-
Mfumo Tata wa ViumbeAmkeni!—2001 | Novemba 22
-
-
Je, Twahitaji Aina Zote Hizo?
Je, kuna haja ya kuhangaikia kuangamia kwa aina mbalimbali za viumbe? Je, kweli twahitaji aina tofauti-tofauti za viumbe? Wataalamu wengi wanaoheshimiwa husisitiza kwamba twahitaji aina hizo. Aina za viumbe duniani huwaandalia wanadamu chakula, kemikali muhimu, na bidhaa na huduma nyinginezo. Pia, fikiria kuhusu faida zinazoweza kutokana na aina ambazo hazijagunduliwa. Kwa mfano, imekadiriwa kwamba dawa 120 kati ya dawa 150 kuu ambazo madaktari huwapendekezea watu nchini Marekani, hutengenezwa kwa mali asili. Hivyo, aina za mimea zinapoangamia, wanadamu hupoteza njia ya kuvumbua dawa na kemikali mpya. Bwana Ghillean Prance, mkurugenzi wa Bustani za Kew huko London, alisema hivi: ‘Kila mara aina moja ya kiumbe inapoangamia, tunapoteza kitu ambacho tungetumia siku za baadaye. Tunapoteza dawa inayoweza kutibu UKIMWI, au zao linaloweza kukinza virusi. Hivyo, ni lazima tukomeshe uharibifu wa viumbe, si kwa faida ya dunia tu bali kwa ajili ya . . . mahitaji na matumizi yetu.’
Pia, twahitaji mazingira yanayoweza kudumisha uhai wa viumbe vyote. Mazingira yasiyo na kasoro hutimiza kazi muhimu kama vile kutengeneza oksijeni, kusafisha maji, kuondoa vichafuzi, na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Wadudu huchavusha mimea. Vyura, samaki, na ndege huangamiza wadudu waharibifu; kome na viumbe vingine vinavyoishi majini husafisha maji; mimea na vijidudu hutengeneza udongo. Huduma hizo hutokeza faida kubwa sana za kiuchumi. Kulingana na kadirio la kiwango cha chini lililofanywa kupatana na bei za 1995, aina mbalimbali za viumbe ulimwenguni pote huleta faida ya dola bilioni 3,000 za Marekani kila mwaka.
-
-
Mfumo Tata wa ViumbeAmkeni!—2001 | Novemba 22
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Uhai Una Thamani Gani?
Huenda mazungumzo kuhusu umuhimu wa kuwa na aina mbalimbali za viumbe yakaelekea kuonyesha kwamba twapaswa kujali viumbe vingine iwapo tu vinatufaidi. Wengine wanaonelea kwamba hayo ni mawazo yasiyofaa. Mtaalamu wa elimu ya visukuku Niles Eldredge alionyesha thamani ya uhai kwa kusema hivi: “Sisi wanadamu huthamini pia viumbe katika mazingira yetu—aina za viumbe vinavyovutia, maeneo ya pori yenye kupendeza—kwa sababu ya thamani yake muhimu. Kitu fulani ndani yetu hutambua kwamba tuna uhusiano fulani na mazingira hayo ya asili na kwamba twapata utulivu na furaha tunapokuwa katika mazingira hayo inapowezekana.”
-