Kioo Hufunua Nini?
TAZAMA kioo. Unaona nini? Nyakati nyingine, kutupia jicho kioo hufunua kasoro yenye kuaibisha katika sura yako ambayo unafurahi kuirekebisha kabla wengine hawajaiona.
Biblia inafanana sana na kioo. Inaweza kutusaidia kupata maoni manyoofu kujielekea, ambayo yatatuzuia kutofikiri mengi mno—au machache mno—juu ya kustahili kwetu machoni pa Mungu. (Mathayo 10:29-31; Warumi 12:3) Kuongezea hilo, Biblia inaweza kufunua kasoro katika maneno yetu, matendo, au mitazamo ambayo tunahitaji kurekebisha. Jambo hili litokeapo, je, utapuuza yale kioo chafunua?
Mwandikaji wa Biblia Yakobo asema: “Mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.”—Yakobo 1:23, 24.
Kinyume na hayo, Yakobo amfafanua mtu mwingine, “achunguaye ndani ya sheria kamilifu iliyo ya uhuru na ambaye hudumu katika hiyo.” (Yakobo 1:25, NW) Neno la Kigiriki lililotafsiriwa ‘chungua’ humaanisha kuinama kando au kuinama mbele ili kutazama. “Mengi zaidi ya kutupa jicho yanahusika katika maana hiyo,” yasema Theological Dictionary of the New Testament. Neno hilo lamaanisha kuchunguza kwa makini kitu kilichofichika. “Kuna kitu cha maana ambacho mtazamaji anatamani kuona, ingawa huenda ikawa vigumu kwake kukiona na kuelewa maana yacho mara moja tu,” aandika mfafanuzi wa Biblia R. V. G. Tasker.
Basi je, utajichunguza kwa kioo cha Neno la Mungu kisha uishi kulingana na yale linaagiza? Yakobo aendelea: “Mtu huyu, kwa sababu amekuwa, si msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, atakuwa mwenye furaha katika kutenda hiyo.”—Yakobo 1:25, NW.