Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Tatizo la Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2001 | Oktoba 22
    • Tatizo la Ulimwenguni Pote

      “Kujiua ni tatizo kubwa kwa afya ya jamii.”—David Satcher, ofisa mkuu wa afya wa Marekani, mwaka wa 1999.

      HIYO ndiyo mara ya kwanza kabisa kwa ofisa mkuu wa afya wa Marekani kutaarifu kwamba tatizo la kujiua ni jambo la kuhangaikiwa na jamii. Idadi ya watu wanaojiua nchini humo yazidi idadi ya watu wanaouawa. Haishangazi kuwa Bunge la Marekani lilitangaza kwamba kuzuia visa vya kujiua ni jambo linalopasa kushughulikiwa kwanza kotekote nchini humo.

      Hata hivyo, visa vya kujiua nchini Marekani, ambavyo vilikuwa 11.4 kati ya kila watu 100,000 mwaka wa 1997, havijafikia vile vya ulimwenguni pote vilivyochapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni mnamo mwaka wa 2000, yaani, visa 16 kati ya kila watu 100,000. Visa vya kujiua ulimwenguni pote vimeongezeka kwa asilimia 60 katika miaka 45 iliyopita. Sasa, katika mwaka mmoja tu, watu wapatao milioni moja ulimwenguni pote hujiua. Yaani, yakadiriwa kuwa baada ya kila sekunde 40, mtu mmoja hujiua!

      Hata hivyo, takwimu hazionyeshi tatizo hilo waziwazi. Katika visa vingi, familia nyingi hukana kwamba mshiriki wao alijiua. Isitoshe, yakadiriwa kwamba kila mara mtu mmoja anapojiua, watu 10 hadi 25 huwa wamejaribu kujiua. Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba asilimia 27 ya wanafunzi wa shule za sekondari nchini Marekani walikubali kwamba walikuwa wamefikiria sana kujiua katika mwaka uliotangulia; asilimia 8 ya wale waliohojiwa walisema kwamba walijaribu kujiua. Uchunguzi mwingine umefunua kwamba asilimia 5 hadi 15 ya watu wazima wamefikiria kujiua wakati fulani.

      Tofauti za Kitamaduni

      Watu huwa na maoni yanayotofautiana kuhusu kujiua. Wengine huona kujiua kuwa uhalifu, wengine huona ni tendo la woga, na bado wengine huona ni njia ya heshima ya kuomba radhi kwa kosa. Hata wengine huona kujiua kuwa njia bora ya kuendeleza harakati fulani. Kwa nini kuna maoni tofauti-tofauti? Utamaduni huchangia sana. Kwa hakika, jarida la habari la The Harvard Mental Health Letter ladokeza kwamba huenda hata utamaduni “ukachangia uwezekano wa kujiua.”

      Fikiria nchi moja katika Ulaya ya kati—Hungaria. Dakt. Zoltán Rihmer afafanua kiwango cha juu cha kujiua nchini humo kuwa “‘utamaduni’ unaohuzunisha” wa Hungaria. Béla Buda, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Afya nchini Hungaria, alisema kwamba Wahungaria huwa tayari kujiua kwa sababu yoyote. Kulingana na Buda, hili ni itikio moja la kawaida: “Anaugua kansa—anajua jinsi ya kukomesha hali hiyo.”

      Hapo zamani kulikuwa na desturi ya kidini nchini India iliyoitwa suttee. Ijapokuwa desturi hiyo ya mjane kujitupa juu ya rundo la kuni za kuchomea mwili wa mumewe ilikatazwa kwa muda mrefu, bado haijakwisha kabisa. Mwanamke mmoja alipojiua kwa njia hiyo, watu wengi wa eneo hilo walisifu sana msiba huo. Kwa mujibu wa gazeti la India Today, katika eneo hilo la India ‘wanawake wapatao 25 wamejichoma kwenye marundo ya kuni za kuchomea miili ya waume zao katika kipindi cha miaka 25.’

      Kwa kushangaza, idadi ya watu wanaojiua nchini Japani ni mara tatu ya idadi ya wanaokufa kupitia aksidenti za barabarani! Kichapo Japan—An Illustrated Encyclopedia chasema hivi: ‘Utamaduni wa Japani ambao haujashutumu kamwe kujiua, unatambuliwa kwa desturi fulani maarufu ya kujipasua matumbo (seppuku au hara-kiri).’

      Katika kitabu chake Bushido—The Soul of Japan, Inazo Nitobe, ambaye baadaye alikuwa msaidizi wa katibu mkuu wa Ushirika wa Mataifa, alieleza desturi hiyo ya kufurahia kifo. Aliandika hivi: ‘Desturi hiyo [seppuku] iliyoanzishwa katika enzi za kati, ilitumiwa na maaskari wa vita kulipia matendo yao ya uhalifu, kuomba radhi kwa makosa yao, kuhepa aibu, kulipia maovu waliyowatendea rafiki zao, au kuonyesha unyofu wao.’ Ijapokuwa desturi hiyo ya kujiua haionekani sana siku hizi, bado watu wachache huitumia ili kuathiri jamii.

      Kwa upande mwingine, katika Jumuiya ya Wakristo, kujiua kulionwa kwa muda mrefu kuwa uhalifu. Kufikia karne ya sita na ya saba, Kanisa Katoliki liliwatenga watu waliokuwa wamejiua na likakataa kuwafanyia ibada ya mazishi. Katika sehemu fulani, ushupavu wa kidini umetokeza desturi za kiajabu kuhusu watu waliojiua kama vile kuning’iniza mwili wa mtu aliyejiua, na hata kudunga moyo wake kwa mti uliochongoka.

      Kwa kushangaza, wale waliojaribu kujiua wangeweza kuhukumiwa kifo. Mwingereza mmoja wa karne ya 19 alinyongwa kwa sababu alijaribu kujiua kwa kujikata koo. Hivyo, wenye mamlaka walitimiza jambo ambalo mtu huyo alishindwa kufanya. Ijapo adhabu ya jaribio la kujiua ilibadilika baadaye, ni katika mwaka wa 1961 tu ndipo Bunge la Uingereza lilitangaza kwamba kujiua na majaribio ya kujiua hayakuwa tena matendo ya uhalifu. Katika Ireland, kujiua kulionwa kuwa uhalifu hadi mwaka wa 1993.

      Siku hizi waandishi fulani husema kwamba kujiua ni njia nyingine ya kusuluhisha matatizo. Kitabu kimoja cha mwaka wa 1991 kilichozungumzia jinsi watu wanaougua ugonjwa usio na tiba wanavyoweza kusaidiwa kujiua, kilidokeza njia mbalimbali za kufanya hivyo. Baadaye, watu wengi ambao hawakuugua ugonjwa usio na tiba walitumia mojawapo ya madokezo hayo.

      Je, kweli kujiua husuluhisha matatizo? Au, je, kuna sababu nzuri za kuendelea kuishi? Kabla hatujajibu maswali hayo, acheni kwanza tuchunguze mambo yanayofanya watu wajiue.

      [Blabu katika ukurasa wa 4]

      Katika mwaka mmoja tu, watu wapatao milioni moja ulimwenguni pote hujiua. Yaani, baada ya karibu kila sekunde 40, mtu mmoja hujiua!

  • Kwa Nini Watu Hukata Tamaa ya Kuishi?
    Amkeni!—2001 | Oktoba 22
    • Kwa Nini Watu Hukata Tamaa ya Kuishi?

      “Kila mtu anayejiua huwa na sababu zake mwenyewe: za kibinafsi, zisizojulikana, na zinazohangaisha.”—Kay Redfield Jamison, mtaalamu wa magonjwa ya akili.

      “KUISHI ni kuteseka.” Hivyo ndivyo Ryunosuke Akutagawa, mwandishi maarufu wa Japani aliyeishi katika miaka ya mapema ya karne ya 20, alivyoandika muda mfupi kabla ya kujiua. Hata hivyo, alianza sentensi hiyo kwa maneno haya: “Kwa wazi, sitaki kufa, lakini . . . ”

      Kama Akutagawa, watu wengi wanaojiua hawataki kufa lakini wanataka “kukomesha mambo yanayotukia,” ndivyo alivyosema profesa mmoja wa saikolojia. Barua ambayo watu wanaojiua huandika huonyesha hivyo. Sentensi kama vile ‘Singevumilia zaidi ya hapo’ au ‘Kwa nini niendelee kuishi?’ huonyesha tamaa kubwa ya kuepuka magumu ya maisha. Lakini kama vile mtaalamu mmoja alivyoeleza, kujiua ni “kama kutibu mafua kwa kutumia bomu la nyukilia.”

      Ijapokuwa visababishi vya kujiua hutofautiana, kwa ujumla mambo fulani hususa maishani huwachochea watu kujiua.

      Mambo Yanayowachochea

      Si ajabu kwamba vijana hufadhaika na kujiua hata kwa sababu ya mambo yanayoonekana kuwa madogo kwa watu wengine. Wanapofadhaika na kutoweza kubadili hali hiyo, huenda vijana wakaona kuwa wakijiua watakuwa wakilipiza kisasi dhidi ya watu waliowaumiza. Hiroshi Inamura, mtaalamu anayeshughulika na watu wanaotaka kujiua nchini Japani, aliandika hivi: ‘Watoto hukuza tamaa ya kumwadhibu mtu aliyewanyanyasa kwa kujiua.’

      Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi huko Uingereza ulionyesha kwamba watoto wanapodhulumiwa sana, uwezekano wa kujiua huwa karibu mara saba zaidi ya ilivyo kawaida. Watoto hao huumia sana kihisia. Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 13 aliyejitia kitanzi, aliacha barua iliyowataja vijana watano waliomnyanyasa na kumlazimisha awape pesa. Aliandika hivi: “Tafadhali waokoeni watoto wengine.”

      Huenda wengine wakajaribu kujiua wanapokuwa na matatizo shuleni au wanapovunja sheria, uhusiano wao wa kimapenzi unapovunjika, wanapoanguka mtihani, wanapofadhaishwa na mitihani, au wanapolemewa sana na mahangaiko kuhusu maisha ya baadaye. Vijana wanaobalehe ambao hufanya vyema shuleni na kupenda kufanya mambo barabara kabisa wanaweza kujaribu kujiua wasipofanikiwa au wanapokabili kipingamizi iwe ni jambo halisi au la kuwazia tu.

      Mara nyingi, matatizo ya kiuchumi au ya kikazi huwachochea watu wazima kujiua. Baada ya uchumi kuzorota kwa miaka mingi nchini Japani, hivi karibuni watu zaidi ya 30,000 walijiua katika mwaka mmoja. Kwa mujibu wa gazeti la Mainichi Daily News, robo tatu hivi ya watu wa umri wa makamo waliojiua walifanya hivyo “kwa sababu ya matatizo yanayosababishwa na madeni, kufilisika kwa biashara, umaskini na kukosa kazi.” Matatizo ya familia yanaweza pia kuwafanya watu wajiue. Gazeti moja la Finland liliripoti kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa “wanaume wa umri wa makamo waliopata talaka hivi majuzi” kujiua. Uchunguzi uliofanywa huko Hungaria ulifunua kwamba wasichana wengi wanaofikiria kujiua ni wale waliolelewa katika familia zilizovunjika.

      Kustaafu na ugonjwa ni mambo mengine pia yanayochochea watu kujiua, hasa wazee-wazee. Mara nyingi mgonjwa huamua kujiua ili kuepuka mateso, si tu anapougua ugonjwa usio na tiba, bali wakati anapoona kuwa hawezi kuvumilia kuteseka.

      Hata hivyo, si watu wote wanaojiua wanapokabili matatizo hayo. La, watu wengi wanapokabili hali hizo zenye mikazo hawajiui. Basi, ni kwa nini watu fulani hufikiri kujiua ni suluhisho, na wengine hawafikiri hivyo?

      Visababishi Visivyoonekana Wazi

      Kay Redfield Jamison, profesa wa magonjwa ya akili kwenye Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, asema hivi: “Uamuzi wa kujiua hutegemea hasa jinsi mtu anavyoelewa mambo.” Aongezea hivi: “Akili za watu wengi, zinapokuwa timamu, hazioni kuwa jambo lolote lile linaweza kumfadhaisha mtu hata ajiue.” Eve K. Mościcki, wa Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili, asema kwamba visababishi vingi—vingine visivyoonekana wazi—hujumlika kuwaongoza watu kujiua. Visababishi hivyo visivyoonekana wazi vyatia ndani magonjwa ya akili na magonjwa yanayosababishwa na uraibu, maumbile ya chembe za urithi, na utendaji wa kemikali ubongoni. Tutachunguza baadhi ya visababishi hivyo.

      Visababishi vikuu zaidi ni magonjwa yanayosababishwa na uraibu na magonjwa ya akili, kama vile kushuka moyo, magonjwa ya hisia zinazobadilika-badilika, sizofrenia (kuchanganyikiwa kiakili), na kutumia vibaya vileo au dawa za kulevya. Uchunguzi uliofanywa huko Ulaya na Marekani unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaojiua huugua magonjwa hayo. Kwa kweli, watafiti wa Sweden waligundua kwamba visa vya kujiua miongoni mwa wanaume wasiougua magonjwa hayo vilikuwa 8.3 kati ya wanaume 100,000, lakini miongoni mwa wale walioshuka moyo viliongezeka hadi visa 650 kati ya wanaume 100,000! Na wataalamu wanasema kwamba hivyo ndivyo visababishi vya kujiua pia katika nchi za Mashariki. Lakini, hata mambo yanayochochea watu kujiua yakijumlishwa pamoja na kushuka moyo, bado yawezekana kuepuka kujiua.

      Profesa Jamison, ambaye wakati mmoja alijaribu kujiua, asema hivi: “Watu huonekana kuwa wanaweza kustahimili au kuvumilia kushuka moyo maadamu wanatumai kwamba mambo yatakuwa afadhali.” Hata hivyo, amegundua kwamba mtu asipoweza kustahimili mfadhaiko unaoongezeka hatua kwa hatua, uwezo wa mfumo wa akili wa kuzuia tamaa ya kujiua hupungua pole kwa pole. Analinganisha hali hiyo na jinsi breki za gari zinavyokwisha kwa sababu ya mkazo mwingi.

      Ni muhimu kutambua mwelekeo huo kwani yawezekana kutibu mshuko wa moyo. Mtu anayehisi kuwa hajiwezi anaweza kurudia hali yake ya kawaida. Visababishi visivyoonekana wazi vikishughulikiwa, watu wanaweza kutenda kwa njia tofauti wanapokumbwa na maumivu ya kihisia na mikazo ambayo mara nyingi huchochea watu kujiua.

      Watu fulani hufikiri kwamba maumbile ya chembe za urithi ni kisababishi kisichoonekana wazi cha visa vingi vya kujiua. Ni kweli kwamba chembe za urithi huchangia hisia za mtu kwa njia fulani, na uchunguzi umefunua kwamba familia nyingine huwa na visa vingi vya kujiua zaidi ya nyingine. Lakini, “mwelekeo wa kujiua uliorithiwa haumaanishi kamwe kwamba mtu hawezi kuepuka kujiua,” asema Jamison.

      Utendaji wa kemikali ubongoni ni kisababishi kingine kisichoonekana wazi. Mabilioni ya chembe za neva huwasiliana ubongoni kupitia utendaji wa kemikali. Kwenye ncha zilizotengana za nyuzi za neva kuna mapengo madogo yanayoitwa sinapsi. Vitu fulani hupitisha habari kwenye sinapsi kupitia utendaji wa kemikali. Huenda kiasi cha serotonin, kimojawapo cha vitu vinavyopitisha habari, huchangia uwezekano wa kibiolojia wa mtu kujiua. Kitabu Inside the Brain chaeleza hivi: “Kiasi kidogo cha serotonin . . . chaweza kumnyang’anya mtu furaha maishani, kwa kupunguza tamaa yake ya kuishi na kuongeza uwezekano wa kushuka moyo na kujiua.”

      Hata hivyo, jambo la hakika ni kwamba hakuna mtu aliyepangiwa kujiua. Mamilioni ya watu hukabiliana na maumivu ya kihisia na mikazo. Wengine hujiua kutokana na jinsi ubongo na moyo unavyotenda wanapokabili mikazo. Mbali na kushughulikia mambo yanayochochea watu kujiua, ni lazima visababishi visivyoonekana wazi vishughulikiwe pia.

      Hivyo basi, ni jambo gani linalopasa kufanywa ili mtu awe na maoni yanayofaa yatakayomfanya afurahie tena kuishi?

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Jinsia na Kujiua

      Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa huko Marekani, ingawa uwezekano wa wanawake kujaribu kujiua ni mara mbili au tatu ya ule wa wanaume, uwezekano wa wanaume kufaulu kujiua ni mara nne ya ule wa wanawake. Uwezekano wa wanawake kushuka moyo ni mara mbili ya ule wa wanaume. Huenda hilo likaonyesha ni kwa nini wanawake wengi hujaribu kujiua. Hata hivyo, huenda magonjwa yao ya kushuka moyo hayawafanyi kuwa hatari sana. Hivyo hawatumii njia hatari sana za kujiua. Kwa upande mwingine, huenda wanaume wakatumia njia hatari za kujiua ili kuhakikisha kwamba watafaulu.

      Hata hivyo, nchini China, wanawake ndio hufaulu kujiua zaidi ya wanaume. Kwa hakika, uchunguzi unafunua kwamba asilimia 56 hivi ya visa vya wanawake wanaojiua ulimwenguni hutukia China, hasa katika maeneo ya mashambani. Yasemekana kuwa mojawapo ya sababu za wanawake kujaribu na kufaulu kujiua nchini humo ni kwamba ni rahisi kupata dawa hatari za kuua wadudu.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Kujiua na Upweke

      Upweke ni mojawapo ya mambo yanayofanya watu washuke moyo na kujiua. Jouko Lönnqvist, ambaye aliongoza uchunguzi mmoja kuhusu visa vya kujiua nchini Finland, alisema hivi: “Watu wengi [waliojiua], walihisi upweke kila siku. Walikuwa na wakati mwingi lakini hawakushirikiana sana na watu.” Kenshiro Ohara, mtaalamu wa magonjwa ya akili kwenye Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Hamamatsu nchini Japani, alitaarifu kwamba “kujitenga” kulisababisha ongezeko la hivi majuzi la idadi ya wanaume wa makamo waliojiua nchini humo.

      [Picha katika ukurasa wa 5]

      Mara nyingi, matatizo ya kiuchumi au ya kikazi huwachochea watu wazima kujiua

  • Unaweza kupata Msaada
    Amkeni!—2001 | Oktoba 22
    • Unaweza kupata Msaada

      ‘MNA tembe 49 za usingizi ndani ya kikombe. Je, nizimeze au nisizimeze?’ Hivyo ndivyo mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 28 nchini Uswisi alivyojiuliza. Mkewe na watoto walikuwa wamemwacha, na alikuwa ameshuka moyo sana. Hata hivyo, baada ya kumeza tembe hizo, alijiambia hivi: ‘La. Sitaki kufa!’ Jambo zuri ni kwamba hakufa. Nyakati nyingine watu wanaotaka kujiua hawafaulu.

      Alex Crosby wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa alisema hivi kuhusu matineja waliojaribu kujiua: ‘Ukiwazuia hata kwa saa chache tu wasijiue, unaweza kukomesha nia hiyo. Unaweza kuwazuia wengi wasijiue kwa kuingilia kati. Unaweza kuokoa uhai wao.’

      Profesa Hisashi Kurosawa alipokuwa akifanya kazi kwenye Kituo cha Dharura cha Kuokoa Uhai kwenye Chuo cha Mafunzo ya Tiba cha Japani, aliwasaidia mamia ya watu waliotaka kujiua watamani tena kuishi. Naam, nia hiyo ikizuiwa kwa njia fulani, uhai unaweza kuokolewa. Ni msaada gani unaohitajiwa?

      Kushughulikia Matatizo Yasiyoonekana Wazi

      Kama ilivyoonyeshwa katika makala iliyotangulia, watafiti wanasema kwamba asilimia 90 ya watu waliojiua walikuwa na magonjwa ya akili au walitumia vileo kupita kiasi au dawa za kulevya. Hivyo, Eve K. Mościcki wa Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili, asema hivi: “Njia kuu ya kuzuia watu wa kila umri wasijiue ni kuzuia magonjwa ya akili na uraibu.”

      Inahuzunisha kwamba wengi wanaougua magonjwa hayo hawataki kutafuta msaada. Kwa nini? ‘Ni kwa sababu watu wengi wana maoni mabaya,’ asema Yoshitomo Takahashi wa Taasisi ya Magonjwa ya Akili ya Mji wa Tokyo. Anaongezea kwamba kutokana na hilo, hata watu wanaohisi wanaugua kidogo husita kutafuta matibabu mara moja.

      Hata hivyo, watu fulani hawaaibiki kutafuta msaada. Hiroshi Ogawa, mtangazaji maarufu wa televisheni ambaye ameendesha kipindi chake mwenyewe kwa miaka 17 nchini Japani, alikubali hadharani kwamba ameshuka moyo na kwamba alikuwa karibu kujiua. Ogawa alisema hivi: “Kushuka moyo ni kama mafua yanayoathiri akili.” Alieleza kwamba mtu yeyote anaweza kuambukizwa lakini anaweza kupona.

      Zungumza na Mtu Fulani

      Béla Buda, afisa wa afya wa Hungaria aliyenukuliwa hapo awali, asema hivi: “Mtu asipolitaja tatizo lake, kwa kawaida yeye huliona kuwa kubwa sana na lisiloweza kutatuliwa.” Maoni yake yanakazia hekima ya mithali ya kale ya Biblia: “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; hushindana na kila shauri jema.”—Mithali 18:1.

      Zingatia maneno hayo ya hekima. Usiumie peke yako unapokumbwa na matatizo mengi ya kibinafsi yenye kulemea. Tafuta mtu anayeaminika unayeweza kumfunulia matatizo hayo. Huenda ukasema, ‘Lakini sina mtu yeyote ninayeweza kumfunulia matatizo.’ Dakt. Naoki Sato, mtaalamu wa magonjwa ya akili, alisema kwamba watu wengi huhisi hivyo. Sato alisema kwamba huenda wagonjwa wengi huepuka kuwaeleza wengine matatizo yao kwa kuwa hawataki kufunua udhaifu wao.

      Mtu atapata wapi atakayemsikiliza? Katika sehemu nyingi anaweza kutafuta msaada kutoka kwa kituo kinachozuia watu kujiua au kuwapigia simu watu wanaoandaa msaada kwa matatizo ya kibinafsi au kumwona daktari anayeaminika ambaye hushughulikia matatizo ya kihisia. Lakini wataalamu fulani pia hung’amua kwamba kuna chanzo kingine cha msaada—dini. Dini yaweza kusaidiaje?

      Kupata Msaada Unaohitajiwa

      Mtu mmoja mlemavu huko Bulgaria anayeitwa Marin, alitaka sana kujiua. Siku moja aliliona gazeti la kidini la Mnara wa Mlinzi, linalochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Alikubali mwaliko wa kutembelewa na Mashahidi wa Yehova uliotolewa katika gazeti hilo. Marin anaeleza matokeo: “Walinifundisha kwamba uhai ni zawadi kutoka kwa Baba yetu wa kimbingu na hatuna haki ya kujidhuru wala kujiua kimakusudi. Basi niliacha kutamani kujiua na nikapenda tena kuishi!” Marin pia alisaidiwa kwa upendo na kutaniko la Kikristo. Ijapokuwa bado yeye ni mlemavu, asema hivi: “Sasa siku zangu ni zenye shangwe na utulivu, na kuna mambo mengi ya kufanya yanayopendeza—mengi zaidi hata sina wakati wa kutosha! Yote hayo yamewezekana kwa sababu ya Yehova na Mashahidi wake.”

      Yule mwanamume kijana Mswisi aliyetajwa hapo mwanzoni alisaidiwa pia na Mashahidi wa Yehova. Sasa anasimulia kuhusu “fadhili ya familia moja ya Kikristo” ambayo ilikubali kuishi naye. Aongezea hivi: “Baadaye, washiriki wa kutaniko [la Mashahidi wa Yehova] walinialika kwenye milo kwa siku nyingi. Kilichonisaidia hasa si tu kutendewa kwa ukarimu bali pia kuweza kuzungumza na mtu fulani.”

      Mwanamume huyo alitiwa moyo sana na yale aliyojifunza katika Biblia, hasa alipojifunza kuhusu upendo ambao Mungu wa kweli, Yehova, anao kwa wanadamu. (Yohana 3:16) Kwa kweli, Yehova Mungu anakusikiliza ‘unapofunua moyo wako’ mbele zake. (Zaburi 62:8) ‘Macho yake hukimbia-kimbia duniani mwote,’ si ili atafute makosa ya wanadamu, bali “ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake.” (2 Mambo ya Nyakati 16:9) Yehova atuhakikishia hivi: “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”—Isaya 41:10.

      Mwanamume huyo Mswisi alisema hivi kuhusu ahadi ya Mungu ya ulimwengu mpya: “Imepunguza sana fadhaa yangu.” Tumaini hilo, linalofafanuliwa kuwa “nanga ya nafsi,” latia ndani ahadi ya uhai udumuo milele katika Paradiso duniani.—Waebrania 6:19; Zaburi 37:10, 11, 29.

      Maisha Yako Ni Yenye Thamani kwa Wengine

      Ni kweli kuwa unaweza kukabili hali zinazokufanya uhisi kwamba u peke yako kabisa na kwamba ukifa hakuna atakayejali. Lakini kumbuka: Kuna tofauti kubwa kati ya kuhisi u peke yako na kuwa peke yako. Katika nyakati za Biblia, nabii Eliya alifadhaika maishani mwake. Alimwambia Yehova hivi: ‘Wamewaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu.’ Naam, Eliya alihisi kwamba alikuwa peke yake kabisa—na alihisi hivyo kwa sababu fulani. Manabii wenzake wengi walikuwa wameuawa. Alikuwa ametishwa kuuawa, na alikuwa anakimbia ili kujiokoa. Lakini je, kweli alikuwa peke yake? La. Yehova alimjulisha kwamba kulikuwa na watu 7,000 waaminifu ambao, kama yeye, walikuwa wanajitahidi kumtumikia Mungu wa kweli kwa uaminifu katika nyakati hizo za kuhuzunisha. (1 Wafalme 19:1-18) Lakini, vipi wewe? Je, yawezekana kwamba huko peke yako kama unavyohisi?

      Kuna watu wanaokujali. Unaweza kufikiria wazazi wako, mwenzi wako, watoto wako, na rafiki zako. Lakini kuna wengi zaidi. Katika kutaniko la Mashahidi wa Yehova, unaweza kuwapata Wakristo wakomavu wanaopendezwa nawe, watakaokusikiliza kwa subira, na kusali pamoja nawe na kwa ajili yako. (Yakobo 5:14, 15) Na hata kila mtu asiyekamilika akikutupa, kuna Mmoja ambaye hatakuacha. Mfalme Daudi wa kale alisema hivi: “Baba yangu na mama yangu wameniacha, bali BWANA atanikaribisha kwake.” (Zaburi 27:10) Naam, Yehova ‘anakujali.’ (1 Petro 5:7) Katu usisahau kwamba una thamani machoni pa Yehova.

      Uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ni kweli kwamba nyakati nyingine uhai unaweza kuonekana kuwa mzigo mzito badala ya zawadi. Hata hivyo, je unaweza kuwazia jinsi ungehisi iwapo ungempa mtu zawadi yenye thamani kisha aitupe hata kabla ya kuitumia? Sisi wanadamu wasiokamilika hatujatumia kikamili zawadi ya uhai. Kwa hakika, Biblia huonyesha kwamba machoni pa Mungu uhai tulio nao sasa hivi si “uhai ulio halisi.” (1 Timotheo 6:19) Naam, karibuni uhai wetu utakuwa kamili, wenye maana zaidi, na wenye kufurahisha zaidi. Jinsi gani?

      Biblia yasema hivi: “[Mungu] atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.” (Ufunuo 21:3, 4) Hebu wazia jinsi uhai wako utakavyokuwa maneno hayo yatakapotimia. Tulia. Jaribu kupiga picha kamili yenye kuvutia akilini. Picha hiyo si ndoto tu isiyo na maana. Unapotafakari jinsi Yehova alivyoshughulika na watu wake zamani, utamwamini zaidi na utaona picha hiyo kihalisi zaidi.—Zaburi 136:1-26.

      Huenda ikachukua muda fulani kabla hujawa tena na tamaa ya kuishi. Endelea kusali kwa “Mungu wa faraja yote, ambaye hutufariji katika dhiki yetu yote.” (2 Wakorintho 1:3, 4; Waroma 12:12; 1 Wathesalonike 5:17) Yehova atakupa nguvu unayohitaji. Atakufundisha kwamba uhai una thamani.—Isaya 40:29.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

      Utamsaidiaje Mtu Anayeonyesha Dalili za Kujiua?

      Unapaswa kufanya nini mtu akikuambia kwamba anataka kujiua? Shauri la Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) ni hili: “Sikiliza kwa makini.” Acha aeleze jinsi anavyohisi. Hata hivyo, katika visa vingi, mtu anayetaka kujiua hujitenga na kunyamaza. Tambua kwamba maumivu au hali ya kukosa tumaini inayomkumba ni halisi. Ukimtajia kwa upole mabadiliko fulani mahususi ambayo umeona katika tabia yake, huenda utamfanya akufunulie matatizo yake yote.

      Onyesha huruma unapomsikiliza. “Ni muhimu kukazia kwamba uhai wake ni wenye thamani kwako na kwa wengine,” lasema shirika la CDC. Mjulishe jinsi kifo chake kitakavyokuumiza na kuwaumiza wengine vilevile. Msaidie mtu huyo atambue kwamba Muumba wake anamjali.—1 Petro 5:7.

      Wataalamu pia wanadokeza kwamba vitu vyovyote ambavyo mtu huyo aweza kutumia kujiua viondolewe—hasa bunduki. Hali ikionekana kuwa hatari, huenda ukapenda kumtia moyo mtu huyo amwone daktari. Katika hali mbaya zaidi huenda wewe mwenyewe ukalazimika kuomba huduma ya kitiba ya dharura.

      [Sanduku katika ukurasa wa 11]

      ‘Je, Mungu Atanisamehe kwa Kuhisi Hivi?’

      Kushirikiana na Mashahidi wa Yehova kumewasaidia watu wengi kukomesha nia ya kujiua. Hata hivyo, leo hakuna mtu asiyeweza kukumbwa na mikazo au kushuka moyo. Mara nyingi, Wakristo waliofikiria kujiua hujilaumu sana kwa kufikiri hivyo. Kujilaumu huzidisha tu matatizo yao. Basi mtu anaweza kukabilianaje na hisia hizo?

      Yafaa kung’amua kwamba wanaume na wanawake fulani waaminifu wa nyakati za Biblia walieleza juu ya hisia zao zisizofaa kuhusu uhai. Wakati mmoja Rebeka, mke wa yule mzee wa ukoo Isaka, alihuzunishwa sana na tatizo la familia kiasi cha kusema hivi: “Sina raha kabisa maishani.” (Mwanzo 27:46, Biblia Habari Njema) Yobu, aliyepoteza watoto wake, afya yake, mali yake, na hadhi yake ya kijamii, alisema hivi: “Nayachukia maisha yangu!” (Ayubu 10:1, BHN) Wakati fulani Musa alimlilia Mungu akisema: “Nakuomba uniulie mbali.” (Hesabu 11:15) Eliya, nabii wa Mungu, alisema hivi wakati fulani: “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu.” (1 Wafalme 19:4, BHN) Naye nabii Yona alirudia kusema hivi: “Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.”—Yona 4:8.

      Je, Yehova aliwashutumu watu hao kwa kuhisi hivyo? La. Hata alihifadhi maneno yao katika Biblia. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba hakuna hata mmoja wa waaminifu hao aliyeruhusu hisia zake zimchochee kujiua. Yehova aliwathamini; alitaka waishi. Jambo la hakika ni kwamba, Mungu hujali hata uhai wa watu waovu. Anawasihi wabadilike ‘waendelee kuishi.’ (Ezekieli 33:11, NW) Jinsi angependa wale wanaohangaikia kupata kibali chake waendelee kuishi!

      Mungu ameandaa dhabihu ya fidia ya Mwanawe, kutaniko la Kikristo, Biblia, na pendeleo la sala. Njia hiyo ya mawasiliano pamoja na Mungu—sala—yaweza kutumiwa nyakati zote. Mungu anaweza na atawasikiliza wote wanaomfikia wakiwa na moyo mweupe na mnyenyekevu. “Kwa hiyo, acheni tukaribie kwa uhuru wa usemi kwenye kiti cha ufalme cha fadhili isiyostahiliwa, ili tuweze kupokea rehema na kupata fadhili isiyostahiliwa kwa msaada katika wakati ufaao.”—Waebrania 4:16.

      [Sanduku katika ukurasa wa 12]

      Je, Mpendwa Wako Amejiua?

      Mtu anapojiua, washiriki wa familia na rafiki wa karibu huumia sana kiakili. Wengi hujilaumu kwa msiba huo. Wanasema mambo kama vile: ‘Laiti ningalitumia wakati mwingi zaidi naye siku hiyo,’ ‘Laiti ningalizuia ulimi wangu wakati huo,’ ‘Laiti ningalimsaidia zaidi.’ Yaani wanamaanisha, ‘Laiti ningalifanya hivi au vile, mpendwa wangu bado angalikuwapo.’ Hata hivyo, je, yafaa kujilaumu mtu anapojiua?

      Kumbuka kwamba ni rahisi sana kujua dalili za mtu anayenuia kujiua baada ya mtu huyo kujiua. Kabla ya hapo si rahisi kuzijua. Biblia husema: “Moyo waujua uchungu wake wenyewe, wala mgeni hawezi kushiriki furaha yake.” (Mithali 14:10, BHN) Nyakati nyingine, haiwezekani kujua mambo ambayo mtu mwingine anafikiri au kuhisi. Watu wengi wanaotaka kujiua hawawezi kuwaeleza wengine hisia zao za ndani vizuri, hata kama ni washiriki wa karibu wa familia.

      Kitabu Giving Sorrow Words chasema hivi kuhusu dalili za mtu anayetaka kujiua: “Ukweli ni kwamba kwa kawaida si rahisi kutambua dalili hizo.” Kitabu hichohicho chaongezea kusema kwamba hata ikiwa ulitambua dalili fulani, hiyo haimaanishi kwamba ungemzuia mtu huyo asijiue. Badala ya kujiumiza, unaweza kufarijiwa na maneno haya ya Mfalme Solomoni mwenye hekima: “Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote.” (Mhubiri 9:5) Mpendwa wako hateswi motoni. Na yale mateso ya kiakili au ya kihisia yaliyomfanya ajiue yamekwisha. Hateseki; anapumzika tu.

      Kwa sasa, huenda ingefaa kuhangaikia hali ya walio hai, kutia ndani wewe. Solomoni aliendelea kusema hivi: “Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako” ukiwa hai. (Mhubiri 9:10) Unaweza kuwa na hakika kwamba mataraja ya uhai ya wakati ujao kwa wale waliojiua yako mikononi mwa Yehova, “Baba ya rehema nyororo na Mungu wa faraja yote.”—2 Wakorintho 1:3.a

      [Maelezo ya Chini]

      a Utapata maoni yaliyosawazika kuhusu mataraja ya wakati ujao kwa wale waliojiua katika makala “Maoni ya Biblia: Kujiua—Kuna Ufufuo?” katika toleo la Amkeni! la Septemba 8, 1990.

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Zungumza na mtu fulani

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Uhai wako una thamani kwa wengine

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki