Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Samoa
    2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • WAMISHONARI WARUHUSIWA KUINGIA SAMOA

      Kabla ya mwaka 1974, haikuwa rahisi kuhubiri nchini Samoa kwa kuwa serikali iliweka vizuizi vingi vilivyowazuia wamishonari kuingia nchini humo. Mwaka huo, akina ndugu wenyeji wenye kuongoza walimwendea waziri mkuu kuzungumzia jambo hilo. Mmoja wa ndugu hao, Mufaulu Galuvao, anaandika: “Wakati wa mazungumzo hayo tuligundua kwamba ofisa mmoja wa serikali alikuwa ameunda tume isiyo halali ya kukagua maombi yote ya wamishonari. Tume hiyo ya watu wa dini wasiopenda kazi yetu, ilikataa kuidhinisha maombi ya akina ndugu ya kuomba vibali vya kukaa nchini bila hata kumwarifu waziri mkuu.

      “Waziri mkuu hakuwa na habari yoyote kuhusu hila hiyo; hivyo, akaamuru mara moja ofisa mkuu wa uhamiaji amletee faili la Mashahidi wa Yehova. Papo hapo mbele yetu akavunjilia mbali tume hiyo bandia, na kuwapa Paul na Frances Evans, vibali vya kukaa nchini kwa miaka mitatu wakiwa wamishonari, na muda huo ungeweza kuongezwa ukimalizika.” Habari zenye kusisimua kama nini! Baada ya kusubiri kwa miaka 19, hatimaye waliingia rasmi Samoa wakiwa wamishonari!

      Mwanzoni, Paul na Frances waliishi pamoja na familia ya Mufaulu Galuvao, lakini John na Helen Rhodes walipofika mwaka wa 1977, walihamia makao mapya ya wamishonari yaliyokuwa yamekodiwa huko Vaiala, Apia. Wamishonari wengine ni Robert na Betty Boies waliokuja mwaka wa 1978, David na Susan Yoshikawa waliokuja mwaka wa 1979, na Russell na Leilani Earnshaw waliokuja mwaka wa 1980.

      KUZOEA MAISHA YA KISIWANI

      Kwa miaka mingi, Mashahidi wa nchi nyingine waliohamia Samoa walitambua kwamba hata kisiwa hicho maridadi kina matatizo yake. Mojawapo ya matatizo hayo ni usafiri. John Rhodes anasema: “Miaka miwili ya kwanza tuliyokaa Apia, mara nyingi tulitembea kwa muda mrefu ili kuhudhuria mikutano na kwenda kuhubiri. Nyakati nyingine tulisafiri kwa mabasi ya umma yenye madoido.”

      Kwa kawaida mabasi huwa na kichwa cha lori na bodi za mbao. Abiria hujazana ndani pamoja na mizigo yao, nao hubeba kila kitu, iwe ni majembe, au vyakula. Muziki unaofunguliwa kwa sauti ya juu na nyimbo zinazoimbwa kwa sauti ni mambo ya kawaida wakati wa safari. Vituo vya mabasi, ratiba, na barabara ambazo mabasi hayo hupitia hubadilika-badilika sana. “Basi la kwenda Vava‘u,” asema kiongozi mmoja wa safari, “halichelewi kamwe, saa zake za kufika ni wakati wowote ambapo litafika.”

      “Tulipotaka kununua kitu njiani,” asema John, “tulimwambia dereva asimamishe basi. Kisha baada ya kununua tulichotaka, tulipanda basi tena na kuendelea na safari yetu. Ajabu ni kwamba hakuna yeyote aliyejali.”

      Basi lilipojaa, abiria waliokuwa wameketi waliwapakata abiria wapya. Hivyo, akina ndugu wamishonari wakajifunza kuwapakata wake zao. Safari ilipofika mwisho, abiria wote, watoto kwa wakubwa walibandua sarafu ndogo iliyokuwa sikioni na kulipa nauli yao—pochi ya ajabu!

      Wamishonari walisafiri toka kisiwa kimoja hadi kingine kwa ndege na mashua ndogo. Safari zilikuwa zenye kuchosha; na mara nyingi walichelewa kufika. “Tulilazimika kujifunza kuwa wenye subira na kuwa wacheshi,” asema Elizabeth Illingworth, ambaye kwa miaka mingi aliandamana na mume wake, Peter, katika kazi ya kuzungukia makutaniko kotekote katika Pasifiki ya Kusini.

      Haikuwa rahisi kusafiri kwa barabara wakati wa mvua—hasa msimu wa tufani. Alipokuwa akijaribu kuvuka kijito kilichofurika akielekea kuhudhuria Funzo la Kitabu la Kutaniko, mmishonari Geoffrey Jackson aliteleza na kutumbukia katika kijito hicho. Aliibuka akiwa amelowa maji na matope, akaendelea na safari yake. Alipofika, wenye nyumba inayotumiwa kwa mkutano huo walimpangusa na kumvisha lavalava ndefu nyeusi (kikoi cha Kipolinesia ambacho wanaume hasa hujifunga kiunoni). Wenzake walishindwa kujizuia kucheka wakati ambapo mtu mmoja anayependezwa alimwona na kudhani kwamba ni padri wa Katoliki! Ndugu Jackson sasa ni mshiriki wa Baraza Linaloongoza.

      Hali nyingine ngumu ambazo wageni kutoka nchi nyingine walikumbana nazo zinatia ndani kujifunza lugha mpya, kuzoea joto jingi, magonjwa mapya, ukosefu wa vifaa vingi vya kisasa, na wadudu wengi ambao huuma. “Wamishonari kwa kweli walijitoa kwa ajili yetu,” asema Mufaulu Galuvao, “na hivyo, wazazi wengi waliothamini jitihada zao waliwapa watoto wao majina ya ndugu hao wapendwa, waliokuwa wametusaidia kwa upendo.”

  • Samoa
    2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Miaka sita baadaye, dada wawili wamishonari—Tia Aluni, Msamoa wa kwanza kuhudhuria Shule ya Gileadi, na mwenzake Ivy Kawhe—waliombwa wahame kutoka Samoa ya Marekani na kwenda Savaii. Walipofika mwaka wa 1961, dada hao waliishi na mume na mke waliokuwa wazee kwa umri huko Fogapoa, kijiji kilicho upande wa mashariki wa kisiwa hicho. Baadaye, dada mwingine painia wa pekee, ambaye wakati mmoja alikuwa akiishi Savaii, akajiunga nao kwa muda. Ili kukitia moyo na kukitegemeza kikundi hicho kipya cha watu sita hadi nane hivi, akina ndugu kutoka Apia walizuru mara moja kwa mwezi na kutoa hotuba ya watu wote. Mikutano hiyo ilifanyiwa katika nyumba ndogo huko Fogapoa.

      Tia na Ivy waliendelea kukaa Savaii hadi 1964, walipopewa mgawo wa kuhamia kisiwa kingine.

  • Samoa
    2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • Kuanzia 1979, wamishonari zaidi walipewa mgawo wa kwenda Savaii kuwaunga mkono wahubiri wenyeji. Walitia ndani Robert na Betty Boies, John na Helen Rhodes, Leva na Tenisia Faai‘u, Fred na Tami Holmes, Brian na Sue Mulcahy, Matthew na Debbie Kurtz, na Jack na Mary Jane Weiser. Wamishonari hao walitoa mwongozo unaohitajika nayo kazi kisiwani Savaii ilisonga mbele.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki