Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kesi Iliyoendeshwa Vibaya Zaidi Kuliko Zote
    Mnara wa Mlinzi—2011 | Aprili 1
    • Utaratibu wa Kisheria Wavunjwa

      Sheria ambayo Musa aliwapa Waisraeli imetajwa kuwa “mfumo bora zaidi wa sheria kuwahi kuwekwa rasmi.” Hata hivyo, kufikia wakati wa Yesu, marabi ambao walipenda kutunga sheria kwa ajili ya kila jambo, walikuwa wameongeza sheria nyingi ambazo hazikuwa katika Biblia, na nyingi kati ya sheria hizo ziliingizwa katika Talmud. (Ona sanduku “Sheria za Wayahudi Katika Karne za Kwanza,” kwenye ukurasa wa 20.) Je, kesi ya Yesu iliendeshwa kulingana na sheria hizo za Biblia na zile ambazo hazikuwa katika Biblia?

      Je, kukamatwa kwa Yesu kulitokana na ushahidi unaofanana uliotolewa na mashahidi wawili kuhusu kosa lilelile? Ili kukamatwa kuwe halali ushahidi ulipaswa kufanana. Huko Palestina katika karne ya kwanza, Myahudi ambaye alikuwa na hakika kwamba sheria imevunjwa alipeleka mashtaka yake mahakamani saa za kawaida za kazi. Mahakama hazingeanza kusikiliza kesi kabla ya kufanya uchunguzi wa mashtaka yaliyoletwa. Mashahidi wa shtaka lililotolewa ndio waliokuwa waendeshaji wa kesi. Kesi ingeanza kusikilizwa ikiwa kuna angalau ushahidi wa mashahidi wawili wa kosa lilelile. Ushahidi wao ungekuwa ndio msingi wa kuunda shtaka, na hivyo mshtakiwa angekamatwa. Ushahidi wa mtu mmoja haungekubaliwa. (Kumbukumbu la Torati 19:15) Hata hivyo, katika kesi ya Yesu, Wayahudi wenye mamlaka walitafuta “njia bora” ya kumwondolea mbali. Alikamatwa wakati “nafasi nzuri” ilipotokea—usiku na “bila umati kuwa karibu.”—Luka 22:2, 5, 6, 53.

      Wakati Yesu alipokamatwa hakukuwa na shtaka lolote lililokuwa limewasilishwa. Makuhani na washiriki wa Sanhedrini, mahakama kuu ya Wayahudi, walianza kuwatafuta mashahidi baada tu ya kumkamata Yesu. (Mathayo 26:59) Hawakupata mashahidi wawili ambao ushahidi wao ulifanana. Hata hivyo, haikuwa kazi ya mahakama kutafuta mashahidi. “Kumshtaki mtu hasa kwa shtaka linalohusisha uhai, bila kutaja mapema kosa alilofanya, ni kitendo kiovu na cha kikatili,” anasema mwanasheria A. Taylor Innes ambaye pia ni mwandishi.

      Umati uliomkamata Yesu ulimpeleka katika nyumba ya Anasi, ambaye zamani alikuwa Kuhani Mkuu, naye akaanza kumuuliza maswali. (Luka 22:54; Yohana 18:12, 13) Anasi alivunja sheria ambayo ilisema kwamba mashtaka yanayohusisha adhabu ya kifo yalipaswa kusikilizwa mchana, bali si usiku. Zaidi ya hayo, uchunguzi ulipaswa kufanywa katika mahakama ya wazi, bali si mahali pa faragha. Akijua kwamba hatua ya Anasi ilikuwa kinyume cha sheria, Yesu alimjibu: “Kwa nini unaniuliza? Waulize wale ambao wamesikia lile nililowaambia. Ona! Hawa wanajua lile nililosema.” (Yohana 18:21) Anasi alipaswa kuwahoji mashahidi, bali si mshtakiwa. Maneno ya Yesu yangemchochea hakimu mnyofu kufuata utaratibu uliowekwa, lakini Anasi hakutaka kufuata haki.

      Maelezo ambayo Yesu alitoa yalifanya apigwe kofi na ofisa mmoja—huo haukuwa ujeuri pekee aliokabiliana nao usiku huo. (Luka 22:63; Yohana 18:22) Sheria iliyo katika kitabu cha Biblia cha Hesabu sura ya 35, kuhusu majiji ya makimbilio, inasema kwamba washtakiwa walipaswa kulindwa dhidi ya kutendwa vibaya hadi walipothibitika kuwa na hatia. Yesu alipaswa kupewa ulinzi huo pia.

      Umati uliomkamata Yesu ulimpeleka nyumbani kwa Kuhani Mkuu Kayafa, ambako kesi isiyo halali iliendeshwa usiku. (Luka 22:54; Yohana 18:24) Wakivunja kanuni zote za haki, makuhani walitafuta “ushahidi wa uwongo juu ya Yesu ili wamuue,” hata hivyo, hakuna mashahidi wawili ambao ushahidi wao ulifanana kuhusiana na yale ambayo Yesu alisema. (Mathayo 26:59; Marko 14:56-59) Hivyo, kuhani mkuu alijaribu kumfanya Yesu ajifunge kwa maneno yake mwenyewe. Hivyo, akamuuliza: “Je, hujibu lolote? Watu hawa wanashuhudia nini juu yako?” (Marko 14:60) Mbinu hiyo ilikuwa kinyume cha sheria. “Kumuuliza mshtakiwa maswali, ili kutafuta nafasi ya kumnasa katika majibu anayotoa, ilikuwa ni uvunjaji wa haki ya kisheria,” anasema Innes, aliyenukuliwa awali.

      Hatimaye watu hao waliamua kutumia maneno ambayo Yesu alisema. Alipoulizwa: “Wewe ndiye Kristo Mwana wa yule Mbarikiwa?” Yesu alijibu: “Mimi ndiye; nanyi mtamwona Mwana wa binadamu akiwa ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu akija pamoja na mawingu ya mbinguni.” Makuhani walisema kuwa Yesu amekufuru, na “wao wote wakamhukumu kwamba anastahili kufa.”—Marko 14:61-64.b

      Kulingana na Sheria ya Musa, kesi ilipaswa kuendeshwa mahali palipo wazi. (Kumbukumbu la Torati 16:18; Ruthu 4:1) Kwa upande mwingine, kesi hii iliendeshwa kisiri. Hakuna mtu aliyejaribu au kuruhusiwa kumtetea Yesu. Hakuna uchunguzi uliofanywa kuthibitisha madai ya Yesu kwamba alikuwa Masihi. Yesu hakupewa nafasi ya kuita mashahidi wa kumtetea. Waamuzi hawakupiga kura ili kuamua ikiwa Yesu alikuwa na hatia au hakuwa na hatia.

  • Kesi Iliyoendeshwa Vibaya Zaidi Kuliko Zote
    Mnara wa Mlinzi—2011 | Aprili 1
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]

      Sheria za Wayahudi Katika Karne za Kwanza

      Mapokeo ya Wayahudi yaliyopitishwa kwa mdomo ambayo yaliandikwa katika karne za mapema W.K. na yanayoaminika kuwa ya zamani sana, yanatia ndani kanuni zifuatazo:

      ▪ Katika kesi ambazo adhabu yake ni kifo, hoja za kutokuwa na hatia zilisikilizwa kwanza

      ▪ Waamuzi walipaswa kufanya kila jitihada ili kumwokoa mshtakiwa

      ▪ Waamuzi wangeweza tu kutoa hoja za kumtetea mshtakiwa bali si za kumtia hatiani

      ▪ Mashahidi walionywa kuhusu uzito wa daraka lao

      ▪ Mashahidi walihojiwa kila mmoja akiwa peke yake, bali si wakiwa pamoja

      ▪ Ushahidi ulipaswa kufanana katika mambo yote muhimu, kama vile, tarehe, mahali, wakati ambapo tukio lilitokea, na kadhalika

      ▪ Mashtaka katika kesi ambazo adhabu yake ni kifo yalipaswa kusikilizwa mchana na kumalizwa mchana

      ▪ Kesi ambazo adhabu yake ni kifo haikusikilizwa siku ya kuamkia Sabato au sherehe fulani

      ▪ Kesi ambazo adhabu yake ni kifo zingeweza kuanza na kumalizwa siku hiyohiyo ikiwa uamuzi ungempendelea mshtakiwa; ikiwa uamuzi haungempendelea mshtakiwa, kesi ingeamuliwa siku iliyofuata, wakati ambapo uamuzi ungetangazwa na adhabu kutekelezwa

      ▪ Kesi ambazo adhabu yake ni kifo zilisikilizwa na angalau waamuzi 23

      ▪ Waamuzi walipiga kura kwa zamu ili kumwachilia au kumhukumu mshtakiwa, wakianza na aliyekuwa mdogo zaidi kwa umri; waandishi waliandika maneno ya wale waliotaka mshtakiwa aachiliwe huru na ya wale waliotaka ahukumiwe

      ▪ Mshtakiwa angeweza kuachiliwa huru kwa kura 12, lakini ili mtu ahukumiwe kifo, kura 13 zilihitajika; ikiwa kura za kumhukumu mtu kifo zilikuwa 12, waamuzi wawili waliongezwa mara kwa mara ilipohitajika hadi uamuzi sahihi ulipofikiwa

      ▪ Uamuzi wa kwamba mshtakiwa ana hatia bila angalau mwamuzi mmoja kumtetea ulionwa kuwa si halali; ikiwa waamuzi wote walikubaliana kuwa mshtakiwa ana hatia, hiyo “ilionwa kuwa ni njama”

      Jinsi Sheria Zilivyovunjwa Wakati wa Kesi ya Yesu

      ▪ Mahakama haikusikiliza hoja au mashahidi ambao wangemtetea Yesu

      ▪ Hakuna mwamuzi hata mmoja aliyejaribu kumtetea Yesu; walikuwa maadui wake

      ▪ Makuhani walitafuta mashahidi wa uwongo ili wamhukumu Yesu kifo

      ▪ Kesi iliendeshwa usiku kisiri, hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia

      ▪ Kesi ilifanywa siku moja, usiku wa kuamkia sherehe

      ▪ Hakukuwa na tuhuma, au mashtaka, kabla ya kukamatwa kwa Yesu

      ▪ Dai la Yesu kwamba yeye ndiye Masihi lilisemwa kuwa ni ‘kukufuru,’ lakini halikuchunguzwa

      ▪ Mashtaka yalibadilishwa kesi ilipopelekwa kwa Pilato

      ▪ Mashtaka yalikuwa ya uwongo

      ▪ Pilato hakumpata Yesu na hatia, hata hivyo, alimtoa ili auawe

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki