-
Sehemu Zenye Shida ZaidiAmkeni!—1997 | Agosti 22
-
-
Sehemu Zenye Shida Zaidi
MARY, aishiye Marekani, huanza siku yake kwa kuoga katika bafu ya manyunyu, kupiga meno yake mswaki kwa maji ya mfereji yanayotiririka, kuvuta maji ya choo, halafu yeye hunawa mikono. Hata kabla ya kuketi ili apate kiamsha-kinywa, yeye aweza kutumia maji ya kuweza kujaza hodhi ya wastani. Kufikia mwisho wa siku, Mary, kama ilivyo na watu wengineo wengi waishio Marekani, huwa ametumia zaidi ya lita 350 za maji, za kutosha kujaza hodhi mara mbili na nusu. Kwake, maji safi na yaliyo mengi yako karibu sana kwenye mfereji tu. Hayo yanapatikana sikuzote; naye huyaona kuwa kitu cha kawaida tu.
Kwa Dede, aishiye Afrika Magharibi, hali ni tofauti. Yeye huamka kabla ya mapambazuko, huvaa, hubeba beseni kubwa kichwani bila kuishika, na kutembea kilometa nane hadi kwenye mto ulio karibu zaidi. Huko yeye huoga, hujaza beseni maji, kisha hurudi nyumbani. Kawaida hii ya kila siku huchukua muda wa saa nne hivi. Kwa saa nyingine ifuatayo, yeye huyachuja maji hayo ili kuondoa vimelea na kuyatenganisha katika viwekeo vitatu—kimoja cha kunywa, kimoja cha matumizi ya nyumbani, na kingine cha kuogea jioni. Nguo zozote ni lazima zifuliwe mtoni.
“Njaa ya maji inatuua hapa,” Dede asema. “Baada ya kutumia karibu nusu ya asubuhi kuchota maji, ni muda gani wa siku ubakio wa kulima na wa utendaji mwingine mbalimbali?”
Hali ya Dede si ya kipekee hata kidogo. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), jumla ya wakati unaotumiwa kila mwaka na wanawake wengi na watoto wengi waendao kuchota na kubeba maji kutoka mbali, ambayo mara nyingi yamechafuliwa, hufikia miaka milioni kumi!
Wengine Wanayo, Wengine Hawana
Kwa hiyo ingawa kuna maji matamu tele ulimwenguni pote, hayapo kila mahali kwa kiwango kilekile. Hilo ndilo tatizo kuu la kwanza. Kwa mfano, wanasayansi wanakadiria kwamba ingawa Asia ina asilimia 36 ya maji yanayojaza maziwa na mito ya ulimwengu, kontinenti hiyo ni makao ya asilimia 60 ya watu ulimwenguni. Tofauti na hiyo, Mto Amazon una asilimia 15 ya maji ya mito ya ulimwengu, lakini ni asilimia 0.4 tu ya watu wa ulimwenguni waishio karibu sana kuweza kuutumia. Usambazaji usio sawa pia unahusu mvua. Maeneo fulani ya dunia ni karibu makame daima; mengine, ingawa si makame sikuzote, mara kwa mara hupatwa na vipindi vya ukame.
Wataalamu kadhaa waamini kwamba huenda wanadamu wamesababisha mabadiliko fulani katika tabia ya nchi inayohusiana na mvua. Ukataji wa miti, kulima eneo fulani kupita kiasi, kulisha mifugo eneo fulani kupita kiasi vyote hufanya bara libaki bila mimea. Watu wengine wasababu kwamba hilo litokeapo, uso wa dunia huakisi nuru ya jua zaidi kurudi kwenye angahewa. Tokeo: Angahewa yapata kuwa yenye joto zaidi, mawingu hutawanyika, na mvua hupunguka.
Bara kame laweza pia kufanya mvua ipunguke kwa sababu sehemu kubwa ya mvua inayonyesha kwenye misitu ni maji ambayo kwanza yalivukizika kutoka kwenye mimea yenyewe—kutoka kwenye majani ya miti na vichaka. Yaani, mimea hutenda kama sifongo kubwa ambayo hufyonza na kushikilia mvua. Ukiondoa miti na vichaka, ni maji machache yatakayovukizika na kufanyiza mawingu ya mvua.
Kadiri ambavyo matendo ya binadamu yanaathiri mvua bado ni jambo linalojadiliwa; utafiti zaidi wabaki kufanywa. Lakini hili ni hakika: Upungufu wa maji umeenea sana. Tayari, upungufu watisha uchumi na hali ya afya katika nchi 80, yaonya Benki ya Ulimwengu. Na tayari, asilimia 40 ya wakazi wa dunia—zaidi ya watu bilioni mbili—hawana maji safi au hawana njia za kuondoa uchafu.
Yanapokabiliwa na upungufu wa maji, kwa kawaida mataifa tajiri hufaulu kuepuka matatizo makubwa. Hayo hujenga mabwawa, hutumia tekinolojia iliyo ghali ili kurejesha maji yake, au hata kutoa chumvi katika maji ya bahari. Mataifa maskini hayawezi kufanya hivyo. Mara nyingi yanalazimika kuchagua ama kupima maji safi, jambo liwezalo kuzuia maendeleo na kupunguza utokezaji wa chakula, au kutumia tena maji yasiyotiwa dawa, jambo ambalo hueneza maradhi. Uhitaji wa maji uongezekapo kila mahali, wakati ujao waonekana kuwa wenye upungufu mkubwa sana wa maji.
Mwongo wa Tumaini
Siku ya Novemba 10, 1980, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilisema kwa uhakika juu ya “Mwongo [uliokuwa ukija] wa Kupatikana Kimataifa kwa Maji ya Kunywa na Usafi wa Kutunza Afya.” Baraza hilo lilisema kwamba mradi ulikuwa kuandaa, kufikia mwaka wa 1990, maji safi kwa wote na usafi wa kutunza afya kwa watu wote waishio katika nchi zinazoendelea. Kufikia mwisho wa mwongo huo, dola bilioni 134 hivi zilikuwa zimetumiwa ili kuleta maji safi kwa zaidi ya watu bilioni moja na vifaa vya kuondoa maji machafu kwa zaidi ya watu milioni 750—matokeo yenye kuvutia sana.
Hata hivyo, maongezeko haya yalisawazishwa na ongezeko la watu milioni 800 katika nchi zinazoendelea. Hivyo, kufikia 1990, kulibaki zaidi ya watu bilioni moja ambao walikosa maji safi na vifaa vya kutosha vya usafi wa kutunza afya. Ilionekana kwamba hali hii ilikuwa ikionyesha kile ambacho malkia alimwambia Alice katika hadithi za watoto Through the Looking-Glass: “Waona, wapaswa kukimbia mbio kadiri uwezavyo, ili kudumisha hali yako ya wakati huu. Ikiwa wataka kufika mahali pengine, ni lazima ukimbie kasi kwa mara mbili zaidi kuliko ukimbiavyo!”
Tangu 1990, maendeleo ya jumla katika kuboresha hali ya wale wasio na maji na usafi wa kutunza afya, kulingana na WHO, ni “vichache sana.” Alipokuwa naibu-msimamizi wa utafiti kwenye Worldwatch Institute, Sandra Postel aliandika: “Yabaki kuwa kasoro kubwa sana ya maadili kwamba watu bilioni 1.2 hawawezi kunywa maji bila kujihatarisha kupatwa na maradhi au kifo. Sababu haihusiani hasa na uhaba wa maji au ukosefu wa tekinolojia bali ni ukosefu wa ujitoaji wa kijamii na wa kisiasa katika kutosheleza mahitaji ya msingi ya maskini. Itachukua dola zipatazo bilioni 36 zaidi kwa mwaka, sawa na asilimia 4 hivi ya matumizi ya kijeshi ulimwenguni, ili kuletea binadamu kile ambacho wengi wetu twakiona kuwa cha kawaida tu—maji safi ya kunywa na njia safi ya kuondoa uchafu.”
Idadi ya Watu Inayoongezeka, Ongezeko la Uhitaji
Usambazaji usio sawa wa maji unafanywa kuwa tata na tatizo la pili: Kadiri idadi za watu ziongezekavyo, ndivyo uhitaji wa maji uongezekavyo. Mvua ulimwenguni pote hubaki kwa kiwango kilekile, lakini idadi za watu huongezeka. Utumizi wa maji umerudufika angalau mara mbili karne hii, na wengine wakadiria kwamba waweza kurudufika tena kwa miaka 20 ijayo.
Bila shaka, idadi zinazoongezeka za watu huhitaji si maji zaidi ya kunywa tu bali pia chakula zaidi. Nao utokezaji wa chakula wahitaji kiwango kikubwa zaidi cha maji. Hata hivyo, ni lazima kilimo kishindane na uhitaji wa maji wa viwanda na wa watu mmoja-mmoja. Kadiri majiji na maeneo ya viwanda yazidivyo kupanuka, mara nyingi kilimo hushindwa. “Chakula kitatoka wapi?” auliza mtafiti mmoja. “Twaweza kutoshelezaje mahitaji ya watu bilioni 10 wakati tunashindwa kutosheleza mahitaji ya watu bilioni 5 na kwa hakika tukipokonya kilimo maji?”
Ongezeko kubwa la idadi ya watu latukia katika nchi zinazoendelea, ambapo mara nyingi kuna uhaba wa maji. Kwa kuhuzunisha, nchi hizo haziwezi kushughulikia matatizo ya maji kifedha na vilevile kiufundi.
Uchafuzi
Ongezea matatizo yaliyopo ya upungufu wa maji na mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka, lile tatizo la tatu: uchafuzi. Biblia husema juu ya “mto wa maji ya uhai,” lakini mito mingi leo ni mito ya kifo. (Ufunuo 22:1) Kulingana na kadirio moja, kiwango cha maji machafu—ya nyumbani na ya viwanda—yanayoingia katika mito ya ulimwengu kila mwaka hufikia kilometa 450 za kyubiki. Mito mingi na vijito vingi vimechafuliwa tangu mwanzo wake hadi mwisho wake.
Katika mataifa ya ulimwengu yanayoendelea, maji machafu yasiyotiwa dawa huchafua karibu kila mto mkubwa. Uchunguzi wa mito mikubwa 200 ya Urusi ulionyesha kwamba 8 kati ya 10 ilikuwa na viwango vya juu vilivyo hatari vya vitu vilivyo na bakteria na virusi. Mito hiyo na tabaka za maji za nchi zilizoendelea sana, ingawa hazijajaa maji machafu, mara nyingi zina kemikali zenye sumu, kutia ndani zile zitokazo katika mbolea za kilimo. Katika karibu sehemu zote za ulimwengu, nchi zilizo kando ya bahari hupiga pampu maji machafu yasiyotiwa dawa katika maji yasiyo na kina kwenye pwani zake, zikichafua vibaya sana fuo.
Hivyo, uchafuzi wa maji ni tatizo la tufeni pote. Kikijumlisha hali yote, kijitabu cha Audubon Society, Water: The Essential Resource hutaarifu hivi: “Thuluthi moja ya wanadamu husedeka daima katika ugonjwa au udhaifu kwa sababu ya maji yasiyo safi; thuluthi nyingine inatishwa na kule kutiwa majini kwa vitu vya kemikali ambavyo athari yake ya muda mrefu haijulikani.”
Maji Yasiyofaa, Afya Mbaya
Dede, aliyetajwa mapema, aliposema kwamba “njaa ya maji inatuua,” alikuwa akisema kitamathali. Hata hivyo, ukosefu wa maji safi na yaliyo matamu huua, kihalisi. Kwake yeye na kwa mamilioni ya watu kama yeye, hakuna namna ila kutumia maji ya vijito na mito, ambavyo mara nyingi ni kama tu mitaro ya maji machafu. Si ajabu kwamba, kulingana na WHO, mtoto mmoja hufa kwa sababu ya maradhi yanayohusiana na maji kwa kila sekunde nane!
Katika nchi zinazoendelea, kulingana na gazeti World Watch, asilimia 80 ya maradhi yote huenezwa kwa sababu ya kutumia maji yasiyo safi. Vijiumbe vya kuleta maradhi katika maji na uchafuzi huua watu milioni 25 kila mwaka.
Maradhi yenye kuua yahusianayo na maji—kutia ndani maradhi fulani ya kuhara, kipindupindu, na homa ya matumbo—huua watu wengi katika maeneo ya Kitropiki. Hata hivyo, maradhi yasababishwayo na maji hayako tu katika nchi zinazoendelea. Mwaka wa 1993, nchini Marekani, watu 400,000 walikuwa wagonjwa katika Milwaukee, Wisconsin, baada ya kunywa maji ya mfereji yaliyokuwa na kijiumbe-maradhi ambacho hakikuweza kuuawa na klorini. Katika mwaka huohuo, vijiumbe-maradhi vilivyo hatari viliingia katika mifumo ya maji ya majiji mengine Marekani—Washington, D.C.; New York City; na Cabool, Missouri—vikilazimisha wakazi wachemshe maji yaliyotoka miferejini.
Kushiriki Maji ya Mito
Matatizo yanayohusiana ya upungufu wa maji, uhitaji wa ongezeko la idadi za watu, na uchafuzi unaotokeza afya mbaya yote ni mambo yanayoweza kusababisha mkazo na mzozo. Kwa vyovyote, maji si anasa. Mwanasiasa fulani aliyekuwa akipambana na shida ya maji Hispania alisema hivi: “Si tena pambano la kiuchumi, bali ni pigano la kusalimika.”
Kisababishi kikubwa cha mkazo ni kushiriki maji ya mito. Kulingana na Peter Gleick, mtafiti nchini Marekani, asilimia 40 ya watu huishi katika mabonde 250 ya mito ambayo maji yake yanashindaniwa na zaidi ya taifa moja. Mito Brahmaputra, Indus, Mekong, Niger, Naili, na Tigris kila mmoja hupitia nchi nyingi—nchi zinazotaka kutoa maji mengi kadiri iwezekanavyo kutoka mito hiyo. Tayari, kumekuwa na mabishano.
Kadiri uhitaji wa maji uzidivyo kuongezeka, mikazo kama hiyo itaongezeka. Naibu-msimamizi wa Maendeleo Yasiyodhuru Mazingira ya Benki ya Ulimwengu atabiri hivi: “Vita vingi katika karne hii vilikuwa juu ya mafuta, lakini vita vya karne ifuatayo vitakuwa juu ya maji.”
-
-
Suluhisho Ni Nini?Amkeni!—1997 | Agosti 22
-
-
Suluhisho Ni Nini?
WATAALAMU wana mijadala motomoto kuhusu masuluhisho ya matatizo tata ya maji ya wanadamu. Benki ya Ulimwengu yataka dola bilioni 600 zitumiwe kwa usafi wa kutunza afya na mipango ya maji kwa miaka kumi ijayo. Gharama ya kutotumia pesa hizo yaweza kuwa juu hata zaidi. Kwa mfano, nchini Peru, mweneo wa kipindupindu kwa majuma kumi, uliosababishwa na maji machafu, hivi majuzi uligharimu karibu dola bilioni 1—mara tatu ya fedha zilizotumiwa katika ugavi wa maji wa hiyo nchi katika mwongo wote wa miaka ya 1980.
Hata hivyo, japo makusudio mazuri ya wale wanaoiendeleza, miradi ya maji mara nyingi haisaidii sana wale walio maskini zaidi. Ongezeko katika majiji makubwa ya nchi zinazoendelea ni la haraka sana na la kiholela. Maskini huishi katika vibanda hafifu vilivyosongamana kupita kiasi na visivyo na maji au usafi wa kutunza afya. Kwa kuwa hawawezi kufikia huduma za maji zinazotolewa na serikali, ni lazima wanunue maji kwa bei ghali kutoka kwa watu binafsi, mara nyingi maji machafu.
Kwa wazi, shida ya maji tufeni pote ni tata na huhusisha visababishi vinavyohusiana: upungufu wa maji, uchafuzi, umaskini, maradhi, na uhitaji unaoongezeka wa idadi za watu zenye kuongozeka. Vivyo hivyo ni wazi kwamba wanadamu hawawezi kutatua matatizo haya.
Msingi wa Kutazamia Mazuri
Hata hivyo, wakati ujao si wenye kuhuzunisha kama wengi watabirivyo. Kwa nini? Kwa sababu suluhisho la shida ya maji ya ulimwengu haliwezi kutolewa na mwanadamu; laweza kutolewa na Mungu. Ni yeye peke yake aliye na uwezo na vilevile nia ya kutatua matatizo yote ya maji.
Si jambo la kutiliwa shaka kwamba Yehova Mungu aweza kutatua matatizo haya. Yeye ndiye Mbuni na Muumba si wa dunia tu bali pia wa maji yaliyo ndani ya dunia. Ni yeye aliyeanzisha duru ya maji ya ajabu pamoja na duru nyinginezo zote za kiasili ambazo hufanya maisha duniani yawezekane. Ufunuo 14:7 humtambulisha Yehova kuwa “Yeye aliyezifanya mbingu na dunia na bahari na mabubujiko ya maji.”
Yehova ana uwezo wa kudhibiti maji ya ulimwengu. Ni “Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi, na kuyapeleka maji mashambani.” (Ayubu 5:10) Juu yake Biblia husema: “Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.”—Zaburi 107:35.
Tena na tena amethibitisha uwezo wake wa kuandaa maji. Kwa mfano, yeye aliwaandalia Waisraeli maji wakati wa miaka 40 jangwani, nyakati fulani kimwujiza. “Akatokeza na vijito gengeni, akatelemsha maji kama mito,” husema Biblia. “Tazama, aliupiga mwamba; maji yakabubujika, ikafurika mito.”—Zaburi 78:16, 20.
Atakalofanya Mungu
Mungu hataruhusu shida ya maji iendelee milele. Biblia hutabiri kwamba wakati waja ambapo atatenda kwa niaba ya wale wote ulimwenguni pote ambao hutamani kuishi chini ya utawala wenye upendo wa serikali yake ya kimbingu, ambayo hivi karibuni itachukua uongozi wa dunia.—Mathayo 6:10.
Serikali hiyo, au Ufalme, itamaliza maradhi yasababishwayo na maji, pamoja na magonjwa mengineyo. Biblia huhakikishia waaminifu-washikamanifu wa Mungu hivi: ‘Mungu atakibarikia chakula chako, na maji yako; naye atakuondolea ugonjwa kati yako.’ (Kutoka 23:25) Isitoshe, wachafuzi wa maji ya dunia wataharibiwa ‘atakapoleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.’—Ufunuo 11:18.
Dunia yote itasitawi chini ya utunzi wenye upendo wa Mungu. Watu hawatapata kung’ang’ana tena kamwe kutafuta maji safi yaliyo matamu. Mungu Mweza Yote, ambaye sikuzote husema kweli, alimpulizia nabii wake aandike hivi kuhusu wakati ujao: “Maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji.”—Isaya 35:6, 7; Waebrania 6:18.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mungu aahidi: “Katika nyika maji yatabubujika; . . . na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji.”—Isaya 35:6, 7
-