-
Ukamilifu wa Ayubu—Kwa Sababu Gani Unastaajabisha Sana?Mnara wa Mlinzi—1986 | Machi 1
-
-
Ukamilifu wa Ayubu—Kwa Sababu Gani Unastaajabisha Sana?
“Mpaka nitakapokufa mimi sitaondoa ukamilifu kwangu mwenyewe!”—AYUBU 27:5, Biblia ya New World Translation.
1. Ayubu alikuwa nani, na tunajuaje kwamba yeye alikuwa mtu halisi?
AYUBU alikuwa mwanamume wa kutokeza katika historia. Hakuwa na utajiri mwingi tu wa vitu vya kimwili, bali pia aliheshimiwa kuwa mwamuzi na kiongozi mwenye huruma. Biblia inasema kwamba alikuja kuwa “mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.” (Ayubu 1:3; 29:12-25) Yeye, pamoja na Noa na Danieli, anajulikana sana kuwa mtu mwenye uadilifu mwingi. (Ezekieli 14:14, 20) Pia Biblia inamwonyesha Ayubu kuwa mfano unaopasa kufuatwa na Wakristo, hivyo ikionyesha kwamba yeye alikuwa mtu wa kweli katika historia.—Yakobo 5:11.
2. Tunaweza kukadiriaje ni wakati gani Ayubu alijaribiwa na Shetani?
2 Ayubu aliishi katika nchi ya Usi, katika ile sasa inayoitwa Uarabu. Ingawa hakuwa Mwisraeli, Ayubu alikuwa mwabudu wa Yehova, na Yehova alimweleza Shetani jambo hilo. Maneno ya Mungu kwamba “hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu” yanafunua kwamba hakukuwa na mtumishi mwingine wa Mungu mwenye kutokeza aliyekuwa akiishi wakati huo. (Ayubu 1:8) Hivyo, pasipo shaka kujaribiwa kwa Ayubu na Shetani kulitukia wakati binamu zake wenye uhusiano wa mbali naye, yaani Waisraeli, walipokuwa utumwani Misri—wakati fulani katika ile miaka iliyofuata kifo cha mshika-ukamilifu wa kutokeza Yusufu mwaka 1657 K.W.K.. na kabla Musa hajauanza mwendo wake wa ukamilifu.
3. Ni nani aliyeandika kitabu cha Ayubu, na kwa sababu gani aliweza kupata habari hizo?
3 Kwa wazi Musa ndiye aliyekiandika kitabu cha Ayubu. Angeweza kuwa alipataje habari za kujaribiwa kwa Ayubu? Basi, Musa alipokwisha kulazimika kuondoka Misri mwaka 1553 K.W.K. alikaa Midiani, nchi isiyokuwa mbali na nchi ya Uzi. (Kutoka 2:15-25; Matendo 7:23-30) Wakati huo, Ayubu alikuwa akiimalizia miaka 140 ya mwisho ya maisha yake aliyobarikiwa na Yehova. (Ayubu 42:16) Baadaye, wakati Waisraeli walipokuwa karibu na Usi kuelekea mwisho wa safari yao ya jangwani, Musa angeweza kuwa alisikia habari za miaka ya mwisho ya maisha na kifo cha Ayubu.
Maarifa ya Ayubu Yenye Kikomo
4. (a) chanzo cha maarifa ya Ayubu ya kumjua Yehova kilikuwa nini, na kwa sababu gani bila shaka yeye angekuwa amekuwa akiwasiliana na Abrahamu na wazao wa Isaka? (b) ayubu alipataje kuwa mtu mwenye ukamilifu wa kutokeza?
4 Ayubu alipojaribiwa, maarifa yake ya kumjua Mungu na makusudi yake yalikuwa yenye kikomo, kwa kuwa hakuna sehemu ya Biblia iliyokuwa imekwisha kuandikwa. Lakini, Ayubu bila shaka alijua mambo fulani juu ya shughuli za Yehova pamoja na Abrahamu, Isaka, Yakobo, na Yusufu. Hiyo ni kwa sababu kwa wazi Ayubu alikuwa mzazo wa Nahori ndugu ya Abrahamu, kupitia Usi mwana mzaliwa wa kwanza wa Nahori. Tena, ndugu yake Usi alikuwa Bethueli, aliyekuwa baba ya Rebeka mke wa Isaka na pia babu mkuu wa Yusufu. (Mwanzo 22:20-23) Bila shaka Ayubu alipata kuyahifadhi sana maarifa yo yote aliyokuwa nayo juu ya mawasiliano ya Yehova na Abrahamu na wazao wake, naye alitaka sana kumpendeza Yehova. Hivyo Ayubu akawa mtu wa ukamilifu wenye kutokeza, mtu asiye na lawama na mwenye kujitoa kabisa kwa Yehova.
5. Ni jambo gani hasa linalofanya ukamilifu wa Ayubu uwe wa kutokeza sana?
5 Muda mfupi baada ya kifo cha Yusufu katika Misri, ukamilifu wa Ayubu ukawa jambo la kubishaniwa kati ya Yehova Mungu na Shetani katika mbingu zisizoonekana. Hata hivyo Ayubu hakujua lo lote juu ya ubishi uliotegemea ukamilifu wake. Na hasa kutokujua sababu yake ya kutaabika ndiko kunakofanya ukamilifu wa Ayubu usiovunjika uwe wa kustaajabisha sana. Lakini, kwa faida ya watumishi wote wa Mungu baadaye Yehova alimwagiza Musa aandike mambo yote ya ubishi uliohusu ukamilifu wa Ayubu.
Suala la Ukamilifu wa Ayubu
6. (a) Kusanyiko moja katika mbingu lilifunuaje kuwako kwa suala fulani kati ya Mungu na Shetani? (b) Ni wakati gani suala hilo lilipoanza, nalo lilitia ndani nini?
6 Kitabu cha Ayubu kinalifungua pazia la mambo yasiyokuwa yanaonekana halafu tunapewa maono ya mkutano wa malaika waliokusanyika mbele za Yehova Mungu. Humo Yehova anamkumbusha Shetani, ambaye pia yupo, kwamba “hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.” (Ayubu 1:8) Kwa wazi, kuna suala fulani linalotia ndani ukamilifu wa Ayubu. Lakini si suala jipya. Suala hilo liligusiwa wakati Shetani alipogeuza Adamu na Hawa, wakamwacha Mungu, kwa njia hiyo akawa ni kama anasema: ‘Wewe nipe tu nafasi nami naweza kugeuza mtu ye yote asikutumikie.’—Mwanzo 3:1-6.
7. Shetani alilazimika kutoa madokezo gani juu ya ukamilifu wa Ayubu, na Shetani alimtolea Mungu mwito gani wa ushindani?
7 Sasa, wakati wa mkutano huu rasmi mbinguni, Shetani analazimika kutoa maelezo kuhusu ulio msingi wa ukamilifu wa Ayubu. “Je! huyo Ayubu yuamcha [Yehova] bure?” anauliza. “Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake. Na vitu wote alivyo navyo? . . . Lakini nyosha mkono wako sasa,” Shetani anatokeza mwito wa ushindani, “uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”—Ayubu 1:9-11.
8. (a) Yehova aliitikiaje mwito wa ushindani wa Shetani? (b) Shetani alimwangushia Ayubu dharuba gani kali kali?
8 Yehova anaukubali mwito wa ushindani unaotokezwa na Shetani. Yeye anautumaini kabisa ukamilifu wa Ayubu, akimjibu Shetani: “Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe.” (Ayubu 1:12) Shetani anampiga Ayubu haraka. Waseba wavamizi wanatoroka na ng’ombe 1,000 na punda-jike 500 wa Ayubu, wakiwaua watunzaji wao wote isipokuwa mmoja. Ndipo Shetani anapeleka moto kutoka mbinguni ukawale kondoo 7,000 wa Ayubu pamoja na watunzaji wao, wakiachilia mmoja tu. Halafu anavifanya vikosi vitatu vya Wakaldayo vitoroke vikiwa na ngamia 3,000 wa Ayubu, navyo vinaua watunzaji wote isipokuwa mmoja. Mwishowe, Shetani anapeleka upepo mkubwa unaopiga nyumba walimo watoto kumi wa Ayubu wanaokula karamu, na wote wanakufa. Baadaye, kwa mfuatano wa haraka, waokokaji wa misiba hiyo wanamletea Ayubu habari hizo zilizo mbaya sana.—Ayubu 1:13-19.
9. Ni jambo gani lililofanya misiba ya Ayubu iwe migumu zaidi kuvumiliwa, hata hivyo Ayubu alitendaje alipopatwa nayo?
9 Loo, maafa yaliyoje! Hata kama Ayubu angefahamu ni nani mwenye kuyatokeza, bado ingekuwa vigumu kuyavumilia. Lakini yeye hafahamu! Yeye hajui kwamba ni kumhusu yeye hasa kwamba ubishi ulitokea mbinguni na kwamba Yehova alikuwa akimtumia yeye ili aonyeshe kwamba kuna watu watakaoshika ukamilifu wao zijapokuwa taabu zote za udhalimu ambazo Shetani anaweza kuwaletea. Hata hivyo, kwa kupigwa na kihoro na hata akifikiri kwamba kwa njia fulani Mungu amehusika katika kuleta hasara zilizompata, Ayubu anapaaza sauti: “[Yehova] alitoa, na [Yehova] ametwaa; jina la [Yehova] na libarikiwe.” Ndiyo, “katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.”—Ayubu 1:20-22.
10. (a) Ni ruhusa gani nyingine ambayo Shetani aliomba apewe kuhusiana na Ayubu, na kwa sababu gani Yehova alikuwa na nia ya kumpa ruhusa hiyo? (b) Matokeo yalikuwa nini kwa Ayubu juu ya hali yenye kusikitisha aliyoingizwa ndani?
10 Kwenye mkutano mwingine wa malaika, Shetani alishushiwa heshima kama nini kwa kukumbushwa na Yehova hivi juu ya Ayubu: “Hata sasa bado anashika sana ukamilifu wake”! Lakini Shetani hachoki. Sasa anatoa mwito wa ushindani kwa kusema kwamba akipewa nafasi ya kumpiga Ayubu kimwili, Ayubu atamlaani Mungu mbele ya uso wake. Kwa kuutumaini ukamilifu wa Ayubu kwa kadiri hiyo, Yehova anatoa ruhusa. Onyo moja tu analompa Shetani ni kwamba asiondoe uhai wa Ayubu. Kwa hiyo Shetani ‘anampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.’ (Ayubu 2:1-8) Hali ya Ayubu inazorota vibaya sana mpaka watu wa ukoo na marafiki wanamkwepa, nao waliokuwa wanafahamiana naye wanamdhihaki.—Ayubu 12:4; 17:6; 19:13-19; 30:1, 10-12.
11. Ni dharuba gani nyingine ambayo Ayubu alipaswa kuvumilia, na ni jambo gani jingine lililofanya ushikaji ukamilifu wake uwe wa kusifika sana katika taabu zake zote?
11 Halafu pigo jingine tena! Imani ya mke wa Ayubu inadhoofika. Yeye anamwambia “Je! wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? umkufuru Mungu, ukafe”! Lakini yeye anamwambia mkeye: “Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya?” Kama yanavyosema masimulizi, “Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.” (Ayubu 2:9, 10) Nawe unapokumbuka kwamba sababu ya Ayubu kutaabika imefichwa asiijue, ukamilifu wake unaonekana kuwa wa kustaajabisha kama nini!
Namna Nyingine ya Shambulio
12. (a) Wanaume waliokuja kumfariji Ayubu walikuwa akina nani? (b) Shetani aliwatumiaje wanaume hao kuzidi kumjaribu Ayubu?
12 Lakini Shetani hajamaliza mambo yake. Anainua wanaume watatu wanaosemekana kuwa wenye hekima ambao ama walimjua Ayubu kibinafsi, ama walipata habari za sifa yake, kwamba “alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa mashariki.” Kwa wazi wao ni wazee sana kwa umri kuliko Ayubu. (Ayubu 1:3; 15:10; 32:6) Wawili kati yao ni watu wa ukoo ulio wa mbali. Elifazi Mtemani ni mzao wa Abrahamu kupitia Temani, mjukuu wa Esau, na Bildadi Mshuhi ni mzao wa Shua mwana wa Abrahamu. (Ayubu 2:11; Mwanzo 36:15; 25:2) Ukoo wa Sofari haujulikani kwa uhakika, Wanasingizia kwamba wamekuja kumfariji Ayubu, lakini kwa kweli Shetani anawatumia katika jitihada ya kubomoa ukamilifu wa Ayubu. Sawa na vile wanasiasa wenye kuuliza wafungwa maulizo ya kuwachunguza wamewafanya wabomoe ushikamanifu wao na kuwapinganisha na serikali zao wenyewe, ndivyo Shetani alivyotumainia kuwatumia “wafariji” wake wampinganishe Ayubu na Mungu.—Ayubu 16:2, 3.
13. (a) Wageni wa Ayubu walifanya nini walipofika? (b) Wakati maneno yalipoanza kusemwa, yalichukua mwendo gani?
13 Wanapofika, wageni watatu hao wanakaa siku saba na mausiku saba wakichungua kwa ukimya maumivu makali na matwezo mengi mno ya Ayubu. (Ayubu 2:12, 13) Elifazi, ambaye kwa wazi ndiye aliyekuwa na umri mkubwa kuliko wote, mwishowe anaongoza katika kunena, akianzishia wale wengine maoni na habari ya ujumla ya majadiliano ya vipindi vitatu. Hotuba ya Elifazi, na pia zile zinazofuata za wenzake, ni za mashtaka hasa. Baada ya kila mmoja wa washtaki wake kunena, naye Ayubu anajibu akikanusha hoja zao. Sofari hashiriki kipindi cha tatu cha majadiliano, kwa wazi akijisikia kwamba amekwisha sema ya kutosha. Hivyo Sofari anatoa hotuba mbili tu, hali Elifazi na Bildadi wanatoa tatu kila mmoja.
14. Ni hoja za namna gani ambazo wanaume hao watatu walitumia dhidi ya Ayubu, na Shetani alitumiaje mbinu kama hiyo kuhusiana na Yesu?
14 Hotuba za Elifazi ni ndefu zaidi, na maneno anayotumia ni mapole kidogo. Maneno ya Bildadi yanauma kama meno, nayo ya Sofari ni zaidi. Hoja zao zimetungwa kwa ujanja kutimiza kusudi la Shetani la kuvunja ukamilifu wa Ayubu. Mara nyingi wao wanataja mambo ya hakika, lakini hali na njia ya kuyatumia haifai. Shetani alitumia mbinu iyo hiyo dhidi ya Yesu. Akinukuu andiko linalosema malaika wa Mungu angemlinda mtumishi wake asipatwe na dhara. Shetani alimwalika Yesu athibitishe ni mwana wa Mungu kwa kujitupa chini kutoka juu hekaluni. (Mathayo 4:5-7; Zaburi 91:11, 12) Kwa kipindi kirefu, Ayubu alikabili wazo la kishetani la mfano huo.
15. Elifazi alitoa hoja ya kwamba chanzo cha taabu za Ayubu kilikuwa nini?
15 Katika hotuba yake ya kufungua, Elifazi anabisha kwamba matata ya Ayubu ni malipo ya Mungu kwa dhambi zake. “Ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? anauliza. “Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.” (Ayubu 4:7, 8) Akiendelea kusema, Elifazi anadai kwamba Mungu hawatumaini watumishi wake. “Katika watumishi wake hana imani,” Elifazi anasema, “na [malaika] zake anawashtakia ukosaji. Si zaidi sana wale wanaokaa katika nyumba za udongo.”—Ayubu 4:18, 19, NW.
16. Bildadi aliendelezaje ushambulizi wa Elifazi, naye alitumia mfano gani usiofaa?
16 Bildadi anauendeleza ushambulizi huo wa maneno. “Ikiwa wewe umetakata na u mnyofu,” anasema, “kufikia sasa [Mungu] angeamka kwa ajili yako naye hakika angekurudishia kao lako lenye uadilifu.” Bildadi anasema kwamba mafunjo na matete yanakauka na kunyauka yakikosa maji, kisha anakata shauri kikweli kwamba ndivyo pia itakavyokuwa kwa “wote wale wanaomsahau Mungu.” Lakini ni kosa kama nini kutumia mfano huo umhusu Ayubu, kisha kuongeza, “Hata lile tumaini alilo nalo mwasi-imani litatoweka”!—Ayubu 8:6, 11-13, NW.
17. Ni maelezo gani makali ambayo Sofari alitoa?
17 Maneno ya Sofari ni yenye nguvu hata zaidi. Anasema jambo kama hili, ‘Laiti Mungu angenena akuambie anavyofikiri! Mungu anajua lile ambalo umefanya. Yeye anakuadhibu kwa kipimo kilicho kidogo sana kuliko kile unachostahili. Ondolea mbali dhambi zako na kuacha ubaya wako wote, kisha utakuwa na usalama na rafiki wengi.’—Ayubu 11:4-6, 14-20.
18. Katika kipindi cha pili cha majadiliano yale, wanaume hao watatu waliendelezaje ushambulizi wao juu ya Ayubu?
18 Katika kipindi cha pili cha majadiliano, Elifazi anaendeleza ushambulizi juu ya ukamilifu wa Ayubu. ‘Ala, Mungu hata hawatumaini malaika, sembuse mtu kama wewe! Mtu mwovu sikuzote anakuwa matatani.’ (Ayubu 15:14-16, 20, NW) Kwa kukasirishwa na upinzani thabiti wa Ayubu kwa hoja zao, Bildadi anasema jambo kama hili: ‘Nuru yako itazimishwa. Kumbukumbu lote la kuwako kwako litafifia liishe. Hilo ndilo linalowapata wale wanaomsahau Mungu.’ (Ayubu 18:5, 12, 13, 17-21) Sofari anagusia ufanisi ambao Ayubu alikuwa nao, na kuuliza: Wewe hujui kwamba shangwe ya mwovu ni fupi, na kufurahi kwa mwasi-imani ni kwa dakika? Mbingu inafunua makosa ya mwovu.’—Ayubu 20:4, 5, 26-29, NW.
19. (a) Kulingana na Elifazi, Mungu anaona kuna thamani gani ya mwanadamu kuwa na ukamilifu? (b) Bildadi alimaliziaje ushambulizi wa maneno juu ya Ayubu?
19 Akifungua kipindi cha tatu cha majadiliano, Elifazi anauliza: ‘Je! mwanadamu ye yote anaweza kuwa mwenye thamani kwa Mungu? Hata kama ungekuwa asiye na lawama, je, Mungu angefaidika kutokana na jambo hilo? Mrudie Mungu,’ anasema, ‘nawe unyooshe mambo yako, Ndipo utakapoponywa.’ (Ayubu 22:2, 3, 21-23, NW) Bildadi anamalizia ushambulizi huo wa maneno. ‘Ni nani duniani anayeweza kujisifu kuwa ni safi?’ anauliza. ‘Mungu ni mtukufu sana kwamba hata mwezi na nyota si kitu kabisa mbele yake. Sembuse mwanadamu, ambaye ni mdudu tu machoni pake!’—Ayubu 25:2-6, NW.
Kujitetea kwa Ayubu na Kusahihishwa Kwake
20. (a) Ayubu alijibuje hoja ya kwamba kutaabika ni adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya dhambi? (b) Ayubu aalikaza moyo afanye nini, nasi tunajuaje kwamba kwa kweli Mungu aliuona ukamilifu wake kuwa jambo lenye thamani?
20 Ijapokuwa anataabika vibaya sana, Ayubu hajiachi kamwe akubaliane na hoja za udanganyifu za hao wenye kumtesa-tesa. Ikiwa kutaabika ni adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya dhambi zake, yeye anauliza: “Mbona waovu wanaishi, na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu [katika utajiri]”? (Ayubu 21:7-13) Na kinyume cha vile washtaki wa Ayubu wanavyosema, Yehova anawathamini washika-ukamilifu ambao kwa njia hiyo wanamwandalia jibu kwa madharau ya Shetani kwamba yeye anaweza kugeuza mtu ye yote aache kumtumikia Mungu. (Mithali 27:11; Zaburi 41:12) Ayubu ana uhakika juu ya ukamilifu wake mwenyewe, akipaaza sauti hivi: “Mpaka nitakapokufa mimi sitaondoa ukamilifu kwangu mwenyewe!” (Ayubu 27:5, NW) Hapana, yeye hakufanya jambo lo lote hata astahili yaliyompata.
21. Elihu aliwaambia nini wafariji wa uwongo wa Ayubu, naye alimpa Ayubu sahihisho gani lililohitajiwa?
21 Kijana Elihu anasikiliza kwa makini kila neno la majadiliano hayo marefu. Sasa yeye, ananena akiwafariji wa uwongo wa Ayubu hakuna lo lote ambalo wamesema limemthibitisha Ayubu kuwa mtenda dhambi (Ayubu 32:11, 12) Halafu, akimgeukia Ayubu, Elihu anasema: “Nimesikia sauti ya maneno yako, ukisema, Mimi ni safi, sina makosa; sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu. Tazama, yuaona sababu za kufarakana nami, hunihesabu kuwa ni adui yake . . . Katika neno hili [umekosea].” (Ayubu 33:8-13; 6:29; 13:24, 27; 19:6-8) Ndiyo, Ayubu alihangaikia mno kuondoa malawama juu ya ukamilifu wake mwenyewe. Hata hivyo, wakati uo huo, yeye hakumlaumu Mungu kamwe wala hakupoteza tumaini hakika la kwamba Mungu angetenda linalofaa.
22. (a) Baada ya kumsikiliza Yehova, itikio la Ayubu lilikuwa nini? (b) Mungu alitaka nini kwa wafariji wa uwongo wa Ayubu, na matokeo ya mwisho kwa Ayubu yalikuwa nini?
22 Upepo unaanza kupiga kwa nguvu wakati Elihu anapomaliza hotuba yake, na Yehova mwenyewe ananena kutoka kwa upepo wa kisulisuli: “Ni nani huyu atiaye mashauri giza kwa maneno yasiyo na maarifa? Basi jifunge viuno . . . Maana nitakuuliza neno, nawe niambie.” Baada ya kumsikiliza Yehova, Ayubu anatambua kwamba alinena haraka haraka, bila maarifa kamili, kisha anatubu “katika mavumbi na majivu.” Halafu Yehova anamkanusha vikali Elifazi na wenzi wake wawili, na kumwagiza Ayubu awaombee. Baada ya hapo Ayubu anarudishwa kwenye hali yake ya kwanza, naye anabarikiwa akiwa na watoto saba wa kiume na binti watatu warembo na mifugo iliyo mara mbili ya ile aliyokuwa nayo zamani. Ayubu anaishi muda wa miaka 140 zaidi, na anakufa “mzee sana mwenye kujawa na siku.”—Ayubu 38:1-4; 42:1-17.
23. Ukamilifu wa Ayubu unapasa kuwa na matokeo gani juu yetu?
23 Kweli Ayubu alikuwa mtu wa kusifika mwenye ukamilifu! Yeye hakuwa na njia ya kujua kwamba alikuwa akifanywa awe lengo la shtaka bovu la Shetani. Jambo hilo linaukazia hata zaidi ukamilifu wake kwa sababu ingawa aliamini kwamba taabu zote zilizompita zilitoka kwa Mungu, bado yeye hangemkana Mungu wala kumlaumu. Ni somo lililoje kwetu, kwa kuwa sisi tunajua chanzo cha majaribu ya ukamilifu wetu! Hakika tunapaswa kusukumwa na moyo tuige mfano wa Ayubu na kusonga mbele katika kazi ya Yehova hata Adui ya Mungu alete jambo liwalo lote dhidi yetu.
-
-
Ukamilifu wa Ayubu—Ni Nani Anayeweza Kuuiga?Mnara wa Mlinzi—1986 | Machi 1
-
-
Ukamilifu wa Ayubu—Ni Nani Anayeweza Kuuiga?
“Yeye atanipima katika mizani zilizo sahihi naye Mungu atapata kujua ukamilifu wangu.”—AYUBU 31:6, Biblia ya New World Translation.
1. Kwa sababu gani ni vizuri kufikiria mfano wa Ayubu, na ni maulizo gani yanayotokezwa?
AYUBU alikuwa na uhakika juu ya ukamilifu wake na kwa hiyo akakubali kuchunguzwa na Mungu. Mfano wake unaweza kuwa kitia-moyo kikubwa kwetu leo, hasa wakati huu ambapo Shetani Ibilisi anajaribu sana kuvunja ukamilifu wa wote wanaomtumikia Mungu. (1 Petro 5:8) Kwa kutambua hivyo, mwanafunzi Yakobo alisema ‘tuchukue manabii kama kielelezo cha kupatwa na uovu na kujizoeza subira,’ hasa Ayubu. (Yakobo 5:10, 11, NW) Lakini ni nani anayeweza kuiga ukamilifu wa Ayubu? Je, sisi tunaweza? Ni kwa njia zipi Ayubu alituwekea mfano wa kushika ukamilifu?
2. (a) Jina Ayubu lina maana gani? (b) Ni jambo gani lililotimizwa na mwendo wa Ayubu wa kushika ukamilifu?
2 Jina Ayubu linamaanisha “kitu cha kutendwa uhasama,” na hakika hivyo ndivyo yeye akawa. Lakini wakati Yehova alipomruhusu Shetani afanye kulingana na ombi lake kisha akauondoa ukigo wa ulinzi uache kumzunguka Ayubu, hakuna jambo ambalo Shetani angeweza kufanya auvunje ukamilifu wa Ayubu kwa Mungu. (Ayubu 1:1–2:10) Kwa njia hiyo Ayubu aliandaa jibu la kutolea laumu la Shetani kwamba yeye angeweza kugeuza mtu ye yote aache kumtumikia Mungu. (Mithali 27:11) Kwa mwendo wake wa kushika ukamilifu, Ayubu ni kama alikuwa akitolea ulimwengu mzima tangazo la kwamba, ‘Shetani, wewe ni mwongo mwenye kudharaulika, kwa sababu Yehova ni Mungu wangu, nami nitashika ukamilifu kuelekea yeye hata kutokee nini!’—Ayubu 27:5, NW.
Wale Walio Kama Ayubu
3. Ni nani aliyelindwa mbinguni, na ni maulizo gani yaliyotokezwa juu yake?
3 Ni jambo la maana kuangalia kwamba suala kati ya Yehova na Shetani lilihusu ulimwengu mzima, kutia na makao ya kiroho. “Uzao” ulioahidiwa alikuwa kule mbinguni akiwa amezungushiwa ukigo kwa ulinzi wa Yehova, na kupitia kwake Mungu alinuia kutimiza makusudi Yake makuu. (Mwanzo 3:15) Hata hivyo, wakati ‘ukigo wa ulinzi’ ungeondolewa, je, huyo kweli angeiga ukamilifu wa Ayubu? Je, angeonyesha kwamba mwanadamu mkamilifu, kama alivyokuwa Adamu, angeweza kushika ukamilifu usiopunguka kuelekea Mungu? (1 Wakorintho 15:45) Shetani alifanya matayarisho ya kuutia “uzao” huo kwenye jaribu kali sana ukiisha kutokea duniani.
4. (a) Ni nani akawa ndiye kitu kikuu cha kutendwa uhasama na Shetani, nasi tunajuaje Mungu aliondoa ulinzi wake kwa mtu huyo? (b) Yesu alimwandalia Yehova nini?
4 Yesu Kristo akawa ndiye “uzao” uliopelekwa kutoka mbinguni. Hivyo akawa ndiye hasa wa kuelekezewa fikira na Shetani, ndiyo, kitu kikuu cha kutendwa uhasama na Shetani. Kuonyesha ushuhuda wa kwamba Yehova alikuwa ameondoa ukigo wa ulinzi wake, Kristo alipiga kelele hivi alipokuwa juu ya mti wa mateso: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Mathayo 27:46; Zaburi 22:1) Ingawa alihisi sana kwamba Mungu alikuwa ameondoa ulinzi wake, Yesu alifanya kama Ayubu kwa ‘kutokufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.’ (Ayubu 1:22) Yeye alimwiga Ayubu, akashika ukamilifu usiopunguka kuelekea Mungu, na hivyo akathibitisha kwamba ‘hapana mmoja aliyekuwa kama yeye duniani.’ (Ayubu 1:8) Hivyo ni katika Yesu peke yake Yehova Mungu ana jibu kamili na la milele kwa shtaka la uwongo la Shetani la kwamba Mungu hawezi kuweka duniani mwanadamu atakayebaki akiwa mwaminifu kwake chini ya jaribu lililo kubwa zaidi.
5. (a) Shetani anaendelea kufanya nini? (b) Shetani alifanya nini alipoondolewa mbinguni?
5 Bado akitaka jibu zaidi, Shetani anaendelea kuwashtaki ndugu za kiroho wa Yesu, ambao, wakiwa pamoja na Yesu, ndio wanaokuwa “uzao” wa tengenezo la Mungu lililo mfano wa mwanamke. Wakati inapoeleza juu ya kusimamishwa kwa Ufalme mbinguni, Biblia inasema hivi juu ya Shetani: “Ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu”! Lakini, Shetani hashtaki tu na kuachia hapo, bali anatokeza shambulio lenye uhasama! Biblia inaeleza kwamba baada ya yeye kuporomoshwa kutoka mbinguni, “joka [Shetani] akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu.”—Ufunuo 12:7-12, 17.
6. (a) Ni akina nani leo wanaoongoza kazi ya kuhubiri, na ni akina nani wamejiunga nao? (b) Shetani anajaribu kuwafanya nini wote hao?
6 ‘Wazao wa mwanamke waliosalia’ ni Mashahidi wapakwa mafuta wa Yehova waliobaki duniani leo. Wao ndio wanaoongoza “kuwa na ushuhuda wa Yesu,” wakitangaza waziwazi ulimwenguni pote kwamba sasa yeye amekwisha kutawazwa kuwa Mfalme na karibuni ataukomesha mfumo huu wa mambo usio mwadilifu. (Mathayo 24:14; Danieli 2:44) Lakini hawako peke yao hata kidogo! Sasa mkutano mkubwa sana wa watu zaidi ya milioni tatu wamejiunga nao kuwa tengenezo lenye umoja la washika ukamilifu ulimwenguni pote. Washika-ukamilifu wote hao, pia, wamekuwa vitu vya kuletewa mateso yasiyo na mwisho ya Shetani, naye Yehova Baba yao wa kimbingu anafurahia ukamilifu wao.—2 Timotheo 3:12; Mithali 27:11.
7. Kwa sababu gani tunaweza kuwa na tumaini hakika tunapokabili mashambulio ya Shetani?
7 Hakika inafaa kutambua kwa uzito kwamba, kama ilivyokuwa kwa Ayubu, fikira mbovu za Shetani zimeelekezwa juu yetu sisi tunaojaribu kushika ukamilifu kuelekea Mungu. Lakini, hatuhitaji kutiwa kasirani na jambo hilo. Kwa sababu gani? Kwa sababu “Yehova ni mwororo sana katika upendo wenye shauku na ni mwenye rehema,” tena “hatakupungukia wala kukuacha.” (Yakobo 5:11, NW; Kumbukumbu la Torati 31:6, UV) Ndiyo, Yehova atatutegemeza. “Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu,” Biblia inasema. (Mithali 2:7) Ingawa hivyo, hiyo haimaanishi kwamba Yehova hataturuhusu tujaribiwe. Atafanya hivyo, sawa na alivyomruhusu Ayubu ajaribiwe. “Ila Mungu ni mwaminifu,” akasema mtume Paulo, “ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”—1 Wakorintho 10:13.
Tunapokuwa Chini ya Jaribu
8. Mfano wa Ayubu unaweza kutufaidije leo?
8 Mfano wa Ayubu wa ukamilifu unaweza kutusaidia hasa tunapokabili majaribu makali. Ayubu alitaabika sana hata akajisikia ni afadhali afe na kufichwa katika Sheoli, kaburi la ujumla la wanadamu. (Ayubu 14:13) Watu fulani wamejisikia ivyo hivyo leo, wakasema kwamba wangeweza kuhusianisha hali yao na ile ya Ayubu wakati alipokuwa akitaabika sana. Labda pindi fulani wewe umejisikia ivyo hivyo. Kwa kweli, kusoma habari za kutaabika kwake kunaweza kuwa kama kupokea kitia-moyo kutoka kwa rafiki ambaye amepitia jaribu lililo kali zaidi ya lile letu wenyewe. Kujua kwamba mtu mwingine amevumilia, naye anafahamu, hakika kunatusaidia sisi pia tuvumilie.
9. Tunafaidiwaje na ushikaji ukamilifu wa wengine?
9 Kwa kuwa anatambua mahitaji yetu, Yehova aliagiza kitabu cha Ayubu kiandikwe ili kitusaidie tushike ukamilifu kama Ayubu. (Warumi 15:4; Yakobo 5:10, 11) Mungu anajua kwamba, kama vile sehemu moja ya mwili inavyotegemea nyingine, ndivyo watumishi wake waaminifu wanavyohitajiana. (1 Wakorintho 12:20, 26) Kumbuka mikusanyiko ile ya karibuni ya “Washika Ukamilifu” iliyohudhuriwa na mamilioni ya wasomaji wa gazeti hili. Wale waliokuwako watakumbuka jinsi walivyojisikia vizuri kuwa katika ushirika wa wengi sana ambao shabaha yao kuu ni kudumisha ukamilifu kwa Mungu. Wahudhuriaji walitiwa moyo sana washike ukamilifu kwa kujua kwamba maelfu mengi waliokuwa karibu nao wanashika ukamilifu pia chini ya majaribu magumu wanapokuwa katika mahali pao pa kazi au shuleni katika mitaa ya kwao wenyewe!—1 Petro 5:9.
10. (a) Ni kwa njia gani mtu anaweza kushindwa kuendeleza maoni yanayofaa? (b) Ayubu alianza kutia shaka juu ya nini?
10 Hata hivyo huenda tukashindwa kudumisha maoni yanayofaa sikuzote, kama vile Ayubu. Mtu anayetaabika sana, na aliye katika hali ya kushuka moyo, huenda akafikiri au kusema, ‘Jamani, mbona Mungu ananifanyia hivi? Mbona anaruhusu jambo hili litukie?’ Huenda hata akafikia hatua ya kuuliza, ‘Kuna faida gani kwamba namtumikia Mungu?’ Kwa sababu ya kutokujua chanzo cha taabu yake, Ayubu alitia shaka juu ya kama kuna faida ya kuwa mwadilifu wakati wa sasa, kwa kuwa watu wema walionekana kuwa wakitaabika sana, na hata zaidi ya wabaya. (Ayubu 9:22) Kulingana na Elihu, Ayubu alisema: “Mimi napata faida gani? Napata faida gani inayozidi ile ambayo ningalipata kama ningalitenda dhambi?” (Ayubu 35:3, An American Translation) Lakini hatuwezi kujiacha tuhangaishwe mno na taabu zetu wenyewe hata tupoteze maoni yanayofaa na kutilia shaka ubora wa kumtumikia Mungu.
11. Elihu alimwandalia Ayubu sahihisho gani zuri?
11 Elihu alimwandalia Ayubu usahihisho uliohitajiwa, akanyoosha mambo kwa kuonyesha kwamba Yehova ametukuka zaidi ya Ayubu. (Ayubu 35:4, 5) Alionyesha kwamba, hata litukie jambo gani, haitupasi kamwe kukata shauri kwamba Mungu hajali na kuwaza kwa njia fulani kwamba tunaweza kumpuuza Yeye kwa sababu ya kumfikiria kuwa mwenye hali fulani za udhalimu. “Ukifanya dhambi kwa kweli,” Elihu akamuuliza Ayubu, “unakuwa umetimiza nini dhidi yake? Nayo maasi yako yakiongezeka kwa kweli, wewe unakuwa umemfanya nini?” (Ayubu 35:6, NW) Ndiyo, ukijaribu kumpuuza Mungu kwa kuziacha njia zake au utumishi wake, unajiumiza mwenyewe tu, wala si Mungu.
12. Ushikaji ukamilifu wetu unamhusuje Mungu?
12 Kwa upande mwingine, Elihu alionyesha kwamba sisi hatuwi tunampa Yehova faida ya kibinafsi tukitenda yanayofaa. Bila shaka, Mungu anafurahi sana tukishika ukamilifu. Hata hivyo, yeye hategemezwi kwa vyo vyote na ibada yetu, kama inavyoonyeshwa na ulizo ambalo Elihu alimuuliza Ayubu: “Ikiwa umetenda yanayofaa kweli kweli, unakuwa umempa nini, au yeye anakuwa amepokea nini kutoka mkono wako mwenyewe?” (Ayubu 35:7, NW) Mungu alitupa sisi uhai, na kwa sababu yake tunapumua na kwenda na kuwapo. Kila kitu ni chake! (Matendo 17:25; 1 Mambo ya Nyakati 29:14) Hivyo uovu wala uadilifu wetu hauwezi kuwa na matokeo ya kibinafsi juu ya Mungu.—Ayubu 35:8.
Tunaposahihishwa
13. (a) Ayubu alitendaje juu ya sahihisho alilopewa? (b) Sisi sote tuna tatizo gani?
13 Ayubu alitendaje alipopewa sahihisho, kwanza na Elihu kisha na Yehova mwenyewe? Alilikubali, akatubu “katika mavumbi na majivu.” (Ayubu 42:6) Ndiyo, Ayubu alijinyenyekeza, akakubali kosa lake. Na je, sisi hatuvutiwi na unyenyekevu wa namna hiyo? Lakini namna gani sisi? Ingawa huenda ikawa sisi ni washika-ukamilifu walio thabiti kama Ayubu, sisi sote tunaelekea kufanya makosa na kupoteza usawaziko kwa njia moja au nyingine. (Yakobo 3:2; Wagalatia 2:11-14) Tufanye nini tukionyeshwa kosa letu au hali ya kutokukamilika, hata ikiwa tumeonyeshwa na mtu wa umri mdogo kama Elihu?—Ayubu 32:4.
14. (a) Ni elekeo gani lililo la kawaida wakati mtu anaposahihishwa? (b) Ni jambo gani linaloweza kuhusika katika kutokeza makosa au maamuzi yasiyofaa, na ni mfano gani ambao Ayubu aliweka aliposahihishwa?
14 Si jambo jepesi sikuzote kukubali sahihisho. (Waebrania 12:11; Mithali 3:11, 12) Tuna elekeo la kujaribu kujitetea. Kama vile Ayubu, huenda ikawa hatukusema au kufanya ubaya wo wote kwa makusudi. Huenda ikawa kusudio letu lilikuwa zuri. Lakini huenda ikawa tulinena bila maarifa kamili, kwa kukosa ufahamu au bila hisia. Labda maelezo yetu yalionyesha hali ya majivuno ya kikabila au kujiona kwamba taifa letu ni bora kuliko la wengine, au kushikilia sana jambo fulani lisiloungwa mkono na Maandiko. Huenda ikawa tutajulishwa kwamba tuliyosema ni maoni ya kibinafsi tu na kwamba yameumiza wengine kwa kiasi cha kuhatirisha hali yao ya kiroho. Tunaposahihishwa, je, tutakuwa kama Ayubu tukubali ‘tulisema maneno tusiyoyafahamu’ na ‘kutubu’?—Ayubu 42:3, 6.
Kumtumaini Mungu, Wala si Mali
15. Tunajuaje kwamba tumaini la Ayubu halikuwa katika mali zake?
15 Bildadi alitia shaka juu ya chanzo ambacho Ayubu alitumainia, akidokeza kwamba yeye alikuwa amemsahau Mungu na kwamba alikuwa ameweka tumaini lake mahali pengine. (Ayubu 8:13, 14) Hata hivyo, ingawa Ayubu alikuwa amebarikiwa kwa vitu vingi vya kimwili, tumaini lake halikuwa katika vitu hivyo. Ukamilifu wake haukutikisika hata kidogo alipopoteza mali zake zote. (Ayubu 1:21) Alipokuwa akimaliza kujitetea, Ayubu alisema: “Ikiwa nimeifanya dhahabu kuwa tumaini langu, na kuiambia dhahabu safi, Wewe u tegemeo langu; kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi . . . hilo nalo lingekuwa uovu wa kuadhibiwa na waamuzi; kwani [ningemkana] Mungu aliye juu.”—Ayubu 31:24-28.
16. (a) Inatupasa tujichunguzeje wenyewe? (b) Mungu anawatolea ahadi zipi wale wanaomtumaini yeye?
16 Namna gani sisi? Sisi tunaweka wapi tumaini letu—katika Yehova au katika mali za kimwili? Kama tungepimwa katika mizani iliyo sahihi, kama vile Ayubu alivyotaka afanywe, je, Mungu angejua kwamba sisi tuna ukamilifu katika jambo hilo? Je, kweli hangaikio letu kuu maishani ni lile la kumwandalia Yehova mwendo wa kushika ukamilifu ili autumie kujibu malaumu ya Shetani? Au sisi tunahangaikia hasa kutosheleza tamaa zetu za kutaka anasa na mali? Ingekuwa vizuri kama nini tukiwa kama Ayubu na kuufurahisha moyo wa Yehova kwa kumtumaini Yeye, tusipojihesabia sisi wenyewe au vitu vya kimwili tulivyo navyo umaana usiostahili! Tukimtumaini Yehova, tuweke faida zake kwanza, yeye anaahidi hatatuacha kamwe wala kutuondoka.—Mathayo 6:31-33; Waebrania 13:5, 6.
Maadili Katika Ngono
17. Ni vidokezo gani ambavyo “wafariji” wa Ayubu walitokeza, lakini Ayubu alisema nini juu ya mwenendo wake wa kiadili?
17 Wafariji wa uwongo wa Ayubu hawakumshtaki juu ya mwenendo mbaya wa ngono kwa njia ya moja kwa moja, lakini walidokeza-dokeza kwamba alikuwa na hatia ya kosa fulani la siri ambalo Mungu alikuwa akimwadhibia. Kwa kuwa alikuwa mtu mwenye mali nyingi, akiwa ndiye “mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki,” hakika Ayubu alitokewa na nafasi za kumwezesha kufanya ngono nje ya mpango wa ndoa kama angalitaka. (Ayubu 1:3; 24:15) Watumishi wengine wa Mungu, wa kabla na baada ya wakati wa Ayubu, waliangukia vishawishi vya ngono. (Mwanzo 38:15-23; 2 Samweli 11:1-5) Lakini, Ayubu alijitetea kuwa hakuwa na mipango ya ujanja ya kutenda kosa hilo, akitangaza hivi: “Nilifanya agano na macho yangu; basi nawezaje kumwangalia msichana? Kama moyo wangu ulishawishwa kwa mwanamke, nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu . . . hilo lingekuwa kosa kuu; naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi.”—Ayubu 31:1, 9-11.
18. Kwa sababu gani ni vigumu sana kudumisha maadili ya ngono, hata hivyo ni kwa sababu gani sisi tutakuwa wenye furaha tukiyadumisha?
18 Labda hakuna njia nyingine ambayo kwayo Shetani amefanikiwa sana kubomoa ukamilifu wa watumishi wa Mungu kama vile alivyofanikiwa kwa kuwashawishi wafanye uasherati. (Hesabu, sura ya 25) Je, wewe unaweza kuiga ukamilifu wa Ayubu kwa kupinga sana vishawishi vyote vya kuwa na mwendo mbaya wa ngono? Huo ni mwito mkubwa wa ushindani, hasa katika ulimwengu huu ambamo ukosefu wa adili unapatikana sana. Lakini fikiria ni vizuri kama nini, wakati unapoombwa utoe hesabu, kuweza kusema kwa uhakika kama vile Ayubu alivyofanya: “Mungu atapata kuujua ukamilifu wangu”!—Ayubu 31:6.
Kinachoweza Kutusaidia
19. Ni jambo gani linalohitajiwa sana litusaidie kushika ukamilifu?
19 Si jambo jepesi kuiga ukamilifu wa Ayubu, kwa kuwa leo Shetani anajaribu kwa bidii kuvunja ukamilifu wetu kama alivyojaribu kuuvunja wa Ayubu. Basi, inahitajiwa kwamba tuvae suti kamili ya silaha kutoka kwa Mungu. (Waefeso 6:10-18) Jambo hilo linahusu kuwa watu wenye kushikilia mambo ya Mungu, kama Ayubu, kufikiria daima kumpendeza Yeye katika lo lote ambalo sisi au jamaa zetu tunafanya. (Ayubu 1:5) Hivyo funzo la Biblia, ushirika wa kawaida pamoja na waamini wenzetu, na tangazo la waziwazi la imani yetu ni mambo yanayohitajiwa sana.—2 Timotheo 2:15; Waebrania 10:25; Warumi 10:10.
20. (a) Ni tumaini gani linaloweza kututegemeza wakati wa majaribu? (b) Ni thawabu gani ya kushika ukamilifu iliyotajwa na mtunga zaburi tunayoweza kupokea?
20 Lakini jambo hasa linaloweza kututegemeza zaidi wakati wa jaribu ni lile lililotegemeza Ayubu, tumaini lake hakika la kwamba maisha siyo aya haya tu. “Mtu hodari akifa, je, anaweza kuishi tena?” Ayubu akauliza. Na kwa kujibu alisema hivi: “Wewe utaita, nami nitakujibu.” (Ayubu 14:13-15, NW) Kuwa na uhakika kamili uo huo kwamba Yehova atafufua watumishi wake waamini kunaweza pia kutusaidia tukabili jaribu lo lote ambalo huenda Shetani akaweka juu yetu. (Waebrania 6:10) Zamani za kale mtunga zaburi wa Biblia aliandika hivi: “Nami katika ukamilifu wangu umeitegemeza, umeniweka mbele za uso wako milele.” (Zaburi 41:12) Huo na uwe ndio wakati ujao wenye furaha wa kila mmoja wetu—kuja kutegemezwa na Yehova na kuhifadhiwa naye milele kwa sababu ya kuwa watumishi wake washika ukamilifu!
-