-
Maswali Kutoka kwa WasomajiMnara wa Mlinzi—1997 | Aprili 1
-
-
Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Mkristo apaswa kufanya nini aitwapo kwa ajili ya kazi ya baraza la mahakama?
Katika nchi fulani, mfumo wa kisheria hutumia mabaraza ya mahakama yenye watu waliochaguliwa kutoka kwa raia. Mahali ambapo hayo hutumika, Mkristo apaswa aamue jinsi ya kuitikia aelekezwapo aripoti kwa ajili ya kazi ya baraza la mahakama. Wakiwa na dhamiri nzuri Wakristo wengi wamefikia mkataa wa kwamba kanuni za Biblia hazikatazi kuhudhuria, kama vile Shadraka, Meshaki, na Abednego walivyotii mwelekezo wa serikali ya Babiloni, waende kwenye uwanda wa Dura na kama vile Yusufu na Maria walivyoenda Bethlehemu kufuatia mwelekezo wa wenye mamlaka wa Roma. (Danieli 3:1-12; Luka 2:1-4) Hata hivyo, kuna mambo ambayo Wakristo wenye moyo mweupe wanaweza kufikiria.
Mabaraza ya mahakama hayatumiwi kila mahali. Katika nchi fulani, kesi za raia na za uhalifu huamuliwa na hakimu wa kitaaluma au kikundi cha mahakimu. Kwingineko, ile ijulikanayo kuwa sheria ya kawaida ndiyo hutumika, na mabaraza ya mahakama ni sehemu ya utaratibu wa kihukumu. Hata hivyo, watu walio wengi wanajua machache sana juu ya jinsi mabaraza ya mahakama yanavyochaguliwa na kazi yanayofanya. Kwa hiyo kuwa na habari juu ya mambo makuu kwaweza kusaidia iwe utakabiliwa na kazi ya baraza la mahakama au la.
Watu wa Mungu humtambua Yehova kuwa Hakimu Mkuu Kuliko Wote. (Isaya 33:22) Katika Israeli la kale, wanaume wenye uzoefu waliokuwa wanyoofu na wasiopendelea walitumika wakiwa waamuzi ili kusuluhisha ugomvi na kuamua maswali ya sheria. (Kutoka 18:13-22; Mambo ya Walawi 19:15; Kumbukumbu la Torati 21:18-21) Kufikia wakati ambapo Yesu alikuwa hapa duniani, kazi ya hukumu ilishughulikiwa na Sanhedrini, mahakama kuu ya Kiyahudi. (Marko 15:1; Matendo 5:27-34) Hakukuwa na uandalizi wowote kwa Myahudi wa kawaida kuwa kwenye baraza la mahakama la raia.
Nchi nyingine zilitumia mabaraza ya mahakama yaliyofanyizwa kwa raia. Socrates alifanyiwa kesi na washiriki 501 wa baraza la mahakama. Kufanywa kesi na baraza la mahakama kulikuwako pia katika Jamhuri ya Roma, ingawa hilo lilikomeshwa chini ya utawala wa maliki mbalimbali. Baadaye, Mfalme Henry 3 wa Uingereza alifanya uandalizi mshtakiwa ahukumiwe na jirani zake. Ilihisiwa kwamba kwa kuwa walimjua mshtakiwa, hukumu yao ingekuwa ya haki zaidi kuliko utaratibu mbalimbali ambamo mshtakiwa alijaribu kuthibitisha kutokuwa na hatia kwake kwa kupigana au kwa kuokoka masaibu ya aina fulani. Kadiri wakati ulivyopita, mfumo wa baraza la mahakama ulibadilika na kuwa mpango ambamo kikundi cha raia kilipaswa kusikiliza kesi na kufikia uamuzi unaotegemea uthibitisho. Hakimu wa kitaaluma aliwaongoza kwenye hoja mbalimbali za uthibitisho.
Kuna aina nyingi mbalimbali za mabaraza ya mahakama, idadi ya washiriki wa baraza la mahakama, na yanayohusishwa katika kufikia uamuzi. Kwa kielelezo, Marekani, baraza la mahakama kuu lenye washiriki kuanzia 12 hadi 23 huamua ikiwa kuna uthibitisho wa kutosha ili mtu ashtakiwe kosa la uhalifu; haliamui kuwa au kutokuwa na hatia. Vivyo hivyo, katika baraza la mahakama la uchunguzi, washiriki wa baraza la mahakama hupima uthibitisho ili kuamua ikiwa uhalifu ulifanywa.
Watu walio wengi wanapofikiria juu ya baraza la mahakama, wao hufikiria kikundi cha raia 12 kesini—ama ugomvi wa kiraia ama kesi ya uhalifu—ambao husikiliza ushuhuda ili kuamua kuwa au kutokuwa na hatia. Hilo ni baraza dogo la mahakama, kwa kutofautishwa na baraza la mahakama kuu. Kwa ujumla, mahakama hutuma notisi za kuja kwa kazi ya baraza la mahakama kwa watu mmoja-mmoja waliochaguliwa kutoka kwa orodha ya wapiga-kura, madereva wenye leseni, na kadhalika. Huenda wengine waonwe kuwa wasiostahili, kama vile waliothibitishwa kuwa wakosaji na wasio na akili timamu. Ikitegemea sheria za nchi—watu kama vile madaktari, makasisi, wanasheria, au wenye biashara ndogo-ndogo—waweza kuomba kuachiliwa. (Huenda wengine wakaachiliwa kwa sababu wanapinga kwa dhati kibinafsi na kwa kudhamiria utumishi wa baraza la mahakama.) Hata hivyo, wenye mamlaka wanazidi kufuta kuachiliwa hivi kwamba wote wanalazimika kuripoti kwa ajili ya kazi ya baraza la mahakama, labda tena na tena kwa miaka kadhaa.
Si wote wanaoripoti kwa ajili ya kazi ya baraza la mahakama wanaoshiriki katika baraza la mahakama wakati wa kesi. Kutoka kwa kikundi cha watu walioitwa, baadhi yao wanachaguliwa kishelabela kuwa walio na uwezekano wa kuwa washiriki wa baraza la mahakama kwa ajili ya kesi mahususi. Kisha hakimu hutambulisha mlalamishi na mshtakiwa na mawakili wao na hufafanua aina ya hiyo kesi. Yeye na hao mawakili huchunguza kila mmoja aliye na uwezekano wa kuwa mshiriki wa baraza la mahakama. Huo ndio wakati wa mtu kusema msimamo wake ikiwa ana sababu ya kidhamiri ya kutotumikia kwa sababu ya jinsi kesi ilivyo.
Hicho kikundi huhitaji kupunguzwa kufikia idadi ya watu watakaosikiliza kesi hiyo. Hakimu atamwachilia mbali yeyote ambaye upendeleo wake waweza kuzusha shaka kwa sababu ya upendezi unaoweza kutokea katika hiyo kesi. Pia, mawakili wa kila upande wana haki ya kuwaachilia mbali wachache kati ya washiriki wa baraza la mahakama. Wowote wanaoachiliwa mbali kutoka kwa hilo baraza la mahakama hurudi kwenye kile kikundi cha watu ili kungoja uteuzi mwingine wa kishelabela kwa ajili ya kesi nyinginezo. Wakristo fulani walio katika hali hizo wametumia huo wakati kutoa ushahidi wa vivi hivi. Baada ya siku kadhaa, kazi ya mtu wa baraza la mahakama huisha, awe amesikiliza kesi akiwa mshiriki wa baraza la mahakama au la.
Wakristo hujitahidi ‘kushughulika na mambo yao wenyewe,’ bila kuhusika katika “mambo ya watu wengine.” (1 Wathesalonike 4:11; 1 Petro 4:15) Myahudi fulani alipomwuliza Yesu kutoa hukumu juu ya jambo lililohusu urithi, aliitikia hivi: “Wewe mtu, nani aliyeniweka mimi rasmi hakimu au mgawaji-fungu juu ya nyinyi watu?” (Luka 12:13, 14) Yesu alikuja kutangaza habari njema ya Ufalme, wala si kutoa maamuzi juu ya mambo ya kisheria. (Luka 4:18, 43) Huenda itikio la Yesu likawa lilimsukuma mtu huyo kutumia njia za kusuluhisha ugomvi zilizo katika Sheria ya Mungu. (Kumbukumbu la Torati 1:16, 17) Ingawa hoja hizo ni halali, kuitikia mwelekezo wa kuripoti kwa ajili ya kazi ya baraza la mahakama ni tofauti na kujishughulisha katika mambo ya watu wengine. Kwafanana zaidi na ile hali ya Danieli na waandamani wake watatu. Serikali ya Babiloni iliwaamuru waende kwenye uwanda wa Dura, na kufanya kwao hivyo hakukuvunja Sheria ya Mungu. Walilofanya baada ya hapo lilikuwa jambo tofauti, kama vile Biblia inavyoonyesha.—Danieli 3:16-18.
Watumishi wa Mungu walipoacha kuwa chini ya Sheria ya Kimusa, walilazimika kushughulika na mahakama za kilimwengu katika nchi mbalimbali. Mtume Paulo aliwahimiza “watakatifu” katika Korintho kusuluhisha tofauti zao kutanikoni. Akirejezea mfumo wa kisheria wa mahakama za kilimwengu kuwa “watu wasio waadilifu,” Paulo hakupinga kwamba mahakama hizo zilikuwa na sehemu katika kushughulikia mambo ya kilimwengu. (1 Wakorintho 6:1) Alijitetea mwenyewe katika kikao cha kisheria cha Kiroma, hata kukata rufani ya kesi yake kwa Kaisari. Haikuwa kana kwamba mahakama za kilimwengu ni zenye kosa kimsingi.—Matendo 24:10; 25:10, 11.
Mahakama za kilimwengu ni utendaji wa “mamlaka zilizo kubwa.” Hizo “zimesimama zikiwa zimewekwa na Mungu katika mahali pa vyeo vyazo vyenye kuhusu,” nazo hufanyiza na kutekeleza sheria. Paulo aliandika hivi: “Ni mhudumu wa Mungu kwako kwa faida yako. Lakini ikiwa unafanya lililo baya, uwe katika hofu: kwa maana haichukui upanga bila kusudi; kwa maana hiyo ni mhudumu wa Mungu, mlipiza-kisasi ili kuonyesha hasira ya kisasi juu ya yeye anayezoea kufanya lililo baya.” Wakristo ‘hawaipingi hiyo mamlaka’ itekelezapo utendaji huo wa kisheria, kwa kuwa hawataki ‘kuchukua msimamo dhidi yayo’ na kupokea hukumu.—Waroma 13:1-4; Tito 3:1.
Katika kusawazisha maoni, Wakristo wapaswa kufikiria ikiwa wanaweza kujitiisha chini ya madai fulani yanayotolewa na Kaisari. Paulo alishauri hivi: “Walipeni wote [mamlaka zilizo kubwa] haki zao, kwa yeye atakaye kodi, kodi; kwa yeye atakaye ushuru, ushuru; kwa yeye atakaye hofu, hofu hiyo; kwa yeye atakaye heshima, heshima hiyo.” (Waroma 13:7) Habari hiyo ni ya moja kwa moja kama kodi ya fedha. (Mathayo 22:17-21) Kaisari akisema kwamba raia lazima watoe wakati na jitihada zao kusafisha barabara au kufanya kazi nyingine ambayo ni miongoni mwa utendaji wa Kaisari, kila Mkristo lazima aamue ikiwa atajitiisha.—Mathayo 5:41.
Wakristo fulani wameuona utumishi wa baraza la mahakama kuwa kumpa Kaisari yaliyo ya Kaisari. (Luka 20:25) Katika kazi ya baraza la mahakama, kazi ni kusikiliza uthibitisho na kutoa maoni yenye kufuatia haki juu ya hoja za mambo hakika au sheria. Kwa kielelezo, kwenye baraza la mahakama kuu, washiriki wa baraza la mahakama huamua ikiwa uthibitisho watoa sababu ya mtu kufanyiwa kesi; hawachanganui kama ana hatia. Namna gani juu ya kesi ya kawaida? Kwenye kesi ya raia, baraza la mahakama laweza kutoa ridhaa au fidia. Katika kesi ya uhalifu, wanachanganua waone ikiwa uthibitisho wategemeza uamuzi wa kuwa na hatia. Nyakati nyingine wanapendekeza ni hukumu gani iliyowekwa na sheria ipaswayo kutumika. Kisha serikali hutumia mamlaka yayo “kuonyesha hasira ya kisasi juu ya yeye anayezoea kufanya lililo baya,” au “kupasisha adhabu juu ya watenda-maovu.”—1 Petro 2:14.
Vipi ikiwa Mkristo hahisi kwamba dhamiri yake yamruhusu kutumikia katika baraza la mahakama fulani? Biblia haitaji kazi ya baraza la mahakama, kwa hiyo hawezi kusema kwamba, ‘Kutumika katika baraza la mahakama hakupatani na dini yangu.’ Ikitegemea kesi, aweza kusema kwamba kutumika katika baraza la mahakama kwa ajili ya kesi mahususi kwapingana na dhamiri yake mwenyewe. Hilo laweza kuwa hivyo ikiwa kesi yahusu ukosefu wa adili katika ngono, utoaji-mimba, uchinjaji-binadamu, au suala lingine ambalo kufikiri kwake juu yalo kumeelekezwa na ujuzi wa Biblia, wala si na sheria ya kilimwengu. Hata hivyo, kihalisi, yawezekana kwamba kesi ambayo amechaguliwa kwa ajili yayo haihusishi masuala hayo.
Mkristo mkomavu angeweza pia kufikiria ikiwa angekuwa na daraka lolote kwa ajili ya hukumu inayotolewa na mahakimu. (Linganisha Mwanzo 39:17-20; 1 Timotheo 5:22.) Ikiwa uamuzi wa kuwa na hatia ni wenye kosa na hukumu ya kifo inatolewa, je, Mkristo kwenye baraza la mahakama angeshiriki hatia ya damu? (Kutoka 22:2; Kumbukumbu la Torati 21:8; 22:8; Yeremia 2:34; Mathayo 23:35; Matendo 18:6) Kwenye kesi ya Yesu, Pilato alitaka kuwa ‘bila hatia ya damu ya mtu huyu.’ Wayahudi walisema hivi kwa utayari: “Damu yake ije juu yetu na juu ya watoto wetu.”—Mathayo 27:24, 25.
Ikiwa Mkristo ameenda kwa kazi ya baraza la mahakama, kama ilivyoelekezwa na serikali, lakini kwa sababu ya dhamiri yake ya kibinafsi akakataa kutumika kwenye kesi mahususi kujapokuwa kusisitiza kwa hakimu, huyo Mkristo apaswa kuwa tayari kukabili matokeo—yawe faini au kifungo.—1 Petro 2:19.
Mwishowe, kila Mkristo akabiliwaye na kazi ya baraza la mahakama lazima aazimie ni mwendo gani wa kufuata, kwa kutegemea uelewevu wake wa Biblia na dhamiri yake mwenyewe. Wakristo fulani wameenda kwa ajili ya kazi ya baraza la mahakama na wametumika kwenye mabaraza fulani ya mahakama. Wengine wamehisi wakilazimika kukataa hata wakabilipo adhabu. Kila Mkristo lazima ajiamulie mwenyewe atakalofanya, na wengine hawapaswi kuchambua uamuzi wake.—Wagalatia 6:5.
-
-
Mashahidi wa Yehova Watafanya Mikusanyiko ya KimataifaMnara wa Mlinzi—1997 | Aprili 1
-
-
Mashahidi wa Yehova Watafanya Mikusanyiko ya Kimataifa
Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova linapanga kufanya mikusanyiko ya kimataifa katika 1998. Tangazo hilo lilipokewa kwa itikio lenye idili kwenye mkutano wa kila mwaka wa Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania, uliofanywa katika Jumba la Kusanyiko la Jiji la Jersey siku ya Jumamosi, Oktoba 5, 1996.
Pamoja na mikusanyiko ya wilaya ya kawaida, mikusanyiko ya kimataifa kadhaa itafanywa Amerika Kaskazini katikati ya mwaka wa 1998. Yatarajiwa kwamba mikusanyiko hiyo itaunganisha mamia ya maelfu ya Mashahidi kutoka sehemu nyingi za dunia. Ili kuwezesha nchi nyingi iwezekanavyo kuwakilishwa, kila moja ya zile ofisi za tawi zaidi ya 100 za Watch Tower Society itakuwa na wajumbe kadhaa kwa ajili ya jiji hususa la mkusanyiko wa kimataifa katika Amerika Kaskazini.
Kwa wazi, si wote ambao wangependa kusafiri hadi Amerika Kaskazini watakaoweza kufanya hivyo. Hata hivyo, huenda ikawezekana kwa maelfu ya watu kuhudhuria mkusanyiko wa kimataifa karibu zaidi na kwao. Mipango inafanywa kwa ajili ya mikusanyiko ya kimataifa kufanywa katika nchi mbili au tatu za Ulaya na mingine katika Afrika, Asia, Amerika ya Latini, Pasifiki Kusini, na Karibea.
Kwenye wakati ufaao, ofisi za tawi za Sosaiti zitajulisha makutaniko katika maeneo yazo juu ya jiji au majiji ya mkusanyiko ambako yamealikwa. Habari juu ya tarehe mbalimbali za mkusanyiko na mipango ya kuwachagua wajumbe itatolewa. Wale wafikiriao kujaza fomu za maombi kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe huenda wakataka kuanza kuhifadhi kiasi fulani cha fedha zao wakitarajia matukio hayo ya pekee.
Mashahidi wa Yehova wote ulimwenguni pote wanaweza kutazamia kilicho akibani kwenye mikusanyiko hiyo ya kimataifa ya mwaka wa 1998. Mikusanyiko ya wilaya katika nchi zote itakuwa na programu ileile.
-