-
Nimebarikiwa kwa Urithi wa PekeeMnara wa Mlinzi—2000 | Oktoba 1
-
-
Mnamo Desemba 1894 mhudumu wa wakati wote wa Wanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, alimtembelea babu yangu, Clayton J. Woodworth, nyumbani kwake huko Scranton, Pennsylvania, Marekani. Clayton alikuwa ametoka tu kuoa. Alimwandikia barua msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society, Charles Taze Russell, nayo ikachapishwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi Juni 15, 1895, la Kiingereza. Alieleza hivi:
“Sisi ni wenzi wachanga wa ndoa ambao tumekuwa washiriki wa kanisa la Kiprotestanti kwa miaka kumi hivi; lakini kwa sasa, twaamini kwamba tunatoka kwenye giza kuingia kwenye nuru ya siku mpya ambayo sasa yapambazuka kwa wana waliojiweka wakfu wa Aliye Juu Zaidi. . . . Zamani kabla ya mimi na mke wangu kujuana tulikuwa na tamaa kubwa ya kumtumikia Bwana, ikiwa ni mapenzi yake, tukiwa wamishonari katika eneo la kigeni.”
-
-
Nimebarikiwa kwa Urithi wa PekeeMnara wa Mlinzi—2000 | Oktoba 1
-
-
Mwaka huohuo, 1903, Cora na Washington Howell walipata binti waliyemwita Catherine. Jinsi alivyokuja kuolewa hatimaye na baba yangu, Clayton J. Woodworth, Jr., naamini ni kisa chenye maana na chenye kupendeza. Chaonyesha ufahamu wenye upendo na hangaikio la mzazi la babu yangu Clayton J. Woodworth, Sr.
Baba Yangu Apokea Msaada Wenye Upendo
Baba yangu, Clayton mdogo, alizaliwa huko Scranton mwaka wa 1906, umbali wa kilometa 80 hivi kutoka shamba la Howell. Miaka hiyo ya mapema, Babu Woodworth alijuana vizuri na familia kubwa ya Howell, mara nyingi akifurahia ukaribishaji-wageni wao uliojulikana sana. Alisaidia sana kutaniko la Wanafunzi wa Biblia katika eneo hilo. Muda si muda, Babu akaitwa kuandikisha ndoa za wana watatu wa Howell, na kwa kufikiria masilahi ya mwana wake mwenyewe, aliazimia kuwa akienda naye kwenye kila mojawapo ya arusi hizo.
Wakati huo baba hakuwa amejihusisha sana na huduma ya Wanafunzi wa Biblia. Alimpeleka Babu kwa gari kwenda kufanya ziara zake za huduma, lakini kijapokuwa kitia-moyo cha Babu, Baba hakuchukua hatua yoyote. Wakati huo, baba yangu alipenda muziki kuliko kitu kingine chochote, naye alikuwa akijitahidi kuwa mwanamuziki wa kulipwa.
Catherine, binti ya Cora na Washington Howell, alikuwa pia amekuwa mwanamuziki mashuhuri, akipiga na kufundisha piano. Lakini wakati alipokuwa tu aanze kuwa mwanamuziki wa kulipwa, aliacha muziki, akaanza kushiriki katika huduma ya wakati wote. Babu aliona kwamba Catherine angekuwa mwandamani bora wa mwanawe—angalau kulingana na maoni yangu! Baba alibatizwa na kumwoa Mama miezi sita baadaye, mwezi wa Juni 1931.
Sikuzote Babu alijivunia kipawa cha muziki cha mwanawe. Alifurahi sana Baba alipoombwa kufundisha kikundi cha okestra cha mkusanyiko mkubwa kwa ajili ya mkusanyiko wa kimataifa wa 1946 huko Cleveland, Ohio. Miaka iliyofuata, Baba aliongoza okestra kwenye mikusanyiko kadhaa mingine ya Mashahidi wa Yehova.
Kesi ya Babu na Maisha Yake Gerezani
Katika sebule ya Patterson, mimi na Paul tuliona pia picha iliyo kwenye ukurasa unaofuata. Niliitambua picha hii mara moja, kwa kuwa Babu alinitumia nakala moja miaka 50 iliyopita. Ndiye aliyesimama mwisho kulia.
Wakati wa msisimko wa kizalendo uliotokea wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, hao Wanafunzi wanane wa Biblia—kutia ndani Joseph F. Rutherford (aliyeketi katikati), msimamizi wa Watch Tower Society—walitiwa gerezani kimakosa na kuzuiwa bila dhamana. Mashtaka dhidi yao yalihusu taarifa zilizo katika buku la saba la Studies in the Scriptures, lenye kichwa The Finished Mystery. Taarifa hizo zilieleweka vibaya kuwa zenye kuvunja moyo Marekani isishiriki katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.
Kwa kipindi cha miaka mingi, Charles Taze Russell aliandika mabuku sita ya Studies in the Scriptures, lakini alikufa kabla hajaandika buku la saba. Kwa hiyo Babu na Mwanafunzi wa Biblia mwingine walipewa maandishi yake, nao wakaandika buku la saba. Hilo lilitolewa mwaka wa 1917, kabla ya mwisho wa vita. Kwenye kesi hiyo, Babu na wengi wa wale wenzake walihukumiwa vifungo vinne, kila mmoja kifungo cha miaka 20, vyote vikiambatana pamoja.
Maelezo ya picha kwenye sebule ya Patterson yasema: “Miezi tisa baada ya Rutherford na wenzake kuhukumiwa—na vita ikiwa imekwisha—Machi 21, 1919, mahakama ya rufani iliamuru washtakiwa wote wanane waachiliwe kwa dhamana, na Machi 26, walifunguliwa huko Brooklyn kwa dhamana ya dola 10,000 kila mmoja. Mei 5, 1920, J. F. Rutherford na wenzake waliondolewa mashtaka.”
Baada ya kuhukumiwa, lakini kabla ya kupelekwa kwenye gereza kuu la serikali la Atlanta, Georgia, ndugu hao wanane walikaa kwa siku chache kifungoni katika jela ya Raymond Street huko Brooklyn, New York. Akiwa huko Babu aliandika akieleza jinsi alivyowekwa ndani ya seli ya meta 1.8 kwa meta 2.4 “katikati ya uchafu wenye kutisha na mvurugo.” Alisema: “Unaona rundo la magazeti, na ukiyapuuza mara ya kwanza, unakuja kugundua kwamba makaratasi hayo na sabuni na kitambaa cha kuogea, humaanisha fursa yako ya kuwa safi na kujipatia heshima.”
Hata hivyo, Babu alidumisha ucheshi wake, akiita jela hiyo “Hôtel de Raymondie” na kusema, “Nitaondoka hapa siku zangu za malazi zitakapokwisha.” Pia alifafanua matembezi yake ya uani. Wakati mmoja aliposimama ili achanwe nywele zake, mnyakuzi wa mifukoni aliiba saa yake ya mfukoni, lakini kama alivyoandika, “Mnyororo wake ulikatika nami nikaiokoa.” Nilipokuwa nikitembelea Betheli ya Brooklyn mwaka wa 1958, Grant Suiter, aliyekuwa mwandishi mweka-hazina wa Watch Tower Society, aliniita kwenye ofisi yake na kunipa saa hiyo. Ningali naithamini sana.
Jinsi Baba Alivyoathiriwa
Babu alipotiwa gerezani isivyo haki mwaka wa 1918, baba yangu alikuwa na umri wa miaka 12 tu. Nyanya alifunga nyumba yao na kumchukua wakaishi naye pamoja na mama yake na dada zake watatu. Jina la familia la mama lilikuwa Arthur, na familia hiyo ilidai kwa fahari kwamba mmoja wa watu wao wa ukoo, Chester Alan Arthur, alikuwa rais wa 21 wa Marekani.
Baada ya Babu Woodworth kuhukumiwa kifungo kirefu kwa madai ya uhalifu dhidi ya Marekani, kwa wazi familia ya akina Arthur ilihisi kwamba ameliaibisha jina lao la familia. Kilikuwa kipindi chenye kuumiza kihisia-moyo kwa baba yangu. Labda jambo hilo ndilo lililomfanya asishiriki katika huduma ya hadharani mwanzoni.
Babu alipofunguliwa kutoka gerezani, alihamisha familia yake kwenda kwenye nyumba kubwa iliyokandikwa kwa lipu kwenye barabara ya Quincy Street huko Scranton. Nikiwa mtoto, niliijua vema nyumba hiyo kutia ndani vyombo maridadi vya kauri vya Nyanya vilivyokuwa humo. Tuliviita vyombo vyake vitakatifu kwa sababu hakuna mtu aliyeruhusiwa kuviosha isipokuwa Nyanya. Baada ya Nyanya kufa mwaka wa 1943, Mama alivitumia vyombo hivyo maridadi mara nyingi alipokuwa na wageni.
Mwenye Shughuli Katika Utumishi wa Ufalme
Siku nyingine kwenye chuo cha Patterson, niliona picha ya Ndugu Rutherford akitoa hotuba kwenye mkusanyiko wa 1919 huko Cedar Point, Ohio. Aliwatia moyo wote washiriki kwa bidii kutangaza Ufalme wa Mungu na kutumia gazeti jipya lililotolewa mkusanyikoni, The Golden Age. Babu aliwekwa kuwa mhariri wake, naye alichangia makala zake hadi miaka ya 1940, muda mfupi kabla ya kifo chake. Mwaka wa 1937 jina la gazeti hilo likabadilishwa kuwa Consolation na mwaka wa 1946 likawa Awake!
Babu alifanyia kazi yake ya kuandika akiwa nyumbani huko Scranton na Makao Makuu ya Watch Tower huko Brooklyn yaliyokuwa kilometa 240 hivi kutoka Scranton, akitumia majuma mawili kila mahali. Baba asema kwamba akumbuka mara nyingi alisikia taipureta ya Babu ikichapa saa kumi na moja asubuhi. Hata hivyo, Babu pia alilichukua kwa uzito daraka la kushiriki katika kazi ya kuhubiri. Hata alitengeneza fulana iliyokuwa na mifuko ya ndani mikubwa ya kubebea vichapo vya Biblia. Mke wa mjombangu mwenye umri wa miaka 94, Naomi Howell, angali na fulana moja. Pia alitengeneza mkoba wa vitabu wa wanawake.
Wakati mmoja baada ya mazungumzo ya Biblia yenye kusisimua, mtumishi mwenzi wa Babu alisema hivi: “C. J., umefanya kosa moja.”
“Kosa gani?” Babu akauliza. Akaangalia fulana yake. Mifuko yote miwili ilikuwa mitupu.
“Umesahau kumtolea andikisho la The Golden Age.” Walicheka kwa sababu mhariri alisahau kutoa gazeti lake.
Kumbukumbu za Kukua
Nakumbuka Babu akiniweka kwenye mapaja yake nikiwa mtoto, akiwa ameshika mkono wangu mdogo aliponisimulia “Hadithi ya Vidole.” Kuanzia dole gumba kisha kidole shahada yeye alisema jambo fulani la pekee kuhusu kila kidole. Kisha akavifunga vidole vyote pamoja na kutoa fundisho hili la maadili: “Vyote vyafanya kazi pamoja kwa umoja, kila kimoja kikisaidia mwenzake.”
-
-
Nimebarikiwa kwa Urithi wa PekeeMnara wa Mlinzi—2000 | Oktoba 1
-
-
Babu na Kuhitimu Kwangu
Wakati wa miaka yangu ya shule ya sekondari, Babu alikuwa mwepesi wa kuandika barua. Barua zake zilitia ndani picha za zamani za familia zikiwa na maandishi yaliyochapwa nyuma, zikieleza historia ya familia. Hivyo ndivyo nilivyopokea nakala yangu ya picha yake akiwa na wenzake waliotiwa gerezani isivyo haki.
Kufikia mwisho wa mwaka wa 1951, Babu alikuwa amepoteza zoloto yake kwa sababu ya kansa. Bado alikuwa na akili ya kuandika mambo kwa njia ya ucheshi, lakini ilimbidi aandike maneno yake kwenye kitabu kidogo alichobeba. Darasa langu la sekondari lilipaswa kuhitimu katikati ya muhula, Januari 1952. Mwanzoni mwa Desemba, nilimtumia Babu hotuba nitakayotoa siku yangu ya kuhitimu. Aliifanyia marekebisho fulani kisha kwenye ukurasa wa mwisho akaandika maneno mawili yaliyonigusa moyo: “Babu afurahia.” Alimaliza mwendo wake wa dunia akiwa na umri wa miaka 81, Desemba 18, 1951.a Ningali nina maandishi hayo yangu yaliyochakaa ya hotuba ya kuhitimu kwangu ikiwa na maneno hayo mawili kwenye ukurasa wa mwisho.
Mara tu baada ya kuhitimu kwangu, nilianza utumishi wa painia, kama vile ambavyo Mashahidi wa Yehova huita kazi ya kuhubiri wakati wote. Mwaka wa 1958, nilihudhuria mkusanyiko mkubwa zaidi katika New York City, ambapo kilele cha watu 253,922 kutoka katika nchi 123 walijaza Yankee Stadium na Polo Grounds. Nikiwa huko siku moja nilikutana na mjumbe kutoka Afrika aliyevaa beji yenye jina “Woodworth Mills.” Alikuwa amepewa jina hilo la babu miaka 30 iliyopita!
-