Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mbele ya Sanhedrini, Kisha kwa Pilato
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 121

      Mbele ya Sanhedrini, Kisha kwa Pilato

      USIKU unakaribia mwisho. Petro amekana Yesu kwa mara ya tatu, na washiriki wa Sanhedrini wamemaliza kesi yao ya bandia na wametawanyika. Hata hivyo, wanakutana tena asubuhi ya Ijumaa mara tu kunapopambazuka, wakati huu wakiwa kwenye jumba la Sanhedrini yao. Inaelekea kusudi lao ni kufanya ionekane eti kesi yao ya usiku ilifuata uhalali wa sheria. Yesu anapoletwa mbele yao, wanasema hivi, kama vile walivyofanya usiku: “Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie.”

      “Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa,” Yesu anajibu. “Tena, nikiwauliza, hamtajibu.” Hata hivyo, kwa moyo mkuu Yesu anaelekeza kwenye utambulishi wake, akisema: “Tangu sasa Mwana wa Adamu [Mwana wa binadamu, NW] atakuwa ameketi [akiketi, NW] upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi.”

      “Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu?” wote wataka kujua.

      “Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye,” Yesu ajibu.

      Kwa wanaume hawa ambao wameazimia kuua, jibu hili linatosha. Wanaliona kuwa kufuru. “Tuna haja gani tena ya ushuhuda?” wanauliza. “Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake.” Hivyo basi wanamfunga Yesu, wanamwongoza kutoka hapo, na kumpa kwa gavana Mroma Pontio Pilato.

      Yudasi, msaliti wa Yesu, amekuwa akitazama hatua za mambo hayo. Anapoona kwamba Yesu amelaaniwa vikali, ahisi majuto. Hivyo yeye aendea makuhani wakuu na wanaume wazee kurudisha vile vipande 30 vya fedha, akieleza hivi: “Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.”

      “Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe”! wajibu bila moyo wa huruma. Hivyo basi Yuda atupa vile vipande vya fedha hekaluni na kwenda zake na kujaribu kujinyonga. Hata hivyo, inaonekana kwamba tawi ambalo Yuda afungilia kamba linakatika, na mwili wake waporomoka kwenye miamba iliyoko chini, ambako wapasuka-pasuka.

      Makuhani wakuu hawana hakika wafanye nini na vile vipande vya fedha. “Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka,” wakata shauri, “kwa kuwa ni kima cha damu.” Hivyo basi, baada ya kushauriana, kwa pesa hizo wanunua shamba la mfinyanzi ili kuzika wageni. Hivyo shamba hilo laja kuitwa “konde la damu.”

      Bado ni mapema asubuhi wakati Yesu anapopelekwa kwenye jumba la gavana. Lakini Wayahudi ambao wameandamana naye wakataa kuingia kwa sababu wanaamini kwamba huo uhusiano wa kindani pamoja na Wasio Wayahudi utawatia unajisi. Hivyo basi ili ajipatanishe na maoni yao, Pilato aja nje. “Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?” auliza.

      “Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako,” wajibu.

      Akitaka kuepuka kuhusika, Pilato ajibu hivi: “Haya! mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!”

      Wakifunua azimio lao la uuaji, Wayahudi wadai hivi: “Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.” Kwa kweli, kama wangeua Yesu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa, inaelekea ingeleta msukosuko wa watu wote, kwa kuwa wengi wamheshimu Yesu sana. Lakini wakiweza kufanya Waroma wamuue kwa shtaka la kisiasa, hiyo itaelekea kuwaondolea daraka mbele ya watu.

      Hivyo basi viongozi wa kidini, bila kutaja kesi yao ya mapema ambamo walilaani Yesu vikali juu ya kukufuru, sasa watunga mashtaka tofauti. Wafanyiza lile shtaka lenye sehemu tatu: “Tumemwona huyu [1] akipotosha taifa letu, na [2] kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, [3] akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.”

      Lile shtaka la kwamba Yesu adai kuwa mfalme ndilo lahangaisha Pilato. Kwa hiyo, yeye aingia tena katika jumba, aita Yesu aende alipo, na kuuliza: “Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Ndiyo kusema, je! umevunja sheria kwa kujijulisha wazi kuwa mfalme kwa kupinga Kaisari?

      Yesu ataka kujua ni mengi kadiri gani ambayo tayari Pilato amesikia juu yake, hivyo basi auliza hivi: “Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?”

      Pilato adai hana maarifa yoyote juu yake na ana tamaa ya kujua mambo hakika. “Ama! Ni Myahudi mimi!” ajibu. “Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?”

      Yesu hajaribu kwa njia yoyote kuepa suala hilo, ambalo ni la kuwa na ufalme. Jibu ambalo Yesu anatoa sasa bila shaka lashangaza Pilato. Luka 22:66–23:3; Mathayo 27:1-11; Marko 15:1; Yohana 18:28-35; Matendo 1:16-20.

      ▪ Sanhedrini yakutana tena asubuhi kwa kusudi gani?

      ▪ Yuda afaje, na ni jambo gani lafanywa na vile vipande 30 vya fedha?

      ▪ Badala ya Wayahudi wamuue Yesu wao wenyewe, kwa nini wataka Waroma wamuue Yesu?

      ▪ Ni mashtaka gani ambayo Wayahudi wafanyia Yesu?

  • Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi Tena
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 122

      Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi Tena

      INGAWA Yesu hafanyi jaribio lolote la kumficha Pilato kwamba yeye ni mfalme, aeleza kwamba Ufalme wake si tisho kwa Roma. “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu,” Yesu asema. “Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Hivyo Yesu akiri mara tatu kwamba yeye ana Ufalme, ingawa si wa chanzo cha kidunia.

      Hata hivyo, Pilato amkaza zaidi: “Wewe u mfalme basi?” Yaani, wewe ni mfalme hata ingawa Ufalme wako si sehemu ya ulimwengu huu?

      Yesu amjulisha Pilato kwamba amekata shauri vizuri, akijibu: “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.”

      Ndiyo, kusudi hasa la Yesu kuwako duniani ni kuitolea “kweli” ushahidi, hasa ile kweli juu ya Ufalme wake. Yesu yuko tayari kuwa mwaminifu kwa kweli hiyo hata ikiwa itamgharimu uhai wake. Ingawa Pilato auliza: “Kweli ni nini?” hangojei maelezo zaidi. Amesikia ya kutosha ili atoe hukumu.

      Pilato arudia umati unaongoja nje ya jumba lile. Kwa wazi Yesu akiwa kando yake, awaambia makuhani wakuu na wale walio pamoja nao: “Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.”

      Kwa kukasirishwa na uamuzi huo, umati unaanza kusisitiza hivi: “[Yeye] huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi wote, tokea Galilaya mpaka huku.”

      Ni lazima ushupavu huo usiotumia akili kufikiri wa Wayahudi uwe unashangaza Pilato. Hivyo basi, makuhani wakuu na wanaume wazee wanapoendelea kupaaza sauti, Pilato ageukia Yesu na kuuliza: “Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?” Bado, Yesu hafanyi jaribio la kujibu. Utulivu wake katika kukabiliana na yale mashtaka yasiyo na msingi wowote wafanya Pilato kustaajabu.

      Anapojua kwamba Yesu ni Mgalilaya, Pilato aona njia ya kujiondoa asiwe na daraka juu yake. Mtawala wa Galilaya, Herode Antipa (mwana wa Herode Mkuu), yumo Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa, hivyo basi Pilato ampeleka Yesu kwake. Mapema kidogo, Herode Antipa alikuwa ameagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa, halafu Herode akaogopa aliposikia juu ya kazi za kimuujiza ambazo Yesu alikuwa akifanya, akihofu kwamba huenda ikawa kwa kweli Yesu ni Yohana ambaye ameinuliwa kutoka kwa wafu.

      Sasa, Herode ana shangwe mno kwa tazamio la kumwona Yesu. Hii si kwa sababu ahangaikia hali njema ya Yesu au kwamba ataka kufanya jaribio lolote halisi juu ya kama mashtaka anayofanyiwa ni ya kweli au sivyo. Bali, yeye ni mdadisi tu na atumainia kuona Yesu akifanya muujiza fulani.

      Hata hivyo, Yesu akataa kutosheleza udadisi wa Herode. Kwa uhakika, Herode anapokuwa akimuuliza maswali, yeye hasemi neno. Kwa kukata tamaa, Herode na askari-walinzi wake wamdhihaki Yesu. Wamvika vazi jangavu na kumfanyia mzaha. Halafu wampeleka tena kwa Pilato. Tokeo ni kwamba, Herode na Pilato, ambao hapo kwanza walikuwa wamekuwa maadui, wanakuwa marafiki wakubwa.

      Yesu anaporudi, Pilato aita makuhani wakuu, watawala wa Wayahudi, na watu wakusanyike pamoja na kusema hivi: “Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilotenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua.”

      Hivyo, Pilato amejulisha rasmi mara mbili kwamba Yesu hana hatia. Ana hamu ya kumwacha huru, kwa maana afahamu kwamba ni kwa sababu ya wivu tu kwamba makuhani wamemtia mikononi mwake. Lakini Pilato anapoendelea kujaribu kumwachilia Yesu, apata kichocheo kingine imara afanye hivyo. Anapokuwa katika kiti chake cha hukumu, mke wake apeleka ujumbe, akimhimiza hivi: “Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto [kwa wazi yenye asili ya kimungu] kwa ajili yake.”

      Hata hivyo, Pilato aweza kufunguaje mwanamume huyu asiye na hatia, kama vile anavyojua inampasa? Yohana 18:36-38; Luka 23:4-16; Mathayo 27:12-14, 18, 19; 14:1, 2; Marko 15:2-5.

      ▪ Yesu ajibuje swali kuhusu ufalme wake?

      ▪ Ni nini “kweli” ambayo Yesu alitumia maisha yake ya kidunia akiitolea ushahidi?

      ▪ Hukumu ya Pilato ni nini, watu waitikiaje, na Pilato afanyia Yesu nini?

      ▪ Herode Antipa ni nani, kwa nini ana shangwe nyingi mno kumwona Yesu, naye amfanyia nini?

      ▪ Kwa nini Pilato ana hamu ya kumweka Yesu huru?

  • “Tazama, Mtu Huyu!”
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 123

      “Tazama, Mtu Huyu!”

      KWA kuvutiwa na utulivu wa Yesu na akitambua kwamba hana kosa, Pilato afuatia njia nyingine ya kumwachilia. “Kwenu kuna desturi,” aambia umati wa watu wale, “ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka [Sikukuu ya Kupitwa, NW].”

      Baraba, muuaji mwenye sifa mbaya, amefungwa pia akiwa mfungwa-gereza, hivyo basi Pilato auliza: “Mnataka niwafungulie yupi? yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo?”

      Kwa kuvutwa na usadikisho wa makuhani wakuu ambao wamewachochea, watu waomba Baraba aachiliwe lakini Yesu auawe. Bila kukata tamaa, Pilato ajibu, akiuliza tena: “Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili?”

      “Baraba,” wapaaza sauti.

      “Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo?” Pilato auliza kwa kufadhaika.

      Kwa mngurumo mmoja wenye kishindo cha kuziba masikio, wajibu: “Asulibiwe [acha atundikwe, NW]”! “Msulibishe! Msulibishe [mtundike, NW]!”

      Kwa kujua kwamba wadai kifo cha mtu asiye na hatia, Pilato asihi hivi: “Kwa sababu gani? huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi [kumwadhibu] nitamfungua.”

      Japo majaribio yake, umati huo wenye hasira, kwa kuchochewa na viongozi wao wa kidini, waendelea kupiga kelele: “Asulibiwe [atundikwe, NW]”! Kwa kuchochewa sana na makuhani, umati wataka damu. Na ebu fikiri, siku tano tu kabla ya hapo, wengine wao labda walikuwa miongoni mwa wale waliokaribisha Yesu kuingia Yerusalemu akiwa Mfalme! Muda wote huu, wanafunzi wa Yesu, ikiwa wapo, wabaki kimya na bila kujitokeza wazi.

      Pilato, akiona kwamba maneno yake ya kusihi hayafai kitu, bali kunatokea fujo, achukua maji na kunawa mikono mbele ya ule umati, na kusema: “Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.” Hapo watu hao wajibu: “Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”

      Hivyo basi, kulingana na madai yao—naye akitaka kufurahisha umati huo kuliko kufanya analojua kuwa haki—Pilato awafungulia Baraba. Achukua Yesu na kuagiza avuliwe mavazi halafu apigwe mijeledi. Huku hakukuwa kupiga viboko vya kawaida. The Journal of the American Medical Association linaeleza zoea la Kiroma la kupiga mijeledi:

      “Chombo cha kawaida kilikuwa kiboko kifupi (flagramu au flagelamu) chenye kamba kadhaa moja moja za ngozi-kavu au zilizosokotwa zikiwa na marefu mbalimbali, ambamo vipande vidogo vya chuma au vipande vyenye ncha kali vya mifupa ya kondoo vilifungwa kwa kuachana. . . . Askari Waroma walipopiga-piga mgongo wa mfungwa kwa nguvu kamili, vile vipande vya chuma vya mfiringo vingesababisha michubuo ya kina kirefu, na zile kamba za ngozi-kavu na mifupa ya kondoo zingekata ndani ya ngozi na sehemu zilizo chini ya ngozi ya mwili. Halafu, kupigwa mijeledi kulipoendelea, miraruko ya ngozi ingeingia chini ya nyuzi za mnofu chini kwenye mifupa ya mwili na kutokeza nyuzinyuzi zenye kuning’inia za mnofu wenye kutoka damu.”

      Baada ya kupigwa huko kenye mateso makali, Yesu apelekwa ndani ya jumba la gavana, na kikundi kizima cha askari kinaitwa kikusanyike. Humo askari warundika matukano zaidi juu yake kwa kusokota taji la miiba na kulisukuma juu ya kichwa chake. Watia mwanzi katika mkono wake wa kulia, nao wamvika vazi la zambarau, namna inayovaliwa na watu wa kifalme. Halafu wamwambia hivi kwa dhihaka: “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!” Pia, wamtemea mate na kumpiga kofi usoni. Wakichukua ule mwanzi imara kutoka mkononi mwake, wautumia kumpiga kichwani, hiyo ikizidi kuisukuma ndani ya ngozi ya kichwa chake ile miiba iliyochongoka ya “taji” lake lenye kumshushia heshima.

      Fahari na imara ya kusifika ambayo Yesu anayo katika kuelekeana na kutendewa vibaya huko inavutia sana Pilato hivi kwamba inamsukuma kufanya jaribio jingine la kumwachilia. “Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake,” awaambia umati wa watu. Inawezekana kuwa awazia kwamba sura ya hali ya kuteswa-teswa kwa Yesu italainisha mioyo yao. Yesu anapokuwa amesimama mbele ya watu hao wenye fujo wasio na moyo wa huruma, akiwa amevaa taji la miimba na lile vazi la nje la zambarau na huku uso wake wenye kutoka damu ukiwa na maumivu, Pilato atangaza: “Tazama, mtu huyu!”

      Ingawa amechubuliwa na kutwangwa, hapa amesimama mtu mwenye kutokeza zaidi katika historia yote, kwa kweli binadamu wa kutokeza zaidi aliyepata kuishi! Ndiyo, Yesu aonyesha fahari ya unyamavu na utulivu unaoonyesha ukuu ambao hata Pilato alazimika kuukubali wazi, kwa maana inaonekana maneno yake ni mchanganyiko wa heshima na huruma pia. Yohana 18:39–19:5; Mathayo 27:15-17, 20-30; Marko 15:6-19; Luka 23:18-25.

      ▪ Pilato ajaribu kwa njia gani kufanya Yesu aachiliwe?

      ▪ Pilato ajaribuje kujiondolea daraka?

      ▪ Ni nini kinachohusika katika kupigwa mijeledi?

      ▪ Yesu adhihakiwaje baada ya kupigwa mijeledi?

      ▪ Ni jaribio gani zaidi ambalo Pilato afanya ili kumwachilia Yesu?

  • Atiwa Mikononi na Kuchukuliwa
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 124

      Atiwa Mikononi na Kuchukuliwa

      WAKATI Pilato, kwa kusukumwa na fahari tulivu ya Yesu aliyeteswa, ajaribupo tena kumfungua, makuhani wakuu wakasirika hata zaidi. Wamepiga moyo konde kutoacha chochote kivuruge kusudi lao bovu. Hivyo basi wao warudia tena kupaaza sauti hivi: “Msulibishe! Msulibishe [Mtundike, mtundike, NW]!”

      “Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe,” Pilato ajibu. (Tofauti na madai yao ya mapema kidogo, Wayahudi waweza kuwa na mamlaka ya kufisha wahalifu kwa makosa ya kidini yaliyo na uzito wa kutosha.) Halafu, kwa mara kama ya tano, Pilato amtangaza Yesu kuwa hana hatia, akisema hivi: “Mimi sioni hatia kwake.”

      Wayahudi, kwa kuona kwamba mashtaka yao ya kisiasa yameshindwa kuleta matokeo, warudia tena lile shtaka la kidini la kukufuru lililotumiwa mapema kidogo kwenye kesi ya Yesu mbele ya Sanhedrini. “Sisi tunayo sheria,” wao wasema, “na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”

      Shtaka hilo ni jipya kwa Pilato, nalo lafanya awe na hofu zaidi. Kufikia sasa afahamu kwamba Yesu si mtu wa kawaida tu, kama vile ndoto ya mke wake na nguvu nyingi ajabu za utu wa Yesu vyaonyesha. Lakini eti “Mwana wa Mungu”? Pilato ajua kwamba Yesu ni wa kutoka Galilaya. Hata hivyo, je! angeweza kuwa aliishi kabla ya hapo? Akimrudisha tena ndani ya jumba la utawala, Pilato auliza: “Wewe umetokapi?”

      Yesu akaa kimya. Mapema kidogo alikuwa amemwambia Pilato kwamba yeye ni mfalme, lakini kwamba Ufalme wake si sehemu ya ulimwengu huu. Sasa hakuna elezo lolote zaidi lingetimiza kusudi lenye mafaa. Hata hivyo, fahari ya Pilato yaumizwa na katao la kujibu, naye amwakia Yesu kwa maneno haya: “Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha [kukutundika, NW]?”

      “Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu,” Yesu ajibu kwa staha. Amaanisha mamlaka ambayo Mungu amewapa watawala wa kibinadamu kusimamia mambo ya kidunia. Yesu aongezea hivi: “Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.” Kwa kweli, kuhani mkuu Kayafa na wenzi wake na Yuda Iskariote wote wana daraka zito kuliko Pilato kwa ajili ya kutendwa kwa Yesu isivyo haki.

      Kwa kuvutiwa hata zaidi na Yesu na akiwa na hofu kwamba huenda ikawa Yesu ana asili ya kimungu, Pilato ajitahidi tena kumwachilia. Hata hivyo, Wayahudi wamjibu vikali Pilato. Wao warudia shtaka lao la kisiasa, wakitisha hivi kwa ujanja: “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.”

      Ijapokuwa hilo lamaanisha matokeo ya kuogopesha sana, Pilato amleta Yesu nje tena. “Tazama, Mfalme wenu!” bado awasihi tena.

      “Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe [Mtundike, NW]!”

      “Je! nimsulibishe [nimtundike, NW] mfalme wenu!” Pilato auliza kwa kukata tamaa.

      Wayahudi wamekuwa wakiudhika chini ya utawala wa Waroma. Kwa kweli, wao wadharau kutawalwa na Roma! Na bado, kwa unafiki, makuhani wakuu wasema hivi: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”

      Akihofia cheo na sifa yake ya kisiasa, Pilato mwishowe ashindwa na madai ya Wayahudi yasiyokoma. Amtia Yesu mikononi mwao. Askari wamvua Yesu joho la zambarau na kumvika mavazi yake ya nje. Yesu achukuliwapo kutundikwa, alazimishwa abebe mti wake mwenyewe wa mateso.

      Kufikia sasa ni asubuhi katikati siku ya Ijumaa, Nisani 14; labda yakaribia kuwa mchana katikati. Yesu amekuwa macho tangu mapema asubuhi ya Alhamisi, naye amepatwa na mateso makali moja baada ya jingine. Basi inaeleweka kwa nini nguvu zinamwishia chini ya uzito wa ule mti. Hivyo basi mpitaji njia, Simoni fulani wa Kirene katika Afrika, alazimishwa katika utumishi ambebee mti huo. Wanaposonga mbele, watu wengi, kutia na wanawake, wafuata, wakijipiga-piga kwa huzuni kuu na kumwombolezea Yesu.

      Akigeukia wanawake hao, Yesu asema: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri [wenye furaha ni, NW] walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. . . . Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”

      Yesu anarejezea mti wa taifa la Kiyahudi, ambao ungali una umajimaji fulani wa uhai ndani yao kwa sababu ya kuwapo kwa Yesu na kuwako kwa mabaki wanaomwamini. Lakini hao wakiisha kuondolewa katika taifa lile, ni mti mfu tu wa kiroho utabaki, ndiyo, tengenezo la kitaifa lililonyauka. Loo, kutakuwa na sababu iliyoje ya kulia machozi wakati majeshi ya Kiroma, yakitumiwa kuwa wafishaji wa Mungu, yatakapoliacha ukiwa taifa la Kiyahudi! Yohana 19:6-17; 18:31; Luka 23:24-31; Mathayo 27:31, 32; Marko 15:20, 21.

      ▪ Ni shtaka gani ambalo viongozi wa kidini wanafanya dhidi ya Yesu wakati mashtaka yao ya kisiasa yanaposhindwa kuleta matokeo?

      ▪ Kwa nini Pilato awa mwenye hofu zaidi?

      ▪ Ni nani wanaochukua dhambi iliyo kubwa zaidi kwa ajili ya yale yanayopata Yesu?

      ▪ Makuhani wanamfanyaje Pilato amtie Yesu mikononi ili auawe?

      ▪ Yesu awaambia nini wanawake wanaomlilia, naye amaanisha nini kwa kurejezea mti kuwa “mbichi” kisha “mkavu”?

  • Maumivu Makali Juu ya Mti
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 125

      Maumivu Makali Juu ya Mti

      PAMOJA na Yesu wanyang’anyi wawili wachukuliwa nje wakauawe. Si mbali na jiji, andamano lasimama mahali paitwapo Golgotha, au Fuvu la Kichwa.

      Wafungwa hao wavuliwa mavazi yao. Halafu wapewa divai iliyotiwa manemane ambayo ni dawa ya kulevya. Inaonekana imetayarishwa na wanawake wa Yerusalemu, na Waroma huwa hawawanyimi wenye kutundikwa mchanganyo huu wa kinywaji chenye kumaliza maumivu. Hata hivyo, Yesu anapokionja, akataa kunywa. Kwa nini? Kwa wazi ataka kuwa na nguvu zake zote za kufikiri wakati wa jaribu hili la imani yake lililo kubwa kupita yote.

      Sasa Yesu amenyooshwa juu ya mti huku mikono yake ikiwa imewekwa juu ya kichwa chake. Ndipo askari wanapopigilia misumari mikubwa katika mikono yake na katika miguu yake. Yeye ajigeuza-geuza kwa maumivu wakati misumari inapochoma mnofu na nyuzi za mwili. Mti unaposimamishwa wima, maumivu yazidi kweli kweli, kwa maana uzito wa mwili wake wapasua sehemu za majeraha yenye misumari. Hata hivyo, badala ya kutisha, Yesu asali hivi kwa ajili ya askari hao Waroma: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.”

      Pilato amebandika juu ya mti huo ishara ambayo inasema: “YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” Inaonekana, yeye aandika hivi si kwa sababu tu aheshimu Yesu bali pia kwa sababu achukizwa sana na makuhani Wayahudi kwa kuwa wamemkaza mpaka akalazimika kuhukumia Yesu kifo. Ili wote waweze kusoma ishara hiyo, Pilato aagiza iandikwe katika lugha tatu—katika Kiebrania, katika Kilatini rasmi, na katika Kigiriki cha kawaida.

      Makuhani wakuu, kutia na Kayafa na Anasi, wafadhaika. Tangazo hili la hakika linaharibu saa yao yenye shangwe ya ushindi. Kwa hiyo wapinga hivi: “Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.” Akiudhika kwa kuwa ametumika kama chombo cha kutimizia nia ya makuhani hao, Pilato ajibu kwa madharau yenye kukata maneno: “Niliyoandika nimeyaandika.”

      Makuhani, pamoja na umati mkubwa, sasa wakusanyika mahali pa mauaji, na makuhani wajaribu kukanusha ushuhuda wa ile ishara. Warudia ule ushuhuda wa bandia uliotolewa mapema kidogo kwenye majaribu ya Sanhedrini. Kwa hiyo, haishangazi kwamba wapita njia waanza kusema kwa matusi, wakitikisa vichwa vyao kwa mzaha na kusema: “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani [kutoka kwenye mti wa mateso, NW]”!

      “Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe”! nao makuhani wakuu na marafiki wao wa kidini waingilia kama kwamba ni kwa sauti moja. “Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani [kutoka kwenye mti wa mateso, NW], nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama amtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”

      Kwa kunaswa katika roho hiyo, askari wajiunga pia katika kufanyia Yesu mzaha. Wamtolea divai kali kwa mzaha, yaonekana ikiwa imepita kidogo tu mbele ya midomo yake iliyokauka. “Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi,” wanadhihaki vikali, “ujiokoe mwenyewe.” Hata wale wanyang’anyi—mmoja akiwa ametundikwa kulia kwa Yesu, na yule mwingine kushoto kwake—wamdhihaki. Fikiria hilo! Binadamu mkubwa zaidi aliyepata kuishi, ndiyo, yule aliyeshiriki pamoja na Yehova Mungu katika kuumba vitu vyote, apatwa na fedheha yote hiyo akiwa ameazimia kabisa!

      Askari wachukua mavazi ya Yesu ya nje na kuyagawanya sehemu nne. Wapiga kura kuona yatakuwa ya nani. Hata hivyo, lile vazi la ndani halina mshono wa kuliunga, kwa kuwa ni la ubora mwingi. Hivyo basi askari hao waambiana: “Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani.” Hivyo, bila kujua, watimiza andiko linalosema: “Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura.”

      Baada ya muda, mmoja wa wanyang’anyi aja kuthamini kwamba kwa kweli ni lazima iwe Yesu ni mfalme. Kwa hiyo, akikemea mwandamani wake, asema hivi: “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.” Halafu aongea na Yesu, na kutoa ombi hili: “Nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”

      “Kweli kweli mimi nakuambia wewe leo,” Yesu ajibu, “Wewe utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.” (NW) Ahadi hii itatimizwa wakati Yesu atakapotawala mbinguni na kufufua mtenda maovu huyo mwenye kutubu kwenye uhai duniani katika Paradiso ambayo waokokaji wa Har–Magedoni na waandamani wao watakuwa na pendeleo la kuisitawisha. Mathayo 27:33-44; Marko 15:22-32; Luka 23:27, 32-43; Yohana 19:17-24.

      ▪ Kwa nini Yesu akataa kunywa divai iliyotiwa manemane ambayo ni dawa ya kulevya?

      ▪ Yaonekana ni kwa nini ile ishara imebandikwa juu ya mti wa Yesu, nayo yaanzisha maneno gani kati ya Pilato na makuhani wakuu?

      ▪ Yesu adhihakiwa zaidi namna gani juu ya mti wa mateso, na kwa wazi ni nini kinachoongoza jambo hilo?

      ▪ Unabii watimizwaje katika linalofanywa na mavazi ya Yesu?

      ▪ Mmoja wa wanyang’anyi afanya badiliko gani, na Yesu atatimizaje ombi lake?

  • “Hakika Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 126

      “Hakika Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”

      YESU hajawa juu ya ule mti kwa muda mrefu wakati ambapo, katika mchana kakati, giza la kifumbo, lenye urefu wa saa tatu latukia. Halisababishwi na kupatwa kwa jua, kwa kuwa kupatwa kwa jua hutukia tu wakati wa mwezi mpya na mwezi ni mpevu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa. Zaidi ya hilo, kupatwa kwa jua huwa kwa dakika chache tu. Hivyo basi giza hili lina chanzo cha kimungu! Labda lawaachisha kidogo wale wanaomdhihaki Yesu, hata kusababisha dhihaka zao kali zikome.

      Ikiwa ajabu hii yenye kutia woga yatukia kabla ya yule mtenda maovu mmoja kumtia adabu mwandamani wake na kumwomba Yesu amkumbuke, huenda hilo likawa ni jambo moja linaloleta toba yake. Labda ni wakati wa giza hilo kwamba wanawake wanne, yaani, mama ya Yesu na Salome dada yake, Mariamu Magdalene, na Mariamu mama ya mtume Yakobo Mdogo, wasogelea kuja karibu na mti wa mateso. Yohana, mtume mpendwa wa Yesu, yupo hapo pamoja nao.

      Lo, jinsi moyo wa mama ya Yesu ‘wachomwa’ atazamapo mwana aliyemlea na kumtunza kwa mapenzi akining’inia hapo kwa maumivu makali! Lakini Yesu afikiria, si maumivu yake mwenyewe, bali hali njema ya mama yake. Kwa jitihada kubwa, amtolea Yohana ishara kwa kichwa chake na kusema hivi kwa mama yake: “Mama [mwanamke, NW], tazama, mwanao”! Halafu, akitoa ishara iyo hiyo kuelekea Mariamu, asema hivi kwa Yohana: “Tazama, mama yako”!

      Kwa njia hiyo Yesu akabidhi utunzaji wa mama yake, ambaye ushuhuda waonyesha kwamba sasa yeye ni mjane, mikononi mwa mtume wake aliyependwa kipekee. Afanya hivyo kwa sababu wana wengine wa Mariamu hawajadhihirisha bado imani katika yeye. Hivyo yeye aweka mfano mzuri wa kutoa riziki si kwa mahitaji ya kimwili tu ya mama yake bali pia kwa mahitaji yake ya kiroho.

      Karibu saa tisa mchana, Yesu asema hivi: “Naona kiu.” Yesu ajisikia ni kama kwamba Baba yake ameondoa ulinzi kutoka kwake ili ukamilifu wake ujaribiwe kabisa. Hivyo apaaza sauti hivi: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Wasikiapo hayo, watu fulani waliosimama karibu washangaa na kusema kwa sauti kubwa: “Tazama, anamwita Eliya.” Mara hiyo mmoja wao akimbia na, akitia sifongo iliyofyonza divai chungu kwenye ncha ya kishina cha hisopo, ampa kinywaji. Lakini wengine wasema hivi: “Acheni; na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha.”

      Yesu apokeapo ile divai chungu, alia kwa sauti kubwa: “Imekwisha.” Ndiyo, amemaliza kila jambo ambalo Baba yake amemtuma duniani afanye. Mwisho, asema hivi: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Kwa njia hiyo Yesu amkabidhi Mungu nguvu ya uhai wake akiwa na hakika kwamba Mungu atamrudishia huo. Halafu ainamisha kichwa chake na kufa.

      Yesu avutapo pumzi yake ya mwisho, tetemeko kali la dunia latukia, likipasua wazi miamba. Tetemeko hilo lina nguvu sana hivi kwamba maziara ya ukumbusho nje ya Yerusalemu yaachwa wazi na maiti zatupwa nje yayo. Wapita-njia, ambao waona miili mifu ambayo imefichuliwa wazi, waingia katika jiji na kuripoti jambo hilo.

      Zaidi ya hilo, Yesu afapo, lile pazia kubwa sana ligawanyalo Patakatifu na Patakatifu Zaidi katika hekalu la Mungu lapasuliwa mara mbili, kutoka juu hadi chini. Kwa wazi pazia hilo lililopambwa vizuri lina urefu wa kwenda juu wa meta 18 na ni zito sana! Muujiza huo wa kushangaza sana si kwamba wadhihirisha tu hasira kali ya Mungu juu ya walioua Mwana Wake bali pia wamaanisha kwamba njia ya kuingia Patakatifu Zaidi, mbinguni penyewe, sasa imewezeshwa na kifo cha Yesu.

      Basi, watu hao waonapo tetemeko hilo la dunia na kuona mambo yanayotendeka, waogopa sana. Ofisa wa jeshi mwenye kusimamia mambo kwenye mahali hapo pa mauaji hayo ampa Mungu utukufu. “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu,” atangaza. Yaelekea alikuwapo wakati dai la uana wa kimungu lilipozungumzwa kwenye jaribu la Yesu mbele ya Pilato. Na sasa yeye asadiki kwamba Yesu ndiye Mwana wa Mungu, ndiyo, kwamba kweli yeye ndiye binadamu mkubwa zaidi aliyepata kuishi.

      Wengine pia washangazwa mno na matukio hayo ya kimuujiza, nao waanza kurudi nyumbani wakijipiga-piga vifua vyao kama ishara ya huzuni kuu na aibu yao nyingi sana. Wanafunzi wengi wa Yesu wa kike ambao waguswa moyo sana na matukio hayo ya maana sana wanatazama tamasha hii kwa mbali. Mtume Yohana yupo pia.  Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; 2:34, 35; Yohana 19:25-30.

      ▪ Kwa nini kupatwa kwa jua hakuwezi kuwa ndiko kumesababisha zile saa tatu za giza?

      ▪ Muda mfupi kabla ya kifo chake, Yesu aweka mfano gani mzuri kwa ajili ya wale walio na wazazi wazee?

      ▪ Yesu asema maneno gani ya mwisho kabla ya kufa?

      ▪ Tetemeko la dunia latimiza nini, na ni nini maana ya kupasuliwa kwa pazia la hekalu vipande viwili?

      ▪ Miujiza hiyo yawa na matokeo gani juu ya ofisa wa jeshi mwenye kusimamia mambo kwenye mahali hapo pa mauaji?

  • Azikwa Ijumaa—Ziara Tupu Jumapili
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
    • Sura 127

      Azikwa Ijumaa—Ziara Tupu Jumapili

      KUFIKIA sasa inakaribia jioni ya Ijumaa, na Sabato ya Nisani 15 itaanza wakati wa jua kutua. Maiti ya Yesu yanyong’onyea juu ya mti, lakini wale wezi wawili walio kando zake bado wako hai. Alasiri ya Ijumaa yaitwa Maandalio kwa sababu huu ndio wakati ambao watu hutayarisha vyakula na kumaliza kazi nyingine yoyote inayopasa kufanywa ambayo haiwezi kungoja mpaka baada ya Sabato.

      Sabato ambayo iko karibu kuanza si kwamba tu ni Sabato ya kawaida (ile siku ya saba ya juma) bali pia ni Sabato mara mbili, au Sabato “kubwa.” Inaitwa hivyo kwa sababu Nisani 15, ambayo ndiyo siku ya kwanza ya ile Sikukuu ya siku saba ya Mikate Isiyotiwa Chachu (na sikuzote hiyo huwa sabato bila kujali inakuwa siku gani ya juma), imekuwa siku ile ile ya Sabato ya kawaida.

      Kulingana na Sheria ya Mungu, miili haipasi kuachwa juu ya mti usiku kucha. Kwa hiyo Wayahudi wamwomba Pilato kwamba vifo vya hao wanaouawa viharakishwe kwa kuivunja miguu yao. Kwa hiyo, askari wavunja miguu ya wale wezi wawili. Lakini kwa kuwa Yesu aonekana kuwa amekufa, miguu yake haivunjwi. Hilo latimiza andiko hili: “Hapana mfupa wake utakaovunjwa.”

      Hata hivyo, ili kuondoa shaka lolote kwamba kwa kweli Yesu amekufa, askari mmoja adunga upande wake kwa mkuki. Mkuki huo wachoma sehemu iliyo karibu na moyo wake, na mara hiyo damu na maji vyatoka. Mtume Yohana ambaye ni shahidi anayeyaona hayo, aripoti kwamba hilo latimiza andiko jingine: “Watamtazama yeye waliyemchoma.”

      Yusufu wa kutoka jiji la Arimathea, ambaye ni mshiriki wa Sanhedrini mwenye sifa njema, yupo pia mahali pale pa mauaji hayo. Yeye alikataa kupiga kura ya kuunga mkono kitendo kisicho cha haki cha mahakama kuu dhidi ya Yesu. Kwa kweli Yusufu ni mwanafunzi wa Yesu, ingawa amekuwa na woga kujitambulisha kuwa mmoja wao. Hata hivyo, sasa, yeye aonyesha ujasiri kwa kumwendea Pilato kumwomba mwili wa Yesu. Pilato amwita ofisa mkuu wa jeshi, na baada ya ofisa huyo kuthibitisha kwamba Yesu amekufa, Pilato aagiza Yusufu apewe maiti hiyo.

      Yusufu autwaa mwili na kuufunga kwa nguo nzuri ya kitani kuutayarisha kwa ajili ya maziko. Asaidiwa na Nikodemo, mshiriki mwingine wa Sanhedrini. Nikodemo pia ameshindwa kuungama imani yake katika Yesu kwa sababu ahofia kupoteza cheo chake. Lakini sasa yeye aleta furushi ambalo lina kilo 33 za manemane na uudi ambavyo ni vya bei kubwa. Wafunga mwili wa Yesu kwa vitambaa ambavyo vina viungo hivyo, kama vile Wayahudi walivyo na desturi ya kutayarisha miili kwa ajili ya maziko.

      Halafu mwili huo walazwa katika ziara (kaburi) jipya la ukumbusho la Yusufu ambalo limechongwa katika mwamba kwenye bustani iliyo karibu. Mwishowe, jiwe kubwa lavingirishwa penye mlango wa ziara. Ili kumaliza mazishi kabla ya Sabato, mwili watayarishwa kwa haraka. Kwa hiyo, Mariamu Magdalene na Mariamu mama wa Yakobo Mdogo, ambao labda wamekuwa wakisaidia katika matayarisho, warudi nyumbani haraka ili watayarishe viungo zaidi pamoja na mafuta yenye manukato. Baada ya Sabato, wao wanapanga kuutia mwili wa Yesu viungo zaidi ili kuuhifadhi kwa muda mrefu zaidi.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki