Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ni Nani Awezaye Kusimama Dhidi ya mkuu wa Wakuu?
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
    • 13. Ni nini kilichotokea kwenye moja ya zile pembe nne, nacho kilitendaje?

      13 Sehemu inayofuata ya ono hilo yaenea zaidi ya miaka 2,200, ikiwa na utimizo leo. Danieli aandika hivi: “Katika moja ya pembe hizo [zile pembe nne] ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri. Nayo ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga. Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini. Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.”—Danieli 8:9-12.

      14. Malaika Gabrieli alisema nini juu ya utendaji mbalimbali wa ile pembe ndogo ya mfano, nayo ingepatwa na nini?

      14 Kabla hatujaweza kuelewa maana ya maneno yaliyotoka kunukuliwa, lazima tumsikilize malaika wa Mungu. Baada ya kutaja juu ya kupata mamlaka kwa zile falme nne zilizotokana na milki ya Aleksanda, malaika Gabrieli asema hivi: “Wakati wa mwisho wa ufalme wao, wakosao watakapotimia, mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo, atasimama. Na nguvu zake zitakuwa nyingi mno, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe; naye ataharibu kiasi cha kustaajabisha watu, na kufanikiwa, na kutenda apendavyo; naye atawaangamiza hao walio hodari na watu watakatifu. Na kwa mashauri yake atafanikisha hila mkononi mwake; naye atajitukuza nafsi yake moyoni mwake; naye atawaangamiza wengi katika hali yao ya salama; naye atasimama kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu; lakini atavunjika, bila kazi ya mikono.”—Danieli 8:23-25.

  • Ni Nani Awezaye Kusimama Dhidi ya mkuu wa Wakuu?
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
    • ILE PEMBE NDOGO YAPATA NGUVU NYINGI

      16. (a) Ile pembe ndogo ilitokana na pembe gani ya mfano? (b) Roma ilipataje kuwa serikali ya ulimwengu ya sita ya unabii wa Biblia, lakini kwa nini haikuwa ile pembe ndogo ya mfano?

      16 Kulingana na historia, ile pembe ndogo ilitokana na mojawapo ya zile pembe nne za mfano—ile pembe iliyokuwa mbali zaidi upande wa magharibi. Hiyo ilikuwa ufalme wa Kigiriki wa Jenerali Kasanda aliyetawala Makedonia na Ugiriki. Baadaye, ufalme huo ulitwaliwa na Jenerali Lisimako, mfalme wa Thrasi na Asia Ndogo. Katika karne ya pili kabla ya Wakati wetu wa Kawaida, maeneo hayo ya magharibi ya utawala wa Kigiriki yalishindwa na Roma. Na kufikia mwaka wa 30 K.W.K., milki ya Roma ilitwaa falme zote za Kigiriki, na hivyo kuwa serikali ya ulimwengu ya sita ya unabii wa Biblia. Lakini Milki ya Roma haikuwa ile pembe ndogo ya ono la Danieli, kwa kuwa milki hiyo haikuendelea kuwapo hadi “wakati wa mwisho ulioamriwa.”—Danieli 8:19.

      17. (a) Uingereza ilikuwa na uhusiano gani na Milki ya Roma? (b) Milki ya Uingereza yahusianaje na ufalme wa Makedonia na Ugiriki?

      17 Kwa hiyo, basi, historia yamtambulisha yule “mfalme mwenye uso mkali” na mwenye ujeuri kuwa nani? Uingereza ilichipuka upande wa kaskazini-magharibi kutoka katika Milki ya Roma. Kufikia mwanzoni mwa karne ya tano W.K., kulikuwa na mikoa ya Roma mahali ilipo Uingereza ya sasa. Hatimaye, Milki ya Roma ikadidimia, lakini ustaarabu wa Ugiriki na Roma uliendelea kuwa na uvutano katika Uingereza na katika sehemu nyingine za Ulaya zilizokuwa chini ya milki ya Roma. “Milki ya Roma ilipoanguka, Kanisa lilichukua mahali pake,” akaandika mshindi wa Tuzo la Nobeli Octavio Paz, mshairi aliyekuwa pia mwandishi huko Mexico. Aliongezea kusema hivi: “Wakuu wa Kanisa, na pia wasomi wa baadaye, waliingiza falsafa za Kigiriki katika fundisho la Kikristo.” Na mwanafalsafa aliye pia mwana-hisabati wa karne ya 20, Bertrand Russell alionelea hivi: “Ustaarabu wa Magharibi, uliotokana na Ugiriki, wategemea desturi za kifalsafa na kisayansi zilizoanzia Mileto [jiji la Kigiriki katika Asia Ndogo] miaka elfu mbili na nusu iliyopita.” Kwa hiyo, tungeweza kusema kwamba utamaduni wa Milki ya Uingereza ulitokana na ufalme wa Makedonia na Ugiriki.

      18. Ile pembe ndogo iliyopata kuwa “mfalme mwenye uso mkali” katika “wakati wa mwisho” ni nini? Fafanua.

      18 Kufikia mwaka wa 1763 Milki ya Uingereza ilikuwa imeshinda washindani wake wenye nguvu, Hispania na Ufaransa. Tangu wakati huo na kuendelea milki hiyo ilijidhihirisha kuwa mtawala wa bahari na pia serikali ya ulimwengu ya saba ya unabii wa Biblia. Hata baada ya zile koloni 13 za Amerika kujitenga na Uingereza mwaka wa 1776 na kuwa Marekani, Milki ya Uingereza ilipanuka na kufikia robo ya uso wa dunia na robo ya wakazi wa dunia. Serikali ya ulimwengu ya saba ilizidi kupata nguvu wakati ambapo Marekani ilishirikiana na Uingereza ili kufanyiza serikali ya ulimwengu ya Uingereza na Marekani. Kiuchumi na kijeshi, kwa kweli serikali hiyo ilikuwa imepata kuwa “mfalme mwenye uso mkali.” Kwa hiyo, ile pembe ndogo iliyokuwa kali kisiasa katika “wakati wa mwisho” ni Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani.

      19. “Nchi ya uzuri” inayotajwa katika ono ni nini?

      19 Danieli aliona kwamba ile pembe ndogo ‘ilikua sana’ kuelekea “upande wa nchi ya uzuri.” (Danieli 8:9) Lile Bara Lililoahidiwa, ambalo Yehova aliwapa wateule wake, lilikuwa zuri sana hivi kwamba liliitwa “utukufu wa nchi zote,” yaani, wa dunia yote. (Ezekieli 20:6, 15) Ni kweli kwamba Uingereza iliteka Yerusalemu Desemba 9, 1917, na katika mwaka wa 1920, Ushirika wa Mataifa uliipa Uingereza mamlaka juu ya Palestina, iendelee hadi Mei 14, 1948. Lakini ono hilo ni la kiunabii, na lenye ufanani mwingi. “Nchi ya uzuri” iliyotajwa katika ono yafananisha hali ya kidunia ya watu ambao Mungu awaona kuwa watakatifu wakati wa ile serikali ya saba ya ulimwengu, wala haifananishi Yerusalemu. Acheni tuone jinsi Serikali hii ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani inavyojaribu kuwatisha watakatifu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki