-
Sheria ya Mdomo—Kwa Nini Iliandikwa?Mnara wa Mlinzi—1999 | Januari 15
-
-
KWA nini Wayahudi wa karne ya kwanza walishindwa kumkubali Yesu kuwa Mesiya? Shahidi mmoja wa kujionea aripoti: “Baada ya [Yesu] kwenda ndani ya hekalu, makuhani wakuu na wanaume wazee wa watu wakamjia alipokuwa akifundisha nao wakasema: ‘Ni kwa mamlaka gani wewe wafanya mambo haya? Na ni nani aliyekupa wewe mamlaka hii?’” (Mathayo 21:23) Kwa maoni yao, Mweza Yote alikuwa amelipa taifa la Wayahudi Torati (Sheria), nayo iliwapa wanaume fulani mamlaka yenye kupewa na Mungu. Je, Yesu alikuwa na mamlaka hayo?
Yesu aliistahi sana Torati na pia wale ambao Torati hiyo iliwapa mamlaka ya kweli. (Mathayo 5:17-20; Luka 5:14; 17:14) Lakini mara nyingi alishutumu wale waliokiuka amri za Mungu. (Mathayo 15:3-9; 23:2-28) Wanaume hao walifuata mapokeo yaliyokuja kuitwa sheria ya mdomo. Yesu alikataa mamlaka ya sheria hiyo. Nao wengi wakakataa kuwa yeye ndiye Mesiya. Waliamini kwamba mtu aliyeunga mkono mapokeo ya wale waliokuwa mamlakani, ndiye tu angeweza kuungwa mkono na Mungu.
-
-
Sheria ya Mdomo—Kwa Nini Iliandikwa?Mnara wa Mlinzi—1999 | Januari 15
-
-
“Ni Nani Aliyekupa Wewe Mamlaka Hii?”
Kwa wazi, Sheria ya Kimusa iliwapa makuhani, wazao wa Aroni, mamlaka ya msingi ya kidini na ufundishaji. (Mambo ya Walawi 10:8-11; Kumbukumbu la Torati 24:8; 2 Mambo ya Nyakati 26:16-20; Malaki 2:7) Hata hivyo, kwa karne kadhaa zilizofuata, baadhi ya makuhani hao walikosa uaminifu, wakawa wafisadi. (1 Samweli 2:12-17, 22-29; Yeremia 5:31; Malaki 2:8, 9) Katika enzi ya kutawaliwa na Wagiriki, makuhani wengi waliridhiana kuhusiana na masuala ya kidini. Katika karne ya pili K.W.K., Mafarisayo—kikundi kipya ndani ya Dini ya Kiyahudi ambacho hakikuuamini ukuhani—kilianza kutokeza mapokeo ambayo kwake mtu wa kawaida angejiona kuwa mtakatifu sawa tu na kuhani. Mapokeo hayo yaliwavutia wengi, lakini yalikuwa mambo yasiyokubalika yaliyoongezwa kwenye Sheria.—Kumbukumbu la Torati 4:2; 12:32 (13:1 katika tafsiri za Kiyahudi).
Mafarisayo walikuja kuwa wasomi wapya wa Sheria, wakifanya kazi ambayo walihisi makuhani hawakuwa wakifanya. Kwa kuwa Sheria ya Kimusa haikuwaruhusu kuwa na mamlaka hayo, walitokeza njia mpya za kufasiri Maandiko kupitia vidokezi visivyoeleweka na njia nyinginezo zilizoonekana kuunga mkono maoni yao.a Wakiwa watunzaji na vilevile waendelezaji wakuu wa mapokeo haya, walitokeza msingi mpya wa mamlaka katika Israeli. Kufikia karne ya kwanza W.K., Mafarisayo walikuwa na nguvu nyingi katika Dini ya Kiyahudi.
Walipokusanya mapokeo ya mdomo yaliyokuwepo na kutafuta vidokezi vya Kimaandiko ili waanzishe mapokeo zaidi, yaliyokuwa yao wenyewe, Mafarisayo waliona uhitaji wa kuzidisha mamlaka ya utendaji wao. Dhana mpya kuhusu chanzo cha mapokeo haya ilianzishwa. Marabi walianza kufundisha hivi: “Musa aliipokea Torati katika Sinai, akaipitisha kwa Yoshua, Yoshua akaipitisha kwa wazee, nao wazee wakaipitisha kwa manabii. Nao manabii wakaipitisha kwa wanaume wa kusanyiko kubwa.”—Avot 1:1, Mishnah.
Kwa kusema, “Musa aliipokea Torati,” marabi hawakuwa wakirejezea sheria zilizoandikwa tu, bali pia mapokeo yao yote. Walidai kwamba Mungu alimpa Musa mapokeo hayo—yaliyobuniwa na kuendelezwa na wanadamu—huko Sinai. Nao walifundisha kwamba Mungu hakuwaruhusu wanadamu wafasili Torati, lakini alikuwa amefasili kwa maneno kile ambacho Sheria iliyoandikwa haikutaja. Kulingana nao, Musa alipitisha hiyo sheria ya mdomo kwa vizazi vingi na si kwa makuhani, bali kwa viongozi wengine. Mafarisayo wenyewe walidai kuwa warithi wa asili wa mamlaka hiyo iliyopitishwa kwa kufuatana bila “kuwepo na pengo.”
-