-
Teknolojia Imeenea kwa Kasi SanaAmkeni!—2009 | Novemba
-
-
Teknolojia Imeenea kwa Kasi Sana
HUKO Albania, si jambo la ajabu kumwona mzee aliyepanda punda akizungumza kwenye simu yake ya mkononi. Huko India, maskini fulani anaacha kuombaomba ili apige au ajibu simu yake ya mkononi. Naam, simu za mkononi, kompyuta, na televisheni zimeenea kokote ulimwenguni kwa matajiri na maskini pia.
Kuongezeka kwa simu za mkononi kunaonyesha jinsi ambavyo teknolojia imeenea, na nyingi ya simu hizo si simu tu. Simu za hali ya juu humwezesha mtu kutumia Intaneti, kutuma na kupokea barua pepe na ujumbe mfupi, kutazama televisheni, kusikiliza muziki, kupiga picha, kumwelekeza mahali anapoenda kwa kutumia Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti (GPS), na—bila shaka—hata kupiga simu!
Kulingana na ripoti moja iliyotolewa katika gazeti Washington Post, simu fulani ya hali ya juu sana “sasa ina uwezo mkubwa wa kufanya mambo kuliko uwezo ambao Kituo cha Amerika Kaskazini cha Ulinzi wa Angani kilikuwa nao katika mwaka wa 1965.” Gazeti hilohilo linasema hivi pia: “Kwa kila wanadamu wawili duniani, mmoja ana simu ya mkononi,” na angalau nchi 30 zina simu nyingi kuliko watu. Kwa kweli, tunajionea “kuenea kwa kasi sana kwa teknolojia kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya wanadamu,” linasema gazeti hilo.
Ulimwenguni pote, karibu asilimia 60 ya watumiaji wa simu za mkononi wanaishi katika nchi zinazoendelea. Kwa sababu hiyo, simu za mkononi ndicho kifaa cha teknolojia kinachotumiwa zaidi na watu katika nchi hizo. Kwa mfano, nchini Afghanistan, kulikuwa na watumiaji wapya 140,000 hivi kila mwezi katika mwaka wa 2008, na katika miaka ya karibuni bara la Afrika limeshuhudia ongezeko la asilimia 50 hivi la watumiaji wa simu za mkononi kila mwaka.
Hata hivyo, maendeleo makubwa katika teknolojia ya mawasiliano yameleta matatizo. Simu za mkononi, peja, na kompyuta zinazoweza kubebwa zimefanya watu waweze kufikiwa kwa urahisi wakati wowote, mahali popote pale. Hilo limefanya watu wengine wahisi wamenaswa na teknolojia. Kwa upande ule mwingine, kuna “waraibu” wa teknolojia, ambao huhisi kwamba ni lazima wajue kila kitu kinachoendelea.
“Uraibu,” kukengeushwa, kuvurugwa—huenda hayo ndiyo matatizo makubwa zaidi yanayosababishwa na teknolojia ya mawasiliano na ya kutoa habari.a Lakini vifaa hivyo pia vina faida zake. Basi, unaweza kuvitumiaje kwa usawaziko, hekima, na kwa kuwajali wengine? Makala zinazofuata zitajibu swali hilo.
[Maelezo ya Chini]
a Mfululizo wa makala hizi utazungumzia vifaa kama vile simu za mkononi, kompyuta, na televisheni, na pia kuhusu Intaneti. Kwa hiyo, isipokuwa iwe imeelezwa vingine, neno “teknolojia” linamaanisha vifaa hivyo.
-
-
Je, Ni Baraka au Laana?Amkeni!—2009 | Novemba
-
-
Je, Ni Baraka au Laana?
Dereva anashindwa kulidhibiti gari lake na kugonga mlingoti na kumjeruhi vibaya abiria wake. Mara moja, anatumia simu yake ya mkononi kuomba msaada. Lakini kwa nini alishindwa kulidhibiti gari lake? Alikengeushwa fikira kidogo alipokuwa akijibu simu yake ya mkononi.
KAMA mfano huo unavyoonyesha, kifaa cha teknolojia kinaweza kuwa baraka au laana—uamuzi ni wako. Hata hivyo, watu wengi hawangependa kutumia vifaa vya zamani vilivyopitwa na wakati. Kwa mfano, kompyuta inatupunguzia kazi nyingi, inatuwezesha kununua vitu na kufanya shughuli za benki kupitia Intaneti, na hata inatuwezesha kuwasiliana na wengine.
Juzijuzi tu watu wa familia walikuwa wakiachana asubuhi na hawakuwasiliana tena hadi jioni. Lakini sasa, “asilimia 70 ya wenzi wa ndoa walio na simu za mkononi hupigiana simu kila siku ili kujuliana hali, asilimia 64 huwasiliana ili kupanga ratiba zao, na asilimia 42 ya wazazi huwasiliana na watoto wao kila siku kupitia simu ya mkononi,” inasema ripoti katika gazeti USA Today.
Usipuuze Madhara ya Teknolojia
Je, mtu anaweza kupata madhara ya kiakili na kimwili kwa kuitumia teknolojia kupita kiasi au vibaya? Fikiria mfano wa wenzi waliooana hivi karibuni katika nchi moja huko Ulaya. Kulingana na ripoti moja, wenzi hao “walikuwa wakiwasiliana kila mara kupitia simu za mkononi—wakiwa ndani ya magari yao, kwenye chumba cha kufanyia mazoezi, hata waliwasiliana kwa simu nyumbani wakiwa katika vyumba tofauti.” Pindi fulani, walizungumza kwenye simu kwa dakika 4,000 kwa mwezi, yaani, zaidi ya saa 66, na walisema kwamba hawawezi kuishi bila simu zao. Dakt. Harris Stratyner, mtaalamu wa matatizo ya akili alisema ni “wazi kwamba wana dalili za uraibu. Ni kana kwamba uhusiano wao unategemea kifaa fulani.”
Huenda mfano huo ukaonekana kuwa wenye kupita kiasi, lakini unaonyesha tabia inayozua wasiwasi. Watu wengi wanaona kwamba hawawezi kukaa bila kutumia mfumo fulani wa kuwasiliana hata kwa saa moja. “Kila mara tunahitaji kusoma barua pepe, kutumia Intaneti, na kuwatumia marafiki wetu ujumbe mfupi,” anasema mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 20 na kitu.
Ikiwa kutumia teknolojia “kunachukua wakati wako mwingi na ndilo jambo la maana zaidi unalopenda kufanya kuliko jambo lingine lolote, hiyo ni ishara ya wazi kwamba kuna shida fulani,” anasema Dakt. Brian Yeo katika gazeti The Business Times of Singapore. Isitoshe, mara nyingi watu wanaojitenga kwa saa nyingi sana ili kutumia vifaa vyao hawafanyi mazoezi ya kutosha na hivyo wanakabili hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kisukari, au magonjwa mengine mabaya.
Madhara mengine hutukia papo hapo. Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba watu wanaoendesha gari huku wakizungumza kwenye simu walizoshika mkononi au kwa kutumia vifaa vya kuzungumza bila kuishika, hawana uwezo kamili wa kudhibiti gari kama tu dereva anayeendesha akiwa amelewa! Pia, ni hatari kuandika ujumbe mfupi wa simu huku ukiendesha gari. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 40 hivi ya madereva walio na umri wa kati ya miaka 16 na 27 huandika ujumbe mfupi huku wakiendesha gari. Na pia, ikiwa unataka kutumia simu yako ya mkononi kuzungumza au kutuma ujumbe huku ukiendesha gari, kumbuka kwamba iwapo utapata aksidenti, polisi na kampuni ya bima watachunguza ikiwa simu yako ilikuwa ikitumiwa muda mfupi kabla ya aksidenti hiyo. Kuzungumza kwenye simu au kuandika ujumbe mfupi kunaweza kukugharimu sana!a Uchunguzi uliofanywa baada ya aksidenti ya gari-moshi iliyosababisha vifo vya watu 25 iliyotokea mwaka wa 2008 huko California, Marekani, ulionyesha kwamba dereva alikuwa ametuma ujumbe mfupi sekunde chache tu kabla ya aksidenti hiyo. Hata hakuwa na wakati wa kufunga breki.
Kwa sababu watoto wengi hutumia simu za mkononi na kompyuta, na pia vifaa vingine vya teknolojia, wanahitaji kujifunza jinsi ambavyo wanaweza kutumia vifaa hivyo vizuri. Wanaweza kusaidiwa jinsi gani? Tafadhali soma makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Wote wanaojitahidi kuishi kupatana na mafundisho ya Biblia wanapaswa kuwa waangalifu wasikengeushwe na kitu chochote kinachoweza kusababisha hali yoyote hatari.—Mwanzo 9:5, 6; Waroma 13:1.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Je, kutumia teknolojia kunachukua wakati wako mwingi?
-
-
Wazazi—Waongozeni Watoto WenuAmkeni!—2009 | Novemba
-
-
Wazazi—Waongozeni Watoto Wenu
“Zamani tulikuwa na wasiwasi kwamba watoto walikuwa wakitumia wakati mwingi wakitazama televisheni. Sasa tuna michezo ya video, kompyuta, na simu za mkononi. Watoto hawawezi kujidhibiti wasitumie vitu hivyo kupita kiasi na kwa sababu hiyo ni kana kwamba wanakuwa waraibu wa teknolojia . . . Ubongo wao huzoea kusisimuliwa na mambo wanayoona na kusikia—na wanapokosa vitu hivyo, hawajui la kufanya.”—Mali Mann, M.D.
TUNAISHI katika ulimwengu “uliounganishwa” kwa sababu ya maendeleo katika teknolojia ya mawasiliano na Intaneti. Vijana wengi hawawezi kuondoka nyumbani bila vifaa vyao vidogo vya kuchezea muziki au video au simu zao za mkononi. Na kadiri vifaa hivyo na vinginevyo vinavyozidi kuwa vya hali ya juu, vyenye matumizi mengi, na kupatikana kwa bei nafuu, ndivyo vifaa vya mawasiliano ambavyo tayari viko kwa wingi vitakavyozidi kuongezeka na kufanya iwe vigumu hata zaidi kwa wazazi kuwasimamia, kuwazoeza, na kuwatia nidhamu watoto wao.
Wazazi wanaweza kukabiliana na hali hiyo iwapo watafanya mambo mawili muhimu. Kwanza, watambue ukweli wa maneno yafuatayo yanayopatikana katika Biblia kwenye Methali 22:15: “Mtoto hupenda mambo ya kijinga moyoni, lakini fimbo ya nidhamu humwondolea hayo.” (Biblia Habari Njema) Pili, waelewe kwamba teknolojia inaweza kuwa na uvutano mzuri au mbaya kwa watoto wao, na wajitahidi kuwasaidia waitumie kwa njia nzuri.
Anza Mapema!
Katika nyumba nyingi, televisheni ndio teknolojia ya kwanza ambayo huwa na uvutano kwa watoto. Kwa kweli, televisheni hutumiwa kama mlezi wa watoto. Hata hivyo, wataalamu fulani wa magonjwa ya akili wanaamini kwamba watoto wanapoanza kutazama televisheni wakiwa wachanga sana au wanapoitazama kupita kiasi, hilo linaweza kuwafanya wasipende kufanya mazoezi, wasiweze kupambanua kati ya mambo halisi na ya kuwaziwa, wawe na matatizo ya kihisia, na baadaye wakiwa shuleni, wasiweze kukaza fikira. Dakt. Mali Mann, anasema kwamba huenda baadhi ya watoto “wakafikiriwa kimakosa kwamba wana Tatizo la Upungufu wa Makini [ADD] au Tatizo la Upungufu wa Makini Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi [ADHD] au hata kwamba wana ugonjwa wa kubadilika-badilika hisia.” Kwa hiyo, wataalamu fulani wanapendekeza kwamba watoto walio na umri wa chini ya miaka miwili wasitazame televisheni.
“Jambo muhimu zaidi ambalo hutukia katika miaka ya kwanzakwanza ya mtoto ni kwamba anasitawisha uhusiano wa karibu sana pamoja na wazazi wake,” anasema Dakt. Kenneth Ginsburg, msemaji wa Chuo cha Marekani cha Tiba ya Watoto. Uhusiano huo husitawishwa wazazi wanapozungumza na kucheza na watoto wao na hata kuwasomea vitabu. Na kama wazazi wengi wanavyojua, watoto ambao husomewa kwa ukawaida wanakuwa na hamu ya kusoma, na hilo ni jambo lingine muhimu.
Kwa kweli, kuwa na ujuzi wa kutumia kompyuta na teknolojia nyingine zinazohusiana nayo ni muhimu, na huenda hata ni lazima kwa mamilioni ya watoto. Hata hivyo, unapotambua kwamba watoto wanakazia fikira kwa njia isiyo ya kawaida kompyuta, michezo ya kompyuta, Intaneti, na vitu kama hivyo, lingekuwa jambo la busara kuwasaidia wapendezwe na mambo mengine. Jinsi gani? Mbona usiwafundishe sanaa au ala ya muziki—jambo lolote litakalowafanya wakaze fikira zao, na kuwasisimua?
Huenda utendaji uliochaguliwa vizuri ukatimiza mengi zaidi ya kuburudisha tu. Huenda ukamsaidia mtoto wako kuwa na sifa kama vile udumifu, ubunifu, subira, na kujizuia. Sifa hizo ni muhimu maishani hasa wakati ambapo teknolojia haiwezi kutatua matatizo yetu yote.
Watoto Wanahitaji ‘Hekima na Uwezo wa Kufikiri’
Biblia inawatia moyo watu wazima na watoto wasitawishe ‘nguvu za kufikiri,’ au uwezo wa kufikiri. (Waroma 12:1; Methali 1:8, 9; 3:21) Hilo hutusaidia si kutofautisha tu yaliyo sawa na yaliyo makosa, bali pia mambo yenye hekima na yale yasiyo ya hekima. Kwa mfano, si makosa kutumia wakati mwingi kucheza michezo ya kompyuta au kutazama televisheni, lakini je, hilo ni jambo lenye hekima? Si makosa kununua vifaa vipya vya kiteknolojia, lakini je, hilo ni jambo lenye hekima? Basi, utawasaidia watoto wako jinsi gani kufanya maamuzi yenye hekima kuhusu teknolojia?
◼ Waeleze hatari zinazohusika. Ni rahisi sana kwa watoto kujifunza kutumia vifaa vya teknolojia na Intaneti, lakini kwa kuwa hawana hekima na ujuzi, nyakati nyingine wao hutenda kwa njia ya kijinga. Kwa hiyo, waeleze hatari zinazohusika na jinsi ambavyo wanaweza kuziepuka. Kwa mfano, fikiria vituo vya mawasiliano. Ni kweli kwamba huenda vituo hivyo vikawawezesha vijana kujitambulisha na kukutana na vijana wengine, lakini vituo hivyo pia hutumiwa na watu wanaowavizia watoto ili wafanye ngono nao na pia watu wengine wenye nia mbaya.a (1 Wakorintho 15:33) Kwa sababu hiyo, wazazi wenye hekima huwashauri watoto wao wasiweke habari zao za kibinafsi kwenye Intaneti.b
Bila shaka, watoto wana haki ya kuwa na faragha ikitegemea kiwango cha ukomavu wao. Lakini ukiwa mzazi, una mamlaka na daraka kutoka kwa Mungu la kuwazoeza na kuwasimamia watoto wako. (Methali 22:6; Waefeso 6:4) Inatumainiwa kwamba hawataona ni kana kwamba unawaingilia bila sababu bali watatambua kwamba unawajali na kuwapenda.
Huenda ukasema, “Ninaweza kuwasaidiaje watoto wangu ikiwa sijui kutumia vifaa wanavyotumia?” Mbona usijifunze mambo machache kuhusu vifaa hivyo? Melba, mwenye umri wa zaidi ya miaka 90 hakuwa amewahi kugusa kompyuta hadi alipokuwa na umri wa zaidi ya miaka 80. Anasema hivi: “Nilipojaribu kutumia kitu hicho, nilitaka kukitupa nje. Lakini baada ya miezi kadhaa, niliweza kukitumia, na sasa ninaweza kuandika barua pepe na kufanya mambo mengine kwa urahisi.”
◼ Mpangie mtoto wako wakati hususa wa kutumia vifaa vya teknolojia. Ikiwa mtoto wako anajitenga kwa saa nyingi akitazama televisheni, akitumia Intaneti, au kucheza michezo ya kompyuta, mbona usifikirie kutenga wakati au mahali ndani ya nyumba ambapo vifaa vya teknolojia havitatumiwa? Hilo linaweza kumsaidia mtoto wako ajifunze umuhimu wa kufuata kanuni hii ya Biblia: “Kuna wakati uliowekwa wa kila kitu.” Hilo linamaanisha kwamba kuna wakati wa kuwa pamoja na familia, wakati wa kuwa pamoja na marafiki, wakati wa kufanya kazi za shule, wakati wa kula, wakati wa kufanya mazoezi, na kadhalika. (Mhubiri 3:1) Kuweka sheria zenye usawaziko zisizobadilishwa-badilishwa, kunafanya familia iwe thabiti na kunawasaidia watoto wasitawishe tabia nzuri, wafikirie hisia za wengine, na kushirikiana nao.
Katika makala ya mwisho ya mfululizo huu, tutachunguza kanuni fulani zinazoweza kutusaidia sisi sote—watu wazima kwa watoto—tuwafikirie wengine na gharama zinazohusika, tunapotumia teknolojia.
[Maelezo ya Chini]
a Wazazi watafaidika wakisoma makala “Watoto na Intaneti—Mambo Ambayo Wazazi Wanapaswa Kujua,” katika toleo la Amkeni! la Oktoba (Mwezi wa 10) 2008. Matoleo ya Machi (Mwezi wa 3) na Desemba (Mwezi wa 12) 2007 na Januari (Mwezi wa 1) 2008 yana makala zinazofaa kuhusu ponografia, michezo ya video, na Intaneti.
b Vijana fulani pia hutumia simu zao za mkononi kuwatumia marafiki picha zao chafu. Mbali na kuwa zoea la kipumbavu na linalowashushia heshima, picha hizo husambazwa kwa wengine hata iwe mwenye kuzituma alikuwa na kusudi tofauti.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Watoto wanahitaji kuwa na utendaji mbalimbali ili waweze kupanua akili na wajifunze kuwa na subira na udumifu
-
-
Teknolojia—Fikiria Wengine na GharamaAmkeni!—2009 | Novemba
-
-
Teknolojia—Fikiria Wengine na Gharama
Katherine, ambaye ana umri wa miaka 20 na kitu, hutumia kompyuta kazini. Lakini akiwa nyumbani, yeye hujipata akitumia Intaneti kutafuta habari, kununua vitu, na kuwasiliana kupitia barua-pepe. Hata hivyo, yeye hatumii teknolojia sana akilinganishwa na wafanyakazi wenzake wenye umri mdogo. “Kwa nini wananisumbua kwa kunitumia ujumbe wa kijinga kila mara?” anauliza. “Si mimi ni mwanadamu! Mbona wasizungumze nami kwenye simu?”
SWALI hilo la Katherine linachekesha kwa kuwa mtu anapotumia simu bado hawasiliani na mwenzake uso kwa uso. Hata hivyo, hoja ya Katherine ina msingi: Huenda vifaa vingi vya teknolojia ambavyo vimekusudiwa kuwaunganisha watu, vikawatenganisha kihisia. Ili uwe na usawaziko unapotumia teknolojia, fikiria kanuni zifuatazo za Biblia.
◼ “Kwa hiyo, mambo yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, lazima mwatendee wao pia vivyo hivyo.” (Mathayo 7:12) Tukifuata maneno hayo ya Yesu Kristo tunapotumia simu za mkononi na kompyuta, tutawatendea wengine kwa heshima na kuwa na adabu. Mwanamke mmoja anayeitwa Anne anasema hivi: “Mimi na mume wangu tulikuwa katika mkahawa mmoja. Wanaume wawili walikuwa wakila chakula meza iliyokuwa kando yetu. Hata hivyo, mmoja wao alitumia muda wote akizungumza kwenye simu na kula. Tulimhurumia sana mwenzake, ambaye ni kana kwamba alikuwa akila peke yake.” Ungehisije ikiwa ungekuwa pamoja na mwanamume huyo? Ungeumia? Au ungeudhika? Hata kama tunaweza kutumia simu zetu za mkononi mahali popote, wakati wowote, haimaanishi kwamba tufanye hivyo. Kanuni iliyo katika maneno ya Yesu inapaswa kutuongoza.
◼ “Endeleeni kuangalia sana kwamba jinsi mnavyotembea si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima, mkijinunulia wakati unaofaa.” (Waefeso 5:15, 16) Wakati ni zawadi yenye thamani kutoka kwa Mungu na haupaswi kupotezwa. Ni kweli kwamba teknolojia inaweza kuokoa wakati. Kwa mfano, mtu anaweza kufanya utafiti, shughuli za benki, na kununua vitu haraka akitumia Intaneti. Lakini pia anaweza kupoteza muda mwingi akirandaranda kwenye Intaneti bila kusudi lolote.
Pia mtu anaweza kupoteza wakati mwingi akijaribu kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja, kama vile, kutumia kompyuta huku ukitazama televisheni, kuzungumza kwenye simu, au kujaribu kutuma barua-pepe huku ukijaribu kufungua programu nyingine za kompyuta. Kwa nini kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja hakuleti matokeo mazuri?
Dakt. Jordan Grafman mtaalamu wa mfumo wa neva anasema kwamba “mtu hawezi kupata ujuzi mwingi wa kazi yoyote anapojaribu kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja.” Hatuwezi kukazia fikira mambo kadhaa wakati uleule; kuna jambo fulani ambalo hatutafanya vizuri. Tunapojaribu kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja huenda tukayafanya kijuujuu tu na hatutayakumbuka vizuri. Pia, kufanya jambo moja na kisha kubadilika haraka kufanya lingine, huwafanya watu wakosee mara nyingi zaidi na “kunachukua muda mrefu zaidi—huenda hata mara mbili au zaidi ya wakati ambao wangetumia ikiwa wangefanya kazi hizo kwa mpango,” inasema ripoti fulani katika gazeti Time. Kwa hiyo, usifanye mambo kadhaa kwa wakati mmoja; huenda usitimize mambo ambayo ulitaka kutimiza!
◼ “Mjilinde na kila namna ya tamaa, kwa sababu hata wakati mtu ana vitu vingi uzima wake hautokani na vitu alivyo navyo.” (Luka 12:15) Vitu vya kimwili hata viwe vya gharama au vya kifahari namna gani haviwezi kumpa mtu uhai au furaha ya kweli. Ni Mungu peke yake anayeweza kufanya hivyo. Yesu alisema: “Wenye furaha ni wale wanaotambua uhitaji wao wa kiroho.” (Mathayo 5:3) Kwa upande ule mwingine, ulimwengu wa kibiashara unasema kwamba furaha ya kweli inatokana na vitu vya kimwili. ‘Nunua, nunua, nunua,’ ndivyo ulimwengu huo unavyosema. ‘Unapaswa kuwa na vitu vya kisasa zaidi.’ Usidanganyike. Badala yake, uwe na hekima. Kabla ya kutumia pesa, chunguza nia yako ni nini na kama unahitaji kitu fulani. Kumbuka pia kwamba vifaa vingi vya hali ya juu hupoteza thamani upesi sana. Kwa hiyo, ikiwa unahitaji kifaa fulani, jiulize hivi: ‘Je, ni lazima niwe na kifaa cha kisasa zaidi? Na je, ninahitaji kifaa kilicho na mambo ya ziada yanayogharimu sana, ambayo huenda sitawahi kuyatumia?’
Baraka au Laana—Uamuzi Ni Wako
Katherine, aliyetajwa awali, alipatwa na wasiwasi mwingi kompyuta yake ya nyumbani ilipoharibika. “Mwanzoni nilipatwa na mshtuko,” anasema, “lakini nikaamua sitanunua nyingine haraka. Baada ya mwezi mmoja, nilitulia na nikapata muda mwingi wa kusoma. Ninatumia kompyuta kazini, kwa hiyo ninaweza kuendelea kuwasiliana na rafiki zangu baada ya kazi. Lakini sihisi tena ni kana kwamba ninahitaji kupata habari kila wakati. Teknolojia haiongozi maisha yangu tena.”
Kwa kweli, vifaa vingi vya sayansi na teknolojia vinafaa na vinaweza kuokoa wakati na nguvu zetu nyingi. Vitumie ikiwa tu ni lazima, lakini ufanye hivyo kwa hekima na kwa kuwafikiria wengine. Jinsi gani? Watangulize wanadamu wenzako badala ya kutanguliza teknolojia. Usipoteze wakati na pesa kwa kununua vifaa au programu za kompyuta usizohitaji. Usitumie Intaneti na vifaa vingine kutazama picha chafu na jeuri. Na usiwe “mraibu” wa teknolojia. Kwa ufupi, uwe na hekima—tumia kanuni ambazo zimethibitika kuwa zinafaa, zilizoongozwa na roho ya Mungu ambazo zinapatikana katika Biblia Takatifu, Neno la Mungu lililoandikwa. Naam, “Yehova mwenyewe anatoa hekima; kinywani mwake hutoka ujuzi na utambuzi.”—Methali 2:6.
[Sanduku katika ukurasa wa 9]
KUTUMIA SIMU NA KOMPYUTA KWA ADABU
Unaweza kutumiaje simu ya mkononi na kompyuta kwa njia inayoonyesha kwamba unawajali wengine? Fikiria mambo yafuatayo.
◼ Epuka kupiga au kupokea simu wakati na mahali ambapo utawasumbua wengine. Ikiwezekana, zima simu yako.
◼ Ikiwa unazungumza na mtu ana kwa ana, usiruhusu simu ikatize mazungumzo hayo isipokuwa iwe lazima kufanya hivyo.
◼ Unapozungumza kwenye simu, mkazie fikira yule unayezungumza naye.
◼ Usimpige mtu picha kwa kutumia simu yako ya mkononi ikiwa utamkosea heshima au utamwaibisha kwa kufanya hivyo.
◼ Epuka kishawishi cha kuwatumia watu barua-pepe yoyote unayopata hata ingawa huenda ikaonekana kuwa yenye kupendeza sana. Huenda wale unaowatumia wasifurahie kuipokea.
-