-
Yaani Kunanyesha Tena?Amkeni!—2004 | Februari 8
-
-
Mvukizo
Karibu asilimia 97 ya maji duniani yanapatikana baharini. Maji yaliyosalia yanapatikana katika mito ya barafu, maziwa, na visima vya chini ya ardhi. Bila shaka, hatuwezi kunywa maji ya bahari. Kama vile yule baharia mwenye taabu alivyosema katika shairi linaloitwa “Shairi la Baharia wa Kale,”a baharini kuna ‘maji, maji, kila mahali, lakini hakuna hata tone moja la kunywa.’
Kabla maji ya baharini yaweze kunywewa, hatua nyingi huhusika. Kwanza yanakuwa mvuke. Joto la jua huvukiza maji yanayotoshea kilometa 400,000 za mchemraba kutoka nchi kavu na baharini kila mwaka. Nyakati za kale, mtu mmoja aliyeitwa Elihu alimsifu Mungu kwa kutokeza utaratibu huo akisema: “Yeye huyavuta kwake maji ya bahari, na kutoka ukungu hufanya matone ya mvua.”—Ayubu 36:27, Biblia Habari Njema.
Angahewa ni “eneo tata sana,” lenye urefu wa zaidi ya kilometa 400. Maji ya mvua hufanyizwa kilometa 10 mpaka 20 kutoka duniani. Kitabu Our Fragile Water Planet hufafanua sehemu hiyo kuwa “eneo linalopakana na uso wa dunia, lenye mawingu, mvua, theluji, tufani, na vimbunga.”
Hewa hubeba maji mengi zaidi kadiri inavyokuwa na joto jingi zaidi. Ndiyo sababu nguo zilizooshwa hukauka haraka siku yenye joto na upepo. Angahewa la maeneo ya tropiki ndilo lenye maji mengi zaidi. Kwa hiyo huenda ukauliza, ‘Maji hayo yote hufikaje kwenye maeneo mengine ambako yanahitajiwa?’ Ni kupitia pepo kali zinazozunguka dunia. Pepo hizo hufanyizwa kutokana na jinsi ambavyo dunia inazunguka mhimili wake na kwa sababu sehemu fulani za dunia hupata joto jingi kuliko nyingine, hivyo angahewa huwa na upepo daima.
Angahewa lina makundi makubwa ya hewa. Makundi hayo ya hewa huwa na karibu kiwango kilekile cha joto. Ni makubwa kadiri gani? Yanaweza kufikia ukubwa wa kilometa milioni kadhaa za mraba. Makundi ya hewa yenye joto hufanyizwa kwenye maeneo ya Tropiki, na yale yenye hewa baridi hufanyizwa kwenye maeneo ya Aktiki na Antaktiki. Makundi hayo ya hewa husafirisha maji mengi katika angahewa.
Ubuni mwingine wa ajabu ni jinsi ambavyo mvuke husonga katika angahewa. Mvuke huondoa joto kutoka kwenye maeneo yenye joto jingi, kama vile maeneo ya Tropiki, hadi maeneo yenye baridi. La sivyo, joto lingeendelea kuongezeka zaidi na zaidi katika maeneo fulani ya dunia.
Mtonesho
Naam, mvuke ni muhimu katika angahewa, lakini ikiwa ungebaki huko juu haungetufaidi. Kwa mfano, angahewa la Jangwa la Sahara lina mvuke mwingi sana, lakini eneo hilo ni kame. Mvuke hurudi duniani kwa njia gani? Kwanza, hubadilika na kuwa maji.
Unapochemsha maji kwenye sufuria iliyofunikwa, mvuke hubadilika kuwa matone ya maji unapofika kwenye kifuniko kilicho baridi. Jambo hilohilo hutukia hewa inapopoa wakati inapoendelea kupaa kwenye maeneo yenye baridi. Ni nini hufanya hewa ipae? Hilo linaweza kutukia wakati kundi la hewa yenye joto linapoinuliwa juu zaidi na kundi la hewa baridi lililo zito zaidi. Wakati mwingine hewa husukumwa juu na milima. Nyakati nyingine, hasa katika maeneo ya tropiki, hewa baridi huinua hewa yenye joto.
Huenda ukauliza, ‘Lakini, mvuke unapopoa unajikusanya wapi?’ Angahewa lina chembechembe nyingi ndogo sana kama za moshi, vumbi, na chumvi ya bahari. Mvuke unapopoa, unafanyiza matone ya maji kwenye chembechembe hizo. Kisha matone hayo madogo ya maji hufanyiza mawingu.
Hata hivyo, maji hayo hayaanguki mara moja duniani. Kwa nini? Labda unajiuliza hilo linawezekanaje kwani uzito wa maji unazidi uzito wa hewa mara 800. Hiyo ni kwa sababu kila tone la maji ni dogo na jepesi sana hivi kwamba linaweza kuelea hewani. Elihu, aliyetajwa mapema, alistaajabishwa na jambo hilo la kupendeza kuhusu mzunguko wa maji alipoeleza jinsi “mawingu yanavyoelea angani” na kusema kwamba ni “kazi za ajabu za yule [Muumba] aliye mkamilifu wa maarifa!” (Ayubu 37:16, BHN) Je, hushangazwi kujua kwamba wingu dogo jepesi linaloelea angani linaweza kuwa na tani 100 mpaka 1,000 za mvuke?
Mvua
Mawingu mengi hayatokezi mvua. Ni rahisi kueleza jinsi maji yanavyofanyizwa kwenye angahewa na jinsi mawingu yanavyoelea angani. Lakini mwandishi mmoja anasema “ugumu ni kueleza jinsi maji yanavyorudi chini” tena.—The Challenge of the Atmosphere.
Tone moja la mvua linaweza kufanyizwa na “matone ya mawingu milioni moja au zaidi.” Inaonekana hakuna anayejua kabisa jinsi matone hayo madogo ya mawingu hufanyiza tani bilioni moja hivi za maji zinazoanguka duniani kila dakika na kila siku. Je, matone ya mawingu huungana na kufanyiza matone makubwa ya mvua? Nyakati nyingine yanafanya hivyo. Jambo hilo linaelezea jinsi matone ya mvua hufanyizwa katika maeneo fulani kama vile ya Tropiki. Lakini halielezei “fumbo la jinsi ambavyo matone ya mvua hufanyizwa” katika maeneo mengine kama vile Pwani ya Bahari ya Atlantiki huko Ireland.
Katika eneo hilo, matone ya mawingu hayaungani tu, bali yanafanyiza madonge madogo ya barafu kwa njia zisizoeleweka. Madonge hayo huungana na kufanyiza “mojawapo ya vitu vya ajabu zaidi vya uumbaji,” yaani, chembe za theluji. Chembe za theluji huanguka duniani zinapokuwa kubwa na nzito kuliko pepo zinazoinuka. Kunapokuwa na baridi sana, mabilioni ya chembe hizo huanguka zikiwa theluji. Lakini zinapopitia kwenye hewa yenye joto, chembe hizo za theluji huyeyuka na kufanyiza matone ya maji. Hivyo, mvua ya theluji haifanyizwi na matone ya maji yaliyoganda. Badala yake, mvua nyingi inayonyesha katika maeneo yenye joto la wastani huanza ikiwa theluji, kisha huyeyuka inapokuwa ikinyesha.
-
-
Yaani Kunanyesha Tena?Amkeni!—2004 | Februari 8
-
-
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 16, 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Asilimia 97 ya maji ya dunia yanapatikana baharini
Joto la jua huvukiza maji
Mvuke hubadilika kuwa matone na kufanyiza mawingu
Matone ya mvua na chembe za theluji yanapatikana baharini
Matone ya mvua na theruji
-