-
Kinga Mpya Dhidi ya Kifua KikuuAmkeni!—1999 | Mei 22
-
-
Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
KIFUA KIKUU ni maradhi ya kuambukizwa ambacho ni kisababishi cha kifo cha kale zaidi miongoni mwa wanadamu, na bado kingali tisho kubwa kwa afya hivi kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lakilinganisha na bomu linaloelekea kulipuka. Kuhusu kifua kikuu, ripoti moja ya WHO yaonya kwamba “tunakimbizana na wakati.” Mwanadamu akishindwa kukomesha kifua kikuu, huenda siku moja atakabili maradhi sugu “yanayoenezwa kupitia hewa, na ambayo hayawezi kutibiwa kama vile UKIMWI.” Shirika la WHO lahimiza kwamba wakati umewadia wa kuzinduka na kutambua madhara yawezayo kuletwa na kifua kikuu. “Kila mtu anayepumua hewa . . . , anapaswa kuhangaikia hatari hii.”
Je, kusema hivyo ni kutia chumvi? La. Kwa mfano, ebu wazia jinsi ambavyo ulimwengu ungezinduka iwapo maradhi fulani yangetisha kusababisha vifo vya watu wote nchini Kanada kwa miaka kumi! Ingawa jambo hilo laonekana kama haliwezekani, lakini kwa kweli tisho hilo lipo. Ulimwenguni pote, kifua kikuu husababisha vifo vya watu kuliko jumla ya vifo vyote vinavyosababishwa na UKIMWI, malaria, na maradhi ya kanda za joto: watu 8,000 kila siku. Watu wapatao milioni 20 sasa wanaugua kifua kikuu, na watu wapatao milioni 30 wanaweza kufa kutokana na kifua kikuu kwa miaka kumi ijayo—idadi kubwa kuliko watu wote nchini Kanada.—Ona Sanduku “Kifua Kikuu Chakumba Dunia Yote,” kwenye ukurasa wa 22.
-
-
Kinga Mpya Dhidi ya Kifua KikuuAmkeni!—1999 | Mei 22
-
-
Kwa Nini Kifua Kikuu Kimeibuka—TENA?
Tiba ya kifua kikuu (TB) iligunduliwa zaidi ya miongo minne iliyopita. Tangu wakati huo, zaidi ya watu milioni 120 wamekufa kwa kifua kikuu, na karibu milioni 3 watakufa mwaka huu. Lakini, kwa nini watu wengi wangali wanakufa kwa kifua kikuu ilhali kuna tiba? Kuna sababu tatu za msingi: kupuuza, virusi vya HIV/UKIMWI, na kifua kikuu sugu.
Kupuuza. Ulimwengu umezingatia maradhi yenye kuambukiza kama vile UKIMWI na Ebola. Hata hivyo, kwa kila mtu mmoja aliyekufa kwa Ebola, watu 12,000 walikufa kwa kifua kikuu. Kwani, kifua kikuu kimeenea sana katika nchi zinazositawi hivi kwamba watu wanakiona kuwa sehemu ya maisha. Na katika nchi tajiri, kifua kikuu kimeachiliwa kitawale ingawa dawa nzuri za kukitibu zinaozeana bila kutumiwa. Upuuzaji huo ulimwenguni kote umekuwa kosa lenye kusababisha maafa. Huku hangaiko la ulimwengu juu ya kifua kikuu likizidi kupoa, vijidudu vya kifua kikuu navyo vinazidi kuimarika. Leo, vinashambulia watu wengi zaidi katika nchi nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya wanadamu.
Virusi vya HIV/UKIMWI. Kifua kikuu huandamana na virusi vya HIV na UKIMWI. Watu wanapoambukizwa virusi vya HIV—ambavyo hudhoofisha kinga yao—wao wana uwezekano wa mara 30 wa kuambukizwa kifua kikuu kuliko wengine. Si ajabu kwamba mweneo wa sasa wa virusi vya HIV umesababisha ongezeko la wagonjwa wa kifua kikuu vilevile! Inakadiriwa kwamba watu 266,000 waliothibitishwa kuwa na virusi vya HIV walikufa kwa kifua kikuu mwaka wa 1997. “Hao ni wanaume na wanawake,” asema Peter Piot, mkurugenzi wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa HIV/UKIMWI, “ambao hawakunufaika na dawa zisizo ghali za kifua kikuu ambazo walihitaji ili kutibu kifua kikuu.”
Kifua Kikuu Sugu. “Vijidudu sugu,” ambavyo vina kinga dhidi ya dawa zote za wanadamu, ni mambo tu ya kubuniwa na hadithi za sayansi, lakini kwa habari ya kifua kikuu, jambo hilo ni ukweli mtupu. Tayari huenda zaidi ya watu milioni 50 wameambukizwa kifua kikuu sugu (MDR). Wagonjwa wa kifua kikuu ambao huacha kutumia dawa baada ya majuma machache eti kwa sababu wanahisi nafuu, au kwa sababu dawa zimekwisha, au kwa sababu maradhi haya yanafanya mtu adharauliwe hawaui vijidudu vyote vya kifua kikuu katika mwili wao. Kwa mfano, katika nchi moja ya Asia watu 2 kati ya kila 3 wanaougua kifua kikuu huacha matibabu mapema. Wanapokuwa wagonjwa tena, ugonjwa huo waweza kuwa mgumu zaidi kutibu kwa sababu vijidudu vinavyobaki hupigana na kushinda dawa yoyote ile ipatikanayo ya kifua kikuu. Basi, mwishowe mgonjwa huyo hushikwa na kifua kikuu kisichoweza kutibiwa—wao na mtu mwingine yeyote ambaye huenda wakamwambukiza. Na vijidudu hivyo vikipata tu kuwa hewani, tunabaki tukijiuliza, Je, mwanadamu ataweza kudhibiti tena kifua kikuu sugu?
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Kifua Kikuu Chakumba Dunia Yote
Kifua kikuu kinazidi kuenea, kugharimu zaidi kitiba, na kuzidi kuwa hatari kila mwaka. Ripoti zilizokusanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni laonyesha mweneo wa ugonjwa huu wenye kusababisha vifo bila kutambulikana. Hapa pana mifano kadhaa: “Pakistan hoi mbele ya kifua kikuu.” “Kifua kikuu kimerudi Thailand kwa kishindo.” “Leo, kifua kikuu ni mojawapo ya visababishi vikuu vya ugonjwa na kifo nchini Brazili.” “Kifua kikuu chaendelea kuwaponda watu wa Mexico.” Nchini Urusi “kifua kikuu chaongezeka upesi.” Katika Ethiopia “kifua kikuu kimewaka nchini kote.” “Afrika Kusini ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vilivyorekodiwa vya kifua kikuu ulimwenguni.”
Ingawa watu 95 kati ya kila 100 wanaougua kifua kikuu wanaishi katika nchi maskini za ulimwengu, kifua kikuu kinazidi kukumba nchi tajiri vilevile. Nchini Marekani, kuliripotiwa ongezeko kubwa la wagonjwa wa kifua kikuu mapema katika miaka ya 1990. Mwandishi wa habari Mmarekani Valery Gartseff asema kwamba kifua kikuu “kimerudi tena kuwatesa Wamarekani.” Vivyo hivyo, Dakt. Jaap Broekmans, mkurugenzi wa shirika la Royal Netherlands TB Association alisema hivi majuzi kwamba kifua kikuu “kimeanza kuponda vibaya Ulaya Mashariki na sehemu fulani za Ulaya Magharibi.” Si ajabu kwamba jarida Science, la Agosti 22, 1997, lasema kwamba “kifua kikuu chaendelea kuwa tisho kuu kwa afya.”
-