Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Alikata “Kauli Moyoni Mwake”
    Mnara wa Mlinzi—2008 | Oktoba 1
    • Maria na Yosefu walipata kijiji hicho kikiwa kimejaa watu. Wengi walikuwa wamefika mapema kabla yao ili kuandikishwa, kwa hiyo, hakukuwa na nafasi katika chumba cha kukaa.b Walilazimika kulala kwenye zizi. Tunaweza kuwazia jinsi Yosefu alivyohangaika alipomwona mke wake akiwa na uchungu mkali uliozidi kuongezeka. Uchungu wake wa kuzaa ulianzia papo hapo zizini.

      Wanawake ulimwenguni pote wanaweza kuelewa jinsi Maria alivyohisi. Miaka 4,000 hivi mapema, Yehova alikuwa ametabiri kwamba wanawake wangehisi uchungu walipokuwa wakizaa kwa sababu ya kurithi dhambi. (Mwanzo 3:16) Hakuna uthibitisho unaoonyesha kwamba Maria hakupata uchungu wa kuzaa. Simulizi la Luka halitaji uchungu ambao Maria alipata, linasema tu: “Akamzaa mwana wake, mzaliwa wa kwanza.” (Luka 2:7) Ndiyo, alikuwa amemzaa mwana “mzaliwa wa kwanza,” kati ya watoto wake saba hivi. (Marko 6:3) Hata hivyo, mwana huyu angekuwa wa pekee. Si eti alikuwa mwana wake mzaliwa wa kwanza tu bali pia alikuwa kwa Yehova “mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Mwana mzaliwa-pekee wa Mungu!—Wakolosai 1:15.

      Sasa simulizi hilo linataja jambo linalojulikana sana: “Akamfunga vitambaa na kumlaza katika hori.” (Luka 2:7) Ulimwenguni pote michezo ya kuigiza, michoro, na mandhari zinazoonyesha kuzaliwa kwa Yesu zinakazia sana tukio hilo. Hata hivyo, fikiria mambo haya ya hakika. Hori ni chombo cha kuweka chakula kwa ajili ya mifugo. Kwa hiyo, familia hiyo ilikuwa ikilala katika zizi ambalo kwa kawaida halina hewa au mazingira safi. Ni wazazi gani ambao wangechagua kumzaa mtoto wao mahali kama hapo ikiwa kungekuwa na mahali bora? Wazazi wengi wanataka kuwapa watoto wao vitu bora zaidi. Basi lazima Maria na Yosefu wawe walitaka kumzaa Mwana wa Mungu mahali bora zaidi!

      Hata hivyo, hawakuruhusu hali zao ziwakatishe tamaa; walifanya yote wawezayo. Kwa mfano, ona kwamba Maria alimtunza mtoto huyo na kumfunga kwa vitambaa ili awe na joto, kisha akamlaza kwa uangalifu ndani ya hori ili alale akihakikisha kwamba atakuwa salama. Maria hangeruhusu wasiwasi kuhusu hali yake imkengeushe asimwandalie mtoto wake kilicho bora. Pia, yeye na Yosefu walijua kwamba kumtunza mtoto huyo kiroho ndilo lingekuwa jambo muhimu zaidi ambalo wangeweza kumfanyia. (Kumbukumbu la Torati 6:6-8) Leo, wazazi wenye hekima wanatanguliza mambo ya kiroho wanapowalea watoto wao katika ulimwengu huu uliopotoka.

  • Alikata “Kauli Moyoni Mwake”
    Mnara wa Mlinzi—2008 | Oktoba 1
    • b Ilikuwa kawaida kwa miji kuwa na chumba cha kulala kwa ajili ya wasafiri.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki