-
Mtetezi wa Vita Au Mteteaji wa Amani?Amkeni!—2002 | Mei 8
-
-
Mtetezi wa Vita Au Mteteaji wa Amani?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SWEDEN
Kila mwaka, watu au mashirika ambayo yamejitahidi sana kuboresha hali za wanadamu katika fani mbalimbali hupewa tuzo ya Nobeli. Zoea hilo lilianza lini, na linahusianaje na jitihada za kupata amani ya ulimwenguni pote?
ANAJULIKANA kwa kuchangia maendeleo ya wanadamu. Hata hivyo, alitajirika sana kwa kuuza silaha za vita. Ni nani huyo? Ni Alfred Bernhard Nobel, mwenyeji wa Sweden aliyekuwa mtaalamu wa kemia ambaye alimiliki viwanda. Nobel amesifiwa kwa matendo yake ya fadhili, lakini pia ameitwa “mwuzaji wa kifo.” Kwa nini? Kwa sababu Nobel alibuni baruti kali na alitajirika sana kwa kuunda na kuuza makombora hatari.
Hata hivyo, uvumbuzi fulani wenye kustaajabisha ulifanywa baada ya kifo cha Nobel mnamo mwaka wa 1896. Wasia wake ulisema kwamba dola milioni 9 za Marekani zitengwe na kwamba kila mwaka watu wanaopata mafanikio makubwa ya fizikia, kemia, tiba, fasihi, na amani wapewe riba inayotokana na fedha hizo.
Hapo mwanzoni, watu wengi walishangaa. Inawezekanaje mwuzaji wa makombora kutaka sana kuwakabidhi tuzo watu waliofanya matendo ya fadhili na hata ya kuleta amani? Wengine walidhani kwamba Nobel alisumbuliwa na dhamiri yake kwa sababu alikuwa ametengeneza silaha hatari. Hata hivyo, wengine waliamini kwamba Nobel alikuwa akijitahidi kuleta amani. Yaonekana aliamini kwamba silaha zikiwa hatari zaidi, vita haingetokea. Inaripotiwa kwamba alimwambia hivi mwandishi mmoja: “Huenda viwanda vyangu vitakomesha vita haraka kuliko mabaraza yenu.” Kisha akaongeza hivi: “Wakati ambapo vikosi viwili vya jeshi vitaangamizana mara moja, huenda mataifa yote yaliyostaarabika yataogopa na kuvunja majeshi yao.”
Je, maneno ya Nobel yalitimia? Ni masomo gani ambayo watu walijifunza katika karne iliyofuata kifo cha Nobel?
[Blabu katika ukurasa wa 3]
“Ninataka kubuni kifaa au mashine itakayoweza kuharibu vitu vingi sana hivi kwamba vita itakoma kabisa”—ALFRED BERNHARD NOBEL
-
-
Karne ya UjeuriAmkeni!—2002 | Mei 8
-
-
Karne ya Ujeuri
ALFRED NOBEL aliamini kwamba amani ingeweza kudumishwa iwapo mataifa yangekuwa na silaha hatari. Kwani, mataifa yangeweza kuungana upesi na kumwangamiza adui yeyote. Aliandika kwamba “jambo hilo lingekomesha vita kabisa.” Nobel alionelea kwamba hakuna taifa lolote timamu ambalo lingezusha mapigano iwapo lingeathiriwa vibaya na mapigano hayo. Lakini matukio ya karne iliyopita yameonyesha nini?
Miaka isiyozidi 20 baada ya kifo cha Nobel, Vita ya Kwanza ya Ulimwengu ilianza ghafula. Silaha mpya zilizo hatari zilitumiwa katika mapigano hayo, kama vile bunduki za rashasha, gesi yenye sumu, vifaa vya kurusha mafuta moto, vifaru, ndege, na nyambizi. Wanajeshi wapatao milioni kumi waliuawa, na zaidi ya milioni ishirini wakajeruhiwa. Ukatili uliofanywa katika Vita ya Kwanza ya Ulimwengu uliwafanya watu watamani tena amani. Kwa hiyo, Ushirika wa Mataifa ukaanzishwa. Rais Woodrow Wilson wa Marekani, ambaye alihusika sana katika harakati hizo, alishinda Tuzo ya Nobeli ya Amani mwaka wa 1919.
Hata hivyo, matumaini ya kukomesha vita yaliambulia patupu mnamo mwaka wa 1939, wakati Vita ya Pili ya Ulimwengu ilipozuka. Katika njia nyingi vita hiyo ilikuwa yenye kuogofya kuliko Vita ya Kwanza ya Ulimwengu. Wakati wa mapigano hayo, Adolf Hitler alipanua kiwanda cha Nobel huko Krümmel kikawa mojawapo ya viwanda vikubwa zaidi vya silaha huko Ujerumani, kikiwa na zaidi ya wafanyakazi 9,000. Kisha, mwishoni mwa vita hiyo, kiwanda cha Nobel kiliharibiwa kabisa na ndege za vita za Mataifa ya Muungano, ambazo ziliangusha zaidi ya mabomu elfu moja. Inashangaza kwamba mabomu hayo yalitengenezwa kwa vifaa ambavyo Nobel alibuni.
-