Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Madhara ya Ufisadi Katika Serikali
    Mnara wa Mlinzi—2015 | Januari 1
    • Polisi akipokea rushwa

      HABARI KUU | SERIKALI ISIYO NA UFISADI

      Madhara ya Ufisadi Katika Serikali

      Ufisadi katika serikali umefafanuliwa kuwa matumizi mabaya ya mamlaka ili kujinufaisha kibinafsi. Ufisadi ulianza zamani. Kwa mfano katika Biblia, kuna sheria iliyowakataza watu kula rushwa walipokuwa wakishughulikia kesi, kuonyesha kwamba zoea hilo lilikuwepo zaidi ya miaka 3,500 iliyopita. (Kutoka 23:8) Bila shaka, ufisadi unahusisha mambo mengi, si kula rushwa tu. Nyakati nyingine maofisa wa umma huiba mali, hukubali kupokea huduma ambazo hawastahili, au hata kuiba pesa. Hata wakati mwingine wao hutumia vibaya vyeo vyao kuwanufaisha marafiki na pia watu wao wa ukoo.

      Ingawa ufisadi unaweza kutendeka katika shirika lolote lile la kibinadamu, inaonekana kwamba ufisadi katika serikali umeenea zaidi. Ripoti ya mwaka wa 2013 ya Kipimo cha Ulimwenguni Pote cha Ufisadi (Global Corruption Barometer) iliyochapishwa na shirika la Transparency International, ilisema kwamba ulimwenguni pote watu huviona vyama vya kisiasa, polisi, maofisa wa umma, bunge, na mahakama kuwa taasisi zenye ufisadi mwingi zaidi. Acheni tuchunguze ripoti kadhaa zinazozungumzia tatizo hilo.

      • AFRIKA: Mwaka wa 2013, maofisa wapatao 22,000 wa umma nchini Afrika Kusini walishtakiwa mahakamani kwa sababu ya kujihusisha na ufisadi.

      • AMERIKA KUSINI: Mwaka wa 2012, nchini Brazili, watu 25 walipatikana na hatia ya kutumia pesa za umma kuwashawishi wapiga kura wawaunge mkono. Miongoni mwa watu hao alikuwa waziri mkuu wa zamani, mtu wa pili mwenye cheo kikubwa nchini humo.

      • ASIA: Mwaka wa 1995, watu 502 walifia ndani ya duka moja kubwa jijini Seoul, nchini Korea Kusini. Wachunguzi waligundua kwamba wajenzi waliojenga jengo hilo walijenga kwa saruji ya hali ya chini na walipuuza viwango vya usalama. Walifanya hivyo kwa kuwa maofisa wa jiji walikuwa tayari wamehongwa.

      • ULAYA: Cecilia Malmström, Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Tume ya Ulaya anasema, “Inastaajabisha sana kuona jinsi tatizo hilo [ufisadi] lilivyoenea Ulaya. Viongozi wa kisiasa wameshindwa kulikomesha.”

      Si rahisi hata kidogo kwa wanadamu kukomesha ufisadi katika serikali. Profesa Susan Rose-Ackerman, mtaalamu wa kupambana na janga la ufisadi aliandika kwamba ili mabadiliko yapatikane serikali inapaswa izingatie “kufanya mabadiliko makubwa kuhusu utenda-kazi wake.” Ingawa huenda likaonekana kuwa jambo lisilowezekana kupambana na ufisadi, Biblia inatuhakikishia kwamba kuna mabadiliko makubwa yanayokuja, na hakika yatatimia.

  • Ufalme wa Mungu​—Serikali Isiyo na Ufisadi
    Mnara wa Mlinzi—2015 | Januari 1
    • Yesu Kristo akikataa rushwa ya Ibilisi ya kumpa falme zote za dunia

      HABARI KUU | SERIKALI ISIYO NA UFISADI

      Ufalme wa Mungu​—Serikali Isiyo na Ufisadi

      Akieleza sababu inayofanya iwe vigumu kuukomesha ufisadi katika serikali, msimamizi mkuu wa ukaguzi wa serikali ya Nikaragua alisema hivi: “Hata maofisa wa umma ni raia tu na ikiwa raia ni wafisadi maofisa wa umma watakuwa wafisadi vilevile.”

      Bila shaka utakubali kwamba ikiwa wanadamu ni wafisadi, basi serikali yoyote watakayounda itakuwa na ufisadi. Kwa sababu hali iko hivyo, basi serikali ambayo haina ufisadi haiwezi kutoka katika chanzo cha kibinadamu. Biblia huzungumza kuhusu serikali hiyo, yaani, Ufalme wa Mungu. Hiyo ndiyo serikali ambayo Yesu aliwafundisha wafuasi wake wasali ije.—Mathayo 6:9, 10.

      Ufalme wa Mungu ni serikali halisi inayotawala kutoka mbinguni. Serikali hiyo itakuja kuzikomesha serikali zote za wanadamu. (Zaburi 2:8, 9; Ufunuo 16:14; 19:19-21) Mojawapo ya baraka ambazo Ufalme wa Mungu utawaletea wanadamu ni kukomesha ufisadi. Acheni tuchunguze mambo sita yanayotuhakikishia kuwa jambo hilo litawezekana.

      1. MAMLAKA

      TATIZO: Serikali za wanadamu hutegemezwa na raia wenyewe hasa kupitia ushuru na kodi wanazotoa. Jambo hilo huwafanya maofisa fulani washawishike kuiba pesa hizo, huku wengine wakikubali kupokea rushwa kutoka kwa watu wanaotaka kupunguziwa ushuru, au wanaoepuka kutoa malipo mengine yanayopaswa kwenda serikalini. Hilo huenda likasababisha serikali iongeze kodi ili iweze kufidia hasara inayopata, kisha kodi inapoongezwa maofisa huendelea kula rushwa hata zaidi, jambo linalofanya iwe vigumu kukomesha ufisadi. Katika hali hiyo, mara nyingi watu wanyoofu ndio wanaoumia zaidi.

      SULUHISHO: Mamlaka ya Ufalme wa Mungu inatoka kwa Mungu mweza-yote, Yehova.a (Ufunuo 11:15) Ufalme huo hauhitaji kukusanya kodi au ushuru ili kutegemeza shughuli zake. Kwa kuwa Mungu ni “hodari katika nguvu” na mkarimu kwelikweli tuna uhakika kwamba Ufalme wake utatosheleza kwa wingi mahitaji ya raia zake wote.—Isaya 40:26; Zaburi 145:16.

      2. MTAWALA

      TATIZO: Profesa Susan Rose-Ackerman aliyetajwa katika makala iliyotangulia anasema kwamba jitihada za kukomesha ufisadi “zinapaswa kuanza na viongozi wenyewe.” Serikali hukosa kuaminika wakati inapojaribu kukomesha ufisadi miongoni mwa maofisa wa polisi au wa kutoza ushuru huku ikiendelea kuwavumilia maofisa wakuu serikalini wakiendeleza uovu huo. Isitoshe, hata mtawala wa kibinadamu mwenye maadili bora amerithi dhambi. Hiyo ndiyo sababu Biblia husema, “hakuna mwanadamu aliye mwadilifu duniani ambaye huendelea kufanya mema.”—Mhubiri 7:20.

      Yesu alikataa kupokea rushwa kubwa zaidi kuwahi kutolewa

      SULUHISHO: Tofauti na watawala wa kibinadamu, Yesu Kristo, ambaye Mungu amemchagua kuwa Mfalme wa Ufalme wake, hawezi kamwe kushawishika kufanya mambo mabaya. Yesu alithibitisha ukweli wa jambo hilo alipokataa kupokea rushwa kubwa zaidi kuwahi kutolewa—“falme zote za ulimwengu na utukufu wazo.” Yesu aliahidiwa falme hizo ikiwa angefanya tendo moja la ibada ya uwongo kwa Ibilisi, mtawala wa ulimwengu. (Mathayo 4:8-10; Yohana 14:30) Hata alipokuwa akiteswa, Yesu aliazimia kubaki mwaminifu hadi kifo na alikataa kunywa dawa ambayo ingepunguza makali ya maumivu aliyokuwa akihisi na ambayo ingepumbaza hisia zake. (Mathayo 27:34) Yesu alifufuliwa na sasa yuko mbinguni. Amethibitisha kabisa kwamba anastahili kuwa Mfalme wa Ufalme wa Mungu.—Wafilipi 2:8-11.

      3. UTHABITI

      TATIZO: Raia wa nchi nyingi hufanya uchaguzi kwa ukawaida wakiwa na nia ya kuwaondoa viongozi wafisadi mamlakani. Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kwamba hata katika nchi zilizoendelea huenda kampeni za uchaguzi na uchaguzi wenyewe ukaathiriwa na ufisadi. Wakati wa kampeni, matajiri wanaweza kutumia mali zao na hata mbinu nyinginezo kuwashawishi viongozi walio madarakani na hata watakaochaguliwa.

      John Paul Stevens, hakimu anayefanya kazi kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani aliandika kwamba jambo kama hilo huathiri “si tu ubora au uhalali wa Serikali kutawala bali pia imani ambayo wananchi wanayo kuhusu serikali yenyewe.” Haishangazi kwamba watu wengi husema kwamba vyama vya kisiasa ndivyo vinavyoongoza kwa ufisadi kati ya taasisi zote duniani.

      SULUHISHO: Serikali ya Mungu ni thabiti na itadumu milele. Basi serikali hiyo haina udanganyifu wowote, kwa sababu haitakuwa na kampeni wala uchaguzi. (Danieli 7:13, 14) Isitoshe, kwa kuwa Mtawala wa Ufalme wa Mungu amechaguliwa na Mungu mwenyewe, basi hakuna kampeni za uchaguzi wala mtu yeyote anayeweza kumwondoa mamlakani Mtawala huyo. Raia wa Serikali ya Mungu wanafaidika sikuzote kwa kuwa Serikali hiyo ni thabiti na hivyo inahakikisha kwamba hatua zozote inazochukua zitawanufaisha watu kwelikweli.

      4. SHERIA

      Yesu Kristo akiwa ameketi kwenye kiti cha enzi akitawala dunia

      Ufalme wa Mungu ni serikali halisi inayotawala kutoka mbinguni

      TATIZO: Mwanzoni huenda ukadhani kwamba kutunga sheria mpya kunaweza kuboresha mambo. Kinyume na hilo, wataalamu wamegundua kwamba kuongeza idadi ya sheria mara nyingi huongeza uwezekano wa kuendeleza ufisadi. Isitoshe, mara nyingi imeonekana kwamba gharama za kutekeleza sheria zilizokusudiwa kupunguza ufisadi zinazidi faida.

      SULUHISHO: Sheria za Ufalme wa Mungu ni bora kabisa kuliko sheria za serikali za wanadamu. Kwa mfano, badala ya kutunga orodha ndefu ya sheria, Yesu alitoa Kanuni Bora. Alisema: “Kwa hiyo, mambo yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, lazima mwatendee wao pia vivyo hivyo.” (Mathayo 7:12) Sheria za Ufalme wa Mungu hukazia kuhusu nia na matendo ya raia wake. Yesu alisema hivi: “Mpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Mathayo 22:39) Bila shaka, haishangazi kwamba Mungu anatupatia sheria kama hiyo, kwani anaweza kusoma mioyo ya watu.—1 Samweli 16:7.

      5. NIA

      TATIZO: Visababishi vikuu vya ufisadi ni pupa na ubinafsi. Mara nyingi viongozi na raia wa serikali huwa na sifa hizo zisizofaa. Katika kisa tulichozungumzia kwenye makala iliyotangulia ambapo jengo la duka moja kubwa jijini Seoul liliporomoka, viongozi katika serikali walikubali kupokea rushwa kutoka kwa wajenzi ambao waliamua kutumia vifaa vya ujenzi visivyofaa na kufuata mbinu zisizofaa za ujenzi.

      Basi ili kukomesha ufisadi watu wanapaswa kuelimishwa kuhusu jinsi ya kushinda mazoea yaliyokita mizizi kama vile pupa na ubinafsi. Hata hivyo, inaonekana kwamba serikali za wanadamu hazina nia wala uwezo wa kufanya hivyo.

      SULUHISHO: Ufalme wa Mungu hupambana na chanzo au mzizi wenyewe wa ufisadi kwa kuwafundisha watu jinsi ya kushinda mielekeo au nia zisizofaa zinazosababisha ufisadi.b Elimu hiyo huwasaidia watu “kufanywa upya katika nguvu zinazoendesha akili [zao].” (Waefeso 4:23) Watu wanajifunza jinsi ya kuacha pupa na ubinafsi na badala yake kuridhika na vitu walivyo navyo na hata kutanguliza masilahi ya wengine.—Wafilipi 2:4; 1 Timotheo 6:6.

      6. RAIA

      TATIZO: Hata wafundishwe maadili bora kadiri gani na hata chini ya mazingira bora, watu wengine huchagua kuwa wafisadi na hukosa unyoofu. Wataalamu wanakiri kwamba hiyo ndiyo sababu serikali za wanadamu haziwezi kukomesha ufisadi. Serikali hizo zinaweza tu kupunguza kuenea kwa ufisadi na madhara yake.

      SULUHISHO: Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Ufisadi unasema kwamba ili kupambana na ufisadi, serikali zinapaswa kuendelea kuhimiza raia wake wawe na sifa kama vile “uaminifu, unyoofu, na kuwa tayari kuwajibika.” Ingawa kwa kweli hilo ni lengo linalofaa sana, Ufalme wa Mungu unatimiza mambo mengi zaidi ya kuwahimiza raia wake waonyeshe sifa hizo. Ufalme huo huwataka raia wake wawe na sifa hizo. Biblia husema kwamba “watu wenye pupa” na “waongo” hawataurithi Ufalme.—1 Wakorintho 6:9-11; Ufunuo 21:8.

      Watu wanaweza kuishi kulingana na maadili haya ya kiwango cha juu kama walivyofanya Wakristo zamani. Kwa mfano, mwanafunzi aliyeitwa Simoni alipojaribu kuwahonga mitume ili wamuuzie roho takatifu, mitume walikataa rushwa hiyo na kumwambia: “Tubu ubaya wako huu.” Mara moja Simoni alipotambua hatari ambayo ingemkabili kwa sababu ya tamaa yake mbaya, aliwasihi mitume wasali kwa niaba yake ili asipatwe na hatari hiyo.—Matendo 8:18-24.

      UTAFANYA NINI ILI UWE RAIA WA UFALME WA MUNGU?

      Hata iwe unatoka nchi gani, una fursa ya kuwa raia wa Ufalme wa Mungu. (Matendo 10:34, 35) Programu ya elimu inayotolewa na Ufalme wa Mungu ulimwenguni pote leo, itakusaidia kuwa raia wa Ufalme. Mashahidi wa Yehova watafurahi kukuonyesha utaratibu wa kujifunza Biblia nyumbani kwako bila malipo na mafunzo hayo yanaweza kuchukua angalau dakika kumi kila juma. Miongoni mwa mambo utakayojifunza yanatia ndani “habari njema ya Ufalme wa Mungu,” na jinsi Ufalme huo utakavyokuja kukomesha ufisadi. (Luka 4:43) Unaweza kuwasiliana na Mashahidi wa Yehova katika eneo lako au kutembelea Tovuti yetu ya jw.org/sw.

      Mtu akifundishwa Biblia nyumbani kwake bila malipo

      Je, ungependa kujifunza Biblia bila malipo?

      a Yehova ni jina la Mungu kama linavyofunuliwa katika Biblia.

      b Kwa mfano, soma makala yenye kichwa “Je, Inawezekana Kuwa Mnyoofu Katika Ulimwengu Wenye Ufisadi?” inayopatikana kwenye gazeti la Mnara wa Mlinzi la Oktoba 1, 2012.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki