-
Uasilishaji—Kwa Nini na Jinsi Gani?Amkeni!—1996 | Mei 8
-
-
Uasilishaji—Kwa Nini na Jinsi Gani?
KWA nini idadi ya watoto walioasilishwa katika Uingereza imeshuka kwa njia ya kutazamisha katika miaka 20 iliyopita? Sababu mbili zimedokezwa—kupatikana kwa utoaji-mimba wa kihalali na ukubali unaoongezeka wa mama kumlea mtoto wake bila mume. Kuwa familia ya mzazi mmoja sasa kwaonwa kuwa tatizo linaloweza kukabiliwa kwa mafanikio katika jamii ya kisasa.
Hata hivyo, zaidi tu ya miaka 100 iliyopita mambo yalikuwa tofauti. Wakati Polly, mama ya Edgar Wallace, mwandikaji Mwingereza wa riwaya za uhalifu, alipotungwa mimba na mwana wa mwajiri wake, alienda zake na kuzaa kisiri. Edgar alikuwa na umri wa siku tisa wakati mkunga alipanga atunzwe na mke wa George Freeman, mpagazi kwenye soko la samaki la Billingsgate la London. Akina Freeman tayari walikuwa na watoto wao wenyewe kumi, naye Edgar akakua akiitwa Dick Freeman. Polly alitoa malipo ya kawaida ya kusaidia kumtegemeza mtoto wake, na baba yake hakupata kujua kamwe kuhusu kuwapo kwa mwana wake.
Leo wakati watoto hawatakikani, mamlaka za serikali mara nyingi huchukua daraka la kuwatunza. Watoto wengi hutunzwa na mamlaka za serikali kwa sababu wanahitaji ulinzi kutokana na kutendwa vibaya au kwa sababu wana ulemavu wa kimwili au kiakili. Wale waliofanywa mayatima kwa sababu ya maogofyo ya vita na watoto wanaotokea kwa sababu ya ulalwaji kinguvu huongezeka daima kwa watoto wanaohitaji sana shauku na ulinzi wa kimzazi—katika neno moja, uasilishaji.
Kuasilisha au Kutoasilisha?
Kumwasilisha mtoto si rahisi kamwe, na si jambo la hekima kamwe kufanya uamuzi wa ghafula unapotafakari jambo hilo. Ikiwa mtoto wako amekufa, huenda likawa jambo jema zaidi kungoja hadi mshtuko au huzuni iishe kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu kuasilisha. Hilo ni kweli pia kwa mume na mke wanaoambiwa kwamba hawawezi kuzaa.
Kila mtoto hurithi tabia za kipekee za kijeni. Wazazi mara nyingi hushangazwa na mielekeo ya watoto wao wenyewe, lakini ni vigumu kupima uwezo wa mtoto wa kiakili na kihisia-moyo ikiwa wazazi wake hawajulikani.
Je, unaweka thamani ya juu kwenye matimizo ya kielimu? Ikiwa ndivyo, utahisije ikiwa mtoto unayemwasilisha hafikii matarajio yako? Je, utaona mtoto aliye punguani au mlemavu kimwili kuwa tatizo ambalo unaweza kulikabili?
Wafanyakazi waliozoezwa kwenye ofisi za uasilishaji watoto au wafanyakazi wa kijamii wa serikali watakuuliza maswali kama hayo kabla hujafanya uamuzi wa mwisho. Hangaiko lao la kwanza lazima liwe kwa usalama na furaha ya huyo mtoto.
Ukiamua Kuasilisha . . .
Kila nchi ina sheria zayo na maagizo yayo yenyewe ya uasilishaji ambayo yapaswa kuchunguzwa. Katika Uingereza kuna mamia ya mashirika ya uasilishaji, nayo kwa kawaida hushirikiana na mamlaka za serikali za mahali. Mashirika yote yana sheria zayo yenyewe.
Zilizo mashuhuri hasa katika Uingereza ni tafrija za uasilishaji, ambapo idadi kadhaa ya wanaotazamiwa kuwa wazazi wanaweza kuchangamana na watoto wanaopatikana kwa ajili ya kuasilishwa, bila mkazo wowote wa kihisia-moyo ambao huwa katika kukutana na mtoto mmoja-mmoja. Hali hiyo iliyotulia hufanya iwe rahisi kwa wanaotazamiwa kuwa wazazi kukataa mtoto fulani nalo hufanya isiwe rahisi kwa watoto kutamauka, kwa kuwa hakuna mtoto fulani hususa ambaye hutengwa kuelekezewa fikira.
Kwa kawaida viwango vya mwisho vya umri huwekwa kwa wale wanaoasilisha, labda umri wa miaka 35 au 40 hivi—ingawa hili mara nyingi hutumika kwa kuasilisha vitoto, sanasana si watoto wenye umri mkubwa zaidi. Mashirika ya uasilishaji husema kwamba kiwango cha mwisho cha umri hufikiria pia muda wa kuishi unaotarajiwa wa wanaotazamiwa kuwa wazazi. Hata hivyo, wanatambua kwamba uzoefu huja na umri.
Miaka mingi iliyopita uasilishaji ulipangiwa mume na mke tu. Leo, waseja wanaweza kutoa maombi na kufanikiwa kuasilisha watoto fulani. Pia, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa na ulemavu si lazima ziwe sababu za wanaotazamiwa kuwa wazazi kukataliwa. Swali la msingi ni, Mpango huo utamwandalia mtoto nini?
Hata wakati taratibu za uasilishaji zinapomalizwa hatimaye, huenda wazazi wakachunguzwa ili kuhakikisha kwamba mambo yanaenda sawasawa.
Kutoka Jamii Nyingine?
Miaka 30 iliyopita ilikuwa vigumu kwa watoto weusi katika Uingereza kuchukuliwa na familia za weusi, tokeo likiwa kwamba wengi walienda kwa wazazi weupe. Tangu 1989 imekuwa sera ya kitaifa katika Uingereza kuweka watoto kwa wazazi-walezi walio na malezi yaleyale ya kikabila. Inahisiwa kwamba kwa njia hii mtoto atajipatanisha kwa utayari zaidi na jamii na utamaduni wake. Hata hivyo, hilo liliongoza kwenye hali zenye kupingana.
Hivi majuzi The Sunday Times liliripoti kwamba wazazi fulani weupe “wamejiainisha upya kuwa ‘weusi’” ili kuwawezesha kumwasilisha mtoto mweusi. Ni jambo la kawaida kwa wazazi weupe kutunza mtoto mweusi, jambo linalomaanisha wanamtunza kwa muda tu. Lakini baadaye wakinyimwa haki ya kumwasilisha huyo mtoto daima, tokeo ni hali mbaya ya kihisia-moyo kwa mtoto na wazazi.
Mume na mke kutoka Scotland, ambao walitunza watoto wawili Wahindi kwa miaka sita, hivi majuzi walikabili tatizo linalofanana na hilo la uasilishaji wa jamii mchanganyiko. Mahakama iliruhusu uasilishaji kwa kufahamu kwamba wazazi hao “watumie jitihada zao bora zaidi kuhakikisha kwamba hao watoto watajulishwa utambulisho wao [wa kikabila] na kulelewa wakiwa na uelewevu wa vyanzo vyao vya kikabila na desturi,” laripoti The Times. Katika kisa hiki wazazi-walezi walikuwa tayari wakifanya hivyo. Watoto hao walikuwa wakifundishwa Kipunjabi, na nyakati fulani walikuwa wakivishwa mavazi ya kienyeji.
Wengi watakubaliana na maoni ya msemaji mwanamke wa huduma za kijamii wa Uingereza ambaye alisema kwamba uasilishaji wa jamii mchanganyiko wapaswa kuruhusiwa kwa uhuru zaidi. “Twaishi katika jamii ya tamaduni nyingi,” yeye akasema, “na kutunza mtoto asiye wako na uasilishaji wapaswa kuonyesha hilo.”
Kutoka Ng’ambo?
Uasilishaji wa watoto wa kutoka nchi za kigeni ni ‘biashara inayositawi,’ kulingana na gazeti la habari The Independent. Ingawa ripoti zinaonyesha kwamba shughuli fulani huenda zisiwe halali, Ulaya Mashariki ndiyo chanzo kikuu cha ugavi kwa Uingereza.
Kwa kielelezo, baadhi ya watoto waliozaliwa kwa sababu ya ulalwaji kinguvu wakati wa kuvunjika kwa iliyokuwa Yugoslavia wameachwa. Inadaiwa kwamba wengine wangetolewa kama si mwingilio wa “wakala wa watoto,” ambaye aliahidi uasilishaji wa mtoto ikiwa alizaliwa baada ya miezi tisa. Hata hivyo, serikali za nchi za Magharibi, zinahangaikia malipo yanayofanywa ili kupata uasilishaji huu.
Kisababishi cha hangaiko kuu huhusiana na madai ya udanganyaji wa hati unaofanywa na madaktari wakati wa watoto kuzaliwa. Gazeti la habari The European liliripoti madai kwamba akina mama fulani katika Ukrainia waliambiwa kwamba vitoto vyao vilizaliwa vikiwa vimekufa. Ilidaiwa pia kwamba vitoto hivi viliuzwa hatimaye. Akina mama wengine huenda walikuwa wamejulishwa kwamba watoto wao walikuwa mapunguani. Chini ya msongo kama huo, akina mama wenye wasiwasi wanahimizwa kwa urahisi kutia sahihi watoto wao waasilishwe. Hata hivyo watoto wengine huenda hawakufika kwenye makao ya kutunzia watoto ambapo walikuwa wakipelekwa badala ya hivyo huenda waliishia katika nchi za kigeni.
Chuki hutokea katika nchi zinazositawi. Hizo hudai kwamba Magharibi yenye utajiri yapaswa kusaidia familia za kienyeji kutunza watoto wazo katika mazingira ya nyumbani badala ya kuwachukua kwa ajili ya kuwaasilisha katika utamaduni wa kigeni.
Nchi za Magharibi lazima zifahamu pia desturi ya kale sana ya familia zilizoenea, ambazo ndizo utegemezo wa jamii katika tamaduni nyingi. Kwa kawaida mtoto hatanyimwa utunzi anapoishi katika vikundi vya kikabila, hata wazazi wake wakifa. Kando na washiriki wa karibu wa familia, kama vile wazazi-wakuu, familia iliyoenea ya shangazi na wajomba zitamwona huyo mtoto kuwa wazo, na toleo lolote la uasilishaji kutoka nje laweza kueleweka vibaya na kuonwa kuwa mwingilio usiokubaliwa.a
Kupanga uasilishaji si rahisi, na hata wakati ambapo taratibu hiyo imemalizwa, kazi ngumu inahitajika ili kuufanikisha. Lakini kama tutakavyoona, pia kuna shangwe nyingi.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mazungumzo kamili ya zoea la kupatia washiriki wengine wa familia watoto, ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1988, kurasa 28-30, lililotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Sanduku katika ukurasa wa5]
Je, Mwana Wangu Atanitafuta?
WAZAZI wangu walitalikiana nilipokuwa na umri wa miaka 11. Nilitamani sana upendo. Nilipokuwa chuoni, nilijihusisha katika uhusiano wa kimahaba; ilikuwa njia yangu ya kupata shauku. Kisha, kwa fadhaiko, nikapata kwamba nilikuwa mja-mzito. Lilikuwa upuuzi sana. Mwanafunzi mwenzangu nami tulikuwa wachanga sana. Sikuwa nimepata kutumia dawa za kulevya, alkoholi, au tumbaku, lakini mvulana-rafiki wangu alikuwa ameharibiwa sana kutokana na siku alizokuwa akitumia LSD.
Nilishauriwa nitoe mimba, lakini baba yangu akanihimiza nisifanye hivyo. Sikutaka kuwa mja-mzito, lakini pia sikutaka kuharibu uhai. Mwana wangu alipozaliwa 1978, niliamua kutoweka jina la baba yake katika cheti chake cha kuzaliwa ili kuhakikisha kwamba baba yake hangeweza kumfikia. Kwa hakika, nilikubali mtoto huyo aasilishwe tangu kuzaliwa kwake; kwa hiyo alichukuliwa mara moja na kuwekwa kwa utunzi wa muda. Hata sikumwona. Kisha nikabadili mawazo yangu. Nilimtoa mtoto wangu kwenye utunzi na kujaribu sana kumlea peke yangu. Lakini sikuweza, kidogo nipate tatizo la kiakili.
Mwana wangu alikuwa na umri wa miezi sita hivi wakati agizo la uasilishaji lilipokubaliwa nikahitajiwa kumwacha achukuliwe. Nakumbuka nikihisi kana kwamba mtu fulani alikuwa amenidunga kisu. Nilikufa kihisia-moyo. Ni tangu nipate ushauri wa kitaalamu kwa miaka miwili iliyopita ndipo nimeweza kujenga mahusiano yenye maana. Singeweza kuomboleza—mwana wangu hakuwa amekufa. Lakini singeweza kumfikiria—nilikataa kujiruhusu kufanya hivyo. Ilikuwa vibaya mno.
Linaloumiza sana ni kusikia watu wakisema: “Ukimwacha mtoto wako aasilishwe, humpendi mtoto wako.” Lakini hilo halikuwa kweli katika kisa changu! Ilikuwa kwa sababu nilimpenda mwana wangu kwamba nilimwacha achukuliwe! Hadi dakika ya mwisho, nilikuwa nikijiuliza: ‘Nitafanya nini jamani? Naweza kufanya nini?’ Hakukuwa na njia ya badala. Nilijua kwamba singeweza kushinda hili tatizo na kwamba kitoto changu kingeteseka ikiwa ningejaribu kukaa nacho.
Katika Uingereza, jamii sasa yakubali familia za mzazi mmoja—lakini si wakati nilipozaa. Laiti ningaliweza kumlea mwana wangu ifaavyo. Ushauri ambao nimekuwa nikipata hivi majuzi nafikiri ungalisaidia, lakini ni kuchelewa mno sasa. Je, mwana wangu yuko hai bado? Amekua na kuwa mvulana wa aina gani? Wanapofikia umri wa miaka 18 watoto walioasilishwa huruhusiwa kisheria kutafuta wazazi wao. Mara nyingi mimi hujiuliza kama mwana wangu atanitafuta.—Imechangwa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Tulifanikiwa
TUKIWA na wavulana wetu wawili matineja, tulikuwa familia ya Waingereza iliyoridhika na iliyoungana. Wazo la kuwa na binti—wa jamii tofauti—halikuwa jambo lililotujia akilini. Kisha Cathy akaja katika maisha zetu. Cathy alizaliwa London, Uingereza. Alilelewa akiwa Mkatoliki wa Kiroma, lakini akiwa mtoto mchanga, alihudhuria mikutano michache pamoja na mama yake kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, alipokuwa na umri wa miaka 10, alipelekwa katika makao ya kutunzia watoto.
Ingawa mambo yalikuwa magumu kwake huko, alifaulu kuhudhuria mikutano peke yake kwenye Jumba la Ufalme, ambapo tulikutana naye. Cathy alikuwa msichana mwenye kufikiri. Mke wangu nami tulipomtembelea kwenye makao ya kutunzia watoto, tuligundua kwamba ukuta kando ya kitanda chake ulikuwa umefunikwa kwa picha za wanyama na mandhari za mashambani, tofauti na vibandiko vya watu mashuhuri wa muziki ambavyo wale wasichana wengine walikuwa wamebandika.
Wakati fulani baadaye Cathy alilazimika kutokea mbele ya halmashauri ya ukaguzi, ambayo ilimuuliza ikiwa angependa kuondoka kwenye makao hayo na kuishi pamoja na familia. “Ni pamoja na familia ya Mashahidi wa Yehova tu!” akajibu. Cathy alipotuambia kuhusu hilo na alichokuwa amesema, hilo likatupatia jambo la kufikiria. Tulikuwa na chumba cha ziada. Je, tungeweza kuchukua daraka hilo? Tukiwa familia, tulilizungumzia na kusali kulihusu. Ilikuwa baadaye sana ambapo tuligundua kwamba mfikio huu—kumuuliza mtoto maoni—ulikuwa jaribio jipya kwa upande wa huduma za kijamii, jaribio lililokuwa likithibitishwa.
Huduma za kijamii zilichunguza hali yetu ya maisha kutoka kwa polisi na daktari wetu na kupata marejezo ya kibinafsi. Upesi mkataba ukafanywa. Tukaambiwa kwamba tungempata Cathy kwa kipindi cha jaribio na kwamba tungemrudisha ikiwa hatukumpenda! Hilo lilituogofya, nasi tulikuwa thabiti kabisa katika kusema kwamba hatungefanya hivyo kamwe. Cathy alikuwa na umri wa miaka 13 tulipomchukua kirasmi nyumbani kwetu.
Kile kifungo cha kipekee cha upendo kati yetu sote huendelea kuimarika. Cathy sasa ni painia wa kawaida (mweneza-evanjeli wa wakati wote) katika kutaniko la Kifaransa la Mashahidi wa Yehova katika kaskazini mwa London. Mwaka alioondoka nyumbani kwenda kupainia, alituandikia barua ndogo yenye kugusa moyo: “Kuna msemo usemao ‘huwezi kuchagua familia yako.’ Hata hivyo, ningependa kuwashukuru kutoka moyoni kwa kunichagua.”
Tunashukuru sana kwamba Cathy alijiunga nasi. Kumfanya sehemu ya familia yetu kuliboresha maisha zetu. Tulifanikiwa!—Imechangwa.
-
-
Uasilishaji—Napaswa Kuuonaje?Amkeni!—1996 | Mei 8
-
-
Uasilishaji—Napaswa Kuuonaje?
NI DHAHIRI kwamba matatizo yanaweza kuzuka ikiwa wazazi-walezi wanatalikiana au mwenzi mmoja anakufa. Lakini huenda ni mtoto aliyeasilishwa ambaye mara nyingi huhisi mkazo mwingi zaidi. Kwa nini?
Wengi wetu tunawajua wazazi wetu wa kiasili. Hata kama walikufa tulipokuwa wachanga, tuna kumbukumbu, au labda picha, za kukamilisha muunganisho. Ingawa hivyo, namna gani juu ya mtoto ambaye alipelekwa akaasilishwe mara tu baada ya kuzaliwa? Shirika la uasilishaji huweka habari kumhusu mama, lakini habari hiyo mara nyingi haitolewi hadi mtoto anapokuwa na umri wa kutosha. Katika visa vingine, mama husajili jina lake mwenyewe kwenye cheti cha kuzaliwa lakini huacha lile la baba. Vitoto fulani ni vipatikanwaji—vilivyopatwa baada ya wazazi wavyo wasiojulikana kuviacha. Watoto katika hali hizi zote hukosa misingi ya kiasili—huenda wakahisi kuwa wameondoshwa kutoka vyanzo au asili yao.
Ni Imara Kadiri Gani?
Miti huhitaji mfumo mzuri wa mizizi ili usimame imara. Chipukizi jipya lililopandikizwa kwenye shina lililokomaa huenda likasitawi vyema, lakini huenda likanyauka pia na kukosa kutokeza matunda. Vivyohivyo, ingawa huenda wazazi-walezi wakaandaa utunzi wote na ujitoaji wenye upendo iwezekanavyo, watoto fulani hawaponi kamwe mshtuko wa kuondoshwa kutoka vyanzo vyao.
Fikiria kisa cha Kate.a Akizaliwa na wazazi kutoka West Indies, akiwa kitoto Kate aliasilishwa na mume na mke weupe wenye upendo, lakini hakuweza kujipatanisha na mazingira yake mapya. Alipokuwa na umri wa miaka 16, aliondoka nyumbani na kutorudi tena kamwe. Kufikia wakati huo uchungu ulikuwa umegeuka kuwa chuki isiyosababu. “Kwa nini mama yangu alinipa kwenu?” akataka kujua. Kwa kuhuzunisha, familia hii ilishindwa kuweza tatizo hilo.
Mervyn aliwekwa katika utunzi wa mamlaka ya mahali alipoishi baada ya kuzaliwa tu na kisha kwa wazazi-walezi. Alipokuwa na umri wa miezi tisa, aliasilishwa. Malezi yake ya mwanzoni yasiyo salama, pamoja na chuki yenye kuwaka kwa kuwa wa jamii iliyochanganyika, ilisitawi na kuwa mtazamo wa uasi ukimletea taabu nyingi na huzuni yenye kina kwa wazazi-walezi wake, ambao walimfanyia mengi sana. “Ikiwa mtu yeyote angeniuliza shauri kuhusu uasilishaji,” mama yake akasema, “sasa ningesema, ‘Lifikirie jambo hilo kwa uangalifu.’”
Kinyume na hilo, fikiria ono la Robert na Sylvia. Walikuwa na mwana mmoja na hawakuweza kupata watoto zaidi. “Je, mmepata kufikiria juu ya kuasilisha mtoto wa taifa jingine?” waliulizwa. Upesi walichukua Mak-Chai, kitoto kisichana chenye umri wa miezi tisa kutoka Hong Kong ili kukiasilisha. “Mara nyingi mimi hujiuliza ni kwa nini niliachwa,” asema Mak-Chai, “na ikiwa nina ndugu au dada wowote. Lakini nafikiri niko karibu zaidi na mama na baba-mlezi wangu kuliko watoto wengi wa kiasili kwa wazazi wao. Ikiwa ningewajua wazazi wangu wa kiasili, hilo halingetokeza tofauti yoyote, isipokuwa kwamba labda, ningeweza kufahamu tabia zangu chache vyema zaidi.” Je, wazazi wake walezi wanapendekeza uasilishaji? “Ndiyo,” wao wasema, “kwa sababu kwetu limekuwa ono zuri ajabu!”
Sababu za Kutahadhari
Graham na Ruth waliasilisha watoto wawili walipokuwa vitoto, mvulana na msichana, ili kuwachangamanisha pamoja na mwana na binti yao. Watoto wote wanne walilelewa wakiwa familia moja iliyoungana katika mazingira yenye furaha. “Watoto wetu wote waliondoka nyumbani miaka mingi iliyopita na kuishi maisha ya kujitegemea. Sisi hudumisha mawasiliano ya kawaida na twawapenda wote,” asema Ruth. Lakini kwa kuhuzunisha, watoto wote wawili wa kuasilishwa walikuwa na matatizo mazito. Kwa nini?
“Daktari wetu alituambia kwamba mazingira ya mtoto ni jambo la maana sana,” asema Graham, ambaye sasa ahisi kwamba vitabia vilivyorithiwa ni kisababishi kikuu. Yeye aongeza: “Pia, namna gani afya ya mama alipokuwa mja-mzito? Sasa twajua kwamba dawa za kulevya, vileo, na tumbaku, zaweza kuathiri mtoto asiyezaliwa bado. Napendekeza uchunguzi mkali ufanywe kwa wazazi wote, na hata wazazi-wakuu ikiwezekana, kabla ya kuasilisha.”
Mama ya Peter aliolewa tena, na Peter akatendwa vibaya na baba yake wa kambo kimwili na kiakili. Alipokuwa na umri wa miaka mitatu, akapelekwa akaasilishwe. “Niliwakataa wazazi-walezi wangu mara tu nilipotoka nje ya mahakama,” akasema Peter. Yeye akaongeza: “Niliharibu kila kitu kilichokuwa karibu nami. Nilipolala, nilipata ndoto zenye kutisha. Nikitazama nyuma sasa, naweza kuona jinsi nilivyosumbuka. Baada ya wazazi-walezi wangu kutalikiana pia, mambo yakawa mabaya hata zaidi kwangu—dawa za kulevya, kuiba, kuharibu vitu, karamu za ukosefu wa adili za kila siku.
“Nilipokuwa na umri wa miaka 27, sikuweza kuona sababu ya kuendelea kuishi nikafikiria kujiua kimakusudi. Kisha siku moja mtu nisiyemjua akanipa trakti ya Biblia ambayo ilitaarifu kwamba karibuni dunia hii itakuwa paradiso. Ujumbe huo ulinifurahisha. Ulisikika kuwa na kweli. Nilianza kusoma na kujifunza Biblia na kuanza kufanya mabadiliko katika maisha na tabia yangu, lakini mara kwa mara niliangukia njia zangu za kale. Baada ya kitia-moyo kingi na ushirika wa Kikristo wenye msaada, sasa nahisi nikiwa na furaha zaidi na usalama katika kumtumikia Mungu zaidi kuliko vile nilivyoweza kuwazia miaka michache iliyopita. Nimeweza pia kuamsha tena uhusiano wenye shauku pamoja na mama yangu, jambo ambalo ni lenye kufurahisha.”
Kukabili Uhalisi
Inapohusu kuasilisha mtoto asiye wako, hisia-moyo huwa nyingi mno. Upendo mwingi mno na shukrani zinaonyeshwa na vilevile uchungu na ukosefu wa shukrani. Kwa kielelezo, Edgar Wallace, hakumsamehe kamwe mama yake kwa kumwacha, njia ambayo yeye alipima matendo yake. Mama yake alienda kumwona katika mwaka wake wa mwisho wa uhai, akiomba kwa kusita-sita msaada wa kifedha, lakini Edgar, ingawa alikuwa tajiri sana wakati huo, alikataa waziwazi kumsaidia mamake. Muda mfupi baadaye, alipopata habari kwamba mama yake angalizikwa katika kaburi la watu maskini ikiwa si kwa fadhili za marafiki ambao walilipia maziko yake, Edgar alighairi sana ukosefu wake wa huruma.
Ni lazima watu wanaofikiria uasilishaji watoto wasio wao wajitayarishe kukabili kihalisi matatizo na magumu ambayo huenda yakazuka. Watoto hawawi wenye shukrani kila wakati kwa kile wazazi wao—walezi au wa kiasili—wanachowafanyia, hata katika hali bora kabisa. Kwa hakika, Biblia husema juu ya watu mmoja-mmoja katika siku yetu kuwa “wasio na shauku ya asili” na “wasio na shukrani” na “wasio waaminifu-washikamanifu.”—2 Timotheo 3:1-5, New World Translation.
Kwa upande ule mwingine, kufungua nyumba yako—na moyo wako—kwa mtoto anayehitaji wazazi kwaweza kuwa jambo bora na lenye kuthawabisha. Kwa mfano, Cathy, anashukuru sana wazazi-walezi wake kwa kumwandalia nyumba ya Kikristo na kutunza mahitaji yake ya kimwili na ya kiroho.—Ona sanduku “Tulifanikiwa,” ukurasa 8.
Wanapofafanua jinsi wanavyohisi kuhusu wana na mabinti wao wa kuasilisha, wazazi wa watoto kama hao huenda wakakumbuka maneno ya mtunga-zaburi: “Watoto ni zawadi kutoka kwa Bwana; wao ni baraka kwelikweli.”—Zaburi 127:3, Today’s English Version.
-