma.”—1 Wathesalonike 5:8; Zaburi 37:29; Ufunuo 21:3, 4.

      Tumaini hilo linaendeleza uhai. Katika Paradiso inayokuja, badala ya upweke kutakuwapo machozi ya shangwe wapendwa wetu wanapofufuliwa na “Mungu awafufuaye wafu.” (2 Wakorintho 1:9) Kisha kuvunjika moyo kunakosababishwa na udhaifu wa kimwili, maumivu, na ulemavu kutasahauliwa, kwa kuwa “mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu.” ‘Nyama ya mwili wa [mtu] itakuwa laini kuliko ya mtoto,’ naye ‘atarudia siku za ujana wake.’—Isaya 35:6; Ayubu 33:25.

      Wakati huo, wakati ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, ‘Mimi mgonjwa,’” kukata tamaa kwa sababu ya maradhi sugu kutakuwa tu kumbukumbu linalodidimia. (Isaya 33:24) Utupu unaosababishwa na mshuko-moyo mkali sana utageuzwa kuwa “furaha ya milele.” (Isaya 35:10) Kukatishwa tumaini na habari za kwamba una ugonjwa unaofisha kutatokomea pamoja na kifo, adui wa kale wa wanadamu.—1 Wakorintho 15:26.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki