-
Kusamehe na Kusahau Je, Kwawezekana?Amkeni!—1998 | Agosti 8
-
-
Kusamehe na Kusahau Je, Kwawezekana?
ZAIDI ya nusu-karne imepita tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, mwaka wa 1945. Vita hiyo ya duniani pote ilikuwa yenye ukatili zaidi na yenye hasara zaidi kuliko vita vyote katika historia ya wanadamu.
Vita ya Ulimwengu ya Pili ilidumu kwa miaka sita na kusababisha vifo vya watu wapatao milioni 50, kutia ndani raia. Wengine wengi walilemazwa kimwili, na kuvurugika kiakili na kihisia-moyo. Wengi ambao walipitia miaka hiyo ya vita yenye msiba, wangali wanakumbuka kwa uchungu ukatili uliofanywa na kuwakumbuka wapendwa wao waliokufa.
Kuna kumbukumbu za ukatili uliofanywa na Wanazi wakati wa yale Maangamizi Makubwa, wakati ambapo mamilioni ya watu wasio na hatia waliuawa kinyama. Katika Ulaya na Asia, ukatili mwingi ulifanywa na majeshi yenye kushambulia, ambayo yaliua, yalibaka, yalipora, na kuhofisha raia. Vilevile, watu wengi waliathiriwa na mashambulizi ya ndege za kijeshi ambazo zilisababisha uharibifu mkubwa, majeruhi, na vifo vya wanaume, wanawake, na watoto wengi wasio na hatia. Mamilioni ya wanajeshi pia walipata magumu katika vita mbalimbali duniani.
Athari za Kiakili na za Kihisia-Moyo
Athari nyingi za kiakili na za kihisia-moyo zilizosababishwa na matukio yenye kuogofya sana ya wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili zingali dhahiri shahiri katika akili za watu wengi walioishi wakati huo ambao bado wangali hai. Wangependa kuzisahau kumbukumbu hizo mbaya na zenye uchungu. Lakini wameshindwa. Wengine hurudiwa na picha za ukatili huo ambao huwatesa kama ndoto za kutisha zenye kujirudia-rudia.
Hata hivyo, wengine hawataki kusahau ama kwa sababu wanataka kulipiza kisasi ama kwa sababu wanataka kuwakumbuka wenzao waliouawa. Na pia kuna maoni yaliyoenea kwamba ukatili uliofanywa zamani wapaswa kukumbukwa na wanadamu kwa ujumla kwa matumaini ya kwamba hautarudiwa kamwe.
Miaka michache iliyopita, katika kipindi cha 1994-1995, hisia zilizoenea wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Siku Kubwa (siku ambayo mataifa yenye Muungano yalipoanza mashambulizi katika Normandy Juni 1944) na mwisho wa vita ya ulimwengu ya pili katika Ulaya (mnamo Mei 1945) yalidhihirisha kwamba ilikuwa vigumu sana kwa wengi waliojionea mambo hayo kusamehe na kusahau. Mara nyingi, pendekezo lolote la kutaka mapatano kati ya wale ambao zamani walikuwa maadui hukataliwa. Kwa hiyo, mashujaa wa vita wa Uingereza walikataa kualika wawakilishi wa Ujerumani katika maadhimisho ya kuingia kwa majeshi ya Muungano katika Normandy.
Kuhusu ukatili uliofanywa na Wanazi katika Vita ya Ulimwengu ya Pili na ugumu wa kusamehe na kusahau, mwandikaji Vladimir Jankélévitch alijieleza hivi: “Kuhusu uhalifu wenye kuchukiza sana hivyo, elekeo la kawaida . . . ni kughadhabika na kukataa katakata kusahau na kuwasaka wahalifu hao—kama walivyoahidi mahakimu wa Mahakama ya Mataifa yenye Muungano ya Nuremberg—hadi mwisho wa dunia.” Mwandikaji uyo huyo aliendelea kusema: “Tungefurahi kusema, tukifuata kinyume cha ile sala ambayo Yesu alimtolea Mungu katika Gospeli kulingana na Mtakatifu Luka: Bwana, usiwasamehe, kwa kuwa wanajua wanachofanya.”—Linganisha Luka 23:34.
Kwa kuhuzunisha, tangu 1945 na kuendelea, hadi wakati wetu, ukatili mwingine mwingi umeendelea kumwaga damu duniani—nchini Kambodia, Rwanda, Bosnia, tukitaja kifupi tu. Ukatili huo umesababisha vifo vya mamilioni ya watu, na vilevile kuacha idadi kubwa sana ya wajane na mayatima, maisha yaliyoharibiwa, na kuacha wengi wakiwa na kumbukumbu zenye kusikitisha sana.
Bila shaka, karne hii ya 20 imekuwa wakati wa ukatili mbaya zaidi. Ni kama tu Biblia ilivyotabiri kwa usahihi muda mrefu kabla ya wakati huu—watu wamekuwa “wakali” na “wasio na upendo wa wema.”—2 Timotheo 3:1-5; Ufunuo 6:4-8.
Tufanye Nini?
Watu wakikabili ukatili kama huo, wao hutenda kwa njia tofauti-tofauti. Lakini vipi sisi? Je, tuukumbuke? Au tuusahau? Je, kukumbuka kwamaanisha kuwafungia kinyongo cha ndani maadui wa zamani, tukikataa kusamehe? Kwa upande mwingine, je kusamehe kwamaanisha kwamba mtu aweza kusahau kabisa kumbukumbu zote zenye uchungu?
Muumba wa wanadamu, Yehova Mungu, anafikiri nini juu ya uhalifu wenye ukatili ambao umefanywa katika wakati wetu na katika nyakati zilizopita? Je, atawasamehe waliofanya ukatili? Na je, haijachelewa mno kwa Mungu kuwapa ridhaa watu waliokufa katika ukatili huo? Je, kuna tumaini lolote thabiti kwamba ukatili utapata kwisha, kwa kuwa umekuwa ukiendelea kwa maelfu ya miaka? Mungu Mweza-Yote atasuluhishaje mambo hayo yenye kutatanisha?
-
-
Je, Tuyakumbuke Yaliyopita?Amkeni!—1998 | Agosti 8
-
-
Je, Tuyakumbuke Yaliyopita?
“JE, WAYAHUDI waweza kusahau yale Maangamizi Makubwa?” Swali hili lilizushwa na Virgil Elizondo, msimamizi wa Kituo cha Utamaduni wa Kimexico na Kimarekani katika San Antonio, Texas. Linatukumbusha kwamba ukatili ambao umefanywa katika karne hii unaweza kuacha kumbukumbu zisizoweza kusahaulika katika akili za watu kwa ujumla. Yale maangamizi ya Waarmenia (1915-1923) na mauaji makubwa ya Wakambodia (1975-1979) ni lazima pia yatiwe ndani ya ukatili ambao umefanywa katika karne ya 20. Na bado kuna mengine.
Wakijaribu kupatanisha watu walioathiriwa na watesi wao, viongozi wa kidini na wa kisiasa wamewaomba watu mara nyingi wasahau ukatili waliotendwa. Kwa mfano, jambo hilo lilitendeka Athens, Ugiriki, mwaka wa 403 K.W.K. Jiji hilo lilikuwa limetoka tu kutawalwa kimabavu na wale walioitwa Wakatili Thelathini, ambao ulikuwa utawala wa wachache ulioondolea mbali, hata kihalisi, karibu maadui wake wote. Magavana wapya walijaribu kurudisha utengamano wa raia kwa kuamuru kusamehewa kwa watu waliounga mkono utawala uliopita.
Je, Inawezekana Kusahau kwa Sababu ya Amri ya Kusamehe?
Inaweza kuwa rahisi kujaribu kufuta kwa amri kumbukumbu za ukatili waliotendwa watu wasio na hatia. Watawala waweza kuamua kufanya hivyo kwa faida yao ya kisiasa, kama ilivyofanyika katika Ugiriki ya kale na katika nchi kadhaa za Ulaya mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Kwa mfano, nchini Italia amri moja katika mwaka wa 1946 ilitangaza kuachiliwa kwa zaidi ya raia 200,000 ambao “walikuwa na hatia ya kushiriki, kwa njia moja au nyingine, katika maovu ya utawala wa Kifashisti,” likasema gazeti la habari La Repubblica.
Ni rahisi kwa serikali au mashirika ya umma kufanya maamuzi. Lakini ni vigumu kuondoa hisia za watu mmoja-mmoja. Haiwezekani kuweka sheria ya kushurutisha raia mmoja-mmoja—labda watu wasio na kinga walioathiriwa na vita vikatili, mauaji, au ukatili mwingine wowote—wasahau jinsi walivyoteseka wakati uliopita.
Zaidi ya watu milioni mia moja wamekufa vitani katika karne hii pekee, wengi wakafa baada ya kuteseka vibaya sana. Tukiongezea wale wote ambao wamekufa katika mauaji ya wakati wa amani, ukatili huo ungekuwa mwingi usiweze kuhesabika. Watu wengi hujitahidi sana kuhakikisha kwamba hata jambo moja halisahauliki.
Wale Ambao Wangependa Kufuta Kumbukumbu Hizo
Watu wanaowahimiza wale walioathiriwa na ukatili au wazao wao wasahau na kusamehe mara nyingi husisitiza kwamba kukumbuka yaliyopita husababisha tu mgawanyiko, hasa ikiwa miongo mingi imepita. Wao husema kwamba kusahau huleta muungano, na kukumbuka ni kama maji yaliyokwisha kumwagika, hayawezi kuzoleka hata kama kuteseka kulikuwa msiba ulioje.
Lakini wakijaribu kuwafanya watu wasahau, wengine wamefikia hatua ya kukana uhalisi wa uhalifu mbaya zaidi waliofanyiwa wanadamu. Wakiungwa mkono na watu wanaojiita eti wasahihishaji wa historia, wengine hudai, kwa mfano, kwamba yale Maangamizi Makubwa hayakutokea kamwe.a Hata wamepanga safari za kuzuru kambi za mauaji, kama Auschwitz au Treblinka, nao wamewaambia wageni kwamba vyumba vya kuulia watu kwa gesi havikuwapo kamwe katika kambi hizo—na wanasema hayo japo uthibitisho mwingi ajabu wa mashahidi waliojionea na hati nyingi sana.
Inakuwaje kwamba mawazo ya wasahihishaji hao bandia wa historia yanakubaliwa na watu fulani? Kwa sababu watu wengine hutaka kusahau hatia zao na za watu wao. Kwa nini? Kwa sababu ya uzalendo, dhana zao wenyewe, au uhasama dhidi ya Wayahudi au uhasama mwingine kama huo. Wasahihishaji hao wa historia wakata kauli kwamba mara ukatili huo usahauliwapo, hatia huisha. Lakini watu wengi huwapinga sana wasahihishaji hao wasiowajibika, ambao wameitwa na mwanahistoria mmoja Mfaransa “wauaji wa kumbukumbu.”
Hawasahau
Bila shaka ni vigumu sana kwa waokokaji kusahau wapendwa wao waliokufa vitani au katika ukatili. Lakini, wengi wa wale wanaotaka kukumbuka yale mauaji na maangamizi wanafanya hivyo kwa sababu wanatumaini kwamba somo linalotokana na kuteseka kwao na kuteseka kwa wapendwa wao litasaidia kuepusha kurudiwa kwa ukatili kama huo.
Basi, serikali ya Ujerumani imeamua kuadhimisha siku ya kugunduliwa kwa ukatili wa Wanazi katika kambi ya mateso ya Auschwitz. Kulingana na rais wa Ujerumani kusudi ni kwamba “kukumbuka kutakuwa onyo kwa vizazi vya wakati ujao.”
Vivyo hivyo, kwenye mwadhimisho wa mwaka wa 50 wa mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, papa John Paul wa Pili alisisitiza: “Miaka ipitapo, kumbukumbu za Vita hazipaswi kudidimia; badala yake, zinapasa kuwa somo kali kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.” Lakini, ni lazima itajwe kwamba si kawaida kwa Kanisa Katoliki kukumbuka ukatili uliofanywa na vilevile waathiriwa wa miaka hiyo.
Ili vizazi vipya pia vipate somo na maonyo kutokana na maangamizi ya jamii katika karne hii na nyinginezo, majumba kadhaa ya makumbusho yamefunguliwa—kama vile Jumba la Makumbusho la Maangamizi Makubwa katika Washington, D.C., na Beit Hashoah Museum of Tolerance katika Los Angeles. Kwa sababu iyo hiyo, sinema za mambo halisi zenye kugusa moyo zinazohusu habari hii zimefanyizwa. Hayo yote yamefanywa ili kujaribu kuzuia wanadamu wasisahau watu walioteswa na wengine.
Kwa Nini Tukumbuke?
“Wale ambao hawawezi kukumbuka yaliyopita ni sharti watarudia kuyafanya,” akaandika mwanafalsafa mmoja Mhispania aliyezaliwa Marekani, George Santayana. Kwa kusikitisha, inaonekana kwamba katika maelfu ya miaka mwanadamu husahau haraka wakati wake uliopita, na kuyafanya tena na tena makosa yaleyale yenye msiba.
Mfululizo mrefu wa mauaji ya kikatili yaliyofanywa na wanadamu wakazia kwamba binadamu ameshindwa kabisa kumtawala binadamu. Kwa nini? Kwa sababu wanadamu wamerudia daima kufanya kosa lilelile la msingi—wamemkataa Mungu na sheria zake. (Mwanzo 3:1-6; Mhubiri 8:9) Na leo, kama ilivyotabiriwa katika Biblia, “kizazi kilichopotoka” kinafanya kosa ilo hilo na kuvuna tufani.—Wafilipi 2:15; Zaburi 92:7; 2 Timotheo 3:1-5, 13.
Kwa kuwa tumemhusisha Muumba, Yehova, katika mazungumzo yetu, yeye ana maoni gani? Yeye husahau nini, naye hukumbuka nini? Je, historia yenye uchungu wa ukatili unaofanywa na wanadamu unaweza kusahaulika? Je, ‘ubaya wao wasio haki utakoma’?—Zaburi 7:9.
-
-
Ukatili—Mungu Ana Suluhisho Gani?Amkeni!—1998 | Agosti 8
-
-
Ukatili—Mungu Ana Suluhisho Gani?
UKATILI unaweza kuzuiwaje? Kuna suluhisho gani? Tunapojifunza historia, inakuwa wazi kwamba masuluhisho ya wanadamu yameshindwa. Kwa hakika, kuna kujipinga kwingi, au hata unafiki wa wazi, katika njia ambayo viongozi wa kibinadamu wameshughulikia jambo hili.
Kwa mfano, fikiria mwaka wa 1995. Huo ulikuwa uadhimisho wa mwaka wa 50 wa mwisho wa Maangamizi Makubwa ya Nazi, wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, na kulipuliwa kwa bomu la atomu. Mwaka huo, sherehe za ukumbusho zilizohudhuriwa na viongozi wa ulimwengu zilifanywa katika sehemu nyingi za ulimwengu. Kwa nini? Ili kuonyesha jinsi wanavyokirihi ukatili uliofanywa ili usipate kurudiwa tena. Lakini, wachunguzi fulani waliona tu kujipinga kubaya katika sherehe hizo.
Unafiki
Katika sherehe hizo zilizotangazwa sana, wawakilishi wote wa kidini na wa kiserikali walitaka waonwe kuwa wafadhili au angalau wasionwe kuwa waovu. Lakini, mataifa yaliyoshutumu ukatili uliofanywa wakati uliopita yamejirundikia silaha, yakipanga bajeti ya pesa nyingi sana kwa sababu ya vita. Wakati uo huo, hayajasuluhisha matatizo mazito kama vile umaskini, kupotoka kwa maadili, na uchafuzi, mara nyingi yakisema kwamba hayana pesa za kutosha.
Dini ya kilimwengu inataka kuandika upya historia ambayo inafunika ukimya wake wa muda mrefu juu ya ukatili wa utawala wa kimabavu na kuficha ushirikiano wake na watawala hao wa kimabavu. Dini hizo hazikuzuia kamwe watu wa dini moja wasiuane. Kwa mfano, katika Vita ya Ulimwengu ya Pili, Mkatoliki alimwua Mkatoliki na Mprotestanti alimwua Mprotestanti eti kwa sababu walikuwa watu wa mataifa tofauti na kwenye pande zinazopigana. Pande zote mbili zilidai kuwa za Kikristo lakini zikafanya mambo yaliyokuwa tofauti kabisa na mafundisho ya Yesu. (Mathayo 26:52; Yohana 13:34, 35; 1 Yohana 3:10-12; 4:20, 21) Dini nyinginezo zimefanya vivyo hivyo. Leo, katika sehemu nyingi za ulimwengu, ukatili ungali unafanywa na watu wa dini hizo.
Wakati wa Yesu, viongozi wa kidini walikuwa wanafiki. Yesu aliwashutumu, akisema: “Ole wenu nyinyi, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu nyinyi mwajenga makaburi ya manabii na kuyarembesha makaburi ya ukumbusho ya waadilifu, nanyi mwasema, ‘Kama tungekuwa katika siku za baba zetu wa zamani, hatungekuwa washiriki pamoja nao katika damu ya manabii.’ Kwa hiyo mnatoa ushahidi dhidi yenu wenyewe kwamba nyinyi ni wana wa wale waliowaua manabii kimakusudi.” (Mathayo 23:29-31) Viongozi hao wa kidini walidai kuwa wenye kumcha Mungu lakini walikuwa wanafiki ambao walimnyanyasa Yesu na wanafunzi wake.
Masomo Tunayopata Katika Biblia
Masomo yaweza kupatikana katika historia ya kilimwengu, lakini Biblia ndiyo chanzo cha masomo yenye kunufaisha zaidi. Haimwachii mwanadamu ajifasirie mwenyewe historia yake kwa kupatana na uamuzi wake au ubaguzi wake. Biblia yafafanua historia na wakati ujao katika njia ya Mungu ya kufikiri.—Isaya 55:8, 9.
Maandiko yasema juu ya matukio mema na mabaya na vilevile juu ya watu wema na wabaya. Mara nyingi somo lenye kufaa, lenye kupatana na mapenzi ya Mungu, laweza kupatikana katika masimulizi hayo. Baada ya kutaja matukio kadhaa katika historia ya Israeli la kale, mtume Paulo alimalizia hivi: “Basi mambo hayo yaliendelea kuwapata kuwa vielelezo, nayo yaliandikwa kuwa onyo kwetu sisi.” (1 Wakorintho 10:11) Yesu mwenyewe alitaja somo la historia alipowaambia wanafunzi wake: “Mkumbukeni mke wa Loti.”—Luka 17:32.
Mambo Anayoyakumbuka Mungu na Anayoyasahau
Twajifunza katika Biblia kwamba Mungu huwakumbuka watu au huwasahau kwa kutegemea matendo yao. Wale wanaotenda dhambi lakini wanatubu husamehewa na Mungu “kabisa.” (Isaya 55:7) Mwovu akitubu na ‘kuacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki; dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake.’—Ezekieli 33:14-16.
Paulo aliandika kwamba “Mungu si asiye mwadilifu ili asahau kazi yenu na upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake.” (Waebrania 6:10) Basi, Yehova atawathawabisha wale ambao yeye awakumbuka kwa mema. Yobu mwaminifu alisali hivi: “Laiti ungenificha kuzimuni [kaburi la kawaida la wanadamu wote], . . . na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!”—Ayubu 14:13.
Kwa kutofautisha, Mungu atashughulikia mwovu asiyetubu kupatana na maneno ambayo Yeye alimwambia Musa: ‘Nitamfuta katika kitabu changu.’ (Kutoka 32:33) Ndiyo, Mungu atawasahau waovu milele.
Hakimu wa Mwisho
Mungu ndiye Hakimu wa mwisho wa historia. (Mwanzo 18:25; Isaya 14:24, 27; 46:9-11; 55:11) Kulingana na hukumu yake bora, hatasahau ukatili mwingi ambao wanadamu wametendwa. Katika siku ya hasira yake yenye uadilifu, atawahukumu watu wote na mashirika yote yenye hatia.—Ufunuo, sura ya 18 na 19.
Miongoni mwa hao kutakuwamo mfumo wa ulimwengu wa dini isiyo ya kweli, ambao Maandiko yameupa jina la ufananisho “Babiloni Mkubwa.” Imeandikwa hivi juu yake: “Dhambi zake zimetungamana pamoja hadi mbinguni, na Mungu amekumbuka matendo yake yasiyo ya haki.”—Ufunuo 18:2, 5.
Dini hizi zilitakikana zifundishe wafuasi wake kufanya yaliyo mema lakini zilishindwa. Hivyo, Neno la Mungu lasema hivi kuhusu dini yote ya kilimwengu: “Katika yeye ilipatikana damu ya manabii na ya watakatifu na ya wote wale ambao wamechinjwa juu ya dunia.” (Ufunuo 18:24) Kwa sababu ya kushindwa kuagiza wafuasi wao wapende watu na wanadini wenzao, dini hizo zina hatia ya damu.
Ulimwengu Mpya U Karibu!
Siku ambayo maovu yataondolewa i karibu. (Sefania 2:1-3; Mathayo 24:3, 7-14) Baada ya wakati huo, kutakuwa na wakati ambapo hakutakuwapo tena ‘ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu’ kwa wakazi wenye furaha wa dunia. (Ufunuo 21:3-5) Ukatili na mauaji ya kikatili hayatatukia tena kwa sababu utawala wa dunia hii utachukuliwa kutoka kwa wanadamu na kupewa Ufalme wa kimbingu wa Mungu utakaokuwa mikononi mwa “Mfalme wa Amani,” Yesu Kristo.—Isaya 9:6, 7; Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10.
Wakati huo unabii ulio katika Zaburi 46:9 utatimizwa kabisa: “[Mungu] avikomesha vita hata mwisho wa dunia.” Amani hiyo itadumu milele kwa sababu, kama Isaya 2:4 linavyotabiri, “taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” Hivyo Zaburi 37:11 inatabiri: “Wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.” Ndiyo, ndipo itakaposemwa kwamba “dunia yote inastarehe na kutulia; hata huanzilisha kuimba.”—Isaya 14:7.
Yote haya yamaanisha kwamba ulimwengu mpya wenye uadilifu u karibu. Na katika ulimwengu huo mpya, chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu wa kimbingu, tukio jingine zuri ajabu litatukia—ufufuo wa wafu! Neno la Mungu lahakikisha hivi: “Kutakuwa na ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu pia.”—Matendo 24:15.
Alipokuwa duniani, Yesu alidhihirisha jambo hilo kwa kuwafufua watu. Kwa mfano, alipomfufua msichana mmoja, masimulizi hayo yanasema: “Na mara yule mwanamwali akainuka akaanza kutembea . . . Na mara moja [watazamaji] wakapigwa na bumbuazi ya upeo wa shangwe kubwa.” (Marko 5:42) Katika ufufuo wale waliouawa katika ukatili uliofanywa na vilevile wengine ambao walikufa zamani watainuliwa kutoka kwa wafu na kupewa fursa ya kuishi milele katika dunia paradiso. (Luka 23:43) Na baada ya muda “mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.”—Isaya 65:17.
Ni jambo la hekima kupata ujuzi sahihi wa Neno la Mungu, Biblia, na kufanya mapenzi yake. Ndipo Mungu atakapokukumbuka kwa mema wakati ambapo atasuluhisha kwa umilele tatizo la ukatili na kurudisha hai wanadamu walioathiriwa. Yesu alisema: “Hii yamaanisha uhai udumuo milele, wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.”—Yohana 17:3.
-