Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho
    Amkeni!—1996 | Juni 22
    • Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho

      “KUSUDI lililo wazi zaidi la likizo ni kupata hali tofauti, kipumziko, badiliko katika kawaida ya kila siku,” akaandika mwandikaji wa habari Lance Morrow. Hata hivyo, alionelea kwamba wengine hurudi nyumbani kutoka likizoni wakiwa wameungua nishati hivi kwamba wanaapa kutoenda likizoni tena.

      Hata hivyo, badala ya kusahau wazo la kwenda likizoni, lingekuwa jambo la hekima kuchunguza kimbele mitego iwezayo kutokea na kuchukua hatua za kuiepuka.

      Linda Vitu Vyako vya Thamani

      Wengi wamerudi kutoka likizoni na kupata kwamba wakati hawakuwapo nyumba yao ilivunjwa. Kwa hiyo kabla ya kwenda likizoni, waombe marafiki au majirani wawe wakitunza nyumba yako kwa ukawaida. Huenda hata wakaweza kutumia wakati fulani huko ili kuondosha wazo la kwamba hauko.

      Pia wahitaji kulinda vitu vyako vya thamani mahali ulipo likizoni. Katika nchi fulani wageni huonwa kuwa matajiri, na kila mtalii aweza kunyang’anywa vitu. Kwa hivyo, zoea zuri ni kuacha pesa taslimu za ziada na hati zenye thamani katika mahali salama hotelini au mahali penginepo palipo salama. Uwe mwangalifu kuhusu watu usiowajua, bila kukosa fadhili.

      Kila mwaka Miami, Florida, Marekani huwa na mamilioni ya waenda-likizo wa kigeni na wenyeji. Wahalifu hutenda kazi sana hasa katika maeneo hayo yenye watalii. Gazeti Time liliripoti, kwamba katika 1992, “katika Florida pekee, wageni 36,766 kutoka nchi nyinginezo na wenyeji, waliuawa kimakusudi, kulalwa kinguvu, kunyang’anywa au kuhasiriwa kwa njia fulani.”

      Unapokuwa likizoni, jihadhari hasa na sinzia (wezi wa mifukoni). Wanaume wapaswa kuweka mapochi yao mahali pasipoonekana kwa urahisi na palipolindwa, kama vile mfuko wa ndani wa koti au mfuko wa mbele wa suruali. Wasafiri wazoefu mara nyingi huficha fedha zao kwa njia za kiakili. Kwa kielelezo, wengine hubeba fedha zao, pasipoti, na visa katika mapochi madogo yaliyo bapa yaliyofungwa shingoni na kutiwa ndani ya mavazi. Wanawake wapaswa kuwa waangalifu ama sivyo waendesha-baiskeli au pikipiki wanyakue mikoba isiyoshikiliwa kwa nguvu.

      Wahalifu huendelea kupata njia mpya za kuwinda watalii. Kwenye magari-moshi ya moja kwa moja ya mwendo mrefu, abiria wanaolala katika nchi za Ulaya wamenyang’anywa wakati wa usiku. Vichochea usingizi vyaweza kuingizwa ndani ya vyumba ili kuhakikisha walio ndani ya vyumba hawaamki vitu vyao vinapoibwa. Katika pindi moja, kulingana na The European, “wanyang’anyi walifikiriwa kuwa waliondoka kimya-kimya katika gari moshi wakiwa na zaidi ya dola 845,000 pesa taslimu na vitu vilivyoibwa.”

      Epuka Aksidenti

      “Suluhisho langu la pekee kwa tatizo la aksidenti ambazo hunipata,” akasema mcheshi Robert Benchley, “ni kubaki kitandani siku nzima.” Lakini kisha akaongeza: “Hata wakati huo, sikuzote yawezekana kwamba utaanguka kutoka kitandani.” Kwa hakika, aksidenti hutokea kila mahali! Kwa hiyo hofu ya kupatwa na aksidenti unapokuwa likizoni haipasi kukutia woga na kukufanya ubaki nyumbani. Lakini kuna sababu ya pekee ya kuwa mwangalifu unapokuwa likizoni.

      Hali za trafiki haziwezi kutegemeka katika pindi za likizo. Wajerumani wamezoea msongamano wa magari wenye urefu wa kilometa 80 katika nyakati hizo. Gazeti Time la Agosti 14, 1989, lilitaarifu hivi: “Kote katika Ulaya juma lililopita, mamilioni ya familia yalianza sikukuu yao ya kidesturi ya Agosti—na kila mtu alipatwa na wakati mbaya sana na wenye kuchosha. . . . Karibu kila barabara kuu itokayo Paris ilijaa na kusababisha magari kusimama. . . . Kati ya Julai 28 na Agosti 1, watu 102 walikufa katika migongano ya barabara kuu.” Kwa hiyo, kwa hekima simama kifupi ujipumzishe na mkazo uletwao na kusonga-songa na kusimama-simama.

      Gazeti The European lilitoa ripoti ya mapendekezo kwamba waendesha-magari “wakawize safari zao hadi Jumapili—au wasafiri usiku.” Hata hivyo lilikubali kwamba waenda-likizo wengi “bado husisitiza kuondoka wakati huohuo.” Tokeo ni nini? Ulaya yenye msongamano wa magari. Ingawa ni jambo la hekima kusafiri wakati barabara hazijasongamana sana, usisahau uhakika wa kwamba kusafiri usiku kwaweza kuwa hatari. Mtu haoni vizuri sana usiku, na hivyo uwezekano wa kupata aksidenti waweza kuongezeka. Wakati mzuri zaidi wa kusafiri waweza kuwa mapema asubuhi.

      Usipuuze vitu vingine viwezavyo kuwa vyanzo vya aksidenti baada ya kufika mahali unapoenda likizoni. Ikiwa hujatumia misuli yako kwa muda mrefu mwakani, hiyo itaumia unapojikaza sana usipokuwa katika hali nzuri sana. Kwa hiyo wekea mipaka michezo siku za kwanza-kwanza, wakati mwili wako uwezapo kujeruhiwa kwa urahisi.

      Dumisha Afya Nzuri

      Kulingana na kitabu 2,000 Everyday Health Tips for Better Health and Happiness, “matatizo ya kawaida sana ya afya ambayo wasafiri hukumbana nayo wakiwa safarini ng’ambo yanahusu hasa chakula, maji na maradhi machache yenye kuambukiza.” Maajenti wa usafiri wanaweza kuandaa shauri jinsi ya kuepuka matatizo hayo, nalo ni jambo lifaalo kufuata madokezo yao.

      Katika maeneo mengi ni jambo la maana kuepuka kunywa maji ya mfereji. Na kumbuka, vijiwe vya barafu yaelekea vimetengenezwa kwa maji hayo. Huenda pia likawa jambo la hekima kuepuka kula mboga za majani, mayonnaise, vyakula vilivyotayarishwa kwa krimu, nyama mbichi au ambayo haijaiva vizuri ndani, kombe, na matunda yasiyopikwa, isipokuwa unaweza kuyaambua mwenyewe. Katika nchi za kitropiki, maziwa yapaswa kushemshwa kabla hujayanywa.

      Chanzo kikubwa cha hatari kwa waenda-likizo wenye kuvaa mavazi mepesi ni jua, na katika miaka ya majuzi hatari hiyo imeongezeka kwa kutazamisha kwa sababu ya kupungua kwa ozoni katika angahewa. Idadi ya visa vipya vya malignant melanoma, aina hatari sana ya kansa ya ngozi, ilirudufika katika Marekani kati ya 1980 na 1993. T-shati zimeonwa katika Australia zenye maneno “Vaa shati na kofia na ujipake kizuia-miale ya jua.” Lakini usitulizwe na hisi bandia ya usalama. Vizuia-miale ya jua havitegemeki.

      Usafiri wa hewani unaovuka kanda kadhaa za majira waweza kutokeza uchovu utokanao na kupitia kanda tofauti za majira. Ingawa wenyewe si maradhi, uchovu utokanao na kupitia kanda tofauti za majira waweza kuvuruga hali-njema ya kimwili ya mtu, hasa ikiwa mtu si mwenye afya nzuri. Uchunguzi uliofanyiwa wasafiri wa hewani kati ya London na San Francisco, tofauti ya muda wa saa nane, ulifunua kwamba “kujipatanisha kimwili . . . kulihitaji angalau siku kumi.” Kitabu The Body Machine pia kiliripoti kwamba wasafiri fulani ambao huvuka haraka kanda za majira walikuwa na “mwelekeo wa kuwa wasioweza kujieleza vyema, wenye kusita-sita na walielekea kufanya makosa mara mbili kuliko wengine. Kukaza fikira na kumbukumbu pia viliathiriwa.”a

      Kwa kuongezea, usafiri wa ndege huwezesha kuenea kwa maradhi kutoka bara moja hadi jingine kwa muda wa saa chache tu. Gazeti la habari la Ujerumani Nassauische Neue Presse lilitaja: “Madaktari wana wasiwasi hasa kuhusu maradhi ‘ya kigeni’ kama vile malaria au mchochota wa ini ambayo waenda-likizo hurudi nayo kutoka Afrika, Asia au Amerika Kusini. Kila mwaka Wajerumani 2,000 hivi hurudi nyumbani wakiwa na malaria.” Baada ya tauni iitwayo bubonic plague kusababisha vifo katika India katika 1994, hatua kali za kuzuia zilichukuliwa ili kuizuia isienee katika nchi nyinginezo.

      Watu wenye matatizo yenye kudumu ya afya, na vilevile wanawake wenye mimba, wapaswa kutahadhari zaidi wanaposafiri. Ingawa katika visa vingi hakuna sababu muhimu ya watu kama hao kuepuka kusafiri, wanapaswa kutafuta ushauri kutoka kwa daktari wao kimbele. Ni jambo la hekima kwa yeyote anayesafiri kubeba jina, anwani, na nambari ya simu ya rafiki au mtu wa ukoo awezaye kufikiwa wakati wa dharura.

      Mtu anayehitaji sindano za kawaida za insulini ili kusawazisha kiwango chake cha sukari katika damu apaswa kukumbuka kwamba kuvuka kanda kadhaa za majira kutavuruga ratiba yake angalifu ya chakula na sindano. Atalazimika kupanga ifaavyo. Pia msafiri mwenye kisawazisha-mpigo-moyo apaswa kuhakikisha kwamba ana nambari ya simu ya daktari wake wa maradhi ya moyo.

      Isitoshe, yeyote anayetegemea dawa fulani atataka kuibeba katika mzigo wake wa kuchukulika kwa sababu mzigo uliopotea au ulioelekea mahali pasipofaa waweza kusababisha msiba kwa msafiri. Kutokuwa na mavazi safi ya kubadilisha kwa siku kadhaa kwaweza kuudhi; kukaa bila dawa muhimu kwa saa chache kwaweza kutisha uhai.

      Hatari za safari ya likizo hazipasi kuchukuliwa vivi hivi. Hata hivyo, hakuna sababu nzuri ya kuruhusu zikutie woga na kufanya ubaki nyumbani. Uwe mwangalifu tu. Kumbuka: Kujitayarisha kufaako husaidia kupambana na hatari ziwezazo kutokea. Fuata shauri lenye hekima: “Mtu mwerevu huona taabu ikija na kujibanza; yule mpumbavu huingia ndani yayo na kulipa adhabu.”—Mithali 22:3, The New English Bible.

  • Furahia Likizo Bila Majuto!
    Amkeni!—1996 | Juni 22
    • Uwe na Usawaziko

      Sawa na vikolezo katika chakula chetu, likizo huwa na mafanikio bora zaidi zinapotumiwa kwa uchache. Ingawa maisha ya tajiri asafiriye kwa ukawaida hasa kwa ajili ya anasa huenda yakavutia, hayo hukosa usawaziko na hayatokezi furaha ya kweli.

      Hasa kuhusiana na likizo, usawaziko katika kutumia fedha ni wa muhimu sana. Panga kwa uangalifu kabla ya kwenda, na ujaribu kufanya matumizi kulingana na bajeti yako. Epuka kudanganywa na matoleo ya pekee yafanywayo na maajenti wa usafiri ambao hukutia moyo “furahia sasa, lipa baadaye.”

      Pia, usijawe kupita kiasi na hisia za hatari ziwezazo kutokea hivi kwamba hali ya uhuru na starehe ambayo hufanya likizo zivutie ikandamizwe. Kwa kuongezea, usawaziko ufaao hutia ndani kutambua hatari kubwa zaidi ambayo yaweza kutufanya tutazame nyuma kwa likizo yetu tukiwa na majuto. Haihusiani kwa vyovyote na aksidenti, ugonjwa, au uhalifu, bali na mahusiano ya kibinafsi.

      Kudumisha Mahusiano Mema

      Likizo pamoja na familia au marafiki zaweza kuimarisha vifungo vya upendo. Kwa upande ule mwingine, likizo zaweza kusababisha mvunjiko katika uhusiano uwezao kuwa vigumu sana kurekebisha baadaye. Mwandikaji wa habari Lance Morrow alisema hivi: “Hatari halisi ya likizo iko katika uwezo wayo wa kufanya kutoafikiana katika familia kuwe dhahiri zaidi. . . . Watu katika maisha yao ya kawaida wana kazi, madaraka, marafiki na taratibu ambazo hueneza na kufyonza hisia-moyo. Katika mazingira ya nyumba inayotumiwa kwa ajili ya likizo, masuala ya familia yaliyokandamizwa kwa miaka 20 yaweza kuzuka kama mlipuko.”

      Kwa hiyo kabla ya kwenda likizoni, azimieni kikweli kuifanya iwe pindi yenye kufurahisha. Kumbukeni kwamba mapendezi hutofautiana. Huenda watoto wakawa wanatafuta utendaji wenye kujasiria, wazazi huenda wanatafuta pumziko. Uwe tayari kuacha mapendezi ya kibinafsi ya jambo la kufanya au mahali pa kwenda. Ikiwa ni jambo la hekima na la kiakili, afikianeni kuruhusu kila mtu kwa kipindi fulani afuatie kile ambacho kinampendeza hasa. Jifunzeni kudhihirisha sifa za roho ya Mungu kila siku katika mwaka wote, kisha haitakuwa vigumu kuendelea kufanya hivyo wakati wa likizo yenu.—Wagalatia 5:22, 23.

      Ingawa kudumisha uhusiano mzuri pamoja na familia na marafiki ni jambo la maana, uhusiano wetu pamoja na Mungu ni wa maana hata zaidi. Tukiwa likizoni mara nyingi sisi hukutana na watu ambao hawashiriki maoni yetu ya Kikristo juu ya Mungu na matakwa yake. Kushirikiana karibu nao—labda hata kwenda mara kwa mara mahali penye vitumbuizo vyenye kutilika shaka—kwaweza kutuongoza kwenye matokeo yenye kuleta majuto. Kumbuka Biblia huonya: “Msiongozwe vibaya. Mashirika mabaya huharibu mazoea yenye mafaa.”—1 Wakorintho 15:33, NW.

      Unapokuwa likizoni, wakati wowote ukigundua ndani yako mwenyewe tamaa ya kutoroka viwango na mazoea ya Kikristo, kwa hekima kabili udhaifu huo bila woga ukiomba msaada wa kimungu ili kupambana na tamaa hiyo!

      Ni Nini Kinachopendekezwa Likizoni?

      Watu wasiofinyanga maisha zao kulingana na kanuni za Kikristo huenda wakahisi kwamba wanapokuwa likizoni mwenendo wowote unakubaliwa. Katika nchi fulani za Ulaya, utalii wa ngono ni biashara yenye faida kubwa, na baadhi ya maajenti wa usafiri huipendekeza. Gazeti The European laandika kwamba ‘mambo yenye kuchukiza ambayo wanaume wa Ulaya hufanya katika makao fulani ya waenda-likizo ya Asia yamejulikana kwa muda mrefu.’ Likirejezea kwa nchi moja ya Asia, gazeti la Ujerumani Der Spiegel lilikadiria kwamba kufikia asilimia 70 ya wageni wote wanaume ni “watalii wa ngono.”

      Watalii wanawake sasa wanafuata kielelezo cha wenzao wa kiume. Kampuni ya Ujerumani ya ndege za kukodiwa ambayo husafiri hasa safari za kwenda Karibea hukadiria kwamba asilimia 30 ya abiria wayo wa kike huenda huko likizoni kwa kusudi dhahiri la ngono haramu. Gazeti The European lilimnukuu mwandikaji habari Mjerumani akisema: “Wanaiona kuwa njia rahisi na isiyo tata ya kupata raha—mchezo wa kigeni.”

      Hata hivyo, Wakristo wa kweli hawaioni ngono haramu kuwa njia inayokubalika ya kupata raha. Hiyo huvunja kanuni za Kikristo na imejawa na hatari. Ingawa hatari hutambuliwa kwa kawaida, watu wengi hujaribu tu kuepuka matokeo badala ya zoea hilo. Mfano mzuri ni tangazo katika magazeti ya habari ya Ujerumani lionyeshalo mwavuli na viti viwili vya ufuoni vilivyo vitupu. Maelezo husomeka hivi: “Safiri salama, na urudi bila UKIMWI.”

      Tokeo baya sana la utalii wa ngono ni kutendwa vibaya kingono kwa watoto. Kwa kupendeza, katika 1993 serikali ya Ujerumani ilipitisha sheria ifanyayo Wajerumani waweze kupata adhabu wapatikanapo na hatia ya kufanya ngono na watoto—hata wakiwa likizoni katika nchi za kigeni. Hata hivyo, kufikia sasa matokeo mazuri yamekuwa ya chini sana. Umalaya wa watoto umekuwa—na wabaki ukiwa—uhalisi wenye kuumiza na kutaabisha jamii ya kibinadamu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki