-
Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya YanayotarajiwaAmkeni!—2002 | Mei 22
-
-
Kuhofu Kwamba Ulimwengu Utagawanyika Zaidi
Huenda hangaiko kuu kuhusu utandaridhi ni jinsi ambavyo umezidisha ile tofauti kati ya matajiri na maskini. Ijapokuwa ni wazi kwamba utajiri wa ulimwengu umeongezeka, ni watu wachache zaidi na nchi chache zaidi zilizo na utajiri huo. Sasa mali halisi za watu 200 matajiri zaidi ulimwenguni ni nyingi kuliko jumla ya mapato ya watu bilioni 2.4 hivi wanaoishi duniani—asilimia 40 ya watu wote duniani. Na ijapokuwa mapato yanaendelea kuongezeka katika nchi tajiri, mapato ya wastani katika nchi 80 zenye umaskini yamepungua katika muda wa miaka kumi iliyopita.
Hangaiko jingine la maana linahusu mazingira. Utandaridhi wa kiuchumi umechochewa na shughuli za biashara zinazokazia faida za kiuchumi kuliko kuhifadhi mazingira. Agus Purnomo, msimamizi wa Hazina ya Mazingira ya Ulimwenguni Pote huko Indonesia, anaeleza tatizo hilo hivi: ‘Tunataka maendeleo daima. Nina wasiwasi kwamba baada ya miaka kumi, tutakuwa tumefahamu umuhimu wa kutunza mazingira, lakini hakutakuwa na viumbe wa kuhifadhi.’
Watu pia wanahangaikia kazi zao. Imekuwa rahisi zaidi kupoteza kazi na mapato kwa sababu mashirika yanayoungana ulimwenguni pote na mashindano makali katika biashara yanalazimu makampuni kuboresha huduma zao. Makampuni yanayohangaikia kupata faida kubwa huona kwamba ni jambo la busara kuwaajiri na kuwafuta wafanyakazi kwa kutegemea faida inayopatikana, lakini jambo hilo huwaletea watu matatizo makubwa.
Kuongezeka kwa mikopo na fedha za kigeni ulimwenguni pote kumetokeza tatizo jingine. Watega-uchumi wa kimataifa wanaweza kukopesha nchi zinazoendelea fedha nyingi sana lakini baadaye kuondoa fedha zao kwa ghafula wakati hali ya uchumi inapozorota. Wakati fedha hizo zinapoondolewa nchi zinazohusika zinaweza kukumbwa na matatizo ya kiuchumi. Mnamo mwaka wa 1998, watu milioni 13 walifutwa kazi huko Asia Mashariki kwa sababu ya hali mbaya za kiuchumi. Huko Indonesia, mapato halisi ya wale wafanyakazi ambao hawakufutwa kazi yalipungua kwa asilimia 50.
-
-
Je, Kuunganisha Ulimwengu Kutatatua Matatizo Yetu Kweli?Amkeni!—2002 | Mei 22
-
-
Tofauti Inayozidi Kuongezeka
Sikuzote kumekuwa na matajiri na maskini ulimwenguni pote, lakini utandaridhi wa kiuchumi umeongeza ile tofauti kati ya matajiri na maskini. Ni kweli kwamba inaonekana nchi fulani zinazoendelea zimefaidika tangu zilipoingia katika biashara ya ulimwenguni pote. Wataalamu wanasema kwamba katika miaka kumi iliyopita, idadi ya watu maskini huko India ilipungua toka asilimia 39 hadi asilimia 26 na kwamba maendeleo kama hayo pia yamekuwako katika bara lote la Asia. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kufikia mwaka wa 1998, asilimia 15 tu ya watu huko Asia Mashariki ndio walioishi kwa dola 1 kwa siku, ikilinganishwa na asilimia 27 miaka kumi mapema. Hata hivyo, hali ulimwenguni pote si nzuri hivyo.
Katika eneo lililoko kusini mwa jangwa la Sahara huko Afrika na katika maeneo fulani mengine yanayoendelea, mapato yameshuka katika muda wa miaka 30 iliyopita. Kofi Annan, katibu-mkuu wa UM, anasema hivi: “Jumuiya ya kimataifa . . . inakubali watu wapatao bilioni 3—karibu nusu ya wanadamu wote—kuishi kila siku kwa dola 2 za Marekani au chini ya hapo katika ulimwengu wenye utajiri mwingi sana.” Ubinafsi katika biashara ni jambo moja kuu linalosababisha tofauti hiyo kubwa ya kijamii. Larry Summers, aliyekuwa waziri wa fedha wa Marekani anasema hivi: ‘Ulimwenguni pote, taasisi za watu binafsi zinazoshughulika na mikopo na fedha za kigeni huwapuuza maskini hohehahe. Benki kubwakubwa hazianzishwi katika sehemu zenye umaskini—kwa sababu hazitapata faida.’
Tofauti hiyo kubwa katika mapato ya matajiri na maskini huwafanya watu na nchi mbalimbali kugawanyika. Muda mfupi uliopita, mali za yule mtu tajiri zaidi huko Marekani zilizidi jumla ya mali halisi za Wamarekani wengine zaidi ya milioni 100. Utandaridhi pia umesaidia makampuni tajiri ya kimataifa kuimarika na kudhibiti kwa kadiri kubwa biashara ya bidhaa fulani ulimwenguni. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, makampuni kumi tu ndiyo yaliyodhibiti asilimia 86 ya biashara ya mawasiliano ya simu ambayo ina thamani ya dola bilioni 262 za Marekani. Mara nyingi, makampuni hayo ya kimataifa huwa na uwezo mkubwa kuliko serikali mbalimbali na, kama vile shirika la Amnesty International linavyosema, makampuni hayo “hayatilii maanani haki za binadamu na za wafanyakazi.”
Mashirika ya haki za binadamu yanahangaikia jinsi watu wachache wanavyomiliki mali nyingi, na hilo linaeleweka. Je, ungependa kuishi mahali ambapo matajiri, ambao wanafanyiza asilimia 20 ya idadi ya watu, wanachuma mapato yanayozidi yale ya maskini kwa mara 74? Na kupitia televisheni, watu hao maskini, ambao wanafanyiza asilimia 20 ya idadi ya watu, wanafahamu vyema jinsi matajiri wanavyoishi, ijapokuwa hawana njia ya kuboresha maisha yao. Ukosefu huo mwingi wa haki katika ulimwengu wetu huchochea sana fujo na mfadhaiko.
-