Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Maji Yanazidi Kupungua Ulimwenguni?
    Amkeni!—2001 | Juni 22
    • Je, Maji Yanazidi Kupungua Ulimwenguni?

      “Maji salama, safi na ya kutosha ni muhimu sana kwa uhai wa wanadamu. Ni muhimu pia kwa afya na maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi. Hata hivyo, tunaendelea kufikiri kwamba maji safi ni tele mno. Lakini sivyo ilivyo.”—KOFI ANNAN, KATIBU-MKUU WA UMOJA WA MATAIFA.

      KILA siku ya Alhamisi wakati wa adhuhuri, mahakama fulani ya pekee imekuwa ikifanya vikao katika jiji la Valencia huko Hispania kwa muda wa zaidi ya miaka elfu moja sasa. Mahakama hiyo husuluhisha migogoro inayohusu maji.

      Wakulima wanaoishi kwenye uwanda wenye rutuba wa Valencia humwagilia mashamba yao maji, na kilimo hicho huhitaji maji mengi sana. Na eneo hilo la Hispania limekuwa na upungufu mkubwa wa maji. Wakulima wanaweza kuomba msaada wa mahakama hiyo wanapohisi kwamba wamenyimwa maji. Migogoro kuhusu maji ni ya kawaida, lakini inasuluhishwa vyema sana huko Valencia.

      Miaka 4,000 hivi iliyopita, kulikuwa na mgogoro mkali kati ya wachungaji fulani kwa sababu ya kisima cha maji karibu na Beer-sheba huko Israeli. (Mwanzo 21:25) Na kumekuwa na matatizo makubwa zaidi ya maji katika Mashariki ya Kati tangu wakati huo. Viongozi wawili mashuhuri wa eneo hilo wamesema kwamba mojawapo ya mambo ambayo yanaweza kuwafanya washambulie Nchi jirani ni tatizo la maji.

      Maji yamesababisha migogoro mikali katika nchi zenye ukame ulimwenguni. Ni kwa sababu moja tu: Maji ni muhimu kwa uhai. Kama Kofi Annan alivyosema, “maji safi ni muhimu sana: hatuwezi kuishi bila maji safi. Hakuna kitu kinachoweza kuchukua mahali pake: hayana kibadala. Yanaweza kuathiriwa kwa urahisi: shughuli za wanadamu zinaathiri sana kiasi na hali ya maji.”

      Leo kuliko wakati mwingine wowote, kiasi na hali ya maji duniani imo hatarini. Hatupaswi kudhani kwamba hatari haipo eti kwa sababu sehemu nyingine ulimwenguni zina maji ya kutosha.

      Akiba ya Maji Inapungua

      “Tabia moja yenye kustaajabisha sana ya wanadamu ni kwamba wanathamini vitu wakati tu vinapokosekana,” asema Katibu-Mkuu Msaidizi wa UM Elizabeth Dowdeswell. “Tunathamini umuhimu wa maji wakati visima vinapokauka. Visima vinakauka katika maeneo yanayokumbwa na ukame mara nyingi na hata katika maeneo ambayo kwa kawaida huwa na maji mengi.”

      Inasikitisha kwamba wale wanaokosa maji kila siku ndio wanaofahamu tatizo hilo vyema zaidi. Asokan, anayefanya kazi ofisini huko Madras, India, huamka saa mbili kabla ya mapambazuko kila asubuhi. Yeye hutembea kwa mwendo unaochukua dakika tano akiwa amebeba ndoo tano ili kuteka maji kwenye bomba la umma. Yeye huenda kupiga foleni na kusubiri maji mapema alfajiri kwa kuwa maji huja tu kati ya saa 10 usiku na saa 12 asubuhi. Maji anayoteka ni kwa matumizi ya siku nzima. Wahindi wenzake wengi na watu wengine bilioni moja ulimwenguni hawapati maji kama yeye. Hakuna bomba, mto, au kisima karibu na makao yao.

      Abdullah, mvulana anayeishi katika jangwa la Sahel katika Afrika, ni mmojawapo wa watu wasio na maji. Ishara ya barabarani inaonyesha kwamba kijiji chao kidogo ni eneo lenye maji na miti jangwani; lakini maji hayo yalikauka kitambo sana, na miti imetoweka. Abdullah huteka maji kwenye kisima kilicho umbali wa zaidi ya kilometa moja kwa ajili ya familia yao.

      Katika sehemu fulani ulimwenguni, maji safi na salama hayatoshi kwa matumizi yote. Ni kwa sababu moja tu: Idadi kubwa ya wanadamu huishi kwenye maeneo yenye ukame, ambayo yamekuwa na upungufu wa maji kwa muda mrefu sana. (Ona ramani kwenye ukurasa wa 3.) Taasisi ya Mazingira ya Stockholm inasema kwamba theluthi ya watu wote ulimwenguni tayari wanaishi kwenye maeneo yenye upungufu wa maji au yasiyo na maji kabisa. Na uhitaji wa maji umeongezeka maradufu zaidi ya ongezeko la idadi ya watu.

      Kwa upande mwingine maji hayaongezeki. Kuchimba visima vyenye kina na hifadhi mpya za maji husuluhisha tatizo hilo kwa muda tu. Lakini kiasi cha mvua inayonyesha na kiasi cha maji yaliyohifadhiwa ardhini hakiongezeki. Kwa hiyo, watabiri wa hali ya hewa hukisia kwamba baada ya miaka 25, kiasi cha maji kinachohitajiwa kwa kila mtu duniani kitapungua maradufu.

      Jinsi Upungufu wa Maji Unavyoathiri Afya na Chakula

      Upungufu wa maji huathirije watu? Kwanza kabisa, unadhuru afya yao. Si kwamba watakufa kwa kiu; la, bali maji machafu wanayokunywa na kupikia yanaweza kuwaletea magonjwa. Elizabeth Dowdeswell asema kwamba “asilimia 80 hivi ya magonjwa yote na zaidi ya theluthi ya vifo katika nchi zinazositawi husababishwa na maji machafu.” Katika nchi zenye ukame, maji huchafuliwa mara nyingi na kinyesi cha wanadamu au cha wanyama, madawa ya kuua wadudu, mbolea, au kemikali za viwanda. Familia maskini hulazimika kutumia maji hayo machafu.

      Kama vile maji yanavyohitajiwa ili kuondoa uchafu mwilini mwetu, vivyo hivyo maji mengi yanahitajiwa ili kudumisha usafi ifaavyo. Wanadamu wengi hawana maji. Idadi ya watu wanaoishi katika mazingira machafu iliongezeka kutoka bilioni 2.6 mwaka wa 1990 hadi bilioni 2.9 mwaka wa 1997. Idadi hiyo ni karibu nusu ya watu wote duniani. Na usafi ni jambo muhimu sana kwa uhai. Maofisa wa Umoja wa Mataifa, Carol Bellamy na Nitin Desai walionya hivi katika taarifa ya pamoja waliyotoa: “Watoto wanapokosa maji safi ya kunywa na mazingira safi, afya yao na ukuzi wao huwa hatarini.”

      Uzalishaji wa chakula hutegemea maji. Bila shaka mimea mingi ya mazao hukuzwa kwa maji ya mvua, lakini katika nyakati za karibuni umwagiliaji-maji mashamba umekuwa njia kuu ya kukuza chakula kinacholiwa na idadi inayoongezeka ya watu ulimwenguni. Leo asilimia 36 ya mazao yote ulimwenguni hutegemea kilimo cha umwagiliaji-maji mashamba. Mashamba yanayomwagiliwa maji ulimwenguni yalisitawi sana miaka 20 hivi iliyopita, lakini tangu hapo mashamba hayo yamezidi kupungua.

      Ni vigumu sana kuamini kwamba maji yanazidi kupungua ulimwenguni tunapokuwa na maji mengi nyumbani mwetu na choo safi yenye maji. Hata hivyo, twapaswa kukumbuka kwamba ni asilimia 20 tu ya wanadamu wote wanaofurahia hali kama hizo. Wanawake wengi barani Afrika huteka maji kwa muda wa saa sita kila siku—na mara nyingi maji hayo huwa machafu. Wanawake hao wanaelewa vyema zaidi hali ngumu iliyopo: Kuna uhaba wa maji safi na salama, nayo yanazidi kupungua.

      Je, tekinolojia inaweza kusuluhisha tatizo hilo? Je, maji yaliyopo yanaweza kutumiwa ifaavyo? Mbona kuna upungufu wa maji? Makala zifuatazo zitajibu maswali hayo.

  • Je, Maji Yanazidi Kupungua Ulimwenguni?
    Amkeni!—2001 | Juni 22
    • [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      TATIZO LA MAJI

      ◼ UCHAFUZI Nchini Poland ni asilimia 5 tu ya maji ya mito yanayofaa kunywewa, na asilimia 75 ni machafu mno hivi kwamba hayawezi kutumiwa viwandani.

      ◼ KIASI CHA MAJI MAJIJINI Katika jiji la Mexico City, ambalo ni jiji la pili kwa ukubwa duniani, tabaka la maji, ambalo huandaa asilimia 80 ya maji jijini humo, linapungua kasi sana. Matumizi ya maji yanazidi kiasi kilichopo kiasili kwa zaidi ya asilimia 50. Beijing, jiji kuu la China, linakumbwa na tatizo hilohilo. Tabaka lake la maji, linapungua kwa zaidi ya meta moja kwa mwaka, na theluthi ya visima nchini humo vimekauka.

      ◼ UMWAGILIAJI-MAJI MASHAMBA Hifadhi kubwa ya maji ya Ogallala nchini Marekani imepungua sana hivi kwamba mashamba yaliyokuwa yakimwagiliwa maji kaskazini-magharibi mwa Texas yamepungua ukubwa kwa theluthi kwa sababu ya ukosefu wa maji. China ambayo ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa chakula ulimwenguni na India ambayo ni nchi ya tatu, zinakabili tatizo hilohilo. Katika jimbo la Tamil Nadu lililo kusini mwa India, umwagiliaji-maji mashamba umefanya tabaka la maji lipungue kwa zaidi ya meta 23 katika muda wa miaka kumi.

      ◼ MITO INAYOTOWEKA Kunapokuwa na ukame, Mto Ganges ulio mkubwa haufiki tena baharini, kwani maji yake yote huelekezwa kwingineko kabla ya kufika baharini. Ndivyo inavyokuwa kwa habari ya Mto Colorado katika Amerika Kaskazini.

      [Ramani katika ukurasa wa 3]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      SEHEMU ZISIZOKUWA NA MAJI YA KUTOSHA

      Maeneo yenye ukosefu wa maji

  • Mbona Kuna Ukosefu wa Maji?
    Amkeni!—2001 | Juni 22
    • Mbona Kuna Ukosefu wa Maji?

      Cherrapunji, nchini India, ni mojawapo ya sehemu zenye mvua nyingi zaidi duniani. Wakati wa pepo za msimu, mvua nyingi ya kipimo cha milimeta 9,000 hunyesha kwenye vilima vilivyo karibu na Milima ya Himalaya. Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kuwa Cherrapunji pia hukumbwa na ukosefu wa maji.

      MAJI ya mvua hutiririka kasi sana kwani hakuna mimea inayoweza kuhifadhi maji hayo kwenye udongo. Kunakuwa na ukosefu mkubwa wa maji miezi miwili hivi baada ya mvua ya msimu kunyesha. Miaka mingi iliyopita Robin Clarke, katika kitabu chake Water: The International Crisis, alisema Cherrapunji ni “jangwa lenye mvua nyingi zaidi duniani.”a

      Bangladesh iko upande wa chini wa Cherrapunji. Bangladesh ni nchi yenye watu wengi, iliyo kwenye uwanda wa chini, ambayo huathiriwa sana na mafuriko ya mvua ya msimu. Mafuriko hayo hutiririka kutoka sehemu zenye vilima nchini India na Nepal. Katika miaka mingine, theluthi mbili ya eneo la Bangladesh hufurika maji. Lakini mafuriko yanapopungua, maji ya Mto Ganges hupungua sana na nchi hukauka. Kila mwaka zaidi ya watu milioni 100 nchini Bangladesh hukumbwa na mafuriko na ukame unaosababisha hasara. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba maji ya visima nchini humo yamechafuliwa na kemikali ya aseniki, na yaelekea sumu hiyo imeathiri mamilioni ya watu.

      Maji katika jiji la Nukus, nchini Uzbekistan, karibu na Bahari ya Aral, yamejaa chumvi wala si aseniki. Mimea ya pamba imefunikwa na chumvi ambayo inaizuia kukua. Chumvi kutoka kwenye udongo wa chini uliojaa maji hurundikana juu ya ardhi. Tatizo hilo, la mrundikano wa chumvi si jipya. Miaka 4,000 iliyopita, kilimo kilididimia nchini Mesopotamia kwa sababu ya tatizo hilohilo. Umwagiliaji-maji mashamba kupita kiasi pamoja na kukwama kwa maji hufanya chumvi iliyo kwenye udongo irundikane juu. Ni lazima maji mengi yasiyo na chumvi yatumiwe ili kukuza mazao ya kutosha. Hata hivyo, mwishowe udongo hukosa rutuba kabisa kwa miaka mingi ijayo.

      Mbona Kuna Ukosefu wa Maji?

      Inasikitisha kwamba mara nyingi ni mvua kubwa inayonyesha kwenye eneo hilo. Hilo husababisha mafuriko na maji kutiririka kasi sana kuelekea baharini. Sehemu fulani hupata mvua nyingi ilhali nyingine hupata mvua kidogo. Cherrapunji imekuwa na sifa ya kurekodi mvua inayozidi milimeta 26,000 kwa muda wa miezi 12, ilhali Jangwa la Atacama kaskazini mwa Chile laweza kukosa mvua nyingi kwa miaka kadhaa.

      Isitoshe, watu wengi duniani wanaishi sehemu zisizokuwa na maji ya kutosha. Kwa kielelezo, ni watu wachache sana wanaoishi kwenye maeneo ya kitropiki ya Afrika na Amerika Kusini yanayopata mvua nyingi sana. Asilimia 15 ya maji ya mvua inayonyesha duniani kila mwaka hutiririka kwenye Bahari ya Atlantiki kutoka kwenye Mto Amazon ulio mkubwa. Lakini eneo hilo lina wakazi wachache kwa hiyo ni kiasi kidogo sana cha maji hayo kinachotumiwa. Kwa upande mwingine, watu wapatao milioni 60 huishi nchini Misri, ambako mvua ni haba, na kiasi kikubwa cha maji wanayotumia hutoka kwenye Mto Nile uliopungua.

      Miaka iliyopita upungufu huo wa maji haukusababisha matatizo makubwa. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba katika mwaka wa 1950, hakuna sehemu hata moja duniani iliyokuwa na upungufu mkubwa sana wa maji. Lakini mambo yamebadilika. Kiasi cha maji yanayotumiwa na kila mtu katika maeneo yenye ukame ya Afrika Magharibi na Asia ya Kati, kimepungua hadi sehemu moja kwa kumi ya kiasi kilichotumiwa mwaka wa 1950.

      Uhitaji mkubwa wa maji umesababishwa na hali nyinginezo mbali na kuongezeka kwa idadi ya watu na uhaba wa mvua katika maeneo yenye watu wengi. Katika ulimwengu wa leo, ufanisi na maendeleo huhusiana moja kwa moja na kuwapo kwa maji ya kutosha.

      Uhitaji Unaoongezeka wa Maji

      Iwapo unaishi katika nchi iliyositawi kiviwanda, bila shaka umeona kwamba viwanda vingi hujengwa karibu na mito mikubwa. Ni kwa sababu moja tu. Viwanda vinahitaji maji ili kutengeneza karibu kila bidhaa, kutia ndani kompyuta na vibanio vya karatasi. Viwanda vinavyotengeneza chakula pia hutumia maji mengi sana. Vituo vya nguvu za umeme hutumia maji mengi kupindukia na kwa hivyo hujengwa kandokando ya maziwa au mito.

      Kilimo hutumia maji mengi hata zaidi. Maeneo mengi yanapata kiasi kidogo sana cha mvua au hainyeshi kwa ukawaida na hivyo si rahisi kupata mavuno mazuri. Kwa hiyo, umwagiliaji-maji mashamba ulionwa kuwa njia ifaayo ya kukuza chakula kwa ajili ya wanadamu wenye njaa. Kilimo cha umwagiliaji-maji mashamba kimesitawi sana hivi kwamba kiasi kikubwa cha maji safi duniani hutumiwa kwa kilimo.

      Isitoshe, kiasi cha maji yanayotumiwa nyumbani kimeongezeka. Katika miaka ya 1990, idadi kubwa sana ya wakazi wapya wa mijini wapatao milioni 900 walihitaji maji safi na mazingira safi. Vyanzo vya asili vya maji, kama vile mito na visima, haviwezi kuandaa maji ya kutosha kwa majiji makubwa. Kwa mfano, Mexico City sasa inahitaji kusambaza maji kwa mabomba kwa umbali wa kilometa 125 na kuyasukuma kwa mashine kupitia milima yenye kimo cha meta 1,200 juu ya usawa wa bahari wa jiji hilo. Katika ripoti yake ya Water: The Life-Giving Source, Dieter Kraemer asema kwamba mabomba hayo ni “kama mikono ya pweza; yanaenea kutoka jijini ili kujaribu kuvuta maji.”

      Kwa hiyo, viwanda, kilimo, na miji imekuwa iking’ang’ana ili kupata maji zaidi. Na kwa sasa sehemu hizo zimefaulu kupata maji kwa kuvuta maji yaliyo ardhini. Tabaka lenye maji ni mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi za maji yasiyo na chumvi duniani. Lakini hifadhi hizo za maji zinaweza kwisha. Hifadhi hizo za maji zinaweza kulinganishwa na pesa katika benki. Pesa zilizo akibani zitakwisha iwapo utazitumia tu bila kuweka pesa zaidi katika akiba hiyo. Muda si muda, hutakuwa na pesa za kutoa.

      Matumizi Yanayofaa na Yasiyofaa ya Maji ya Ardhini

      Maji ya ardhini ni maji tunayoteka visimani. Ripoti ya Groundwater: The Invisible and Endangered Resource iliyoandikwa na Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa yakadiria kwamba nusu ya maji yanayotumiwa nyumbani na katika kilimo hutoka visimani. Watu wa mijini na mashambani hupenda kunywa maji ya visima kwa sababu huwa si machafu kama maji yanayotiririka mitoni. Maji ya visima yangedumu kwa muda mrefu iwapo watu wangeyatumia kwa kiasi, kwa kuwa hifadhi hizo za ardhini hujaa wakati maji ya mvua yanapopenya taratibu ardhini. Lakini kwa miaka mingi wanadamu wamekuwa wakitumia maji mengi kupita ujazo wake wa kiasili.

      Tokeo ni kwamba maji ya visima yanazidi kupungua, na basi kuyavuta maji hayo ni kazi bure kwa sababu inagharimu pesa nyingi sana na si kazi rahisi. Uchumi huzorota na watu huteseka wakati visima vinapokauka. Magumu hayo yameanza kuikumba India. Hali hiyo inatisha kwa sababu wakazi bilioni moja wa nyanda za kati za China na India hutegemea maji ya visima ili kupata chakula.

      Mbali na kutumiwa kupita kiasi, maji ya visima yanachafuliwa sana. Maji hayo huchafuliwa na mbolea za kilimo, vinyesi vya wanadamu na wanyama na kemikali za viwandani. “Maji yaliyo katika tabaka la ardhini yanapochafuliwa, kazi ya kuyasafisha hugharimu pesa nyingi na huchukua muda mrefu, na huenda hata isiwezekane,” yaeleza ripoti moja iliyochapishwa na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni. ‘Yasemekana kwamba kuchafuliwa polepole kwa maji ya visima kunawafanya wanadamu wahofu kuzuka kwa msiba mbaya kwa sababu ya maji yenye kemikali. Wanadamu wamo hatarini.’

      Jambo la kushangaza ni kwamba huenda maji yanayovutwa kutoka visimani yakaharibu ardhi badala ya kuboresha kilimo kama ilivyokusudiwa. Sehemu kubwa sana ya mashamba yanayomwagiliwa maji katika nchi zenye ukame ulimwenguni imeharibiwa na chumvi. Huko India na Marekani—nchi zinazoandaa chakula kingi zaidi ulimwenguni—asilimia 25 ya mashamba yanayomwagiliwa maji tayari yameharibika kabisa.

      Kuhifadhi Hufaidi

      Licha ya matatizo hayo yote, hali haingekuwa mbaya kama maji muhimu sana yaliyo duniani yangetumiwa kwa uangalifu. Umwagiliaji-maji mashamba kwa njia isiyofaa hufanya asilimia 60 ya maji yapotee bure. Kutumia tekinolojia mpya na mbinu zifaazo kwaweza kupunguza maradufu matumizi ya maji viwandani. Na kiasi cha maji yanayotumiwa mijini kinaweza kupunguzwa kwa asilimia 30 ikiwa mabomba yaliyotoboka yatarekebishwa mara moja.

      Jitihada za kuhifadhi maji zitafaulu watu wakiwa na nia na njia za kufanya hivyo. Je, kuna sababu nzuri za kutufanya tuamini kuwa maji muhimu ya dunia yetu yatahifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo? Makala yetu ya mwisho itajibu swali hilo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona makala “Cherrapunji—Mojawapo ya Sehemu Zenye Mvua Nyingi Zaidi Duniani,” katika gazeti la Amkeni! la Mei 8, 2001.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      MAJI HUENDELEZA MAISHA DUNIANI

      Karibu shughuli zote za viwandani hutumia maji mengi sana.

      ◼ Utengenezaji wa tani moja ya feleji waweza kutumia tani 280 za maji.

      ◼ Kutengeneza kilogramu moja ya karatasi kwaweza kutumia kilogramu 700 za maji (ikiwa kiwanda hakisafishi na kutumia maji yaleyale).

      ◼ Watengenezaji wa magari hutumia kiasi cha maji ambacho ni mara 50 zaidi ya uzito wa gari lenyewe.

      Maji mengi sana hutumika kwa kilimo hasa ikiwa mifugo imefugwa kwenye maeneo yenye ukame duniani.

      ◼ Ili kutayarisha kilogramu moja ya nyama ya ng’ombe kutoka California, lita 20,500 za maji zinahitajika.

      ◼ Kumsafisha na kumhifadhi kuku mmoja kwenye friji hutumia angalau lita 26 za maji.

      [Grafu/Picha katika ukurasa wa 8]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      MAJI HUTUMIWA WAPI?

      Kilimo asilimia 65

      Viwandani asilimia 25

      Nyumbani asilimia 10

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Mamilioni ya lita za maji humwagika kwa sababu ya mabomba yaliyotoboka na mifereji inayoachwa bila kufungwa

      [Picha zimeandaliwa]

      AP Photo/Richard Drew

  • Maji Halisi na ya Kiroho Ni Muhimu kwa Uhai
    Amkeni!—2001 | Juni 22
    • Maji Halisi na ya Kiroho Ni Muhimu kwa Uhai

      ZAIDI ya miaka 2,000 iliyopita, jiji moja mashuhuri lenye wakazi 30,000 lilisitawi katika Jangwa la Arabia. Ijapokuwa jiji hilo la Petra lilikuwa na ukame, na kwa wastani lilipata mvua yenye kipimo cha milimeta 150 kwa mwaka, wakazi wake walizoea kuishi bila maji ya kutosha. Jiji la Petra lilisitawi sana na kuwa na ufanisi.

      Wakazi wa Petra (Wanabatea) hawakuwa na mashine za umeme za kupiga maji. Hawakujenga mabwawa makubwa ya maji. Hata hivyo, walijua jinsi ya kuvuta na kuhifadhi maji. Walisambaza maji jijini na kwenye mashamba yao madogo kwa mifereji, mabwawa, na matangi ya kuhifadhia maji. Walihifadhi maji kwa udi na uvumba. Walijenga visima na matangi yao kwa njia nzuri sana hivi kwamba Wabedui wa kisasa bado huyatumia.

      “Mfumo wa maji wa Petra unavutia ajabu,” asema mtaalamu mmoja wa maji kwa mshangao. ‘Wakazi wa Petra walikuwa na akili na uwezo usio wa kawaida.’ Hivi karibuni, wataalamu wa Israeli wamejaribu kuiga ustadi wa wakazi hao wa Petra. Wakazi hao walikuza mimea katika Negebu, ambako mvua isiyozidi milimeta 100 hunyesha kila mwaka. Wataalamu wa kilimo wamechunguza maelfu ya mashamba madogo yaliyosalia ya wakazi hao. Wakazi hao walikusanya maji ya mvua kwa ustadi kupitia mifereji na kuyaelekeza kwenye mashamba yao.

      Tayari wakulima wanaoishi kwenye nchi zenye ukame katika jangwa la Sahel barani Afrika wanatumia mbinu za wakazi wa Petra. Hata hivyo, mbinu za kisasa za kuhifadhi maji zina matokeo pia. Katika Lanzarote, kimojawapo cha Visiwa vya Canary, kilicho karibu na pwani ya Afrika, wakulima wamejifunza kukuza zabibu na tini kwenye maeneo yasiyopata mvua kabisa. Wao hupanda mizabibu au mitini ndani ya mashimo halafu hutia majivu ya volkano juu ya udongo ili kuzuia maji yasiwe mvuke. Umande wa kutosha hutiririka mizizini na hivyo wanavuna kwa wingi.

      Utatuzi kwa Kutumia Mbinu Sahili

      Kotekote ulimwenguni watu fulani wamefaulu kuishi kwenye maeneo yenye ukame—kutia ndani Wabishnoi, wanaoishi kwenye Jangwa la Thar huko India; wanawake Waturkana wanaoishi Kenya; na Wahindi wa Navajo wanaoishi Arizona, Marekani. Mbinu wanazotumia kukusanya maji ya mvua, ambazo wamejifunza kwa karne nyingi, zinawasaidia kujiruzuku kupitia kilimo kuliko mbinu za kisasa za tekinolojia.

      Mabwawa mengi yalijengwa katika karne ya 20. Watu walitumia maji ya mito mikubwa, na mifumo mikubwa ya umwagiliaji-maji mashamba ilibuniwa. Mwanasayansi mmoja akadiria kwamba asilimia 60 ya mito na vijito vyote ulimwenguni vimedhibitiwa kwa njia fulani. Ijapokuwa miradi hiyo ilileta manufaa fulani, wataalamu wa mazingira na viumbe wanaeleza jinsi ambavyo mazingira yameharibiwa na jinsi ambavyo mamilioni ya watu wameathiriwa baada ya kupoteza makao yao.

      Isitoshe, wakulima wanaohitaji maji sana hawafaidiki kutokana na miradi hiyo iliyoanzishwa kwa makusudi mazuri. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa India Rajiv Gandhi alisema hivi kuhusiana na miradi ya umwagiliaji-maji mashamba nchini humo: “Kwa miaka 16 tumetumia pesa nyingi. Watu hawajafaidika kwa vyovyote, mashamba hayamwagiliwi maji, hakuna maji, uzalishaji haujaongezeka, maisha ya watu yangali magumu.”

      Kwa upande mwingine, mbinu sahili za kilimo ziliboresha hali na hazikuharibu mazingira. Vidimbwi vidogo na mabwawa milioni sita yaliyojengwa na jumuiya yamewasaidia sana watu nchini China. Nchini Israel, watu wamegundua kwamba maji yaliyotumiwa nyumbani yanaweza kutumiwa tena katika kilimo cha umwagiliaji-maji mashamba.

      Mbinu nyingine inayofanya kazi ni kudondosha matone ya maji mashambani (drip irrigation). Mbinu hiyo huhifadhi udongo na hutumia asilimia 5 tu ya maji yanayotumiwa katika mbinu za kawaida za kumwagilia maji mashamba. Kutumia maji kwa hekima kwamaanisha pia kupanda mazao ambayo yanasitawi katika maeneo yenye ukame, kama vile mawele au mtama, badala ya mazao yanayohitaji maji mengi, kama vile miwa au mahindi.

      Wale walio nyumbani na viwandani wanaweza kujitahidi kupunguza kiasi cha maji wanachotumia. Kwa mfano, kilogramu moja ya karatasi inaweza kutengenezwa kwa lita moja hivi ya maji ikiwa kiwanda kinasafisha na kutumia maji yaleyale—na hivyo kuhifadhi zaidi ya asilimia 99 ya maji. Jiji la Mexico City limeacha kutumia vyoo vya kawaida na badala yake linatumia vyoo vinavyotumia theluthi ya maji waliyotumia mbeleni. Jiji hilo pia lilifadhili kampeni ya kuelimisha watu ili kupunguza matumizi ya maji.

      Utatuzi Unategemea Nini?

      Utatuzi wa matatizo ya maji—na matatizo mengi ya mazingira—unategemea kubadili mitazamo. Watu wanahitaji kushirikiana badala ya kuwa na ubinafsi, kujidhabihu iwezekanapo, na kuazimia kutunza dunia kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kuhusiana na hilo Sandra Postel, aeleza hivi katika kitabu chake Last Oasis—Facing Water Scarcity: “Tunahitaji kuwa na kanuni za maji—ili kutusaidia kutenda ifaavyo tunapokabili maamuzi magumu kuhusu mifumo ya asili ambayo hatuelewi na tusiyoweza kuelewa kikamili.”

      Bila shaka, ni lazima hizo “kanuni za maji” zimhusu kila mtu. Nchi zinahitaji kushirikiana na nchi jirani, kwa kuwa mito hutiririka katika nchi mbalimbali. Ismail Serageldin asema hivi katika ripoti yake Beating the Water Crisis (Kutatua Tatizo la Maji): “Sasa ni lazima mahangaiko kuhusu kiasi na hali ya maji—mambo ambayo hapo awali yalionwa kuwa hayahusiani—yaonwe kuwa matatizo yanayoathiri ulimwengu wote.”

      Lakini Katibu-Mkuu wa UM Kofi Annan akiri kwamba kuunganisha mataifa ili yashughulikie matatizo yanayoathiri ulimwengu wote si kazi rahisi. Asema hivi: “Mbinu zilizopo leo za kutatua tatizo la maji ulimwenguni pote ni za hali ya chini sana. Huu ndio wakati ufaao wa kuzingatia kwa uzito wazo la ‘jamii ya kimataifa.’”

      Kwa wazi, kuwa na afya bora na maisha yenye furaha hakutegemei kuwa na maji safi ya kutosha peke yake—japo maji ni muhimu. Ni lazima wanadamu watambue wajibu wao kwa Yule aliye chanzo cha maji na uhai. (Zaburi 36:9; 100:3) Na badala ya kutumia vibaya dunia na rasilimali zake, wanahitaji ‘kuilima na kuitunza,’ kama Muumba wetu alivyowaagiza wazazi wetu wa kwanza.—Mwanzo 2:8, 15; Zaburi 115:16.

      Maji Bora Zaidi

      Kwa kuwa maji ni muhimu sana, si ajabu kwamba Biblia huyatumia kwa njia ya mfano. Kwa kweli, ili kufurahia maisha kama ilivyokusudiwa, ni lazima tutambue chanzo cha maji hayo ya mfano. Ni lazima tujifunze pia kuwa na mtazamo kama ule wa mwanamke aliyeishi katika karne ya kwanza aliyemwomba hivi Yesu Kristo: “Bwana, nipe maji hayo.” (Yohana 4:15) Fikiria jambo lililotukia.

      Yesu alisimama penye kisima chenye kina kirefu karibu na mji wa kisasa wa Nablus. Mara nyingi watu kutoka kote ulimwenguni hutembelea kisima hicho hata leo. Wakati huo, mwanamke Msamaria alifika pia kisimani. Kama wanawake wengi walioishi karne ya kwanza, bila shaka alienda mara nyingi kuteka maji kisimani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Lakini Yesu alimwambia kwamba angempa “maji yaliyo hai”—maji ambayo yatabubujika milele.—Yohana 4:10, 13, 14.

      Kwa wazi, mwanamke huyo alipendezwa na habari hiyo. Lakini, bila shaka, “maji yaliyo hai” ambayo Yesu alirejezea hayakuwa maji halisi. Yesu alikuwa akizungumzia maandalizi ya kiroho ambayo yatawawezesha watu kuishi milele. Hata hivyo, kuna uhusiano kati ya maji halisi na maji ya mfano—tunahitaji yote ili kufurahia maisha kikamilifu.

      Pindi kwa pindi, Mungu aliwapa watu wake maji halisi kulipokuwa na ukosefu wa maji. Kwa mwujiza aliuandalia umati mkubwa wa Waisraeli wakimbizi maji walipokuwa wakivuka jangwa la Sinai kuelekea Bara Lililoahidiwa. (Kutoka 17:1-6; Hesabu 20:2-11) Elisha, nabii wa Mungu, alikitakasa kisima cha Yeriko kilichokuwa na maji machafu. (2 Wafalme 2:19-22) Na mabaki ya Waisraeli wenye kutubu waliporejea nyumbani kutoka Babiloni, Mungu aliwapa “maji jangwani.”—Isaya 43:14, 19-21.

      Dunia inahitaji kwa haraka ugavi usiokwisha wa maji leo. Kwa kuwa Muumba wetu, Yehova Mungu, alitatua matatizo ya maji hapo kale, je, hatafanya hivyo wakati ujao? Biblia inatuhakikishia kwamba atafanya hivyo. Mungu aeleza hivi kuhusu hali zitakazoletwa na Ufalme ambao ameahidi: “Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji, . . . ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo.”—Isaya 41:18, 20.

      Biblia inatuahidi kwamba wakati huo, watu “hawataona njaa, wala hawataona kiu.” (Isaya 49:10) Utawala mpya wa dunia utatatua kabisa tatizo la maji. Utawala huo—Ufalme, ambao Yesu alitufundisha kusali juu yake—utategemezwa “kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele.” (Isaya 9:6, 7; Mathayo 6:9, 10) Tokeo ni kwamba mwishowe watu wote duniani watakuwa jamii ya kimataifa ya kweli.—Zaburi 72:5, 7, 8.

      Tukitafuta maji ya kiroho sasa, tutakuwa na tumaini la kuishi wakati ambapo kila mtu atakuwa na maji ya kutosha kabisa.

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Juu: Wakazi wa kale wa Petra walijua kuhifadhi maji

      Chini: Mfereji wa maji uliojengwa na Wanabatea huko Petra

      [Hisani]

      Garo Nalbandian

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Wakulima kwenye kimojawapo cha Visiwa vya Canary wamejifunza kukuza mimea kwenye maeneo yasiyopata mvua kabisa

      [Picha katika ukurasa wa 13]

      Yesu alimaanisha nini alipoahidi kumpa huyo mwanamke “maji yaliyo hai”?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki