Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Watoto Watishwa
    Amkeni!—2006 | Juni
    • Watoto Watishwa

      Inapofika jioni, utaona maelfu ya watoto wakitembea miguu mitupu kwenye barabara zilizo kaskazini mwa Uganda. Wao huondoka vijijini mwao kabla ya giza kuingia wakielekea kwenye miji kama vile Gulu, Kitgum, na Lira. Wanapofika huko, wanatawanyika na kuelekea kwenye majengo, vituo vya basi, bustani, na nyua. Kunapopambazuka, unawaona tena barabarani wakirudi nyumbani. Kwa nini kila siku wao hufunga safari hiyo isiyo ya kawaida?

      WATU fulani huwaita wasafiri wa usiku. Lakini watoto hao hawaendi kufanya kazi usiku. Wao huondoka nyumbani jioni kwa sababu giza linapoingia, sehemu za mashambani wanakoishi huwa hatari.

      Kwa miaka 20 hivi, waasi wamekuwa wakivamia sehemu hizo za mashambani na kuwateka nyara watoto. Kila mwaka wao huteka mamia ya wavulana na wasichana kutoka nyumbani na kupotelea msituni. Mara nyingi watoto hao hutekwa nyara usiku nao hutumiwa na waasi hao kama askari, wabebaji wa mizigo, na wasichana wa kufanya ngono nao. Mateka hao wasipotii, huenda wakakatwa pua au midomo. Wale ambao hujaribu kutoroka hukamatwa na kuuawa kikatili.

      Kuna wahasiriwa wengine wachanga wa ugaidi. Huko Sierra Leone, vijana ambao ni vilema walikuwa wachanga sana wakati wanaume wenye mapanga walipokata miguu na mikono yao. Wavulana na wasichana huko Afghanistan hucheza na mabomu ya ardhini yanayofanana na vipepeo nao hupoteza vidole na macho yao vitu hivyo vya kuchezea vyenye kuvutia vinapolipuka.

      Vijana fulani huathiriwa kwa njia tofauti kunapotokea shambulizi la kigaidi. Kwa mfano, katika shambulizi la kigaidi lililofanywa 1995 huko Oklahoma City, Marekani, kati ya watu 168 waliouawa kulikuwa na watoto 19 na baadhi yao walikuwa vitoto. Kama tu upepo wenye nguvu unavyozima mishumaa, bomu hilo lilikomesha mara moja uhai wa vitoto hivyo. Shambulizi hilo la kigaidi liliwapokonya watoto hao maisha yao, likawazuia wasicheze, wasicheke wala kupakatwa na mama na baba zao.

      Hayo ni matukio ya hivi karibuni, lakini kama tutakavyoona, wanadamu wamekumbwa na vitendo vya kigaidi kwa miaka mingi.

      [Sanduku katika ukurasa wa 3]

      KUJITAYARISHIA KIFO CHA MTOTO

      “Leo asubuhi nilipomwamsha mwanangu mwenye umri wa miaka 11, aliniuliza, ‘Je, tayari magaidi wameshambulia leo?’” Ndivyo alivyoandika mwandishi David Grossman kuhusu jeuri inayoendelea katika nchi anamoishi. Aliendelea kusema hivi: “Mwanangu anaogopa.”

      Katika miaka ya karibuni, watoto wengi sana wamekufa katika mashambulizi ya kigaidi hivi kwamba wazazi wengi hujitayarisha iwapo mtoto wao anaweza kuuawa kijeuri. “Sitasahau kamwe jinsi wapenzi wawili walivyonieleza kuhusu mipango yao ya wakati ujao,” akaandika Grossman. “Walisema watafunga ndoa na kupata watoto watatu. Si wawili, bali watatu. Ili iwapo mmoja atakufa, wawili watabaki.”

      Hawakusema jambo watakalofanya iwapo watoto wawili wangekufa, au wote watatu.a

      [Maelezo ya Chini]

      a Manukuu haya yametoka katika kitabu Death as a Way of Life, cha David Grossman.

  • Historia Iliyojaa Umwagaji wa Damu
    Amkeni!—2006 | Juni
    • Historia Iliyojaa Umwagaji wa Damu

      MIAKA michache tu iliyopita, ilionekana kwamba ugaidi ulitukia tu katika sehemu chache kama vile Ireland Kaskazini, eneo la Basque huko kaskazini mwa Hispania, na sehemu nyingine za Mashariki ya Kati. Sasa, hasa tangu Septemba 11, 2001, wakati majengo ya Twin Towers yalipoharibiwa huko New York, ugaidi umeongezeka haraka ulimwenguni pote. Umetukia kwenye kisiwa maridadi cha Bali; Madrid, Hispania; London, Uingereza; Sri Lanka; Thailand, na hata Nepal. Hata hivyo, ugaidi si jambo geni. Neno “ugaidi” linamaanisha nini?

      Ugaidi umefafanuliwa kuwa “matumizi au vitisho vya kutumia nguvu kiharamu au jeuri inayofanywa na mtu ama kikundi dhidi ya watu au mali kwa lengo la kutisha au kulazimisha jamii ama serikali, kwa sababu ya kutekelezwa kwa mawazo yao au kwa sababu za kisiasa.” (The American Heritage Dictionary of the English Language) Hata hivyo, mwandishi Jessica Stern anasema: “Mtu anayechunguza ugaidi hupata kwamba neno hilo lina ufafanuzi mwingi . . . Lakini ni mambo mawili tu ambayo hutofautisha ugaidi na jeuri ya aina nyingine.” Ni mambo gani hayo? “Kwanza, ugaidi hulenga raia. . . . Pili, magaidi hutumia jeuri kutimiza kusudi kubwa: kuwafanya walengwa waogope huwa muhimu kuliko madhara yanayotokana na ugaidi. Kutokeza woga kimakusudi kwa njia hiyo ndiko hutofautisha ugaidi na mauaji au mashambulizi ya kawaida.”

      Ugaidi Ulianza Zamani

      Katika Yudea ya karne ya kwanza, kikundi fulani cha Wayahudi washupavu kilipigania uhuru kutoka kwa Waroma. Baadhi ya wafuasi wake sugu waliitwa Wasikarii, au wanaume wenye kutumia visu, jina linalotokana na panga fupi walizoficha ndani ya nguo zao. Wakichangamana na umati uliokuja kwenye sherehe huko Yerusalemu, Wasikarii walikata koo za adui zao au kuwadunga kisu mgongoni.a

      Mnamo 66 W.K., kikundi hicho shupavu kilitwaa ngome ya Masada karibu na Bahari ya Chumvi. Walichinja kikosi cha askari Waroma na kufanya ngome hiyo ya mlimani kuwa kituo chao. Kwa miaka mingi, walitumia kituo hicho kuwashambulia na kuwasumbua wanajeshi Waroma. Mnamo 73 W.K., Kikosi cha Kumi cha Roma kikiongozwa na Gavana Flavio Silva kiliteka tena Masada lakini hakikushinda washupavu hao. Mwanahistoria mmoja aliyeishi wakati huo anadai kwamba badala ya kusalimu amri ya Roma, washupavu 960 kati yao walijiua isipokuwa tu wanawake wawili na watoto watano.

      Watu fulani huona uasi huo wa washupavu hao kuwa mwanzo wa ugaidi. Vyovyote vile, tangu wakati huo, ugaidi umeathiri sana ulimwengu.

      Ugaidi Umetumiwa na Jumuiya ya Wakristo

      Kuanzia mwaka wa 1095 na kuendelea kwa karne mbili, majeshi yaliyopigana “vita vitakatifu” yalipitapita kwa ukawaida kati ya Ulaya na Mashariki ya Kati. Majeshi ya Waislamu kutoka Asia na Afrika Kaskazini yalipigana nao. Wote walitaka kumiliki Yerusalemu, na kila upande ulijaribu kuushinda ule mwingine. Katika vita vingi walivyopigana, hao “wapiganaji watakatifu” walichinjana kikatili. Pia waliwakatakata watu wasio na hatia kwa mapanga na mashoka. William wa Tyre, kasisi aliyeishi karne ya 12, alieleza hivi kuhusu jinsi “wapiganaji watakatifu” walivyovamia Yerusalemu mnamo 1099:

      “Wote waliandamana barabarani wakiwa wamebeba mapanga na mikuki. Walikatakata na kuua kila mtu waliyekutana naye, wanaume, wanawake, na watoto, bila kuacha yeyote. . . . Waliua watu wengi sana hivi kwamba maiti zilitapakaa barabarani na ilibidi watu wapite juu ya miili hiyo. . . . Kulikuwa na umwagaji mwingi sana wa damu hivi kwamba mitaro ilijaa damu na barabara zote za mji zilijaa maiti.”b

      Katika karne zilizofuata, magaidi walianza kutumia vitu vinavyolipuka na bunduki zinazoweza kuua kikatili.

      Mamilioni Wafa

      Wanahistoria huona Juni 28, 1914, kuwa siku iliyobadili historia ya Ulaya. Kijana mmoja, ambaye watu fulani humwona kuwa shujaa alimpiga risasi Mwana-mfalme wa Austria, Francis Ferdinand. Tukio hilo liliwatumbukiza wanadamu kwenye Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Kabla ya hivyo Vita Vikuu kwisha, watu milioni 20 walikuwa wamekufa.

      Juni 28, 1914, ulimwengu uliingia vitani

      Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilifuatwa na Vita vya Pili vya Ulimwengu ambavyo vilikuwa na kambi za mateso, raia waliuawa kwa mabomu, na matendo ya kulipiza kisasi kwa kuua watu wasio na hatia. Baada ya vita hivyo, mauaji yaliendelea. Zaidi ya watu milioni moja waliuawa katika vita huko Kambodia miaka ya 1970. Na bado Wanyarwanda hawajasahau mauaji ya watu zaidi ya 800,000 katika miaka ya 1990.

      Tangu mwaka wa 1914 hadi wakati wetu, wanadamu wameteseka sana kwa sababu ya matendo ya ugaidi katika nchi nyingi. Hata hivyo, watu fulani leo hutenda kana kwamba hawajajifunza chochote kutokana na historia. Kwa kawaida, mashambulizi ya kigaidi yameua mamia, yakalemaza maelfu, na kuwapokonya mamilioni amani ya akili na usalama. Mabomu hulipuka kwenye masoko, vijiji huteketezwa kabisa, wanawake hulalwa kinguvu, watoto hutekwa nyara, na watu hufa. Licha ya sheria na shutuma za ulimwenguni pote, matendo haya ya kinyama hayakomi. Je, kuna tumaini lolote kwamba ugaidi utakwisha?

      a Kama inavyotajwa katika Matendo 21:38, kamanda mmoja wa jeshi la Roma alimshtaki isivyo haki mtume Paulo kuwa kiongozi wa wanaume 4,000 “wenye kutumia visu.”

      b Yesu aliwafundisha wanafunzi wake ‘wawapende adui zao,’ badala ya kuwachukia na kuwaua.—Mathayo 5:43-45.

  • Hatimaye Amani Duniani!
    Amkeni!—2006 | Juni
    • Hatimaye Amani Duniani!

      WATU fulani wanaamini kwamba wanaweza kupata uhuru wa kisiasa na kuwa safi kiroho kupitia tu jeuri. Wanaamini kwamba viongozi wasiotakikana wanaweza kuondolewa tu kupitia jeuri. Pia serikali fulani hutumia vitisho ili kudumisha utengamano na kudhibiti raia zake. Lakini ikiwa ni kweli kwamba kutumia vitisho ndiyo njia bora ya kutawala na kuleta mabadiliko ya kijamii, basi mambo hayo yanapaswa kuleta amani, ufanisi, na utulivu. Baada ya muda, jeuri na hofu zinapaswa kupungua. Je, imekuwa hivyo?

      Ukweli ni kwamba ugaidi hufanya watu wasiheshimu uhai na husababisha umwagaji wa damu na ukatili. Kwa sababu ya uchungu wanaohisi, mara nyingi wahasiriwa wa ugaidi hulipiza kisasi, jambo ambalo hufanya wakandamizwe zaidi, na hilo hufanya walipize kisasi tena.

      Jeuri Haisuluhishi Matatizo Yetu

      Kwa maelfu ya miaka, wanadamu wamekuwa wakijaribu kujisuluhishia matatizo yao ya kisiasa, kidini, na kijamii. Lakini hawajafua dafu. Ni kama vile isemavyo Biblia: “Ninajua vema, Ee Yehova, kwamba njia ya mtu wa udongo haimo katika uwezo wake. Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.” (Yeremia 10:23) Yesu alisema: “Hekima husimama na kuanguka kwa matokeo [yake].” (Mathayo 11:19, The New Testament in Modern English, ya J. B. Phillips) Kanuni hizo za Biblia zinaweza kutumiwa kuonyesha kwamba ugaidi ni tumaini bandia. Badala ya kutokeza uhuru na furaha, ugaidi umetokeza kifo, taabu, na uharibifu. Matunda hayo yasiyofaa yalienea katika karne ya 20 na yanaanza kuenea pia katika karne ya 21. Watu wanasema kwamba badala ya kutatua matatizo, ugaidi ni mojawapo ya matatizo hayo.

      “Kila siku mimi huomba kwamba mtu yeyote katika familia yetu au rafiki yangu asife . . . Labda tunahitaji muujiza.” Akasema msichana mmoja mchanga ambaye nchi yao ilikuwa imekumbwa na ugaidi. Maneno yake yanaunga mkono mkataa ambao watu wengi wamefikia: Wanadamu hawawezi kutatua matatizo yao. Ni Muumba wa mwanadamu peke yake anayeweza kutatua matatizo yanayoukumba ulimwengu sasa kutia ndani ugaidi. Lakini kwa nini tumtumaini Mungu?

      Kwa Nini Tumtumaini Mungu?

      Sababu moja ni kwamba akiwa Muumba, Yehova alitupa uhai naye anataka tuufurahie tukiwa na amani na uradhi. Nabii wa Mungu Isaya alichochewa kuandika: “Sasa, Ee Yehova, wewe ni Baba yetu. Sisi ni udongo, nawe ni Mfinyanzi wetu; nasi sote ni kazi ya mkono wako.” (Isaya 64:8) Yehova ndiye Baba ya wanadamu wote, na watu wa mataifa yote ni wenye thamani kwake. Hapaswi kulaumiwa kwa ukosefu wa haki na chuki inayotokeza ugaidi. Mfalme Sulemani mwenye hekima alisema hivi pindi moja: “Mungu wa kweli aliwafanya wanadamu wakiwa wanyoofu, lakini wao wenyewe wametafuta mipango mingi.” (Mhubiri 7:29) Ugaidi hautokezwi kwa sababu Mungu hana uwezo wa kuuzuia bali unatokezwa na uovu wa wanadamu na uvutano wa roho waovu.—Waefeso 6:11, 12.

      Sababu nyingine ya kumtumaini Yehova ni kwamba kwa kuwa yeye amewaumba wanadamu, anaelewa vizuri kuliko mtu mwingine yeyote kile kinachosababisha matatizo ya wanadamu na jinsi yanavyopaswa kutatuliwa. Biblia inataja ukweli huo kwenye Methali 3:19: “Kwa hekima Yehova mwenyewe aliuweka msingi wa dunia. Aliziweka mbingu imara kwa utambuzi.” Akiwa na tumaini kamili katika Mungu, mwanamume fulani wa zamani za kale aliandika hivi: “Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu unatoka kwa Yehova, Mtengenezaji wa mbingu na dunia.”—Zaburi 121:1, 2.

      Kuna sababu ya tatu ya kumtumaini Mungu: Ana nguvu za kuzuia umwagaji wa damu. Katika wakati wa Noa ‘dunia ilijaa jeuri.’ (Mwanzo 6:11) Hukumu ya Mungu ilikuja kwa ghafula na ilikuwa kamili: “[Mungu] hakujizuia kuuadhibu ulimwengu wa kale . . . alipoleta gharika juu ya ulimwengu wa watu wasiomwogopa Mungu.”—2 Petro 2:5.

      Biblia inataja jambo ambalo tunapaswa kujifunza kutokana na Gharika ya siku za Noa: “Yehova anajua jinsi ya kuwakomboa watu wenye ujitoaji-kimungu kutoka katika jaribu, lakini kuwaweka akiba watu wasio waadilifu kwa ajili ya ile siku ya hukumu ili wakatiliwe mbali.” (2 Petro 2:9) Mungu anaweza kutofautisha kati ya watu wanaopenda kuishi maisha bora na wale wanaofanya maisha ya wengine yawe machungu. Amewaweka akiba wale wanaofanya maisha ya wengine yawe machungu kwa ajili ya “kuangamizwa kwa watu wasiomwogopa Mungu.” Lakini kwa wote wanaopenda amani, anatayarisha dunia mpya ambamo uadilifu utakaa.—2 Petro 3:7, 13.

      Amani ya Kudumu Duniani!

      Mara nyingi waandikaji wa Biblia walitumia neno “dunia” kumaanisha wanadamu. Kwa mfano, andiko la Mwanzo 11:1 linasema kwamba “dunia yote,” yaani, wanadamu wote waliokuwa hai wakati huo, walizungumza lugha moja. Mtume Petro alimaanisha hilo alipoandika kuhusu “dunia mpya.” Yehova Mungu atafanya upya jamii ya kibinadamu katika njia ya kwamba jeuri na chuki itaondolewa kabisa na badala yake uadilifu na haki “zitakaa” duniani. Biblia inatuambia hivi katika unabii wa Mika 4:3: “Naye hakika atafanya hukumu kati ya vikundi vingi vya watu, na kunyoosha mambo kuhusu mataifa yenye nguvu yaliyo mbali. Nao watafua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu. Hawatainua upanga, taifa juu ya taifa, wala hawatajifunza vita tena.”

      Watu wataishije unabii huo utakapotimizwa? Andiko la Mika 4:4 linasema: “Nao wataketi, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakutakuwa na mtu yeyote anayewatetemesha.” Katika dunia hiyo itakayokuwa Paradiso hakuna mtu atakayeishi kwa woga wa kushambuliwa na magaidi. Je, unaweza kuamini ahadi hiyo? Ndiyo, “kwa maana kinywa cha Yehova wa majeshi kimesema hivyo.”—Mika 4:4.

      Kwa hiyo, huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuongezeka na mataifa kuishi kwa woga kwa sababu ya jeuri, suluhisho kwa watu wanaopenda amani ni kumtumaini Yehova. Hakuna tatizo asiloweza kutatua. Ataondoa majeraha, kuteseka, na hata kifo. Biblia inasema: “Yeye kwa kweli atameza kifo milele, na Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova hakika atafuta machozi katika nyuso zote.” (Isaya 25:8) Nchi nyingi nzuri ambazo sasa zimejaa taabu na woga kwa sababu ya ugaidi, hivi karibuni zitakuwa na amani tele. Amani hiyo, iliyoahidiwa na Mungu “asiyeweza kusema uwongo,” ndiyo wanadamu wanahitaji haraka.—Tito 1:2; Waebrania 6:17, 18.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

      BADALA YA KUTUMIA RISASI NA MABOMU . . .

      Yafuatayo ni maelezo ya watu waliokuwa wakiamini kwamba matendo ya jeuri yanaweza kutokeza mabadiliko ya kisiasa.

      ◼ “Niliposoma vitabu vya historia, niligundua kwamba sikuzote wafalme na wakuu wa serikali wamewakandamiza maskini. Ningeweza kuhisi jinsi watu wa hali ya chini walivyoteseka. Nilipofikiria jinsi mambo hayo mabaya yanavyoweza kukomeshwa, nilikata kauli kwamba tutahitaji kupigana, kutumia silaha ili kulipiza kisasi.”—Ramon.a

      ◼ “Nilipigana kwa kutumia silaha. Kusudi langu lilikuwa kukaidi mamlaka zilizokuwapo na kuanzisha jamii ambayo itaondoa ukosefu wa usawa uliopo ulimwenguni.”—Lucian.

      ◼ “Tangu nilipokuwa mtoto, nilikerwa na ukosefu wa haki. Hilo lilitia ndani umaskini, uhalifu, elimu duni, na ukosefu wa huduma za afya. Niliamini kwamba kwa kutumia silaha, watu wote wangeweza kupata elimu, huduma za afya, nyumba na kazi. Pia niliamini kwamba mtu yeyote asiye na adabu na asiyemheshimu jirani yake anapaswa kuadhibiwa.”—Peter.

      ◼ “Mimi na mume wangu tulikuwa wanachama wa shirika fulani la siri lililochochea uasi wenye jeuri. Tulitumaini kwamba tungeanzisha serikali ambayo ingeleta hali nzuri, utengamano na usawa kwa wote. Tulihisi kwamba kupinga serikali ndiyo njia pekee ya kupata haki katika nchi yetu.”—Lourdes.

      Watu hao walijaribu kusaidia wanadamu wanaoteseka kwa kutumia nguvu. Lakini walipojifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, walitambua kwamba Neno la Mungu lina suluhisho bora. Biblia inasema hivi kwenye Yakobo 1:20: “Kwa maana ghadhabu ya mwanadamu haitokezi uadilifu wa Mungu.” Biblia Habari Njema inasema: “Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.”

      Ni utawala wa Mungu tu unaoweza kubadili jamii ya kibinadamu. Unabii wa Biblia kama ule unaopatikana katika Mathayo sura 24 na 2 Timotheo 3:1-5 unaonyesha kwamba serikali ya Mungu iko karibu kutekeleza jambo hilo. Tunakutia moyo uchunguze kweli hizo kwa kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova.

      [Maelezo ya Chini]

      a Majina yamebadilishwa.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki