-
Wanusurika KifoAmkeni!—2000 | Mei 8
-
-
Wanusurika Kifo
“Nyakati nyingine mimi huwaza kwamba nina miguu miwili tena. . . . Miaka mingi iliyopita, nilipokuwa mtoto, nilienda kucheza na rafiki zangu karibu na nyumba yetu. Ghafula, nilisikia ‘BUUM’ . . . Mguu wangu wa kulia ulilipuliwa wote.”—Song Kosal, mwenye umri wa miaka 12, Kambodia.
Kila siku, watu 70 kwa wastani hulemazwa au kuuawa na mabomu ya ardhini. Wahasiriwa wengi si wanajeshi. Badala yake, ni raia—wanaume wanaochunga ng’ombe, wanawake wanaoteka maji, na watoto wanaocheza. Kwa mfano, Rukia mwenye umri wa miaka minane tuliyemwonyesha kwenye jalada la gazeti hili, alikatwa kiungo cha mwili na bomu la ardhini lililoua nduguze watatu na shangaziye.
Bomu la ardhini laweza kubaki likiwa hatari kwa zaidi ya miaka 50 tangu linapotegwa. Hivyo, “ hiyo ndiyo silaha pekee inayoua watu wengi zaidi baada ya kukoma kwa vita kuliko wakati wa vita,” lasema gazeti la The Defense Monitor. Hakuna mtu ajuaye ni mabomu mangapi ya ardhini yametegwa ulimwenguni pote. Ni kawaida kusikia idadi ikikadiriwa kuwa angalau mabomu milioni 60. Ni kweli kwamba mabomu mengi ya ardhini yanaondolewa. Hata hivyo, hivi majuzi katika mwaka wa 1997, shirika la Umoja wa Mataifa liliripoti kwamba “bomu moja linapoondolewa, mabomu mengine 20 hutegwa ardhini. Mnamo mwaka wa 1994, mabomu yapatayo 100,000 yaliondolewa, na mabomu mengine milioni 2 yakategwa.”
Kwa nini mababe wengi wa vita leo wanapendelea mabomu ya ardhini? Yanaathirije uchumi na jamii? Manusura huathiriwaje? Je, sayari yetu itawahi kuwa bila mabomu ya ardhini?
-
-
Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari ZakeAmkeni!—2000 | Mei 8
-
-
Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari Zake
Katika Desemba 26, 1993, Augusto mwenye umri wa miaka sita alikuwa akitembea katika sehemu iliyo wazi karibu na Luanda, mji mkuu wa Angola. Kwa ghafula aliona kitu chenye kung’aa ardhini. Kilimvutia sana, akaamua kukiokota. Bomu hilo la ardhini lililipuka alipoligusa.
Ilibidi Augusto akatwe mguu wake wa kulia kwa sababu ya mlipuko huo. Sasa akiwa na umri wa miaka 12, anatembea kwa kiti cha magurudumu, naye ni kipofu.
AUGUSTO alilemazwa na bomu la ardhini linalokusudiwa kujeruhi watu, kwa sababu lengo lake ni watu wala si vifaru au magari mengine ya vita. Inakadiriwa kwamba kufikia sasa, zaidi ya aina 350 za mabomu ya ardhini yanayokusudiwa kujeruhi watu yametengenezwa angalau katika nchi 50. Mengi yake yamekusudiwa kujeruhi pasipo kuua. Kwa nini? Kwa sababu wanajeshi waliojeruhiwa huhitaji msaada, na mwanajeshi aliyejeruhiwa hupunguza utendaji wa kijeshi—fursa nzuri kwa maadui. Isitoshe, kilio cha kuomba msaada cha mwanajeshi aliyejeruhiwa chaweza kuwatia woga wanajeshi wenzake. Hivyo, kwa kawaida wahasiriwa wanapoponea chupuchupu ndipo mabomu ya ardhini yaonwapo kuwa na matokeo sana.
Hata hivyo, kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, wahasiriwa wengi wa mabomu ya ardhini huwa raia, si wanajeshi. Haitukii tu kwa nasibu sikuzote. Kulingana na kitabu Landmines—A Deadly Legacy, baadhi ya mabomu ya ardhini “hutegwa kimakusudi ili kuwafukuza raia kutoka kwenye maeneo, kuharibu maeneo yanayotoa chakula, kutokeza wakimbizi, au kueneza hofu tu.”
Kwa mfano, katika pambano moja huko Kambodia, mabomu ya ardhini yalitegwa kuzunguka vijiji vya maadui, kisha vijiji hivyo vikashambuliwa kwa mizinga. Raia walipojaribu kutoroka waliingia moja kwa moja katika maeneo yenye mabomu yaliyotegwa ardhini. Wakati huohuo, wanamgambo wa Khmer Rouge walitega mabomu katika mashamba ya mpunga huku wakijaribu kuilazimisha serikali ikubali majadiliano, hatua hiyo iliwatia hofu kubwa wakulima na kukomesha kilimo.
Jambo lililotukia Somalia mwaka wa 1988 huenda lilikuwa bovu zaidi. Mji wa Hargeysa ulipolipuliwa kwa mabomu, wakazi walilazimika kukimbia. Kisha wanajeshi wakatega mabomu ya ardhini katika nyumba zilizoachwa. Wakimbizi waliporejea baada ya mapigano kukoma, walilemazwa au kuuawa na mabomu yaliyofichwa.
Mbali na kuua na kulipua viungo vya mwili, mabomu ya ardhini hutokeza madhara zaidi. Fikiria baadhi ya athari nyingine za silaha hizi hatari.
Athari za Kiuchumi na Kijamii
Katibu-mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan asema hivi: “Kuwapo—au hata hofu ya kuwapo kwa bomu moja la ardhini kwaweza kuzuia shamba zima lisilimwe, kusababisha njaa kijijini, kuzuia kujenga upya na maendeleo nchini.” Hivyo, katika Afghanistan na Kambodia, zaidi ya asilimia 35 hivi ya ardhi ingelimwa endapo wakulima hawangehofu kukanyaga udongo. Baadhi yao hujihatarisha. “Naogopa sana mabomu ya ardhini,” asema mkulima mmoja wa Kambodia. “Lakini nisipoenda kufyeka nyasi na mianzi, tutakufa.”
Mara nyingi, manusura wa mabomu ya ardhini hulipia gharama kubwa sana. Kwa mfano, katika nchi inayositawi, mtoto anayepoteza mguu akiwa na umri wa miaka kumi huenda akahitaji viungo bandia 15 hivi maishani mwake, kila kiungo kikigharimu dola 125 za Marekani kwa wastani. Ni kweli kwamba huenda wengine wanaweza kumudu gharama hizo. Lakini kwa wakazi wengi wa Angola, dola 125 za Marekani ni mshahara wa zaidi ya miezi mitatu!
Fikiria pia athari mbaya za kijamii. Kwa mfano, raia wa nchi moja ya Asia huepuka kushirikiana na watu waliokatwa viungo, kwa sababu ya kuhofia “bahati mbaya.” Mtu aliyekatwa kiungo cha mwili aweza kukosa tumaini la kufunga ndoa. “Mimi sipangi kuoa,” asikitika mwanamume mmoja wa Angola ambaye alikatwa mguu baada ya kujeruhiwa na mlipuko wa bomu la ardhini. “Mwanamke hutaka mwanamume anayeweza kufanya kazi.”
Kwa wazi, wahasiriwa wengi hukumbwa na hisia za kutojistahi. “Siwezi tena kulisha familia yangu,” asema mwanamume mmoja wa Kambodia, “na hilo huniaibisha.” Nyakati nyingine hisia hizo zaweza kumdhoofisha mtu hata kuliko kupoteza kiungo. “Naamini kwamba niliumia zaidi kihisia-moyo,” asema Artur, mhasiriwa wa Msumbiji. “Mara nyingi nilikasirika kwa sababu tu ya kuangaliwa na mtu. Nilidhani kwamba hakuna mtu aliyenistahi tena na kwamba sitawahi kuishi maisha ya kawaida tena.”a
Vipi Juu ya Kuondoa Mabomu ya Ardhini?
Katika miaka ya majuzi mataifa yametiwa moyo sana yapige marufuku utumiaji wa mabomu ya ardhini. Pia, serikali fulani zimeanza kazi hatari ya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini. Lakini kuna vizuizi kadhaa. Kizuizi cha kwanza ni wakati. Kuondoa mabomu ya ardhini ni kazi inayofanywa miaka nenda miaka rudi. Kwa hakika, wateguaji wa mabomu hayo hukadiria kwamba kwa wastani, muda unaohitajiwa kuondoa bomu lililotegwa ardhini ni mara 100 zaidi ya muda unaotumiwa kulitega. Kizuizi kingine ni gharama. Bomu moja hugharimu kati ya dola 3 hadi 15 za Marekani, lakini kuliondoa kwaweza kugharimu dola zipatazo 1,000.
Kwa hiyo, yaonekana kuondoa mabomu yote yaliyotegwa ni jambo lisilowezekana. Kwa mfano, kuondoa mabomu yote ya ardhini huko Kambodia, kutamaanisha kwamba kila mtu nchini humo atoe mshahara wake wote kwa miaka kadhaa kwa ajili ya kazi hiyo. Inakadiriwa kwamba hata fedha zikiwapo, kuondoa mabomu yote ya ardhini yaliyotegwa huko kungechukua muda wa karne moja. Hali ya ulimwenguni pote ni yenye kusikitisha hata zaidi. Inakadiriwa kwamba kuondoa mabomu yote duniani kwa kutumia tekinolojia ya kisasa, kungegharimu dola bilioni 33 za Marekani na kungechukua muda wa zaidi ya miaka 1,000!
Ni kweli kwamba mbinu mpya za kuondoa mabomu ya ardhini zimependekezwa—kutoka kutumia nzi-tunda ambao wametiwa chembe za kuwasaidia kugundua mabomu hadi kutumia magari makubwa yenye kuelekezwa kwa mawimbi ya redio ambayo yangeondoa mabomu kwenye eneo la ekari tano kwa kila saa moja. Lakini, itahitaji muda fulani kabla ya mbinu hizo kuweza kutumiwa kila mahali, na yaelekea zitatumiwa katika nchi tajiri tu.
Hivyo, nchi nyingi hutumia mbinu za kale za kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini. Mtu hujikokota kwa tumbo huku akichimba-chimba mbele kwa kijiti, sentimeta kwa sentimeta, eneo la meta 20 hadi 50 za mraba kwa siku. Ni hatari, sivyo? Ndivyo! Kwa kila mabomu 5,000 yanayoondolewa, mteguaji mmoja hufa na wawili hujeruhiwa.
Waungana Kukomesha Mabomu ya Ardhini
Mnamo Desemba 1997, wawakilishi kutoka nchi kadhaa walitia sahihi Mkataba wa Kupiga Marufuku Utumiaji, Urundikaji, Utengenezaji na Uuzaji wa Mabomu ya Ardhini na wa Kuharibu mabomu hayo, pia huitwa mkataba wa Ottawa. “Hayo ni mafanikio yasiyo na kifani katika sheria ya kimataifa ya upunguzaji wa silaha au sheria ya kimataifa inayotetea haki za binadamu,” asema Jean Chrétien, waziri mkuu wa Kanada.b Hata hivyo, nchi zipatazo 60—kutia ndani baadhi ya watengenezaji mashuhuri wa mabomu ya ardhini ulimwenguni—hazijatia sahihi mkataba huo.
Je, mkataba wa Ottawa utafaulu kukomesha kabisa tatizo la mabomu ya ardhini? Labda kwa kiasi fulani. Lakini wengi wana shaka. “Hata nchi zote ulimwenguni zikifuata mkataba wa Ottawa,” asema Claude Simonnot, mkurugenzi-msaidizi wa Shirika la Handicap International, katika Ufaransa, “hiyo itakuwa hatua moja tu katika kukomesha hatari ya mabomu ya ardhini duniani.” Kwa nini? “Mamilioni ya mabomu yangali yametegwa ardhini, yakisubiri kuwalipua watu,” asema Simonnot.
Mwanahistoria wa kijeshi John Keegan ataja sababu nyingine. Yeye asema kwamba vita “huathiri hisia-moyo za mwanadamu, . . . ambazo ni chimbuko la fahari, hisia zenye nguvu, na tabia za kiasili zilizojificha.” Mikataba haiwezi kubadili tabia za binadamu zilizokita mizizi kama vile chuki na pupa. Lakini je, hilo lamaanisha kwamba wanadamu wataendelea kuwa wahasiriwa wa mabomu ya ardhini daima?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi juu ya kushughulikia kupoteza kiungo cha mwili, ona makala kuu ya mfululizo yenye kichwa “Tumaini kwa Walemavu,” katika ukurasa wa 3-10 wa toleo la Amkeni! la Juni 8, 1999.
b Mkataba huo ulianza rasmi Machi 1, 1999. Kufikia Januari 6, 2000, ulikuwa umetiwa sahihi na nchi 137 na kuidhinishwa na nchi 90 kati yake.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Je, Wanachuma Fedha Maradufu?
Kanuni ya msingi ya biashara ni kwamba makampuni yanapasa kushtakiwa bidhaa zao zinapodhuru watu. Hivyo, Lou McGrath, wa shirika la Mines Advisory Group, asema kwamba makampuni ambayo yamefaidika kutokana na utengenezaji wa mabomu ya ardhini yapasa kushurutishwa kulipia hasara. Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba watengenezaji wengi ndio wanaochuma fedha kwa kuondoa mabomu hayo. Kwa mfano, imeripotiwa kwamba kampuni moja ya Ujerumani iliyokuwa ikitengeneza mabomu ya ardhini ilipata kandarasi ya dola milioni 100 za Marekani ili kuondoa mabomu ya ardhini huko Kuwait. Na huko Msumbiji, shirika lenye makampuni matatu—mawili kati yake yalikuwa yametengeneza mabomu ya ardhini—lilipata kandarasi ya dola milioni 7.5 ya kuondoa mabomu kwenye barabara zilizoteuliwa.
Baadhi ya watu wanahisi kwamba ni ukosefu mkubwa wa adili kwa makampuni yanayotengeneza mabomu ya ardhini kuchuma fedha kwa kuondoa mabomu hayo. Wanadai kwamba kwa njia fulani watengenezaji wa mabomu ya ardhini huchuma fedha maradufu. Kwa vyovyote vile, kutengeneza na kuondoa mabomu ya ardhini bado ni biashara zinazositawi.
[Mchoro katika ukurasa wa 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Idadi ya wastani ya mabomu ya ardhini kwenye eneo la kilometa 2.5 za mraba katika nchi tisa zenye mabomu mengi yaliyotegwa
BOSNIA na HERZEGOVINA 152
KAMBODIA 143
KROATIA 137
MISRI 60
IRAKI 59
AFGHANISTAN 40
ANGOLA 31
IRAN 25
RWANDA 25
[Hisani]
Kutoka kwa: United Nations Department of Humanitarian Affairs, 1996
[Picha katika ukurasa wa 7]
Huko Kambodia, mabango na ishara kubwa huonya juu ya mabomu ya ardhini
Kwa kila mabomu 5,000 yanayoondolewa, mteguaji mmoja hufa na wawili hujeruhiwa
[Hisani]
Mandhari nyuma: © ICRC/Paul Grabhorn
© ICRC/Till Mayer
© ICRC/Philippe Dutoit
-
-
Dunia Isiyokuwa na Mabomu ya ArdhiniAmkeni!—2000 | Mei 8
-
-
Dunia Isiyokuwa na Mabomu ya Ardhini
NI NANI awezaye kutatua tatizo la mabomu ya ardhini? Kama tulivyokwisha kuona, wanadamu hawawezi kukomesha chuki, ushupavu, na pupa. Hata hivyo, wanafunzi wa Biblia hung’amua kwamba Muumba anaweza kutatua tatizo hilo kabisa. Atalitatuaje?
Kutokeza Jamii Yenye Amani
Watu ndio wanaopigana vita, si silaha. Kwa hiyo, chuki inayowatenganisha wanadamu kwa vikundi vya kijamii, kikabila, na kitaifa sharti ikomeshwe kabisa iwapo twataka amani. Mungu aahidi kuikomesha kupitia kwa Ufalme wake, ambao mamilioni ya watu duniani wamefunzwa kusali juu yake.—Mathayo 6:9, 10.
Biblia humtaja Yehova kuwa “Mungu apaye amani.” (Waroma 15:33) Amani anayotoa Mungu haitegemei marufuku na mikataba, wala haitegemei hofu ya ulipizaji kisasi wa taifa adui lenye silaha kali. Kinyume cha hilo, amani itokayo kwa Mungu huhusisha mabadiliko katika njia ya watu ya kufikiri na mitazamo yao kuelekea wanadamu wenzao.
Yehova Mungu atawafundisha wanyenyekevu njia zake za amani. (Zaburi 25:9) Neno lake, Biblia, huahidi wakati ambapo wote walio hai “watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.” (Isaya 54:13) Jambo hilo tayari linatukia kwa kadiri fulani. Ulimwenguni pote, Mashahidi wa Yehova wana sifa ya kudumisha amani hata miongoni mwa watu wenye malezi mbalimbali. Watu wanaofundishwa kanuni bora za Biblia hujitahidi kuishi kwa umoja bila kujali maswala yanayoweza kuwatenganisha. Elimu ya Biblia hubadili kabisa mtazamo wa chuki waliokuwa nao kuwa wa upendo.—Yohana 13:34, 35; 1 Wakorintho 13:4-8.
Mbali na elimu, uhitaji wa ushirikiano wa ulimwenguni pote umeonwa kwa muda mrefu kuwa jambo muhimu katika kuharibu silaha. Kwa mfano, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu linapendekeza kwamba jumuiya ya kimataifa ishirikiane katika kudumisha hali zitakazozuia na kukomesha kabisa tisho la mabomu ya ardhini.
Yehova anaahidi kutimiza mengi zaidi. Nabii Danieli alitabiri hivi: “Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele. . . . Utavunja falme hizi zote [zilizopo] vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”—Danieli 2:44.
Ufalme wa Mungu utatimiza mambo ambayo mwanadamu hawezi kutimiza. Kwa mfano, Zaburi 46:9 yatabiri: “[Yehova] avikomesha vita hata mwisho wa dunia. Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari.” Ufalme wa Mungu utatokeza mazingira ambamo mwanadamu atafurahia kabisa amani kati yake na Muumba wake na mwanadamu mwenzake.—Isaya 2:4; Sefania 3:9; Ufunuo 21:3, 4; 22:2.
Augusto, aliyetajwa mwanzoni mwa makala iliyotangulia, hufarijiwa na ujumbe huo wa Biblia. Wazazi wake, ambao ni Mashahidi wa Yehova, wanamsaidia kujenga imani katika ahadi nzuri ajabu za Biblia. (Marko 3:1-5) Bila shaka, hana budi kuvumilia sasa maumivu yanayotokana na mlipuko wa bomu la ardhini lililomlemaza. Hata hivyo, Augusto atazamia wakati ambapo ahadi ya Mungu ya paradiso duniani itakapotimizwa. “Ndipo,” akatabiri nabii Isaya, “macho ya vipofu yatafumbuliwa, na . . . mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu.”—Isaya 35:5, 6.
Katika Paradiso ijayo, mabomu ya ardhini hayatahatarisha tena uhai na viungo vya mwili. Badala yake, watu wataishi kwa usalama duniani kote. Nabii Mika alisema hivi: “Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.”—Mika 4:4.
Je, ungependa kujifunza mengi juu ya ahadi za Mungu zilizo katika Neno lake Biblia? Wasiliana na Mashahidi wa Yehova walio karibu nawe, au andika kwa anwani ifaayo iliyoorodheshwa kwenye ukurasa wa 5 wa gazeti hili.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Chini ya Ufalme wa Mungu, mabomu ya ardhini hayatakuwa tisho tena
-