-
Uguo Kali Katika BustaniYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 117
Uguo Kali Katika Bustani
YESU amalizapo kusali, yeye na mitume wake waaminifu 11 wamwimbia Yehova nyimbo za sifa. Halafu washuka kutoka chumba cha juu, na kuingia ndani ya giza la usiku lenye baridi, na kusonga mbele warudi ng’ambo ya Bonde la Kidroni kuelekea Bethania. Lakini wakiwa njiani, wasimama mahali wapapendapo sana, bustani ya Gethsemane. Iko juu ya au katika ujirani wa Mlima wa Mizeituni. Mara nyingi Yesu amekutana na mitume wake hapa katikati ya mizeituni.
Akiacha wanane wa mitume—labda karibu na mwingilio wa bustani—yeye awaagiza hivi: “Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.” Halafu awachukua wale wengine watatu—Petro, Yakobo, na Yohana—na kusonga mbali zaidi katika bustani. Yesu aingiwa na kihoro na kufadhaika sana. “Roho [nafsi, NW] yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa,” awaambia. “Kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”
Akisonga mbele kidogo, Yesu ajibwaga chini kifudifudi na kuanza kusali hivi kwa moyo wa bidii: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” Amaanisha nini? Kwa nini ‘ana huzuni nyingi kiasi cha kufa’? Je! anaepa uamuzi wake wa kufa na kuandaa ukombozi?
Sivyo hata kidogo! Yesu hasihi kwamba aepushwe na kifo. Hata ile fikira ya kuepuka kifo cha dhabihu, iliyodokezwa na Petro wakati mmoja, yamchukiza sana. Bali, yeye ana uguo kali kwa sababu ahofu kwamba njia ambayo karibuni atakufa kwayo—akiwa mhalifu mwenye kudharaulika—italeta suto juu ya jina la Baba yake. Sasa yeye ahisi kwamba katika muda wa saa chache atatundikwa juu ya mti kama mtu wa aina mbaya kabisa—mkufuru dhidi ya Mungu! Hilo ndilo lamfadhaisha sana.
Baada ya kusali kirefu, Yesu arudi na kukuta wale mitume watatu wamelala. Akielekeza maneno kwa Petro, yeye asema hivi: “Je! hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni.” Hata hivyo, akikiri kwamba wamekuwa chini ya mkazo na kwamba usiku umendelea sana, asema hivi: “Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Ndipo Yesu aenda zake mara ya pili na kuomba kwamba Mungu amwondolee “kikombe hiki,” yaani, kisehemu au mapenzi aliyogawiwa na Yehova. Arudipo, akuta tena wale watatu wamelala wakati ambapo wangalipaswa kuwa wakisali ili wasiingie katika kishawishi. Yesu asemapo nao, hawajui la kumjibu.
Mwishowe, mara ya tatu, Yesu aenda umbali kama ule unaoweza kutupa jiwe, na akiwa amepiga magoti na kwa vilio vikali na machozi, asali hivi: “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki.” Yesu ahisi maumivu makali kwa sababu ya suto ambalo kifo chake kama mhalifu kitaleta juu ya jina la Baba yake. Kwani, kushtakiwa kuwa mkufuru—mtu alaaniye Mungu—ni jambo linalokaribia sana kutoweza kuvumilika!
Hata hivyo, Yesu aendelea kusali hivi: “Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” Kwa utiifu Yesu atiisha mapenzi yake kwa yale ya Mungu. Iwapo hivyo, malaika kutoka mbinguni atokea na kumwimarisha kwa maneno ya kutia moyo. Yaelekea, malaika amwambia Yesu kwamba yeye ana tabasamu ya kibali cha Baba yake.
Hata hivyo, mabega ya Yesu yalemewa na uzito ulioje! Uhai wa milele wake mwenyewe na wa jamii nzima ya kibinadamu umo katika hatari ya kuponyoka. Mkazo wa kihisia-moyo ni mwingi mno. Hivyo basi Yesu aendelea kusali kwa moyo wa bidii zaidi, na jasho lake lawa kama matone ya damu liangukapo chini. “Ingawa hii ni ajabu itukiayo mara chache sana,” lasema The Journal of the American Medical Association, “jasho lenye damu . . . laweza kutukia katika hali zenye hisia-moyo nyingi.”
Baadaye, Yesu awarudia mitume wake mara ya tatu, na tena awakuta wamelala. Wamenyong’onyea kwa kuwa na kihoro kibisa. “Laleni sasa, mpumzike [wakati wa jinsi hii nyinyi mnalala na kupata pumziko lenu, NW]!” yeye apaaza mshangao. “Yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu [wa binadamu, NW] anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.”
Huku akiwa angali katika kusema, Yuda Iskariote akaribia, ameandamwa na umati mkubwa uliochukua mienge na taa na silaha. Mathayo 26:30, 36-47; 16:21-23; Marko 14:26, 32-43; Luka 22:39-47; Yohana 18:1-3; Waebrania 5:7.
▪ Baada ya kuondoka kwenye chumba cha juu, Yesu awaongoza mitume wapi, naye afanya nini huko?
▪ Huku Yesu akiwa katika kusali, mitume wanafanya nini?
▪ Kwa nini Yesu ana uguo kali, naye amwomba Mungu nini?
▪ Ni nini chaonyeshwa na kuwa kwa jasho la Yesu kama matone ya damu?
-
-
Kusalitiwa na KukamatwaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 118
Kusalitiwa na Kukamatwa
UMEPITA sana katikati ya usiku wakati Yuda aongozapo umati mkubwa wa askari, wakuu wa makuhani, Mafarisayo, na wengine kuingia katika bustani ya Gethsemane. Makuhani wameafikiana na Yuda kumlipa vipande 30 vya fedha ili amsaliti Yesu.
Mapema kidogo, Yuda alipoagizwa aondoke kwenye mlo wa Sikukuu ya Kupitwa, kwa wazi aliwaendea moja kwa moja wakuu wa makuhani. Nao wakawakusanya maofisa wao wenyewe mara hiyo, na pia kikosi cha askari. Labda kwanza Yuda aliwaongoza mahali Yesu na mitume walikuwa wameadhimisha Sikukuu ya Kupitwa. Kwa kugundua kwamba walikuwa wameondoka, ule umati mkubwa wenye kubeba silaha na kuchukua taa na mienge ulimfuata Yuda kutoka Yerusalemu na kwenda ng’ambo ya Bonde la Kidroni.
Yuda aongozapo msafara huo kuupanda Mlima wa Mizeituni, ahisi akiwa na uhakika kwamba ajua mahali pa kumpata Yesu. Wakati wa juma lililopita, Yesu na mitume walipokuwa wakisafiri huku na huku kati ya Bethania na Yerusalemu, walisimama mara nyingi katika bustani ya Gethsemane kupumzika na kuongea. Lakini, sasa, kukiwa na uwezekano wa kwamba Yesu amefichika gizani chinichini ya ile mizeituni, askari watamtambuaje? Huenda ikawa walikuwa hawajapata kumwona kamwe. Hivyo Yuda aandaa ishara, akisema: “Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.”
Yuda aongoza ule umati mkubwa kuingia bustanini, amwona Yesu pamoja na mitume wake, na kumwendea moja kwa moja. “Salamu [Siku njema, NW] Rabi,” asema na kumbusu kwa wororo sana.
“Rafiki, fanya ulilolijia [Jamaa, wewe upo hapa kwa kusudi gani?, NW] Yesu ajibu vikali. Ndipo, akijibu swali lake mwenyewe, asema hivi: “Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu [wa binadamu, NW] kwa kumbusu?” Lakini hataki mengi zaidi na msaliti wake! Yesu apiga hatua mbele kuingia katika ile nuru ya mienge na taa zinazowaka na kuuliza hivi: “Ni nani mnayemtafuta?”
“Ni Yesu Mnazareti,” jibu laja.
“Ni mimi,” Yesu ajibu, huku akisimama kwa moyo mkuu mbele yao wote. Kwa kugutushwa na ujasiri wake na bila kujua watarajie nini, wanaume hao warudi nyuma na kuanguka chini.
“Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi,” Yesu aendelea kwa utulivu. “Basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” Kitambo kifupi kabla ya hapo akiwa katika kile chumba cha juu, Yesu alikuwa amemwambia Baba yake katika sala kwamba alikuwa amewatunza mitume wake waaminifu na hakuna hata mmoja wao aliyekuwa amepotezwa “ila yule mwana wa upotevu [uharibifu, NW].” Hivyo basi, ili neno lake liweze kutimizwa, yeye aomba kwamba wafuasi wake waachwe waende zao.
Askari wanaporudiwa na umakini wao, wasimama, na kuanza kumfunga Yesu, mitume watambua likaribialo kutendeka. “Bwana, tuwapige kwa upanga?” wao wauliza. Kabla Yesu hajajibu, Petro, akitumia mmoja wa panga mbili ambazo mitume wameleta, amshambulia Malko, mtumwa wa kuhani wa juu. Pigo la Petro lakikosa kichwa cha mtumwa huyo lakini akata sikio lake la kulia.
“Mwe radhi kwa hili [acheni ifike hapo, NW],” Yesu asema akiingilia. Kwa kugusa sikio hilo, aponya lile jeraha. Halafu afundisha somo la maana, akimwamuru Petro hivi: “Rudisha upanga wako mahali pake; maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?”
Yesu ana nia ya kukamatwa, kwa maana aeleza hivi: “Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?” Na aongeza hivi: “Je! kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” Yeye aafikiana kabisa na mapenzi ya Mungu kwake!
Halafu Yesu aelekeza maneno yake kwenye ule umati. “Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika?” auliza. “Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe.”
Hapo kile kikosi cha askari na yule amiri wa kijeshi na wale maofisa wa Wayahudi wamkamata Yesu na kumfunga. Kuona hilo, mitume wamwacha Yesu na kukimbia. Hata hivyo, mwanamume kijana—yaelekea ni mwanafunzi Marko—abaki miongoni mwa umati. Huenda akawa alikuwa kwenye makao ambapo Yesu aliadhimisha Sikukuu ya Kupitwa na baadaye akaufuata umati kutoka huko. Hata hivyo, sasa yeye atambuliwa, na jaribio la kumkamata lafanywa. Lakini yeye aacha nyuma vazi lake la kitani na kutoroka. Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-52; Luka 22:47-53; Yohana 17:12; 18:3-12.
▪ Kwa nini Yuda ahisi akiwa na uhakika kwamba atampata Yesu katika bustani ya Gethsemane?
▪ Yesu adhihirishaje hangaiko kwa ajili ya mitume wake?
▪ Petro afanya kitendo gani kumkinga Yesu, lakini Yesu asema nini kwa Petro kukihusu?
▪ Yesu afunuaje kwamba yeye aafikiana kabisa na mapenzi ya Mungu kwake?
▪ Mitume wamwachapo Yesu, nani abaki, naye apatwa na nini?
-
-
Apelekwa kwa Anasi, Kisha kwa KayafaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 119
Apelekwa kwa Anasi, Kisha kwa Kayafa
YESU, akiwa amefungwa kama mhalifu wa kawaida, aongozwa kwenda kwa Anasi, ambaye hapo kwanza alikuwa kuhani mkuu aliye mashuhuri. Anasi alikuwa kuhani mkuu wakati Yesu akiwa kivulana wa miaka 12 aliwastaajabisha walimu wa kirabi hekaluni. Wana kadhaa wa Anasi walitumikia baadaye wakiwa makuhani wakuu, na wakati uliopo Kayafa mwana-mkwe wake ashikilia cheo hicho.
Labda kwanza Yesu aongozwa kwenda nyumbani kwa Anasi kwa sababu ya umashuhuri wa muda mrefu wa huyo aliye mkuu wa makuhani katika maisha ya kidini ya Kiyahudi. Kituo hiki cha kumwona Anasi chamruhusu wakati Kayafa Kuhani Mkuu kuikusanya Sanhedrini, ile mahakama kuu ya Kiyahudi yenye washiriki 71, na pia kukusanya mashahidi bandia.
Sasa Anasi kuhani mkuu amuuliza Yesu maswali juu ya wanafunzi wake na juu ya fundisho lake. Hata hivyo, Yesu asema hivi kwa kujibu: “Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.”
Hapo, mmoja wa maofisa waliosimama karibu na Yesu ampiga kofi usoni, akisema: “Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?”
“Kama nimesema vibaya,” Yesu ajibu, “ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?” Baada ya kujibiana maneno hayo, Anasi apeleka Yesu kwa Kayafa akiwa amefungwa.
Kufikia sasa makuhani wote wakuu na wanaume wazee na waandishi, ndiyo, Sanhedrini yote, inaanza kukusanyika. Kwa wazi mahali pao pa mkutano ni kao la Kayafa. Hata hivyo, kufanya kesi kama hiyo katika usiku wa Sikukuu ya Kupitwa kwa wazi ni jambo lililo dhidi ya sheria ya Kiyahudi. Lakini hilo halizuii viongozi wa kidini kutofanya kusudi lao ovu.
Tayari, majuma kadhaa kabla ya hapo wakati Yesu alipomfufua Lazaro, Sanhedrini ilikuwa imeamua miongoni mwao wenyewe kwamba ni lazima afe. Na siku mbili tu mapema kidogo, siku ya Jumatano, wenye mamlaka wa kidini walifanya shauri pamoja kumkamata Yesu kwa mbinu ya ujanja ili wamuue. Wazia, yeye kwa kweli alikuwa amehukumiwa adhabu kabla ya kufanyiwa kesi!
Sasa jitihada zaendelea kutafuta mashahidi watakaotoa uthibitisho bandia ili kesi ikuzwe dhidi ya Yesu. Hata hivyo, hakuwezi kupatikana mashahidi wenye kuafikiana katika ushuhuda wao. Hatimaye, wawili waja mbele na kushikilia hivi: “Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.”
“Hujibu neno?” Kayafa auliza. “Hawa wanakushuhudia nini?” Lakini Yesu abaki kimya. Hata katika shtaka hili bandia, kwa aibu ya Sanhedrini, mashahidi hao hawawezi kufanya hadithi zao ziafikiane. Hivyo basi kuhani mkuu ajaribu mbinu tofauti.
Kayafa ajua jinsi Wayahudi walivyo wepesi kukasirikia mtu yeyote anayedai kuwa ndiye Mwana halisi wa Mungu. Katika pindi mbili mapema kidogo, wao walikuwa wamefanya haraka-haraka kumbandika Yesu jina la kuwa mkufuru astahiliye kifo, mara moja wakikosea kwa kuwazia kwamba alikuwa akidai kwamba yuko sawa na Mungu. Sasa Kayafa adai kwa ujanja hivi: “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”
Bila kujali ni nini Wayahudi wafikiri, kwa kweli Yesu ndiye Mwana wa Mungu. Na kubaki kimya kungeweza kueweleka kwamaanisha kwamba anakana kuwa ndiye Kristo. Hivyo basi Yesu ajibu kwa ujasiri hivi: “Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.”
Hapo, Kayafa, akijionyesha kwa njia ya kutazamisha, ararua mavazi yake na kupaaza sauti: “Amekufuru; tuna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi?”
“Imempasa kuuawa,” Sanhedrini yapiga mbiu. Halafu waanza kumfanyia mzaha, nao wasema mambo mengine ya kufuru dhidi yake. Wampiga kofi katika uso wake na kuutemea mate. Wengine wafunika uso wake wote na kumpiga kwa ngumi zao na kusema hivi kimadharau: “Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?” Mwenendo huu wa kutukana, usio wa kisheria watukia wakati wa ile kesi ya usiku. Mathayo 26:57-68; 26:3, 4; Marko 14:53-65; Luka 22:54, 63-65; Yohana 18:13-24; 11:45-53; 10:31-39; 5: 16-18.
▪ Yesu aongozwa wapi kwanza, na ni nini lampata huko?
▪ Kisha Yesu apelekwa wapi, na kwa kusudi gani?
▪ Kayafa amewezaje kuifanya Sanhedrini ipige mbiu kwamba Yesu astahili kifo?
▪ Ni mwenendo gani wa kutukana, ulio kinyume cha sheria watukia wakati wa ile kesi?
-
-
Akanwa Katika UaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 120
Akanwa Katika Ua
BAADA ya kumwacha Yesu katika bustani ya Gethsemane na kukimbia kwa hofu pamoja na mitume wale wengine, Petro na Yohana wasimama katika kimbio lao. Labda wao wamfikia Yesu apelekwapo kwenye makao ya Anasi. Anasi aagizapo apelekwe kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, Petro na Yohana wafuata wakiwa umbali wa kutosha, yaonekana wakiwa wametatizika kati ya kuhofia uhai wao wenyewe na hangaiko lao la kina kirefu juu ya yatakayopata Bwana-Mkubwa wao.
Awasilipo kwenye makao ya Kayafa yenye nafasi kubwa, Yohana aweza kuingia katika ua, kwa kuwa yeye ajulikana na kuhani mkuu. Hata hivyo, Petro aachwa akisimama nje ya mlango. Lakini muda si muda Yohana arudi na kusema na bawabu, aliye kijakazi, na Petro aruhusiwa kuingia.
Kufikia sasa kuna baridi, na watumishi wa nyumba na maofisa wa kuhani mkuu wamewasha moto wa makaa. Petro ajiunga nao ili apate joto huku akingojea matokeo ya kesi ya Yesu. Huko, katika nuru ya ule moto mwangavu, bawabu aliyekuwa ameruhusu Petro aingie amtazama vizuri zaidi. “Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya”! apaaza sauti.
Akiudhika kwa kutambulishwa, Petro akana mbele yao wote kwamba hajapata kumjua Yesu. “Sijui wala sisikii unayoyasema wewe,” yeye asema.
Hapo basi, Petro aenda nje karibu na njia ya lango. Hapo, msichana mwingine amwona naye pia awaambia wale waliosimama karibu: “Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti.” Kwa mara nyingine, Petro akana, akiapa hivi: “Simjui mtu huyu”!
Petro abaki katika ua, akijaribu kutoonekana wazi kwa kadiri iwezekanavyo. Labda hapo agutushwa na kuwika kwa jogoo katika giza la asubuhi na mapema. Kwa sasa, kesi ya Yesu yaendelea, yaonekana ikiendeshwa katika sehemu ya nyumba iliyo juu ya ua. Labda Petro na wengine wanaongojea chini waona mashahidi mbalimbali wakija na kwenda ambao waletwa ndani ili kushuhudia.
Karibu saa moja imepita tangu Petro alipotambulishwa mara ya mwisho kuwa mshirika wa Yesu. Sasa watu kadhaa kati ya wale wenye kusimama hapo wamjia na kusema: “Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako [lahaja yako, NW] wakutambulisha.” Mmoja wa kikundi hicho ni mtu wa ukoo wa Malko, ambaye Petro alikuwa amekata sikio lake. “Je! mimi si[ni]mekuona wewe bustanini pamoja naye?” asema.
“Simjui mtu huyu”! Petro ashikilia sana kauli. Kwa hakika, ajaribu kuwasadikisha kwamba wote wanakosea kwa kulaani na kuapa juu ya jambo hilo, maana yake, kujilaani mwenyewe ikiwa hasemi ukweli.
Mara Petro akanapo mara hii ya tatu, jogoo awika. Na wakati huo, Yesu, ambaye kwa wazi ametoka nje akaja kwenye roshani juu ya ua, ageuka na kumtazama. Mara hiyo, Petro akumbuka aliyosema Yesu saa chache tu mapema kidogo katika chumba cha juu: “Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.” Kwa kulemewa sana na uzito wa dhambi yake, Petro aenda nje na kulia machozi kwa uchungu.
Hilo lingewezaje kutukia? Baada ya kuwa na uhakika sana juu ya imara yake ya kiroho, ikawaje kwamba Petro aweze kukana Bwana-Mkubwa wake mara tatu kwa mfululizo wenye kufuatana haraka-haraka? Bila shaka hali zamnasa Petro bila kutarajia. Ukweli unapotoshwa, na Yesu anaonyeshwa kuwa mhalifu mwovu. Lililo sawa lafanywa lionekane kuwa kosa, asiye na hatia kuwa mwenye hatia. Hivyo basi kwa sababu ya mikazo ya ile pindi, Petro akosa usawaziko. Ghafula hisia yake ifaayo ya uaminifu-mshikamanifu yavurugika. Kuhofu binadamu kwamshika hata kumletea majonzi. Jambo hilo na lisitupate sisi kamwe! Mathayo 26:57, 58, 69-75; Marko 14:30, 53, 54, 66-72; Luka 22:54-62; Yohana 18:15-18, 25-27.
▪ Petro na Yohana wapataje kuingia katika ua wa kuhani mkuu?
▪ Petro na Yohana wakiwa wangali katika ua, ni nini kinachoendelea katika nyumba?
▪ Jogoo awika mara ngapi, na Petro akana mara ngapi kwamba hamjui Kristo?
▪ Yamaanisha nini kwamba Petro alaani na kuapa?
▪ Ni nini chasababisha Petro akane kwamba hamjui Yesu?
-