Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mifano Miwili Kuhusu Mashamba ya Mizabibu
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Wakulima wakimuua mwana wa mmiliki wa shamba la mizabibu

      SURA YA 106

      Mifano Miwili Kuhusu Mashamba ya Mizabibu

      MATHAYO 21:28-46 MARKO 12:1-12 LUKA 20:9-19

      • MFANO KUHUSU WANA WAWILI

      • MFANO WA WAKULIMA WA SHAMBA LA MIZABIBU

      Akiwa hekaluni, Yesu ametoka kuwashangaza wakuu wa makuhani na wazee wa watu, ambao walikuwa wamemuuliza kuhusu mamlaka anayotumia kufanya mambo. Jibu la Yesu linawanyamazisha. Kisha anatoa mfano unaofunua jinsi walivyo kihalisi.

      Yesu anasimulia hivi: “Mtu fulani alikuwa na watoto wawili. Akamwendea wa kwanza, akamwambia, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Akamjibu, ‘Sitaenda,’ lakini baadaye akajuta na akaenda. Akamwendea wa pili na kumwambia jambo hilohilo. Naye akamjibu, ‘Nitaenda Baba,’ lakini hakwenda. Kati ya hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya baba yake?” (Mathayo 21:28-31) Jibu ni wazi—yule wa kwanza ndiye ambaye mwishowe alifanya mapenzi ya baba yake.

      Basi, Yesu anawaambia hivi wapinzani wake: “Kwa kweli ninawaambia wakusanya kodi na makahaba wanawatangulia ninyi kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Mwanzoni, wakusanya kodi na makahaba hawakutaka kumtumikia Mungu. Hata hivyo, kama yule mwana wa kwanza, baadaye walitubu na sasa wanamtumikia Mungu. Kinyume chake, viongozi wa kidini ni kama yule mwana wa pili, wanadai kwamba wanamtumikia Mungu lakini kwa kweli hawamtumikii. Yesu anasema hivi: “Yohana [Mbatizaji] alikuja kwenu katika njia ya uadilifu, lakini hamkumwamini. Hata hivyo, wakusanya kodi na makahaba walimwamini, nanyi, ijapokuwa mliona hilo, hamkujuta na kumwamini.”​—Mathayo 21:31, 32.

      Baada ya kutoa mfano huo, Yesu anasimulia mfano mwingine. Pindi hii Yesu anaonyesha kwamba kosa la viongozi wa kidini sio tu kukataa kumtumikia Mungu. Kwa kweli wao ni waovu. Yesu anasimulia hivi: “Mtu fulani alipanda shamba la mizabibu akalizungushia ua, akachimba shinikizo la divai, akajenga mnara, kisha akalikodisha kwa wakulima, naye akasafiri kwenda ng’ambo. Majira yalipofika akatuma mtumwa kwa wakulima ili achukue kutoka kwao baadhi ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wakamkamata, wakampiga na kumfukuza mikono mitupu. Akamtuma tena mtumwa mwingine kwao, na huyo wakampiga kichwani na kumwaibisha. Akamtuma mwingine, na huyo wakamuua, akawatuma wengine wengi, wakawapiga baadhi yao na kuwaua wengine.”—Marko 12:1-5.

      Je, wale wanaomsikiliza Yesu wataelewa mfano huo? Huenda wakakumbuka maneno haya ya shutuma yaliyosemwa na Isaya: “Shamba la mizabibu la Yehova wa majeshi ni nyumba ya Israeli; watu wa Yuda ndilo shamba alilolipenda sana. Aliendelea kutumaini haki itendwe, lakini tazama! kulikuwa na ukosefu wa haki.” (Isaya 5:7) Mfano wa Yesu unafanana na maneno hayo. Yehova ndiye anayemiliki shamba, nalo shamba la mizabibu ni taifa la Israeli, ambalo limezunguzishiwa ua na kulindwa na Sheria ya Mungu. Yehova aliwatuma manabii wawafundishe watu wake na kuwasaidia wazae matunda mazuri.

      Hata hivyo, “wakulima” waliwatendea vibaya na kuwaua “watumwa” waliotumwa kwao. Yesu anaeleza hivi: “[Mwenye shamba la mizabibu] alikuwa na mmoja zaidi, mwana wake mpendwa. Mwishowe akamtuma kwao akisema: ‘Watamheshimu mwanangu.’ Lakini wakulima wakaambiana, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, na urithi utakuwa wetu.’ Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua.”—Marko 12:6-8.

      Sasa Yesu anauliza: “Mwenye shamba la mizabibu atafanya nini?” (Marko 12:9) Viongozi wa kidini wanajibu: “Kwa sababu ni waovu, atawaangamiza kabisa na kulikodisha shamba la mizabibu kwa wakulima wengine, ambao watampa matunda yatakapoiva.”—Mathayo 21:41.

      Hivyo, bila kujua wanajihukumu wao wenyewe, kwa maana wao ni kati ya “wakulima” wa “shamba la mizabibu” la Yehova, taifa la Israeli. Matunda ambayo Yehova anatazamia kutoka kwa wakulima hao yanatia ndani kumwamini Mwana wake, yaani, Masihi. Yesu anawatazama moja kwa moja viongozi hao wa kidini na kusema: “Je, hamkusoma kamwe andiko hili: ‘Jiwe ambalo wajenzi walilikataa, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Hili limetoka kwa Yehova, na ni lenye kustaajabisha machoni petu’?” (Marko 12:10, 11) Kisha Yesu anakazia jambo kuu: “Ndiyo sababu ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa taifa linalozaa matunda yake.”—Mathayo 21:43.

      Waandishi na wakuu wa makuhani wanatambua kwamba “mfano aliosema uliwahusu.” (Luka 20:19) Kuliko wakati mwingine wowote, wanataka kumuua yule aliye na haki ya kuwa “mrithi.” Lakini wanauogopa umati, ambao unamwona Yesu kuwa nabii, basi hawajaribu kumuua wakati huo.

      • Wana wawili katika mfano wa Yesu wanafananisha nani?

      • Katika mfano wa pili ni nani wanaofananishwa na ‘mtu aliyemiliki shamba,’ “shamba la mizabibu,” “wakulima,” “watumwa,” na “mrithi”?

      • Ni nini kitakachowapata “wakulima” wakati ujao?

  • Mfalme Awaita Wale Walioalikwa Kwenye Karamu ya Ndoa
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Mfalme aagiza mtu asiye na mavazi ya ndoa atupwe nje ya karamu ya ndoa

      SURA YA 107

      Mfalme Awaita Wale Walioalikwa Kwenye Karamu ya Ndoa

      MATHAYO 22:1-14

      • MFANO WA KARAMU YA NDOA

      Huduma ya Yesu inapokaribia kwisha, anaendelea kutumia mifano ili kufunua uovu wa waandishi na wakuu wa makuhani. Basi, wanataka kumuua. (Luka 20:19) Lakini bado Yesu hajamaliza kufunua uovu wao. Anasimulia mfano mwingine.

      “Ufalme wa mbinguni ni kama mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya ndoa. Akawatuma watumwa wake wawaite wale walioalikwa kwenye karamu ya ndoa, lakini hawakutaka kuja.” (Mathayo 22:2, 3) Yesu anaanza mfano huo kwa kutaja “Ufalme wa mbinguni.” Basi, kwa hakika “mfalme” ni Yehova Mungu. Namna gani mwana wa mfalme na wale walioalikwa kwenye karamu ya ndoa? Pia, si vigumu kutambua kwamba mwana wa mfalme ni Mwana wa Yehova ambaye yuko hapo akisimulia mfano huo, na pia kuelewa kwamba wale walioalikwa ndio watakaokuwa pamoja na Mwana katika Ufalme wa mbinguni.

      Ni nani wanaoalikwa kwanza? Yesu na mitume wamekuwa wakiwahubiria nani kuhusu Ufalme? Wamewahubiria Wayahudi. (Mathayo 10:6, 7; 15:24) Taifa hilo lilikubali agano la Sheria mwaka wa 1513 K.W.K., na hivyo kupata nafasi ya kwanza ya kutokeza “ufalme wa makuhani.” (Kutoka 19:5-8) Lakini ni wakati gani hasa ambapo wangealikwa kwenye “karamu ya ndoa”? Inapatana na akili kwamba mwaliko huo ulitolewa mwaka wa 29 W.K., Yesu alipoanza kuhubiri kuhusu Ufalme wa mbinguni.

      Waisraeli wengi waliitikiaje mwaliko huo? Kama Yesu alivyosema, “hawakutaka kuja.” Idadi kubwa ya viongozi wa kidini na watu hawakukubali kwamba Yesu ndiye Masihi na Mfalme aliyechaguliwa na Mungu.

      Hata hivyo, Yesu anaonyesha kwamba Wayahudi wangepewa nafasi nyingine: “Tena [mfalme] akawatuma watumwa wengine, akasema, ‘Waambieni wale walioalikwa: “Tazameni! Nimetayarisha chakula changu cha mchana, ng’ombe dume wangu na wanyama waliononeshwa wamechinjwa, na vitu vyote viko tayari. Njooni kwenye karamu ya ndoa.”’ Lakini wakapuuza na kwenda zao, wengine kwenye mashamba yao, na wengine kwenye biashara zao; lakini wengine wakawakamata wale watumwa wakawatendea kwa dharau na kuwaua.” (Mathayo 22:4-6) Hilo linapatana na jambo ambalo lingetokea baada ya kutaniko la Kikristo kuanzishwa. Wakati huo bado Wayahudi walikuwa na nafasi ya kuwa katika Ufalme. Hata hivyo, wengi walikataa mwaliko huo hata wakawatendea vibaya ‘watumwa wa mfalme.’​—Matendo 4:13-18; 7:54, 58.

      Taifa hilo litapatwa na matokeo gani? Yesu anasimulia hivi: “Mfalme akakasirika sana, akatuma majeshi yake yakawaue wauaji hao na kulichoma jiji lao.” (Mathayo 22: 7) Wayahudi walipatwa na jambo hilo mwaka wa 70 W.K. Waroma walipoharibu “jiji lao,” Yerusalemu.

      Wanapokataa mwaliko wa mfalme, je, inamaanisha kwamba hakuna watu wengine watakaoalikwa? Mfano wa Yesu hauonyeshi hivyo. Anaendelea kusema hivi: “Kisha [mfalme] akawaambia watumwa wake, ‘Karamu ya ndoa iko tayari, lakini walioalikwa hawakustahili. Kwa hiyo, nendeni kwenye barabara zinazotoka jijini, na kumwalika kwenye karamu ya ndoa mtu yeyote mtakayemwona.’ Basi watumwa wakaenda barabarani na kuwaalika wote waliowaona, waovu na wema; na chumba cha sherehe za harusi kikajaa wageni.”—Mathayo 22:8-10.

      Kwa kupatana na jambo hilo, baadaye mtume Petro angeanza kuwasaidia Watu wa Mataifa—watu ambao hawakuwa Wayahudi kwa kuzaliwa au kwa kugeuzwa imani—wawe Wakristo. Katika mwaka wa 36 W.K., ofisa wa jeshi Mroma, Kornelio na familia yake walipokea roho ya Mungu, na hivyo wakawa na tumaini la kuwa katika Ufalme wa Mbinguni ambao Yesu alitaja.—Matendo 10:1, 34-48.

      Yesu anaonyesha kwamba si wote wanaokuja kwenye karamu ambao mwishowe watakubalika mbele za “mfalme.” Anasema: “Mfalme alipoingia kuwakagua wageni, akamwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi la ndoa. Basi akamuuliza, ‘Mwenzangu, umeingiaje humu bila vazi la ndoa?’ Akakosa la kusema. Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu, kisha mmtupe nje gizani. Huko ndiko atalia na kusaga meno yake.’ Kwa maana kuna wengi walioalikwa, lakini waliochaguliwa ni wachache.”—Mathayo 22:11-14.

      Huenda viongozi wa kidini wanaomsikiliza Yesu wasielewe maana au matokeo ya mambo anayosema. Hata hivyo, wanakasirika na kuazimia hata zaidi kumuua mtu anayewaaibisha hivyo.

      • Katika mfano wa Yesu, “mfalme” ni nani, “mwanawe” ni nani, na ni nani walioalikwa kwanza kwenye karamu ya ndoa?

      • Ni wakati gani ambapo Wayahudi wanaalikwa tena, na baadaye ni nani wanaoalikwa?

      • Ni nini maana ya kwamba wengi waliitwa lakini ni wachache waliochaguliwa?

  • Yesu Apangua Njama za Kumtega
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Yesu akiwa ameshika sarafu ya kodi huku akijibu maswali ya Mafarisayo yenye hila

      SURA YA 108

      Yesu Apangua Njama za Kumtega

      MATHAYO 22:15-40 MARKO 12:13-34 LUKA 20:20-40

      • VITU VYA KAISARI KWA KAISARI

      • JE, KUTAKUWA NA NDOA KATIKA UFUFUO?

      • AMRI KUU ZAIDI

      Viongozi wa kidini ambao ni maadui za Yesu wamekasirika. Ametoka tu kusimulia mifano inayofunua uovu wao. Sasa Mafarisayo wanapanga njama ili kumnasa. Wanajaribu kumfanya aseme jambo litakalofanya wamkabidhi kwa gavana Mroma, basi wanawalipa baadhi ya wanafunzi wao ili wamtege.—Luka 6:7.

      Wanasema: “Mwalimu, tunajua wewe husema na kufundisha kwa usahihi na huna ubaguzi, bali unafundisha njia ya Mungu kupatana na kweli: Je, ni halali au si halali kwetu kumlipa Kaisari kodi?” (Luka 20:21, 22) Yesu hapumbazwi wanapomsifu-sifu, kwa maana wamejaa unafiki na hila moyoni. Akisema, ‘Hapana, si halali kulipa kodi,’ anaweza kushtakiwa kwa uchochezi dhidi ya Roma. Lakini akisema, ‘Ndiyo, lipeni kodi hiyo,’ watu waliochoshwa kuwa chini ya utawala wa Roma, wanaweza kumwelewa vibaya na kuanza kumshambulia. Basi anajibuje?

      Yesu anajibu hivi: “Kwa nini mnanijaribu, ninyi wanafiki? Nionyesheni sarafu ya kodi.” Wanaleta dinari, kisha anawauliza: “Sura hii na maandishi haya ni ya nani?” Wanajibu: “Ni ya Kaisari.” Kisha Yesu anatoa mwongozo huu thabiti: “Basi, mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, na Mungu vitu vya Mungu.”—Mathayo 22:18-21.

      Watu hao wanashangazwa na maneno ya Yesu. Wakiwa wamenyamazishwa baada ya Yesu kuwajibu kwa ustadi, wanaondoka. Lakini bado siku haijaisha, wala jitihada za kumnasa hazijakwisha. Mafarisayo wanapokosa kufanikiwa, viongozi wa kikundi kingine cha kidini wanamkaribia Yesu.

      Masadukayo, ambao husema hakuna ufufuo, wanauliza swali linalohusu ufufuo na desturi ya mtu kuoa mke wa ndugu yake aliyekufa. Wanauliza hivi: “Mwalimu, Musa alisema: ‘Mtu yeyote akifa bila kupata watoto, ndugu yake anapaswa kumwoa mke wake ili kumwinulia ndugu yake uzao.’ Basi kulikuwa na ndugu saba kati yetu. Wa kwanza akaoa kisha akafa, na kwa sababu hakuwa na watoto, akamwachia ndugu yake mke wake. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa pili na wa tatu, na kwa wote saba. Mwishowe, yule mwanamke akafa. Basi, katika ufufuo, atakuwa mke wa nani kati ya wale saba? Kwa maana aliolewa na wote.”—Mathayo 22:24-28.

      Akirejelea maandishi ya Musa, ambayo Masadukayo wanayakubali, Yesu anajibu hivi: “Ninyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko wala nguvu za Mungu. Kwa maana wanapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawaoi wala wanawake hawaolewi, bali wao ni kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamkusoma katika kitabu cha Musa, simulizi kuhusu kile kichaka cha miiba kwamba Mungu alimwambia: ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Mmekosea sana.” (Marko 12:24-27; Kutoka 3:1-6) Umati unashangazwa na jibu lake.

      Yesu amewanyamazisha Mafarisayo na Masadukayo, basi wapinzani hao wa kidini wanaungana kisha wanakuja kumjaribu tena. Mwandishi mmoja anauliza: “Mwalimu, ni amri gani iliyo kuu zaidi katika Sheria?”—Mathayo 22:36.

      Yesu anajibu: “Ya kwanza ni hii, ‘Sikilizeni, enyi Waisraeli, Yehova Mungu wetu ni Yehova mmoja, nawe lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.’ Ya pili ni hii, ‘Lazima umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ Hakuna amri nyingine iliyo kubwa kuliko amri hizi.”—Marko 12:29-31.

      Yule mwandishi anaposikia jibu hilo anasema: “Mwalimu, umesema vema kupatana na kweli, ‘Yeye ni Mmoja, na hakuna mwingine isipokuwa yeye’; na kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa uelewaji wote na kwa nguvu zote na pia mtu kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko matoleo yote mazima ya kuteketezwa na dhabihu.” Yesu anapoona kwamba mwandishi huyo amejibu kwa kutumia akili, anamwambia hivi: “Wewe huko mbali na Ufalme wa Mungu.”—Marko 12:32-34.

      Kwa siku tatu (Nisani 9, 10, na 11) Yesu amekuwa akifundisha hekaluni. Baadhi ya watu, kama vile mwandishi huyo, wamefurahia kumsikiliza. Lakini sivyo kwa viongozi wa kidini ambao sasa ‘hawathubutu tena kumuuliza swali.’

      • Mafarisayo wanafanya mpango gani ili kumtega Yesu, na matokeo yanakuwaje?

      • Masadukayo wanapojaribu kumnasa Yesu, anapanguaje njama yao?

      • Yesu anapojibu swali la mwandishi fulani, ni mambo gani anayokazia kuwa muhimu sana?

  • Awashutumu Wapinzani wa Kidini
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Yesu anafunua wapinzani wake wa kidini

      SURA YA 109

      Awashutumu Wapinzani wa Kidini

      MATHAYO 22:41–23:24 MARKO 12:35-40 LUKA 20:41-47

      • KRISTO NI MWANA WA NANI?

      • YESU AWAFUNUA WAPINZANI WANAFIKI

      Wapinzani wa kidini wanashindwa kumharibia sifa Yesu au kumnasa na kumkabidhi kwa Waroma. (Luka 20:20) Sasa wakiwa bado hekaluni Nisani 11, Yesu anawageukia na kuwaonyesha utambulisho wake halisi. Kwanza anawauliza: “Mna maoni gani kuhusu Kristo? Ni mwana wa nani?” (Mathayo 22:42) Ni wazi kwamba Kristo au Masihi, atatoka katika ukoo wa Daudi. Hivyo ndivyo wanavyojibu.—Mathayo 9:27; 12:23; Yohana 7:42.

      Yesu anauliza: “Basi, kwa nini Daudi akiongozwa na roho anamwita Bwana, akisema, ‘Yehova alimwambia Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kuume mpaka niwaweke maadui wako chini ya miguu yako”’? Basi ikiwa Daudi anamwita Bwana, anawezaje kuwa mwanawe?”—Mathayo 22:43-45.

      Mafarisayo wananyamaza, kwa kuwa wanatumaini kwamba mtu kutoka ukoo wa Daudi atawakomboa kutoka kwa utawala wa Roma. Lakini Yesu anatumia maneno ya Daudi katika Zaburi 110:1, 2, kuonyesha kwamba Masihi atakuwa zaidi ya mtawala wa kibinadamu. Yeye ndiye Bwana wa Daudi, na baada ya kukaa katika mkono wa kuume wa Mungu, atakuwa mtawala. Maneno ya Yesu yanawanyamazisha wapinzani wake.

      Wanafunzi na wengine wengi wamekuwa wakisikiliza. Sasa Yesu anazungumza nao, akiwaonya kuhusu waandishi na Mafarisayo. Watu hao “wamejiketisha kwenye kiti cha Musa” ili kufundisha Sheria ya Mungu. Yesu anawaambia hivi wasikilizaji wake: “Fanyeni mambo yote wanayowaambia, lakini msitende kama wao, kwa maana wao husema lakini hawatendi mambo wanayosema.”—Mathayo 23:2, 3.

      Kisha Yesu anatoa mifano kuhusu unafiki wao, akisema: “Wanapanua visanduku vyenye maandiko wanavyovaa kama ulinzi.” Baadhi ya Wayahudi walivaa kwenye paji la uso au mkononi visanduku hivyo vidogo vilivyokuwa na mafungu mafupi ya Sheria. Mafarisayo huongezea ukubwa wa visanduku vyao ili kujionyesha kwamba wana bidii ya kufuata Sheria. Pia, ‘wanarefusha pindo zenye nyuzi za mavazi yao.’ Waisraeli walipaswa kutengeneza pindo kwenye mavazi yao, lakini Mafarisayo wanahakikisha kwamba pindo zao ni ndefu sana. (Hesabu 15:38-40) Wanafanya mambo yote hayo “ili waonwe na watu.”—Mathayo 23:5.

      Hata wanafunzi wa Yesu wanaweza kuathiriwa na tamaa ya umashuhuri, hivyo anawashauri hivi: “Msiitwe Rabi, kwa maana Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Zaidi ya hayo, msimwite mtu yeyote baba yenu duniani, kwa maana Baba yenu ni mmoja, Yule aliye mbinguni. Wala msiitwe viongozi, kwa maana Kiongozi wenu ni mmoja, Kristo.” Hivyo basi, wanafunzi wanapaswa kujionaje na kutendaje? Yesu anawaambia: “Aliye mkuu zaidi kati yenu lazima awe mhudumu wenu. Yeyote anayejiinua atanyenyekezwa, na yeyote anayejinyenyekeza atainuliwa.”—Mathayo 23:8-12.

      Kisha Yesu anawatangazia ole waandishi na Mafarisayo wanafiki: “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu mnawafungia watu Ufalme wa mbinguni; kwa maana ninyi wenyewe hamwingii, na mnawazuia wale wanaotaka kuingia.”—Mathayo 23:13.

      Yesu anawashutumu Mafarisayo kwa sababu hawathamini mambo ya kiroho, kama inavyoonyeshwa na maamuzi yao yasiyo na msingi. Kwa mfano, wanasema: “Yeyote akiapa kwa hekalu, si kitu; lakini yeyote akiapa kwa dhahabu ya hekalu, yuko chini ya wajibu.” Hivyo wanaonyesha jinsi walivyo vipofu kimaadili, kwa maana wanakazia zaidi dhahabu ya hekalu kuliko thamani ya kiroho ya mahali pa kumwabudu Yehova. Nao ‘wamepuuza mambo mazito zaidi ya Sheria, yaani, haki, rehema, na uaminifu.’—Mathayo 23:16, 23; Luka 11:42.

      Yesu anawaita Mafarisayo hao “viongozi vipofu, ambao huchuja mbu lakini hummeza ngamia!” (Mathayo 23:24) Wanachuja mbu kutoka kwenye divai yao kwa sababu mdudu huyo si safi kisherehe. Lakini wanapopuuza mambo mazito ya Sheria ni kama wanammeza ngamia, ambaye pia ni mnyama asiye safi kisherehe, lakini mkubwa zaidi.—Mambo ya Walawi 11:4, 21-24.

      • Yesu anapowauliza Mafarisayo kuhusu maneno yaliyosemwa na Daudi katika Zaburi 110, kwa nini wanakaa kimya?

      • Kwa nini Mafarisayo wanavifanya visanduku vyao vya maandiko kuwa vikubwa na kurefusha pindo za mavazi yao?

      • Yesu anawapa wanafunzi wake ushauri gani?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki