-
Jinsi Mambo YalivyoanzaAmkeni!—2003 | Januari 8
-
-
Jinsi Mambo Yalivyoanza
JAMII ndogo ya watu inaishi katika eneo la Stratton huko Ohio, Marekani, karibu na Mto Ohio. Mto huo unapita kati ya jimbo la Ohio na jimbo la West Virginia. Stratton ni kijiji ambacho kina meya. Mnamo mwaka 1999, mgogoro ulizuka katika jamii hiyo ndogo yenye wakazi wasiofika 300 wakati wenye mamlaka wa eneo hilo walipojaribu kuwashurutisha Mashahidi wa Yehova, na wengine, kupata kibali kabla ya kuwatembelea watu nyumbani kwao kuwaeleza ujumbe wa Biblia.
Kwa nini hilo ni jambo zito? Unapoendelea kusoma simulizi hili, utaona kwamba amri hiyo ya wenye mamlaka haingedhibiti tu haki ya uhuru wa kusema ya Mashahidi wa Yehova bali pia ya watu wote wanaoishi Marekani.
Jinsi Mgogoro Huo Ulivyoanza
Wahudumu wa Kutaniko la Mashahidi wa Yehova la Wellsville lililo karibu walikuwa wamewatembelea wakazi wa Stratton kwa miaka mingi. Tangu mwaka 1979, wahudumu hao walikuwa wametatizwa na maafisa kadhaa wa eneo hilo kuhusu kazi yao ya kuhubiri nyumba hadi nyumba. Mapema katika miaka ya 1990, polisi mmoja wa eneo hilo alifukuza kikundi cha Mashahidi mjini, akisema: “Mimi sijali haki zenu.”
Mambo yalichacha mnamo mwaka 1998 wakati meya wa Stratton alipowakabili Mashahidi wanne wa Yehova ana kwa ana. Walikuwa wakitoka kwenye kijiji hicho kwa gari baada ya kuwatembelea tena wakazi waliopendezwa na mazungumzo ya Biblia. Kulingana na mmoja wa wanawake waliokabiliwa, meya alisema kwamba kama wangekuwa wanaume, angewafunga gerezani.
Mgogoro wa hivi majuzi ulisababishwa na amri ya wenye mamlaka wa kijiji hicho ambayo “Ilikataza Kuuza na Kuombaomba Kwenye Makao ya Watu Bila Ruhusa.” Amri hiyo ilisema kwamba watu wanaotaka kwenda nyumba hadi nyumba kufanya shughuli mbalimbali wanapaswa kupata kibali kutoka kwa meya bila malipo. Mashahidi wa Yehova walionelea kwamba amri hiyo inaingilia uhuru wa kusema, uhuru wa dini, na uhuru wa kusambaza habari. Basi, wakawasilisha kesi mbele ya mahakama ya serikali kwa kuwa wenye mamlaka wa kijiji hicho walikataa kubatilisha amri hiyo.
Mnamo Julai 27, 1999, kesi hiyo ilisikilizwa na jaji wa mahakama moja ya wilaya katika Wilaya ya Kusini ya Ohio. Jaji huyo aliamua kwamba amri hiyo ya kuomba kibali ni halali. Baadaye, mnamo Februari 20, 2001, Mahakama ya Rufaa ya Marekani ya Eneo la Sita iliamua tena kwamba amri hiyo inapatana na katiba.
Ili mgogoro huo utatuliwe, shirika la Watchtower Bible and Tract Society of New York na Kutaniko la Mashahidi wa Yehova la Wellsville liliomba Mahakama ya Juu ya Marekani isikilize tena kesi hiyo.
-
-
Mahakama ya Juu Yakubali Kusikiliza KesiAmkeni!—2003 | Januari 8
-
-
Mahakama ya Juu Yakubali Kusikiliza Kesi
KATIKA MIAKA YA HIVI MAJUZI, Mahakama ya Juu imekubali kusikiliza kesi 80 hadi 90 tu kila mwaka kati ya maombi zaidi ya 7,000 yanayofanywa. Hiyo ni asilimia 1 hivi ya maombi yote. Katika kesi hizo Mahakama hiyo hutoa hati rasmi inayoonyesha sababu za uamuzi wake.
Mnamo Mei 2001, Mashahidi wa Yehova waliwasilisha Maombi ya Hati ya Kuhawilisha Kesi (ruhusa ya kusikiliza tena kesi) kwenye Mahakama ya Juu, wakiuliza hivi: “Je, ni kweli kwamba kulingana na katiba wahudumu wa kidini wanaofanya kazi ya kueleza imani yao nyumba hadi nyumba ambayo inapatana na Maandiko na ambayo imefanywa kwa karne nyingi, wako sawa na wachuuzi wa bidhaa, na wanapaswa kupata kibali kutoka kwa manispaa ili kuongea kuhusu Biblia au kutoa vichapo vyao vya Biblia bila malipo?”
Mnamo Oktoba 15, 2001, Idara ya Sheria ya Watchtower ilifahamishwa kwamba Mahakama ya Juu ya Marekani imekubali kusikiliza upya kesi ya Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., et al. v. Village of Stratton et al!
Mahakama ilikubali kusikiliza kesi hiyo kwa msingi wa suala linalohusiana hasa na uhuru wa kusema, yaani, ikiwa kweli haki za uhuru wa kusema zilizo katika Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani zinatia ndani haki ya watu ya kuongea na wengine juu ya jambo fulani bila kuhitaji kujitambulisha kwa wawakilishi wa serikali.
Sasa mjadala wa kesi hiyo ungefanywa mbele ya majaji tisa wa Mahakama ya Juu ya Marekani. Mashahidi walileta mawakili wao, na Kijiji cha Stratton kilikuwa pia na mawakili. Ikawaje?
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
MAREKEBISHO YA KWANZA NI NINI?
“MAREKEBISHO YA KWANZA (KUANZISHA DINI; UHURU WA DINI, WA KUSEMA, WA KUSAMBAZA HABARI, WA KUKUSANYIKA, WA KUWASILISHA MAOMBI) Bunge halitatunga sheria yoyote kuhusiana na kuanzisha dini, wala kuwazuia watu kufuata dini kwa uhuru; wala kuwanyima uhuru wa kusema au wa kusambaza habari; au haki ya kukusanyika kwa amani, na kuomba Serikali iondoe kisababishi cha malalamiko yao.”—The U.S. Constitution (Katiba ya Marekani).
“Marekebisho ya Kwanza ndiyo msingi wa demokrasia nchini Marekani. Marekebisho ya Kwanza yanazuia Bunge kutunga sheria zinazodhibiti uhuru wa kusema, wa kusambaza habari, wa kukusanyika kwa amani, au wa kuwasilisha maombi. Watu wengi huonelea kwamba uhuru wa kusema ndiyo uhuru muhimu zaidi na msingi wa uhuru mwingine wowote. Marekebisho ya Kwanza pia yanazuia Bunge kutunga sheria ya kuanzisha dini ambayo inaungwa mkono na serikali au kuzuia uhuru wa dini.” (The World Book Encyclopedia) Yafaa kutambua kwamba uamuzi muhimu ulifanywa pia kuhusiana na Mashahidi wa Yehova katika kesi ya Cantwell v. Connecticut, 310 U.S. 296 (1940), wakati Mahakama ya Juu ya Marekani ilipoamua kwamba haki zilizo katika Marekebisho ya Kwanza zinazuia “Bunge la Marekani” (serikali) na vilevile mamlaka za mitaa (za serikali na za manispaa) kutunga sheria ambazo zitaingilia haki za Marekebisho ya Kwanza isivyo halali.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Suala lililohusika linaathiri shughuli mbalimbali za kwenda nyumba hadi nyumba
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
Photograph by Franz Jantzen, Collection of the Supreme Court of the United States
-
-
Hatua ya Kwanza Mjadala Katika Mahakama ya JuuAmkeni!—2003 | Januari 8
-
-
Hatua ya Kwanza Mjadala Katika Mahakama ya Juu
FEBRUARI 26, 2002, ndiyo siku ambayo mjadala wa kesi ulifanywa mbele ya Jaji Mkuu William Rehnquist na majaji wanane wengine wa Mahakama ya Juu. Mashahidi wa Yehova waliwakilishwa na mawakili wanne.
Wakili aliyeongoza upande wa Mashahidi alianza hoja zake kwa utangulizi wenye kuvuta fikira: “Tuseme hii ni siku ya Jumamosi mwendo wa saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Stratton. [Kisha akagonga kinara cha msemaji mara tatu.] ‘Habari za asubuhi. Kutokana na matukio ya hivi majuzi, nimekuja kwako kuzungumza nawe kuhusu jambo zuri ambalo Nabii Isaya alilitaja. Hiyo ni habari njema ambayo Kristo Yesu alizungumzia, habari njema ya Ufalme wa Mungu.’”
Aliendelea kusema: “Katika Kijiji cha Stratton, ni hatia kwenda nyumba hadi nyumba kuwaeleza watu ujumbe huo isipokuwa kwanza uwe umepata kibali cha wenye mamlaka wa kijiji hicho.”
‘Nyinyi Hamwombi Pesa?’
Jaji Stephen G. Breyer aliwauliza Mashahidi maswali hususa. Aliuliza hivi: “Je, ni kweli kwamba Mashahidi hawaombi pesa zozote, hata peni moja, na [kwamba] hawauzi Biblia, wala kitu chochote, kwamba wanataka tu kuzungumza na watu kuhusu dini?”
Wakili wa Mashahidi akajibu: “Mheshimiwa, mambo ya hakika yanaonyesha wazi kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuomba pesa katika Kijiji cha Stratton. Katika maeneo mengine, mambo ya hakika pia yanaonyesha kwamba nyakati nyingine wao hutaja mchango wa hiari. . . . Sisi hatuombi-ombi pesa. Tunataka tu kuzungumza na watu kuhusu Biblia.”
Je, Kibali cha Serikali Kinahitajiwa?
Jaji Antonin Scalia aliuliza hivi kwa busara: “Je, nyinyi mnaona kwamba hamhitaji kwenda kwa meya kumwomba ruhusa ya kuzungumza na majirani kuhusu habari ya kupendeza?” Wakili wa Mashahidi akajibu: “Hatufikiri kwamba Mahakama hii inapaswa kuruhusu amri ya Serikali ambayo inadai kwamba ni lazima raia apate leseni ili azungumze na raia mwenzake nyumbani mwake.”
Mjadala Wapamba Moto
Sasa ilikuwa zamu ya Kijiji cha Stratton kutoa malalamiko yake. Wakili aliyeongoza upande wa kijiji hicho alieleza amri ya Stratton kwa kusema hivi: “Stratton inatumia mamlaka yake ili kulinda faragha ya wakazi wake, na kuzuia uhalifu. Amri inayopinga kwenda kwenye makao ya watu ili kuombaomba inataka tu watu wasajiliwe kwanza na kubeba kibali wakati wanapoenda nyumba hadi nyumba.”
Jaji Scalia aliingia kwenye kiini cha kesi yenyewe alipouliza hivi: “Je, mnajua kesi nyingine [ya Mahakama ya Juu] iliyohusiana na amri ya aina hii, amri inayohusu kuombaomba, wala si kuomba pesa wala kuuza bidhaa, bali, kuwaeleza watu kuhusu Yesu Kristo, au kuongea juu ya kulinda mazingira? Je, tumewahi kushughulikia kesi ya aina hiyo?”
Jaji Scalia aliendelea kusema: “Sijawahi kusikia kesi ya aina hii kwa zaidi ya miaka 200.” Kisha Jaji Mkuu Rehnquist akamfanyia utani kwa kusema: “Hujaishi muda mrefu hivyo.” Maneno hayo yalisababisha kicheko mahakamani. Jaji Scalia akaendelea na hoja yake: “Sijawahi kamwe kusikia jambo la aina hii.”
Je, Unafikiri Hilo Ni Wazo Mwafaka?
Jaji Anthony M. Kennedy aliuliza swali hili hususa: “Je, unafikiri ni wazo mwafaka kwamba ni lazima niiombe Serikali ruhusa kabla ya kwenda mtaani, ambako sijui watu wote, ili niwaambie kwamba ningependa kuzungumza nao kwa sababu ninahangaikia ukusanyaji wa takataka, au juu ya Mbunge wetu, na kadhalika? Je, lazima niombe Serikali ruhusa kabla ya kufanya hivyo?” Kisha akaongeza hivi: “Hilo ni wazo la kiajabu.”
Kisha Jaji Sandra Day O’Connor akajiunga na mjadala huo, kwa kuuliza: “Vipi juu ya wale watoto ambao huenda nyumba hadi nyumba wakiomba peremende wakati wa sikukuu ya Halloween? Je, wanapaswa kupata kibali?” Jaji O’Connor na Jaji Scalia waliendelea kujadili wazo hilo. Jaji O’Connor alianzisha hoja nyingine: “Vipi juu ya kumwomba jirani yako sukari? Je, ninahitaji kwanza kupata kibali ili nimwombe jirani yangu sukari?”
Je, Mashahidi Ni Waombaji?
Jaji David H. Souter aliuliza: “Kwa nini amri hii inawahusu Mashahidi wa Yehova? Je, wao ni waombaji, wachuuzi, wafanyabiashara wanaozunguka mitaani wakiuza bidhaa au huduma? Wao si watu wa aina hiyo, sivyo?” Wakili wa Kijiji hicho alinukuu amri iliyotolewa na wenye mamlaka wa Stratton na akasema kwamba mahakama ya wilaya ilikuwa imewafafanua Mashahidi wa Yehova kuwa waombaji. Kisha Jaji Souter akaongeza: “Ikiwa mnawaona Mashahidi wa Yehova kuwa waombaji, basi mnaelewa neno waombaji kwa njia pana sana.”
Kisha Jaji Breyer akasoma ufafanuzi wa neno hilo katika kamusi ili kuonyesha kwamba haliwahusu Mashahidi. Halafu akaongeza: “Sijasoma hata jambo moja katika hati yenu ya malalamishi linaloonyesha kusudi la kuwataka watu hawa [Mashahidi wa Yehova] ambao hawaombi pesa, wala kuuza bidhaa, wala kuomba kura, waende kwenye ofisi ya baraza la jiji ili kusajiliwa. Kwani jiji lenu linataka nini?”
“Pendeleo” la Kuzungumza na Watu
Kisha wakili wa Kijiji hicho akasema kwamba “jiji linataka kuzuia wenye nyumba wasisumbuliwe.” Aliendelea kusema kwamba kusudi lilikuwa kuwalinda wakazi dhidi ya ulaghai na wahalifu. Jaji Scalia alinukuu amri iliyotolewa na wenye mamlaka wa kijiji kuonyesha kwamba meya anaweza kuomba habari zaidi kuhusu mtu anayetaka kusajiliwa na kuhusu kusudi lake ili “kubainisha kwa usahihi pendeleo analotaka.” Halafu akatoa kauli hii: “Eti ni pendeleo kwenda kuzungumza na raia wenzako kuhusu mambo mawili matatu—ni ajabu.”
Jaji Scalia alizidi kukazia hoja yake: “Kwa hiyo, je, kila mtu anayetumia kengele mlangoni anapaswa kwenda kwenye ofisi ya baraza la jiji ili alama zake za vidole zichukuliwe kabla hajabonyeza kengele mlangoni? Je, inafaa kuwalazimisha watu wote wanaotaka kubonyeza kengele mlangoni waende kwenye baraza la jiji ili wasajiliwe eti kwa sababu ya uwezekano mdogo wa kutokea kwa uhalifu? La hasha.”
Je, Amri Hiyo Iliwalinda Wakazi?
Baada ya dakika zake 20 kumalizika, wakili wa upande wa Kijiji cha Stratton aliacha mwanasheria mkuu wa jimbo la Ohio aendeleze mjadala huo. Mwanasheria huyo alibisha kwamba amri hiyo inayozuia kuombaomba iliwalinda wakazi wasitembelewe na mtu wasiyemjua, “mtu asiyealikwa, [ambaye] amekuja nyumbani.” Kisha akasema: “Ninafikiri kuwa wanakijiji wana haki ya kusema kwamba wana wasiwasi kuhusu shughuli ya aina hiyo.”
Jaji Scalia akasema: “Eti wanakijiji wanasema kwamba watu hawa [Mashahidi wa Yehova] bado wanahitaji kwenda kusajiliwa na meya ili wapate pendeleo la kuwatembelea watu nyumbani mwao, hata ingawa watu hao ambao wanawakaribisha Mashahidi wa Yehova wanahisi upweke na wangependa kuzungumza na mtu kuhusu jambo lolote.”
“Amri Isiyodai Mambo Mengi”
Wakati wa kuuliza maswali ya kuthibitisha ushahidi ulipofika, Jaji Scalia alitoa hoja nzito aliposema hivi: “Sote twaweza kukubali kwamba jamii salama zaidi ulimwenguni ni zile za udikteta. Hakuna uhalifu mwingi katika jamii hizo. Huu ndio ukweli wa mambo. Hasara moja inayosababishwa na uhuru katika jamii ni uhalifu mwingi. Basi suala ni hili, je, amri hii inaweza kuzuia uhalifu vya kutosha hivi kwamba inafaa kuwashurutisha watu kuomba ruhusa ili kutembelea nyumba za watu?” Kisha mwanasheria mkuu akajibu kwa kusema kwamba hiyo ni “amri isiyodai mambo mengi.” Naye Jaji Scalia akajibu kwamba ikiwa amri hiyo haidai mengi mno mbona “hakuna hata manispaa moja ambayo imewahi kutoa amri kama hiyo. Kwa maoni yangu, huko ni kudai mengi mno.”
Hatimaye, baada ya kushinikizwa na jaji mmoja, mwanasheria mkuu alilazimika kukubali hivi: “Siwezi kusema kwa uhakika kwamba unaweza kuwazuia watu kabisa wasibonyeze kengele mlangoni au kubisha hodi.” Na hoja yake ikakomea hapo.
Wakati wa kukanusha hoja ulipofika, wakili wa Mashahidi alisema kwamba amri hiyo haina njia ya kuhakikisha ikiwa mtu anasema kweli au uwongo. “Ninaweza kwenda kwenye ofisi za usimamizi wa kijiji hicho na niseme, ‘Mimi ni [Fulani wa Fulani],’ kisha nipate kibali cha kwenda nyumba hadi nyumba.” Pia alitaja kwamba meya ana mamlaka ya kutompa kibali mtu anayesema kwamba yeye si mshiriki wa shirika lolote. Wakili huyo alisema: “Tunaamini kwamba kufanya hivyo ni kutumia mamlaka kuwaamulia wengine mambo.” Kisha akaongeza hivi: “Ninasema kwa heshima kwamba shughuli yetu [Mashahidi wa Yehova] inahusiana kabisa na kiini cha Marekebisho ya Kwanza.”
Muda mfupi baadaye, Jaji Mkuu Rehnquist alifunga mjadala huo kwa kusema: “Kesi hii imewasilishwa [kwa Mahakama ya Juu].” Mjadala huo ulichukua zaidi ya saa moja tu. Umuhimu wa saa hiyo umeonyeshwa katika hati yenye uamuzi ambayo ilitangazwa mwezi Juni.
[Picha katika ukurasa wa 6]
Jaji Mkuu Rehnquist
Jaji Breyer
Jaji Scalia
[Credit lines]
Rehnquist: Collection, The Supreme Court Historical Society/Dane Penland; Breyer: Collection, The Supreme Court Historical Society/Richard Strauss; Scalia: Collection, The Supreme Court Historical Society/Joseph Lavenburg
[Picha katika ukurasa wa 7]
Jaji Souter
Jaji Kennedy
Jaji O’Connor
[Hisani]
Kennedy: Collection, The Supreme Court Historical Society/Robin Reid; O’Connor: Collection, The Supreme Court Historical Society/Richard Strauss; Souter: Collection, The Supreme Court Historical Society/Joseph Bailey
[Picha katika ukurasa wa 8]
Ndani ya mahakama
[Hisani]
Photograph by Franz Jantzen, Collection of the Supreme Court of the United States
-
-
Mahakama ya Juu Yatetea Uhuru wa KusemaAmkeni!—2003 | Januari 8
-
-
Mahakama ya Juu Yatetea Uhuru wa Kusema
JUNI 17, 2002, ilikuwa siku muhimu wakati ambapo Mahakama ya Juu ilichapisha hati yenye uamuzi wake. Mahakama iliamuaje? Vichwa vya habari magazetini vilitangaza uamuzi huo. Gazeti The New York Times lilitangaza hivi: “Mahakama Yaondoa Vizuizi vya Ziara za Mashahidi wa Yehova.” Gazeti The Columbus Dispatch la Ohio lilisema: “Mahakama Kuu Yabatilisha Amri ya Kutaka Kibali.” Gazeti The Plain Dealer la Cleveland, Ohio, lilikuwa na kichwa hiki sahili: “Waombaji Hawahitaji Kibali cha Baraza la Jiji.” Na katika gazeti USA Today, ukurasa unaoambatana na ule wa mhariri ulitangaza hivi: “Uhuru wa Kusema Washinda.”
Maamuzi ya mahakama za chini dhidi ya Mashahidi wa Yehova yalibatilishwa kwa kura ya 8 kwa 1! Hati rasmi yenye uamuzi wa Mahakama ambayo ilikuwa na kurasa 18, iliandikwa na Jaji John Paul Stevens. Kwa mara nyingine tena, uamuzi huo uliunga mkono haki zinazoonyeshwa katika Marekebisho ya Kwanza ambazo zinatetea huduma ya hadharani ya Mashahidi wa Yehova. Katika hati hiyo, Mahakama ilieleza kwamba Mashahidi hawakuomba kibali kwa sababu wanadai kuwa “mamlaka yao ya kuhubiri inatoka katika Maandiko.” Kisha Mahakama ikanukuu ushahidi uliotolewa katika hati ya malalamishi ya Mashahidi: “Kwa maoni yetu, kuomba kibali cha manispaa ili kuhubiri ni kama kumtukana Mungu.”
Hati yenye uamuzi wa Mahakama ilisema: “Kwa zaidi ya miaka 50, Mahakama imeondoa vizuizi vya kwenda nyumba hadi nyumba na kugawanya vijitabu. Haishangazi kwamba kesi nyingi kati ya hizo zilihusu haki za Marekebisho ya Kwanza zilizowasilishwa na Mashahidi wa Yehova, kwani dini yao inawataka waende kuzungumza na watu nyumba hadi nyumba. Kama tulivyoona katika kesi ya Murdock v. Pennsylvania,. . . (1943), Mashahidi wa Yehova wanadai kufuata mfano wa Paulo, kwa kufundisha “hadharani na kutoka nyumba hadi nyumba.” Matendo 20:20. Wanafuata kabisa agizo hili la Maandiko, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.” Marko 16:15. Kwa kufanya hivyo wanaamini kwamba wanatii amri ya Mungu.’”
Kisha Hati yenye uamuzi ikanukuu tena kesi ya mwaka 1943: “Katika Marekebisho ya Kwanza, shughuli hiyo ya kidini ina umuhimu uleule kama ibada inayofanywa makanisani na mahubiri yanayofanywa na mapadri. Haki zinazohusu shughuli nyingine za kawaida za kidini ambazo zinakubalika zinahusu pia shughuli hiyo.” Hati hiyo pia ilinukuu kesi nyingine ya mwaka 1939 iliyosema: ‘Kuweka mipaka kwa kuwadai watu wapate leseni huzuia ugawanyaji wa vijitabu kwa uhuru na bila vizuizi na kuingilia haki za msingi za kikatiba.’
Kisha Mahakama ikatoa taarifa hii muhimu: “Kesi hizo zinaonyesha kwamba kwa kupinga vizuizi vya uhuru wa kusema Mashahidi wa Yehova hawajapigania haki zao wenyewe tu.” Hati hiyo ilieleza kwamba ‘si Mashahidi tu wanaokabili hatari ya kunyamazishwa na amri kama ile iliyotolewa na wenye mamlaka wa Stratton.’
Hati hiyo iliendelea kusema kwamba amri hiyo “inadharau kanuni zinazotetewa na Marekebisho ya Kwanza na vilevile wazo la kuwa na jamii huru. Ni jambo lenye kuudhi kwamba katika mazungumzo ya kawaida, raia anapaswa kwanza kuifahamisha serikali kuwa angependa kuzungumza na majirani wake kisha apate kibali cha kufanya hivyo. . . . Sheria inayodai watu wapate kibali ili wawe na mazungumzo hayo inakiuka kabisa urithi wetu wa kitaifa na katiba yetu.” Kisha Hati hiyo ikataja “athari kubwa sana za amri hiyo ya kupata kibali.”
Hatari ya Uhalifu
Vipi juu ya yale maoni ya kwamba kibali hicho kinawalinda watu dhidi ya wakora wanaovunja nyumba na wahalifu wengine? Mahakama ilitoa kauli hii: “Ijapokuwa tunakubali kwamba mahangaiko hayo ni ya kweli, kesi zinazotangulia zinaonyesha wazi kwamba tunapaswa kuwa na usawaziko tunapozingatia mahangaiko hayo na vilevile jinsi ambavyo amri zinazotolewa zinavyoathiri haki za Marekebisho ya Kwanza.”
Hati hiyo ya Mahakama iliendelea kusema: “Haielekei kwamba wahalifu watazuiwa wasifike kwenye nyumba za watu na kuzungumza mambo ambayo hayakutajwa katika amri hiyo eti kwa sababu hawana kibali. Wahalifu wanaweza kuomba waonyeshwe njia au kuomba ruhusa ya kutumia simu, . . . au huenda wakapata kibali kwa kutumia jina bandia na waepuke kuadhibiwa.”
Kwa kurejelea maamuzi yaliyofanywa katika miaka ya 1940, Mahakama iliandika hivi: “Maneno yaliyo katika hati za maamuzi za kipindi cha Vita ya Pili ya Ulimwengu ambazo zilizuia washiriki wenzi wa walalamishi [Watch Tower Society] wasishtakiwe kwa mashtaka madogo-madogo, yanaonyesha jinsi Mahakama inavyozingatia haki zinazopatikana katika Marekebisho ya Kwanza ambazo zinahusiana na kesi hii.”
Uamuzi wa mwisho wa Mahakama ulikuwa nini? “Hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa imebatilishwa, na kesi imerudishwa kwenye mahakama hiyo ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe kupatana na hati hii. Hiyo ndiyo amri ya mahakama.”
Basi, kama ilivyotaarifiwa katika gazeti Chicago Sun-Times, ‘Mahakama Iliunga Mkono Mashahidi wa Yehova,’ kwa kura ya 8 kwa 1.
Vipi Juu ya Wakati Ujao?
Mashahidi wa Yehova katika Kutaniko jirani la Wellsville wameuonaje ushindi huo mbele ya Mahakama ya Juu? Ama kweli, hawana haja ya kujivuna wala kuwaaibisha wakazi wa Stratton kwa sababu ya ushindi wao. Mashahidi hawana kinyongo na wakazi wenye kuheshimika wa kijiji hicho. Gregory Kuhar, Shahidi anayekaa katika eneo hilo, alisema: “Hatukudhamiria kuwa na kesi kama hiyo. Amri ya kijiji ndiyo haikuwa halali. Yale tuliyoyafanya hayakuwa kwa faida yetu tu, bali kwa faida ya watu wote.”
Mambo ya hakika yanaonyesha kwamba Mashahidi wameepuka kabisa kuwachokoza wanakijiji hao. Shahidi mwingine anayeitwa Gene Koontz alieleza hivi: “Mara yetu ya mwisho kuhubiri Stratton ilikuwa Machi 7, 1998—zaidi ya miaka minne iliyopita.” Aliongeza hivi: “Niliambiwa kwamba ningekamatwa. Katika miaka iliyopita, ripoti nyingi zilionyesha kwamba polisi walitaka kutukamata. Halafu tulipoomba tuonyeshwe hati rasmi yenye amri hiyo, hatukupata majibu.”
Koontz aliongeza hivi: “Tungependa kuwa na uhusiano mwema na majirani wetu. Ikiwa wengine hawataki tuwatembelee, tunaheshimu uamuzi wao. Lakini kuna wengine ambao ni wenye urafiki na wangetaka tuzungumze nao kuhusu Biblia.”
Gregory Kuhar alieleza hivi: “Hatukufuatilia kesi hiyo ili kuwaudhi wenyeji wa Stratton. Tulitaka tu kutetea kisheria uhuru wetu wa kusema kupatana na Katiba.”
Aliendelea kusema: “Muda si muda, tunatarajia kurudi Stratton. Ningependa kuwa wa kwanza kubisha mlango tunaporudi huko. Kwa kupatana na amri ya Kristo, ni lazima turudi.”
Kesi ya “Watchtower v. Village of Stratton” imekuwa na matokeo makubwa. Baada ya kupata habari kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Juu, maafisa kadhaa wa manispaa huko Marekani walitambua kwamba sheria fulani katika maeneo yao hazistahili tena kutumiwa kuzuia kazi ya kuhubiri ya Mashahidi wa Yehova. Kufikia sasa, vizuizi vya kuhubiri nyumba hadi nyumba vimeondolewa katika maeneo 90 hivi ya Marekani.
-