-
Zambia2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Kutounga Mkono Mambo ya Ulimwengu
Mtume Paulo aliandika hivi: “Mtu anayetumika akiwa askari-jeshi huepuka kujihusisha katika shughuli za ulimwengu, ili ampendeze ofisa aliyemwandika.” (2 Tim. 2:4, Weymouth) Ili Wakristo wawe tayari kabisa kutumiwa na Kiongozi wao, Yesu Kristo, ni lazima waepuke kujihusisha katika shughuli za kisiasa na za kidini za ulimwengu. Kwa sababu ya msimamo huo, Wakristo wa kweli wanaokataa kuunga mkono ulimwengu wamepata matatizo na “dhiki.”—Yoh. 15:19.
Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, wengi walitendwa kinyama kwa sababu hawakuwa “wazalendo.” Benson Judge, ambaye baadaye alikuwa mwangalizi anayesafiri mwenye bidii, anasema: “Tuliwaona wazee wakirushwa garini kama magunia ya mahindi kwa kuwa walikataa kujiunga na jeshi. Tuliwasikia wakisema, ‘Tidzafera za Mulungu’ (Tutakufa kwa ajili ya Mungu).”
Ingawa Mukosiku Sinaali hakuwa amebatizwa, anakumbuka kwamba wakati huo wa vita, suala la kutounga mkono vita lilizuka mara nyingi. “Kila mtu alipaswa kuchimbua na kukusanya mizizi ya mmea wa mambongo, ambayo hutoa utomvu wenye thamani. Mizizi hiyo ilitolewa maganda kisha ikapondwapondwa na kutumiwa badala ya mpira kutengeneza viatu vya wanajeshi. Mashahidi walikataa kuchimbua mizizi hiyo kwa kuwa kazi hiyo ilihusiana na vita. Ndugu waliadhibiwa kwa kukataa kufanya kazi hiyo. Walionwa kuwa ‘wenye kuchukiza.’”
Joseph Mulemwa alikuwa mmoja wa watu hao “wenye kuchukiza.” Yeye ni mwenyeji wa Rodeshia Kusini aliyehamia Mkoa wa Magharibi wa Rodeshia Kaskazini katika 1932. Watu fulani walidai kwamba aliwahimiza watu waache kulima mashamba yao kwa kuwa ‘Ufalme umekaribia.’ Kasisi wa misheni ya Mavumbo aliyemdharau Joseph alieneza dai hilo la uwongo. Joseph alikamatwa na kufungwa pingu pamoja na mwenda-wazimu fulani. Watu fulani walitarajia kwamba mwenda-wazimu huyo atampiga Joseph. Hata hivyo, Joseph alimtuliza. Alipofunguliwa, Joseph aliendelea kuhubiri na kutembelea makutaniko. Alikufa akiwa mwaminifu katikati ya miaka ya 1980.
Kuimarishwa ili Kukabili Majaribu
Kwa sababu ya uzalendo na uhasama kati ya jamii mbalimbali, watu waliofuata dhamiri zao na kukataa kuunga mkono siasa walinyanyaswa. Ijapokuwa hali nchini Zambia ilikuwa mbaya, Kusanyiko la Kitaifa la “Wahudumu Wajasiri” la 1963, lililofanywa huko Kitwe, lilionyesha kwamba kuna amani na umoja miongoni mwa Mashahidi wa Yehova. Baadhi ya wahudhuriaji 25,000 hivi walikuja na mahema nao walisafiri katika misafara ya magari. Wote walisikiliza programu hiyo ya siku tano katika lugha waliyoipenda kati ya lugha nne zilizotumiwa. Milton Henschel, alitoa hotuba muhimu iliyohusu uhusiano wa Mkristo na Serikali. Frank Lewis anasema: “Twakumbuka kwamba alituambia tuwasaidie ndugu zetu wafahamu msimamo wa Wakristo wa kutounga mkono ulimwengu. Tulifurahi sana kupata mashauri hayo ya wakati unaofaa, kwa sababu ndugu wengi nchini Zambia walikabili majaribu makali lakini wakadumisha uaminifu wao kwa Yehova!”
Katika miaka yote ya 1960, Mashahidi wa Yehova kotekote nchini Zambia walikabili mateso makali na mali zao zikaharibiwa. Nyumba za akina ndugu na Majumba ya Ufalme yaliteketezwa. Serikali ilifanya vema kuwafunga wengi kati ya wale waliowatesa Mashahidi. Rodeshia Kaskazini ilipopata uhuru na kuwa Jamhuri ya Zambia, Mashahidi wa Yehova walivutiwa hasa na sheria za haki za kibinadamu katika katiba mpya ya nchi hiyo. Lakini, roho ya uzalendo ingefanya watu fulani washambuliwe ghafula.
Nembo za Kitaifa
Katika enzi ya ukoloni, watoto wa Mashahidi wa Yehova waliadhibiwa walipokataa kusalimu bendera ya Uingereza kupatana na imani yao. Waliadhibiwa pia kwa kukataa kuimba wimbo wa taifa. Mashahidi walipowalalamikia wenye mamlaka, idara ya elimu ilibadili maoni yake na kuandika: “Maoni ya [kikundi chenu] kuhusu kusalimu bendera yanajulikana sana na kuheshimiwa, na mtoto yeyote asiadhibiwe kwa njia yoyote kwa kukataa kusalimu bendera.” Katiba mpya ya jamhuri iliwafanya watu watarajie kwamba haki za msingi, kutia ndani haki ya mtu ya kufuata dhamiri yake, maoni yake, na dini yake, zingeimarishwa. Lakini bendera mpya na wimbo mpya wa taifa ziliamsha hisia za uzalendo. Kusalimu bendera na kuimba wimbo wa taifa kulianzishwa tena na kukaziwa sana shuleni. Ingawa vijana fulani Mashahidi hawakuhusishwa, vijana wengi walipigwa na hata kufukuzwa shuleni.
Sheria mpya ya elimu iliyopitishwa katika 1966 iliwapa watu matumaini. Kifungu fulani cha sheria hiyo kiliruhusu mzazi au mlezi aombe mtoto asihusishwe katika shughuli au sherehe za kidini. Hivyo, watoto wengi waliokuwa wamefukuzwa shuleni wakarudishwa. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, vifungu fulani viliongezwa kwa siri katika sheria hiyo. Vifungu hivyo vilionyesha kwamba bendera na wimbo wa taifa ni nembo za serikali za kuwahamasisha watu. Licha ya akina ndugu kuzungumza na wakuu wa serikali, kufikia mwisho wa 1966, watoto zaidi ya 3,000 walikuwa wamefukuzwa kwa sababu ya msimamo wao.
Feliya Hakubaliwi Katika Shule Yoyote
Wakati wa kutatua tatizo hilo kisheria uliwadia. Kisa fulani kilichaguliwa. Feliya Kachasu alikuwa akisoma kwenye Shule ya Buyantanshi katika eneo la shaba. Alikuwa amefukuzwa shuleni licha ya kwamba alikuwa mwanafunzi mzuri. Frank Lewis anakumbuka jinsi kesi hiyo ilivyowasilishwa mahakamani: “Bw. Richmond Smith aliwasilisha kesi yetu, ambayo haikuwa rahisi kwani tulikuwa tukiishtaki serikali. Alimsikiliza Feliya akieleza kwa nini hakuisalimu bendera na hivyo akaamua kumtetea.”
Dailes Musonda, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi huko Lusaka, anasema: “Kesi ya Feliya ilipowasilishwa mahakamani, tulitarajia sana kupata ushindi. Ndugu kutoka Mufulira walikuja kusikiliza kesi hiyo. Mimi na dada yangu tulialikwa. Namkumbuka Feliya alipokuwa mahakamani akiwa amevalia kofia nyeupe na nguo yenye rangi iliyofifia. Kesi hiyo ilisikizwa kwa siku tatu. Bado wamishonari kadhaa walikuwamo nchini; Ndugu Phillips na Ndugu Fergusson walikuja kusikiliza kesi hiyo. Tulifikiri kuwapo kwao kungesaidia.”
Hakimu mkuu alikata kauli hii: “Hakuna jambo lolote linaloonyesha kwamba kwa matendo yao Mashahidi wa Yehova wanadharau wimbo wa taifa au bendera.” Hata hivyo, aliamua kuwa hizo ni taratibu za kitaifa na kwamba licha ya Feliya kushikilia imani yake kwa unyoofu, hawezi kutumia sheria za elimu kuomba asihusishwe katika taratibu hizo. Aliamini kwamba taratibu hizo zilihitajiwa ili kuwe na usalama nchini. Lakini hakuonyesha wazi jinsi kumlazimisha mtoto ndogo kufuata takwa hilo kunavyonufaisha watu. Feliya hangekubaliwa katika shule yoyote kwa muda wote ambao angeendelea kushikilia imani yake ya Kikristo!
Dailes anasema: “Tulivunjika moyo sana. Hata hivyo, tulimwachia Yehova mambo.” Matatizo yaliongezeka, na Dailes na dada yake wakaacha shule katika 1967. Kufikia mwisho wa 1968, karibu watoto 6,000 wa Mashahidi wa Yehova walikuwa wamefukuzwa shuleni.
Mikutano ya Umma Yapigwa Marufuku
Kulingana na Sheria ya Usalama wa Umma ya 1966, mikutano yote ya umma ilipaswa kufunguliwa na kufungwa kwa kuimba wimbo wa taifa. Hivyo ikawa vigumu kufanya makusanyiko ya watu wote. Akina ndugu walitii sheria hiyo kwa kufanya makusanyiko makubwa katika viwanja vyenye ua wa nyasi vya watu binafsi na pia vya Majumba ya Ufalme. Watu wengi sana waliopendezwa walivutiwa na wakaja kuchunguza yaliyokuwa yakiendelea. Kwa hiyo, idadi ya wahudhuriaji ilipanda haraka sana hivi kwamba katika 1967, watu 120,025 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo.
Lamp Chisenga anasema: “Katika kipindi hicho wapinzani wetu walitushambulia kijeuri. Katika eneo la Samfya, kikundi cha wafanya-ghasia kilimshambulia na kumuua Ndugu Mabo wa Kutaniko la Katansha. Nyakati nyingine akina ndugu walishambuliwa wakiwa mikutanoni na Majumba ya Ufalme mengi yakateketezwa. Hata hivyo, wakuu wa serikali waliendelea kuwaheshimu Mashahidi, na wapinzani kadhaa wakakamatwa na kuadhibiwa.”
Jeshi Lao Wenyewe la Angani!
Wapinzani waliendelea kusingizia kwamba Mashahidi wa Yehova ni matajiri kupita kiasi na wataunda serikali ambayo ingefuata. Siku moja, katibu wa chama kilichotawala alikuja bila kutarajiwa kwenye ofisi ya tawi ya Kitwe. Kabla hajawasili, polisi wengi walifika langoni, na hiyo ikawa ishara ya kwanza ya ziara yake. Katibu huyo alipokuwa kwenye mkutano pamoja na wawakilishi wa ofisi ya tawi alikasirika na kusema hivi kwa sauti: “Tuliwapa kibali mjenge majengo haya. Mnayatumia kwa kazi gani? Je, hizi ndizo ofisi za serikali yenu?”
Wakuu fulani waliendelea kuamini uvumi usio wa kweli. Katika Mkoa wa Kaskazini-Magharibi wa Zambia, polisi walijaribu kuvunja kusanyiko fulani kwa kurusha gesi ya machozi. Akina ndugu walifaulu kutuma ujumbe wa haraka kwenye ofisi ya tawi. Mkulima fulani asiye mwenyeji alitumia ndege yake ndogo kuwapeleka upesi wawakilishi wengine wa ofisi ya tawi huko Kabompo ili wasaidie kutuliza hali na kutatua tatizo hilo. Inasikitisha kwamba jitihada hizo hazikufua dafu badala yake watu fulani walianza kudai kwamba Mashahidi wana jeshi lao wenyewe la angani!
Ndugu walikusanya mikebe mitupu ya gesi ya machozi waliyokuwa wamerushiwa. Wakati wawakilishi wa ofisi ya tawi walipowaendea maofisa wa serikali waliwaonyesha mikebe hiyo ili kuthibitisha kwamba polisi walitumia nguvu isivyo lazima. Habari za tukio hilo zilienea sana na watu waliona jinsi Mashahidi walivyojiendesha kwa amani.
Kufafanua Msimamo Wetu
Jitihada ya kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova ilipamba moto. Ofisi ya tawi ilitaka kuifafanulia serikali msimamo wetu wa kutounga mkono mambo ya ulimwengu. Smart Phiri na Jonas Manjoni waliteuliwa ili waende kukutana na mawaziri wengi wa serikali. Walipokuwa wakizungumza nao, waziri mmoja aliwakashifu akina ndugu. Alisema: “Ningefurahia sana kuwatoa nje na kuwatandika! Je mnafahamu kile ambacho mmefanya? Mmechukua raia wetu bora, fahari yetu, na mmetuachia nini? Tazama, mmetuachia wauaji, wazinzi, na wezi!”
Ndugu hao wakajibu haraka: “Lakini hivyo ndivyo baadhi yao walivyokuwa! Walikuwa wezi, wazinzi, na wauaji, lakini kwa nguvu za Biblia watu hao wamefanya mabadiliko maishani mwao na kuwa raia bora wa Zambia. Hiyo ndiyo sababu inayotufanya tuwasihi mturuhusu kuhubiri kwa uhuru.”—1 Kor. 6:9-11.
-
-
Zambia2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 232, 233]
Ilinibidi Kukimbia ili Niokoe Uhai Wangu
Darlington Sefuka
Alizaliwa: 1945
Alibatizwa: 1963
Maelezo mafupi kumhusu: Alikuwa painia wa pekee, mwangalizi wa mzunguko, na pia alifanya kazi kwenye Betheli nchini Zambia.
Kulikuwa na msukosuko nchini Zambia katika mwaka wa 1963. Mara nyingi tulipohubiri, magenge ya vijana waliounga mkono harakati za kisiasa walitutangulia ili wawaonye watu wasitusikilize na kuwatisha kwamba milango na madirisha ya nyumba zao yangevunjwa kama wangetusikiliza.
Jioni moja, siku mbili tu baada ya kubatizwa, nilipigwa vibaya na genge la vijana 15. Nilitokwa na damu nyingi mdomoni na puani. Jioni nyingine mimi na ndugu mwingine tulishambuliwa na kikundi cha watu 40 hivi waliokuwa wametuandama hadi mahali tulipoishi. Kufikiria mfano wa Bwana Yesu kuliniimarisha. Hotuba iliyotolewa na John Jason wakati wa ubatizo wangu ilionyesha wazi kwamba kila Mkristo atapata matatizo maishani. Basi nilipopatwa na matatizo hayo, sikushtuka bali nilitiwa moyo.
Wakati huo, wanasiasa walitaka watu waunge mkono harakati zao za kupigania uhuru, na kwa sababu sisi hatukujiingiza katika siasa walidhani tunawaunga mkono Wazungu na Wamarekani. Viongozi wa dini waliounga mkono vyama vya kisiasa walieneza habari hizo za uwongo kutuhusu. Mambo yalikuwa magumu kabla na baada ya uhuru. Ndugu wengi walipoteza biashara zao kwa sababu hawakukubali kununua kadi ya chama. Baadhi yao walihama mijini na kurudi vijijini mwao ambako walifanya kazi zisizokuwa na mapato mazuri ili waepuke kuombwa pesa kwa ajili ya harakati za kisiasa.
Nilipokuwa kijana, nilikaa na binamu yangu ambaye hakuwa Shahidi. Familia yake ilitishwa kwa sababu sikuunga mkono siasa. Walikuwa na wasiwasi. Siku moja kabla ya kwenda kazini, binamu yangu aliniambia: “Nitakaporudi jioni, sitaki kukukuta hapa.” Kwanza nilifikiri alikuwa anacheza tu, kwa sababu sikuwa na mtu mwingine wa ukoo mjini humo wala sikuwa na mahali pa kwenda. Baadaye niligundua kwamba hakuwa akicheza. Aliporudi na kunipata nyumbani, alifoka kwa hasira. Aliokota mawe na kuanza kunikimbiza, akisema kwa sauti kubwa: “Nenda kwa mbwa wenzako!” Ilinibidi kukimbia ili niokoe uhai wangu.
Baba yangu alisikia habari hizo na akatuma ujumbe huu: “Ukiendelea kushikilia msimamo wako wa kutounga mkono siasa, usikanyage kwangu tena.” Nilikuwa taabani kwelikweli, kwani nilikuwa na umri wa miaka 18 tu. Ningeenda wapi? Ndugu kutanikoni walinikaribisha. Mara nyingi ninatafakari maneno haya ya Mfalme Daudi: “Hata ikiwa baba yangu na mama yangu wangeniacha, Yehova mwenyewe angenichukua.” (Zab. 27:10) Ninakuambia, Yehova hakosi kutimiza ahadi zake.
-
-
Zambia2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 236, 237]
Mwenendo Wangu Uliwavutia Walimu Wengi
Jackson Kapobe
Alizaliwa: 1957
Alibatizwa: 1971
Maelezo mafupi kumhusu: Yeye ni mzee wa kutaniko.
Watoto walifukuzwa shuleni kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1964. Ofisi ya tawi iliwasaidia wazazi kuelewa umuhimu wa kuwatayarisha watoto. Nakumbuka kwamba baada ya shule Baba alizungumzia andiko la Kutoka 20:4, 5 pamoja nami.
Tulipokusanyika ili kuimba wimbo wa taifa shuleni, nilisimama nyuma ya wanafunzi wengine ili nisionekane. Wale ambao hawakuimba wimbo wa taifa waliitwa mbele. Mwalimu mkuu aliponiuliza kwa nini sikuimba, nilimjibu kwa kutumia Biblia. Huyo mwalimu mkuu akasema kwa mshangao: “Unasoma, lakini unakataa kuimba!” Alimaanisha kwamba ninapaswa kuunga mkono serikali ambayo imeandaa shule inayonifundisha kusoma.
Hatimaye, mnamo Februari 1967, nilifukuzwa shuleni. Nilivunjika moyo kwa sababu nilipenda masomo na nilikuwa mwanafunzi mwenye bidii. Ijapokuwa baba yangu alishinikizwa na wafanyakazi wenzake na watu wa ukoo wasiokuwa Mashahidi, alinihakikishia kwamba uamuzi wangu ulikuwa mzuri. Mama yangu alishinikizwa pia. Nilipoandamana naye kufanya kazi shambani, wanawake wengine walitudhihaki kwa kuuliza: “Kwa nini mtoto huyu hajaenda shuleni?”
Lakini sikukosa elimu. Madarasa ya kusoma na kuandika yalizingatiwa zaidi kutanikoni kuanzia mwaka wa 1972. Hatimaye hali ilibadilika shuleni. Nyumba yetu ilikuwa karibu na shule. Mwalimu mkuu alikuja kwetu mara kwa mara kuomba maji ya kunywa au fagio za kufagia madarasa. Hata siku moja aliomba mkopo! Bila shaka matendo ya fadhili ya familia yetu yalimgusa moyo kwa sababu siku moja alimuuliza baba yangu: “Je, mwanao anataka kuendelea na masomo?” Baba alimkumbusha kwamba bado mimi ni Shahidi wa Yehova. Mwalimu huyo mkuu akasema: “Hakuna matata.” Kisha akaniuliza: “Unataka kuanza darasa gani?” Nilichagua darasa la sita, na nikarudi kwenye shule ileile, na mwalimu mkuu alikuwa yuleyule, na wanadarasa wenzangu walikuwa walewale. Jambo moja tu ndilo lililokuwa tofauti, yaani, niliwashinda wengi wa wanadarasa wenzangu katika ustadi wa kusoma kwa sababu nilikuwa nimehudhuria madarasa ya kusoma na kuandika kwenye Jumba la Ufalme.
Bidii yangu na mwenendo wangu uliwavutia walimu wengi, kwa hiyo hali haikuwa mbaya sana shuleni. Nilifanya mitihani fulani iliyonistahilisha kupata kazi nzuri katika migodi. Baadaye kazi hiyo iliniwezesha kuruzuku familia yangu. Ninafurahi kwamba sikukana kamwe imani yangu kwa kuimba.
-