-
Sikukuu ya Kupitwa Iliyo ya Mwisho kwa Yesu YakaribiaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 112
Sikukuu ya Kupitwa Iliyo ya Mwisho kwa Yesu Yakaribia
JUMANNE, Nisani 11, ikaribiapo, Yesu amaliza kufundisha mitume juu ya Mlima wa Mizeituni. Lo, imekuwa siku yenye mikazo na shughuli kama nini! Sasa, labda akiwa anarudi Bethania akakae huko usiku huo, awaambia hivi mitume wake: “Nyinyi mwajua kwamba siku mbili kuanzia sasa sikukuu ya Kupitwa yatukia, na Mwana wa binadamu atatolewa atundikwe.”
Siku inayofuata, Jumatano, Nisani 12, yaonekana Yesu ajitenga ili kwa utulivu awe na mitume wake. Siku iliyotangulia, alikuwa amewakemea peupe viongozi wa kidini, naye ang’amua kwamba wanatafuta kumwua. Kwa hiyo siku ya Jumatano hajionyeshi waziwazi, kwa kuwa hataki kitu chochote kikatize kuadhimisha kwake Sikukuu ya Kupitwa pamoja na mitume wake jioni inayofuata.
Wakati uo huo, makuhani wakuu na wanaume wazee wa watu wamekusanyika katika ua wa kuhani wa juu, Kayafa. Wakiwa na udhia wa kushambuliwa na Yesu siku iliyotangulia, wanafanya mipango ya kumbamba kwa mbinu ya ujanja na kufanya auawe. Na bado wanafuliza kusema hivi: “Si kwenye ule msherehekeo, ili kwamba zahama yoyote isitokee miongoni mwa watu.” Wanawahofu watu, ambao Yesu huonea shangwe ya kibali chao.
Huku viongozi wa kidini wakitunga kwa uovu njama ya kumwua Yesu, wapokea mgeni. Wao washangazwa na jambo la kwamba ni mmoja wa mitume wa Yesu mwenyewe, Yuda Iskariote, mmoja ambaye Shetani amepanda ndani yake lile wazo bovu la kusaliti Bwana-Mkubwa wake! Wao wapendezwa kama nini Yuda aulizapo hivi: “Nyinyi mtanipa nini nikimsaliti yeye kwenu?” Wao waafikiana kwa mteremo kumlipa vipande 30 vya fedha, bei ya mtumwa kulingana na agano la Sheria ya Musa. Tangu hapo na kuendelea, Yuda atafuta fursa nzuri ya kumsaliti Yesu kwao wakati pasipokuwa na umati karibu.
Nisani 13 yaanza kwenye mshuko-jua wa Jumatano. Yesu aliwasili kutoka Yeriko siku ya Ijumaa, kwa hiyo huu ndio usiku wa sita na wa mwisho ambao atumia akiwa Bethania. Siku inayofuata, Alhamisi, matayarisho ya mwisho yatahitaji kufanywa kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa, ambayo yaanza kwenye mshuko-jua. Huo ndio wakati ambapo ni lazima mwana-kondoo wa Sikukuu ya Kupitwa achinjwe halafu achomwe akiwa mzima. Wataadhimisha wapi karamu hiyo, na ni nani atafanya matayarisho?
Yesu hajaandaa maelezo hayo, labda ili kumzuia Yuda asiwapashe habari makuhani wakuu ili waweze kumkamata Yesu wakati wa mwadhimisho wa Sikukuu ya Kupitwa. Lakini sasa, labda ikiwa ni mapema alasiri ya Alhamisi, Yesu awatuma Petro na Yohana kutoka Bethania, akisema: “Endeni mkatutayarishie sikukuu ya kupitwa ili tule.”
“Wataka tuitayarishe wapi?” wao wauliza.
“Mwingiapo jijini,” Yesu aeleza, “mwanamume mmoja mwenye kubeba nyungu ya maji atawalaki. Mfuateni ndani ya nyumba ambamo yeye aingia. Nanyi ni lazima mseme kwa mmiliki-ardhi wa ile nyumba, ‘Mwalimu asema kwako hivi: “Kiko wapi chumba cha mgeni ambamo mimi naweza kula sikukuu ya kupitwa pamoja na wanafunzi wangu?”’ Na mwanamume huyo atawaonyesha chumba cha juu kikubwa chenye vifaa. Itayarisheni humo.”
Bila shaka mmiliki-ardhi huyo ni mwanafunzi wa Yesu ambaye labda atazamia ombi la Yesu kutumia nyumba yake kwa pindi hii maalumu. Vyovyote vile, Petro na Yohana wawasilipo katika Yerusalemu, wakuta kila kitu kama vile Yesu alivyotabiri. Kwa hiyo wao wawili wahakikisha kwamba mwana-kondoo yuko tayari na kwamba mipango mingine yote yafanywa ili kutimiza mahitaji ya waadhimishi wale 13 wa Sikukuu ya Kupitwa, Yesu na mitume wake 12. Mathayo 26:1-5, 14-19; Marko 14:1, 2, 10-16; Luka 22:1-13; Kutoka 21:32, NW.
▪ Yaonekana Yesu afanya nini Jumatano, na kwa nini?
▪ Ni mkutano gani ambao wafanywa nyumbani kwa kuhani wa juu, na Yuda awazuru viongozi wa kidini kwa kusudi gani?
▪ Yesu atuma nani wakaingie Yerusalemu Alhamisi, na kwa kusudi gani?
▪ Hawa waliotumwa wakuta nini ambacho kwa mara nyingine tena chafunua nguvu za kimwujiza za Yesu?
-
-
Unyenyekevu Kwenye Sikukuu ya Kupitwa ya MwishoYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 113
Unyenyekevu Kwenye Sikukuu ya Kupitwa ya Mwisho
PETRO na Yohana, kwa kuagizwa na Yesu, tayari wamewasili katika Yerusalemu kufanya matayarisho kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa. Yesu awasili baadaye alasiri, yaonekana akiwa na wale mitume wengine kumi. Jua linazama chini kwenye upeo wa macho huku Yesu na kikundi chake wakiteremka chini ya Mlima wa Mizeituni. Hii ndiyo mara ya mwisho ya Yesu kuliona jiji wakati wa mchana kutoka mlima huu mpaka baada ya ufufuo wake.
Muda si muda Yesu na kikundi chake wawasili katika jiji na kushika njia kwenda kwenye nyumba ambamo wataadhimisha Sikukuu ya Kupitwa. Wazipanda ngazi kwenda kwenye chumba kikubwa cha juu, ambamo wapata matayarisho yote yamefanywa kwa ajili ya mwadhimisho wao wa faragha wa Sikukuu ya Kupitwa. Yesu ameitazamia pindi hii, kwa vile asema: “Mimi nimetamani sana kuila sikukuu ya kupitwa hii pamoja na nyinyi kabla sijateseka.”
Kimapokeo, vikombe vinne vya divai hunywewa na washiriki wa Sikukuu ya Kupitwa. Baada ya kupokea kile ambacho yaonekana ndicho kikombe cha tatu, Yesu ashukuru na kusema: “Chukueni hiki na mkipitishe kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine miongoni mwenu wenyewe; kwa maana mimi nawaambia nyinyi, Kuanzia sasa na kuendelea sitakunywa tena kutoka zao la mzabibu mpaka ufalme wa Mungu uwasili.”
Wakati fulani katika mlo huo, Yesu ainuka, aweka kando mavazi yake ya nje, achukua taulo, na kujaza karai maji. Kwa kawaida, mwenye kupokea wageni ndiye angehakikisha kwamba nyayo za mgeni zimeoshwa. Lakini kwa kuwa katika pindi hii hakuna mwenye kupokea wageni, Yesu afanya utumishi huu wa kibinafsi. Yeyote wa mitume angaliweza kuwa amebamba fursa hiyo ili kufanya hivyo; na bado, yaonekana kwa sababu ushindani fulani ungali miongoni mwao, hakuna afanyaye hivyo. Sasa wao waaibika Yesu aanzapo kuosha nyayo zao.
Yesu amjiapo, Petro ateta akisema: “Kwa hakika wewe hutaosha kamwe nyayo zangu.”
“Mimi nisipokuosha wewe, wewe huna sehemu pamoja na mimi,” Yesu asema.
“Bwana,” Petro aitikia, “si nyayo zangu tu, bali pia mikono yangu na kichwa changu.”
“Yeye ambaye ameoga,” Yesu ajibu, “hahitaji kuoshwa zaidi ya nyayo zake, bali ni safi kabisa. Na nyinyi watu ni safi, lakini si nyote.” Asema hivyo kwa sababu ajua kwamba Yuda Iskariote anapanga kumsaliti.
Yesu akiisha kuosha nyayo za wote 12, kutia na nyayo za msaliti wake, Yuda, avaa mavazi yake ya nje na kuegemea mezani tena. Halafu auliza: “Je! nyinyi mwajua lile ambalo mimi nimewafanyia nyinyi? Nyinyi huniita, ‘Mwalimu,’ na, ‘Bwana,’ na mwasema ifaavyo, kwa maana ndivyo nilivyo. Kwa hiyo, ikiwa mimi, ijapokuwa ni Bwana na Mwalimu, nimeosha nyayo zenu, nyinyi pia mwapaswa kuosha nyayo za mmoja na mwenzake. Kwa maana mimi niliwawekea nyinyi kigezo, kwamba, kama vile mimi nilivyowafanyia nyinyi, nyinyi mwapaswa kufanya hivyo pia. Kwa kweli kabisa mimi nasema kwenu nyinyi, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana-mkubwa wake, wala mwenye kutumwa si mkubwa kuliko mwenye kumtuma. Ikiwa mwajua mambo haya, wenye furaha ni nyinyi ikiwa mwayafanya.”
Lo, somo zuri kama nini la utumishi wa unyenyekevu! Mitume hawapaswi kuwa wakitafuta mahali pa kwanza, wakifikiri kwamba wao ni wa maana sana hivi kwamba wengine wapaswa kuwatumikia wao sikuzote. Wao wahitaji kufuata kigezo kilichowekwa na Yesu. Hicho si kigezo cha uoshaji nyayo kidesturi tu. Sivyo, bali ni cha nia ya kutumikia bila upendeleo, hata kama kazi ile ni ya umaana mdogo au isiyopendeza kwa kadiri gani. Mathayo 26:20, 21; Marko 14:17, 18; Luka 22:14-18; 7:44; Yohana 13:1-17, NW.
▪ Ni jambo gani lisilo na kifani juu ya Yesu kuona Yerusalemu aingiapo ili kuadhimisha Sikukuu ya Kupitwa?
▪ Wakati wa Sikukuu ya Kupitwa, yaonekana ni kikombe gani ambacho Yesu apitisha kwa wale mitume 12 baada ya kusema baraka?
▪ Ni utumishi gani wa kibinafsi ulioandaliwa wageni kidesturi Yesu alipokuwa duniani, na kwa nini haukuandaliwa wakati wa Sikukuu ya Kupitwa iliyoadhimishwa na Yesu na mitume?
▪ Kusudi la Yesu lilikuwa nini katika kufanya utumishi huo wenye umaana mdogo wa kuosha nyayo za mitume wake?
-
-
Kijio cha UkumbushoYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 114
Kijio cha Ukumbusho
BAADA ya Yesu kuosha miguu ya mitume wake, yeye anukuu andiko lililo kwenye Zaburi 41:9, NW, akisema: “Yeye aliyekuwa akila mkate wangu ameinua kisigino chake dhidi yangu.” Halafu, akifadhaika katika roho, aeleza hivi: “Mmoja wenu nyinyi atanisaliti.”
Mitume waanza kuwa na kihoro na kumwambia Yesu hivi mmoja baada ya mwingine: “Si mimi, au sivyo?” Hata Yuda Iskariote ajiunga katika kuuliza. Yohana, ambaye amejinyoosha karibu na Yesu mezani, aegemea nyuma kwenye kifua cha Yesu na kuuliza: “Bwana, ni nani?”
“Ni mmoja wa wale kumi na wawili, ambaye anachovya pamoja nami ndani ya bakuli la ujumla,” Yesu ajibu. “Kweli, Mwana wa binadamu anaenda zake, kama vile imeandikwa kuhusu yeye, lakini ole wake mtu huyo ambaye kupitia yeye Mwana wa binadamu asalitiwa! Ingalikuwa vizuri zaidi kwa mtu huyo kama asingalizaliwa.” Baada ya hapo, Shetani amwingia Yuda tena, akitumia kwa faida yake ile nafasi wazi iliyo katika moyo wake, ambao umekuwa mwovu. Baadaye usiku huo, kwa kufaa Yesu amwita Yuda “mwana wa uharibifu.”
Sasa Yesu amwambia Yuda: “Unalolifanya lifanyishe kwa haraka zaidi.” Hakuna yeyote wa wale mitume wengine aelewa Yesu amaanisha nini. Baadhi yao wawazia kwamba kwa kuwa Yuda ndiye mwenye sanduku la pesa, Yesu anamwambia: “Nunua vitu ambavyo twahitaji kwa ajili ya msherehekeo,” au kwamba apaswa kwenda na kuwapa maskini kitu fulani.
Baada ya Yuda kuondoka, Yesu aanzisha mwadhimisho mpya kabisa, au ukumbuko, pamoja na mitume wake waaminifu. Achukua mkate, asema sala ya shukrani, aumega, na kuwapa, akisema: “Chukueni, mle.” Aeleza hivi: “Huu wamaanisha mwili wangu ambao utatolewa kwa ajili yenu. Endeleeni kufanya hivi katika kunikumbuka mimi.”
Kila mmoja aishapo kula kutokana na mkate huo, Yesu achukua kikombe cha divai, ambacho kwa wazi ndicho kikombe cha nne chenye kutumiwa katika sherehe ya Sikukuu ya Kupitwa. Pia asema sala ya shukrani juu yacho, awapitishia, awaomba wanywe kutokana nacho, na kutaarifu hivi: “Kikombe hiki chamaanisha agano jipya kwa nguvu ya damu yangu, ambayo itamwagwa kwa ajili yenu.”
Kwa hiyo, kwa uhakika, huu ni ukumbusho wa kifo cha Yesu. Kila mwaka siku ya Nisani 14 wapasa kurudiwa, kama vile Yesu alivyosema, kwa ukumbusho wake. Utakumbusha waadhimishaji mambo ambayo Yesu na Baba yake wa kimbingu wamefanya kuandalia ainabinadamu mponyoko wa kutoka kwenye laana ya kifo. Kwa Wayahudi ambao huwa wafuasi wa Kristo, mwadhimisho huo utachukua mahali pa Sikukuu ya Kupitwa.
Agano jipya, ambalo hutendeshwa kazi na damu ya Yesu iliyomwagwa, huchukua mahali pa agano la kale la Sheria (Torati). Hilo hupatanishwa na Yesu Kristo kati ya vikundi viwili—kwa upande mmoja, Yehova Mungu, na kwa upande mwingine, Wakristo 144,000 waliozaliwa kwa roho. Zaidi ya kuandaa msamaha wa dhambi, agano hilo huruhusu kufanyizwa kwa taifa la kimbingu la wafalme-makuhani. Mathayo 26:21-29; Marko 14:18-25; Luka 22:19-23; Yohana 13:18-30; 17:12; 1 Wakorintho 5:7, NW.
▪ Yesu anukuu unabii gani wa Biblia kuhusu mwandamani fulani, naye aufanyia utumizi gani?
▪ Kwa nini mitume waingiwa na kihoro kingi, na kila mmoja wao auliza nini?
▪ Yesu amwambia Yuda afanye nini, lakini mitume wale wengine wafasirije maagizo hayo?
▪ Yesu aanzisha mwadhimisho gani baada ya Yuda kuondoka, nao una kusudi gani?
▪ Ni vikundi gani vilivyo katika agano jipya, na agano hilo latimiza nini?
-
-
Bishano LafokaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 115
Bishano Lafoka
MAPEMA kidogo jioni, Yesu alifundisha somo zuri la utumishi wa unyenyekevu kwa kuosha miguu ya mitume wake. Baadaye, alianzisha Ukumbusho wa kifo chake kinachokaribia. Sasa, hasa kwa sababu ya kile ambacho kimetendeka sasa hivi, tukio la kushangaza latukia. Mitume wake wahusika katika bishano kali juu ya ni yupi kati yao aonekana kuwa mkubwa kupita wote! Yaonekana kwamba hii ni sehemu ya ugomvi wenye kuendelea.
Kumbuka kwamba baada ya Yesu kugeuzwa sura mlimani, mitume walibishana juu ya nani miongoni mwao alikuwa mkubwa kupita wote. Zaidi ya hilo, Yakobo na Yohana waliomba vyeo vya umashuhuri katika Ufalme, hiyo ikitokeza ushindani zaidi miongoni mwa mitume. Sasa, katika usiku wake wa mwisho wa kuwa pamoja nao, ni lazima Yesu awe ahuzunika kama nini kuwaona wakizozana tena! Yeye afanya nini?
Badala ya kuwagombeza mitume kwa mwenendo wao, kwa mara nyingine tena Yesu asababu pamoja nao kwa subira: “Wafalme wa mataifa hupiga ubwana juu yao, na wale walio na mamlaka juu yao huitwa Wafadhili. Ingawa hivyo, nyinyi hamtakuwa hivyo. . . . Kwa maana ni yupi aliye mkubwa zaidi, yule anayeegemea kwenye meza au yule anayehudumia? Je! si yule anayeegemea kwenye meza?” Halafu, akiwakumbusha juu ya kielelezo chake, asema hivi: “Lakini mimi niko kati yenu kama yule anayehudumia.”
Wajapokuwa na hali zao za kutokamilika, mitume wameshikamana na Yesu wakati wa majaribu yake. Kwa hiyo yeye asema: “Mimi nafanya agano pamoja nanyi, kama vile Baba yangu amefanya agano pamoja na mimi, kwa ajili ya ufalme.” Agano hili la kibinafsi kati ya Yesu na wafuasi wake waaminifu-washikamanifu huwaunga wao kwake ili washiriki umiliki wake wa kifalme. Ni hesabu ndogo tu ya 144,000 ambao mwishowe hutiwa ndani ya agano hili kwa ajili ya Ufalme.
Ingawa mitume wametokezewa tazamio hili zuri sana la kushiriki pamoja na Kristo katika utawala wa Ufalme, kwa sasa wao ni dhaifu kiroho. “Nyinyi nyote mtajikwaa kuhusiana na mimi usiku huu,” Yesu asema. Hata hivyo, akimwambia Petro kwamba Yeye amesali kwa ajili yake, Yesu ahimiza hivi: “Mara ukiisha kurudi, waimarishe ndugu zako.”
“Watoto wadogo,” Yesu aeleza, “mimi niko pamoja nanyi kitambo kidogo zaidi. Nyinyi mtanitafuta mimi; na kama vile nilivyosema kwa Wayahudi, ‘Niendako nyinyi hamwezi kuja,’ nasema kwenu nyinyi pia kwa sasa. Mimi nawapa nyinyi amri mpya, kwamba mpendane; kama vile mimi nimewapenda nyinyi, ili kwamba nyinyi pia mpendane. Kwa hili wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwa nyinyi wenyewe.”
“Bwana, wewe unaenda wapi?” Petro auliza.
“Niendako huwezi wewe kunifuata sasa,” Yesu ajibu, “lakini utafuata baadaye.”
“Bwana, kwa nini mimi siwezi kukufuata wewe kwa sasa?” Petro ataka kujua. “Mimi nitaitoa nafsi yangu kwa ajili yako.”
“Je! wewe utaitoa nafsi yako kwa ajili yangu?” Yesu auliza. “Kwa kweli mimi nasema kwako wewe, Wewe leo, naam, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, hata wewe utanikana mimi mara tatu.”
“Hata ikinipasa mimi kufa pamoja na wewe,” Petro ateta, “kwa vyovyote mimi sitakukana.” Na ingawa mitume wale wengine wajiunga katika kusema hilo hilo, Petro ajisifu hivi: “Ingawa wengine wote wajikwae kuhusiana na wewe, mimi sitajikwaa kamwe!”
Akirejezea wakati ambao aliwatuma mitume nje kwenye safari ya kuhubiri Galilaya bila kibeti na kifuko cha chakula, Yesu auliza hivi: “Nyinyi hamkukosa kitu chochote, je! mlikosa?”
“La!” wao wajibu.
“Lakini sasa acheni yule mwenye kibeti akichukue, vivyo hivyo pia kifuko cha chakula,” yeye asema, “na acheni yule asiye na upanga auze vazi lake la nje anunue mmoja. Kwa maana mimi nasema kwenu nyinyi kwamba hili ambalo limeandikwa ni lazima litimizwe katika mimi, yaani, ‘Na yeye alihesabiwa pamoja na wasiofuata sheria.’ Kwa maana lile ambalo lanihusu mimi linatimizwa.”
Yesu anaelekeza kwenye wakati ambapo atatundikwa pamoja na watenda maovu, au wasiofuata sheria. Pia anaonyesha kwamba baada ya hapo wafuasi wake watakabili mnyanyaso mkali. “Bwana, tazama! panga mbili hizi,” wao wasema.
“Imetosha,” yeye ajibu. Kama tutakavyoona, kuwa kwao na panga hizo kutaruhusu Yesu karibuni afundishe somo jingine muhimu. Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Luka 22:24-38; Yohana 13:31-38; Ufunuo 14:1-3, NW.
▪ Kwa nini bishano la mitume linashangaza sana?
▪ Yesu ashughulikiaje bishano hilo?
▪ Ni nini kitimizwacho na agano ambalo Yesu afanya na wanafunzi wake?
▪ Yesu atoa amri gani mpya, nayo ni ya maana kadiri gani?
▪ Petro aonyesha uhakika gani wa kupita kiasi, na Yesu asema nini?
▪ Kwa nini maagizo ya Yesu juu ya kuchukua kibeti na kifuko cha chakula ni tofauti na yale aliyotoa mapema kidogo?
-
-
Kuwatayarisha Mitume kwa Ajili ya Kuondoka KwakeYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 116
Kuwatayarisha Mitume kwa Ajili ya Kuondoka Kwake
MLO wa ukumbusho umemalizika, lakini Yesu na mitume wake wangali katika chumba cha juu ghorofani. Ingawa hivi karibuni Yesu atakuwa hayupo, bado yeye ana mambo mengi ya kusema. “Msifadhaike mioyoni mwenu,” yeye awafariji. “Mnamwamini Mungu.” Lakini yeye aongeza: “Niaminini na mimi.”
“Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi,” Yesu aendelea kusema. “Naenda kuwaandalia mahali . . . ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.” Mitume hawafahamu kwamba Yesu aongea juu ya kwenda zake mbinguni, kwa hiyo Tomaso auliza: “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?”
“Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima,” Yesu ajibu. Ndiyo, kukubali na kuiga mwendo wake wa maisha ndiyo njia ya pekee tu ambayo kwayo yeyote aweza kuingia katika nyumba ya kimbingu ya Baba kwa sababu, kama vile Yesu asemavyo: “Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”
“Bwana, utuonyeshe Baba,” Filipo aomba, ‘na yatutosha.’ Yaonekana Filipo ataka Yesu aandae udhihirisho wenye kuonekana kuhusu Mungu, kama ule uliotolewa nyakati za kale katika njozi kwa Musa, Eliya, na Isaya. Lakini, kwa kweli, mitume wana kitu fulani kilicho bora sana kuliko njozi za namna hiyo, kama vile Yesu aoneleavyo: “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba [pia, NW].”
Yesu aonyesha utu wa Baba yake kwa ukamilifu sana hivi kwamba kuishi pamoja naye na kumchunguza ni kama kumwona Baba kikweli. Hata hivyo, Baba ni mkuu kuliko Mwana, kama vile Yesu akirivyo: “Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu.” Kwa kufaa Yesu ampa Baba yake wa kimbingu sifa yote kwa mafundisho yake.
Ni lazima iwe yawatia mitume moyo kama nini kumsikia Yesu sasa akiwaambia: “Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya”! Yesu hamaanishi kwamba wafuasi wake watatumia nguvu za kimuujiza zilizo kubwa kuliko zile ambazo yeye alitumia. Sivyo, bali amaanisha kwamba wataendesha huduma kwa muda mrefu zaidi, katika eneo kubwa zaidi, na kwa watu wengi zaidi.
Yesu hatawaacha wanafunzi wake baada ya kuondoka kwake. “Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu,” yeye aahidi, “nitalifanya.” Zaidi ya hilo, asema hivi: “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli [roho ya kweli, NW].” Baadaye, akiisha kupaa mbinguni, Yesu amimina juu ya wanafunzi wake ile roho takatifu, msaidiaji huyu mwingine.
Kuondoka kwa Yesu ku karibu, kama asemavyo: “Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena.” Yesu atakuwa kiumbe wa roho asiyeweza kuonwa na binadamu yeyote. Lakini Yesu awaahidi tena mitume wake waaminifu hivi: “Ninyi mnaniona [mtaniona, NW] . . . kwa sababu mimi ni hai [na] ninyi nanyi mtakuwa hai.” Ndiyo, si kwamba tu Yesu atawatokea kwa umbo la kibinadamu baada ya ufufuo wake bali pia atawafufua wakati uwadiapo ili wawe pamoja naye kwenye uhai mbinguni wakiwa viumbe wa roho.
Sasa Yesu ataarifu ile kanuni sahili: “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
Hapo mtume Yuda, yule aitwaye pia Thadayo, akatiza mazungumzo hivi: “Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu?”
“Mtu [yeyote, NW] akinipenda,” Yesu ajibu, “atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda . . . Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu.” Tofauti na wafuasi wake watiifu, ulimwengu hupuuza mafundisho ya Kristo. Kwa hiyo yeye hajifunui kwao.
Wakati wa huduma yake ya kidunia, Yesu amefundisha mitume wake mambo mengi. Watayakumbukaje yote, hasa kwa kuwa hata kufikia sasa washindwa kushika mengi sana? Kwa furaha Yesu aahidi hivi: “Huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu [roho takatifu, NW], ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”
Akiwafariji tena, Yesu asema hivi: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa . . . Msifadhaike mioyoni mwenu.” Kweli Yesu anaondoka, lakini aeleza hivi: “Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.”
Wakati wa Yesu unaobaki wa kuwa pamoja nao ni mfupi. “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena,” yeye asema, “kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.” Shetani Ibilisi, yeye aliyeweza kumwingia Yuda na kumwongoza, ndiye mtawala wa ulimwengu. Lakini katika Yesu hamna udhaifu wowote wenye dhambi ambao Shetani aweza kutumia ili amgeuze asitumikie Mungu.
Kuonea Shangwe Uhusiano wa Karibu
Kufuatia mlo wa ukumbusho, Yesu amekuwa akiwatia moyo mitume wake kwa hotuba isiyo rasmi ya kufunuliana yaliyomo moyoni. Yaweza kuwa ni baada ya katikati ya usiku. Kwa hiyo Yesu ahimiza hivi: “Ondokeni, twendeni zetu.” Hata hivyo, kabla hawajaondoka, Yesu, kwa kusukumwa na upendo wake kwa ajili yao, aendelea kunena, akiandaa kielezi chenye kuchochea.
“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima,” aanza. Mkulima Mkuu, Yehova Mungu, alipanda mzabibu huo wa mfano alipompaka mafuta Yesu kwa roho takatifu wakati wa ubatizo wake katika vuli ya 29 W.K. Lakini Yesu aendelea kuonyesha kwamba mzabibu huo wafananisha zaidi ya yeye tu, akionelea hivi: “Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. . . . Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi.”
Wakati wa Pentekoste, siku 51 baadaye, mitume na wengine wakawa matawi ya mzabibu huo wakati roho takatifu inapomiminwa juu yao. Hatimaye, watu 144,000 wakawa matawi ya mzabibu wa kitamathali. Pamoja na shina la mzabibu, Yesu Kristo, wao wajumlika kuwa mzabibu wa ufananisho ambao huzaa matunda ya Ufalme wa Mungu.
Yesu afafanua ufunguo wa kuzaa matunda: “Akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” Hata hivyo, ikiwa mtu ashindwa kuzaa matunda, Yesu asema, “hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.” Kwa upande mwingine, Yesu aahidi hivi: “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.”
Yesu azidi kusema kwa mitume wake: “Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.” Matunda anayotamani Mungu kutoka kwa matawi hayo ni udhihirisho wao wa sifa kama za Kristo, hasa upendo. Zaidi ya hayo, kwa kuwa Kristo alikuwa mpiga mbiu ya Ufalme wa Mungu, tunda lenye kutamanika latia ndani pia utendaji wao wa kufanya wanafunzi sawa na alivyofanya yeye.
“Kaeni katika pendo langu,” sasa Yesu awahimiza. Hata hivyo, mitume wake wawezaje kufanya hivyo? “Mkizishika amri zangu,” yeye asema, “mtakaa katika pendo langu.” Akiendelea, Yesu aeleza hivi: “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”
Baada ya saa chache, Yesu atadhihirisha upendo huu unaozidi kwa kuutoa uhai wake kwa ajili ya mitume wake, na pia kwa ajili ya wengine wote watakaozoea imani katika yeye. Kielelezo chake chapasa kusukuma wafuasi wake wawe na upendo uo huo wa kujidhabihu kwa ajili ya mmoja na mwenzake. Upendo huo utawatambulisha, kama alivyosema Yesu mapema kidogo: “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”
Akitambulisha rafiki zake, Yesu asema: “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.”
Huo ni uhusiano ulio na thamani kama nini kuwa nao—kuwa rafiki za karibu za Yesu! Lakini ili kuendelea kuonea shangwe uhusiano huo, wafuasi wake wapaswa kuendelea ‘kuzaa matunda.’ Wakifanya hivyo, Yesu asema, “lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu a[ta]wapeni.” Hakika, hiyo ni thawabu tukufu kwa ajili ya kuzaa matunda ya Ufalme! Baada ya kuwahimiza tena mitume wake ‘wapendane,’ Yesu aeleza kwamba ulimwengu utawachukia. Hata hivyo, yeye awafariji hivi: “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.” Kisha Yesu afunua ni kwa nini ulimwengu huchukia wafuasi wake, akisema hivi: “Kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.”
Akiendelea kufafanua sababu ya chuki ya ulimwengu, Yesu aendelea kusema hivi: “Haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye [Yehova Mungu] aliyenipeleka.” Kazi za kimuujiza za Yesu, kwa kweli, zawahukumu wale wanaomchukia yeye, kama asemavyo: “Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu na kutuchukia.” Kwa hiyo, kama asemavyo Yesu, andiko limetimizwa: “Walinichukia bure.”
Kama alivyofanya mapema kidogo, kwa mara nyingine tena Yesu awafariji kwa kuahidi kupeleka msaidizi, roho takatifu, ambayo ni kani ya utendaji ya Mungu yenye uwezo. “Yeye atanishuhudia [hiyo itatoa ushahidi juu yangu mimi, NW]. Nanyi pia mnashuhudia.”
Onyo Zaidi la Upole Wakati wa Kuachana
Yesu na mitume wake wamejiandaa kuondoka kwenye chumba cha juu. “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa [mkakwazwa, NW],” yeye aendelea. Halafu atoa onyo hili zito: “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.”
Kwa wazi mitume wafadhaishwa kwa kina kirefu na onyo hilo. Ingawa mapema kidogo Yesu alikuwa amesema kwamba ulimwengu ungewachukia, hakuwa amefunua moja kwa moja jinsi hiyo kwamba wangeuawa. “Sikuwaambia hayo tangu mwanzo,” Yesu aeleza, “kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.” Hata hivyo, ni vizuri kama nini kutangulia kuwatahadharisha kwa habari hiyo kabla hajaondoka!
“Lakini sasa,” Yesu aendelea kusema, “naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?” Mapema kidogo jioni hiyo, walikuwa wameuliza anaenda wapi, lakini sasa wameshtushwa sana na lile ambalo amewaambia hivi kwamba washindwa kuuliza zaidi juu ya jambo hilo. Kama asemavyo Yesu: “Kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.” Mitume wana kihoro si kwa sababu tu wamejifunza kwamba watapatwa na mnyanyaso mbaya sana na kuuawa bali pia kwa sababu Bwana wao anawaacha.
Hivyo basi Yesu aeleza hivi: “Yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” Akiwa binadamu, Yesu aweza kuwa mahali pamoja tu kwa wakati mmoja, lakini awapo mbinguni, aweza kupeleka msaidizi, roho takatifu ya Mungu, kwa wafuasi wake popote walipo duniani. Hivyo basi kuondoka kwa Yesu kutakuwa na manufaa.
Roho takatifu hiyo, Yesu asema, ‘itahakikishia ulimwengu habari ya dhambi, na haki, na hukumu.’ Dhambi ya ulimwengu, kushindwa kwao kujizoeza imani katika Mwana wa Mungu, itafichuliwa. Kwa kuongezea, ithibati yenye kusadikisha juu ya uadilifu wa Yesu itaonyeshwa kwa kupaa kwake kwenda kwa Baba. Na kushindwa kwa Shetani na ulimwengu wake mwovu kuvunja ukamilifu-maadili wa Yesu ni uthibitisho wenye kusadikisha kwamba mtawala wa ulimwengu amehukumiwa vikali.
“Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia,” Yesu aendelea kusema, “lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.” Kwa hiyo Yesu aahidi kwamba wakati amiminapo roho takatifu, ambayo ni kani ya utendaji ya Mungu, itawaongoza katika uelewevu wa mambo hayo kwa kulingana na uwezo wao wa kushika mambo.
Mitume washindwa hasa kuelewa kwamba Yesu atakufa halafu awatokee baada ya yeye kufufuliwa. Kwa hiyo wao waulizana hivi: “Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba?”
Yesu ang’amua kwamba wao wataka kumwuliza swali, kwa hiyo aeleza hivi: “Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.” Baadaye siku hiyo, wakati wa alasiri, Yesu anapouawa, viongozi wa kidini walimwengu washangilia, lakini wanafunzi wana kihoro. Hata hivyo, kihoro chao chabadilika kuwa shangwe, Yesu afufuliwapo! Na shangwe yao yaendelea awatiapo nguvu wakati wa Pentekoste ili wawe mashahidi wake kwa kumimina roho takatifu ya Mungu juu yao!
Akilinganisha hali ya mitume na ile ya mwanamke wakati wa maumivu ya kuzaa, Yesu asema: “Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika.” Lakini Yesu aonelea kwamba yeye hakumbuki tena dhiki yake mtoto wake akiisha kuzaliwa, naye awatia moyo mitume wake, akisema: “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena [nifufuliwapo]; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.”
Kufikia wakati huu, mitume hawajapata kamwe kuomba mambo kwa jina la Yesu. Lakini sasa yeye asema: “Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. . . . Kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba [nilitoka nikiwa mwakilishi wa Baba, NW]. Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.”
Maneno ya Yesu ni kitia-moyo kikubwa kwa mitume. “Kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu,” wao wasema. “Je! mnasadiki sasa?” Yesu auliza. “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mtu kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu.” Hata lionekane kuwa jambo lisilosadikika kama nini, latukia kabla ya usiku huo kwisha!
“Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu [kwa njia yangu mimi, NW].” Yesu amalizia: “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yesu aliushinda ulimwengu kwa kutimiza mapenzi ya Mungu kwa uaminifu japo kila jambo ambalo Shetani na ulimwengu wake walijaribu kufanya ili wavunje ukamilifu wa Yesu.
Sala ya Kumalizia Katika Chumba cha Juu
Kwa kusukumwa na upendo wa kina kirefu kwa mitume wake, Yesu amekuwa akiwatayarisha kwa ajili ya kuondoka kwake kuliko karibu. Sasa, baada ya kuwaonya kwa upole na kuwafariji kirefu, ainua macho yake mbinguni na kumwomba Baba yake dua kwa bidii hivi: “Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele.”
Lo, ni kichwa chenye kuchochea kama nini ambacho Yesu atanguliza—uzima wa milele! Akiisha kupewa “mamlaka juu ya wote wenye mwili,” Yesu aweza kuipa aina ya kibinadamu yote yenye kufa manufaa za dhabihu yake ya ukombozi. Hata hivyo yeye huwapa “uzima wa milele” wale tu ambao Baba awakubali. Akikuza kichwa hiki cha uzima wa milele, Yesu aendelea na sala yake hivi:
“Na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” Ndiyo, wokovu wategemea kutwaa kwetu maarifa juu ya wote wawili, Mungu na Mwana wake. Lakini mengi zaidi yahitajiwa kuliko maarifa ya kichwani tu.
Ni lazima mtu apate kuwajua kindani, akisitawisha urafiki wenye uelewano pamoja nao. Ni lazima mtu ahisi kama vile wao huhisi juu ya mambo na ayaone kupitia macho yao. Na juu ya yote, ni lazima mtu ajitahidi kuiga sifa zao zisizo na kifani katika kushughulika na wengine.
Halafu, Yesu asali hivi: “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.” Akiwa ametimiza mgawo wake hivyo kufikia hapo na kuwa mwenye uhakika juu ya mafanikio yake ya wakati ujao, aomba dua hivi: “Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.” Naam, sasa aomba kwamba kwa njia ya ufufuo aurudishwe kwenye utukufu wa kimbingu aliokuwa nao hapo kwanza.
Akitoa muhtasari wa kazi yake kuu duniani, Yesu asema hivi: “Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwewngu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika.” Yesu alitumia jina la Mungu, Yehova, katika huduma yake na akaonyesha tamko lalo sahihi, lakini alifanya mengi zaidi ya kudhihirisha jina la Mungu kwa mitume. Pia alipanua maarifa na uthamini wao juu ya Yehova, juu ya utu wake, na juu ya makusudi yake.
Akimpa Yehova sifa ya kuwa Mkuu kuliko yeye, Mmoja ambaye yeye hutumika chini yake, Yesu akiri kwa unyenyekevu hivi: “Maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”
Akipambanua kati ya wafuasi wake na na ile sehemu nyingine ya ainabinadamu, Yesu asali tena hivi: “Siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa . . . Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda . . . , nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu,” yaani, Yuda Iskariote. Wakati uo huo, Yuda yuko kwenye safari yake ya kudharaulika ili amsaliti Yesu. Hivyo, bila kujua Yuda anatimiza Maandiko.
“Ulimwengu umewachukia,” Yesu aendelea kusali. “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” Wafuasi wa Yesu wamo katika ulimwengu, jamii hii ya kibinadamu iliyopangwa kitengenezo yenye kutawalwa na Shetani, lakini wao wametengwa nao na ni lazima wabaki sikuzote wakiwa wametengwa nao na uovu wao.
“Uwatakase kwa ile kweli,” Yesu aendelea, “neno lako ndiyo kweli.” Hapa Yesu ayaita “kweli” Maandiko ya Kiebrania, ambayo kwa kuendelea yeye aliyanukuu. Lakini yale aliyowafundisha wanafunzi wake na yale waliyoyaandika baadaye chini ya uvuvio yakiwa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ni “kweli” vilevile. Ukweli huu waweza kutakasa mtu, ubadili maisha yake kabisa, na kumfanya mtu kuwa aliyetengwa na ulimwengu.
Sasa Yesu ‘haombei hao tu; lakini na wale watakaomwamini kwa sababu ya neno lao.’ Kwa hiyo Yesu asali kwa ajili ya wale watakaokuwa wafuasi wake wapakwa-mafuta na wanafunzi wengine wa wakati ujao ambao bado watakusanywa ndani ya “kundi moja.” Yeye aomba nini kwa ajili ya wote hao?
“Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu [ulivyo katika mwungano pamoja nami, NW], nami ndani yako . . . ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja [mmoja, NW].” Yesu na Baba yake si mtu mmoja kihalisi, bali wana mwafaka juu ya mambo yote. Yesu asali kwamba wafuasi wake wapate shangwe ya umoja uo huo ili “ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.”
Kwa ajili ya wale ambao wangekuwa wafuasi wake wapakwa-mafuta, sasa Yesu afanya ombi kwa Baba yake. Ombi la nini? Kwamba “wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi [wa] ulimwengu,” yaani, kabla Adamu na Hawa hawajatunga mimba ya uzao wao. Muda mrefu kabla ya hapo, Mungu alimpenda Mwana wake mzaliwa-pekee, aliyepata kuwa Yesu Kristo.
Akimalizia sala yake, Yesu akazia tena hivi: “Naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; [ili] pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao [katika mwungano pamoja nao, NW].” Kwa mitume, kujifunza jina la Mungu kumetia ndani kupata kuujua kibinafsi upendo wa Mungu. Yohana 14:1–17:26; 13:27, 35, 36; 10:16; Luka 22:3, 4; Kutoka 24:10; 1 Wafalme 19:9-13; Isaya 6:1-5; Wagalatia 6:16; Zaburi 35:19; 69:4; Mithali 8:22, 30.
▪ Yesu aenda wapi, na Tomaso apokea jibu gani kuhusu njia ya kwenda huko?
▪ Kwa ombi lake, yaonekana Filipo ataka Yesu aandae nini?
▪ Kwa nini mtu ambaye amemwona Yesu amemwona Baba pia?
▪ Ni jinsi gani wafuasi wa Yesu hufanya kazi kubwa kuliko zile alizofanya yeye?
▪ Ni katika maana gani Shetani hana kitu kwa Yesu?
▪ Yehova alipanda lini mzabibu wa ufananisho, na wengine wanakuwa sehemu ya mzabibu huo lini na jinsi gani?
▪ Hatimaye, mzabibu wa ufananisho wawa na matawi mangapi?
▪ Mungu atamani matunda gani kutoka kwa matawi hayo?
▪ Twawezaje kuwa rafiki za Yesu?
▪ Ni kwa nini ulimwengu wachukia wafuasi wa Yesu?
▪ Ni onyo gani la Yesu ambalo lafadhaisha mitume wake?
▪ Kwa nini mitume washindwa kumwuliza Yesu swali juu ya anakoenda?
▪ Ni jambo gani hasa ambalo mitume washindwa kuelewa?
▪ Yesu atoaje kielezi cha kwamba hali ya mitume itabadilika iache kuwa ya kihoro iwe ya shangwe?
▪ Yesu asema mitume watafanya nini hivi karibuni?
▪ Yesu ashindaje ulimwengu?
▪ Ni katika maana gani Yesu amepewa “mamlaka juu ya wote wenye mwili”?
▪ Yamaanisha nini kutwaa maarifa juu ya Mungu na Mwana wake?
▪ Ni katika njia zipi Yesu afanya jina la Mungu lidhihirike?
▪ “Kweli” ni nini, nayo ‘yatakasaje’ Mkristo?
▪ Ni jinsi gani Mungu, Mwana wake, na waabudu wote wa kweli walivyo mmoja?
▪ “Kuwekwa msingi [wa] ulimwengu” kulikuwa wakati gani?
-
-
Uguo Kali Katika BustaniYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 117
Uguo Kali Katika Bustani
YESU amalizapo kusali, yeye na mitume wake waaminifu 11 wamwimbia Yehova nyimbo za sifa. Halafu washuka kutoka chumba cha juu, na kuingia ndani ya giza la usiku lenye baridi, na kusonga mbele warudi ng’ambo ya Bonde la Kidroni kuelekea Bethania. Lakini wakiwa njiani, wasimama mahali wapapendapo sana, bustani ya Gethsemane. Iko juu ya au katika ujirani wa Mlima wa Mizeituni. Mara nyingi Yesu amekutana na mitume wake hapa katikati ya mizeituni.
Akiacha wanane wa mitume—labda karibu na mwingilio wa bustani—yeye awaagiza hivi: “Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.” Halafu awachukua wale wengine watatu—Petro, Yakobo, na Yohana—na kusonga mbali zaidi katika bustani. Yesu aingiwa na kihoro na kufadhaika sana. “Roho [nafsi, NW] yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa,” awaambia. “Kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”
Akisonga mbele kidogo, Yesu ajibwaga chini kifudifudi na kuanza kusali hivi kwa moyo wa bidii: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.” Amaanisha nini? Kwa nini ‘ana huzuni nyingi kiasi cha kufa’? Je! anaepa uamuzi wake wa kufa na kuandaa ukombozi?
Sivyo hata kidogo! Yesu hasihi kwamba aepushwe na kifo. Hata ile fikira ya kuepuka kifo cha dhabihu, iliyodokezwa na Petro wakati mmoja, yamchukiza sana. Bali, yeye ana uguo kali kwa sababu ahofu kwamba njia ambayo karibuni atakufa kwayo—akiwa mhalifu mwenye kudharaulika—italeta suto juu ya jina la Baba yake. Sasa yeye ahisi kwamba katika muda wa saa chache atatundikwa juu ya mti kama mtu wa aina mbaya kabisa—mkufuru dhidi ya Mungu! Hilo ndilo lamfadhaisha sana.
Baada ya kusali kirefu, Yesu arudi na kukuta wale mitume watatu wamelala. Akielekeza maneno kwa Petro, yeye asema hivi: “Je! hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni.” Hata hivyo, akikiri kwamba wamekuwa chini ya mkazo na kwamba usiku umendelea sana, asema hivi: “Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
Ndipo Yesu aenda zake mara ya pili na kuomba kwamba Mungu amwondolee “kikombe hiki,” yaani, kisehemu au mapenzi aliyogawiwa na Yehova. Arudipo, akuta tena wale watatu wamelala wakati ambapo wangalipaswa kuwa wakisali ili wasiingie katika kishawishi. Yesu asemapo nao, hawajui la kumjibu.
Mwishowe, mara ya tatu, Yesu aenda umbali kama ule unaoweza kutupa jiwe, na akiwa amepiga magoti na kwa vilio vikali na machozi, asali hivi: “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki.” Yesu ahisi maumivu makali kwa sababu ya suto ambalo kifo chake kama mhalifu kitaleta juu ya jina la Baba yake. Kwani, kushtakiwa kuwa mkufuru—mtu alaaniye Mungu—ni jambo linalokaribia sana kutoweza kuvumilika!
Hata hivyo, Yesu aendelea kusali hivi: “Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” Kwa utiifu Yesu atiisha mapenzi yake kwa yale ya Mungu. Iwapo hivyo, malaika kutoka mbinguni atokea na kumwimarisha kwa maneno ya kutia moyo. Yaelekea, malaika amwambia Yesu kwamba yeye ana tabasamu ya kibali cha Baba yake.
Hata hivyo, mabega ya Yesu yalemewa na uzito ulioje! Uhai wa milele wake mwenyewe na wa jamii nzima ya kibinadamu umo katika hatari ya kuponyoka. Mkazo wa kihisia-moyo ni mwingi mno. Hivyo basi Yesu aendelea kusali kwa moyo wa bidii zaidi, na jasho lake lawa kama matone ya damu liangukapo chini. “Ingawa hii ni ajabu itukiayo mara chache sana,” lasema The Journal of the American Medical Association, “jasho lenye damu . . . laweza kutukia katika hali zenye hisia-moyo nyingi.”
Baadaye, Yesu awarudia mitume wake mara ya tatu, na tena awakuta wamelala. Wamenyong’onyea kwa kuwa na kihoro kibisa. “Laleni sasa, mpumzike [wakati wa jinsi hii nyinyi mnalala na kupata pumziko lenu, NW]!” yeye apaaza mshangao. “Yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu [wa binadamu, NW] anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.”
Huku akiwa angali katika kusema, Yuda Iskariote akaribia, ameandamwa na umati mkubwa uliochukua mienge na taa na silaha. Mathayo 26:30, 36-47; 16:21-23; Marko 14:26, 32-43; Luka 22:39-47; Yohana 18:1-3; Waebrania 5:7.
▪ Baada ya kuondoka kwenye chumba cha juu, Yesu awaongoza mitume wapi, naye afanya nini huko?
▪ Huku Yesu akiwa katika kusali, mitume wanafanya nini?
▪ Kwa nini Yesu ana uguo kali, naye amwomba Mungu nini?
▪ Ni nini chaonyeshwa na kuwa kwa jasho la Yesu kama matone ya damu?
-
-
Kusalitiwa na KukamatwaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 118
Kusalitiwa na Kukamatwa
UMEPITA sana katikati ya usiku wakati Yuda aongozapo umati mkubwa wa askari, wakuu wa makuhani, Mafarisayo, na wengine kuingia katika bustani ya Gethsemane. Makuhani wameafikiana na Yuda kumlipa vipande 30 vya fedha ili amsaliti Yesu.
Mapema kidogo, Yuda alipoagizwa aondoke kwenye mlo wa Sikukuu ya Kupitwa, kwa wazi aliwaendea moja kwa moja wakuu wa makuhani. Nao wakawakusanya maofisa wao wenyewe mara hiyo, na pia kikosi cha askari. Labda kwanza Yuda aliwaongoza mahali Yesu na mitume walikuwa wameadhimisha Sikukuu ya Kupitwa. Kwa kugundua kwamba walikuwa wameondoka, ule umati mkubwa wenye kubeba silaha na kuchukua taa na mienge ulimfuata Yuda kutoka Yerusalemu na kwenda ng’ambo ya Bonde la Kidroni.
Yuda aongozapo msafara huo kuupanda Mlima wa Mizeituni, ahisi akiwa na uhakika kwamba ajua mahali pa kumpata Yesu. Wakati wa juma lililopita, Yesu na mitume walipokuwa wakisafiri huku na huku kati ya Bethania na Yerusalemu, walisimama mara nyingi katika bustani ya Gethsemane kupumzika na kuongea. Lakini, sasa, kukiwa na uwezekano wa kwamba Yesu amefichika gizani chinichini ya ile mizeituni, askari watamtambuaje? Huenda ikawa walikuwa hawajapata kumwona kamwe. Hivyo Yuda aandaa ishara, akisema: “Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.”
Yuda aongoza ule umati mkubwa kuingia bustanini, amwona Yesu pamoja na mitume wake, na kumwendea moja kwa moja. “Salamu [Siku njema, NW] Rabi,” asema na kumbusu kwa wororo sana.
“Rafiki, fanya ulilolijia [Jamaa, wewe upo hapa kwa kusudi gani?, NW] Yesu ajibu vikali. Ndipo, akijibu swali lake mwenyewe, asema hivi: “Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu [wa binadamu, NW] kwa kumbusu?” Lakini hataki mengi zaidi na msaliti wake! Yesu apiga hatua mbele kuingia katika ile nuru ya mienge na taa zinazowaka na kuuliza hivi: “Ni nani mnayemtafuta?”
“Ni Yesu Mnazareti,” jibu laja.
“Ni mimi,” Yesu ajibu, huku akisimama kwa moyo mkuu mbele yao wote. Kwa kugutushwa na ujasiri wake na bila kujua watarajie nini, wanaume hao warudi nyuma na kuanguka chini.
“Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi,” Yesu aendelea kwa utulivu. “Basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” Kitambo kifupi kabla ya hapo akiwa katika kile chumba cha juu, Yesu alikuwa amemwambia Baba yake katika sala kwamba alikuwa amewatunza mitume wake waaminifu na hakuna hata mmoja wao aliyekuwa amepotezwa “ila yule mwana wa upotevu [uharibifu, NW].” Hivyo basi, ili neno lake liweze kutimizwa, yeye aomba kwamba wafuasi wake waachwe waende zao.
Askari wanaporudiwa na umakini wao, wasimama, na kuanza kumfunga Yesu, mitume watambua likaribialo kutendeka. “Bwana, tuwapige kwa upanga?” wao wauliza. Kabla Yesu hajajibu, Petro, akitumia mmoja wa panga mbili ambazo mitume wameleta, amshambulia Malko, mtumwa wa kuhani wa juu. Pigo la Petro lakikosa kichwa cha mtumwa huyo lakini akata sikio lake la kulia.
“Mwe radhi kwa hili [acheni ifike hapo, NW],” Yesu asema akiingilia. Kwa kugusa sikio hilo, aponya lile jeraha. Halafu afundisha somo la maana, akimwamuru Petro hivi: “Rudisha upanga wako mahali pake; maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?”
Yesu ana nia ya kukamatwa, kwa maana aeleza hivi: “Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?” Na aongeza hivi: “Je! kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” Yeye aafikiana kabisa na mapenzi ya Mungu kwake!
Halafu Yesu aelekeza maneno yake kwenye ule umati. “Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika?” auliza. “Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe.”
Hapo kile kikosi cha askari na yule amiri wa kijeshi na wale maofisa wa Wayahudi wamkamata Yesu na kumfunga. Kuona hilo, mitume wamwacha Yesu na kukimbia. Hata hivyo, mwanamume kijana—yaelekea ni mwanafunzi Marko—abaki miongoni mwa umati. Huenda akawa alikuwa kwenye makao ambapo Yesu aliadhimisha Sikukuu ya Kupitwa na baadaye akaufuata umati kutoka huko. Hata hivyo, sasa yeye atambuliwa, na jaribio la kumkamata lafanywa. Lakini yeye aacha nyuma vazi lake la kitani na kutoroka. Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-52; Luka 22:47-53; Yohana 17:12; 18:3-12.
▪ Kwa nini Yuda ahisi akiwa na uhakika kwamba atampata Yesu katika bustani ya Gethsemane?
▪ Yesu adhihirishaje hangaiko kwa ajili ya mitume wake?
▪ Petro afanya kitendo gani kumkinga Yesu, lakini Yesu asema nini kwa Petro kukihusu?
▪ Yesu afunuaje kwamba yeye aafikiana kabisa na mapenzi ya Mungu kwake?
▪ Mitume wamwachapo Yesu, nani abaki, naye apatwa na nini?
-
-
Apelekwa kwa Anasi, Kisha kwa KayafaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 119
Apelekwa kwa Anasi, Kisha kwa Kayafa
YESU, akiwa amefungwa kama mhalifu wa kawaida, aongozwa kwenda kwa Anasi, ambaye hapo kwanza alikuwa kuhani mkuu aliye mashuhuri. Anasi alikuwa kuhani mkuu wakati Yesu akiwa kivulana wa miaka 12 aliwastaajabisha walimu wa kirabi hekaluni. Wana kadhaa wa Anasi walitumikia baadaye wakiwa makuhani wakuu, na wakati uliopo Kayafa mwana-mkwe wake ashikilia cheo hicho.
Labda kwanza Yesu aongozwa kwenda nyumbani kwa Anasi kwa sababu ya umashuhuri wa muda mrefu wa huyo aliye mkuu wa makuhani katika maisha ya kidini ya Kiyahudi. Kituo hiki cha kumwona Anasi chamruhusu wakati Kayafa Kuhani Mkuu kuikusanya Sanhedrini, ile mahakama kuu ya Kiyahudi yenye washiriki 71, na pia kukusanya mashahidi bandia.
Sasa Anasi kuhani mkuu amuuliza Yesu maswali juu ya wanafunzi wake na juu ya fundisho lake. Hata hivyo, Yesu asema hivi kwa kujibu: “Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.”
Hapo, mmoja wa maofisa waliosimama karibu na Yesu ampiga kofi usoni, akisema: “Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?”
“Kama nimesema vibaya,” Yesu ajibu, “ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?” Baada ya kujibiana maneno hayo, Anasi apeleka Yesu kwa Kayafa akiwa amefungwa.
Kufikia sasa makuhani wote wakuu na wanaume wazee na waandishi, ndiyo, Sanhedrini yote, inaanza kukusanyika. Kwa wazi mahali pao pa mkutano ni kao la Kayafa. Hata hivyo, kufanya kesi kama hiyo katika usiku wa Sikukuu ya Kupitwa kwa wazi ni jambo lililo dhidi ya sheria ya Kiyahudi. Lakini hilo halizuii viongozi wa kidini kutofanya kusudi lao ovu.
Tayari, majuma kadhaa kabla ya hapo wakati Yesu alipomfufua Lazaro, Sanhedrini ilikuwa imeamua miongoni mwao wenyewe kwamba ni lazima afe. Na siku mbili tu mapema kidogo, siku ya Jumatano, wenye mamlaka wa kidini walifanya shauri pamoja kumkamata Yesu kwa mbinu ya ujanja ili wamuue. Wazia, yeye kwa kweli alikuwa amehukumiwa adhabu kabla ya kufanyiwa kesi!
Sasa jitihada zaendelea kutafuta mashahidi watakaotoa uthibitisho bandia ili kesi ikuzwe dhidi ya Yesu. Hata hivyo, hakuwezi kupatikana mashahidi wenye kuafikiana katika ushuhuda wao. Hatimaye, wawili waja mbele na kushikilia hivi: “Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.”
“Hujibu neno?” Kayafa auliza. “Hawa wanakushuhudia nini?” Lakini Yesu abaki kimya. Hata katika shtaka hili bandia, kwa aibu ya Sanhedrini, mashahidi hao hawawezi kufanya hadithi zao ziafikiane. Hivyo basi kuhani mkuu ajaribu mbinu tofauti.
Kayafa ajua jinsi Wayahudi walivyo wepesi kukasirikia mtu yeyote anayedai kuwa ndiye Mwana halisi wa Mungu. Katika pindi mbili mapema kidogo, wao walikuwa wamefanya haraka-haraka kumbandika Yesu jina la kuwa mkufuru astahiliye kifo, mara moja wakikosea kwa kuwazia kwamba alikuwa akidai kwamba yuko sawa na Mungu. Sasa Kayafa adai kwa ujanja hivi: “Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”
Bila kujali ni nini Wayahudi wafikiri, kwa kweli Yesu ndiye Mwana wa Mungu. Na kubaki kimya kungeweza kueweleka kwamaanisha kwamba anakana kuwa ndiye Kristo. Hivyo basi Yesu ajibu kwa ujasiri hivi: “Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.”
Hapo, Kayafa, akijionyesha kwa njia ya kutazamisha, ararua mavazi yake na kupaaza sauti: “Amekufuru; tuna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; mwaonaje ninyi?”
“Imempasa kuuawa,” Sanhedrini yapiga mbiu. Halafu waanza kumfanyia mzaha, nao wasema mambo mengine ya kufuru dhidi yake. Wampiga kofi katika uso wake na kuutemea mate. Wengine wafunika uso wake wote na kumpiga kwa ngumi zao na kusema hivi kimadharau: “Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?” Mwenendo huu wa kutukana, usio wa kisheria watukia wakati wa ile kesi ya usiku. Mathayo 26:57-68; 26:3, 4; Marko 14:53-65; Luka 22:54, 63-65; Yohana 18:13-24; 11:45-53; 10:31-39; 5: 16-18.
▪ Yesu aongozwa wapi kwanza, na ni nini lampata huko?
▪ Kisha Yesu apelekwa wapi, na kwa kusudi gani?
▪ Kayafa amewezaje kuifanya Sanhedrini ipige mbiu kwamba Yesu astahili kifo?
▪ Ni mwenendo gani wa kutukana, ulio kinyume cha sheria watukia wakati wa ile kesi?
-
-
Akanwa Katika UaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 120
Akanwa Katika Ua
BAADA ya kumwacha Yesu katika bustani ya Gethsemane na kukimbia kwa hofu pamoja na mitume wale wengine, Petro na Yohana wasimama katika kimbio lao. Labda wao wamfikia Yesu apelekwapo kwenye makao ya Anasi. Anasi aagizapo apelekwe kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, Petro na Yohana wafuata wakiwa umbali wa kutosha, yaonekana wakiwa wametatizika kati ya kuhofia uhai wao wenyewe na hangaiko lao la kina kirefu juu ya yatakayopata Bwana-Mkubwa wao.
Awasilipo kwenye makao ya Kayafa yenye nafasi kubwa, Yohana aweza kuingia katika ua, kwa kuwa yeye ajulikana na kuhani mkuu. Hata hivyo, Petro aachwa akisimama nje ya mlango. Lakini muda si muda Yohana arudi na kusema na bawabu, aliye kijakazi, na Petro aruhusiwa kuingia.
Kufikia sasa kuna baridi, na watumishi wa nyumba na maofisa wa kuhani mkuu wamewasha moto wa makaa. Petro ajiunga nao ili apate joto huku akingojea matokeo ya kesi ya Yesu. Huko, katika nuru ya ule moto mwangavu, bawabu aliyekuwa ameruhusu Petro aingie amtazama vizuri zaidi. “Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya”! apaaza sauti.
Akiudhika kwa kutambulishwa, Petro akana mbele yao wote kwamba hajapata kumjua Yesu. “Sijui wala sisikii unayoyasema wewe,” yeye asema.
Hapo basi, Petro aenda nje karibu na njia ya lango. Hapo, msichana mwingine amwona naye pia awaambia wale waliosimama karibu: “Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti.” Kwa mara nyingine, Petro akana, akiapa hivi: “Simjui mtu huyu”!
Petro abaki katika ua, akijaribu kutoonekana wazi kwa kadiri iwezekanavyo. Labda hapo agutushwa na kuwika kwa jogoo katika giza la asubuhi na mapema. Kwa sasa, kesi ya Yesu yaendelea, yaonekana ikiendeshwa katika sehemu ya nyumba iliyo juu ya ua. Labda Petro na wengine wanaongojea chini waona mashahidi mbalimbali wakija na kwenda ambao waletwa ndani ili kushuhudia.
Karibu saa moja imepita tangu Petro alipotambulishwa mara ya mwisho kuwa mshirika wa Yesu. Sasa watu kadhaa kati ya wale wenye kusimama hapo wamjia na kusema: “Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako [lahaja yako, NW] wakutambulisha.” Mmoja wa kikundi hicho ni mtu wa ukoo wa Malko, ambaye Petro alikuwa amekata sikio lake. “Je! mimi si[ni]mekuona wewe bustanini pamoja naye?” asema.
“Simjui mtu huyu”! Petro ashikilia sana kauli. Kwa hakika, ajaribu kuwasadikisha kwamba wote wanakosea kwa kulaani na kuapa juu ya jambo hilo, maana yake, kujilaani mwenyewe ikiwa hasemi ukweli.
Mara Petro akanapo mara hii ya tatu, jogoo awika. Na wakati huo, Yesu, ambaye kwa wazi ametoka nje akaja kwenye roshani juu ya ua, ageuka na kumtazama. Mara hiyo, Petro akumbuka aliyosema Yesu saa chache tu mapema kidogo katika chumba cha juu: “Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.” Kwa kulemewa sana na uzito wa dhambi yake, Petro aenda nje na kulia machozi kwa uchungu.
Hilo lingewezaje kutukia? Baada ya kuwa na uhakika sana juu ya imara yake ya kiroho, ikawaje kwamba Petro aweze kukana Bwana-Mkubwa wake mara tatu kwa mfululizo wenye kufuatana haraka-haraka? Bila shaka hali zamnasa Petro bila kutarajia. Ukweli unapotoshwa, na Yesu anaonyeshwa kuwa mhalifu mwovu. Lililo sawa lafanywa lionekane kuwa kosa, asiye na hatia kuwa mwenye hatia. Hivyo basi kwa sababu ya mikazo ya ile pindi, Petro akosa usawaziko. Ghafula hisia yake ifaayo ya uaminifu-mshikamanifu yavurugika. Kuhofu binadamu kwamshika hata kumletea majonzi. Jambo hilo na lisitupate sisi kamwe! Mathayo 26:57, 58, 69-75; Marko 14:30, 53, 54, 66-72; Luka 22:54-62; Yohana 18:15-18, 25-27.
▪ Petro na Yohana wapataje kuingia katika ua wa kuhani mkuu?
▪ Petro na Yohana wakiwa wangali katika ua, ni nini kinachoendelea katika nyumba?
▪ Jogoo awika mara ngapi, na Petro akana mara ngapi kwamba hamjui Kristo?
▪ Yamaanisha nini kwamba Petro alaani na kuapa?
▪ Ni nini chasababisha Petro akane kwamba hamjui Yesu?
-
-
Mbele ya Sanhedrini, Kisha kwa PilatoYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 121
Mbele ya Sanhedrini, Kisha kwa Pilato
USIKU unakaribia mwisho. Petro amekana Yesu kwa mara ya tatu, na washiriki wa Sanhedrini wamemaliza kesi yao ya bandia na wametawanyika. Hata hivyo, wanakutana tena asubuhi ya Ijumaa mara tu kunapopambazuka, wakati huu wakiwa kwenye jumba la Sanhedrini yao. Inaelekea kusudi lao ni kufanya ionekane eti kesi yao ya usiku ilifuata uhalali wa sheria. Yesu anapoletwa mbele yao, wanasema hivi, kama vile walivyofanya usiku: “Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie.”
“Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa,” Yesu anajibu. “Tena, nikiwauliza, hamtajibu.” Hata hivyo, kwa moyo mkuu Yesu anaelekeza kwenye utambulishi wake, akisema: “Tangu sasa Mwana wa Adamu [Mwana wa binadamu, NW] atakuwa ameketi [akiketi, NW] upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi.”
“Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu?” wote wataka kujua.
“Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye,” Yesu ajibu.
Kwa wanaume hawa ambao wameazimia kuua, jibu hili linatosha. Wanaliona kuwa kufuru. “Tuna haja gani tena ya ushuhuda?” wanauliza. “Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake.” Hivyo basi wanamfunga Yesu, wanamwongoza kutoka hapo, na kumpa kwa gavana Mroma Pontio Pilato.
Yudasi, msaliti wa Yesu, amekuwa akitazama hatua za mambo hayo. Anapoona kwamba Yesu amelaaniwa vikali, ahisi majuto. Hivyo yeye aendea makuhani wakuu na wanaume wazee kurudisha vile vipande 30 vya fedha, akieleza hivi: “Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.”
“Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe”! wajibu bila moyo wa huruma. Hivyo basi Yuda atupa vile vipande vya fedha hekaluni na kwenda zake na kujaribu kujinyonga. Hata hivyo, inaonekana kwamba tawi ambalo Yuda afungilia kamba linakatika, na mwili wake waporomoka kwenye miamba iliyoko chini, ambako wapasuka-pasuka.
Makuhani wakuu hawana hakika wafanye nini na vile vipande vya fedha. “Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka,” wakata shauri, “kwa kuwa ni kima cha damu.” Hivyo basi, baada ya kushauriana, kwa pesa hizo wanunua shamba la mfinyanzi ili kuzika wageni. Hivyo shamba hilo laja kuitwa “konde la damu.”
Bado ni mapema asubuhi wakati Yesu anapopelekwa kwenye jumba la gavana. Lakini Wayahudi ambao wameandamana naye wakataa kuingia kwa sababu wanaamini kwamba huo uhusiano wa kindani pamoja na Wasio Wayahudi utawatia unajisi. Hivyo basi ili ajipatanishe na maoni yao, Pilato aja nje. “Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?” auliza.
“Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako,” wajibu.
Akitaka kuepuka kuhusika, Pilato ajibu hivi: “Haya! mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!”
Wakifunua azimio lao la uuaji, Wayahudi wadai hivi: “Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.” Kwa kweli, kama wangeua Yesu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa, inaelekea ingeleta msukosuko wa watu wote, kwa kuwa wengi wamheshimu Yesu sana. Lakini wakiweza kufanya Waroma wamuue kwa shtaka la kisiasa, hiyo itaelekea kuwaondolea daraka mbele ya watu.
Hivyo basi viongozi wa kidini, bila kutaja kesi yao ya mapema ambamo walilaani Yesu vikali juu ya kukufuru, sasa watunga mashtaka tofauti. Wafanyiza lile shtaka lenye sehemu tatu: “Tumemwona huyu [1] akipotosha taifa letu, na [2] kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, [3] akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.”
Lile shtaka la kwamba Yesu adai kuwa mfalme ndilo lahangaisha Pilato. Kwa hiyo, yeye aingia tena katika jumba, aita Yesu aende alipo, na kuuliza: “Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Ndiyo kusema, je! umevunja sheria kwa kujijulisha wazi kuwa mfalme kwa kupinga Kaisari?
Yesu ataka kujua ni mengi kadiri gani ambayo tayari Pilato amesikia juu yake, hivyo basi auliza hivi: “Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?”
Pilato adai hana maarifa yoyote juu yake na ana tamaa ya kujua mambo hakika. “Ama! Ni Myahudi mimi!” ajibu. “Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?”
Yesu hajaribu kwa njia yoyote kuepa suala hilo, ambalo ni la kuwa na ufalme. Jibu ambalo Yesu anatoa sasa bila shaka lashangaza Pilato. Luka 22:66–23:3; Mathayo 27:1-11; Marko 15:1; Yohana 18:28-35; Matendo 1:16-20.
▪ Sanhedrini yakutana tena asubuhi kwa kusudi gani?
▪ Yuda afaje, na ni jambo gani lafanywa na vile vipande 30 vya fedha?
▪ Badala ya Wayahudi wamuue Yesu wao wenyewe, kwa nini wataka Waroma wamuue Yesu?
▪ Ni mashtaka gani ambayo Wayahudi wafanyia Yesu?
-
-
Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi TenaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 122
Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi Tena
INGAWA Yesu hafanyi jaribio lolote la kumficha Pilato kwamba yeye ni mfalme, aeleza kwamba Ufalme wake si tisho kwa Roma. “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu,” Yesu asema. “Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Hivyo Yesu akiri mara tatu kwamba yeye ana Ufalme, ingawa si wa chanzo cha kidunia.
Hata hivyo, Pilato amkaza zaidi: “Wewe u mfalme basi?” Yaani, wewe ni mfalme hata ingawa Ufalme wako si sehemu ya ulimwengu huu?
Yesu amjulisha Pilato kwamba amekata shauri vizuri, akijibu: “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.”
Ndiyo, kusudi hasa la Yesu kuwako duniani ni kuitolea “kweli” ushahidi, hasa ile kweli juu ya Ufalme wake. Yesu yuko tayari kuwa mwaminifu kwa kweli hiyo hata ikiwa itamgharimu uhai wake. Ingawa Pilato auliza: “Kweli ni nini?” hangojei maelezo zaidi. Amesikia ya kutosha ili atoe hukumu.
Pilato arudia umati unaongoja nje ya jumba lile. Kwa wazi Yesu akiwa kando yake, awaambia makuhani wakuu na wale walio pamoja nao: “Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.”
Kwa kukasirishwa na uamuzi huo, umati unaanza kusisitiza hivi: “[Yeye] huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi wote, tokea Galilaya mpaka huku.”
Ni lazima ushupavu huo usiotumia akili kufikiri wa Wayahudi uwe unashangaza Pilato. Hivyo basi, makuhani wakuu na wanaume wazee wanapoendelea kupaaza sauti, Pilato ageukia Yesu na kuuliza: “Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?” Bado, Yesu hafanyi jaribio la kujibu. Utulivu wake katika kukabiliana na yale mashtaka yasiyo na msingi wowote wafanya Pilato kustaajabu.
Anapojua kwamba Yesu ni Mgalilaya, Pilato aona njia ya kujiondoa asiwe na daraka juu yake. Mtawala wa Galilaya, Herode Antipa (mwana wa Herode Mkuu), yumo Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa, hivyo basi Pilato ampeleka Yesu kwake. Mapema kidogo, Herode Antipa alikuwa ameagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa, halafu Herode akaogopa aliposikia juu ya kazi za kimuujiza ambazo Yesu alikuwa akifanya, akihofu kwamba huenda ikawa kwa kweli Yesu ni Yohana ambaye ameinuliwa kutoka kwa wafu.
Sasa, Herode ana shangwe mno kwa tazamio la kumwona Yesu. Hii si kwa sababu ahangaikia hali njema ya Yesu au kwamba ataka kufanya jaribio lolote halisi juu ya kama mashtaka anayofanyiwa ni ya kweli au sivyo. Bali, yeye ni mdadisi tu na atumainia kuona Yesu akifanya muujiza fulani.
Hata hivyo, Yesu akataa kutosheleza udadisi wa Herode. Kwa uhakika, Herode anapokuwa akimuuliza maswali, yeye hasemi neno. Kwa kukata tamaa, Herode na askari-walinzi wake wamdhihaki Yesu. Wamvika vazi jangavu na kumfanyia mzaha. Halafu wampeleka tena kwa Pilato. Tokeo ni kwamba, Herode na Pilato, ambao hapo kwanza walikuwa wamekuwa maadui, wanakuwa marafiki wakubwa.
Yesu anaporudi, Pilato aita makuhani wakuu, watawala wa Wayahudi, na watu wakusanyike pamoja na kusema hivi: “Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilotenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua.”
Hivyo, Pilato amejulisha rasmi mara mbili kwamba Yesu hana hatia. Ana hamu ya kumwacha huru, kwa maana afahamu kwamba ni kwa sababu ya wivu tu kwamba makuhani wamemtia mikononi mwake. Lakini Pilato anapoendelea kujaribu kumwachilia Yesu, apata kichocheo kingine imara afanye hivyo. Anapokuwa katika kiti chake cha hukumu, mke wake apeleka ujumbe, akimhimiza hivi: “Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto [kwa wazi yenye asili ya kimungu] kwa ajili yake.”
Hata hivyo, Pilato aweza kufunguaje mwanamume huyu asiye na hatia, kama vile anavyojua inampasa? Yohana 18:36-38; Luka 23:4-16; Mathayo 27:12-14, 18, 19; 14:1, 2; Marko 15:2-5.
▪ Yesu ajibuje swali kuhusu ufalme wake?
▪ Ni nini “kweli” ambayo Yesu alitumia maisha yake ya kidunia akiitolea ushahidi?
▪ Hukumu ya Pilato ni nini, watu waitikiaje, na Pilato afanyia Yesu nini?
▪ Herode Antipa ni nani, kwa nini ana shangwe nyingi mno kumwona Yesu, naye amfanyia nini?
▪ Kwa nini Pilato ana hamu ya kumweka Yesu huru?
-
-
“Tazama, Mtu Huyu!”Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 123
“Tazama, Mtu Huyu!”
KWA kuvutiwa na utulivu wa Yesu na akitambua kwamba hana kosa, Pilato afuatia njia nyingine ya kumwachilia. “Kwenu kuna desturi,” aambia umati wa watu wale, “ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka [Sikukuu ya Kupitwa, NW].”
Baraba, muuaji mwenye sifa mbaya, amefungwa pia akiwa mfungwa-gereza, hivyo basi Pilato auliza: “Mnataka niwafungulie yupi? yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo?”
Kwa kuvutwa na usadikisho wa makuhani wakuu ambao wamewachochea, watu waomba Baraba aachiliwe lakini Yesu auawe. Bila kukata tamaa, Pilato ajibu, akiuliza tena: “Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili?”
“Baraba,” wapaaza sauti.
“Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo?” Pilato auliza kwa kufadhaika.
Kwa mngurumo mmoja wenye kishindo cha kuziba masikio, wajibu: “Asulibiwe [acha atundikwe, NW]”! “Msulibishe! Msulibishe [mtundike, NW]!”
Kwa kujua kwamba wadai kifo cha mtu asiye na hatia, Pilato asihi hivi: “Kwa sababu gani? huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi [kumwadhibu] nitamfungua.”
Japo majaribio yake, umati huo wenye hasira, kwa kuchochewa na viongozi wao wa kidini, waendelea kupiga kelele: “Asulibiwe [atundikwe, NW]”! Kwa kuchochewa sana na makuhani, umati wataka damu. Na ebu fikiri, siku tano tu kabla ya hapo, wengine wao labda walikuwa miongoni mwa wale waliokaribisha Yesu kuingia Yerusalemu akiwa Mfalme! Muda wote huu, wanafunzi wa Yesu, ikiwa wapo, wabaki kimya na bila kujitokeza wazi.
Pilato, akiona kwamba maneno yake ya kusihi hayafai kitu, bali kunatokea fujo, achukua maji na kunawa mikono mbele ya ule umati, na kusema: “Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.” Hapo watu hao wajibu: “Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”
Hivyo basi, kulingana na madai yao—naye akitaka kufurahisha umati huo kuliko kufanya analojua kuwa haki—Pilato awafungulia Baraba. Achukua Yesu na kuagiza avuliwe mavazi halafu apigwe mijeledi. Huku hakukuwa kupiga viboko vya kawaida. The Journal of the American Medical Association linaeleza zoea la Kiroma la kupiga mijeledi:
“Chombo cha kawaida kilikuwa kiboko kifupi (flagramu au flagelamu) chenye kamba kadhaa moja moja za ngozi-kavu au zilizosokotwa zikiwa na marefu mbalimbali, ambamo vipande vidogo vya chuma au vipande vyenye ncha kali vya mifupa ya kondoo vilifungwa kwa kuachana. . . . Askari Waroma walipopiga-piga mgongo wa mfungwa kwa nguvu kamili, vile vipande vya chuma vya mfiringo vingesababisha michubuo ya kina kirefu, na zile kamba za ngozi-kavu na mifupa ya kondoo zingekata ndani ya ngozi na sehemu zilizo chini ya ngozi ya mwili. Halafu, kupigwa mijeledi kulipoendelea, miraruko ya ngozi ingeingia chini ya nyuzi za mnofu chini kwenye mifupa ya mwili na kutokeza nyuzinyuzi zenye kuning’inia za mnofu wenye kutoka damu.”
Baada ya kupigwa huko kenye mateso makali, Yesu apelekwa ndani ya jumba la gavana, na kikundi kizima cha askari kinaitwa kikusanyike. Humo askari warundika matukano zaidi juu yake kwa kusokota taji la miiba na kulisukuma juu ya kichwa chake. Watia mwanzi katika mkono wake wa kulia, nao wamvika vazi la zambarau, namna inayovaliwa na watu wa kifalme. Halafu wamwambia hivi kwa dhihaka: “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!” Pia, wamtemea mate na kumpiga kofi usoni. Wakichukua ule mwanzi imara kutoka mkononi mwake, wautumia kumpiga kichwani, hiyo ikizidi kuisukuma ndani ya ngozi ya kichwa chake ile miiba iliyochongoka ya “taji” lake lenye kumshushia heshima.
Fahari na imara ya kusifika ambayo Yesu anayo katika kuelekeana na kutendewa vibaya huko inavutia sana Pilato hivi kwamba inamsukuma kufanya jaribio jingine la kumwachilia. “Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake,” awaambia umati wa watu. Inawezekana kuwa awazia kwamba sura ya hali ya kuteswa-teswa kwa Yesu italainisha mioyo yao. Yesu anapokuwa amesimama mbele ya watu hao wenye fujo wasio na moyo wa huruma, akiwa amevaa taji la miimba na lile vazi la nje la zambarau na huku uso wake wenye kutoka damu ukiwa na maumivu, Pilato atangaza: “Tazama, mtu huyu!”
Ingawa amechubuliwa na kutwangwa, hapa amesimama mtu mwenye kutokeza zaidi katika historia yote, kwa kweli binadamu wa kutokeza zaidi aliyepata kuishi! Ndiyo, Yesu aonyesha fahari ya unyamavu na utulivu unaoonyesha ukuu ambao hata Pilato alazimika kuukubali wazi, kwa maana inaonekana maneno yake ni mchanganyiko wa heshima na huruma pia. Yohana 18:39–19:5; Mathayo 27:15-17, 20-30; Marko 15:6-19; Luka 23:18-25.
▪ Pilato ajaribu kwa njia gani kufanya Yesu aachiliwe?
▪ Pilato ajaribuje kujiondolea daraka?
▪ Ni nini kinachohusika katika kupigwa mijeledi?
▪ Yesu adhihakiwaje baada ya kupigwa mijeledi?
▪ Ni jaribio gani zaidi ambalo Pilato afanya ili kumwachilia Yesu?
-
-
Atiwa Mikononi na KuchukuliwaYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 124
Atiwa Mikononi na Kuchukuliwa
WAKATI Pilato, kwa kusukumwa na fahari tulivu ya Yesu aliyeteswa, ajaribupo tena kumfungua, makuhani wakuu wakasirika hata zaidi. Wamepiga moyo konde kutoacha chochote kivuruge kusudi lao bovu. Hivyo basi wao warudia tena kupaaza sauti hivi: “Msulibishe! Msulibishe [Mtundike, mtundike, NW]!”
“Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe,” Pilato ajibu. (Tofauti na madai yao ya mapema kidogo, Wayahudi waweza kuwa na mamlaka ya kufisha wahalifu kwa makosa ya kidini yaliyo na uzito wa kutosha.) Halafu, kwa mara kama ya tano, Pilato amtangaza Yesu kuwa hana hatia, akisema hivi: “Mimi sioni hatia kwake.”
Wayahudi, kwa kuona kwamba mashtaka yao ya kisiasa yameshindwa kuleta matokeo, warudia tena lile shtaka la kidini la kukufuru lililotumiwa mapema kidogo kwenye kesi ya Yesu mbele ya Sanhedrini. “Sisi tunayo sheria,” wao wasema, “na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”
Shtaka hilo ni jipya kwa Pilato, nalo lafanya awe na hofu zaidi. Kufikia sasa afahamu kwamba Yesu si mtu wa kawaida tu, kama vile ndoto ya mke wake na nguvu nyingi ajabu za utu wa Yesu vyaonyesha. Lakini eti “Mwana wa Mungu”? Pilato ajua kwamba Yesu ni wa kutoka Galilaya. Hata hivyo, je! angeweza kuwa aliishi kabla ya hapo? Akimrudisha tena ndani ya jumba la utawala, Pilato auliza: “Wewe umetokapi?”
Yesu akaa kimya. Mapema kidogo alikuwa amemwambia Pilato kwamba yeye ni mfalme, lakini kwamba Ufalme wake si sehemu ya ulimwengu huu. Sasa hakuna elezo lolote zaidi lingetimiza kusudi lenye mafaa. Hata hivyo, fahari ya Pilato yaumizwa na katao la kujibu, naye amwakia Yesu kwa maneno haya: “Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha [kukutundika, NW]?”
“Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu,” Yesu ajibu kwa staha. Amaanisha mamlaka ambayo Mungu amewapa watawala wa kibinadamu kusimamia mambo ya kidunia. Yesu aongezea hivi: “Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.” Kwa kweli, kuhani mkuu Kayafa na wenzi wake na Yuda Iskariote wote wana daraka zito kuliko Pilato kwa ajili ya kutendwa kwa Yesu isivyo haki.
Kwa kuvutiwa hata zaidi na Yesu na akiwa na hofu kwamba huenda ikawa Yesu ana asili ya kimungu, Pilato ajitahidi tena kumwachilia. Hata hivyo, Wayahudi wamjibu vikali Pilato. Wao warudia shtaka lao la kisiasa, wakitisha hivi kwa ujanja: “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.”
Ijapokuwa hilo lamaanisha matokeo ya kuogopesha sana, Pilato amleta Yesu nje tena. “Tazama, Mfalme wenu!” bado awasihi tena.
“Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe [Mtundike, NW]!”
“Je! nimsulibishe [nimtundike, NW] mfalme wenu!” Pilato auliza kwa kukata tamaa.
Wayahudi wamekuwa wakiudhika chini ya utawala wa Waroma. Kwa kweli, wao wadharau kutawalwa na Roma! Na bado, kwa unafiki, makuhani wakuu wasema hivi: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”
Akihofia cheo na sifa yake ya kisiasa, Pilato mwishowe ashindwa na madai ya Wayahudi yasiyokoma. Amtia Yesu mikononi mwao. Askari wamvua Yesu joho la zambarau na kumvika mavazi yake ya nje. Yesu achukuliwapo kutundikwa, alazimishwa abebe mti wake mwenyewe wa mateso.
Kufikia sasa ni asubuhi katikati siku ya Ijumaa, Nisani 14; labda yakaribia kuwa mchana katikati. Yesu amekuwa macho tangu mapema asubuhi ya Alhamisi, naye amepatwa na mateso makali moja baada ya jingine. Basi inaeleweka kwa nini nguvu zinamwishia chini ya uzito wa ule mti. Hivyo basi mpitaji njia, Simoni fulani wa Kirene katika Afrika, alazimishwa katika utumishi ambebee mti huo. Wanaposonga mbele, watu wengi, kutia na wanawake, wafuata, wakijipiga-piga kwa huzuni kuu na kumwombolezea Yesu.
Akigeukia wanawake hao, Yesu asema: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri [wenye furaha ni, NW] walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. . . . Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Yesu anarejezea mti wa taifa la Kiyahudi, ambao ungali una umajimaji fulani wa uhai ndani yao kwa sababu ya kuwapo kwa Yesu na kuwako kwa mabaki wanaomwamini. Lakini hao wakiisha kuondolewa katika taifa lile, ni mti mfu tu wa kiroho utabaki, ndiyo, tengenezo la kitaifa lililonyauka. Loo, kutakuwa na sababu iliyoje ya kulia machozi wakati majeshi ya Kiroma, yakitumiwa kuwa wafishaji wa Mungu, yatakapoliacha ukiwa taifa la Kiyahudi! Yohana 19:6-17; 18:31; Luka 23:24-31; Mathayo 27:31, 32; Marko 15:20, 21.
▪ Ni shtaka gani ambalo viongozi wa kidini wanafanya dhidi ya Yesu wakati mashtaka yao ya kisiasa yanaposhindwa kuleta matokeo?
▪ Kwa nini Pilato awa mwenye hofu zaidi?
▪ Ni nani wanaochukua dhambi iliyo kubwa zaidi kwa ajili ya yale yanayopata Yesu?
▪ Makuhani wanamfanyaje Pilato amtie Yesu mikononi ili auawe?
▪ Yesu awaambia nini wanawake wanaomlilia, naye amaanisha nini kwa kurejezea mti kuwa “mbichi” kisha “mkavu”?
-
-
Maumivu Makali Juu ya MtiYule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 125
Maumivu Makali Juu ya Mti
PAMOJA na Yesu wanyang’anyi wawili wachukuliwa nje wakauawe. Si mbali na jiji, andamano lasimama mahali paitwapo Golgotha, au Fuvu la Kichwa.
Wafungwa hao wavuliwa mavazi yao. Halafu wapewa divai iliyotiwa manemane ambayo ni dawa ya kulevya. Inaonekana imetayarishwa na wanawake wa Yerusalemu, na Waroma huwa hawawanyimi wenye kutundikwa mchanganyo huu wa kinywaji chenye kumaliza maumivu. Hata hivyo, Yesu anapokionja, akataa kunywa. Kwa nini? Kwa wazi ataka kuwa na nguvu zake zote za kufikiri wakati wa jaribu hili la imani yake lililo kubwa kupita yote.
Sasa Yesu amenyooshwa juu ya mti huku mikono yake ikiwa imewekwa juu ya kichwa chake. Ndipo askari wanapopigilia misumari mikubwa katika mikono yake na katika miguu yake. Yeye ajigeuza-geuza kwa maumivu wakati misumari inapochoma mnofu na nyuzi za mwili. Mti unaposimamishwa wima, maumivu yazidi kweli kweli, kwa maana uzito wa mwili wake wapasua sehemu za majeraha yenye misumari. Hata hivyo, badala ya kutisha, Yesu asali hivi kwa ajili ya askari hao Waroma: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.”
Pilato amebandika juu ya mti huo ishara ambayo inasema: “YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” Inaonekana, yeye aandika hivi si kwa sababu tu aheshimu Yesu bali pia kwa sababu achukizwa sana na makuhani Wayahudi kwa kuwa wamemkaza mpaka akalazimika kuhukumia Yesu kifo. Ili wote waweze kusoma ishara hiyo, Pilato aagiza iandikwe katika lugha tatu—katika Kiebrania, katika Kilatini rasmi, na katika Kigiriki cha kawaida.
Makuhani wakuu, kutia na Kayafa na Anasi, wafadhaika. Tangazo hili la hakika linaharibu saa yao yenye shangwe ya ushindi. Kwa hiyo wapinga hivi: “Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.” Akiudhika kwa kuwa ametumika kama chombo cha kutimizia nia ya makuhani hao, Pilato ajibu kwa madharau yenye kukata maneno: “Niliyoandika nimeyaandika.”
Makuhani, pamoja na umati mkubwa, sasa wakusanyika mahali pa mauaji, na makuhani wajaribu kukanusha ushuhuda wa ile ishara. Warudia ule ushuhuda wa bandia uliotolewa mapema kidogo kwenye majaribu ya Sanhedrini. Kwa hiyo, haishangazi kwamba wapita njia waanza kusema kwa matusi, wakitikisa vichwa vyao kwa mzaha na kusema: “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani [kutoka kwenye mti wa mateso, NW]”!
“Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe”! nao makuhani wakuu na marafiki wao wa kidini waingilia kama kwamba ni kwa sauti moja. “Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani [kutoka kwenye mti wa mateso, NW], nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama amtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”
Kwa kunaswa katika roho hiyo, askari wajiunga pia katika kufanyia Yesu mzaha. Wamtolea divai kali kwa mzaha, yaonekana ikiwa imepita kidogo tu mbele ya midomo yake iliyokauka. “Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi,” wanadhihaki vikali, “ujiokoe mwenyewe.” Hata wale wanyang’anyi—mmoja akiwa ametundikwa kulia kwa Yesu, na yule mwingine kushoto kwake—wamdhihaki. Fikiria hilo! Binadamu mkubwa zaidi aliyepata kuishi, ndiyo, yule aliyeshiriki pamoja na Yehova Mungu katika kuumba vitu vyote, apatwa na fedheha yote hiyo akiwa ameazimia kabisa!
Askari wachukua mavazi ya Yesu ya nje na kuyagawanya sehemu nne. Wapiga kura kuona yatakuwa ya nani. Hata hivyo, lile vazi la ndani halina mshono wa kuliunga, kwa kuwa ni la ubora mwingi. Hivyo basi askari hao waambiana: “Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani.” Hivyo, bila kujua, watimiza andiko linalosema: “Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura.”
Baada ya muda, mmoja wa wanyang’anyi aja kuthamini kwamba kwa kweli ni lazima iwe Yesu ni mfalme. Kwa hiyo, akikemea mwandamani wake, asema hivi: “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.” Halafu aongea na Yesu, na kutoa ombi hili: “Nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”
“Kweli kweli mimi nakuambia wewe leo,” Yesu ajibu, “Wewe utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.” (NW) Ahadi hii itatimizwa wakati Yesu atakapotawala mbinguni na kufufua mtenda maovu huyo mwenye kutubu kwenye uhai duniani katika Paradiso ambayo waokokaji wa Har–Magedoni na waandamani wao watakuwa na pendeleo la kuisitawisha. Mathayo 27:33-44; Marko 15:22-32; Luka 23:27, 32-43; Yohana 19:17-24.
▪ Kwa nini Yesu akataa kunywa divai iliyotiwa manemane ambayo ni dawa ya kulevya?
▪ Yaonekana ni kwa nini ile ishara imebandikwa juu ya mti wa Yesu, nayo yaanzisha maneno gani kati ya Pilato na makuhani wakuu?
▪ Yesu adhihakiwa zaidi namna gani juu ya mti wa mateso, na kwa wazi ni nini kinachoongoza jambo hilo?
▪ Unabii watimizwaje katika linalofanywa na mavazi ya Yesu?
▪ Mmoja wa wanyang’anyi afanya badiliko gani, na Yesu atatimizaje ombi lake?
-
-
“Hakika Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
-
-
Sura 126
“Hakika Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”
YESU hajawa juu ya ule mti kwa muda mrefu wakati ambapo, katika mchana kakati, giza la kifumbo, lenye urefu wa saa tatu latukia. Halisababishwi na kupatwa kwa jua, kwa kuwa kupatwa kwa jua hutukia tu wakati wa mwezi mpya na mwezi ni mpevu wakati wa Sikukuu ya Kupitwa. Zaidi ya hilo, kupatwa kwa jua huwa kwa dakika chache tu. Hivyo basi giza hili lina chanzo cha kimungu! Labda lawaachisha kidogo wale wanaomdhihaki Yesu, hata kusababisha dhihaka zao kali zikome.
Ikiwa ajabu hii yenye kutia woga yatukia kabla ya yule mtenda maovu mmoja kumtia adabu mwandamani wake na kumwomba Yesu amkumbuke, huenda hilo likawa ni jambo moja linaloleta toba yake. Labda ni wakati wa giza hilo kwamba wanawake wanne, yaani, mama ya Yesu na Salome dada yake, Mariamu Magdalene, na Mariamu mama ya mtume Yakobo Mdogo, wasogelea kuja karibu na mti wa mateso. Yohana, mtume mpendwa wa Yesu, yupo hapo pamoja nao.
Lo, jinsi moyo wa mama ya Yesu ‘wachomwa’ atazamapo mwana aliyemlea na kumtunza kwa mapenzi akining’inia hapo kwa maumivu makali! Lakini Yesu afikiria, si maumivu yake mwenyewe, bali hali njema ya mama yake. Kwa jitihada kubwa, amtolea Yohana ishara kwa kichwa chake na kusema hivi kwa mama yake: “Mama [mwanamke, NW], tazama, mwanao”! Halafu, akitoa ishara iyo hiyo kuelekea Mariamu, asema hivi kwa Yohana: “Tazama, mama yako”!
Kwa njia hiyo Yesu akabidhi utunzaji wa mama yake, ambaye ushuhuda waonyesha kwamba sasa yeye ni mjane, mikononi mwa mtume wake aliyependwa kipekee. Afanya hivyo kwa sababu wana wengine wa Mariamu hawajadhihirisha bado imani katika yeye. Hivyo yeye aweka mfano mzuri wa kutoa riziki si kwa mahitaji ya kimwili tu ya mama yake bali pia kwa mahitaji yake ya kiroho.
Karibu saa tisa mchana, Yesu asema hivi: “Naona kiu.” Yesu ajisikia ni kama kwamba Baba yake ameondoa ulinzi kutoka kwake ili ukamilifu wake ujaribiwe kabisa. Hivyo apaaza sauti hivi: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Wasikiapo hayo, watu fulani waliosimama karibu washangaa na kusema kwa sauti kubwa: “Tazama, anamwita Eliya.” Mara hiyo mmoja wao akimbia na, akitia sifongo iliyofyonza divai chungu kwenye ncha ya kishina cha hisopo, ampa kinywaji. Lakini wengine wasema hivi: “Acheni; na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha.”
Yesu apokeapo ile divai chungu, alia kwa sauti kubwa: “Imekwisha.” Ndiyo, amemaliza kila jambo ambalo Baba yake amemtuma duniani afanye. Mwisho, asema hivi: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Kwa njia hiyo Yesu amkabidhi Mungu nguvu ya uhai wake akiwa na hakika kwamba Mungu atamrudishia huo. Halafu ainamisha kichwa chake na kufa.
Yesu avutapo pumzi yake ya mwisho, tetemeko kali la dunia latukia, likipasua wazi miamba. Tetemeko hilo lina nguvu sana hivi kwamba maziara ya ukumbusho nje ya Yerusalemu yaachwa wazi na maiti zatupwa nje yayo. Wapita-njia, ambao waona miili mifu ambayo imefichuliwa wazi, waingia katika jiji na kuripoti jambo hilo.
Zaidi ya hilo, Yesu afapo, lile pazia kubwa sana ligawanyalo Patakatifu na Patakatifu Zaidi katika hekalu la Mungu lapasuliwa mara mbili, kutoka juu hadi chini. Kwa wazi pazia hilo lililopambwa vizuri lina urefu wa kwenda juu wa meta 18 na ni zito sana! Muujiza huo wa kushangaza sana si kwamba wadhihirisha tu hasira kali ya Mungu juu ya walioua Mwana Wake bali pia wamaanisha kwamba njia ya kuingia Patakatifu Zaidi, mbinguni penyewe, sasa imewezeshwa na kifo cha Yesu.
Basi, watu hao waonapo tetemeko hilo la dunia na kuona mambo yanayotendeka, waogopa sana. Ofisa wa jeshi mwenye kusimamia mambo kwenye mahali hapo pa mauaji hayo ampa Mungu utukufu. “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu,” atangaza. Yaelekea alikuwapo wakati dai la uana wa kimungu lilipozungumzwa kwenye jaribu la Yesu mbele ya Pilato. Na sasa yeye asadiki kwamba Yesu ndiye Mwana wa Mungu, ndiyo, kwamba kweli yeye ndiye binadamu mkubwa zaidi aliyepata kuishi.
Wengine pia washangazwa mno na matukio hayo ya kimuujiza, nao waanza kurudi nyumbani wakijipiga-piga vifua vyao kama ishara ya huzuni kuu na aibu yao nyingi sana. Wanafunzi wengi wa Yesu wa kike ambao waguswa moyo sana na matukio hayo ya maana sana wanatazama tamasha hii kwa mbali. Mtume Yohana yupo pia. Mathayo 27:45-56; Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; 2:34, 35; Yohana 19:25-30.
▪ Kwa nini kupatwa kwa jua hakuwezi kuwa ndiko kumesababisha zile saa tatu za giza?
▪ Muda mfupi kabla ya kifo chake, Yesu aweka mfano gani mzuri kwa ajili ya wale walio na wazazi wazee?
▪ Yesu asema maneno gani ya mwisho kabla ya kufa?
▪ Tetemeko la dunia latimiza nini, na ni nini maana ya kupasuliwa kwa pazia la hekalu vipande viwili?
▪ Miujiza hiyo yawa na matokeo gani juu ya ofisa wa jeshi mwenye kusimamia mambo kwenye mahali hapo pa mauaji?
-