Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Yehova Ni Mfalme
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • 13, 14. (a) Yehova ametoa sheria zipi zinazohusu kuvuna? (b) Isaya atumiaje sheria zinazohusu kuvuna ili kutoa kielezi kwamba watu fulani wataokoka hukumu ya Yehova? (c) Ingawa misimu yenye huzuni ya majaribu inakuja, Wayudea waaminifu waweza kuwa na uhakika gani?

      13 Wanapovuna zeituni, Waisraeli hupiga miti kwa fito ndipo matunda yaanguke. Kulingana na Sheria ya Mungu, hawaruhusiwi kupanda matawi ya miti ili kuvuna zeituni zilizobakia. Wala hawapaswi kukusanya zabibu zilizobaki baada ya kuvuna mashamba yao ya mizabibu. Mabaki ya mavuno yapasa kuachiwa maskini—ili “mgeni, na yatima, na mjane”—wayaokote. (Kumbukumbu la Torati 24:19-21) Kwa kutumia sheria hizo zinazojulikana vema, Isaya atoa kielezi cha jambo linalofariji kwamba kutakuwapo watakaookoka hukumu ya Yehova inayokuja: “Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake. Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele [“watapaza sauti kwa furaha” “NW”]; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini. Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki”!—Isaya 24:13-16a.

      14 Kama vile matunda fulani hubaki mtini au kwenye mzabibu baada ya mavuno, vivyo hivyo kutakuwapo watu fulani watakaobaki baada ya Yehova kutekeleza hukumu yake—“waokotapo zabibu baada ya mavuno yake.” Kama ilivyorekodiwa kwenye mstari wa 6, tayari nabii amewataja, akisema “watu waliosalia wakawa wachache tu.” Lakini, hata kama ni wachache, kutakuwapo watakaookoka uharibifu wa Yerusalemu na Yuda, na baadaye mabaki watarudi kutoka utekwani ili kuijaza nchi tena. (Isaya 4:2, 3; 14:1-5) Ingawa wanyofu wa moyo watapitia misimu ya majaribu, waweza kuwa na hakika kwamba kutakuwapo ukombozi na furaha wakati ujao. Wenye kuokoka wataona neno la unabii la Yehova likiendelea kuwa wazi nao watatambua kwamba Isaya amekuwa nabii wa kweli wa Mungu. Watajawa na furaha waonapo utimizo wa unabii mbalimbali wa urudisho. Toka kokote kule walikotawanyika—iwe katika visiwa vya Mediterania upande wa Magharibi, Babiloni katika Mashariki, au mahali pengine popote palipo mbali—watamsifu Mungu kwa sababu wameokolewa, nao wataimba: “Atukuzwe Mwenye Haki”!

  • Yehova Ni Mfalme
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • 15, 16. (a) Isaya ahisije juu ya mambo yatakayowapata watu wake? (b) Ni mambo gani yatawakumba wakazi wasio waaminifu nchini humo?

      15 Hata hivyo, ni mapema mno kufurahi sasa. Isaya awaleta watu wa siku yake kwenye hali iliyopo, akitaarifu: “Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! kukonda kwangu! ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena.”—Isaya 24:16b-20.

      16 Isaya ahuzunika sana kwa sababu ya mambo yatakayowapata watu wake. Hali ya mambo inayomzunguka yamfanya awe na hisia za ugonjwa na ole. Watendao hila wamejaa nao wasababisha hofu kwa wakazi nchini humo. Yehova atakapoondoa ulinzi wake, wakazi wa Yuda wasio waaminifu watapata hofu mchana na usiku. Maisha yao yatakuwa mashakani. Haitawezekana kuponyoka msiba utakaowakumba kwa sababu ya kuziacha amri za Yehova na kuipuuza hekima yake. (Mithali 1:24-27) Maafa yatakuja hata kama watendao hila nchini humo, wanaojaribu kuwashawishi watu kwamba kila jambo litakuwa sawasawa, watumia maneno yasiyo ya kweli na udanganyifu ili kuwaongoza kwenye uharibifu. (Yeremia 27:9-15) Adui kutoka nje wataingia na kuwapora na kuwateka nyara. Hayo yote yamtaabisha sana Isaya.

  • Yehova Ni Mfalme
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • [Picha katika ukurasa wa 267]

      Isaya ahuzunika juu ya jambo litakalowapata watu wake

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki