Pimbi-Wadogo—Wapendeka na Ni Wenye Hekima ya Kisilika
Na mleta habari za Amkeni! katika Afrika Kusini
NI VIUMBE vipi ambavyo Biblia hutaja kuwa “vina akili nyingi sana [vyenye hekima ya kisilika, NW] . . . dhaifu; lakini hujifanyia nyumba katika miamba.” Jamaa hawa wa kutokeza walio wadogo, wenye ukubwa unaokaribia wa sungura, huitwa wibari katika tafsiri mbalimbali za Biblia.—Mithali 30:24-26.
Pimbi-mdogo ni wibari, anayepatikana katika sehemu za Afrika na ncha ya kusini-magharibi ya Asia. Katika Afrika ya Kusini, anakopatikana kwa wingi sana, yeye huitwa rock dasie, jina linalotolewa kwa neno la Kiholanzi kwa “wibari.”
Ingawa dassie hufanana kidogo na jamii ya panya, wana sura fulani ambazo kwa kweli ni “mchanganyiko wa kila kitu,” kulingana na mwanasayansi Gerrie de Graaff. “Meno yao ya chonge yafanana na yale ya jamii ya panya, magego kama yale ya kifaru, mfumo wao wa mishipa ya damu kama ule wa nyangumi na nyayo zao kama zile za ndovu!” Si ajabu wanashangaza wataalamu wa wanyama!
Kwa kuwa wao si wanyama wenye mwendo wa kasi, wala hawawezi kujikinga wenyewe vizuri sana, kwa hekima dassie huishi katika miamba na mianya ya michongoko ya miamba au majabali. Hiyo hutoa kinga kutokana na upepo na mvua, na pia ulinzi kutokana na wanaomwinda. Basi, yaeleweka ni mara chache wanathubutu kwenda mbali nje isipokuwa kwa ajili ya milo yao miwili mikubwa katika siku moja.
Nayo ni milo iliyoje! Kiasi cha mimea wanachokula ni cha kustaajabisha sana, kwa viumbe wadogo kama wao. Hata cha kustaajabisha zaidi ni haraka ile wanayokibugia chote. Lo! wanatumia muda unaopungua saa moja kwa siku kufanya hivyo! Na mfumo wao wa kusaga chakula, ambao hupatana vizuri na tabia hiyo, waelezwa na mtaalamu wa wanyama J.J.C. Sauer kuwa wa “kipekee katika milki ya wanyama.”
Si Mlo Rahisi
Dassie huonekana kwa kawaida katika maeneo ya miamba, wakiwa wanafanana sana na miamba yenyewe, wakiota jua jangavu la Afrika. Wanashawisha sana tai mweusi, ambaye anapendelea sana dassie. Lakini jamaa huyu mdogo hanaswi rahisi hivyo. Macho yake ni makali sana hivi kwamba aweza kuona kitu kinachosonga kikiwa umbali unaozidi meta 800! Na hata kikiwa tai anaruka jua likiwa nyuma yake, dassie atamwona. Yawezekanaje? Macho yake yametiwa utando wa pekee unaochuja miale ya jua, ukimwezesha atazame jua moja kwa moja bila ya dhara lolote. Adui akiisha kuonekana mara moja onyo linatolewa—mbweko mwembamba unaotolewa na dassie anayeshika doria—na bila kukawia miamba inaachwa tupu, dassie wote wakiwa wameingia ndani ya mianya iliyo katikati na chini ya miamba. Tai atalazimika kujaribu tena kupata mlo wake.
Ni Wenye Ushirikiano Sana
Maisha ya jumuiya—ni faida kama nini wakati wa usiku dassie wanapohisi baridi! Inasaidia sana kulala pamoja na dassie wenzi, wakiwa wamekaribiana sana, wote wakielekeza vichwa mbali na wenzao. Huenda hata wengine wakajirundika juu ya kile kikundi kilicholala karibu-karibu hadi kunapokuwa orofa tatu au nne za dassie—kufikia 25 kwa wakati mmoja—wakipashana joto!
Hata hivyo, hilo laweza kuwa na hasara zalo kwa kuwa wao ni wanyama wadogo wenye kupenda vita. Lakini hekima yao ya kisilika huwaponyoa. Dakt. P. B Fourie aeleza hivi: “Kwa kawaida wao hulala vichwa vyao vikielekea mbali na mwingine, hawali wakiwa wamekaribiana na hutoa milio mbalimbali ya kutuliza wanapolazimika kupitia karibu ya mmoja na mwenzake.” Na kwa sababu milio yao kwa kawaida si ya sauti nyembamba na yaweza kusikiwa tu umbali wa meta chache, wanaweza kuwasiliana bila ya kuvutia wanaowawinda.
Wanyama wa Kufugwa Wepesi kwa Mwendo na wa Kupendeka
Watazamaji wengi wamestaajabishwa na jinsi dassie wanavyoweza kukimbia wakikwea mwamba wenye utelezi ambao umekaribia kusimama imara. Wao hufanyaje hivyo? Kwa kuunda nyayo zao, ambazo zina visigino vipana, vilivyo laini vikawa vyenye mshikilio. Na kwa sababu nyayo zao huwa na umaji-maji sikuzote, vikiwa ndivyo visehemu pekee vya mwili vinavyotoa jasho, mkamato huwa wenye nguvu zaidi.
Viumbe hivi vyenye kupendeka vinafugika kwa urahisi. Na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya usafi wavyo—hujisafisha daima kwa uwayo wa nyuma, ambao una ukucha mdogo unaofaa hasa kwa ajili ya kusudi hilo. Katika kitabu chake Born Free, Joy Adamson akiri alishangazwa hapo kwanza kwa kuwa dassie wake aliyefuga alikuwa na tabia ya kujikuna. Baadaye akatambua kwamba kwa ukucha huo, dassie huyo alilainisha manyoya yake, hivi kwamba wala kiroboto wala kupe hakuweza kupatikana juu yake kamwe.
Mtu angeweza kumfunzaje dassie wa kufugwa kutoenda choo popote? Hakuna haja. Kule porini, wao huweka kando mahali fulani hususa pa kutumiwa kuwa choo na jamii yote. Kwa hiyo wakiwa wa kufugwa, dassie “hujifunza mara moja kutumia choo,” aeleza Fourie. “Bila shaka, hawapigi maji!” aongezea. Na ndivyo ilivyokuwa na dassie wa Joy Adamson. “Tabia zake za kwenda haja zilikuwa za pekee . . . Nyumbani sikuzote Pati alijipachika kwenye ncha ya kikalio cha choo, na akiwa ameketi hivyo alionekana mwenye kuchekesha. Wakati wa safari ambapo vifaa hivyo havikutolewa kwake, aliduwaa kabisa, kwa hiyo hatimaye tulilazimika kuigiza choo kidogo kwa ajili yake.”
Jinsi itakavyopendeza baada ya wakati fulani kuweza kuzoeleana kikamili na viumbe hao pamoja na wengine ambao Yehova amewafanya kuwa ‘wenye hekima kisilika’!