-
Kujiua—Pigo la VijanaAmkeni!—1998 | Septemba 8
-
-
Kujiua—Pigo la Vijana
KANA kwamba vita, mauaji, na maovu mengine hayatoshi kuangamiza vijana wetu, kuna kujiua kwa vijana duniani kote. Kutumia vibaya kileo na dawa za kulevya kunaharibu akili na miili ya vijana, kukisababisha vifo vingi miongoni mwa vijana. Kumbukumbu zinazidi kuonyesha kwamba mtu alikufa kwa kutumia dawa za kulevya kupita kiasi, ama kimakusudi ama kiaksidenti.
Ripoti ya Morbidity and Mortality Weekly Report ya Aprili 28, 1995, ilisema kwamba “nchini Marekani kujiua ni kisababishi nambari tatu cha vifo miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15-19.” Dakt. J. J. Mann aandika hivi katika The Decade of the Brain: “Zaidi ya Wamarekani 30,000 [mwaka wa 1995 walikuwa 31,284] hujiua kila mwaka. Kwa kuhuzunisha, kwa kawaida ni vijana ambao hujiua . . . Watu wazidio 30,000 kwa mara kumi hujaribu kujiua, lakini huokoka. . . . Kuwatambulisha wagonjwa ambao wamo hatarini mwa kujiua ni tatizo kubwa sana kwa sababu matabibu hawawezi kugundua kwa urahisi kati ya wagonjwa wenye mshuko mkubwa wa moyo ambao watajaribu kujiua na wale ambao hawatajaribu.”
Simon Sobo, mkuu wa utibabu wa akili kwenye Hospitali ya New Milford, Connecticut, Marekani, alisema: “Kumekuwa na majaribio mengi zaidi ya kujiua katika masika haya [1995] kuliko niliyoona katika miaka 13 ambayo nimekuwa hapa.” Nchini Marekani, maelfu ya vijana hujaribu kujiua kila mwaka. Kila jaribio la kujiua ni mwito wa kutaka msaada na uangalifu. Ni nani atakayewasaidia kabla haijawa kuchelewa mno?
Tatizo la Ulimwenguni Pote
Hali si tofauti sana katika nchi nyingine za ulimwengu. Kulingana na India Today, vijana wapatao 30,000 walijiua katika mwaka wa 1990 nchini India. Katika nchi za Finland, Hispania, Israeli, Kanada, New Zealand, Thailand, Ufaransa, Uholanzi, na Uswisi, kujiua kumeongezeka miongoni mwa vijana. Ripoti moja ya 1996 ya Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) inasema kwamba vijana wanajiua zaidi katika Finland, Latvia, Lithuania, New Zealand, Slovenia na Urusi.
Australia pia ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya vijana kujiua. Katika nchi hiyo mwaka wa 1995, asilimia 25 ya vifo vyote miongoni mwa vijana wanaume na asilimia 17 miongoni mwa vijana wasichana vilikuwa kujiua, kulingana na ripoti moja katika gazeti la habari la The Canberra Times. Kiwango cha kujiua ambako “kulifaulu” miongoni mwa wavulana wa Australia kinashinda kiwango cha wasichana kwa mara tano. Na ndivyo ilivyo katika nchi nyingi.
Je, hili lamaanisha kwamba wavulana wanaelekea kujiua kuliko wasichana? La. Habari zinazopatikana zaonyesha kwamba hakuna tofauti kubwa kati ya jinsia hizo mbili katika kujaribu kujiua. Lakini, “vijana wanaume hujiua kwa kiwango kinachozidi kiwango cha wasichana kwa mara nne katika nchi zilizoendelea kiviwanda kulingana na tarakimu za karibuni zaidi kutoka kwa Shirika la Afya Ulimwenguni.”—The Progress of Nations, kilichochapishwa na UNICEF.
Lakini hata tarakimu hizo zenye kuogofya huenda zisionyeshe ukubwa wa tatizo hilo. Tarakimu za vijana kujiua, zikifafanuliwa kwa njia ya kitiba na ya uchanganuzi, zaeleweka kwa urahisi sana. Lakini, kile ambacho mara nyingi hakijulikani wala kuonekana katika tarakimu hizo ni zile familia zilizopatwa na pigo na huzuni, uchungu na kukata tamaa kwa wale waliobaki wanapotafuta sababu.
Basi, je, misiba kama vile kujiua kwa vijana yaweza kuzuiwa? Mambo fulani makuu yametambuliwa nayo yaweza kuwa yenye msaada katika kuepuka hali hii yenye kuhuzunisha.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Vichocheo vya Kujiua
Kuna nadharia nyingi sana kuhusu vichocheo vya kujiua. “Kujiua hutokana na jinsi mtu anavyotenda anapokabili jambo analoona kuwa tatizo kubwa ambalo linamshinda, kama vile kujihisi mpweke, kifo cha mpendwa wake (hasa mwenzi wa ndoa), familia iliyovunjika wakati wa utotoni, ugonjwa mbaya, kuzeeka, ukosefu wa kazi, matatizo ya kifedha, na kutumia dawa za kulevya.”—The American Medical Association Encyclopedia of Medicine.
Kulingana na mtaalamu wa mahusiano ya watu Emile Durkheim, kuna aina nne za msingi za kujiua:
1. Kujiua kwa sababu ya upweke—Hali hii ya kujiua “hudhaniwa kuwa inasababishwa na mtu kushindwa kuchangamana na jamii. Wakiwa wapweke, watu wa hali hii hawajihusishi na jumuiya yao, wala hawaitegemei.” Wao huelekea kuwa wapweke.
2. Kujiua kwa ajili ya wengine—“Mtu huwa amejihusisha sana na kikundi fulani hivi kwamba anahisi anaweza kudhabihu chochote.” Mifano inayotolewa ni wale marubani wa Japani wenye kujilipua palipo adui katika Vita ya Ulimwengu ya Pili na washupavu wa kidini ambao hujilipua wanapoua wale wanaowadhania kuwa maadui wao. Mifano mingine inaweza kuwa wale ambao wamejitoa wafe ili kuvuta uangalifu kwenye hali fulani.
3. Kujiua kwa sababu ya matatizo ya kijamii—“Mtu kama huyo hawezi kushughulikia shida kwa njia nzuri naye achagua kujiua kuwa ndilo suluhisho la matatizo. [Hilo] hutukia wakati uhusiano ambao mtu huyo amezoea pamoja na jamii unapobadilishwa kwa ghafula na kwa njia yenye kushtua.”
4. Kujiua kwa kukosa tumaini—Hali hii ya kujiua inadhaniwa “kuwa husababishwa na udhibiti mwingi wa jamii ambao huzuia uhuru wa mtu.” Watu kama hao “huhisi kwamba hawana wakati ujao bora.”—Adolescent Suicide: Assessment and Intervention, cha Alan L. Berman na David A. Jobes.
-
-
Tumaini na Upendo ZitowekapoAmkeni!—1998 | Septemba 8
-
-
Tumaini na Upendo Zitowekapo
MSICHANA mmoja wa Kanada mwenye umri wa miaka 17 aliandika sababu zake za kutaka kufa. Miongoni mwa sababu hizo, yeye aliorodhesha mambo yafuatayo: ‘Nahisi upweke na naogopa wakati ujao; nahisi nikiwa wa hali ya chini mbele ya wafanyakazi wenzangu; vita ya nyuklia; kuharibiwa kwa tabaka ya ozoni; nina sura ya kutisha, kwa hiyo sitapata mume kamwe na nitaishia kuwa peke yangu; sidhani kama kuna mambo mengi ya kufanya nistahili kuishi, basi kwa nini ningoje ili niyagundue; kifo changu kitaondolea kila mtu mzigo; sitaumizwa tena na mtu yeyote kamwe.’
Je, hizo zaweza kuwa baadhi ya sababu zinazofanya vijana wajiue? Nchini Kanada, “bila kuhesabu aksidenti za magari, kujiua ndicho kisababishi kikuu cha vifo miongoni mwao.”—The Globe and Mail.
Profesa Riaz Hassan, wa Chuo Kikuu cha Flinders cha South Australia, asema katika insha yake inayoitwa “Maisha Zilizokatizwa: Mielekeo Katika Kujiua kwa Vijana”: “Kuna sababu kadhaa za kijamii zinazohusu swali hilo na kuonekana kuwa zimechangia sana kujiua kwa vijana. Sababu hizo ni kiwango cha juu cha vijana kukosa kazi; mabadiliko katika familia za Australia; ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya; ongezeko la ujeuri wa vijana; matatizo ya akili; na ongezeko la pengo kati ya ‘uhuru wa kusema tu’ na uhuru wa kujipatia.” Insha hiyo yaendelea kutaja kwamba matokeo ya uchunguzi kadhaa yameonyesha kwamba kuna hali ya kutotumaini wakati ujao na kudokeza kwamba “idadi kubwa ya vijana wana hofu na wasiwasi kuhusu wakati wao ujao na wa ulimwengu. Wao waona ulimwengu ulioharibiwa na vita ya nyuklia na kuharibiwa na uchafuzi na uharibifu wa mazingira, jamii iliyoharibiwa ambamo tekinolojia haiwezi kudhibitiwa na kujaa kwa ukosefu wa kazi.”
Kulingana na uchunguzi wa Gallup uliofanyiwa watu wenye umri wa kati ya miaka 16 na 24, visababishi vingine zaidi vya kujiua ni pengo linalozidi kuongezeka kati ya matajiri na maskini, ongezeko la familia zenye mzazi mmoja, ongezeko la matumizi ya bunduki, kutendwa vibaya kwa watoto, na “kukosa imani [kwa ujumla] juu ya wakati ujao.”
Gazeti Newsweek laripoti kwamba nchini Marekani, “kuwapo kwa bunduki huenda kukawa ndicho kisababishi kikuu cha [kujiua kwa vijana]. Uchunguzi mmoja uliolinganisha kujiua kwa vijana ambao hawakuonekana kuwa na matatizo ya akili na watoto ambao hawakujiua ulipata tofauti moja tu: bunduki yenye risasi nyumbani. Yapinga kabisa wazo la kwamba bunduki haziuwi watu.” Na mamilioni ya familia zina bunduki zenye risasi!
Hofu na jamii isiyojali zaweza kuwasukuma vijana haraka wafikie hatua ya kujiua. Ebu fikiria: Kiwango cha uhalifu wenye ujeuri uliofanyiwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 12-19 kinashinda kwa mara mbili uhalifu uliofanyiwa watu kwa ujumla. Uchunguzi uligundua kwamba “wasichana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24 huelekea zaidi kushambuliwa,” laripoti gazeti Maclean’s. “Wanawake hushambuliwa mara nyingi zaidi na kuuawa na watu wanaodai kuwa wanawapenda.” Matokeo ni nini? Hofu hizi na nyinginezo “hutowesha uhakika na usalama wa wasichana hao.” Katika uchunguzi mmoja, karibu thuluthi moja ya wale waliobakwa ambao walihojiwa walikuwa wamefikiria kujiua.
Ripoti moja ya New Zealand yataja jambo jingine kuhusu kujiua kwa vijana, ikisema: “Maadili ya kilimwengu yaliyoenea ya kufuatia vitu vya kimwili ambayo huona mafanikio ya mtu kuwa mali, sura nzuri, na uwezo huwafanya vijana wengi wahisi kuwa bure kabisa na kupuuzwa na jamii.” Kwa kuongezea, gazeti The Futurist lasema: “[Vijana] wana mwelekeo wenye nguvu wa kutaka kuridhika mara moja, wakitaka vyote na kuvitaka haraka iwezekanavyo. Programu za televisheni ambazo wanapenda zaidi ni vipindi vya mfululizo vyenye kuendelezwa. Wangependa ulimwengu wao ujae watu walewale wenye sura nzuri, wenye kuvalia mavazi ya kisasa zaidi, wenye pesa nyingi na umashuhuri, na wasiohitaji kufanya kazi kwa bidii.” Mambo hayo yote yasiyo halisi na matazamio ambayo hayafanikiwi huonekana kama huwafanya vijana wakate tumaini na kwaweza kufanya wajiue.
Je, Ni Sifa Yenye Kuokoa Uhai?
Shakespeare aliandika: “Upendo hufariji kama jua la baada ya mvua.” Biblia yasema: “Upendo haushindwi kamwe.” (1 Wakorintho 13:8) Katika sifa hiyo kuna suluhisho kwa tatizo la vijana wenye mwelekeo wa kujiua—kutamani kwao upendo na mawasiliano. Kitabu The American Medical Association Encyclopedia of Medicine chasema: “Watu wenye mwelekeo ya kujiua mara nyingi hujihisi wakiwa wapweke sana, na fursa ya kuzungumza na mtu mwenye kusikiliza na mwenye hisia-mwenzi nyakati nyingine hutosha kuzuia tendo hilo la kukata tumaini.”
Mara nyingi vijana huhitaji sana upendo na kujiona kuwa hawako peke yao. Kutimiza uhitaji huo huendelea kuwa kugumu kadiri siku zipitavyo katika ulimwengu huu usio na upendo na wenye uharibifu—ulimwengu ambamo hawana uwezo. Kukataliwa na wazazi kwa sababu ya kuvunjika kwa familia na talaka zaweza kuchangia vijana kujiua. Na kukataliwa huko kwaweza kudhihirika kwa njia nyingi.
Ebu fikiria kisa cha wazazi ambao ni nadra sana wawe pamoja na watoto wao nyumbani. Huenda Mama na Baba wakawa wanajishughulisha mno na kazi zao au wanafuatia sana vitumbuizo fulani ambavyo havihusishi watoto. Ujumbe usio wa moja kwa moja kwa watoto wao ni kukataliwa waziwazi. Mwandishi mashuhuri wa habari aliye pia mtafiti Hugh Mackay asema kwamba “wazazi wanazidi kujipenda. Wanajitanguliza ili waendeleze mitindo yao ya maisha. . . . Tukisema wazi, watoto hawapendwi tena. . . . Maisha ni magumu nayo huwafanya watu waelekee kufuata mambo yao wenyewe.”
Kisha, katika tamaduni fulani watu wenye kutaka waonekane kuwa wanaume hawataki kuonwa kuwa walezi. Mwandishi wa habari Kate Legge asema hivi: “Wanaume wenye mwelekeo wa kupenda kufanya utumishi wa umma kwa kawaida hupendelea kazi zenye kuokoa uhai au ya kuzima moto kuliko kazi za malezi . . . Wao hupendelea ile hali ya kishujaa ya kupambana na mambo ya nje kuliko kazi za malezi.” Na, bila shaka, mojawapo ya kazi za malezi zaidi leo ni kuwa mzazi. Kuwa mzazi mbaya ni kama kumkataa mtoto. Tokeo ni kwamba mwana wako au binti yako aweza kujiona vibaya na asiweze kukuza stadi za kuchangamana na jamii. Gazeti The Education Digest lasema: “Bila kujiona vizuri, watoto hawana msingi wa kufanya maamuzi ya mambo yawafaayo zaidi.”
Kukata Tumaini Kwaweza Kutokea
Watafiti wanaamini kwamba kukata tumaini ni sababu kubwa ya kujiua. Gail Mason, mwandishi juu ya kujiua kwa vijana katika Australia, alisema: “Kukata tumaini huonwa kuwa kunahusiana sana na mawazo ya kujiua kuliko mshuko wa moyo. Nyakati nyingine kukata tumaini husemwa kuwa dalili moja ya mshuko wa moyo. . . . Mara nyingi hiyo huwa kukata tumaini na kukosa tumaini juu ya wakati ujao wa vijana, na hasa kuhusu wakati wao ujao wa kiuchumi: na kwa kiwango kidogo kukata tumaini kuhusu hali ya duniani pote.”
Mifano mibaya inayowekwa na viongozi wa umma wasiofuatia haki haichochei vijana kuinua maadili yao wenyewe. Basi wanakuwa na mtazamo, “Kwa nini nisumbuke kuwa mwenye kufuatia haki?” Gazeti Harper’s Magazine lasema juu ya uwezo wa vijana wa kuona unafiki, likisema: “Vijana, wakijua sana kutambua unafiki, wanajua kusoma sana—lakini si kusoma vitabu. Lakini kile wanachosoma sana ni ishara za kijamii zinazotoka katika ulimwengu ambao wanalazimika kuishi.” Na ishara hizo zasemaje? Mwandishi wa vitabu Stephanie Dowrick asema: “Hatujapata kuwa na habari nyingi hivi juu ya jinsi tunavyopaswa kuishi. Hatujapata kuwa matajiri kiasi hiki na kuwa na elimu hivi, lakini watu wamekata tumaini kotekote.” Na kuna watu wachache sana wenye mifano ya kuigwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa na wa kidini. Dowrick auliza maswali machache yenye kutuhusu: “Tutapataje hekima, kujirekebisha na hata kupata umaana kutokana na kuteseka kusiko na maana? Tutasitawishaje upendo katika hali ya ubinafsi, chuki na pupa?”
Utapata majibu ya maswali haya katika makala yetu ifuatayo, na majibu hayo yaweza kukushangaza.
-
-
Tumaini na Upendo ZirudipoAmkeni!—1998 | Septemba 8
-
-
Tumaini na Upendo Zirudipo
WAZAZI, walimu, na wengine ambao hushughulika na vijana hutambua kwamba wao, vijana, au mtu yeyote yule hawezi kubadili ulimwengu. Kuna mavutano yafananayo na mawimbi ya bahari, ambayo hakuna mtu yeyote awezaye kuyazuia. Lakini, kuna mengi tunayoweza kufanya ili kusaidia vijana wawe wenye furaha zaidi, wenye afya zaidi, na wenye mahusiano mazuri na jamii.
Kwa kuwa kuzuia ni bora kuliko kuponya, wazazi wapaswa kufikiria kwa uangalifu jinsi mtindo wao wa maisha na mambo wanayotanguliza yawezavyo kuathiri mitazamo na tabia za watoto wao. Kuandaa mazingira yenye upendo na yenye kujali nyumbani hufanyiza usalama ambao unaweza kuzuia kwa njia bora zaidi tabia ya kujiharibu. Mojawapo ya mahitaji makubwa zaidi ya vijana ni kuwa na mtu wa kuwasikiliza. Wazazi wasipowasikiliza, labda watu wasiofaa watawasikiliza.
Jambo hilo lamaanisha nini kwa wazazi leo? Weka wakati wa kuwa na watoto wanapouhitaji—wakiwa wachanga. Hilo si rahisi kwa familia nyingi. Familia hujitahidi kupata riziki, wazazi wote wawili wakikosa namna ila tu kufanya kazi. Wale ambao wamekuwa tayari kufanya dhabihu hiyo, na wameweza kufanya hivyo, ili wapate wakati wa kuwa pamoja na watoto wao mara nyingi wamevuna thawabu ya kuona wana wao na binti zao wakifanikiwa maishani. Lakini, kama ilivyotajwa mapema, nyakati nyingine japo jitihada bora zaidi za wazazi, matatizo mazito yaweza kuwapata watoto wao.
Marafiki na Watu Wengine Wazima Waweza Kusaidia
Vita, ubakaji, na kutendwa vibaya kwa vijana huhitaji watu wazima wenye kuwajali vijana watie jitihada nyingi sana ili kushughulikia madhara ya vijana. Huenda hata jitihada za kuwasaidia vijana wenye kusumbuliwa na mambo mabaya kama hayo ziambulie patupu. Huenda hilo likamaanisha kutumia wakati mwingi sana na kujikakamua kwelikweli. Kwa hakika, si jambo la hekima wala lenye upendo kuwashushia hadhi wala kuwakana. Je, twaweza kukuza hisia zaidi ili tuonyeshe fadhili na upendo ili tuwasaidie wale walio hatarini?
Si wazazi tu bali pia marafiki na hata ndugu na dada zao wanahitaji hasa kuwa wenye tahadhari kuona mielekeo katika wachanga hao ambayo yaweza kuashiria hali dhaifu ya kihisia-moyo au isiyo na usawaziko. (Ona sanduku “Msaada wa Wataalamu Wahitajika,” ukurasa wa 8.) Ikiwa kuna dalili hizo, uwe mwepesi kusikiliza. Ikiwezekana, jaribu kuuliza vijana wenye matatizo maswali yenye fadhili na kuwahakikishia kwamba wewe ni rafiki wa kweli. Marafiki na watu wa ukoo wenye kutumainiwa wanaweza kuwategemeza wazazi katika kushughulikia hali ngumu; lakini, bila shaka, wawe waangalifu wasichukue daraka la wazazi. Mara nyingi mielekeo ya vijana kujiua ni ombi la dharura la kutaka uangalifu—uangalifu wa wazazi.
Mojawapo ya zawadi bora zaidi mtu yeyote aweza kuwapa vijana ni tumaini thabiti la wakati ujao wenye furaha, kichocheo cha kuishi. Vijana wengi wametambua ukweli wa ahadi za Biblia za ulimwengu bora ambao utakuja karibuni.
Waokolewa Wakifikiria Kujiua
Kutoka Japani, mwanamke mmoja mchanga ambaye mara nyingi alifikiria kujiua asema: “Ni mara nyingi kadiri gani nilitamani kujiua. Nilipokuwa mtoto mchanga, nilitendwa vibaya kingono na mtu niliyemtumaini. . . . Wakati uliopita, nilikuwa nimeandika habari nyingi sana zilizosema ‘Nataka kufa.’ Sasa nimekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, na sasa natumikia nikiwa mweneza-evanjeli wa wakati wote, lakini hali hiyo bado hunishika mara kwa mara. . . . Lakini Yehova ameniruhusu niendelee kuishi, naye anaonekana kana kwamba ananiambia kwa upole, ‘Endelea kuishi.’”
Msichana mmoja kutoka Urusi mwenye umri wa miaka 15 alieleza hivi: “Nilipokuwa na umri wa miaka minane, nilianza kuhisi kwamba hakuna mtu aliyenihitaji. Wazazi wangu hawakuwa na wakati wa kuzungumza nami, na nilijaribu kujisuluhishia matatizo yangu. Nikawa mnyamavu. Nikawa nagombana daima na watu wa ukoo. Kisha nikafikiria kujiua. Nilifurahi kama nini kukutana na Mashahidi wa Yehova!”
Na kutoka Australia kuna maelezo haya yenye kutia moyo ya Cathy, ambaye sasa yuko katika miaka ya 30, yanayoonyesha kwamba kukata tumaini kwaweza kugeuka kuwa tumaini: “Niliwaza na kuwazua jinsi ya kumaliza uhai wangu na hatimaye nikajaribu. Nilitaka niondoke ulimwengu huu, uliojaa uchungu, hasira, na ubatili. Kushuka moyo kukafanya iwe vigumu sana kuondokea hali hiyo niliyoona imeninasa kama ‘utando wa buibui.’ Basi, ikaonekana kama suluhisho ni kujiua.
“Niliposikia kwa mara ya kwanza uwezekano wa dunia kuwa paradiso, yenye maisha ya amani kwa wote, nikaitamani sana. Lakini ilionekana kama ndoto tu isiyoweza kutimia. Hata hivyo, polepole nilianza kuelewa maoni ya Yehova juu ya uhai na jinsi kila mmoja wetu alivyo na thamani machoni pake. Nikaanza kuwa na uhakika kwamba kuna tumaini kwa wakati ujao. Hatimaye, nilipata njia ya kutoka kwenye hali iliyokuwa imeninasa. Lakini ikawa vigumu sana kutoka. Nyakati nyingine kushuka moyo kungenishinda, nami ningehisi nimevurugika kwelikweli. Lakini, kwa kukaza fikira zangu kwa Yehova Mungu niliweza kumkaribia sana na kuhisi usalama. Namshukuru Yehova kwa yote ambayo amenifanyia.”
Hakuna Vifo vya Vijana Tena
Kwa kujifunza Biblia, kijana aweza kutambua kwamba kuna kitu bora cha kutazamia—kitu ambacho mtume Mkristo Paulo akiita “uhai ulio halisi.” Alimshauri kijana Timotheo: “Uwape maagizo wale walio matajiri . . . waweke tumaini lao, si juu ya mali zisizo hakika, bali juu ya Mungu, ambaye hututolea sisi vitu vyote kwa utajiri kwa ajili ya ufurahio wetu; kufanya mema, kuwa matajiri katika kazi zilizo bora, . . . wakijiwekea wenyewe kuwa hazina salama msingi bora kwa ajili ya wakati ujao, ili wao wapate kuwa na mshiko imara juu ya uhai ulio halisi.”—1 Timotheo 6:17-19.
Basi ni kama shauri la Paulo lamaanisha kwamba twapaswa kujihusisha na watu wengine, tukiwasaidia kuwa na tumaini thabiti la wakati ujao. “Uhai ulio halisi” ndio ambao Yehova ameahidi katika ulimwengu wake mpya wa “mbingu mpya na dunia mpya.”—2 Petro 3:13.
Vijana wengi ambao pindi moja walikuwa hatarini wamepata kuelewa kwamba kutumia dawa za kulevya na mitindo ya maisha yenye kukosa adili ni njia tu zenye kuongoza kwenye kifo, na kujiua kunakuwa njia tu ya mkato. Wametambua kwamba ulimwengu huu, ukiwa na vita vyake, chuki, mwenendo mbaya, na njia zake zisizo za upendo, karibuni utapotelea mbali. Wamejifunza kwamba ulimwengu huu hauwezi kuokolewa. Wameamini kwa dhati kwamba Ufalme wa Mungu ndio tumaini la pekee, kwa kuwa utaleta ulimwengu mpya ambamo vijana na vilevile wanadamu watiifu hawatalazimika kufa kamwe—wala hata hawatataka kufa tena.—Ufunuo 21:1-4.
-