Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Puma—Yupo Kila Mahali na Hayupo Popote
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • Puma—Yupo Kila Mahali na Hayupo Popote

      Na mleta-habari wa Amkeni! katika Brazili

      ANGA lililo juu ya msitu wa mvua wa Amerika Kusini lilikuwa likibadilisha ile rangi isiyoelezeka lililo nayo kabla tu ya usiku wa kitropiki kuifuta rangi hiyo. Kisha, kwa ghafula na kimyakimya, puma akatokea! Alikuwa ameingia kwa hadhari katika sehemu ya nchi iliyokuwa imekatwa miti na kusimama kwa ghafula.

      Kwa muda paka huyo mkubwa alisimama bila kusonga, isipokuwa ncha ya mkia wake, ambao uliendelea kusonga kama kipangusa-maji cha kioo cha gari kisongacho polepole. Kisha, alipotambua kuwa alikuwa akitazamwa, puma aliruka kupitia sehemu iliyokuwa imekatwa miti na kukimbia kuingia msituni. Alasiri hiyo miaka kadhaa iliyopita, niliweza kuona kwa nini viatu vitumiwavyo na wakimbiaji, magari yaendayo kasi, na hata ndege za kivita huitwa kwa jina lake. Kwa wazi, puma au chui mweusi, paka wa pili kwa ukubwa katika Marekani, ameumbwa kwa ajili ya mbio.a

      Tita la Misuli

      Kwa sababu ya rangi yake ya kahawia, puma aweza kukukumbusha simba wa kike. Hata hivyo, sehemu ya uso ya kichwa chake, si ya mstatili sana kama ya binamu yake wa Afrika. Badala ya hivyo, kichwa cha puma ni cha mviringo na ni kidogo na juu yake kuna masikio madogo ya mviringo. Kutoka upande kichwa chake huonekana kama risasi—nyembamba na ndefu. Anakukodolea macho makubwa ya kijani kibichi. Kiraka cha manyoya meupe kuuzunguka mdomo wake hutoa wazo la kwamba alikuwa ametumbukiza kinywa chake katika bakuli la maziwa, akasahau kupangusa mdomo wake. Mwili wake, mwepesi na mwembamba, waweza kuwa na urefu wa meta moja na nusu au zaidi, bila kutia ndani mkia wake mnene, wenye ncha nyeusi.

      Miguu yake ya nyuma mirefu na yenye nguvu hufanya sehemu yake ya nyuma kuwa juu zaidi ya mabega yake. Miguu hiyo yenye nguvu hulipa tita hili la misuli la kilogramu 60 nguvu za kuweza kutimua mbio kama roketi. Puma wameonekana wakiruka juu urefu wa meta tano kwa ruko moja kubwa. Hilo ni kama kuruka juu bila kutumia upondo!

      Anaporuka kuelekea chini, puma ni mwenye kupendeza vilevile. Amejulikana kwa kuruka kana kwamba anaruka kwa mabawa kutoka katika urefu wa meta 18. Hii ni karibu mara mbili ya urefu wa jukwaa linalotumiwa na wapiga-mbizi wa Olimpiki, lakini puma hana manufaa ya kidimbwi cha kuogelea kilichojazwa maji chini. Ijapokuwa hivyo, paka huyu hugonga ardhi akiwa tayari kuenda zake kana kwamba aliangukia wavu ulioshikiliwa na minyororo.

      “Huyu ni mnyama mwenye nguvu, na mwenye kutisha,” asema mwanabiolojia wa wanyama wa pori Kenneth Logan. “Mara ujuapo jinsi wanyama hawa huishi, wanadai staha nyingi sana.” Kwa kupendeza, waelekea kuwa kila mahali—lakini hawapo popote.

      Yupo Karibu Kila Mahali, Lakini Haonekani

      Wakati wakoloni wa kwanza walipofanya makao katika Ulimwengu Mpya, eneo la puma lilikuwa kontinenti nzima kutoka Atlantiki hadi Pasifiki. Aliishi katika milima, kwenye kinamasi, katika mbuga pana za Marekani, na msituni pia. Ijapokuwa wakulima na wawindaji wamemmaliza puma kutoka katika sehemu nyingi za Amerika Kaskazini, angali anabaki kuwa paka wa Amerika yote, akiwa angali anarandaranda kutoka Kanada hadi kwenye ncha ya Amerika Kusini. Ikiwa utakadiria kufaulu kwa mnyama kwa kuangalia jinsi alivyoenea kijiografia na ukubwa wa kao lake, basi puma ndiye mwenye kufaulu zaidi kati ya mamalia wenyeji wa Amerika leo. Siri ya kufaulu kwake ni nini?

      Puma ameandaliwa vizuri kwa ajili ya kuokoka. Tumbo lake ni lenye nguvu naye hutumia njia mbalimbali za kuwinda. Anaweza kuzoea karibu kila aina ya chakula cha mahali alipo. “Anaweza kumwua na kumvuta mnyama mkubwa mara tano kumshinda, lakini pia yeye hula panzi ikiwa hakuna chochote kingine cha kula,” asema daktari wa wanyama ambaye amechunguza vitu vilivyokuwamo katika tumbo za puma kadhaa waliokuwa wameuawa huko Brazili. “Kwa habari ya chakula, puma ni mwenye kubadilikana zaidi kuliko spishi nyingine yoyote ya paka.”

      Chakula mbalimbali pia huhitaji njia mbalimbali za kuwinda. Kwa mfano, ili kunyakua chakula, ndege atahitaji njia tofauti na ambayo hutumika na wanyama wengine kurukia chakula. Puma hufanyaje hivyo? Katika msitu wa Atlantiki wa Brazili, yeye humvutia ndege aitwaye tinamou kwa kuiga kilio cha ndege huyo. “Uigaji sahihi,” asema mtazamaji mmoja. “Tinamou hulia mara chache tu, lakini puma huendelea kulia—mara 10 au 20.” Hata hivyo, yeye hufanikiwa. Tinamou hufikiri kuwa ndege wa kiume mwenye kelele ameingilia eneo lake na anaamua kwenda mbele na kumkabili mpinzani wake—tendo liletalo kifo.

      Kama utamtafuta puma Amerika Kaskazini, Kati, au Kusini, mara nyingi yeye hufaulu kujificha asionekane—kutoonekana kama hewa, ipo kila mahali lakini haionekani. Vivumishi vinavyotumiwa mara nyingi na watafiti wanaomchunguza puma ni “msiri, mtelezi na mwenye uangalifu.” Baada ya kuwaua karibu puma 70, mwindaji mmoja alikiri kwamba “hakuwa amemwona mmoja wa wahasiriwa wake kabla mbwa hawajamlazimisha kupanda mti.” Bila shaka ndiyo sababu watafiti fulani wenye kuvunjika moyo humwita “mtelezi mwenye kutia kichaa”!

      Paka Mwenye Majina Mengi

      Hata hivyo, si kwamba paka huyu apatikanaye kote katika Marekani ni vigumu kumwona tu bali pia ni vigumu kumweleza. Kitabu The Guinness Book of Animal Records, chataarifu kwamba, puma “ana majina mengi kuliko mamalia mwingine yeyote ulimwenguni.” Mbali na majina 40 yasiyo ya kawaida yajulikanayo katika Kiingereza, “pia ana angalau majina 18 ya wenyeji wa Amerika Kusini na mengine zaidi 25 ya wenyeji wa Amerika Kaskazini.”

      Puma, jina linalotumika sana na wanazuolojia, hutokana na lugha ya Quechua ya Peru. Simba wa mlimani na chui mweusi, ni baadhi ya majina mengine anayopewa paka huyu.

      Msimamizi wa Bustani ya Wanyama ya São Paulo na mtaalamu wa puma, Dakt. Faiçal Simon, aonelea: “Tabia ya puma na uwezo wake wa kimwili ni tofauti na paka wengine wakubwa.” Kwa kweli huyu ni paka tofauti na ambaye hutofautiana katika ukubwa na rangi. Zaidi ya spishi ndogondogo 30 za puma zimetambuliwa kote katika Marekani, 6 zikiwa katika Brazili.

      Je, Anapasa Kuondoshwa?

      Kwa wafugaji wengi wa ng’ombe katika Brazili na kwingineko, puma huonwa kuwa asiyetamanika kama mnyama mharibifu na anastahili kupigwa risasi mara aonekanapo tu. Lakini je, puma anastahili jina la kuwa mwuaji wa ng’ombe asiye na huruma? “Ikiwa kuna wanyama wa pori, ni nadra kwa puma kuua ng’ombe,” Dakt. Simon aeleza. “Mara chache hili linapotokea kwa kweli halitetei utaratibu wa kumwangamiza mnyama huyu. Kwa hakika, kwa kuwapiga risasi puma, wafugaji wa ng’ombe wanajiumiza wenyewe.” Katika njia gani?

      Kwa kielelezo, katika eneo lenye kinamasi la Pantanal, katika Brazili lililo kubwa kuliko Korea Kusini, mahali ambapo ng’ombe wengi hutembea huku na huku kwa uhuru, wafugaji huwaua puma. Likiwa tokeo, aeleza Dakt. Simon, idadi ya wanyama wadogo waitwao armadilo—chakula anachopendelea sana puma katika eneo hilo—inaongezeka upesi. Armadilo ni mamalia walio na namna ya kujikinga ambao wana ukubwa kama wa sungura na huchimba mashimo. Bila kuwa na puma karibu, armadilo wanaligeuza eneo la malisho la Pantanal kuwa maeneo ya uuaji. Kwa njia gani?

      Bila shaka, ng’ombe kuingia katika mashimo, huvunjika miguu, na kufa. “Wafugaji hao sasa wanawapoteza ng’ombe wengi kuliko hapo awali kwa sababu wamewaua puma,” asema Dakt. Simon. “Ni kielelezo kingine tu cha linalotukia mwanadamu anapoingilia asili.”

      Idadi inayoongezeka ya watu katika Amerika wanataka kumhifadhi puma. Hivyo, mamlaka katika sehemu fulani za Amerika Kaskazini zimepitisha sheria zinazoonyesha hangaiko kwa puma ambazo zinadhibiti uwindaji na kutunza kao la paka huyo.

      Likiwa tokeo, katika magharibi mwa Marekani, puma anarudi tena, akijaza tena makao ya zamani. Kwa kweli, si kila mtu anayependelea hili, lakini wengi wanalipendelea. Gazeti Smithsonian lataarifu kwamba puma “amefanya badiliko lenye kupendeza . . . katika kipindi kifupi, kutoka kuwa mnyama mharibifu hadi kuwa mnyama anayetamaniwa sana.”

      Puma hutamaniwa na wapenda-asili na wawindaji pia. Kwa wapenda-asili, paka huyo ni ishara ya fahari ya nyikani lakini kwa wawindaji, abaki akiwa kumbukumbu ya ushindi. Swali labakia, Ni kwa muda gani puma ataendelea kuwa yote mawili?

  • Puma—Yupo Kila Mahali na Hayupo Popote
    Amkeni!—1998 | Aprili 22
    • “Kuwa Mwenye Kupenda Kuishi Pamoja”?

      Sheria za kumlinda puma, au chui mweusi, katika magharibi mwa Marekani hazikusaidia tu kuongeza idadi ya puma lakini pia kuongeza migongano kati ya puma na wanadamu. Sababu iko wazi: Idadi inayoongezeka ya watu wanafanya makao katika mipaka ya nyika—katika nchi ya puma—ikitokeza tatizo la usalama wa umma. Hata hivyo, mashambulio ya puma bado ni nadra. Watafiti wana uthibitisho wa mashambulizi 65 ya puma kwa wanadamu katika Marekani na Kanada tangu mwaka wa 1890—hiyo hupungua kuwa karibu mashambulizi 3 baada ya kila miaka mitano. Katika mashambulizi haya 65, labda 10 yalikuwa yenye kufisha. Kwa kulinganisha, katika Marekani pekee, karibu watu 40 hufa kwa mwaka kutokana na kuumwa na nyuki. “Akipewa nafasi zipatikanazo,” asema mwanabiolojia wa wanyama wa pori Kevin Hansen, “mashambulizi kwa watu ni matukio yaliyo nadra kwa hakika, jambo linalodokeza utayari mkubwa kwa upande wa chui mweusi wa kupenda kuishi pamoja, angalau kwa habari ya wanadamu.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki