Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Samoa
    2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • MAENDELEO MJINI APIA

      Richard Jenkins, Mwaustralia mwenye umri wa miaka 23 aliyekuwa ametoka tu kubatizwa, alifika Apia Mei 1954. Anasimulia: “Kabla ya kuondoka Australia, nilishauriwa nisichangamane na ndugu wenyeji hadi nipate kazi ya kudumu. Hata hivyo, baada ya miezi kadhaa, nikaanza kuhisi upweke na kujiona dhaifu kiroho. Basi nikaamua kuwasiliana kwa busara na Pele Fuaiupolu.” Wawili hao walikutana usiku mmoja.

      “Pele aliniambia hatatumia jina langu halisi, ili wenye mamlaka wasianze kushuku kwamba nashirikiana na kutaniko na kunitimua nchini humo,” akumbuka Richard. “Kwa hiyo akanibandika jina la mwana wake aliyezaliwa karibuni, Uitinese, yaani, ‘witness’ (shahidi) katika matamshi ya Kisamoa. Hadi leo hii, ndugu na dada wa Samoa huniita hivyo.”

      Akitumia jina lake jipya, Richard aliendelea kuwasiliana na akina ndugu kwa busara. Pia, alihubiri kwa njia isiyo rasmi na kuanzisha mafunzo kadhaa ya Biblia. Mwanafunzi wake mmoja wa Biblia, Mufaulu Galuvao, kijana aliyekuwa mkaguzi wa afya, baadaye alikuja kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Samoa. Mwanafunzi mwingine pia, Falema‘a Tuipoloa, akawa Shahidi, pamoja na watu wengine kadhaa wa familia yake.

      Mwanafunzi mmoja, aliyekuwa akijifunza Biblia na Richard, kijana Siemu Taase, alikuwa kiongozi wa genge la wezi waliokuwa wakiiba bidhaa za wizara ya ujenzi. Hata hivyo, kabla hajafanya maendeleo ya kiroho, alinaswa na mkono mrefu wa serikali na kutupwa gerezani. Richard hakuchoka. Alimwomba msimamizi wa gereza aendelee kujifunza na Siemu chini ya mwembe uliokuwa mita 100 hivi nje ya jela. Baada ya muda, wafungwa wengine kadhaa wakaanza kushiriki funzo hilo.

      “Ijapokuwa hatukuwa tukilindwa,” akumbuka Richard, “hakuna mfungwa yeyote aliyejaribu kutoroka, na baadhi yao waliikubali kweli.” Alipofunguliwa, hatimaye Siemu alitumikia akiwa mzee wa kutaniko.

      Mwaka wa 1955, Richard alimwoa painia Mwaustralia, Gloria Green. Walikaa miaka 15 nchini Samoa na kuwasaidia watu 35 kujifunza kweli kabla ya kurudi Australia. Sasa wanaishi Brisbane, Australia, ambako Richard anatumikia akiwa mzee katika kutaniko la Kisamoa.

  • Samoa
    2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • [Picha katika ukurasa wa 84]

      Richard na Gloria Jenkins, siku ya harusi yao, Januari 1955

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki