“‘Kweli kweli, mtumishi Wangu . . . alidharauliwa, akaepukwa na watu . . . Tulimchukua kuwa hafai kitu. Hata hivyo magonjwa yetu ndiyo aliyokuwa akichukua, kuteseka kwetu ndiko alikovumilia. . . . Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, akapondwa kwa sababu ya maovu yetu. . . . Sisi sote tulipotea kama kondoo . . . Naye BWANA akampatiliza hatia ya sisi sote.’ . . . Ingawa hakuwa ametenda udhalimu na hakuwa amesema uwongo. . . . ‘Mtumishi Wangu mwadilifu hufanya wengi wawe waadilifu, adhabu yao ndiyo ambayo yeye huchukua . . . Alijiweka wazi mwenyewe [“alimwaga nafsi yake,” NW] kwenye kifo naye alihesabiwa miongoni mwa wenye dhambi, hali alibeba hatia ya wengi na akawaombea wenye dhambi.’”—Isaya 52:13–53:12.
Picha ambayo Isaya hutoa hapa ni ya mtu asiye na hatia kabisa, safi, ambaye kuteseka na kifo chake viliandaa ufuniko kwa ajili ya taifa lake mwenyewe, ambalo halikumkiri.
Hata hivyo, leo, waelezaji wengi Wayahudi hukubali kwa uhakika uliothibitishwa kwamba linalorejezewa ni taifa la Israeli kwa ujumla au kikundi chenye uadilifu ndani ya hilo taifa.
Swali ni, Je, taifa la Israeli, au hata sehemu yalo, lilipata wakati wowote kufaana na elezo hilo, au lahusu mtu mmoja?
Kwa zaidi ya miaka 800 baada ya Isaya kuandika maneno hayo ya unabii (wapata 732 K.W.K.), hakuna rekodi juu ya Myahudi au rabi yeyote aliyefundisha kwamba “mtumishi” huyo angeonwa katika maana ya ujumla. Muda wote wa kipindi hicho, unabii huo ulieleweka na wote kuwa ulirejezea mtu mmoja na ulionwa kwa ujumla kuwa unabii kuhusu yule Mesiya.
Kwa kuongezea, angalia maelezo katika utangulizi wa kitabu The Fifty-Third Chapter of Isaiah According to the Jewish Interpreters: “Ufafanuzi wa Kiyahudi uliokuwako kufikia mwisho wa kipindi cha Kiamora [kufikia karne ya sita W.K.] hudokeza kwamba mara nyingi, wakati ule, labda hata kwa ujumla ilichukuliwa bila kutiliwa shaka kwamba mtu aliyerejezewa alikuwa yule Mesiya, ambavyo bila shaka ndivyo Targum pia, baadaye hivi, huifasiri.”—Iliyohaririwa na H. M. Orlinsky, 1969, ukurasa 17.
Kungekuwa na madhumuni gani kukataa na kufasiri upya ule uelewevu wa kiasili zaidi wa andiko hilo likirejezea mtu mmoja, hata yule Mesiya? Je! haikuwa tu jitihada ya kuepuka uhusiano wowote kati ya unabii huo na Yesu, yule Myahudi wa karne ya kwanza aliyefaana na elezo lao kwa kila jambo dogo?