Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Hali ya Mapigano ya Kisasa
    Amkeni!—2001 | Machi 22
    • Mapigano ambayo watu hao walikuwa wameyakimbia yamekuwa ya kawaida katika miaka ya karibuni. Kulingana na ripoti moja, kati ya mapigano makubwa 49 ambayo yamekuwapo tangu mwaka wa 1990, silaha nyepesi zimetumiwa kwenye mapigano 46. Tofauti na mapigano yenye kutumia upanga au mkuki ambayo huhitaji wapiganaji kuwa na uzoefu mkubwa, silaha nyepesi zinaweza kutumiwa na mtu yeyote, awe ana uzoefu au la.a Mara nyingi vijana na watoto huandikishwa jeshini na kulazimishwa kupora, kukata watu viungo, na kuua.

      Mengi ya mapigano hayo si kati ya nchi moja na nyingine, bali ni ya wenyewe kwa wenyewe. Wapiganaji si wanajeshi waliozoezwa katika viwanja vya vita, bali wengi wao ni wakazi wa majiji, miji na vijiji. Kwa sababu mengi ya mapigano hayo hufanywa na watu wasio na mafunzo ya kijeshi, sheria za kawaida za mapigano huvunjwa mara nyingi. Kwa sababu hiyo, imekuwa kawaida kwa wanaume, wanawake na watoto wasio na silaha kushambuliwa vikali. Inaaminika kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaouawa katika mapigano ya siku hizi ni raia wa kawaida. Katika mapigano hayo silaha ndogo-ndogo na silaha nyepesi zimetumika sana.

      Bila shaka, bunduki hazisababishi mapigano moja kwa moja—watu walikuwa wakipigana hata kabla ya baruti kugunduliwa. Hata hivyo, akiba kubwa ya bunduki huenda ikachochea mapigano badala ya kuchochea majadiliano ya amani. Kuwapo kwa silaha huenda kukarefusha muda wa pigano na kuzidisha mauaji.

      Silaha nyepesi zinazotumika katika mapigano ya siku hizi zimesababisha hasara kubwa. Katika miaka ya 1990, silaha nyepesi zilitumiwa kuua watu zaidi ya milioni nne. Watu wengine zaidi ya milioni 40 wamekuwa wakimbizi au wamekosa makao. Silaha ndogo-ndogo zimeharibu utaratibu wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na mazingira ya watu wanaoishi kwenye maeneo yenye mapigano. Shughuli za kutoa msaada wa dharura, kutunza wakimbizi, kudumisha amani, na kuingilia mambo ya kijeshi zimegharimu jamii ya kimataifa makumi ya mabilioni ya dola za Marekani.

      Kwa sababu gani silaha ndogo-ndogo zimetumiwa sana katika mapigano ya siku hizi? Zinatoka wapi? Je, ni jambo gani liwezalo kufanywa ili kupunguza au kumaliza hatari yake? Tutazungumzia maswali hayo katika makala zifuatazo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Mtajo “silaha ndogo-ndogo” humaanisha bunduki na bastola—silaha zinazobebwa na mtu mmoja; na “silaha nyepesi” hutia ndani bunduki za rasharasha, mizinga na vyombo vya kurushia makombora, ambazo nyakati nyingine huhitaji kushughulikiwa na watu wawili.

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

      UN PHOTO 186797/J. Isaac

  • Silaha Ndogondogo, Matatizo Makubwa
    Amkeni!—2001 | Machi 22
    • Silaha Ndogondogo, Matatizo Makubwa

      KWA makumi ya miaka, mazungumzo yanayokusudiwa kudhibiti silaha yalihusu silaha za nyuklia pekee. Haishangazi kwa sababu bomu moja tu la nyuklia lina uwezo wa kuharibu jiji zima. Hata hivyo, tofauti na silaha ndogondogo, silaha hizo zenye uwezo mkubwa kupindukia hazijatumika katika mapigano kwa zaidi ya miaka 50.

      Mwanahistoria wa kijeshi anayestahiwa, John Keegan, aandika hivi: ‘Silaha za nyuklia hazijaua mtu yeyote tangu Agosti 9, 1945. Wale watu 50,000,000 ambao wamekufa kwenye mapigano tangu tarehe hiyo, hasa, wameuawa kwa silaha za bei duni na risasi za mizinga midogo, zenye gharama sawia na redio za kawaida ambazo zimesambazwa ulimwenguni wakati uleule. Kwa sababu silaha hizo za bei rahisi zimeathiri tu hali ya maisha katika mitaa mahususi yenye shughuli za dawa za kulevya na misukosuko ya kisiasa katika nchi tajiri, watu wanaoishi katika nchi hizo hawatambui haraka maafa yanayotokezwa na silaha hizo.’

      Idadi kamili ya silaha ndogondogo zinazomilikiwa na watu haijulikani, lakini wataalamu wanakadiria kwamba kuna silaha za aina hiyo zilizoundwa kwa matumizi ya kijeshi zipatazo milioni 500 hivi. Isitoshe, makumi ya mamilioni ya bunduki na bastola zilizoundwa zitumiwe na watu wa kawaida ziko mikononi mwa watu binafsi. Zaidi ya hilo, aina mpya ya silaha hutengenezwa na kuuzwa kila mwaka.

      Silaha Zinazopendwa Zaidi

      Kwa nini silaha ndogondogo zimekuwa silaha zinazopendwa zaidi katika mapigano ya hivi karibuni? Kwa sehemu, ni kwa sababu ya uhusiano kati ya mapigano na umaskini. Mengi ya mapigano ya miaka ya 1990, yalikumba nchi maskini—nchi zisizo na uwezo wa kununua mifumo ya silaha tata. Silaha ndogondogo na silaha nyepesi ni za bei ya chini. Kwa mfano, dola milioni 50 za Marekani ambazo ni bei ya ndege moja ya kisasa ya kivita, zaweza kununua bunduki za kutosha kikosi chenye wanajeshi 200,000.

      Nyakati nyingine, silaha ndogondogo na silaha nyepesi hununuliwa kwa bei nafuu kuliko hiyo. Majeshi yanayopunguza askari wake huwapa majeshi mengine makumi ya mamilioni ya silaha bila malipo, au huagizwa kutoka sehemu ambazo mapigano yamekoma. Katika nchi fulani, bunduki zinapatikana kwa wingi hivi kwamba huuzwa kwa bei ndogo ya dola sita za Marekani au kubadilishwa kwa mbuzi, kuku au furushi la nguo kuukuu.

      Hata hivyo, mbali na bei nafuu na kupatikana kwa urahisi, kuna sababu nyingine zinazofanya silaha ndogondogo kuwa maarufu. Ni hatari kupindukia. Bunduki moja yaweza kumimina mamia ya risasi kwa dakika moja. Pia hutumika na kudumishwa kwa urahisi. Mtoto wa miaka kumi aweza kufunzwa jinsi ya kutenganisha na kuunganisha sehemu za bunduki. Mtoto aweza pia kujifunza kwa muda mfupi jinsi ya kulenga na kumimina risasi katikati ya umati.

      Sababu nyingine yenye kufanya bunduki kuwa maarufu ni kwamba hudumu na hutumika kwa miaka nyingi. Bunduki aina ya AK-47 na M16, zilizotumiwa na wanajeshi katika Vita ya Vietnam bado zinatumika katika mapigano leo. Baadhi ya bunduki zinazotumika Afrika zilitumika wakati wa Vita ya Kwanza ya Ulimwengu. Zaidi ya hilo, ni rahisi kusafirisha na kuficha bunduki. Farasi mmoja aweza kubeba bunduki 12 hadi kwa kikundi cha wanamgambo walio msituni au mbali mlimani. Msafara mmoja wa farasi unaweza kubeba bunduki zinazotosha kikosi kidogo cha wanajeshi.

      Bunduki, Dawa za Kulevya, na Almasi

      Biashara ya bunduki yenye kuenea ulimwenguni pote inahusisha mambo mengi. Bunduki chungu nzima husafirishwa kihalali kutoka nchi moja hadi nyingine. Baada ya Vita Baridi kukoma, majeshi ya Mashariki na Magharibi yalipunguza wanajeshi na kuuza silaha za ziada au kuzitoa bure kwa serikali za nchi rafiki. Kwa mujibu wa mwandishi mmoja wa Taasisi ya Utafiti wa Amani huko Oslo, Norway, tangu mwaka wa 1995 nchi ya Marekani pekee imetoa bila malipo bunduki, bastola, bunduki ya rasharasha, na vyombo vya kurusha makombora zaidi ya 300,000. Inadhaniwa kwamba ni rahisi zaidi kutoa silaha bila malipo kuliko kuziharibu au kuziweka katika bohari na kuzilinda. Wachunguzi fulani wanakadiria kwamba silaha ndogondogo na silaha nyepesi zenye thamani ya dola bilioni tatu hivi za Marekani huvuka kihalali mipaka ya nchi mbalimbali kila mwaka.

      Biashara haramu ya silaha hizo huenda ikawa kubwa sana. Silaha zinazouzwa kimagendo lazima zilipiwe. Katika nchi fulani za Afrika, baadhi ya makundi ya wanamgambo yamenunua silaha ndogondogo na silaha nyepesi zenye thamani ya mamia ya dola, si kwa pesa taslimu bali kwa almasi zilizoibwa kutoka maeneo yenye migodi ya almasi. Gazeti la The New York Times lilisema hivi: “Katika maeneo yenye serikali fisadi, waasi ni wakatili na mipaka haina ulinzi wa kutosha . . . Watu wametumikishwa, wameuawa, wamekatwa viungo, na wengi wamekosa makao, mifumo ya uchumi imeporomoka kwa sababu ya almasi hiyo inayong’aa.” Ni ajabu iliyoje kwamba kito ambacho kimebadilishwa kwa bunduki huenda kikauzwa katika duka la vito maridadi kikiwa zawadi ghali sana ya kuashiria upendo wa kudumu!

      Silaha zimehusianishwa pia na biashara haramu ya dawa za kulevya. Mashirika ya wahalifu yametumia njia ileile wanayoingizia bunduki kimagendo katika eneo fulani kuwa njia ya kutolea kimagendo dawa za kulevya kutoka eneo hilo. Hivyo, silaha zimekuwa kama sarafu ya kubadilishana na dawa za kulevya.

      Mapigano Yanapokoma

      Mapigano yanapokoma, mara nyingi bunduki zilizotumika huingia mikononi mwa wahalifu. Fikiria juu ya nchi moja ya kusini mwa Afrika ambamo harakati za kisiasa zenye jeuri ziligeuka kuwa uhalifu wenye jeuri. Watu wapatao 10,000 walikufa kwa muda wa miaka mitatu tu kutokana na jeuri ya kisiasa. Mzozo huo ulipokoma, jeuri ya uhalifu iliibuka. Mashindano kati ya madereva wa teksi yalisababisha “mapigano ya teksi,” ambapo majambazi walikodiwa kuwapiga risasi abiria na madereva wa teksi za makampuni ya wapinzani. Mara nyingi, bunduki za kijeshi zilitumiwa katika wizi na uhalifu mwingineo. Katika mwaka mmoja wa hivi karibuni, watu 11,000 waliouawa kwa bunduki nchini humo, ikawa nchi ya pili ulimwenguni isiyo na vita kuwa na kiwango kikubwa hivyo.

      Kujua kwamba wahalifu wana silaha hatari hutokeza hofu na wasiwasi. Katika nchi nyingi zinazositawi, matajiri huishi katika nyumba zilizo kama ngome, zenye kuzingirwa na kuta na ua wa umeme na kulindwa na askari usiku na mchana. Wakazi wa nchi zilizositawi pia hutahadhari. Hilo limethibitika kuwa kweli hata katika maeneo ambayo hayajakumbwa na mizozo ya raia.

      Kwa hivyo, iwe ni katika nchi zenye mapigano au nchi zenye “amani,” bunduki zimechangia hali ya wasiwasi. Hakuna ajuaye athari kamili ya bunduki; wala hatuwezi kujua idadi ya watu walioangamizwa nazo, majeruhi, waliofiwa, na maisha yaliyoharibiwa. Lakini, tunajua kwamba ulimwengu umejaa silaha na kwamba idadi yake yazidi kuongezeka. Watu wengi wanataka jambo fulani lifanywe kuhusu hali hiyo. Lakini ni nini liwezalo kufanywa? Ni jambo gani litakalofanywa? Maswali hayo yatazungumziwa katika makala ifuatayo.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Askari wa Zamani Ajiona Kuwa “Mpumbavu Sana”

      Askari mmoja mvulana aliyeshiriki mapigano yaliyosababisha kukimbia kwa wakimbizi wanaozungumziwa katika makala ya kwanza alijikuta ghafula akiwa fukara na bila kazi ya kuajiriwa katika mji alioshiriki kuuteka. Alikuwa na uchungu mwingi akizungumzia jinsi mwana wa aliyekuwa mkuu wa kikosi chake alivyokuwa akiendesha pikipiki ghali katika barabara za mji huku wale waliokuwa majemadari waking’ang’ania vyeo na kuwania utukufu. “Ninapokumbuka ile miaka mitano niliyoishi msituni, nikiwaua watu na kurushiwa risasi, najiona kuwa mpumbavu sana,” akasema mpiganaji huyo. “Tulikuwa tukipigania watu ambao hatimaye walisahau jinsi vyeo walivyo navyo vilivyopatikana.”

      [Hisani]

      COVER and page 7: Boy soldier: Nanzer/Sipa Press

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      “Huwezi Kujificha”

      Ingawa bunduki ya kisasa ni chombo hatari, kuna mambo haiwezi kufanya. Ina uwezo wa kurusha risasi pekee. Haiwezi kutumiwa kuua watu waliojificha nyuma ya ukuta au boma. Wakati wa hekaheka za mapigano, huenda askari akashindwa kulenga ifaavyo. Katika hali shwari bunduki hiyo inaweza kulenga shabaha kwa usahihi kwa umbali wa meta 460 pekee.

      Jeshi la Marekani limetoa suluhisho la “matatizo” hayo—bunduki mpya ya kisasa yenye uwezo mkubwa iitwayo Objective Individual Combat Weapon (OICW). Bunduki hiyo ni nyepesi sana, na mbali na kurusha risasi yaweza pia kurusha makombora yenye ukubwa wa milimeta 20—maguruneti. Uwezo mwingine wa bunduki hiyo: Inaweza kuua watu waliojificha kwenye boma. Linalohitajika tu ni askari kulenga juu au kando ya shabaha yake. Kisha bunduki hiyo hupima yenyewe umbali wa shabaha na kuongoza guruneti iliyo na fyuzi ndogo ya elektroni ili kulipua guruneti hiyo mahali barabara na kummiminia adui risasi zenye uwezo wa kutoboa deraya. “Uwezo wake wa pekee utawawezesha askari wa Marekani kulenga penye kona,” akasema mwakilishi mmoja wa kampuni inayotengeneza silaha hiyo. Bunduki hiyo yaweza kutumiwa gizani kwa kutumia darubini ndogo yenye kutoa nuru maalum.

      Watengenezaji wa bunduki hiyo wanajigamba kwamba “huwezi kujificha,” kutokana na bunduki hiyo na kudai kwamba silaha hiyo ina uwezo unaozidi mara tano ule wa bunduki aina ya M16 na wa chombo cha kurusha guruneti cha M203. Askari watakaotumia bunduki hiyo hawatahitaji kuhangaikia kulenga kwa makini; bali wanahitaji tu kuchungulia kupitia darubini na kufyatua risasi na maguruneti mengi sana. Iwapo ratiba ya utengenezaji wa bunduki hiyo itafuatwa barabara, kikosi cha kwanza cha askari kitaanza kutumia bunduki hiyo mwaka wa 2007.

      Hata hivyo, wachambuzi wanauliza hivi: Bunduki hiyo itatumiwaje na askari wanapolinda doria katika maeneo yenye watu wengi ambamo huenda maadui wamechangamana na raia wasio na hatia? Hali itakuwaje silaha hiyo ya OICW itakaponunuliwa na majeshi ulimwenguni pote ambao huenda wakaitumia kuangamiza raia wao? Na itakuwaje silaha hiyo itakapokuwa mikononi mwa magaidi na wahalifu?

      [Hisani]

      Alliant Techsystems

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Silaha ndogondogo na silaha nyepesi mara nyingi hulipiwa kwa almasi na dawa za kulevya

  • Je, Silaha Zitaweza Kudhibitiwa?
    Amkeni!—2001 | Machi 22
    • Je, Silaha Zitaweza Kudhibitiwa?

      KATIKA miaka ya hivi karibuni serikali kote ulimwenguni zimezungumzia mbinu za kupambana na biashara haramu ya silaha ndogondogo. Suala hilo limezungumziwa pia na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Ripoti zimetayarishwa, madokezo yametolewa na maazimio kupitishwa. Hata hivyo, wachambuzi wanasema kwamba kukazia uangalifu soko la magendo pekee kwamaanisha kwamba wale wauzaji wakubwa wa silaha—serikali zenyewe—hawatachunguzwa.

      Kwa kweli, si rahisi kubainisha biashara haramu na biashara halali ya silaha. Silaha nyingi haramu ziliuzwa kihalali wakati mmoja. Mara nyingi, silaha ambazo zimeuzwa kwa idara za kijeshi au za polisi huibwa na kuuzwa kimagendo. Isitoshe, ni kawaida kwa mtu aliyenunua silaha kumwuzia mtu mwingine bila mwuzaji wa kwanza kujua au kutoa idhini. Makala moja katika jarida la Arms Control Today yasema hivi: “Zaidi ya kutegemeza juhudi za kupambana na biashara haramu ya silaha nyepesi, serikali za kitaifa hazina budi kuchunguza utendaji wake katika biashara ya wakati huu ya silaha halali.” Ingawa watu wengi wanatumaini kwamba serikali zitachukua hatua kali dhidi ya biashara ya silaha ndogondogo, mwandishi mmoja wa habari alisema hivi: “Labda hatupaswi kuwa na matumaini makubwa kwa sababu washiriki watano wa kudumu wa baraza [la usalama la Umoja wa Mataifa] peke yake, wanamiliki asilimia 80 ya biashara ya silaha ulimwenguni.”

      Urahisi wa kutokeza silaha nyepesi umetatiza jitihada za kudhibiti ongezeko la silaha hizo. Ingawa ni nchi 12 hivi zinazotengeneza silaha tata kama vile, vifaru, ndege, na manowari, makampuni zaidi ya 300 katika nchi 50 sasa yanatengeneza silaha nyepesi. Idadi kubwa na inayoongezeka ya watengenezaji wa silaha hawaongezi tu mabohari ya silaha ya kitaifa bali pia hutoa fursa nyingi kwa wanamgambo, vikundi vya waasi na mashirika ya wahalifu kupata silaha.

      Masuala Yenye Kubishaniwa Sana

      Kufikia hapo, tumezungumzia jinsi silaha ndogondogo zinavyotumika katika nchi zilizokumbwa na mapigano. Hata hivyo, masuala ya uuzaji wa bunduki hubishaniwa zaidi katika nchi ambazo ni shwari bila mapigano. Wale wanaounga mkono sheria kali za uuzaji wa bunduki wanasema kwamba ongezeko la bunduki huongeza idadi ya mauaji. Wanasababu kwamba katika Marekani, ambako sheria za uuzaji wa bunduki ni hafifu na bunduki ni nyingi, kuna kiwango kikubwa cha mauaji, lakini katika Uingereza ambako kuna sheria kali za uuzaji wa bunduki, kiwango cha mauaji ni cha chini. Wanaopinga sheria hizo, husema upesi kwamba nchi ya Uswisi ambayo imeruhusu watu kupata bunduki kwa urahisi ina kiwango cha chini sana cha mauaji.

      Jambo la kutatanisha hata zaidi ni kwamba uchunguzi waonyesha kwamba Marekani ina kiwango kikubwa zaidi cha mauaji yasiyohusisha bunduki kuliko jumla ya mauaji yote katika nchi nyingi za Ulaya. Na bado kuna nchi nyingine zenye mauaji yasiyohusisha bunduki yanayozidi jumla ya mauaji yote katika Marekani.

      Ni kawaida kutumia—au kughushi takwimu ili kutetea maoni fulani. Na katika suala la uuzaji wa bunduki, inaonekana kwamba kwa kila hoja yenye kuunga mkono kuna hoja nyingine kinyume yenye kukubalika. Masuala hayo ni magumu. Hata hivyo, wataalamu wanakubaliana kwa ujumla kwamba zaidi ya watu kuwa na bunduki, kuna sababu nyinginezo zinazoathiri kiwango cha mauaji na uhalifu.

      Shirika la Kitaifa la Bunduki huko Marekani ambalo lina uwezo mkubwa limesema hivi mara nyingi: “Bunduki haziui watu; watu ndio huua.” Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ingawa bunduki imetengenezwa kwa kusudi la kufisha, yenyewe haiui. Lazima mtu fulani afyatue bunduki, kimakusudi au kwa aksidenti. Bila shaka, watu fulani hubisha kwamba bunduki hufanya iwe rahisi kwa watu kuua watu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki