Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Kuunganisha Ulimwengu Kutatatua Matatizo Yetu Kweli?
    Amkeni!—2002 | Mei 22
    • Tofauti Inayozidi Kuongezeka

      Sikuzote kumekuwa na matajiri na maskini ulimwenguni pote, lakini utandaridhi wa kiuchumi umeongeza ile tofauti kati ya matajiri na maskini. Ni kweli kwamba inaonekana nchi fulani zinazoendelea zimefaidika tangu zilipoingia katika biashara ya ulimwenguni pote. Wataalamu wanasema kwamba katika miaka kumi iliyopita, idadi ya watu maskini huko India ilipungua toka asilimia 39 hadi asilimia 26 na kwamba maendeleo kama hayo pia yamekuwako katika bara lote la Asia. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba kufikia mwaka wa 1998, asilimia 15 tu ya watu huko Asia Mashariki ndio walioishi kwa dola 1 kwa siku, ikilinganishwa na asilimia 27 miaka kumi mapema. Hata hivyo, hali ulimwenguni pote si nzuri hivyo.

      Katika eneo lililoko kusini mwa jangwa la Sahara huko Afrika na katika maeneo fulani mengine yanayoendelea, mapato yameshuka katika muda wa miaka 30 iliyopita. Kofi Annan, katibu-mkuu wa UM, anasema hivi: “Jumuiya ya kimataifa . . . inakubali watu wapatao bilioni 3—karibu nusu ya wanadamu wote—kuishi kila siku kwa dola 2 za Marekani au chini ya hapo katika ulimwengu wenye utajiri mwingi sana.” Ubinafsi katika biashara ni jambo moja kuu linalosababisha tofauti hiyo kubwa ya kijamii. Larry Summers, aliyekuwa waziri wa fedha wa Marekani anasema hivi: ‘Ulimwenguni pote, taasisi za watu binafsi zinazoshughulika na mikopo na fedha za kigeni huwapuuza maskini hohehahe. Benki kubwakubwa hazianzishwi katika sehemu zenye umaskini—kwa sababu hazitapata faida.’

      Tofauti hiyo kubwa katika mapato ya matajiri na maskini huwafanya watu na nchi mbalimbali kugawanyika. Muda mfupi uliopita, mali za yule mtu tajiri zaidi huko Marekani zilizidi jumla ya mali halisi za Wamarekani wengine zaidi ya milioni 100. Utandaridhi pia umesaidia makampuni tajiri ya kimataifa kuimarika na kudhibiti kwa kadiri kubwa biashara ya bidhaa fulani ulimwenguni. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1998, makampuni kumi tu ndiyo yaliyodhibiti asilimia 86 ya biashara ya mawasiliano ya simu ambayo ina thamani ya dola bilioni 262 za Marekani. Mara nyingi, makampuni hayo ya kimataifa huwa na uwezo mkubwa kuliko serikali mbalimbali na, kama vile shirika la Amnesty International linavyosema, makampuni hayo “hayatilii maanani haki za binadamu na za wafanyakazi.”

      Mashirika ya haki za binadamu yanahangaikia jinsi watu wachache wanavyomiliki mali nyingi, na hilo linaeleweka. Je, ungependa kuishi mahali ambapo matajiri, ambao wanafanyiza asilimia 20 ya idadi ya watu, wanachuma mapato yanayozidi yale ya maskini kwa mara 74? Na kupitia televisheni, watu hao maskini, ambao wanafanyiza asilimia 20 ya idadi ya watu, wanafahamu vyema jinsi matajiri wanavyoishi, ijapokuwa hawana njia ya kuboresha maisha yao. Ukosefu huo mwingi wa haki katika ulimwengu wetu huchochea sana fujo na mfadhaiko.

  • Njia ya Kuunganisha Ulimwengu Ambayo Itakufaidi
    Amkeni!—2002 | Mei 22
    • “Ili utandaridhi ufaulu, ni lazima uwafaidi maskini na matajiri kwa usawa. Ni lazima watu wapate haki zao kama wanavyopata mali. Ni lazima utokeze haki na usawa katika jamii sawa na ufanisi wa kiuchumi na maendeleo ya mawasiliano.”—KOFI ANNAN, KATIBU-MKUU WA UMOJA WA MATAIFA.

      KAMA vile Kofi Annan alivyosema, ili utandaridhi ufaulu, ni lazima uboreshe maisha ya watu wote ulimwenguni. Lakini hali ya maisha haijawa nzuri katika miaka ya hivi majuzi. Kumekuwa na ufanisi mwingi wa kiuchumi na maendeleo ya kitekinolojia kuliko maendeleo katika haki za binadamu na usawa katika jamii.

      Tatizo kuu ni kwamba utandaridhi wa kiuchumi unachochewa hasa na tamaa ya kupata mali. Watu wanaoongozwa na tamaa hiyo hawawafikirii maskini wala kutilia maanani masilahi ya siku zijazo ya dunia. Dakt. David C. Korten anasema hivi: “Biashara ya ulimwenguni pote isiyodhibitiwa ambayo inaongozwa na mashirika ambayo yanazingatia tu kupata fedha haiwezi kuwa thabiti . . . na inawafanya wanadamu kuwa maskini katika njia nyingine.”

      Je, serikali za ulimwengu zitaweza kudhibiti biashara ya ulimwenguni pote ili itokeze haki katika jamii? Inaonekana hilo haliwezekani. Kufikia sasa, serikali zimeshindwa kutatua matatizo yoyote ulimwenguni—iwe ni uhalifu wa kimataifa, ongezeko la joto duniani, au umaskini ulimwenguni pote. Annan anasema hivi: ‘Watu wanahitaji kushirikiana kutunza masilahi ya ulimwenguni pote, lakini katika ulimwengu huu wa utandaridhi mbinu za kufanya kazi hiyo ya ulimwenguni pote ni za hali ya chini sana.’

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki