Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • “Biashara Yenye Wafanyakazi Wengi Zaidi”
    Amkeni!—2005 | Agosti 22
    • “Biashara Yenye Wafanyakazi Wengi Zaidi”

      Kila mwaka, zaidi ya watu milioni 600 husafiri katika nchi nyingine. Mamia ya mamilioni zaidi husafiri katika nchi yao kwa sababu za kikazi na tafrija. Matokeo ni kwamba, biashara ya utalii, inayohusisha hoteli, mashirika ya ndege, kampuni zinazoshughulikia usafiri wa watalii, na kampuni nyingine zinazoshughulikia mahitaji ya wasafiri, inatajwa kuwa ndiyo biashara “yenye wafanyakazi wengi zaidi.”

      ULIMWENGUNI pote, utalii huleta dola trilioni nne hivi kila mwaka. Huenda mtalii mmoja-mmoja asijione kuwa sehemu ya wanaharakati wa kuleta amani ulimwenguni, lakini hivyo ndivyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Ulimwenguni linavyoeleza biashara hiyo. Mnamo 2004, Francesco Frangialli, katibu mkuu wa shirika hilo, aliuambia hivi mkutano uliopangwa na waziri mkuu wa Israeli huko Mashariki ya Kati: “Huwezi kutenganisha utalii na amani. Uvutano unaotokezwa na utalii ni wenye nguvu sana hivi kwamba unaweza kubadili hali zinazoonekana kuwa haziwezi kubadilishwa na kuleta mapatano mahali ambapo yalidhaniwa kuwa hayawezekani.”

      Biashara hii yenye uvutano mkubwa ilianzaje? Je, kweli utalii huleta faida? Na je, kweli “uvutano unaotokezwa na utalii” unaweza kuleta amani?

      Kipindi Chenye Mafanikio Katika Utalii

      Mabadiliko katika biashara ya sasa ya utalii katika nchi za Magharibi yalianza hasa katika karne ya 19. Mvuvumko wa kiviwanda ulifanya watu wengi zaidi wa hali ya chini huko Ulaya na Marekani wawe na pesa na wakati wa kusafiri.

      Isitoshe, maendeleo makubwa yalifanywa katika njia za kusafirisha watu wengi. Magari-moshi yenye nguvu yaliwasafirisha abiria kutoka jiji moja kuu hadi lingine, na meli kubwa ziliwasafirisha haraka kutoka bara moja hadi lingine. Ili kuandaa mahitaji ya idadi ya wasafiri iliyokuwa ikiongezeka, hoteli kubwa zilijengwa karibu na vituo vya magari-moshi na kwenye bandari.

      Mnamo 1841, mfanyabiashara Mwingereza Thomas Cook aliona faida ya kuunganisha mambo hayo yote. Alikuwa mtu wa kwanza kupanga kwamba huduma za usafiri, mahali pa kulala, chakula, na tafrija, zigharimiwe kwa ujumla. Mwanasiasa Mwingereza William Gladstone alisema hivi katika miaka ya 1860: “Kutokana na mfumo ulioanzishwa na Bw. Cook, kwa mara ya kwanza watu wa matabaka mbalimbali wameweza kutembelea nchi za kigeni na kuzifahamu kwa kadiri fulani, jambo ambalo limefanya wawatendee kwa fadhili badala ya kuwadharau watu wa nchi hizo.”

      Ongezeko la Watalii Katika Karne ya 20

      Kwa kusikitisha, kuwafahamu watu wa nchi nyingine ambako kulisababishwa na utalii hakukuzuia kuzuka kwa vita viwili vya ulimwengu katika nusu ya kwanza ya karne ya 20. Hata hivyo, badala ya kuharibu utalii, mabadiliko ya kijamii na maendeleo ya kiteknolojia yaliyochochewa na vita hivyo yalifanya biashara hiyo ikue.

      Usafiri wa ndege ulichukua muda mfupi zaidi na kugharimu pesa kidogo zaidi, barabara kuu zilienea kotekote katika mabara mbalimbali, na magari yakaongezeka. Kufikia katikati ya karne ya 20, lilikuwa jambo la kawaida kwa watu katika nchi za Magharibi kwenda likizo na kutalii, kwa kuwa watu wa tabaka mbalimbali wangeweza kugharimia safari hizo. Isitoshe, nyumba nyingi zilianza kuwa na televisheni na hivyo watu walivutiwa sana na picha za maeneo yenye kupendeza ambayo yalichochea hamu ya kusafiri.

      Mwanzoni mwa miaka ya 1960, idadi ya watalii waliozuru nchi nyingine ilifikia milioni 70 kila mwaka. Kufikia katikati ya miaka ya 1990, idadi hiyo iliongezeka sana na kufikia zaidi ya milioni 500! Hoteli za watalii ziliibuka ulimwenguni pote ili kushughulikia wasafiri wenyeji na wa kigeni. Biashara ambazo hazikuhusiana moja kwa moja na utalii zilinufaika, kwa kuwa watalii hutumia vyakula na vinywaji vingi na hununua bidhaa na kulipia huduma nyingine.

      Leo, biashara ya utalii ni muhimu kwa uchumi wa nchi zaidi ya 125. Likikazia manufaa yanayoweza kuletwa na utalii, ripoti moja ya mwaka wa 2004 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Ulimwenguni, inaeleza kwamba utalii unaweza kupunguza umaskini kwa kutokeza biashara ndogo na za kiwango cha kadiri za utalii. Inapotokeza nafasi za kazi, inaweza “kuwahamasisha watu kuhusu masuala ya kimazingira, kitamaduni na kijamii.”

      Lakini huenda ukajiuliza: ‘Utalii unaweza kutimizaje mambo hayo? Na unawezaje kunufaisha mazingira?’

      Kutalii Mazingira ili Kuyahifadhi

      Mwanzoni mwa miaka ya 1980, baadhi ya wanasayansi na watengenezaji wa filamu walianza kupendezwa na kuhifadhi misitu ya mvua, matumbawe na pia viumbe ambao hutegemea vitu hivyo. Ripoti, sinema, na vipindi vya televisheni vinavyosimulia uumbaji vilifanya watu wapendezwe zaidi kutalii maajabu hayo ya uumbaji. Biashara ndogo ambazo zilianzishwa ili kushughulikia mahitaji ya wanasayansi na watengenezaji hao wa filamu zilipanuka ili kushughulikia mahitaji ya watalii wengi wanaovutiwa na mazingira.

      Utalii wa kuhifadhi mazingira umewavutia watu wengi na kuufanya uwe sehemu ya utalii inayokua haraka zaidi. Kwa kweli, kuwachochea watu wapendezwe na maajabu ya uumbaji kumeleta faida kubwa. Mwandishi wa habari, Martha S. Honey, anaeleza hivi: “Katika nchi nyingi, utalii wa kuhifadhi mazingira ulikua haraka na kuwa biashara inayoletea nchi hizo pesa nyingi sana za kigeni kuliko ndizi nchini Kosta Rika, kahawa nchini Tanzania na Kenya, na vitambaa na vito nchini India.”

      Kwa hiyo, utalii umekuwa njia muhimu ya kupata pesa za kuhifadhi mimea na wanyama. Honey alisema: “Nchini Kenya inakadiriwa kwamba simba mmoja huleta dola 7,000 kwa mwaka, nalo kundi la tembo huleta dola 610,000 kila mwaka.” Inakadiriwa kwamba matumbawe ya Hawaii huleta dola milioni 360 kila mwaka!

      Utalii wa Kuhifadhi Mazingira Unahusisha Nini?

      Ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa yenye kichwa, Ecotourism: Principles, Practices and Policies for Sustainability inasema: “Biashara nyingi za usafiri na utalii hutumia maneno ‘utalii wa kuhifadhi mazingira’ katika vichapo vyao, na serikali zimetumia maneno hayo sana ili kuwachochea watu watembelee nchi zao, bila kujaribu kufanya jambo lolote linalohusiana [na utalii wa kuhifadhi mazingira].” Unawezaje kujua ikiwa safari unayopanga itakuwa kweli utalii wa kuhifadhi mazingira?

      Megan Epler Wood, aliyeandika ripoti iliyotajwa anasema kwamba utalii wa kuhifadhi mazingira unatia ndani mambo yafuatayo: Kabla ya safari, watu wanaosimamia safari hizo hutoa habari kuhusu utamaduni na mazingira yatakayotembelewa kutia ndani maagizo kuhusu mavazi na tabia inayofaa; pia wao huwatolea watalii habari ya kutosha kuhusu sura ya nchi, hali ya kijamii na ya kisiasa ya nchi itakayotembelewa na nafasi za kuchangamana na wenyeji katika vikao visivyo vya kibiashara; wao huhakikisha kwamba ada zote za kuingia kwenye mbuga zimelipwa; nao huandaa mahali pa kulala panapofaana na mazingira.

      Utalii wa Kuhifadhi Mazingira Umetimiza Nini?

      Utalii wa kuhifadhi mazingira unatia ndani mengi zaidi ya safari iliyopangwa ya kuzuru eneo fulani la asili. Umefafanuliwa kuwa “safari ya kutembelea mazingira ya asili kwa kusudi la kuelewa utamaduni wa wenyeji, wanyama, na mimea katika eneo hilo bila kuharibu mazingira ya asili na wakati huohuo kutokeza fedha za kuhifadhi maliasili zinazowafaidi wenyeji.”

      Je, utalii wa kuhifadhi mazingira umetimiza mambo hayo? Martin Wikelski, wa Chuo Kikuu cha Princeton anasema: “Utalii wa kuhifadhi mazingira ni mojawapo ya mambo ambayo yamesaidia kuhifadhi [Visiwa vya] Galapagos.” Katika nchi ya Afrika ya Rwanda, inasemekana kwamba kuchochea utalii wa kuhifadhi mazingira, kumechangia kuhifadhiwa kwa idadi ya sokwe wanaoishi milimani ambao huwasaidia wenyeji wajiruzuku kwa njia tofauti badala ya kuwinda wanyama hao. Katika nchi nyingine za Afrika, mbuga za wanyama hutegemea pesa zinazoletwa na watalii.

      Ulimwenguni pote, utalii wa kuhifadhi mazingira umechangia kuboresha mazingira na jamii, na bila shaka biashara ya utalii imeleta faida nyingi za kifedha. Lakini je, biashara hiyo huleta faida nyakati zote? Usafiri ulimwenguni utakuwaje katika siku zijazo?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

      Madokezo kwa Wale Wanaosafiri Nchi za Kigenia

      Kabla ya kusafiri

      1. Andika orodha ya habari muhimu kama vile habari zilizo kwenye pasipoti yako, nambari za kadi ya mkopo, nambari ya tiketi ya ndege, na hundi ya msafiri. Acha nakala moja nyumbani na ubebe nakala nyingine.

      2. Hakikisha kwamba muda wa pasipoti yako haujakwisha na una viza; fanya mpango wa kupata chanjo ambazo huenda zikahitajiwa.

      3. Hakikisha kwamba una bima ya hospitali, kwa kuwa matibabu au usafirishaji wa dharura kutoka nchi za kigeni unaweza kugharimu pesa nyingi. Ikiwa una ugonjwa fulani, beba barua kutoka kwa daktari wako inayoeleza hali yako na dawa unazotumia. (Tahadhari: Huenda ikawa kinyume cha sheria kuingiza dawa fulani katika nchi unayosafiri. Pata habari kutoka kwa ubalozi wa nchi unayopanga kutembelea.)

      Unaposafiri

      1. Usibebe kitu chochote chenye thamani kubwa.

      2. Beba pasipoti yako na vitu vingine vyenye thamani mwilini mwako, si kwenye mkoba au kwenye mifuko. Hati hizo muhimu zisibebwe na mshiriki mmoja tu wa familia.

      3. Ikiwa unabeba pochi ndani ya mfuko, ifunge kwa kamba za mpira ili wezi wasiichomoe kwa urahisi.

      4. Weka rekodi ya vitu unavyonunua kwa kutumia kadi ya mkopo, na usipitishe kiasi ulichopanga kutumia. Huenda ukakamatwa katika nchi fulani ukizidisha kiwango ulichowekewa katika kadi hiyo.

      5. Uwe mwangalifu kuhusu kuwapiga wanajeshi picha au majengo yao au majengo kama vile bandari, reli, au viwanja vya ndege. Nchi fulani zinaweza kuona hilo kuwa tisho kwa usalama.

      6. Usikubali kubeba kifurushi cha mtu usiyemjua vizuri.

      Unaponunua vitu vya kukukumbusha kuhusu safari yako

      1. Kumbuka kwamba nchi nyingi haziruhusu kuingizwa kwa pembe za tembo, kombe za kasa, mimea, sufu, na vitu vingine, hata ikiwa ni vitu vidogo vya kukukumbusha sehemu ulizotembelea.

      2. Jihadhari unaponunua vyombo vya udongo vilivyopakwa rangi na kuchomwa kwani baadhi ya vitu hivyo vinaweza kutokeza sumu ya madini ya risasi ikiwa havijatengenezwa vizuri.

      [Maelezo ya Chini]

      a Habari hii imetolewa kutoka katika Kichapo 10542 cha Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni.

  • Wakati Ujao wa Utalii
    Amkeni!—2005 | Agosti 22
    • Wakati Ujao wa Utalii

      “Kuna mifano kutoka karibu kila nchi ulimwenguni ambako miradi ya utalii imetajwa kuwa kisababishi kikuu cha kuharibiwa kwa mazingira.”—An Introduction to Tourism, cha Leonard J. Lickorish na Carson L. Jenkins.

      MBALI na kuhatarisha mazingira, utalii unaweza kusababisha matatizo mengine pia. Na tuchunguze baadhi ya matatizo hayo. Baadaye, tutazungumzia jinsi tutakavyoweza kutalii dunia yetu maridadi na kujifunza kuhusu maajabu yake, hasa wakazi wake wazuri.

      Matatizo ya Kimazingira

      Idadi kubwa ya watalii leo imetokeza matatizo. Watafiti Lickorish na Jenkins, wanaandika hivi: “Huko India, kaburi la Taj Mahal linachakaa kwa sababu ya kutembelewa na wageni.” Kwa kuongezea, wanasema: “Pia huko Misri, piramidi zinaendelea kuharibika kwa sababu ya kutembelewa na wageni wengi sana.”

      Isitoshe, waandishi hao wanaonya kwamba utalii usiodhibitiwa unaweza kuharibu au kuzuia ukuzi wa mimea wakati wageni wengi wanapokanyaga-kanyaga maeneo yaliyotengwa ili kuhifadhi maliasili. Kwa kuongezea, jamii za viumbe wanaweza kuhatarishwa watalii wanapokusanya vitu visivyopatikana kwa urahisi kama vile makombe ya baharini na marijani au wakati wenyeji wanapokusanya vitu hivyo ili kuwauzia watalii.

      Watalii husababisha uchafuzi. Kulingana na makadirio ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, kila mtalii hutokeza wastani wa kilo moja ya takataka kila siku. Inaonekana kwamba hata maeneo ya mbali zaidi yanaathiriwa. Ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Mvua linasema: ‘Katika vijia vya Himalaya vinavyotumiwa sana na watalii, takataka zimetupwa kotekote na msitu huo wa milimani umeharibiwa na wageni ambao hutafuta kuni za kupasha moto chakula na maji ya kuoga.’

      Isitoshe, mara nyingi watalii hutumia kiasi kikubwa cha mali ambacho kingetumiwa na wenyeji. Kwa mfano, James Mak anaandika hivi katika kitabu chake Tourism and the Economy: “Huko Grenada watalii hutumia mara saba kiasi cha maji ambacho wakazi wa huko hutumia.” Anaongeza hivi: “Asilimia 40 ya nishati inayotumiwa huko Hawaii hutumiwa katika utalii kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, ingawa kwa wastani ni mtu mmoja tu kati ya wanane ambaye ni mtalii.”

      Ingawa watalii hutumia pesa nyingi kutembelea nchi zinazositawi, kiasi kikubwa cha pesa hizo hakiwafaidi wenyeji. Benki ya Dunia inakadiria kwamba asilimia 45 tu ya pesa zinazokusanywa kutokana na utalii ndizo zinazotumiwa na nchi iliyotembelewa, kiasi kikubwa cha pesa hurudia mataifa yaliyositawi kupitia kampuni za kigeni za kupanga safari za watalii na hoteli zinazomilikiwa na wageni.

      Athari za Kijamii

      Watalii walio na utajiri wa kiasi kutoka nchi za Magharibi ambao hutembelea nchi zinazositawi wanaweza kutokeza athari zilizojificha na nyakati nyingine zinazoonekana waziwazi kwa utamaduni wa wenyeji. Kwa mfano, mara nyingi watalii huja na vitu vya anasa. Huenda wenyeji wasiwazie kamwe kuwa na vitu kama hivyo. Wenyeji wengi hutamani vitu hivyo ghali lakini hawawezi kuvigharimia bila kufanya mabadiliko makubwa maishani, mabadiliko ambayo huenda yakaathiri tabia za wenyeji.

      Mak alitaja matatizo yanayoweza kutokea akisema kwamba kuongezeka kwa biashara ya utalii kunaweza “kufanya utamaduni na tabia za pekee za wenyeji zitoweke, kutokeza mizozo katika jamii za kitamaduni kuhusu jinsi mashamba ya jamii na maliasili inavyopaswa kutumiwa, na kueneza tabia zisizokubaliwa na jamii kama vile uhalifu na ukahaba.”

      Mara nyingi leo watalii huhisi kwamba wako huru kufanya watakavyo, kwa hiyo wao hujihusisha na mambo ambayo hawangefanya ikiwa wangekuwa nyumbani pamoja na familia na marafiki wao. Hivyo, ukosefu wa maadili wa watalii umekuwa tatizo kubwa. Akitaja mfano unaojulikana sana, Mak alisema: “Ulimwenguni pote kuna wasiwasi kuhusu jinsi utalii unavyochangia kuongezeka kwa ukahaba wa watoto.” Mnamo 2004, shirika la habari la CNN liliripoti hivi: “‘Makadirio yanayotegemeka yanaonyesha kwamba watoto 16,000 hadi 20,000’ hutendewa vibaya kingono huko Mexico, ‘hasa mipakani, mijini, na katika maeneo ya watalii.’”

      Manufaa ya Kusafiri

      Dunia yetu ni makao yenye mambo mengi ya kupendeza kama vile machweo yenye rangi nyingi, nyota nyingi zenye kumeta-meta, na mimea na wanyama wa aina mbalimbali. Haidhuru mahali tunapoishi, sisi hufurahia mambo hayo kutia ndani maajabu mengine ya dunia yetu. Hata hivyo, ni jambo la kupendeza kama nini tunapopata nafasi ya kusafiri na kuona maajabu mengine ya dunia!

      Hata hivyo, ingawa watalii wengi huvutiwa na mandhari za asili za dunia, wengi wao husema kwamba jambo kuu katika safari zao huwa kufahamiana na watu walio na utamaduni tofauti. Mara nyingi, wasafiri hutambua kwamba maoni yasiyofaa kuhusu watu wa nchi nyingine si ya kweli. Kusafiri huwasaidia wawaelewe watu wa rangi na utamaduni mwingine na kusitawisha urafiki wenye kudumu.

      Watalii wengi hujifunza kwamba si vitu vya kimwili hasa huwafanya watu wawe na furaha. Jambo muhimu ni kuwa na uhusiano mzuri na wengine, yaani, kudumisha urafiki wa muda mrefu na kuanzisha urafiki na wengine. Simulizi fulani la Biblia linaeleza jinsi wasafiri wa karne ya kwanza waliovunjikiwa na meli huko Malta walivyonufaika na “fadhili za kibinadamu” zilizoonyeshwa na wenyeji wa huko “wenye kusema lugha ya kigeni.” (Matendo 28:1, 2) Kutembelea nchi na watu wengine leo kumewasaidia wengi kutambua kwamba kwa kweli sisi sote ni familia moja na tunaweza kuishi pamoja duniani kwa amani.

      Sasa ni watu wachache tu wanaoweza kutembelea sehemu mbalimbali ulimwenguni. Lakini mambo yatakuwaje wakati ujao? Je, itawezekana kwa watu wengi, au hata wote kufanya hivyo?

      Matarajio ya Wakati Ujao

      Ukweli ni kwamba sisi sote tuna ukoo, sisi ni washiriki wa familia ya kibinadamu. Ni kweli kwamba wanadamu wa kwanza wawili walikufa sawa na vile Mungu alivyokuwa amewaonya ingetukia ikiwa wangekosa kumtii. (Mwanzo 1:28; 2:17; 3:19) Kwa hiyo, wazao wao wote, kutia ndani sisi sote leo huzeeka na kufa. (Waroma 5:12) Lakini Mungu anaahidi kuwa kusudi lake la awali kwamba dunia ikaliwe na watu wanaompenda litatimizwa. Neno lake linasema: “Mimi nimesema hilo . . . pia nitalitenda.”—Isaya 45:18; 46:11; 55:11.

      Hebu wazia hilo! Biblia inaahidi kwamba chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu: “Waadilifu wenyewe wataimiliki dunia, nao watakaa milele juu yake.” (Zaburi 37:29; Mathayo 6:9, 10) Ikifafanua hali ya wakati ujao ya watu duniani, Biblia inasema hivi: “Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena.”—Ufunuo 21:3, 4.

      Fikiri kuhusu jinsi itakavyowezekana kutembelea sehemu mbalimbali duniani na kufahamu maajabu yake, hasa watu wake wazuri. Wakati huo hakutakuwa na wasiwasi kuhusu usalama! Watu wote duniani watakuwa marafiki wetu, kwa kweli, watakuwa kama Biblia inavyowaita ‘ushirika mzima wa ndugu ulimwenguni.’—1 Petro 5:9.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki