Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kupigania Kwetu Haki ya Kuhubiri
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Mwanzoni, tulikuwa na mafanikio katika utumishi wetu, Harold na binti ya Violet walikuwa wakifanya vizuri shuleni. Hata hivyo, baada ya Pearl Harbor kupigwa kwa bomu na Wajapani katika Desemba mwaka wa 1941 na Marekani kutangaza vita, mwitikio kuelekea kazi yetu ulibadilika kwa ghafula. Kulikuwa na roho ya uzalendo wa kupita kiasi na hofu ya njama. Kwa sababu ya kutokuwamo kwetu katika siasa, watu walitushuku, hata wakitushtaki kuwa wapelelezi wa Ujerumani.

      Harold alifukuzwa shuleni kwa sababu ya kukataa kushiriki katika sherehe ya kusimamisha bendera. Mwalimu wake aliniambia kuwa Harold alikuwa mwerevu na mwenye tabia nzuri, lakini mkuu wa shule alihisi kuwa alikuwa kielelezo kibaya kwa sababu hakuisalimu bendera. Msimamizi wa shule alikasirishwa sana na uamuzi ambao mkuu wa shule na halmashauri ya shule walifanya katika jambo hili hivi kwamba alijiuzulu akajitolea kumlipia karo Harold katika shule ya kibinafsi!

      Kila siku tulitishwa na vikundi vya wafanya-ghasia wenye jeuri. Katika tukio moja polisi walitusukuma kutoka katika mlango wa nyumba ya mama mmoja, wakavunja vinanda vyetu vya gramafoni kwenye mti, wakavunja rekodi zetu za mihadhara ya Biblia, wakararua Biblia zetu na fasihi vipande-vipande, na mwishowe kuchoma moto kila kitu walichokuwa wametwaa kutoka kwetu. Walituambia tuondoke mjini kabla hakujawa na giza au sivyo tungefukuzwa na kikundi cha wafanya-ghasia. Tuliandika barua upesi na kuzipeleka wenyewe kwa wakuu wa mji, tukiomba ulinzi. Lakini wakakataa kutupatia ulinzi wowote. Hata nilipiga simu kwa Idara ya Upelelezi ya FBI katika Jackson, Mississippi, na kuomba msaada. Wao pia walitushauri tuondoke mjini.

      Usiku huo karibu wanaume mia moja wenye hasira walilizunguka gari letu la kukokotwa. Tulikuwa wanawake wawili peke yetu na watoto wetu. Tulifunga milango, tukazima taa, na kusali kwa Yehova kwa bidii. Mwishowe, umati ulitawanyika bila kutuumiza.

      Baada ya kuona matukio haya, Herbert aliamua kujiunga nasi huko Brookhaven mara moja. Tulimrudisha Harold kwa wazakuu wake huko Robertsdale, ambapo mkuu wa shule wa huko alituhakikishia kuwa atapata elimu. Tuliporudi Brookhaven, gari la kukokotwa lilikuwa limeharibiwa na idhini ya kutukamata ilikuwa imepigiliwa msumari kwenye moja ya kuta za ndani. Licha ya kupingwa huku, tulisimama imara na kuendelea katika huduma yetu.

      Kukamatwa na Kutendwa Vibaya

      Katika Februari ya mwaka wa 1942, Herbert nami tulikamatwa tulipokuwa tukiongoza funzo la Biblia katika nyumba moja ndogo ya wastani. Mwanamume mwenye nyumba alikasirika sana kwa sababu ya jinsi tulivyotendwa hivi kwamba alichukua bunduki yake akatisha kumpiga risasi huyo polisi! Tulishtakiwa kwa kuingia bila ruhusa tukapatwa na hatia katika kesi iliyofanywa siku iliyofuata.

      Tuliwekwa katika seli ndogo chafu, na yenye baridi kwa muda wa siku 11. Mhudumu Mbaptisti wa hapo alitutembelea tulipokuwa huko, akituhakikishia kuwa ikiwa tutakubali kuondoka mjini, angetumia mamlaka yake ili tuachwe huru. Tulifikiri hili lilikuwa kejeli, kwani mamlaka yake ndiyo iliyokuwa imetuingiza pale.

      Pembe moja ya seli yetu ilikuwa imetumika kama choo hapo awali. Mahali hapo palijawa tele na kunguni. Chakula kiliandaliwa katika mikebe michafu, ambayo haikusafishwa. Likiwa tokeo la hali hizo, nilipatwa na nimonia. Daktari aliletwa kuniona, tukaachiliwa. Usiku huo kikundi cha wafanya-ghasia kilikuja kwenye gari letu la kukokotwa, kwa hiyo tulienda nyumbani Robertsdale kungojea kesi yetu.

      Kesi

      Wabaptisti kutoka sehemu zote za jimbo walikuja Brookhaven kwa ajili ya kesi yetu, ili kutegemeza mhudumu Mbaptisti ambaye alihusika katika kukamatwa kwetu. Hili lilinisukuma kumwandikia barua ndugu-mkwe wangu Oscar Skooglund, mhudumu madhubuti wa kanisa la Baptisti. Ilikuwa barua yenye hamaki ambayo haikuandikwa kwa busara sana. Hata hivyo, jinsi nilivyotendwa na kile nilichoandika lazima kilimwathiri Oscar kwa njia yenye mafaa, kwa sababu baada ya muda mfupi, akawa Shahidi wa Yehova mwenye bidii.

      Mawakili wetu, G. C. Clark na Victor Blackwell, Mashahidi wa Yehova wenzetu, walikuwa wamesadiki kuwa hatungefanyiwa kesi ya haki huko Brookhaven. Kwa hiyo wakaamua kupinga kila kitu ili kesi itupiliwe mbali kwa sababu ya kupinga kulikoendelea. Kila wakati mwendesha-mashtaka aliposema jambo, mmoja wa mawakili wetu alilipinga. Walipinga angalau mara 50. Mwishowe, hakimu alitupilia mbali mashtaka yote.

  • Kupigania Kwetu Haki ya Kuhubiri
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Kukamatwa Tena na Kutiwa Gerezani

      Juma lililofuata Aileen nami tulikutana na E. B. Peebles, makamu wa msimamizi wa shirika la Kutengenezea Meli la Gulf tukaeleza umuhimu wa utendaji wetu wa kidini. Alituonya kwamba utendaji wa Mashahidi wa Yehova haungekubaliwa katika Chickasaw. Tulieleza kwamba watu walikuwa wametukaribisha kwa furaha nyumbani mwao. Je, angewanyima haki ya kujifunza Biblia? Akawa mwenye uhasama akatisha kututia gerezani kwa ajili ya kuingia bila ruhusa.

      Nilirudi Chickasaw mara kwa mara na kila wakati nilikamatwa. Lakini kila wakati, niliachiliwa kwa dhamana. Hatimaye, dhamana hiyo iliongezwa kuwa kiasi kikubwa sana cha pesa, na ningetumia wakati mwingi zaidi na zaidi katika gereza hadi tulipoweza kupata hizo pesa. Hali za gerezani zilikuwa chafu—hakukuwa na choo, magodoro yalikuwa machafu bila shuka za kulalia, na blanketi moja chafu ya kujifunikia. Likiwa tokeo, matatizo yangu ya afya yaliibuka tena.

      Katika Januari 27, 1944, kesi za Mashahidi sita ambao walikamatwa Desemba 24, 1943, zilisikizwa pamoja, na ushuhuda wangu ulionwa kuwa mwakilishi wa washtakiwa wale wengine. Hata ingawa kesi hiyo ilionyesha ubaguzi wa wazi dhidi ya Mashahidi wa Yehova, nilipatikana na hatia. Tulikata rufani kwa ajili ya uamuzi huo.

      Katika Januari 15, 1945, mahakama ya kukata rufani ilitangaza uamuzi: Nilipatikana na hatia ya kuingia bila ruhusa. Zaidi ya hilo, Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Alabama ilikataa kusikiliza kesi yangu. Katika Mei 3, 1945, Hayden Covington, mmoja wa Mashahidi wa Yehova aliye wakili jasiri na mwenye nguvu, alitoa ombi la bidii kwa Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Marekani kwa ajili ya kukata rufani.

      Huku Aileen nami tukingojea kusikia kutoka kwa Mahakama Kuu Kuliko Zote, tuligeuza mashtaka kuelekea washtaki wetu na tukafungua mashtaka dhidi ya E. B. Peebles na waliomuunga mkono katika idara ya liwali, tukiomba kulipwa hasara. Washtaki wetu walijaribu kubadili shtaka lao dhidi yetu liwe kwamba tulizuia upitaji wa watu badala ya kuwa tuliingia bila ruhusa, lakini nilipokuwa gerezani, nilikuwa nimechukua kisiri karatasi iliyokuwa na sahihi ya Naibu wa Chatham, ikitushtaki kuwa tuliingia bila ruhusa. Wakati ushuhuda huu ulipotolewa kortini, Liwali Holcombe aliruka akasimama na karibu ameze biri yake! Kesi ya Februari 1945, iliishia na baraza la mahakama lisiloweza kuamua.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki