Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 10/8 kur. 6-11
  • Kusaidia Watoto wa Talaka

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kusaidia Watoto wa Talaka
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wazazi—Daraka Lao Lenye Maana
  • Kutumia Wakati kwa Kufaa
  • Mtoto Aliyegawanywa
  • Je, Wengine Waweza Kusaidia?
  • Wakati Familia Itakapopona
  • Talaka Huwa na Majeruhi
    Amkeni!—1991
  • Mambo Manne Unayopaswa Kujua Kuhusu Talaka
    Amkeni!—2010
  • Jinsi Talaka Inavyowaathiri Watoto
    Msaada kwa Ajili ya Familia
  • Nyumba Iliyogawanyika—Jinsi Talaka Inavyowaathiri Vijana
    Amkeni!—2009
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 10/8 kur. 6-11

Kusaidia Watoto wa Talaka

“Wakati mmoja, nilipokuwa na umri wa miaka mitatu, baba yangu alikuja kunichukua twende kuzuru. Tulienda na akanirudisha nyumbani kwa gari. Tulikaa ndani ya gari pamoja kwa kipindi kidogo. Lakini mara tu mama yangu alipotokea nje kuja kunichukua, yeye na baba yangu walianza kugombezana na kubishana kupitia dirisha la gari—mimi nikiwa katikati.

“Kwa ghafula baba yangu akafungua mlango na kunisukuma nje ya gari. Halafu akaendesha gari kwa kasi sana na kutoweka. Mimi sikujua kilichokuwa kinatendeka. Mama yangu hata hakuniruhusu nimfungue mwanasesere wangu. Sikumwona kamwe baada ya hapo. Na sikumwona baba yangu tena mpaka nilipokuwa na umri wa miaka 19.”—Heidi.

“WAKATI huponya jameraha yote,” ndivyo husema mithali moja. Je, mithali hiyo ni ya kweli? Au watoto huharibiwa kabisa na talaka bila matumaini ya kurudia hali yao ya kwanza?

Kulingana na The Journal of Social Issues, mengi yanategemea yale yanayotukia baada ya talaka. Jarida hilo linasema: “Mahusiano ya kifamilia ambayo hutokea baada ya talaka huathiri watoto kwa njia ile ile ambayo talaka huwaathiri au hata kwa ubaya zaidi.”

Katika kisa cha Heidi, talaka ya wazazi wake ilikuwa tu ndio mwanzo wa matatizo yake. Kama vile itukiavyo kwa kawaida, ndoa ya pili ya mama yake haikufanikiwa kupita ile ya kwanza, na hata ile iliyofuata. Maisha ya Heidi akiwa mtoto yaliokuwa kama kusafiri kwenye basi lenye vishindo ambako vita vingi vyenye mayowe na kuvunjwa kwa vyombo vya jikoni na hali kadhalika siku za kiangazi zenye upweke katika nyumba iliyo tupu, akifikiria kwa hofu ni wakati gani—na kama—mama yake angekuja nyumbani.

Kuna mengi ambayo wazazi waweza kufanya ili kuepusha watoto wao kutokana na matokeo haya yenye msukosuko ya talaka. Talaka, kwa vyovyote vile, hukomesha ndoa, si kuwa mzazi.

Wazazi—Daraka Lao Lenye Maana

“Kile kitendo cha uzazi kinastahilisha watoto kuwa na mama na baba,” wakaandika wanasaikolojia wawili katika Psychology Today. Maneno hayo huenda yakaonekana kwako kama ni yenye kujithibitisha yenyewe. Na bado, talaka hunyima mtoto wazazi wote wawili katika njia fulani kama kwa dhoruba moja.

Kwa mfano, fikiria juu ya United States, ambayo kwa takwimu yaweza kuitwa kitovu kikuu cha talaka ulimwenguni. Huko, zaidi ya asilimia 90 ya watoto wa talaka wanaishi na mama na wana uhusiano wa kiziara na baba. Zaidi ya nusu ya watoto hao huona baba zao mara moja tu kwa mwaka au hata hukosa kumwona kabisa! Na ule wakati ambao mama hutumia na watoto wake hushuka pia baada ya talaka, kwa kadiri ya saa 21 kwa juma, kulingana na uchunguzi mmoja.

Kama wachunguzi hukubaliana kwa chochote kingine, wao wanakubali kwamba watoto huelekea kujipatanisha vema na maisha baada ya talaka ikiwa wao wanaendelea kuwa na uhusiano unaofaa na wenye uendelevu na wazazi wote wawili. Ikiwa hilo haliwezekani, uhusiano mwema na angalau mzazi mmoja bado husaidia kuzimisha mpigo huo wa talaka. Lakini wazazi wawezaje kusitawisha ukaribu huo na watoto wao baada ya talaka?

Kutumia Wakati kwa Kufaa

Ikiwa wewe ni mama uliyetalikiwa, kudumisha ukaribu huenda kukawa jambo gumu la ushindani. Mara nyingi, huenda ukapatwa na kile ambacho jamii nyingi huona kuwa ni alama mbili za aibu: talaka na umaskini. Huku ukiingia katika hali ya kufanya kazi bila ya kuwa umejitayarisha, hali ukijitahidi kujazia malipo ya utegemezo kutoka kwa aliyekuwa mwenzi wako ambayo huwa hayategemeki au hayatoshi, huenda ukahisi kwamba una wakati mchache unaobaki kwa ajili ya watoto wako.

Jibu lenyewe: jitihada na ratiba. Nunua wakati wowote ule unaoweza kuupata, na upange na mtoto wako kile mtakachofanya wakati huo. Hata wakati mchache kila siku wa akili isiyogawanyika ni afadhali zaidi kuliko kukosa kabisa. Kupangia kimbele tafrija yenye maana mkiwa pamoja pia humpa mtoto wako jambo la kutazamia.

Halafu kuna uhitaji wa muhimu wa kumpa mtoto wako mwongozo wa kiroho, nidhamu, na mazoezi. Wakati ulio dhahiri kabisa kwa ajili ya makusudi haya huenda uwe vigumu kuupata. Hivyo Biblia hushauri: “Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena, uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”—Kumbukumbu la Torati 6:7.

Je, huwa mmo “njiani” pamoja kamwe, labda mkisafiri kwa gari lako au mkitumia usafiri wa umma? Nini huvutia uangalifu wako—mtoto wako, au gazeti au redio ya gari? Wakati mnapokula pamoja, je, televisheni huzamisha maongezi yote, au mlo huo huwa ndio wakati wa familia yako kuzungumza kwa amani? Je, kuna kazi mbalimbali unazoweza kushiriki pamoja na mtoto wako, kama vile kutayarisha chakula au kufua nguo?

Bila shaka hiyo haimaanishi kwamba wewe unyakue vipindi hivi ili kuhutubia mtoto wako. Kwa kuwa pamoja tu na mtoto wako na kuzungumza kirafiki na kwa uwazi, pasipo shaka utatia ndani yake baadhi ya sifa zako. Nyakati kama hizi zaweza pia kuwa fursa zifaazo kwako kuwapa watoto wako uhakikisho wanaohitaji sana sasa. Watoto fulani huhisi kwa usiri kuwa wenye lawama kwa mvunjiko wa wazazi wao. Wengine huhisi wamekataliwa na mzazi aliyeondoka nyumbani. Ikiwa unawahakikishia mara kwa mara juu ya upendo wako kwao, ukiwasifu kwa tabia zao nzuri na mambo wanayotimiza, na kuwafanya wahisi kuwa salama vya kutosha kuweza kusema yaliyo akilini kwa unyofu, utakuwa umefanya mengi katika kuzimisha mpigo wa talaka.

Wazazi wengine huachilia nidhamu baada ya talaka, mara nyingi ikiwa ni kutokana na hisia za hatia. ‘Mwanangu ameona magumu ya kutosha siku za hivi karibuni,’ wao waonekana wakisababu. Lakini kupatia watoto wako uhuru wa kufanya watakavyo si kuwaonyesha upendo. Mkurugenzi wa programu ya wabalehe na watoto katika hopitali ya kutibu ugonjwa wa akili aliambia The Washingtonian hivi: “Watoto mara nyingi huniambia hivi, ‘wazazi wangu huniruhusu nifanye nitakavyo. Wao hawanijali.’” Kama vile Biblia isemavyo: “Usipotia mtoto wako nidhamu, wewe humpendi. Iwapo kweli wampenda, utamsahihisha.”—Mithali 13:24, Todays English Version.

Mtoto Aliyegawanywa

Wakati mvulana mmoja mchanga alipoulizwa achore picha katika kliniki ya talaka, alijichora mwenyewe akiwa kama chombo cha kuvutaniwa kati ya wazazi wake wawili wenye hamaki; alikuwa anakongonyolewa kwenye vifundo akitokwa na damu humo. Hivyo ndivyo baadhi ya watoto wa wazazi waliotalikiana huhisi. Hali mtoto anawapenda wazazi wote wawili, hakuna mzazi anayetaka mtoto ampende yule mwingine.

Katika uchungu mkali wa moyo na maneno ambao huambatana na talaka, ni vigumu sana watoto wasitiwe ndani na wazazi wao katika pigano hilo. Wallerstein na Kelly waliripoti kwamba theluthi mbili ya wazazi katika uchunguzi wao walishindania kwa udhahiri upendo na utii wa watoto wao. Dakt. Bienenfeld aonya wazazi kwamba kumfanya mtoto ahisi kuwa amegawanywa kati ya wazazi kunaweza kutokeza hisia za kujichukia na za kuwa na hatia na “kutapunguza nafasi zake za kuwa na furaha, kutosheka na kufanikiwa.”

Biblia hushauri hivi kwa hekima: “Nanyi, akina baba [au akina mama], msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana [Yehova, NW]. (Waefeso 6:4.) Kwa wazi, kumfanya mtoto wako achukie yule mzazi mwingine si kumlea katika njia ya Kikristo.

Kila mtoto ana wazazi wawili. Kifo chaweza kubadilisha hilo, lakini talaka haiwezi. Na isipokuwa korti liwe limezuia mzazi yule mwingine asiwaone watoto (au yule mzazi mwingine anaepa daraka kimakusudi), huenda ukahitaji kushirikiana na aliyekuwa mwenzi wako katika kutunza watoto.

Ni kweli, huenda ukawa na sababu ya haki ya kuwa na uchungu kuelekea aliyekuwa mwenzi wako. Lakini ukitumia watoto wako ili kumwadhibu, ni watoto wako ndio hasa huumia. Dakt. Bienenfeld adokeza kwamba kwa kukubali wewe mwenyewe kwamba huenda ulihusika pia katika matatizo yenu ya ndoa kwaweza kusaidia kuondoa uchungu wako. Gazeti Parents lasema juu ya mwanamke mmoja aliyejaribu kusali kwa niaba ya aliyekuwa mwenzi wake wakati wowote alipokuwa na fikira zisizofaa kumwelekea. Alipata kwamba mbinu hiyo ilimpa hisia ya hali njema na udhibiti iliyokuwa mpya kabisa kwake na iliyomweka huru kutokana na ‘kuganda katika hali ya kudumu ya vita.’—Linganisha Mathayo 5:43-45.

Je, Wengine Waweza Kusaidia?

Wanasaikolojia Julius na Zelda Segal waandika katika gazeti Parents kwamba “watoto katika familia zilizovunjika hutiwa nguvu ikiwa angalau nyuzi fulani za uendelevu zabaki bila kudhuriwa” baada ya dhoruba ya talaka. Kwa kuhuzunisha, kulingana na wanasaikolojia hawa, “kuna mwelekeo wa majirani na marafiki kujiepusha, na ndivyo ilivyo na mababu na nyanya fulani kwa sababu wanajishugulisha kuchukua upande fulani wa ule mzozo wa wazazi.”

Naam, talaka ni yenye ukatili hasa kwa watoto wakati watu wa ukoo wanapowatoweka maishani mwao. Hiyo huongeza hisia zao za kuachwa tupu. Hivyo ikiwa wewe ni shangazi, mjomba, babu au nyanya ya watoto wowote wa talaka, kaza fikira kwenye kuwapa uhakikishio wanohitaji sana sasa badala ya kushiriki katika mzozo wa wazazi wao. Wakati mwingine, hakuna mtu awezaye kutia mtoto nguvu kuliko babu au nyanya mwenye upendo.

Heidi, aliyenukuliwa mwanzoni mwa makala hii, hakupokea utegemezo kama huo. Na bado, hadithi yake ni yenye mafanikio. Leo, akiwa na umri wa miaka 26, yeye ni mwanamke aliyeolewa katika ndoa yenye furaha, mwenye ukunjufu wa moyo, na bidii. Ni nini kimechangia kufaulu kwake?

Kwa neno moja: urafiki. Akiwa tineja, Heidi alianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Kwenye Jumba la Ufalme ambako alihudhuria mikutano, yeye alipata marafiki wa kweli. “Nilikuwa ninafikiri kwamba hali yangu ilikuwa bila matumanini kabisa,” yeye akumbuka. “Lakini kuwa na watu unaoweza kuzungumza nao husaidia. Nilikuwa na rafiki mmoja ambaye ningeweza kumwambia lolote. Yeye wakati wote alijua kama kulikuwa na chochote chenye kasoro, na mwishowe ningemweleza. Yeye alikuwa kama mama kwangu. Lakini kulikuwa na wengine ambao ningeweza kufanya vitu pamoja nao pia.” Heidi alipata ukweli wa ahadi ya Yesu kwamba kundi la Kikristo lingeandaa familia kubwa kwa wale waliopoteza yao.—Marko 10:29, 30.

Lakini si Heidi aliyeanzisha urafiki huo. “Walinitafuta,” yeye asema. Na hilo ni jambo lenye kutukia mara nyingi kati ya watoto wa talaka katika kundi la Kikristo. Kwa mfano, mwanamke mchanga jina lake Meg hukumbuka kwa uchangamshi jinsi wenzi wawili wa ndoa walivyofanya urafiki naye baada ya wazazi wake kuachana: “Wao walijua tu kwamba niliwahitaji, na wao walikuwa karibu nami. Wewe hutaki kusema, ‘Ona, ninakuhitaji. Ninataka unipende sasa.’”

Namna gani wewe? Je, waweza kuwa kama ndugu, dada, mama, baba, babu au nyanya kwa mtoto wa talaka? Huyo kijana labda hatakuuliza ufanye hivyo, lakini hiyo haimaanishi kwamba yeye hakuhitaji.

Bila shaka, wewe hutaweza kamwe kurudisha hali zote za familia iliyounganika. Lakini waweza kuwa rafiki, msikilizaji mzuri, mwenye huruma. Wewe waweza pia kumsaidia mchanga huyo kwa kumwongoza kwenye uhusiano mwema ma Muumba wetu—“Baba wa yatima” aliye wa kweli kweli na Rafiki mkuu zaidi ambaye yeyote angetaka.—Zaburi 68:5.

Hata hivyo je, kuna tumaini la wakati ambapo idadi za talaka zitabadilika, wakati ambapo watoto watakuwa na uhakika wa kukua katika familia nzima nzima zenye furaha?

Wakati Familia Itakapopona

Ikiwa ni lazima tutegemee binadamu kwa suluhisho, basi jibu ni la, hakuna tumaini halisi kwa watoto. Binadamu hawezi hata kuanza kutengeneza familia ya kibinadamu ya tufe lote iliyogawanyika na isiyo na matumaini yoyote, achia mbali familia zisizohesabika ambazo zimegawanyika zinazoifanyiza. Kama vile Linda Bird Francke alivyoandika katika Growing Up Divorced: “Mengi sana yametendeka haraka sana. Korti zinatatanika. Mashule yanatatanika. Familia zinatatanika. Hakuna mtu ajuaye cha kutazamia kutoka kwa mwingine katika hizi siku za wingi wa talaka kwa vile hakuna sheria, hakuna violezo vya kufuatwa.”

Lakini Muumba wa binadamu hatataniki. Yeye anaelewa ulimwengu wetu uliogawanyika, na anaona kwamba hauhitaji “wataalamu” wa kibinadamu ili kuutuliza. Unahitaji kubadilishwa. Naye anaahidi kufanya hivyo. Yeye anaahidi kwamba wale wanaofanya mapenzi yake wataokoka wakati mfumo huu mwovu upitapo na waishi kuona paradiso iliyorudishwa ya tufe lote. (Luka 23:43; 1 Yohana 2:17) Akiishi chini ya utawala wa Mungu, mwanadamu ataponywa kutokana na dhambi ambayo huambukiza asili yake. Ubinafsi na kutokamilika kunakoleta migawanyiko, chuki, na kutokuwa na umoja mwishowe kutapitilia mbali. Familia ya kibinadamu itapona.—Ufunuo 21:3, 4.

Talaka wakati huo itakuwa sazo la wakati uliopita wenye kudidimia.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Mashauri kwa Wazazi Waliotalikiana

Usigombane na aliyekuwa mwenzi wako— iwe ni kwa simu au ana kwa ana—mbele ya watoto.

Usimchambue aliyekuwa mwenzi wako mbele ya watoto. Wakati watoto wako wanapochambua mzazi aliyeondoka, usiwatie moyo au kujiunga nao.

Usiwalazimishe watoto kuchagua kati ya wazazi wao, na usiwageuze dhidi ya mwenzi wako aliyeondoka.

Usiwaruhusu watoto wako wakudhulumu kwa kusema kwamba watajiunga na mzazi aliyeondoka. Kuachilia uhaini kama huo wa mawazo ya moyoni kutawahimiza wakudhibiti na hilo huenda hata likazuia maendeleo yao ya kiadili.

Usiwatumie watoto kumpeleleza mwenzi wako, ukiwalazimisha kutoa habari wanaporudi kutoka kwa kila ziara.

Usiwaulize watoto kupeleka jumbe za hasira au maombi ya pesa yenye kuaibisha kutoka kwako hadi kwa mwenzi wako wa kwanza.

Usimkaripie mtoto wako kwa semi kama, “Wewe ni kama baba yako.” Mtoto huyo hatakuwa na maoni kwamba unamchambua baba tu, bali pia kutamfanya ahisi kuwa tayari ameshindwa na atarudia makosa ya mzazi yule mwingine.

Toa uthibitisho kwamba wewe ni msikilizaji mzuri, ukiacha watoto wako waonyeshe hisia zao—hata zile ambazo hukubaliani nazo.

Toa uasiliano kwa uwazi, uhuru, na kwa udhahiri. Hata hivyo, walinde kutokana na habari wasizohitaji kujua. Mwana au binti yako huenda akaonekana kuwa msiri wa kufaa. Lakini kumbuka, mtoto si mtu mzima wala si yeye aliye mahali pa mwenzi wako, hata akionekana kuwa mkomavu jinsi gani.

Toa kitulizo kwa watoto wako na uwahakikishie kwamba wao hawakusababisha talaka, wala hawawezi kuingilia sasa ili kuokoa ndoa yako.

Toa onyesho la upendo wenye shauku na wa kweli. Huenda watoto wakadhani kwamba wazazi ambao wanaweza kuacha kupendana wao kwa wao wanaweza kwa urahisi kuacha vilevile kuwapenda watoto wao.

Toa ushirikiano na aliyekuwa mwenzi wako katika mipaka ya kadiri nzuri na miradi iliyo halisi.

Toa usawaziko wa sifa na nidhamu, ukiweka mipaka ya kadiri nzuri na miradi iliyo halisi.

Toa mfano wewe mwenyewe, ukijiepusha na tabia ya ukosefu wa adili ambayo unawafunza kujiepusha.

Toa wakati wako mwingi wa mapumziko pamoja na watoto wako kwa kadiri iwezekanavyo.

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Je, Wewe ni Mzazi wa Mwendo Mrefu?

IKIWA ndivyo, huenda ukaliona kuwa jambo rahisi sana kujiondoa kwenye habari hii. Labda unahisi kwamba kupanga ratiba ya ziara hakustareheshi kama vile tu kuuliza mwenzi wako ruhusa ya kuwaona watoto wako mwenyewe. Au labda watoto wako wana mzazi mwingine mpya, nawe unahisi kuwa huhitajiki tena.

Lakini wahitajika. Biblia yahimiza: “Akina baba, msiwachokoze watoto wenu.” (Waefeso 6:4) Ikiwa utatoweka maishani mwa watoto wako, si kwamba wewe utawaudhi tu bali pia utadhoofisha hisia zao za kujithamini, ukiwafanya wahisi kama wasiopendwa na wasiopendeka. Hata uhusiano mdogo tu na watoto wako ni afadhali kuliko kukosa kabisa.

Inaonekana kwamba urefu wa muda unaotumia katika ziara yako ndio wa maana zaidi kuliko ukawaida wa ziara. Kwa kadiri ambayo ziara inavyokuwa ndefu, ndivyo itakavyokuwa hakika zaidi kwamba mtoto wako atakumbuka vipindi hivyo alipokuwa nawe. Miriam Galper Cohen, yeye mwenyewe akiwa mzazi wa mwendo mrefu, aandika katika kitabu chake juu ya habari hiyo kwamba ziara hizi hazihitaji kuwa tafrija zenye kutokeza. Wakati mwingine ni kule kutembea pamoja kwa ukimya, au kupata mlo pamoja, ambako hufanyiza kumbukumbu nzuri kabisa.

Kupiga simu mara nyingi, ukiwa na ratiba ya kawaida ya kufanya hivyo, husaidia pia kukuweka karibu na mtoto wako. Au unaweza kujirekodi katika kanda la utepe ukimsomea mtoto wako hadithi au ukizungumza juu ya siku za utoto wako. Zaidi ya kanda za utepe na barua, unaweza kumtumia mtoto wako picha, michoro, picha za vichekeshi, au makala za magazeti ambazo zakupendeza wewe. Cohen pia adokeza upate kujua ni vitabu gani na programu za televisheni ambazo mtoto wako anapendelea, ukivisoma na kuzitazama wewe mwenyewe, halafu kuzijadili kupitia kwa barua au simu.

Kama vile Cohen anavyosema, “Kutunza watoto kutoka mbali ndio uchaguzi wa mwisho ulio bora katika mipango ile mingime ya utunzi, ikiwa afadhali tu kuliko kukosa kuwaona watoto kabisa.” Walakini, kuna njia za kufanya mtoto wako ajue juu ya upendo wako wenye kuendelea na hangaiko lako. Hata kitendo kidogo sana cha kumfikiria kwaweza kumwokoa mtoto wako kutokana na uchungu mwingi.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Je, kuna mambo mbalimbali ambayo unaweza kuyashiriki na mtoto wako? Talaka hukomesha ndoa, si kuwa mzazi

[Picha katika ukurasa wa 10]

Je, unajua mtoto yeyote wa talaka ambaye anaweza kufurahia urafiki?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki