-
“Taraja Lenye Kuogofya”Amkeni!—2002 | Septemba 22
-
-
“Taraja Lenye Kuogofya”
WAZIA tukio lifuatalo. Magaidi wamesambaza kisiri viini vya ugonjwa wa ndui katika maduka matatu makubwa sana nchini Marekani. Viini hivyo vinawavamia wanunuzi wasiokuwa na habari. Juma moja hivi baadaye, madaktari wanagundua kwamba watu 20 wameambukizwa ndui. Siku zinazofuata, watu zaidi wanaambukizwa viini hivyo. Watu wanashikwa na hofu. Maandamano yapamba moto. Vituo na wahudumu wa afya wamelemewa. Mipaka inafungwa. Uchumi umezorota. Siku 21 baada ya shambulizi la kwanza, ugonjwa wa ndui umeenea katika majimbo 25 ya Marekani na katika nchi nyingine 10. Sasa, watu 16,000 wameambukizwa na 1,000 wamekufa. Madaktari wanakadiria kwamba baada ya majuma matatu, watu 300,000 watakuwa wameambukizwa. Asilimia 75 kati yao watakufa.
Hilo si tukio la kuwaziwa tu katika sinema ya kisayansi. Ni jaribio la kompyuta, lililoonyesha jinsi ambavyo mambo yangekuwa iwapo shambulizi la namna hiyo lingetokea. Jaribio hilo lilifanywa Juni 2001 na kikundi kinachochunguza matatizo ya kijamii.
Watu wengi waliona jaribio hilo likiwa halisi sana na lenye kuogofya baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Mashambulizi ya World Trade Center huko New York na makao makuu ya kijeshi ya Pentagon, huko Washington, D.C., yalionyesha wazi kuwa kuna watu wakatili na wenye chuki wanaoweza kuwaangamiza wanadamu wengi sana. Zaidi ya hilo, mashambulizi hayo yalidhihirisha kuwa Marekani na nchi nyingine yoyote inaweza kushambuliwa. Tunaishi katika ulimwengu ambamo magaidi walioazimia wanaweza kuangamiza maelfu ya watu kwa muda mfupi sana.
Kufuatia mashambulizi ya Septemba 11, wanasiasa na wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini Marekani walikuwa shabaha ya shambulizi la viini hatari vya ugonjwa wa kimeta vilivyotiwa ndani ya barua. Watu waliogopa sana. Vyombo vya habari na wataalamu walizidisha hofu hiyo waliposema kuwa huenda magaidi wangeshambulia kwa viini vya magonjwa hatari zaidi kuliko kimeta—kwa mfano tauni au tetekuwanga. Huenda “mataifa yanayounga mkono ugaidi” yalikuwa yakitengeneza viini hivyo katika maabara za siri. Fikiria baadhi ya mambo ambayo yameandikwa hivi majuzi:
“Shirika la Tiba Ulimwenguni linatambua hatari inayoongezeka iwapo silaha za kibiolojia zitatumiwa kushambulia watu kwa tauni inayoweza kusambaa ulimwenguni pote. Bila shaka, mataifa yote yamo hatarini. Shambulizi la viini vya ugonjwa wa ndui, tauni, na kimeta laweza kuwa hatari sana kwa sababu litaleta magonjwa na vifo, na hofu itakayowakumba watu itafanya tatizo liwe baya hata zaidi.”—Shirika la Tiba la Marekani.
“Tofauti na mabomu na gesi za neva, shambulizi la kibayolojia huwa la siri: ugonjwa huenea pasipo kugunduliwa. Mwanzoni ni watu wachache wanaoenda hospitalini. Dalili zake huwatatanisha madaktari au hufanana na zile za magonjwa ya kawaida. Kabla ya wataalamu wa tiba kujua kinachoendelea, majiji mazima-mazima huenda yakawa yameambukizwa.”—Gazeti Scientific American
“Iwapo watu wangeshambuliwa kwa viini vya ugonjwa wa ndui leo, wengi duniani hawangekuwa na kinga, na karibu bilioni mbili wangekufa, kwa sababu ugonjwa huo huua asilimia 30 ya wale walioambukizwa viini vyake.”—Gazeti Foreign Affairs.
‘Nchi zote ziko hatarini. Majiji mazima-mazima huenda yakaambukizwa. Watu bilioni mbili huenda wakafa.’ Hizo ni taarifa zenye kuogofya. Lakini je, shambulizi la kibayolojia linaweza kutokea? Wataalamu wanalifikiria swali hilo. Makala ifuatayo itakusaidia kuelewa masuala yanayohusika.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Wanajeshi wanapambana na shambulizi la kibiolojia la kuwaziwa
[Hisani]
DoD photo by Cpl. Branden P. O’Brien, U.S. Marine Corps
-
-
Silaha za Kibiolojia—Je, Kweli Ni Hatari?Amkeni!—2002 | Septemba 22
-
-
Silaha za Kibiolojia—Je, Kweli Ni Hatari?
JITIHADA za kuwaua watu vitani kwa kutumia viini vya magonjwa si jambo jipya. Katika karne ya 14, huko Ulaya mashariki, maiti za watu waliouawa kwa tauni zilitupwa ndani ya jiji lililozingirwa. Miaka 400 baadaye, maafisa wa Uingereza waliwapatia Wahindi Waamerika mablanketi yaliyotiwa viini vya ugonjwa wa ndui kimakusudi kwenye mkutano wa amani wakati wa Vita vya Wafaransa na Wahindi. Hilo lilisababisha ugonjwa uliochangia sana Wahindi kusalimu amri. Hata hivyo, mwisho wa karne ya 19 ndipo ilipogunduliwa kwamba magonjwa ya kuambukiza husababishwa na viini. Ugunduzi huo ulifungua njia ya kutumia ugonjwa kama silaha, jambo lenye kuogofya.
Bila shaka, maendeleo ya kitiba na ya kisayansi yameongoza pia kwenye uvumbuzi wa madawa na chanjo mbalimbali, ambazo zimesaidia sana kuzuia na kutibu magonjwa. Hata hivyo, magonjwa ya kuambukiza yanaendelea kuwa tisho kubwa, yakiua zaidi ya watu milioni 17 kila mwaka—karibu 50,000 kila siku. Hilo ni jambo lisiloaminika: Wakati wanaume na wanawake wenye akili wanapoendelea kujitolea mhanga kumaliza magonjwa, wengine wanatumia bidii na ustadi mwingi jinsi hiyo kuwashambulia wanadamu wenzao kwa magonjwa.
Jitihada za Kupiga Marufuku Silaha za Kibiolojia
Kwa zaidi ya miaka 25, Marekani, Muungano wa zamani wa Sovieti, na mataifa mengine machache yalijitahidi sana kutengeneza silaha za kibiolojia. Lakini katika mwaka wa 1972, mataifa hayo yalikubaliana kupiga marufuku silaha hizo. Hata hivyo, mataifa fulani yaliendelea kuboresha na kufanya utafiti kwa siri, huku yakiendelea kurundika silaha hizo hatari na kuvumbua njia za kuzitumia.
Kwa nini silaha hizo zilipigwa marufuku? Kulingana na maoni ya watu katika miaka ya 1970, ingawa silaha za kibiolojia ni hatari sana, hazikuwa na matokeo mazuri vitani. Kwanza, matokeo yake hayaonekani mara moja. Jambo jingine ni kwamba matokeo yake hutegemea mabadiliko ya upepo na hali ya hewa. Zaidi ya hayo, mataifa yaliona kwamba taifa moja likishambulia taifa jingine kwa silaha za kibiolojia, huenda hilo jingine likalipiza kisasi kwa kutumia silaha za kibiolojia au za nyukilia. Hatimaye, watu wengi waliona kwamba haikufaa kutumia viini kuwalemaza au kuwaua wanadamu wenzao.
Yaelekea kwamba sababu hizo haziwezi kuwazuia watu waliojawa na chuki wasiozingatia kanuni zozote za maadili ambazo zimekuwapo tangu zamani. Wale wanaotamani kuua wanavutiwa sana na silaha za kibiolojia. Silaha za kibiolojia zaweza kuundwa na kutumiwa kisiri. Huenda yule anayezitumia asijulikane, na hata akijulikana, ni vigumu kuadhibu makundi ya kigaidi yaliyo katika nchi nyingi. Zaidi ya hilo, shambulizi la kibiolojia lililo kimya, lisiloonekana, linaloendelea kwa muda fulani, na ambalo ni hatari laweza kutatiza watu kwa sababu ya hofu ya ghafula. Kushambulia mimea na mifugo kwa magonjwa kwaweza kusababisha upungufu wa chakula na kuzorota kwa uchumi.
Jambo jingine linalowavutia watu kutumia silaha za kibiolojia ni gharama yake ya chini kwa kulinganisha na silaha nyingine. Uchunguzi mmoja ulilinganisha gharama ya kuua raia walio hoi kwa kutumia silaha mbalimbali katika eneo la kilometa moja ya mraba. Gharama ya kutumia silaha za kawaida ilikadiriwa kuwa dola 2,000 za Marekani, silaha za nyukilia dola 800, gesi ya neva dola 600, na silaha za kibiolojia dola 1.
Magaidi Wakabili Magumu ya Kitekinolojia
Ripoti za magazeti zaonyesha kwamba makundi fulani ya kigaidi yamejaribu kutumia silaha za kibiolojia. Hata hivyo, kuna tofauti kubwa kati ya kujaribu kutumia silaha za kibiolojia na kufaulu kuzitumia vitani.
Ili gaidi au makundi ya kigaidi yafaulu kushambulia kwa silaha hizo ni lazima yashinde magumu mengi ya kitekinolojia. Kwanza, ni lazima gaidi apate viini hatari vya ugonjwa. Pili, ni sharti ajue jinsi ya kuvitumia na kuvihifadhi viini hivyo vizuri na kwa njia iliyo salama. Tatu, ni lazima ajue jinsi ya kutengeneza viini vingi vya aina hiyo. Kiasi kidogo cha viini chaweza kuharibu shamba zima la mimea, kuangamiza kundi kubwa la mifugo, au jiji zima la watu, vikitumiwa ifaavyo. Hata hivyo, viini havinawiri vizuri nje ya maabara. Kwa sababu kiasi kidogo tu cha viini ndicho hufikia watu waliokusudiwa, ni lazima kiasi kikubwa sana kitengenezwe ili kuangamiza watu wengi.
Kuna magumu mengine. Ni sharti gaidi ajue jinsi ya kuhifadhi viini vikiwa hai na katika hali nzuri ya kutenda anapovisafirisha kutoka mahali vinapotengenezewa hadi mahali pa kuvitumia. Hatimaye, ni lazima ajue jinsi ya kusambaza viini hivyo kwa njia yenye matokeo. Hii yatia ndani kuhakikisha kwamba viini vyenye ukubwa unaofaa vinafikia watu waliokusudiwa, vinasambazwa katika eneo kubwa vya kutosha, na vinaweza kuambukiza watu wengi. Watafiti wa silaha za kibiolojia wa Marekani wenye uzoefu mkubwa walitumia miaka kumi kukamilisha mfumo wenye kutegemeka wa kutumia silaha hizo. Viini hivyo hufa vinapotupwa hewani, kwa sababu ya mwangaza wa jua na kubadilika-badilika kwa halijoto. Kwa hiyo, ili mtu atumie viini vya magonjwa katika vita ni lazima ajue hali ya viini hivyo vikiwa hewani.
Kwa kuzingatia magumu mengi ya kitekinolojia ya kutumia silaha za kibiolojia, haishangazi kwamba kumekuwa na mashambulizi machache sana ya silaha hizo. Isitoshe, mashambulizi hayo hayajaleta maafa makubwa. Watu watano walikufa kutokana na shambulizi la hivi majuzi la barua zenye viini vya ugonjwa wa kimeta nchini Marekani. Hilo lilikuwa tukio baya, lakini halikuleta maafa makubwa kama ambayo yangesababishwa na bomu dogo au hata bastola. Wachunguzi wamehesabu watu waliokufa kutokana na mashambulizi ya silaha za kemikali na za kibiolojia tangu mwaka wa 1975, na kuona kwamba katika asilimia 96 ya mashambulizi hayo ni watu watatu waliojeruhiwa au kuuawa katika kila shambulizi.
Kwa kuzingatia ugumu uliopo wa kushambulia kwa silaha za kibiolojia, Shirika la Uingereza na Marekani la Habari za Usalama lilisema: “Ingawa serikali zinakabili matisho mengi kutoka kwa magaidi wanaotumia silaha za kemikali na za kibiolojia, watafiti wanaamini kwamba shambulizi kama hilo, ingawa laweza kutokea, huenda lisisababishe maafa makubwa.” Hata ingawa huenda lisiwepo, lakini matokeo ya shambulizi la silaha hizo yanaweza kuwa mabaya sana.
Habari Isiyopendeza
Tumetaja tu mambo yenye kutia moyo kuhusu silaha za kibiolojia: Magumu ya kitekinolojia na historia yanaonyesha kwamba shambulizi la kibiolojia lenye kuleta maafa makubwa huenda lisitokee. Tukisema kifupi, habari isiyopendeza ni hii: Historia haitoi mwongozo mzuri wa matukio ya wakati ujao. Ingawa mashambulizi ya zamani hayakufaulu, yale yajayo yaweza kufaulu.
Kuna mambo ya kuhangaikia. Inaonekana magaidi wanaozidi kuongezeka wameazimia kuua watu wengi. Magenge ya kigaidi yanazidi kupata tekinolojia nyingi zaidi na mengine hata yana pesa na ufundi mwingi kama serikali fulani.
Wataalamu hawahofu kwamba mataifa yatapatia magenge ya kigaidi silaha za kibiolojia. Mtafiti mmoja alisema: “Hata serikali ziwe na ukatili mwingi jinsi gani, zenye tamaa nyingi, au ziwe na msimamo mkali sana, haielekei zitaachia magenge ya kigaidi silaha za kibiolojia ambazo serikali hizo haziwezi kudhibiti kikamili; labda serikali zitumie silaha hizo kushambulia, halafu zitumie magaidi wakati zitashambuliwa.” Jambo linalohangaisha wataalamu ni kwamba wanasayansi waliozoezwa vizuri waweza kutumiwa na magenge ya kigaidi baada ya kuahidiwa mishahara minono.
Viini Vinavyotumiwa Kushambulia
Jambo jingine linalohangaikiwa ni maendeleo ya kibiolojia. Wanasayansi tayari wanafahamu jinsi ya kubadili viini vilivyopo viwe hatari zaidi na rahisi zaidi kutumia. Pia wanaweza kubadili chembe za viini visivyo hatari na kutokeza sumu. Viini pia vinaweza kugeuzwa ili visigunduliwe kwa kutumia njia za kawaida. Zaidi ya hilo, viini vyaweza kubuniwa ili vihimili viuavijasumu, chanjo za kawaida, na tiba. Kwa mfano, wanasayansi waliohama kutoka uliokuwa Muungano wa Sovieti, walidai kuwa walivumbua tauni ambayo ingehimili viuavijasumu 16.
Uvumbuzi zaidi wa kibiolojia na wa chembe za urithi unatarajiwa kuleta mabadiliko zaidi. Wanasayansi waweza kubadili chembe za urithi na kutokeza viini vingi ambavyo ni hatari zaidi, sugu zaidi, na ambavyo ni rahisi kutokezwa na kutumiwa. Wanaweza kutokeza silaha nyingi za kibiolojia kwa kubadili chembe za urithi. Vinaweza kubuniwa ili hata matokeo yake yajulikane mapema na kudhibitiwa. Viini vinaweza kubuniwa kwa njia ya kwamba vitakufa baada ya kujigawanya kwa mara ambazo vimeratibiwa, hivyo vingeua na kisha kutoweka.
Silaha zisizo za kawaida za siri zaweza kuvumbuliwa wakati ujao. Kwa mfano, silaha fulani hususa zingeharibu kinga ya mwili—na kumfanya mgonjwa akose kinga badala ya kumwambukiza ugonjwa fulani. Kwa mfano, kuhusu virusi vya UKIMWI, ni nani ajuaye kama vilitokana na makosa katika chembe za urithi au adui fulani alivitokeza katika maabara yake kwa kubadili mfumo wa urithi?
Maendeleo ya tekinolojia yamebadili maoni ya wanajeshi. Ofisa mmoja wa majeshi ya wanamaji ya Marekani aliandika: “Huu ni mwanzo tu wa kutumia tekinolojia ya silaha za kibiolojia. Ni jambo la kumfanya mtu atue na kufikiri anapotambua kwamba maendeleo zaidi yanakuja.”
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Vita ya Kibiolojia Ni Nini?
Usemi “vita ya kibiolojia” unamaanisha kusambaza kimakusudi ugonjwa kwa binadamu, wanyama, au mimea. Wale wanaoshambuliwa huugua baada ya kuambukizwa na viini vilivyo hai. Viini hivyo huzaana (vingine hutoa sumu), na baada ya muda fulani dalili za ugonjwa huonekana. Silaha nyingine za kibiolojia hulemaza, na nyingine huua. Nyingine hata hushambulia mimea na kuiharibu.
[SandukuBox/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Silaha za Kibiolojia
Kimeta: Ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria ya spora. Dalili za mapema za ugonjwa wa kimeta unaotokana na kuvuta hewa, zinafanana na zile za mafua. Baada ya siku kadhaa, mgonjwa hushindwa kupumua na hushikwa na mshtuko. Mara nyingi aina hiyo ya kimeta huua.
Watu walio katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo wanaweza kujizuia kwa kutumia viuavijasumu. Ni muhimu mgonjwa atibiwe mapema; kuchelewa hupunguza uwezekano wa kupona.
Si rahisi kuambukizwa ugonjwa wa kimeta kutoka kwa mtu mwingine, na huenda hata isitukie kamwe.
Kuanzia mwaka wa 1950, ugonjwa wa kimeta ulianza kutumiwa kama silaha na nchi kadhaa, kutia ndani Marekani na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Idadi ya mataifa yanayodhaniwa kuwa na silaha za kibiolojia yaliongezeka kutoka 10 mwaka wa 1989 hadi 17 katika 1995. Haijulikani ni mataifa mangapi kati ya hayo yanayotumia ugonjwa wa kimeta. Kulingana na uchunguzi mmoja uliofanywa na serikali ya Marekani, kunyunyiza kilogramu 100 za virusi vya kimeta katika jiji kubwa ni sawa na kurusha bomu la haidrojeni.
Ubotuli: Ugonjwa unaodhoofisha misuli unaosababishwa na bakteria yenye sumu. Dalili za sumu hiyo inayotokana na chakula zatia ndani kuona vitu viwili-viwili au kuona kiwi, kusinzia, kukokoteza maneno, kushindwa kumeza chakula, na kukauka mdomo. Misuli hudhoofika kuanzia mabegani kwenda chini. Kudhoofika kwa misuli ya kupumua kwaweza kusababisha kifo. Ugonjwa huo hauwezi kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Dawa ya kuzuia sumu inapotumiwa mapema vya kutosha, yaweza kupunguza athari za dalili na uwezekano wa kufa.
Sumu ya ubotuli inapendwa sana na wale wanaotengeneza silaha, sio tu kwa sababu ina sumu kali sana bali pia kwa sababu ni rahisi kuitengeneza na kuisafirisha. Isitoshe, wale wanaoambukizwa huhitaji kutunzwa kwa muda mrefu. Mataifa mengi yanadhaniwa kuwa yanatengeneza sumu hiyo ili kuitumia kama silaha.
Tauni: Huo ni ugonjwa unaoambukiza sana unaosababishwa na bakteria. Dalili za kwanza za tauni ya nimonia inayoua ni homa, maumivu ya kichwa, kudhoofika na kukohoa. Mshtuko hufuata, na iwapo mgonjwa hatibiwi mapema kwa kutumia viuavijasumu, anaweza kufa.
Watu huambukizana ugonjwa huo kupitia mate.
Katika karne ya 14, kwa kipindi cha miaka mitano tu, tauni iliua karibu watu milioni 13 nchini China na milioni 20 hadi milioni 30 huko Ulaya.
Katika miaka ya 1950 na 1960, Marekani na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti zilibuni njia za kusambaza tauni ya nimonia. Inaaminika kuwa maelfu ya wanasayansi walijitahidi kuutumia ugonjwa huo kama silaha.
Ndui: Ugonjwa huo husababishwa na virusi na huambukiza upesi. Dalili za kwanza hutia ndani homa, uchovu, maumivu ya kichwa na ya mgongo. Baadaye, vidonda vyenye maumivu hutokea na kujaa usaha. Mgonjwa mmoja kati ya watatu hufa.
Ugonjwa wa ndui ulikomeshwa ulimwenguni katika mwaka wa 1977. Chanjo za kawaida zilimalizika katikati ya miaka ya 1970. Kwa hiyo, hali ya kinga ya watu waliochanjwa kabla ya wakati huo, iwapo ipo, haijulikani. Hakuna tiba iliyothibitishwa ya ugonjwa wa ndui.
Ugonjwa huo husambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia mate yenye viini. Mavazi au kitanda chenye virusi hivyo chaweza pia kusambaza ugonjwa huo.
Kuanzia mwaka wa 1980, Muungano wa Sovieti ulianza programu kabambe ya kutengeneza kiasi kikubwa sana cha virusi vya ndui na kubuni njia ya kuvisambaza kwa kutumia makombora ya masafa marefu. Pia, jitihada ya kutokeza virusi vya ndui ambavyo ni hatari zaidi na vyenye kuambukiza zaidi ilifanywa.
[Picha]
Viini vya kimeta na spora ya mviringo
[Hisani]
Vyanzo: U.S. Centers for Disease Control and Prevention, Johns Hopkins Center for Civilian Biodefense Studies.
Mtu anayeugua ugonjwa wa Kimeta: CDC, Atlanta, Ga.; viini vya kimeta: ©Dr. Gary Gaugler, Photo Researchers; viini vya ubotuli: CDC/Courtesy of Larry Stauffer, Oregon State Public Health Laboratory
Viini vya tauni: Copyright Dennis Kunkel Microscopy, Inc.; virusi vya ndui: ©Meckes, Gelderblom, Eye of Science, Photo Researchers; mtu mwenye ugonjwa wa ndui: CDC/NIP/Barbara Rice
[Picha katika ukurasa wa 7]
Hivi majuzi, barua zilizotiwa viini vya kimeta zilisababisha hofu nyingi
[Hisani]
AP Photo/Axel Seidemann ▼
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mabomu ya kemikali/kibiolojia yanayotupwa angani yaliharibiwa baada ya Vita ya Ghuba
[Hisani]
AP Photo/MOD
-
-
Kutafuta SuluhishoAmkeni!—2002 | Septemba 22
-
-
Kutafuta Suluhisho
MWANZONI mwa mwaka wa 1972 zaidi ya mataifa mia moja yalitia sahihi mkataba wa kimataifa uliopiga marufuku kubuni, kuunda, na kuhifadhi silaha za kibiolojia. Mkataba huo ulioitwa Biological and Toxin Weapons Convention (BTWC), ulikuwa wa kwanza kupiga marufuku silaha zote za aina moja. Lakini mkataba huo haukuonyesha njia ya kuhakikisha kwamba mataifa yaliutii.
Ni vigumu kujua kama mataifa yanaunda silaha za kibiolojia, kwani mbinu na ujuzi ambao hutumiwa kuunda bidhaa nyingine zenye manufaa zinaweza kutumiwa pia kutengeneza silaha. ‘Utumizi huo wenye pande mbili’ hufanya iwe rahisi kuficha uundaji wa silaha katika viwanda vya kuchachusha na kwenye maabara ambazo huonekana zikiendelea na shughuli za kawaida.
Ili kutatua tatizo hilo, wajumbe wa nchi kadhaa walianza kujadili mkataba mwingine katika mwaka wa 1995. Zaidi ya miaka sita ilipita wakijadiliana kuhusu hatua maalumu ambazo zingechukuliwa ili kuhakikisha kwamba mataifa yalifuata kanuni za mkataba wa BTWC. Mnamo Desemba 7, 2001, mkutano wa majuma matatu uliohudhuriwa na mataifa 144 kati ya yale yaliyotia sahihi mkataba wa 1972 ulimalizika kwa vurugu. Tatizo lililetwa na Marekani wakati ilipopinga mapendekezo makuu ya mkutano huo kuhusu jinsi ya kujua kama mataifa yalifuata kanuni za BTWC. Marekani iliona kuwa kuruhusu watu wengine wachunguze vituo vyake vya kijeshi na viwanda kungekuwa ujasusi.
Matazamio ya Wakati Ujao
Ufundi wa kibiolojia unaruhusu watu wafanye mambo mema na mabaya pia. Ufundi wa aina nyingine—kama ufundi wa vyuma, vilipukaji, injini, ufundi wa ndege, elektroni—umetumiwa kwa njia yenye manufaa na katika vita pia. Je, ni hali moja na ufundi wa kibiolojia? Watu wengi wanaamini kuwa jibu la swali hilo ni ndiyo.
Ripoti iliyoandikwa na Tume ya Usalama wa Kitaifa ya Marekani mnamo mwaka wa 1999 ilisema: “Watu mmoja-mmoja na vikundi . . . vitakuwa na mamlaka na ushawishi mwingi zaidi, na watu wengi watakuwa na mbinu zenye kuogofya za kusababisha maafa. . . . Magenge na watu wengi zaidi, walio na bidii ya kidini, wafuasi sugu wa madhehebu, au wenye chuki nyingi kupita kiasi, watafanya kazi hiyo kihususa. Magaidi sasa wanaweza kushambulia vituo muhimu vya kijamii wakitumia tekinolojia ambazo wakati mmoja zilitumiwa na mataifa makubwa pekee.”
Ingawa hatujui mambo yatakayotukia karibuni, tuna uhakika juu ya yale ambayo Mungu amewakusudia wanadamu. Biblia huahidi wakati ambapo watu duniani “watakaa salama salimini, wala hapana mtu atakayewatia hofu.” (Ezekieli 34:28) Ili ufahamu zaidi kuhusu ahadi hiyo yenye kufariji, wasiliana na Mashahidi wa Yehova wa kwenu au utuandikie barua ukitumia anwani ifaayo iliyoonyeshwa katika ukurasa wa 5 wa gazeti hili.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Watafiti wanabuni njia za kukabiliana na ugonjwa wa kimeta
[Hisani]
Photo courtesy Sandia National Laboratories
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mkutano kuhusu Silaha za Kibiolojia, Novemba 19, 2001, Uswisi
[Hisani]
AP Photo/Donald Stampfli
[Picha katika ukurasa wa 11]
Biblia inaahidi wakati ambapo watu wote “watakaa salama salimini”
-