-
Uganda2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Mwezi wa Desemba, Heinz na Marianne Wertholz, kutoka katika Tanzu la Shule ya Gileadi huko Wiesbaden, Ujerumani, walijiunga na Jeff na Ari. Tangu mwanzo, akina Wertholz walichochewa sana na bidii ya ndugu zao wa Uganda licha ya kwamba walikuwa wakiishi katika hali mbovu na hatari.
“Huduma nyingi,” akumbuka Heinz, “kama vile maji na mawasiliano zilikuwa zimezorota. Kulikuwa na migogoro ya kisiasa. Mara kadhaa kulikuwa na uvumi wa kwamba serikali itapinduliwa, na wanajeshi waliweka vizuizi vingi barabarani. Milio ya risasi na unyang’anyi yalikuwa mambo ya kawaida hasa wakati wa usiku. Giza lilipoingia, barabara zilikuwa tupu. Kila mtu alikaa nyumbani akitumaini—na mara nyingi kusali—kwamba usiku utapita salama.”
Heinz na Marianne walikaa na familia ya Sam Waiswa huku wakiendelea kutafuta nyumba ambayo ingekuwa makao ya wamishonari. Ijapokuwa Sam alikuwa na taaluma ya kufundisha, hali za kiuchumi nchini humo zilikuwa zimewalemea sana hivi kwamba ukarimu wa familia yake kwa kweli haukuwa na kifani.
“Haikuwa rahisi kupata nyumba mahali salama,” asema Heinz, “kwa hiyo tulikaa kwa Sam kwa miezi mitano. Katika kipindi hicho tulipata kufahamiana vizuri. Nyakati nyingine walikuwa wakila mlo mmoja tu kwa siku, hata hivyo, walikuwa na furaha sikuzote; nao watoto walikuwa watiifu na wenye heshima. Kwa kuwa maji ya jiji hayakutegemeka, watoto hao walikuwa wakienda kuteka maji kwa mitungi ya lita 20 na kuyabeba kichwani. Tuliporudi nyumbani kutoka shambani, sikuzote kulikuwa na maji ya kutumia. Bila shaka, tulijifunza kuhifadhi maji. Kwa mfano, tulitumia kiasi kidogo cha maji tulipooga, na kuyahifadhi ili yatumike vyooni.”
Mwezi wa Aprili 1983, miaka kumi baada ya wamishonari wa mwisho kuondoka nchini Uganda, wamishonari hao wanne wapya walipata makao mapya mahali palipokuwa salama kiasi. Ukosefu wa usalama na upungufu wa vitu ulifanya hali iwe ngumu, hata hivyo, upendo wa ndugu wenyeji ulifanya wasahau yote hayo.
“Sikuzote tulifurahia kuwahubiria watu habari njema,” asema Marianne. “Walipenda mambo ya dini, walikuwa na Biblia, nao walikuwa tayari kusikiliza. Walikuwa wenye urafiki na adabu. Na licha ya hali ngumu za kiuchumi na nyinginezo, walikuwa na tabasamu sikuzote.”
-
-
Uganda2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 107]
Heinz na Marianne Wertholz walihudhuria darasa la kwanza la Tanzu la Shule ya Gileadi nchini Ujerumani
-